[h=2][/h]
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro
Chama Cha Wananchi (CUF), kimesema maandamano ambayo awali kilipanga
kufanya Juni 29, mwaka huu kuelekea Ikulu lakini yakaahirishwa kutokana
na ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama yako pale pale.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema kwa sasa
viongozi wengi wa chama wapo mikoani, lakini watakaporudi jijini Dar
es Salaam chama kitafanya mkutano utakaopanga lini maandamano hayo
yafanyike.
Hatujakutana bado. Wajumbe wengi tupo mikoani. Sasa tutakaporejea Dar
es Salaam tutapanga siku ya kukutana. Halafu tutapanga siku ya
maandamano na tutawajulisha, alisema Mtatiro.
Kwa mujibu wa CUF, maandamano hayo yana lengo la kumfikishia ujumbe Rais
Jakaya Kikwete, kwa kile wanachodai kuwa vitendo vya ukatili, wizi,
ubakaji na mauaji vinavyofanywa na polisi mkoani Mtwara na kutaka
uchunguzi kuhusu matukio ya Arusha.
Hata hivyo, kuahirishwa kwa maandamano hayo kulikuja baada ya Kamanda wa
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuyapiga marufuku
na kuonya kwamba polisi wangepambana na yeyote ambaye angekaidi amri
hiyo.
CHANZO: NIPASHE