yani yanga hawana maana na wabinafsi, walishindwa muuza Norway kwa USD 50K wamekuja uza kwa 40k tena Tanzania...that tells alot about yangaz viongozi....
BAADA ya kuwekewa ngumu, hatimaye klabu ya Daraja la Pili ya Lov-Ham ya Norway, imeamua kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa Yanga kuhusu nia yake ya kumsajili winga wa timu hiyo, Mrisho Ngassa.
Awali, klabu hiyo ilionyesha nia ya kumtaka mchezaji huyo kwa dau la dola 50,000 za Marekani, sawa na sh mil. 60 na mshahara wa dola 10,000 kwa mwezi sawa na sh mil 12.
Hata hivyo, licha ya timu hiyo kutuma tiketi ya ndege katika Ubalozi wa Norway nchini, kikwazo ilikuwa ni kukosekana kwa mawasiliano kati ya klabu hiyo na uongozi wa Yanga.
Hali hiyo ilitokana na uongozi wa Lov-Ham kufanya mawasiliano na wakala wa wachezaji hapa nchini, Yussuf Bakhressa, badala ya viongozi wa Yanga.
Kwa mazingira hayo, klabu hiyo sasa imelazimika kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kumnasa mchezaji huyo kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.
Akithibitisha hilo jana, Mwenyekiti wa Yanga, Imani Mahugila Madega, alisema tayari klabu ya Lov-Ham imewasiliana naye kwa njia ya barua pepe na simu ya mkononi.
Alisema, klabu hiyo inamtaka Ngassa kwa ajili ya kwenda kukipiga katika timu hiyo na kwamba, wao hawana tatizo kama taratibu zitafuatwa.
"Jana (juzi) tumepokea simu kutoka Norway na ujumbe kupitia website (barua pepe), kuhusiana na klabu hiyo kumtaka Ngassa kwenda kucheza soka nchini humo," alisema Madega.
Madega alisema, baada ya klabu hiyo kuwasiliana rasmi na uongozi wa Yanga, watakutana kujadili suala hilo ili kufikia uamuzi ya nini kifanyike.
Hata hivyo, Madega alizidi kusisitiza kuwa, uongozi wake umekuwa hauna tatizo na wachezaji wanaopata nafasi za kwenda nje kwani hiyo ni manufaa ya mchezaji, Yanga na taifa.
Alisema, kitu muhimu ambacho Yanga imekuwa ikipigania, ni kuona mchezaji anaondoka kwa taratibu sahihi kulingana na sheria zilizopo.
Hatua ya klabu hiyo kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa Yanga, kunatoa mwanga zaidi kwa mchezaji huyo kutimkia Norway, ambako kama atafanikiwa, atakuwa akilipwa mshahara wa sh mil.12 kwa mwezi ndani ya miaka mitatu.
Ngassa, mtoto wa mchezaji wa zamani wa timu ya Pamba ya jijini Mwanza na timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Halfan Ngassa, ni miongoni mwa nyota wa kutumainiwa Yanga na Stars.
Kama Ngassa atafanikiwa kujiunga na Lov-Ham, atakuwa ni mchezaji wa tatu wa Yanga chini ya uongozi wa Madega kwenda nje.
Kabla ya Ngassa, mshambuliaji Said Maulid alisajiliwa na Bravo de Marquiz ya Angola na kipa Ivo Mapunda aliyesajiliwa na St. George ya Ethiopia.