Bomoabomoa inaumiza lakini maisha yetu ni lazima tuyaokoe

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,531
HAKUNA anayependa kuona mwingine anabomolewa nyumba yake wala kibanda chake cha biashara, ndio maana tukaitwa binadamu ikimaanisha kuwa tumeumbwa na huruma.
Ukiona kuna mmoja au kundi linafurahia mwingine akikutwa na majanga basi ujue kuna walakini au sababu zinazomfanya anayefurahi kufanya hivyo. Lakini, hayo yote ni mambo yanayotokea katika maisha kwamba binadamu hatufanani.
Binafsi ninaumia kuona watu wakibomolewa nyumba zao hasa, wale waliojenga kwa kutumia fedha za mikopo na zilizopatikana kwa shida. Ninafahamu kuwa wapo waliotajirika kwa kuwauzia wengine maeneo yaliyo katika sehemu zisizoruhusiwa kujengwa makazi ya kudumu, huku wakijua kuwa wanaonunua hawatadumu nayo, kwa sababu kama hizo za kutakiwa na Serikali waondoke kuepuka balaa la mafuriko wakati wa mvua.
Pia, ninaelewa wako waliofanya ujanja kuwadanganya wenzao wajenge nyumba za kudumu ili wachume fedha kutokana na utaalamu wa ufundi wao. Watu hao, hata kama walijenga nyumba hizo vizuri kiasi gani, wamekiuka maadili ya kazi yao kwa sababu wameangalia na kuacha zijengwe mahali pasipostahili.
Lakini, yote hayo kama nilivyoeleza awali, ni matokeo ya ujanja wa mtu kutafuta kuishi. Kwa wale viongozi wa Serikali za Mitaa waliohusika kwa njia moja au nyingine kuhakikisha uuzaji na ununuzi wa maeneo hatarishi, kama vile bonde la Mto Msimbazi, Dar es Salaam unafanikiwa, nao wamechangia kutia wananchi wa mabondeni hasara na kuhatarisha maisha yao, hivyo, wanapaswa kulaumiwa.
Hata hivyo, kwa wakati kama huu ambapo tunaelekea kuanza kuona mvua kubwa za El nino zikinyesha, lawama na masikitiko hayana nafasi tena na badala yake, kinachotakiwa ni kufanya haraka iwezekanavyo kupisha maeneo hayo ili zitakapoanza kunyesha balaa la mafuriko lipitie mbali bila kuondoka na uhai wa mtu.
Ni kweli bomoabomoa inaumiza sana, lakini, uhai wa mtu unathamani zaidi kuliko nyumba au kibanda cha biashara ambacho kwa hali ya kawaida ya binadamu, kinaweza kujengwa upya ikiwa mhusika aliyekipoteza atawezeshwa.
Uwezeshaji ninaouzungumzia si lazima ufanywe na Serikali na wala si shuruti iwe fedha, bali namna itakayowawezesha wanaobomolewa, hususan ambao hawakufanya makusudi kujenga mabondeni, kupata hifadhi yenye staha, wakati wakitafakari pakwenda kuanzisha makazi mapya.
Msaada wa aina hiyo unaweza kutolewa na yeyote, awe mtu binafsi, shirika na hata taasisi za dini, fedha, vyuo, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia. Awali nilizungumza kuhusu waliojenga mabondeni kwa bahati mbaya. Nilimaanisha kuwa wapo waliofanya hivyo kwa makusudi wakijua kuwa si sahihi.
Hao ni wale wanaoiwekea Serikali mtego kwa fikra kuwa itawalipa ikitaka waondoke na kubomoa nyumba zao. Wanaorubuniwa na kujikuta wakijenga pasipofaa, bila kuujua ukweli kuhusu asili na athari za eneo husika ni pamoja na wale ambao baadhi ya ‘viongozi wa Serikali za Mitaa’ wanawahakikishia usalama na uhalali wa mahali hapo kwa kuwapa ushahidi wa mihuri kwenye hati zao za kuuziana maeneo.
Wanawafanyia hivyo wakijua wanawatumbukiza pasipostahili ili wapoteze na wao wapate kwa kufanikisha uuzaji. Lakini, kwa sababu hayo yanakuwa yamekwishatokea na Serikali kwa upande wake inatakiwa itekeleze wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao unalindwa dhidi ya mafuriko yanayoelezwa kuweza kutokea wakati wowote mwezi huu hadi Machi, wananchi lazima tukubali kutii na kuhamia kwenye usalama zaidi.
Tena inabidi kuchukua tahadhari dhidi ya viongozi wetu wa kisiasa wanaotumia maumivu mlionayo sasa kuwadanganya mambo mengi ili muione Serikali kuwa haifanyi sahihi kuwalazimisha kuondoka.
Wapo wanaoeleza maneno mengi yanayowapa moyo kuwa mna haki zote kuendelea kukaa mabondeni, hao ni lazima muwakataze wasiendelee kuwapotezea muda kwa sababu mvua ndio hizo zinabisha hodi.
Kwa bahati mbaya, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo Umoja wa Mataifa (UN) umetahadharisha kuwa itakumbwa na mafuriko makubwa katika miezi hiyo. Tuchukue tahadhari tusalimike
 
Back
Top Bottom