Mentor
JF-Expert Member
- Oct 14, 2008
- 20,328
- 23,909
BIN ADAM: UNAWEZA KUFANYA HILI?
Siku moja nikiwa kwenye zamu eneo la dharura wakati wa mafunzo kwa vitendo ‘residency’ niligundua jambo.
Alikuwepo mtoto mmoja, umri wake kama miaka kumi (10) hivi. Alikuwa akitembea tu kwenye korido za hospitali karibu na chumba nilichokuwepo. Alifanya vile siku nzima na ilipofika jioni nilihisi kuna tatizo hivyo nilimuita nimuulize kufahamu alikuwa na tatizo gani.
Nilimfuata baada ya yeye kusita kuja na nikamuuliza kama kuna msaada wowote alihitaji. Hakunijibu kwa haraka ila niligundua alikuwa na hofu kubwa machoni. Baada ya muda mrefu wa kumbembeleza ajibu maswali yangu na yeye kujitahidi kukwepa hasa kwa kukaa kimya, aliniomba kama tungeweza kuongea kwa faragha.
Nilimpeleka kwenye wodi ambayo haikuwa ikitumika ndipo aliponyanyua fulana yake na kunionesha kovu kifuani kwake ambalo nilipoliona nilifahamu tu lilitokana na upasuaji wa kutibu moyo ‘heart surgery’.
Aliniambia alikuwa akimtafuta daktari aliyemfanyia upasuaji ule alipokuwa mtoto na akaniuliza ni wapi angeweza kumpata.
Nilimfahamu daktari aliyemfanyia upasuaji ule ila nilitaka kufahamu hasa ni kwa nini alishinda hospitali pale siku nzima akimtafuta daktari huyo.
Kumbe, daktari yule aliyemfanyia upasuaji, si kwamba tu alimfanyia upasuaji bure, lakini pia alilipia gharama nyingine zote za hospitali kwa kuwa wazazi wake hawakuwa na bima ya aina yoyote ile. Zaidi sana, alikuwa akiwatembelea nyumbani kwao kila mara baada ya upasuaji ule akawalipia kodi ya pango, akawanunulia chakula na nguo; na hili lilifanyika kwa miaka mingi baada ya upasuaji ule.
Lakini, kwa mwaka na nusu uliopita hakufika nyumbani kwao na mama yake hakuwa na fedha za kulipa kodi ya pango. Hiyo ndiyo sababu alikuja hospitalini pale akimtafuta daktari huyo.
Jambo ambalo mtoto yule hakulifahamu ni kuwa daktari aliyekuwa akimuulizia alifariki mwaka mmoja na nusu uliopita.. Alilia hadi kuzimia nilipompa taarifa zile.
Kesho yake niliwaeleza wenzangu juu ya mkasa ule. Kumbe kwa mwaka ule mmoja na nusu tangu kifo cha daktari yule wagonjwa wengi walikuwa wakija hospitalini pale karibia kila siku wakimuulizia. Sote hatukuwa tukifahamu kuwa, sio tu kwamba alikuwa akilipia gharama za upasuaji aliokuwa akiufanya (kwa wale wasioweza kumudu gharama husika), lakini pia aliifanya kama dira yake kuwasaidia familia zao kwa njia yoyote ile awezayo. Mkewe na wanawe pia hawakufahamu hilo.
Daktari huyo hakuwahi kumwambia mtu alichokuwa akikifanya kwa wagonjwa wake.
Jina lake ni Muhammad Fayez, Brigedia Jenerali katika hospitali ya ‘Royal Medical Services’, hospitali ya Jeshi la Jordan. Mshauri Mwelekezi wa magonjwa ya moyo na mkuu wa kitengo cha upasuaji wa moyo wakati akifariki akiwa na miaka 52 kwa shambulio la moyo.
Siku yake ilikuwa ikianza saa mbili kamili asubuhi na kuisha saa tano za usiku. Mpole, mwerevu, wa kujitolea, aliyependa kufanya mambo yake nyuma ya pazia, bila ya kutafuta umaarufu au sifa. Binadamu wa kweli.
Kisa hiki nimekitafsiri kutoka kwenye forum ya QUORA: What do doctors do when a patient can't pay for life-saving surgery? - Quora.
Kutokana na kuwa ni kisa cha kweli kimenivutia na kunigusa nikajiuliza, hapa kwetu Bongo, tunao watu wa hivi? Kwenye fani yoyote, tunao watu wanaoweza kujitoa namna hii kwa wenzao kama daktari Fayez?
Wasalaam wapendwa,
Mentor.