Askofu Mwanamapinduzi atuma salamu za mwaka mpya kwa Watanzania

Askofu Mwanamapinduzi atuma salamu za mwaka mpya kwa Watanzania

Pfizer

JF-Expert Member
Joined
Mar 25, 2021
Posts
726
Reaction score
953
PART 1.

Ndugu zangu Watanzania!
Amani ya Bwana na iwe nanyi!
IMG-20260101-WA0047.jpg

Ashukuriwe Mungu kwa kutuwezesha kuuona mwaka mpy kwani siyo jambo rahisi kwetu Sisi watanzania baada ya kushuhudia maelfu ya watu wakiuawa , wengine kutekwa na hawajulikani walipo, na wengine wako magerezani. sio kwamba Sisi tuliouona mwaka kuwa tumejilinda wenyewe, wala kwamba ni wema sana kuliko wengine, la hasha! Ni ni neema zake Mwenyezi Mungu tu.

Ndugu zangu Watanzania,mimi Askofu nikiwa huku Nchi ya Ugeni kwa ukimbizi ninatoa salamu hizi nikiwa nimejawa na simanzi nzito sana juu ya Taifa letu la Tanzania ambalo kwa nyakati hizi limepoteza haki, Amani na utulivu kwa watu wa tabaka la chini yaani Wananchi wa kawaida. Na hii ni kutokana na kushamiri kwa matukio mabaya yanayoharibu taswira ya Taifa letu, ikiwa ni pamoja na uvunjwaji wa haki za Binadamu kama vile utekaji na mauaji ya Raia wasio na hatia.

Ndugu zangu Watanzania hususani Tanganyika,Taifa letu limekuwa kama Nchi ya ukimbizi kwa sasa kwani licha ya kushamiri kwa matukio mengi ya utekaji na mauaji ya wakosoaji wa Serikali, lakini pia Nchi yetu tumepoteza kabisa sifa ya kuitwa Nchi ya Kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi kama ilivyoasisiwa mwaka 1992, kwani siasa za Nchi yetu kwa sasa zinazomilikiwa na Chama kimoja, hasa CCM mtandao, huku Chama kikuu cha upinzani kikizuiliwa kufanya siasa kwa namna yoyote ile na viongozi wake kuwindwa na kutajwa kama magaidi na wahaini.

Ndugu Watanzania, mtakumbuka ya kwamba mwaka 2025 Kanisa letu la Ufufuo na Uzima ambalo mimi ni Naibu katibu mkuu wake tulifutiwa usajili kihuni na kwa uonevu makubwa pasipo kuambiwa sababu za msingi. Hii ni kutokana na msimamo wa Askofu wetu Mkuu Josephat Gwajima kukemea matukio ya utekaji hadharani ambayo yanahisiwa kufanywa na watu wenye jina la "Wasiojulikana" wanaoonekana kuwa na nguvu kuliko vyombo vya ulinzi na usalama.

Mamilioni ya waumini wetu walikosa haki yao ya msingi ya Uhuru wa Kuabudu, katika kudai haki hiyo, watu wetu zaidi ya 160 waliwekwa rumande, wengine kuvunjwa mikono, miguu na viuno na Mali za kanisa kuporwa na jeshi la Polisi. Ni mwaka ambao kwa Mara ya kwanza, watu wamezuiliwa kwenda misikitini na makanisani kumwabundu Mwenyezi Mungu kwa sababu ya lockdown wakati wa uchaguzi. Jambo ambalo halitasahaulika kwa waislamu na wakristo kwenye historia zao za Kuabudu na wala Mwenyezi Mungu hatawasamehe waliofanya hayo.

Mwaka 2025 ,matukio mengi ya utekaji yalishamiri Sana kwani nilipoteza Rafiki yangu Mdude Nyagali ambaye alitekwa Mwezi Mei akiwa nyumbani kwake kule jijini Mbeya mbele ya Mkewe na watoto wake na hivyo mpaka leo hajaweza kupatikana,Ndugu yetu Humphrey Polepole alitekwa Dar es Salaam,Ndugu yetu Amani Manengelo na wengineo wengi ambao walikuwa mstari wa mbele katika Kupigania mabadiliko ya kweli katika Taifa.

Ama hakika machozi yananidondoka kila nikiwakumhmbuka hawa Ndugu zetu hakika Mwenyezi Mungu hatakosa kulipa kisasi kwa waliohusika.

Ndugu zangu,sote tunatambua ya kwamba,mwaka 2025 ni mwaka ambao tulipatwa na msiba mzito kama Taifa kutokana na kuondokewa na Ndugu zetu maelfu waliokuwa wakitumia haki yao ya kikatiba kuandamana kupinga uchaguzi mkuu na hivyo kupigwa risasi za moto na vyombo vya usalama kuanzia Oktoba 29 mpaka 31 katika maeneo mbalimbali Nchini Tanzania na hata wengine ambao hawakuwa katika maandamano hayo!

Lakini jambo la kustaajabu ni kwamba mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa juu ya mauaji hayo na wala hayupo aliyewajibishwa kwa vitendo vile vya unyama.

Ndugu zangu, Nchi yetu inaongozwa na mfumo wa Kidikteta chini ya Utawala wa mama Samia ambaye alijipitisha na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pasipo ridhaa ya Wananchi wa Tanzania na ndiyo maana wanatuona Watanganyika ni kama ngoma ya kuchezea na kuimba mapambio yao ya amani kila kukicha ikiwa ni pamoja na kuwatumia machawa kuhalalisha uchafu wao walioufanya. Mfano kushambulia Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) kisa walikemea utekaji na wizi wa kura,lakini pia kutuma hao machawa waje kumjibu na kumchafua Askofu Gwajima ambaye naye alikemea utekaji unaofanyika hapa Nchini!

Kundi hilo la Machawa ambao wengine ni viongozi wa Dini wameonekana kuwa mbele na kuchafua taswira kwa Waumini wao wanaoamini katika haki kwani madai ya viongozi hawa TEC,Askofu Gwajima na viongozi wa Kiislamu kama Sheikh Ponda na Masheikh wengineo ndiyo madai ya Wananchi.

Ndugu zangu Watanzania,kama nilivyowajulisha hapo mwezi Agosti mimi Askofu Mwanamapinduzi nililazimika kukimbilia uhamishoni katika Nchi ya ugeni kutokana na usalama wangu kuwa hatarini hali iliyopelekewa na misimamo yangu ya kupigania haki katika Taifa langu. Hapo ndipo walipoanza kunitafuta na nilipoamua kuchukua hatua ya kukimbia Nchi ili kuiokoa roho yangu na nisijisalimishe mikononi mwa watesi wetu kwani ndiyo njia niliyoiona ni sahihi kwangu ili nirudi kupigana tena kesho kwa mara nyingine.

Inaendelea Part 2......

ASKOFU MWANAMAPINDUZI,
1/1/2025
 
Mungu wa mbinguni na azidi kukutunza huko huko ulipo
 
SALAAM ZA MWAKA MPYA (2026) KUTOKA KWA ASKOFU MWANAMAPINDUZI KWA WATANZANIA AKIWA UKIMBIZINI .*
IMG-20260102-WA0045.jpg

Ndugu zangu Watanzania!
Mvua ya Haki na Amani toka kwa Mungu wa Mbinguni iwe nanyi!

Ashukuriwe Mungu kwa kutuwezesha kuuona mwaka mpya. Kwani siyo jambo rahisi kwetu sisi Watanzania tuliobaki. Maana tumeshuhudia maelfu ya wenzetu wakiuawa, kutekwa na hawajulikani walipo huko wengine wako magerezani. Sio kwamba sisi tuliouona mwaka mpya kuwa tumejilinda wenyewe, wala kwamba ni wema sana kuliko wengine, la hasha! Ni ni neema zake Mwenyezi Mungu tu!

Ndugu zangu Watanzania! Mimi Askofu Mwanamapinduzi nikiwa huku nchi ya ugenini kama mkimbizi ninatoa salamu hizi nikiwa nimejawa na simanzi nzito sana. Simanzi juu ya taifa letu la Tanzania ambalo kwa nyakati hizi limepoteza haki, Amani na utulivu kwa watu wa tabaka la chini yaani wananchi wa kawaida. Na hii ni kutokana na kushamiri kwa matukio mabaya yanayoharibu taswira ya taifa letu, ikiwa ni pamoja na uvunjwaji wa haki za binadamu kama vile utekaji na mauaji ya raia wasio na hatia.

Ndugu zangu Watanzania hususani Watanganyika! Taifa letu limekuwa taifa lenye usalama mdogo kwa raia wake. Hii inatokana na kushamiri kwa matukio mengi ya utekaji na mauaji kwa wakosoaji wa serikali. Lakini pia nchi yetu imepoteza kabisa sifa ya kuitwa nchi ya kidemokrasia; inayofuata mfumo wa vyama vingi kama ulivyoasisiwa mwaka 1992. Kwa kweli siasa za nchi yetu kwa sasa zinazomilikiwa na chama kimoja hasa CCM mtandao. Hali iko hivyo huku vyama vingine hususani chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) vikizuiliwa kufanya siasa kwa namna yoyote ile. Hali hiyo imepelekea viongozi wengi wa upinzani kuwindwa na kupewa kesi za uongo kama magaidi na wahaini.

Ndugu Watanzania! Mtakumbuka ya kwamba mwaka 2025 kanisa letu la Ufufuo na Uzima ambalo mimi ni naibu katibu mkuu wake tulifutiwa usajili kihuni na kwa uonevu mkubwa pasipo kuambiwa sababu za msingi. Hii ni kutokana na msimamo wa Askofu wetu mkuu Dr.Josephat Gwajima kukemea matukio ya utekaji hadharani ambayo yanafanywa na watu wenye jina la "Wasiojulikana". Hawa wasiojulikana, wanachukuliwa kama ni kundi la wahalifu wenye nguvu kuliko vyombo vya ulinzi na usalama. Kutokana na hatua ya Askofu wetu Mkuu kukemea utekaji na Kisha kanisa kufungwa, mamilioni ya waumini wetu walikosa haki yao ya msingi ya uhuru wa kuabudu. Katika kudai haki hiyo, watu wetu zaidi ya 160 waliwekwa rumande, wengine kuvunjwa mikono, miguu na viuno na mali za kanisa kuporwa na Jeshi la Polisi. Ni mwaka ambao kwa mara ya kwanza, watu wamezuiliwa kwenda Misikitini na Makanisani kumwabundu Mwenyezi Mungu kwa sababu ya lockdown wakati wa mwaka wa uchaguzi mkuu. Jambo ambalo halitasahaulika kwa Waislamu na Wakristo kwenye historia zao za kunyimwa uhuru wa kuabudu na wala Mwenyezi Mungu hatawasamehe waliofanya hivyo.

Ndugu Watanzania! Mwaka 2025,matukio mengi ya utekaji yalishamiri sana. Nipo na majonzi makubwa kwani nilipoteza rafiki yangu Mdude Nyagali ambaye alitekwa mwezi Mei akiwa nyumbani kwake kule jijini Mbeya mbele ya mkewe na watoto wake. Mpaka hivi leo hajaweza kupatikana. Pia ndugu yetu Humphrey Polepole alitekwa Dar es Salaam,ndugu yetu Amani Manengelo na wengineo wengi ambao walikuwa mstari wa mbele katika kupigania mabadiliko ya kweli katika taifa. Ama hakika machozi yananidondoka kila nikiwakumbuka hawa ndugu zetu. Hakika ninaamini kwamba Mwenyezi Mungu atalipa kisasi kwa waliohusika.

Ndugu zangu Watanzania! Sote tunatambua ya kwamba, mwaka 2025 ni mwaka ambao tulipatwa na msiba mzito kama Taifa. Msiba mzito kutokana na kuondokewa na ndugu zetu maelfu waliokuwa wakitumia haki yao ya kikatiba kuandamana kupinga uchaguzi mkuu lakini wakapigwa risasi za moto na vyombo vya usalama kuanzia Oktoba 29 mpaka 3. Hali hii ilitokea katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Vilevile wapo wengine ambao hawakuwa katika maandamano hayo lakini walipigwa risasi.Jambo la kustaajabisha na kushangaza ni kwamba mpaka hivi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa juu ya mauaji hayo na wala hayupo aliyewajibishwa kwa vitendo vile vya unyama.

Ndugu zangu! Nchi yetu inaongozwa na mfumo wa kidikteta chini ya utawala wa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye alijipitisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pasipo ridhaa ya Wananchi wa Tanzania hususani Watanganyika. Kitendo hicho kinawafanya watawala haramu kuwaona Watanganyika kama ni kama ngoma ya kuchezea na kuimba mapambio; wakiwatumia machawa wao hata kuhalalisha uchafu walioufanya kipindi cha mwaka wa uchaguzi mkuu. Mfano kushambulia Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) kisa walikemea utekaji na wizi wa kura. Pia wamewatumia hao machawa wao waje kumjibu na kumchafua Askofu Dr. Josephat Gwajima ambaye naye alikemea utekaji unaofanyika hapa nchini.Kundi hilo la Machawa ambao wengine ni viongozi wa Dini wameonekana kuwa mstari wa mbele; wakichafua taswira njema hawa viongozi mbele ya waumini wao wanaoamini katika haki. Ni ukweli usiopingika kwamba, madai ya viongozi hawa waTEC, Askofu Dr. Josephat Gwajima na viongozi wa Kiislamu kama Sheikh Ponda na Masheikh wengineo ndiyo madai ya Wananchi.

Ndugu Watanzania! Ni jambo la kushangaza sana kwamba wapo mpaka viongozi wa dini ambao ni wadau muhimu kabisa katika taifa lolote ambao wamesahau wajibu wao . Tulishuhudia mwaka 2025 miongoni mwao wakilazimika kutotetea haki zaa Wananchi bali kulinda uovu wa watawala. Hakika wamesahau wajibu wao mkubwa wa kukemea maovu na kuwapa faraja sehemu kubwa waumini wao ambao ni wananchi wa kawaida. Hili jambo ni baya mno kwa Taifa. Ni maombi yangu 2026 likome!

Ndugu zangu Watanzania! Kama nilivyowajulisha hapo mwezi Agosti, mimi Askofu Mwanamapinduzi nililazimika kukimbilia uhamishoni katika nchi ya ugeni kutokana na usalama wangu kuwa hatarini. Hali hiyo ilitokana na misimamo yangu ya kupigania haki katika Taifa langu. Walipoanza kunitafuta, niliamua kuchukua hatua ya kukimbia nchi ili kuiokoa roho yangu ili nisijisalimishe mikononi mwa watesi wangu. Hiyo ndiyo njia niliyoiona ni sahihi zaidi kwangu kama mkakati wa kurudi kupigana kwa mara nyingine na wakati mwingine tena.

Ndugu zangu Watanzania! Si mimi peke yangu tu ninayekumbwa na kadhia mbalimbali kutoka kwa utawala dhalimu.Tuko wengi tu ambao bado tupo hai. Maana Nchi yetu kwa sasa, yeyote anayeonekana kuwa kinyume na kukosoa utawala au kutetea haki za Wananchi anageuka adui mkubwa wa Watawala hata kama hajavunja sheria yoyote ya nchi.Anaweza kutengenezewa kesi mbaya na kuwindwa kutekwa na kuuwawa. Mfano mzuri ni Tundu Lissu, anasota jela bila kosa lolote, Askofu Gwajima ambaye kanisa lake lilifutwa kihuni. Padri C. Kitima ambaye alitaka kuuawa akiwa ofisini kwake, Askofu Mwamakula, Askofu Kabigumila, Mch. Mbarikiwa Mwakipesile, Mch. Abiudi Misholi, baadhi ya Masheikh wa Kiislam kama Sheikh Ponda, Maaskofu wa TEC, Mzee Joseph Warioba,John Heche, John Mnyika. Na wanaharakati wengi kama vile Maria Sarungi, Mange Kimambi, G. Malisa, Hilda Newton,Twaha Mwaipaya, Rose Mayemba na wote waliosimama upande wa wananchi kudai haki zao.

Ndugu zangu Watanzania! Hali isiyo ya haki nchini, inayotendwa na viongozi dhalimu, ipo kinyume kabisa na maandiko matakatifu ya Biblia. Viongozi wengi nchini hawafanani na Yesu wa Nazareth ambaye alienda kuwaganga na kuwaponya watu. Viongozi wetu hawapo kuganga na kuponya watu.Mfano wa maandiko hayo yanapatikana katika Luka 4:16-17 na Isaya 61:1-2.

Mistari ya maandiko matakatifu katika Luka 4:16-17 yanasomeka kuwa Yesu alikwenda Nazareti mahali alipolelewa.Aliingia katika sinagogi siku ya sabato kama ilivyokuwa desturi yake. Alisimama ili asome maandiko. Yesu alipewa Kitabu cha Nabii Isaya. Alipokifunua kitabu hicho alipata mahali palipoandikwa maneno yanayapatikana katika
Isaya 61:1-2: " Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao.

Maneno haya Yesu aliyasoma mwanzoni mwa huduma yake aliyoifanya kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Alitambulisha kazi aliyotumwa kuifanya kwa watu aliowakuta wamejaa habari mbaya, mioyo yao imevunjika, wametekwa na kufungwa. Watu walitaka Mungu alipe kisasi na kuwapa faraja kama ilivyo sasa kwa Wananchi wa Tanzania.

Kutokana na maandiko hayo, tunaona kuwa Yesu akiwa Nazareth alifanya mambo ambayo sisi kama Watanzania hatuyashuhudii kama ifuatayo:

Jambo la kwanza, Yesu akiwa Nazareth alitangaza habari njema kwa watu wote. Tofauti na huko Nazareth, mwaka 2025 Watanzania hatukupata habari njema kwani kila kukicha tulikuwa tunapokea habari mbaya tu. Habari mbaya hususani mauaji, utekaji, ukandamizwaji wa haki na mambo yafananayo na hayo. Tukiachana na matukio ya Mwaka 2025, kama Mungu aishivyo, mimi kama Askofu Mwanamapinduzi, natamka kuwa, kwa nchi ya Tanzania kuna habari njema zinazokuja ili wananchi wapate faraja tena kama huko Nazareth.

Jambo la pili, Yesu akiwa Nazareth alitangaza kuwaganga waliovunjika mioyo. Bahati mbaya sana huku Tanzania, mwaka 2025 Watanzania wengi walivunjika mioyo kushuhudia mauaji ya ndugu zao maelfu, na wengine kukata tamaa kutokana na mambo yaliyowatokea. Wengi pia waliishi kwa kuhofia kutekwa na kuuawa; waliishi maisha magumu yasiyo na matumaini ya kupata nafuu yoyote hasa kutokana na mrundikano wa Kodi na ukosefu wa ajira hususani kwa vijana (GenZ- Tanzania)

Mimi Askofu Mwanamapinduzi natamka kuwa Mwaka 2026 ni mwaka wa kugangwa moyo. Watagangwa mioyoni wale wote waliokata tamaa kwa kutishwa na giza la kutekwa na kuuawa pamoja na mambo mengine yafananayo na hayo. Kwani Mungu anakwenda kutenda jambo jipya!

Jambo la tatu, huko Nazareth Yesu alitangaza uhuru kwa waliotekwa. Tofauti na huko Nazareth, Mwaka 2025 hakukuwa na uhuru kwani watu walioonekana tofauti na watawala walitekwa na kupelekwa sehemu zisizojulikana. Watanzania wengi hususani Watanganyika walipoteza uhuru wao wa kuishi kama binadamu. Hakika walikuwa mateka katika nchi yao.
Mimi Askofu Mwanamapinduzi natangaza kuwa kwa mwaka 2026 kama Mungu aishivyo, ataleta uhuru kwa wote.

Jambo la nne, huko Nazareth Yesu alitangaza kuwafungua waliofungwa magerezani.Katika hali ya kushangaza, huku Tanzania, mwaka 2025 watu wengi wakiwemo viongozi na wanaodai haki walifungwa magerezani kwa kesi za kubumbabumba. Kesi za uhaini zilikuwa nyingi kuliko wakati wowote uliopita katika nchi yetu. Lengo kuu la kesi za uhaini lilikuwa ni watu wafungwe na kukosa dhamana.Mimi Askofu Mwanamapinduzi naapa kuwa mwaka 2026 wote waliofungwa magerezani kwa makosa ya uongo wanaenda kufunguliwa kwa Neema ya Mungu.

Ndugu Watanzania! mwaka 2025 Tanzania tumeshuhudia mambo mengi yafuatavyo:

▪︎ Watawala wanaongoza kama mabepari tofauti na watawaliwa wanaosisitiza ujamaa. Mfano, tabaka la chini wanaosisitiza kwamba changu ni chako na chako ni changu, binadamu wote ni sawa. Hata hivyo tabaka tawala linawapuuza.

▪︎ Watawala wa Tanzania wanazidi kuwa Mabwana huku watawaliwa wanazidi kudidimia kwenye dimbwi la umasikini na kutumikishwa kama watumwa wasio na sauti.

▪︎ Watawala wanatumia kodi za Wananchi hovyo wakijilimbikizia mali,majumba na Magari ya kifahari kila iitwapo leo huku Watawaliwa wakilemewa na mzigo mzito wa kodi.

▪︎ Watawala wa Tanzania wanahubiri na kusisitiza amani kila iitwapo leo huku Watawaliwa wakililia haki, kwani wao wanadai haki ndiyo msingi wa amani na utulivu.

Ndugu Watanzania! Yapo maeneo ambayo yamekuwa yakitumiwa vibaya na watawala kwa uminywaji wa haki nchini. Yamekuwa yakitumiwa kwa miaka mingi hususani mwaka 2025 kama ifuatavyo:

■ Vyombo vya habari: Mwaka 2025 Vyombo vya habari vya Tanzania vimetumika kufunika moavu mengi ya watawala kama vile mauaji ya kimbari ya Oktoba,matukio ya utekaji,wizi wa kura na mengineyo.

Vyombo vya habari vya Tanzania kwa sasa vimegeuka vyombo vya kusifia watawala kwa kila wanachokifanya pasipo kukosoa.Lakini pia vyombo hivi huwa vinashindwa kuripoti matukio muhimu yanayowahusu Wananchi wakidai haki zao au uonevu wanaofanyiwa na watawala, badala yake huwa vinatumika kuwasafisha watawala. Wapo pia wengine huficha ukweli na wengine kufumbwa vinywa kwa kutishiwa kufungiwa vyombo vyao vya habari, hii ni kutokana na impunity katika Taifa.

■ Vyombo vya Dora:

Jeshi la Polisi ambalo kazi yake ya msingi ni kulinda Raia na Mali zake, lakini limegeuka kuwa adui wa Raia na Mali zake. Kazi kuwa kwa sasa ni kulinda watawala na Mali zao za wizi. 2025 limekiuka sheria za Nchi kama vile namna ya kukamata Watuhumiwa na namna ya kufanya treatment kwa Watuhumiwa pale wanaposhikiliwa katika vituo vya Polisi.
Hali ambayo ilizidi kuongeza chuki kati ya polisi na Wananchi.

Jeshi la Wananchi, liliaminika miaka yote kuwa jeshi linalotokana na Wananchi na kazi yao ni kulinda mipaka ya nchi na Wananchi dhidi ya majeshi mengine kutoka nje ya Nchi. Lakini mwaka 2025 Wananchi wameiondoa Imani hiyo kwani limeonyesha kulinda watawala waovu badala ya wananchi. Ni dhambi kubwa mno hii Wananchi kukosa Imani na jeshi lao kwani ikitokea Vita leo Wananchi hawa wanaweza kusaidia majeshi ya nje kuwamaliza wanajeshi wa nchi Yao kama ilvyotokea Uganda 1979 chini ya utawala wa Dictator Idd Amin Dadaa.

Usalama wa Taifa siyo kimbilio la Wananchi tena kwa kutoa taarifa mbaya za maadui wa Nchi, Kwani wanaogopa kwa kufanya hivyo yeye mwenyewe hana uhakika wa usalama wake baada ya kutoa taarifa. 2025 ungelimuuliza Mwananchi wa kawaida usalama wa Taifa ni nini? Angeweza kujibu kivyepesi kabisa kuwa ni usalama wa watawala. Siyo uslama wa Taifa na Rasilimali zake.

■ Wasanii
Wasanii ambao hapo awali walijulikana kama kioo cha jamii Hali hailuwa hivyo 2025, kwani waligeuka ghafra na kuwa kioo cha watawala na kuacha kuyasemea Mambo muhimu ya jamii. Wananchi hao hao waliowafanya kuwa maarufu waliachwa na kugeukia watawala ambao waliwataka baada ya kuwa maarufu.

■Bajeti ya nchi inayowapendelea Watawala kuliko Wananchi: Ukitazama bajeti ya kila mwaka,watawala wa Tanzania wamekuwa wakijipendelea kwani wamewekeza pesa nyingi za bajeti katika matumizi ya kiofisi na viongozi wa serikali kama vile misafara,chakula,ununuzi wa magari ya gharama kubwa, posho n.k
Hali ambayo inazidi kuongeza chuki baina ya matabaka haya mawili.


HITIMISHO NA USHAURI KWA TAIFA
Ndugu Watanzania! Mifumo isiyo ya haki nchini ndio chazo kikuu cha ukosefu wa haki nchini. Hali hii ndiyo iliyoopelekea yale yote yaliyotokea mwaka 2025 hususani kubambikiziwa kesi za uongo, kutekwa na kupotezwa, mauji mbalimbali kabla ya kipindi cha uchaguzi, mauji ya haraiki ya kipindi cha uchaguzi mkuu na matukio mengineyo.

Ndugu Watanzania! ili yasirudie yaliyotokea huko nyuma, wito wangu kwa mwaka huu 2026 kwa watawala wa Tanzania ni kwamba, watawala wanapaswa kusikiliza maoni ya wananchi. Watawala wakubali kuwapa wananchi matakwa ya haki zao.Mfano, wanatakiwa kuwahakikishia usalama wao wa kutotekwa na kupotezwa na kuuwawa, watawala wakubali kupatikana kwa katiba mpya itakayotokana na wananchi.

Kwa hakika watawala wanatakiwa kuwapa habari njema wananchi na siyo kuwatisha tisha. Watawala wanatakiwa kuwaganga waliovunjika mioyo kutokana na mateso waliyoyapitia 2025 hii ni pamoja na kuwakabidhi miili ya ndugu zao wakawazike kwa heshina na Ibada. Kuwafungulia waliofungwa magerezani kwa kesi za kubambikiwa kwa kesi za kisiasa na kuwatangaza uhuru wao mateka wote; wanaoendelea kushikiliwa kusikojulikana.
Mfano, Balozi Polepole, Mdude, Soka, Chaula, Manengero, Dionis, Mbise, Mlai n. K.

Ndugu Watanzania! Napenda kuweka bayana kwamba, hali ya ukosefu wa mifumo ya utoaji haki imesababisha uwepo mgawanyiko kati ya watawala na wananchi. Mgawanyiko huu unaweza kupelekea hali mbaya zaidi kutokea huko mbeleni. Unaweza kusababisha vikundi vya waasi na magaidi kama ilivyo katika nchi ya Congo DRC . Maana huko Congo DRC, wananchi walipopuuzwa na Watawala eti kwa kisingizio ni Wanyamlenge, matokeo yake walianzisha kikundi cha M23 ili kupambana na serikali; kudai haki na matakwa ya wananchi wa hali ya chini. Kwa sasa M23 wanaungwa mkono na wananchi ili kupambana na watawala ndiyo maana vita hiyo imekuwa ngumu sana kuisha, kwani hata baada ya tarehe 4 December 2025 rais Donald Trump wa Marekani kusuluhisha mgogoro huo kati ya rais wa Congo na Rwanda, bado M23 wanazidi kuteka maeneo muhimu kama vile Uvilla.Suluhisho ni watawala kukubali kusikiliza matakwa ya wananchi.

Mimi Askofu Mwanamapinduzi, siungi mkono watu wa nje waje kutuamulia mambo yetu ya ndani na kututawala. Ni dhahiri kuwa tuliwaondoa wakoloni kutokana na unyanyasaji na kutunyima haki kama ambavyo tunapitia kwa sasa. Tuliwaondoa ili tujitawale wenyewe; kulinda na kuzitumia rasilimali zetu kwa maendeleo ya wananchi wetu. Anayeijua historia ya Congo walivyowaruhusu Wabelgiji kubaki Congo na kumiliki siasa na uchumi hata baada ya uhuru wao 1962, kulizua migogoro na baadaye kuomba msaada wa Urusi na Marekani waje wawasuluhishe mpaka leo hawajapata suluhu zaidi ya miaka 60 iliyopita. Magharibi+Mashariki # Tanzania (nimetumia Code)

Naunga mkono wapatikane watu wazima Nchini kwetu wenye Uzalendo ili wawakalishe chini watalawa na wananchi tuyamalize mambo yetu wenyewe huku tukiombana msamaha na kuanza Upya. Tusigombane kwani sisi ni watoto wa baba mmoja wa Taifa.

Ikishindikana njia hiyo nitatoa ushauri mingine mwaka huu 2026 endapo Watawala wataendelea kuwakandamiza wananchi. Nitashauri watawaliwa (wananchi) waungane pamoja kuwakabili wenye nguvu (watawala) pasipo kujiingiza kwenye mitego ya udini wala ukabila, ili kupata haki zao na kwa Hakika Wananchi Watashinda.

Niwatakie kila la kheri katika mwaka huu mpya na Mungu awalinde Watanzania wenzangu popote mlipo Duniani. Nawahakikishia kuwa tupo pamoja katika mapambano haya ya kudai haki! Nami nitaendelea kusimama na Wananchi mwaka huu 2026 kama nilivyofanya mwaka 2025.

Asanteni sana!

Wenu katika mapambano ya kudai haki

Askofu Mwanamapinduzi!
1/1/2026
 
Back
Top Bottom