Biashara isiyokuwa na ubunifu kazima ianguke

LH XiV

JF-Expert Member
Nov 27, 2016
346
350
By Charles Nduku
Wajasiriamali wengi wamekuwa wakidhani ubunifu ni kada ya watu fulani wenye elimu kubwa ya chuo kikuu ambao ndiyo hasa wanatakiwa kuuishi.
Wanasahau, neno ubunifu linasimama katika maana ya kufanya vitu nje ya mazoea na utaratibu wa kujirudia. Ukijua namna ya kufanya kitu kilekile kwa njia tofauti tayari wewe tunakuita mbunifu wenye kuiletea tija biashara yako.
Ubunifu ni sahani muhimu katika biashara kutokana na manufaa yake, mfano mdogo wa kibunifu ni unapokuwa sokoni ambako wote mnauza mchicha unaofanana lakini mmoja kati yenu akianza kuuchambua na kuuosha ukawa tayari kupikwa na mteja atakayeununua atakuwa mbunifu.
Ubunifu huo utakuwa umeuongezea mchicha wake thamani katika biashara yake hivyo kupanua soko lake. Ni suala muhimu wajasiriamali kuelewa haja ya ubunifu kwenye shughuli zao ili kujitofautisha sokoni.
Pamoja na mambo mengine, kabla hajanunua bidhaa au huduma husika, mteja anatafuta kitu cha tofauti na chenye urahisi suala ambalo wafanyabiashara wanatakiwa kulifahamu na kuliishi kwenye mioyo yao.
Ukiweza kufanya mabadiliko kidogo ya bidhaa au huduma yako, wateja wataongezeka kwako maradufu hivyo kukuza biashara kwa muda mfupi. Ubunifu humfanya mteja kuhisi alichokitoa hakilingani thamani na kile alichokipokea.
Ukifanywa kwa namna inayotakiwa, ubunifu utawezesha kumfanya mteja ajihisi katika hali hiyo yaani kuona alichokitoa hakilingani thamani na alichopokea. Kwa maana nyingine muda wote atahisi ameuziwa kwa bei ndogo kuliko ilivyotakiwa kugharimu.
Wakiwa katika hatua hii, wateja watakuwa mabalozi wazuri wa kutangaza bidhaa au huduma za biashara yako jambo litakalokusaidia kukuza na kuimarisha mradi wako.
Wateja wanavutiwa na huduma zenye utofauti kutokana na ubunifu unaofanywa na mmiliki wa biashara au wasimamizi wake. Itapendeza endapo kila biashara itakuwa na kikosi cha ubunifu ili kuendelea kujitofautisha sokoni.
Tunahitaji kutumia muda mwingi kufikiri, kubuni utofauti wa nembo yako sokoni badala ya kutumia fedha nyingi kukuza biashara zetu. Ubunifu huleta ushindi mkubwa kila leo endapo mjasiriamali atafahamu namna sahihi ya kuutumia.
Ubunifu unaleta uhusiano wa karibu baina ya mteja na bidhaa au huduma ambao huimarika pale mteja anapotumia huduma na bidhaa husika mara kwa mara hivyo kuifanya kama sehemu ya maisha yake. Wapo wateja ambao wasiposoma gazeti la Mwananchi, kwa mfano, hawajisikii vizuri kutokana na kulihusudu kutokana na taarifa zake.
Ni jukumu la mzalishaji kufahamu sababu ya wateja kununua bidhaa au huduma yake na kuacha za wengine waliopo sokoni na kujitahidi kuhakikisha anaongeza ubora ili kutowapoteza.
Biashara, bidhaa na huduma bila kuchanganywa na ubunifu thamani yake itabaki kuwa chini na kutomsaidia mmiliki wake kujiimarisha kiuchumi na kuinuka kutoka hatua moja kwenda nyingine.
Wafanyabiashara wote wenye nia ya kufika mbali lazima wajitahidi kuwa wabunifu kila siku.
 
Back
Top Bottom