Chadema Bunda wapinduana

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,860
5,798
Tuesday, 27 September 2011 19:45

Christopher Maregesi, Bunda

MAPINDUZI ya uongozi yamefanyika ndani ya Chadema katika Jimbo la Bunda wilayani hapa, baada ya kundi moja kufanya uchaguzi wa viongozi wake watakaokiongoza kwa miaka mitano huku viongozi walioko madarakani wakiuelezea uchaguzi huo kuwa ni batili.

Jana, katika mkutano wa chama hicho jimboni humo, wajumbe waliwachagua viongozi wapya kwa nafasi za Mwenyekiti, Makamu wake, Katibu mkuu na msaidizi wake pamoja na wajumbe wa kamati tendaji watakaokiongoza chama hicho kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Waliochaguliwa ni Jonathan Matiko kwa nafasi ya Mwenyekiti, Julius Wassira kwa nafasi ya katibu ambapo Samuel Alfred alichaguliwa kuwa mweka hazina wa chama hicho jimboni humo huku Davis Robert akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa baraza la vijana la chama hicho (Bavicha) na Timothy Mburumatale akichaguliwa kuwa katibu mwenezi.

Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, Ferdinand Msilikale, wengine waliochaguliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi ni Godfrey Mkoba (mjumbe wa Bavicha jimboni), wajumbe wengine wa kamati tendaji ni Mohamed Tinga na Baby Mwasi huku Georges Miyawa, akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa baraza la wazee la chama hicho jimboni humo.

Wakati wajumbe hao wapatao 186 wakifanya uchaguzi huo, kwa upande wake uongozi uliko madarakani kupitia Katibu wake, Kaisiki Muyemba, ulisema kamwe hautambui mabadiliko hayo ya uongozi kwa vile mkutano huo uliitishwa na mwanachama wa chama hicho aliyesimamishwa uanachama tangu Mei mwaka huu kwa sababu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kasiki alisema Matiko aliyechaguliwa na wajumbe hao kuwa mwenyekiti alisimamishwa uanachama Mei mwaka huu na uongozi wa tawi lake la Miembeni la mjini hapa baada ya kumtuhumu kukihujumu chama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Huyo aliyeitisha mkutano huo na kisha kachaguliwa kuwa mwenyekiti siyo mwanachama wetu hai kwani alisimamishwa na uongozi wa tawi lake Mei mwaka huu kwa kosa la kukisaliti chama wakati wa uchaguzi uliopita.
Hivyo sisi kama viongozi hatuyatambui mabadiliko hayo ya uongozi,” alisema Kasiki.

Kulingana na katibu huyo mara baada kumsimamisha uanachama uongozi wa tawi lake ulitoa taarifa kwa uongozi wa wilaya ambapo kikao cha kamati tendaji kilichofanyika mapema mwezi huu kiliazimia kulipeleka suala hilo mbele ya mkutano mkuu wa jimbo utakaofanyika mapema mwezi ujao katika Kijiji cha Nyamuswa ili ulitolee uamuzi kama katiba inavyoelekeza.

Hata hivyo, kama kile kinachoonekana kutambua hali halisi ya mambo ilivyo ndani ya chama hicho katika hotuba yake mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti Matiko alitoa rai kwa wanachama wa Chadema jimboni humo kutoruhusu majungu aliyosema yanaweza kukiua chama badala yake washikamane kwa pamoja katika kukiimarisha chama jimboni humo ili kijiwekee mazingira mazuri ya ushindi kwa chaguzi zijazo.
 
Back
Top Bottom