Changamoto za Ufisadi na Uongozi wa Rais Magufuli

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,655
Uongozi ni sehemu ya mahusiano ya watu. Huwezi kuwa kiongozi mzuri kama huna maarifa katika mahusiano ya watu. Hiki ni kionjo muhimu sana katika uongozi. Watu wengi wanapungukiwa nacho, ili uwe kiongozi mzuri ni lazima na ni muhimu kujifunza kuwa na huu uwezo.

Uongozi ni ushawishi ni muhimu sana kiongozi kuwa na ushawishi na sio ulaghai. Ulaghai sio ushawishi. Ushawishi ni uwezo wa kuelezea mawazo yako katika njia nyepesi ambayo watu watakuelewa kile unachotaka kuwafikishia, na kukubali kukufuata, ili kufikia lengo fulani ambao umewashawishi kulifikia na kuweka mipango na mikakati ya pamoja kulifikia lengo hilo.

Ushawishi ni kubadili fikra za watu na mtizamo wa watu kuhusu jambo fulani na kubadili matendo ya jamii husika katika mwelekeo tofauti. Ushawishi ni kufanya watu watende unavyotaka bila kutumia nguvu. Kwahiyo uongozi ni kuongoza watu katika njia fulani na mwelekeo fulani ambao unaweza kuwa na tija au madhara kwa jamii husika kutokana na uwezo wa ushawishi na busara za kiongozi husika.

Tunaweza kushawishi watu kwa mfano ubaya wa ufisadi na kujaribu kubadilisha watu fikra na matendo yao kuelekea katika mkondo tofauti. Watu wakiambiwa madhara ya ufisadi na faida ya kipindi kirefu ambayo wanaweza kuipata kama wakiachana na ufisadi hata kama sio wote kuna watu watakaobadilika mioyo yao. Ushawishi una deal na mioyo na akili za watu. Ikiwa tu serikali yenyewe ikiwa imebadilika na kutenda kwa haki na usawa. Wananchi na hakika watabadilika. Na kuweza kujitolea na kulitumikia taifa lao. Bila kujua kwa undani zaidi madhara ya ufisadi itakuwa ngumu kubadilika kwa urahisi. Watu walio wengi wakibadilika wana uwezo wa kuzuia ufisadi popote utakapo tendeka.

Kwahiyo hili sio suala la kutumia nguvu tu kwasababu tuna deal na kitu ambacho kiko ndani zaidi kuliko nje. Adui yetu ni adui aliyeko ndani sio nje. Kwahiyo nguvu pekee haiwezi kuwa suluhisho. Mabadiliko ya moyo na akili za watu wetu ni muhimu. Mpaka pale watu wetu watakapo kuwa tayari kubadilika wenyewe na kutumikia taifa lao kwa uaminifu ndipo tutakapokuwa tumefanikiwa katika ufisadi na kutowajibika. Hakuna nguvu yeyote kutoka nje itakayowabadilisha zaidi ya nguvu iliyopo ndani yao wenyewe ya kutaka mabadiliko. Kwahiyo ushawishi unahitajika ili kubadili tabia za watu wetu kuelekea katika taifa lao.

Ili uwe kiongozi unahitaji sana imani ya watu kwako. Wakuamini uko kwaajili yao na unauwezo wa kutatua changamoto wanazokabiliana nazo. Tofauti na mtawala ambaye mara zote anajiweka juu ya watu. Lakini kiongozi ni sehemu ya watu ambao kwa pamoja wanafanya kazi kutatua changamoto zinazowakabili. Kwahiyo kiongozi na watu ni lazima wawe kitu kimoja bila ya hivyo changamoto zinazokabili jamii haziwezi kutatuliwa kama kiongozi atakuwa juu na raia watakuwa chini. Kutatua changamoto za nchi lazima viongozi na wananchi wawe kitu kimoja na sio viongozi kuwa mabwana wakubwa au kuwa kama wanyampara wa kusimamia watu. Ni lazima watu na viongozi wao wafanye kazi pamoja.

Mtawala yuko kwaajili ya manufaa yake, manufaa ya jamii kwa ujumla kwake sio ya msingi sana kuliko manufaa binafsi. Utajiri kwake ni kitu cha kwanza, kujikusanyia kadiri ya uwezo wake kwaajili yake na kizazi chake kijacho. Mahusiano yake na jamii sio kitu muhimu sana kwake zaidi ya ''interest '' zake. Lakini kwa kiongozi interest za raia ndio namba moja. Kwahiyo tunaweza kuona hapa tofauti iliyopo kati ya kiongozi na mtawala.

Kwahiyo kiongozi hu order jamii yake na kuhakikisha mahusiano katika jamii yake yanaimarika na watu wanakuwa na malengo mamoja. Mahusiano ni kitu muhimu sana katika jamii yeyote. Bila mahusiano watu hawawezi kufanya kazi pamoja na kuwa na malengo ya pamoja. kwahiyo kiongozi hujenga mifumo mizuri ya mashirikiano katika yale mambo yanayohusu jamii kwa ujumla. Familia yake na mahusiano ya jamii huyaweka imara.

Ni katika mashirikiano mabovu kwenye jamii ndio maana mambo hayaendi sawa. Wakati watu wanapokuwa hawana malengo sawa kwa mambo yanayohusu jamii kwa pamoja.

Watu wanapoacha kuwajibika kwa mambo yanayohusu jamii yao na maendeleo ya jamii yao kwa pamoja. Kutokuwa makini huku kumeharibu mambo mengi. Katika elimu na katika malezi ya watoto na mfumo wa jamii kwa ujumla.

Mfumo wa jamii umeharibika haufanyi kazi ipasavyo hakuna harmony. Watu watakapo weka interests za jamii mbele kuliko interest zao binafsi ni hatua kubwa za maendeleo.

Jamii ambayo kwamfano; imetenga viwanja vya michezo kwaajili ya watoto wao, wanamuona mtu anajenga na wao wanauongozi katika ngazi ya chini na kumuacha aendelee kujenga ni ya kuishangaa. Inaonyesha kutowajibika fulani na kutokuwepo na ushirikiano mzuri miongoni mwa wanachama wa jamii husika. Inaonyesha watu kutokuwa na interest katika mambo yanayohusu jamii yao kwa ujumla. Inaonyesha watu kutokuwa na ufahamu katika mambo yanayowaunganisha kwa pamoja. Familia na mahusiano yake na jamii husika ni muhimu sana.

Kwanza ni lazima tujenge familia zetu na kuziheshimu na kuzithamini na mahusiano yetu katika familia, lakini pili ni lazima tujenge mahusiano yetu na majirani zetu kwakuwa huko chini ndio kunakojenga jamii hadi kuja kwenye taifa. Huku chini pakiimarika juu pataimarika. Kukiwepo na maadili, nidhamu na wajibu wa pamoja katika ngazi za chini huku juu patakuja kuimarika. Ni lazima na muhimu tuanze kujenga huku chini. Ni katika maadili mabovu na nidhamu mbovu katika hatua za awali za ukuaji wa vijana na watoto ndio viongozi wabovu hutokea.

Kwahiyo mkazo unatakiwa huku chini kama tunataka uwajibikaji na vijana wanaowajibika.Tabia njema huundwa hazioti kama uyoga. Kwahiyo kama tunataka kuendelea lazima tujenge tabia za vijana wetu kutoka ngazi ya awali. Tusipofanya haya tusahau kuhusu maendeleo kwasababu hata uwajibikaji hujengwa tokea mtoto akiwa mdogo. Kama tunataka kujenga raia wanaowajibika tuanze sasa.

Matatizo tuliyonayo sasa ambayo tunahangaika nayo na Rais Magufuli anaangaika nayo ni matatizo ya kimaadili na kinidhamu ambayo mizizi yake iko chini. Na dawa yake sio nguvu peke yake bali kuunda upya mfumo wa kijamii na wa kimaadili. Tuna matatizo makubwa ya kimaadili katika taifa letu. Hii ni kazi ya familia na jamii kwa ujumla. Kuangalia mienendo na tabia za watoto wetu. Ni katika tabia zao baadae yetu itakuwa na mwanga. Tuna tatizo kubwa. Ambalo nguvu pekee haitoshi kulimaliza. Tutafunga wengi lakini wengine watachipukia. Tunawaandaaje hawa watoto wengine wanaokuja?

Huu ndio msingi imara ambao tunapaswa kuujenga ambao nina uhakika utadumu kwa muda mrefu zaidi. Na vizazi vyetu vitafurahia msingi huu. Ni jinsi gani tunawatayarisha vijana wetu kuingia kwenye utumishi wa umma kuanzia huko chini kwenye ngazi ya familia na mahusiano yetu katika jamii. Ni katika maadili yao katika hatua za awali kabisa kwenye ukuaji wao ndio huzaa tabia ambazo huingia nazo maofisini na kama elimu yetu haijafanikiwa kuondoa hili ni ngumu kuliondoa. Naomba tuliangalie hili. Polisi wala mahakama hawawezi kumaliza kila kitu kama tunazembea huku chini. Ufisadi unaweza kuwa ndoto kuumaliza kama hatutajenga misingi.

Anachofanya Rais Magufuli kuhusu ufisadi ni udhibiti wa kipindi kifupi tu. Ni muhimu kujenga tabia za watu wetu ili msingi wetu uwe imara. Ili mambo haya yasiwe yanajirudia rudia. Mabadiliko haya yanahitaji watu wote. Na yanahitaji kujitambua kwa watu wetu kwa taifa lao. Elimu ya watoto wetu na makuzi yao ni muhimu sana. Jamii imeharibika na inahitaji great social reform. Taifa linapaswa kubadilika .

Naamini kabisa nilichoandika hapa ndio tiba ya kudumu kwa matatizo ambayo yanatukabili kwa sasa ambayo watu wanayapigia kelele ya ufisadi na nidhamu. Ningependa watu tutafakari kuhusu hili ili tuje na mambo mengi zaidi ambayo yanaweza kulibadili taifa letu.
 
Back
Top Bottom