CHADEMA wasisubiri upepo wa jana kuwavusha ng’ambo hii

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Mojawapo ya mambo yaliyokuwa yakisubiriwa ni kukabidhiwa Uenyekiti wa CCM Rais John Magufuli. Uundwaji wa sekretariati mpya vile vile ni kati ya yaliyokuwa yakisubiriwa.Kati ya hayo, mojawapo limetokea; Rais Magufuli amechaguliwa Mwenyekiti wa CCM lakini hakufanya mabadiliko ya sekretariati.

Kukamilika kwa makabidhiano haya kunatulazimisha kuuliza mwelekeo wa chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) na jinsi kitakavyoitikia mabadiliko haya ndani ya CCM.

Hili ni muhimu kujiuliza kwa sababu CHADEMA imekuwa mhanga mkubwa wa siasa za CCM, kiasi kwamba CCM wakipiga chafya dalili za mafua zikaonekana CHADEMA. Kuna uhusiano fulani mbaya wa vyama hivi viwili kiasi kwamba siasa za nchi yetu zimepata madhara ya kudumu.

Kwa mfano baadhi waliokuwa CCM mwaka jana lakini wakaondoka na wimbi lile la “ulipo tupo” wakimfuata Edward Lowassa CHADEMA lakini kabla hata ya mwaka kuisha wameshindwa kuendelea kukaa naye kule.

Hili linatufanya tuhoji kama kweli walikuwa wanaamini katika upinzani na mabadiliko waliyokuwa wanayaahidi kupitia Lowassa au walikuwa wamepiga hesabu fulani ambayo majibu yake yamegoma na sasa hawana jinsi isipokuwa kurudi kama kungulu aliyekosa mzoga.

Sote tunajua ajenda kubwa ya CHADEMA kwa muda mrefu ilikuwa ni kuliamsha taifa kuhusiana na ufisadi na madhara yake na jinsi gani ufisadi umeligharimu taifa.

Ufisadi huu ulihusishwa siyo tu na serikali lakini baadhi ya viongozi na wachambuzi wengine kama mimi tuliamini kabisa kuwa ufisadi huu kiota chake kilikuwa ndaniya CCM na kwa muda mrefu tuliona ni jinsi gani CCM yenyewe imeshindwa kujisafisha.

Wengi tunakumbuka kuwa ilifika mahali hadi CCM yenyewe ilijaribu kujisafisha kwa kuja na operesheni vua gamba, operesheni ambayo ilifeli. Na kabla ya hapo kulifanyika jitihada mbalimbali za kukisafisha chama lakini jitihada hizo ziligongana na ukuta mkubwa wa watu wasiotaka mabadiliko. Ni katika kushindwa huku ujumbe wa upinzani ulikuwa wazi – CCM ni tatizo na namna pekee ya kuondoa tatizo hilo ni kuiondoa CCM madarakani.

Mwaka jana walipompokea mmoja wa watu waliohusishwa sana na migogoro ndani ya CCM na ufisadi na kumfanya kuwa mgombea wao hoja yao CHADEMA ilikuwa kwamba “lolote ili mradi CCM itoke”. Nakumbuka kuna baadhi ya watu – wakizungumza kwa uchungu na kama wakimaanisha – walisema wazi kuwa hata ikibidi kuchagua jiwe basi watu wachague jiwe kuliko CCM. Ulikuwa ni ugomvi mkubwa na unaoeleweka wa kwa nini hawatakuta kuisikia CCM.

Bahati mbaya ujumbe wao ulipata kutu kubwa kwa sababu katika kukataa CCM walijikuta wao wenyewe ni watu waliokumbatia kile walichokuwa wamekikataa na kukihubiri kwa muda watu wetu wakikatae. Hivyo upepo huo uliwasaidia kwa muda mrefu kupata wanachama na kuonekana wa muhimu katika siasa zetu.

Tatizo ambalo limetokea sasa ni kuwa tangu Rais Magufuli aanze safishasafisha na kuanza kushughulikia baadhi ya kero za muda mrefu za taifa, CHADEMA na hata vyama vingine wanapata shida ya jinsi gani washughulike naye.

Ni vigumu kuanza kulia “Magufuli fisadi” na watu wakaamini; ni vigumu kuimba tena “Serikali inalea mafisadi na viongozi wabovu”. Upepo huu sasa hivi hauvushi hata ngalawa ya karatasi! Ni upepo uliovuma jana.

Kinachojaribiwa sana sasa hivi ni kuwa “Magufuli ni dikteta”. Huu ni upepo mpya lakini nao una kikomo chake! Kwenye ufisadi Watanzania wengi walikuwa wanakubaliana na kuona jinsi gani ufisadi umekithiri nchini na jinsi gani ulikuwa umetamalaki.

Lakini kumuita Magufuli ni “dikteta” sidhani kama watatokea mashabiki wengi hapo. Tatizo la hilo ni kuwa hoja hii inaweza kubakia kwa wasomi wachache (the few elite) ambao wanaangalia mambo kinadharia fulani na hivyo wanaamini mioyoni mwao kuwa kweli Magufuli ni Dikteta.

Tatizo ni kuwa kuna watu na inawezekana wengi sana ambao wanaangalia na kusema kama Tanzania inahitaji kiongozi mkali na anayetumia madaraka yake kiasi cha kudhaniwa ni dikteta basi na iwe hivyo.

Kama kiongozi huyo atahakikisha watoto wetu wanaenda shule, wana mahali pa kukaa, na majengo yenye hadhi ya binadamu; kama kiongozi huyo atahakikisha kuwa wakwepa kodi (bila kujali sura zao) wanabanwa hadi kikomo basi na iwe hivyo; kama wataona kiongozi wanayemtaka anahakikisha uchumi wa Tanzania unakua, elimu yetu inaboreshwa na njia za mkato za kupata ajira zinazibwa ili kila mtu apate nafasi sawa basi watu watasema na iwe hivyo!

Ni katika mazingira hayo changamoto kubwa ipo kwa CHADEMA. Wafanye nini kukabiliana na mtu kama Magufuli? Kumdhiria na kumwacha aendeshe serikali bila kuhojiwa? Je, waendelee kugoma bungeni kwa sababu zisizo na msingi (kama ya kuonekana kwenye TV live!)? Je, wawaachie CCM uwanja wacheze peke yao wakati wananchi wa kawaida wanaonekana hawajali kinachoendelea? Je, wakienda bungeni njia pekee ya kufanya siasa ni kubishana na kutoka; mpaka lini?

Ni hapa ndio naamini uongozi wa CHADEMA unahitaji kujiuliza na kupanga ni wapi wamekosea na ni vipi watarekebisha. Hawana sababu ya kuendelea kufichwa vichwa vyao mchangani.

Nje ya hapo, tunaweza kuwa tunashuhudia kuvunjika kwa upinzani kuelekea 2020. Maana kwa mwendo huu na watu wakaona mabadiliko makubwa wanayoyataka, ni vipi kuna mtu atataka kumchagua hadi mwenyekiti wa kijiji kutoka upinzani 2019 au 2020? Itakuwa vigumu.

Chanzo: Raia Mwema
 
Umemaliza mkuu sema sikio lao tayari ni sikio la kufa lisilo na dawa
 
Back
Top Bottom