*Na Shilatu E.J*
Kinachoendelea sasa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimenifanya nikumbuke kisa cha Muhammad Saeed Al-Sahhaf.
Muhammad Saeed Al-Sahhaf alikuwa Mtu maarufu sana nchini Iraq na Duniani. Umaarufu wake ulitokana na uwezo wake mkubwa wa propaganda. Pia aliwahi kushika nafasi mbalimbali Serikalini.
Muhammad Saeed Al-Sahhaf aliwahi kuwa Waziri wa Habari kuanzia 2001 hadi May 2003 wakati Serikali ya Rais Saadam Hussein ikipinduliwa na Mmarekani. Hapa ndipo umaarufu wake ulipaa zaidi.
Wakati Wamarekani wakiwa kwenye hekaheka ya kumng'oa Saadam Hussein alikuwa akiibuka mbele ya Waandishi wa habari na kupiga propaganda zake ambazo zilikuwa zikiwapa matumaini Raia wa Iraq lakini ukweli hali ilikuwa mbaya.
Muhammad Saeed Al-Sahhaf aliwahi kuwaambia wana Iraq, "Iraq kuna bomu ambalo likipigwa linaenda chini kabisa, kila baada ya dakika mbili linajizalisha mabomu 10 na kujilipua hivyo msiwe na hofu na Wamarekani kwani tunajiweza".
Hakuishia hapo, akaibuka tena na kusema, "Wamarekani karibuni, makaburi yenu yatakuwa hapa hapa Iraq".
Wakati akiyasema haya kwa wana Iraq alikuwa akijua fika kuwa hali ya kiusalama ni mbaya sana nchini humo. Wamarekani wameingia nchini Iraq na wana Iraq wanauawa sana na Wamarekani lakini Muhammad Saeed Al-Sahhaf anawatia moyo kuwa hali ni shwari.
Wana Iraq kufumba na kufumbua wanakuta Saadam Hussein amekamatwa, Serikali imepinduliwa na nchi nzima imetapakaa damu kutokana na vifo vya wana Iraq.
Alichokuwa anakifanya Muhammad Saeed Al-Sahhaf kupitia propaganda hakina tofauti na kinachofanywa na wana Chadema kwa sasa.
Kila kukicha tunashuhudia Madiwani, Wabunge, Viongozi waandamizi wakihama Chadema na kujiunga CCM huku wana Chadema wakijipa moyo kwa propaganda nyepesi wakati wakijua fika hali ndani ya chama chao si shwari kabisa.
Hadharani wanajifariji na maneno ya kudanganyana. Mara utasikia, "Hao wamenunuliwa", Mara "hakuwa na mchango wowote ule, bora ameondoka"; Ama wanasema "Hizo ni takataka ziende tu". Na wengine ambao walikuwa viongozi wakubwa tu leo wanasema walikuwa hawawajui. Astaghafilullah!!
Hata yule waliokuwa wakideki lami ili apite na wakampachika jina la Rais wa Mioyo ambaye alienda kumuona Rais Magufuli nao wanasema bora aende CCM maana hakuna na mchango wowote. Leo hii sio muhimu tena kwao? Kisa amesifia utendaji na uchapakazi wa Rais Magufuli na Serikali yake. Lahaula!
Viongozi wanaondoka, Wanachama wanaondoka, Madiwani wanaondoka, Wabunge wanawakimbia lakini bado wao wanasema wataumia siku akiondoka Lissu, hizo takakata zingine wabebe tu. Chama kitaundwaje na Mtu mmoja?
Ni maneno ya kujifariji tu lakini wanajua fika kuwa chama ni Watu na Watu wenyewe ndio hao wanapukutika kila kukicha lakini wanaleta visa vya kutiana moyo kama alivyokuwa akifanya Muhammad Saeed Al-Sahhaf.
Ukweli wanaujua fika kuwa hali ni mbaya. Hawaaminiani, wanakimbiwa, wanasalitiwa. Kuliko kuendelea kujifariji na kuficha maradhi ni bora waamke, wajitathmini na kisha waamue kusema ukweli hadharani kuliko kuleta maneno ya kujifariji kama ya Muhammad Saeed Al-Sahhaf wakati ukweli wanateketea.
Kuna msemo unaosema, "Kama ukishindwa kupigana nao, jiunge nao"
*Na Shilatu E.J*
Januari 10, 2018