CCM Zanzibar na viti vyao vya barafu

aleesha

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
775
1,117
Jiwe la barafu lililoivia baridi kali liko mithili ya chuma. Hufanana na chuma kwa uzito na hata ugumu wake. LikikuangIkia mguuni ni sawa tu na ulieangukiwa na kipande cha chuma kishindo chake na maumivu yake mguuni. Kitakachokufanya ujuwe kuwa kilichokuangukia mguuni sio chuma ni vile kuzizima kwake. Ugumu, uzito na umadhubuti huu wa jiwe la barafu hutegemea kushuka sana kwa kiwango cha joto pale liilipo. Joto kila likishuka, yaani likipungua ndio barafu nayo huwa madhubuti zaidi. Kinyume chake joto kila likipanda, yaani likiongezeka jiwe hili hupoteza haiba yake, nguvu yake na umadhubuti wake kwa kuyayuka ghafla. Na aibu yake sasa! Likiyayuka halipitii hata katika hatua ya mchanga na vumbi, ni maji moja kwa moja. Hayoooo!

Madaraka, nguvu, jeuri na kiburi cha watawala wa Zanzibar tokea kumalizika kwa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na hasa hivi sasa tunaweza kufananisha na jiwe la barafu lililoshiba baridi kali kama yale mawe ya barafu yaliyoko katika milima ya Alps kule Ulaya. Wameshiba jeuri na kiburi chao hicho kilichotegemea sana msingi mmoja tu wa kuugeuza uongo na kuutegemea uwe kama ndio ukweli kupitia maamuzi ya kinafiki ya CCM kupitia kinywa cha Jecha Salim Jecha alipotangaza eti uchaguzi wa tarehe 25 Octoba, 2015 umeharibika. Hivi sasa watawala wanaendeleza dhulma zao na maovu yao. Wanaendelea kupanga na kutekeleza vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhulumu na kuwabagua wazanzibari kama ilivyo kawaida yao. Hawana wasiwasi, wamejitanafasi katika viti vyao vya barafu wanatikisa miguu huku wakitoa maamuzi na amri za kifedhuli, kibabe na kidhalimu.

Ukiwauliza wana CCM kwani hamyajui yaliyotendeka? Kwani hamjui kwamba chama chenu kimevunja Katiba ya Nchi, sheria, matakwa na matashi ya raia, uhuru wao, haki zao, matmaini yao na hisia zao? Watakujibu yote tunajua na ni kweli tupu. Ukiwauliza tena kwani hamjui kwamba chama chenu kimevunja mikataba ya Demokraisa na Haki za Binadamu ya kiulimwengu na kuipaka kinyesi. Wanakujibu tunajua yote na ni kweli tupu. Ukiwauliza kwani hamjui kwamba chama chenu kimeiingiza Nchi katika mahusiano mabaya ya kidiplomasia na Nchi mbali mbali za ulimwengi na Jamii ya kimataifa kwau jumla, watakujibu tunajua yote na ni ukweli mtupu.

Sasa waulize sasa kwanini hawa CCM wanafanya hivi? Jeuri na kiburi hichi wanatoa wapi? Sikiliza majibu yao sasa. “Nchi hii ni ya kimapinduzi, tulipomfukuza mkoloni tulimwaga damu, hatuwezi kuwapa CUF Nchi kwa kura, CUF hata ishinde kwa kura zote na mara zote milele abadan haipewi hatamu za Nchi hii kuongoza. Dunia nayo haiwezi kutuingilia kwa lolote. Haya ni mambo ya ndani ya Nchi yetu. Hamuoni mmezunguka dunia nzima hakuna mlilolipata. Hakuna mabadiliko yeyote wala uchaguzi mpya mpaka 2020.”

Hayo ndio majibu pekee ya CCM wala hakuna mengine. Hakuna majibu ya utetezi wala ya kihoja. Ni hivo tu. Sasa cha kushangaza kuna wazanzibari wanayaogopa majibu hayo sana. Wanaamini hayo majibu ndio mwisho wa safari. Hakuna la kufanywa wala kuwa. Ndio waladhwaalina Amiina! Labda tujiulize maswali machache. Hivi Zanzibar na Tanzania jeuri hii ni kutokana na kuwa na nguvu kubwa za kijeshi duniani kujilinda na kuingiliwa na Nchi nyengine pale wafanyapo maamuzi yasiyokubalika? Hivi watawala wetu hawa madikteta wameiamini jeuri yao kwa kuwa tuna uchumi mkubwa duniani usiotetereka na usiotegemea misaada kutoka popote na hivyo Nchi yetu haishurutishwi wala haipokei mashinikizo ya kupinga dhuluma dhidi ya raia? Hivi jeuri hii ni kwa sababu Nchi yetu kwenda kinyume na mikataba ya kimataifa bila hofu ni kwa sababu Nchi yetu ni muhimu sana duniani kiasi ambacho haioni haja sana na kuheshimu mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia ya kiulimwengu? Ni kwamba Nchi yetu imekamilika kila idara haitetereki na haitetereshwi? Ina jeuri kama Korea Kaskazini, Urusi na China?

Jawabu hapana Nchi yetu haina jeuri na kiburi cha uchumi, kijeshi wala kidiplomasia. Ni masikini wa kutupwa na wanyonge wa kutupwa. Ubabe, udikteta na udhalimu wetu si kama wa Korea Kaskazini, China wa Urusi. Hivyo basi watawala wetu wasione kimya wakadhani ulimwengu hautachukua nafasi yake. Dunia haikurupuki kuchukua hatua zake dhidi ya Nchi ya madikteta na madhalimu. Wenzetu ni watu wa principles. Wanaongozwa na njia zao na taratibu zao za umakini mkubwa. Mwisho wa siku huhakikisha ni lazima Nchi ziwaheshimu raia, haki zao na matashi yao.

Wazaanzibari tunapaswa tuamini kuwa Dunia haipo kimya na katu haiwezi kukaa kimya dhidi ya madhalimu hawa wa haki za msingi za raia na mahodari wa uonevu. Viti walivyokalia watawala wetu wa Zanzibar ni vya barafu tu. Baridi imeshawadanganya kwa mwaka mmoja wakajiona wako juu ya madaraka madhubuti, yasiolegalega. Sasa joto limepanda na linazidi kupanda kwa kasi kubwa na viti vimeanza kuyayuka. Vinayayuka na muda si mrefu wataanguka chini.

Babu Ali sfari hiyoo imewadia! Unayooo!
 
Back
Top Bottom