Punguzo hilo la bei ni sawa na kutoka Sh. 25 kwa lita mpaka karibu ya bure - Sh. 1.60.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wakazi wa Sengerema walionyesha kufurahia unafuu huo na kuishukuru serikali kwa mradi huo uliogharimu Sh. bilioni 22 na ambao utawanufaisha wakazi zaidi ya 138,000.
Aidha, Mabula Sakambule na Philemon Makelele walisema mradi huo uliozinduliwa na Rais Magufuli Julai 4 utakuwa mkombozi kwao kiuchumi na kijamii.
Makelele aliyedai kuishi Sengerema kwa miaka 34, alisema kwa kipindi chote hicho kero ya maji ilikuwa kikwazo cha kiuchumi na kwamba baadhi ya huduma za kijamii zilidorora, ikiwamo usafi wa soko.
Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Antony Sanga alisema changamoto zote zilizopo zitakamilishwa wakati wa kipindi hiki kinachoendelea cha maboresho.
Alisema maboresho hayo yatahusu pia kubadilisha baadhi ya miundombinu, ikiwamo mabomba na kuwa wakazi wote waliomo katika mradi huo watafikiwa na huduma hiyo baada ya maboresho kufanyika.
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) ameishukuru serikali kwa kumaliza kero hiyo na kuahidi kushirikiana na jamii kulinda miundombinu ya mradi huo. Fedha za mradi huo zimetoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na wadau wengine, ikiwamo Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na Serikali.Mradi huo unatarajiwa kukidhi mahitaji ya mji wa Sengerema hadi mwaka 2030.
Chanzo: Nipashe