By KHATIMU NAHEKA NA WILBERT MOLANDI (email the author)
Posted Jumatatu,Januari6 2014 saa 14:1 PM IN SUMMARY
Mchezaji huyo ambaye kuanzia Ijumaa iliyopita hayupo mazoezini, anadaiwa kuwakera Yanga kwa mambo mawili.
YANGA imemsimamisha kwa muda usiojulikana kiungo, Athuman Idd Chuji huku akidaiwa kuhusishwa na Simba.
Mchezaji huyo ambaye kuanzia Ijumaa iliyopita hayupo mazoezini, anadaiwa kuwakera Yanga kwa mambo mawili.
Kwanza, aliwakera alipocheza chini ya kiwango kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe na alipotolewa kipindi cha kwanza akaonyesha jeuri kwa kwenda moja kwa moja vyumbani.
Pili, anadaiwa kuwakera zaidi Yanga kwani inadaiwa wiki iliyopita alikuwa kwenye starehe maeneo ya Tabata, Dar es Salaam na kumtaja kiongozi mmoja wa Simba (jina tunalo) kwamba ndiye anayemsaidia kwa mambo mengi kuliko viongozi wa Yanga.
Habari za ndani zinadai kwamba mchezaji huyo alikabidhiwa barua yake, Ijumaa na haielezi kusimamishwa huko kutakwisha lini na jana Jumapili viongozi wa Yanga hawakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusu muda wa adhabu, hata hivyo wamethibitisha kumsimamisha.
Awali uongozi wa Yanga baada ya kumalizika mchezo wa Nani Mtani Jembe ambao Yanga ililala mabao 3-1 dhidi ya Simba, walikuwa na vikao vingi vya siri wakiijadili kwa kina timu na miongoni mwa maamuzi waliyoibuka nayo ni kuliondoa benchi la ufundi la kocha Ernest Brandts na wasaidizi wake, Fred Felix Minziro, Razack Siwa na pai daktari, Nassoro Matuzya.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata na kuthibitishwa na mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji, zinasema Chuji alisimamishwa Ijumaa usiku wiki iliyopita, baada ya kikao chake na viongozi wa kamati ya mashindano ambao walimsomea mashitaka na kumkabidhi barua ya kumsimamisha.
Kiongozi huyo alisema baadhi ya makosa ambayo Chuji anatuhumiwa na uongozi wa timu hiyo ni kucheza chini ya kiwango katika mchezo dhidi ya Simba, ambapo pia katika mechi hiyo alifanya kosa jingine la kuondoka uwanjani bila kuaga mara baada ya kutolewa kipindi cha pili.
Kiongozi huyo pia aliliarifu Mwanaspoti kwamba mbali na kiungo huyo, wapo nyota wengine ambao bado wanajadiliwa wakiwamo nahodha, Nadir Haroub Cannavaro na David Luhende.
Lakini Kocha Msaidizi mpya wa Yanga, Charles Mkwasa, akiwa katika mazoezi ya timu yake, alisema hana taarifa za Chuji.
Mwanaspoti lilimsaka Chuji kupitia simu yake ya mkononi lakini hakupatikana lakini baadaye Kocha aliyetimuliwa na Yanga, Fred Minziro alisema: Hata mimi nimesikia kwamba Chuji kasimamishwa, lakini sishangai kwa kuwa awali tuliambiwa baada ya kufukuzwa makocha pia zoezi hilo litaendelea kwa wachezaji.
Hilo la Chuji kuondoka uwanjani bila ruhusa ni kweli tulipomtoa wakati wa mapumziko, kisheria alitakiwa kurudi uwanjani na kukaa benchi kama wenzake, lakini yeye aliondoka.
heri afanyiwe ushauri nasaha, Papic alijitahidi akaweza kumrudisha kwenye kiwango, bado ni mchezaji mzuri na sijaona midfield inayopiga high ball/long pass kama Chuji