CUF, Polisi Z’bar washikana uchawi

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
MGOGORO wa nani anavamia majumbani kwa wananchi, kuwakamata na kuwatesa unatikisa katika visiwa vya Zanzibar, anaandika Mwandishi Wetu.

Chama cha Wananchi (CUF) kimevunja ukimya baada ya kuhusishwa na uhalifu huo huku kikituma ujumbe kwa Jeshi la Polisi kwamba, kama wana ushahidi waende mahakamani.

Katika siku za hivi karibu Zanzibari imekuwa ikitikiswa na vitendo vya kinyama ikiwa ni pamoja na kuvamiwa na kuteswa hususan walioonekana kuunga mkono upinzani kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Unguja, Salim Abdalla Bimani, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa CUF amesema, katika matukio yanayotokea, wanachama wake pamoja na wananchi wanaokiunga mkono chama hicho ndio wanaoathirika zaidi.

“Hata kwa yale matukio yanayopangwa na kuumiza wananchi, wanachama wetu ndio wanaovamiwa majumbani mwao na kuswekwa vituo vya polisi na kukaa muda mrefu bila ya kupelekwa mahakamani,” amesema Bimani.

Amesema, kufikia sasa viongozi 130 wa ngazi ya majimbo wamekamatwa na kushikiliwa vituo vya polisi na baadhi ya viongozi wa kitaifa wanatangazwa redioni kuwa, wajisalimishe kokote waliko.

“Si kweli wanachokisema polisi kwamba matukio ya uhalifu yanafanywa na viongozi wetu. Kila mtu anajua wazi sisi ndio wahanga wakubwa wa visa vya ukandamizaji vinavyofanywa na vyombo vya dola katika sura ya mpango maalum wa kukandamiza haki za watu na uhuru wa wananchi kujishughulisha na siasa,” amesema Bimani.

Anatoa kauli hiyo katika majibu ya swali la kama ni kweli wao CUF ndio wanaohusika na vitendo vya ukataji mimea mashambani ikiwemo mikarafuu kama inavyosemwa na Kamishna Msaidizi Salum Msangi, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DDCI).

Hivi karibuni akisoma hotuba ya kufunga mkutano wa bajeti wa Baraza la Wawakilishi visiwani humo, Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pilisi wa Rais wa Zanzibar amesema, kutokana na uchunguzi wa Jeshi la Polisi, viongozi wakubwa wa CUF ndio wanaohusika na matukio ya uhalifu hayo.

Balozi amesema, viongozi hao bila ya kuhofiwa vyeo vyao, watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa wanashiriki kuvuruga misingi ya amani na utulivu.

Hata hivyo, Bimani amesema kinyume chake, kuna matukio mbalimbali ya majengo ya ofisi ya chama hicho kuvamiwa na kuteketezwa kwa moto na viongozi wa ngazi mbalimbali kukamatwa na kusingiziwa kesi za kuhusika na vitendo vya uhalifu.

“Ofisi yetu ya kisasa Jimbo la Dimani iliteketezwa kwa moto kabla ya Uchaguzi Mkuu. Ofisi yetu ya Wilaya ya Magharibi A iliyopo Mpendae ilivamiwa na askari wa vikosi vya SMZ.

“Vifaa vikachukuliwa na viongozi na wanachama wapatao 20 kukumatwa, lakini hakuna mtu aliyekamatwa au kushitakiwa mpaka leo hii,” amesema.

Bimani alitoa mfano wa watu 27 katika Jimbo la Ziwani kisiwani Pemba wanaoshikiliwa kwa zaidi ya siku tatu bila ya kupelekwa mahakamani na kutangazwa kujisalimisha popote alipo kwa mwakilishi aliyechaguliwa na wananchi himbo la Chake Chake, Pemba, wakati anajuilikana nyumbani kwake na simu yake ni ushahidi wa mpango mahsusi wa polisi kukandamiza wananchi.

Amesema, CUF inajua wazi kuwa mpango huo umeandaliwa kwa lengo la kuinyamazisha isidai haki ya wananchi kukichagua chama hicho.

Amesema, viongozi wao hawatarudi nyuma na wanaendelea kuhimiza wananchi washikilie msimamo wa kuikataa serikali iliyojiweka madarakani baada ya CCM kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama kupindua maamuzi ya wananchi waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Amesema, mpango wa kukiua CUF hautafanikiwa na ushahidi ni kukishuhudia kikishinda uchaguzi wa Zanzibar kwa ushindi mkubwa mwaka jana na wananchi kuitikia wito wake wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio wa 20 Machi mwaka huu aliouita wa haramu.

Uchaguzi wa marudio ulioitishwa baada ya Jecha Salum Jecha kuufuta kibabe 28 Oktoba 2015, umekibakisha CCM madarakani huku CUF kikipinga na kutoitambua serikali yake Dk. Ali Mohamed Shein.
 
Back
Top Bottom