Chadema wanaiga mitindo ya Serikali ya Magufuli

Chadema wanaiga mitindo ya Serikali ya Magufuli

mcubic

JF-Expert Member
Joined
Mar 3, 2011
Posts
10,310
Reaction score
6,546
Ushindi mkubwa ambao Serikali ya Awamu ya Tano inaufurahia kwa sasa ni kuwa na wapinzani waliokosa mbinu sahihi. Serikali haipatii katika mambo mengi lakini joto la wapinzani ni hafifu.

Vyama vya upinzani Tanzania vina bahati ya kufanya siasa katika mazingira ambayo wananchi wanakuwa tayari kuvipokea, tatizo lipo kwa vyama vyenyewe kushindwa kutumia vizuri fursa hiyo.

Viongozi wa vyama vya upinzani hawana mbinu za kuwawezesha kutumia mtaji mzuri wa kukubalika kwa wananchi, wanafanya siasa nyepesi matokeo yake hawavuni kilicho ndani ya matarajio.

Wakati huu ambao mazingira ya kufanya siasa kwa vyama vya upinzani yamekuwa magumu Tanzania, udhaifu mkubwa unaonekana kwenye mbinu za chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema).

Hali halisi ya kisiasa nchini inaonesha kuwa Chadema wanafanya siasa zenye mirindimo inayoshabihiana na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Itazame Serikali na utendaji kazi wake, utaona kuwa matamko mengi yanasikika. Mawaziri wanatoa matamko, wakuu wa mikoa nao wana ya kwao. Watendaji wa Serikali ya Rais Magufuli kwa wingi wao, wamekuwa hodari mno kwa kutoa matamko.

Baada ya hapo geukia Chadema na harakati zao za kisiasa, utakutana na taswira ya oparesheni ambazo kwa tafsiri nyoofu ni kuwa hazieleweki. Ni oparesheni ambazo wanachama wa chama hicho kwa wingi wao pamoja na Watanzania kwa jumla wanabaki wakiwa hawazielewi inavyotakiwa.

Hutakosea endapo utasema kuwa Serikali ya Rais Magufuli inajipambanua kama inayopita kwenye wimbi la matamko yenye kutolewa na viongozi pamoja na watendaji mbalimbali. Utakuwa kwenye ukweli pia kama utasema Chadema ni chama cha oparesheni.

Wakati huohuo, Chama cha ACT-Wazalendo, hakiamki ili kiweze kujipambanua kama kina uwezo wa kufanya siasa bora zenye kuendana na mazingira ya sasa, kipo lakini kama kimelala.

Chama cha Wananchi (Cuf), chenyewe kinapotea kwa kasi kubwa. Muda wa kujipanga chenyewe kinafanya siasa za migogoro, wanaparurana wao kwa wao bila kupata suluhu. Badala ya kutafuta kiini cha mgogoro, wanashutumiana kwa usaliti. Kutahamaki mwaka 2019 utafika kikiwa hoi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Vyama vingine havizungumziki kutokana na hali zao kisiasa. Hii ndiyo sababu Serikali ya Awamu ya Tano inafurahia mno mazingira ya upinzani. Maana vyama havina mikakati yenye nguvu yenye kuifanya Serikali au viongozi wa CCM kuamka kujibu mashambulizi au kuitetea Serikali.

Pale hoja zinapoibuka zinakuwa nyepesi na matokeo yake zinajibiwa kwa wepesi wake. Watanzania wanashindwa kuona hoja kinzani zenye nguvu dhidi ya Serikali. Matokeo yake, inaonekana tu Serikali na matamko, Chadema wao wanaamua kujipambanua kama chama cha oparesheni.

Serikali na matamko

Hakuna ubaya wowote Serikali kutoa matamko, tatizo linaloonekana ni kuwa huo umegeuzwa mtindo. Wizara ya Elimu kuna matamko, vivyo hivyo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wizara ya Fedha ina matamko, hali hiyo unaikuta pia Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Habari, Michezo na Sanaa na wizara nyingine. Si rahisi kupitisha wiki pasipo kusikia tamko jipya.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda naye ana matamko yake. Nenda mikoa mingine utakuta hali hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi naye anayo matamko. Jielekeze wilaya nyingine hali ni hiyohiyo.

Linatoka tamko hili, wakati unasubiri utekelezaji wake mara unashtuliwa na lingine, mara hujakaa vizuri linatolewa jipya. Matokeo yake wananchi wanaamua kuzoea matamko. Ni tatizo kubwa kwa Serikali pale wananchi wanaposikia kauli za viongozi wao kisha waseme; tumeshazowea.

Serikali lazima ijipambanue kwa vitendo kuliko maneno. Vitendo vinakuwa vingi kisha maelezo yanatolewa pale tu inapobidi. Tena yanatolewa na wasemaji wa Serikali. Tatizo la Tanzania wasemaji wanafunikwa, wakuu wao ndiyo wanataka wazungumze na kuonekana kila wakati.

Rais Magufuli na watendaji wa Serikali yake wanapaswa kutambua kuwa matamko mengi husababisha mwangwi. Vilevile ni vizuri kukumbuka kuwa kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, tafsiri yake ni vitendo kuliko maneno.

Watu wa kazi huwa hawazungumzi sana, badala yake wanatenda zaidi. Watendaji wakweli huonekana mara chache kisha muda mwingi wanapotea. Watendaji wa Serikali ya Rais Magufuli wanaonekana sana.

Katika eneo hili, inaweza kuzungumzwa hoja kuwa kuonekana kwao ndiyo urahisi wa vyombo vya habari kupata habari. Ukweli ni kuwa Serikali katika kila wizara kuna ofisa wa mawasiliano. Hao maofisa wa mawasiliano ndiyo hasa wanatakiwa kuonekana wakitoa ufafanuzi wa wizara zao.

Inawezekana kazi inafanyika inavyotakiwa. Hata hivyo, watu wakionekana mara nyingi wakizungumza hufunika yale matendo ambayo hayaonekani wala hayatolewi ufafanuzi kwa ufanisi wake na matokeo.

Chadema na oparesheni

Kama Serikali inavyokwenda na matamko, Chadema nao wanaiga mwendo huohuo. Sasa hivi wamekuja na oparesheni Kata Funua. Hata kama hii ya sasa itakuwa na sura inayoeleweka lakini je, nani wa kuamini?

Kimsingi kitendo cha Chadema kuibuka na oparesheni mpya, kinafanya ionekane Chadema ni ileile na mbinu zake ni zilezile. Chadema ya Serikali ya Awamu ya Nne na oparesheni zao, ndiyo hiyohiyo ya Awamu ya Tano.

Kati ya mwishoni mwa Julai mpaka Septemba mwaka huu, Chadema ilitikisa nchi na oparesheni ambayo waliiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta). Matokeo ya jumla yalionesha kuwa chama hicho kilikuwa kinajaribu, hakikuwa kimejipanga hasa kivitendo.

Suala la Ukuta bado ni deni kubwa kwa Chadema kwenye macho ya Watanzania hususan wanachama na wakereketwa wa chama hicho. Mpaka sasa hawajaambiwa majibu ya kutosha kuhusu malengo ya Ukuta na kuahirishwa kwake.

Je, Ukuta ulikuwa geresha au viongozi wake walihofia vitisho vya dola ambavyo vilitolewa? Je, yale matukio ya polisi kufanya mazoezi hadharani wakiwa na silaha nzito kuelekea Septemba Mosi, mwaka huu, yaliwafanya waogope?

Tamko la kwanza lilikuwa kwamba kilele cha Ukuta kingekuwa Septemba Mosi, mwaka huu. Ilipofika Agosti 31, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kuahirisha oparesheni hiyo mpaka Oktoba Mosi, mwaka huu.

Septemba 30, mwaka huu, Mbowe tena akatokeza kutangaza kuahirisha Ukuta kwa muda usiojulikana mpaka pale itakapotangazwa tena. Mpaka sasa ufafanuzi haujatolewa.

Nilisoma mahojiano ya Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji, akieleza mafanikio ya Ukuta. Yalikuwa majibu yenye propaganda nyepesi ambazo hazipaswi kufanywa na chama chenye madhumuni ya kweli ya kushika dola.

Unawezaje kusema ulifanikiwa katika Ukuta, wakati shabaha nambari moja ambayo mlikuwa mnailenga mlikosa? Je, huo udikteta waliokuwa wanaupinga umekwisha? Rais Magufuli amelegeza kamba? Mazingira ya kufanya siasa yamekuwa na nafuu?

Huwezi kujisifu umefanikiwa ikiwa uliwaweka watu roho juu, huku wengine wakisubiri matokeo, mwisho mkatangaza kuahirisha. Walichokifanya Chadema kupitia Ukuta ni sawa na mbunge anayetoa hoja nzito mpaka misuli inamsimama kueleza makosa yaliyopo kwenye muswada, halafu mwishoni anaunga mkono.

Sasa Ukuta bado deni linadaiwa, Chadema wameamka na Kata Funua. Wanakwenda wapi? Wanachokitafauta ni kipi? Wanajitengenezea taswira ambayo inawafanya watu waseme; ndiyo zao hao.

Ushauri kwa pamoja

Watendaji wa Serikali ya Rais Magufuli wanatakiwa kupunguza kuonekana. Chadema, wanapaswa kujielekeza kwenye misingi ya kukijenga chama kiitikadi na misingi imara kwa wananchi. Oparesheni za mara kwa mara ni siasa ambazo hazina faida.

Katika Serikali ya Awamu ya Nne, Chadema walifanya oparesheni nyingi tu. Hata hivyo, ulipofika mwaka 2015, chama kikawa hakijiamini hata baada ya kuungana na Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD kuunda Ukawa, matokeo yake kikamtegemea zaidi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika tiketi ya urais, ambaye alikatwa CCM.

Oparesheni ni upepo tu, kama ambavyo kuna watu wengi walishasahau kama kulikuwa na oparesheni ya Ukuta, acha ile ya Sangara ambayo ilipita muda mrefu. Kwa kawaida upepo ukipita hufuata utulivu. Chama hakitakiwi kujijenga kwa misingi upepo, maana upepo haukai.

Rais Magufuli na timu yake wanapaswa kufanya kazi kisha kutoka na kufafanua mafanikio yao, siyo matamko, hayajengi hata kidogo. Rais Magufuli atafanya uamuzi mzuri kama atawaelekeza watu wake wajikite kwenye kazi badala ya kuendekeza maonesho.

CHANZO:MAANDISHI GENIUS
 
Nyuzi ndefu zinawashinda wengi.....
 
Back
Top Bottom