BRAZIL, nchi inayoshika nafasi ya nne kwa uzalishaji wa pamba duniani, imedhamiria kusaidia kuliinua zao hilo Ukanda wa Afrika Mashariki ili liweze kuwa na tija kwa wakulima wake. Kwa kuanzia, imeelekeza nguvu katika nchi za Tanzania, Kenya na Burundi ambako imewekeza fedha na teknolojia katika `Mradi wa Pamba Victoria’ na nchi ya Brazil kwa zaidi ya dola za Marekani milioni 9 (Sh bilioni 21 za Kitanzania).
“Tupo hapa kuitumia teknolojia inayotumika Brazil katika uzalishaji wa pamba, lakini sasa katika ardhi na mazingira ya Tanzania na Afrika Mashariki,” alisema Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Antonio Cesar wakati wa mkutano wa kutathimini mafanikio na changamoto katika sekta ya pamba. Balozi Cesar alisema mradi huo ulizinduliwa mwaka 2016 na kuanza rasmi mwaka 2017.
Katika kikao hicho cha tathmini, Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa alikuwepo na kusisitiza kuwa, Tanzania licha ya kuwa moja ya nchi zinazozalisha pamba kwa wingi barani Afrika, ina uhaba wa viwanda vya kusindika zao hilo, jambo linalochangia kuyumbisha soko la wakulima.
Alisema pamba inalimwa katika mikoa 17 na wilaya 56, lakini uzalishaji si mzuri sana kutokana na kukosekana zana na mbinu za kisasa za kilimo hicho. Aidha, kupitia mpango huo ulioletwa na Wabrazili, alisema lengo ni kuzalisha mara tatu zaidi ya sasa kwa kila hekta, kwani Tanzania hekta moja huzalisha kilo 300 ikilinganishwa na kilo 4,200 zinazovunwa Brazil kwa kila hekta.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, alisema Brazil imeanzisha mradi huo katika Afrika Mashariki baada ya nchi hizo kulalamika katika Shirika la Biashara Duniani (WTO) kuwa nchi za Marekani Kusini zimekuwa zikiweka vikwazo vya kibiashara nchi nyingine zinazolima zao hilo. Naye mtati kutoka Taasisi ya Utati wa Kilimo Tanzania (TARI), Everina Lukonge, alisema wadau kadhaa wa Tanzania wameshapelekwa Brazil kujifunza zaidi juu ya kilimo cha kisasa cha pamba, lengo likiwa kukuza uzalishaji nchini.