Anguko la Lowassa na ushindi mwembamba wa Dr. Magufuli

Nyakarungu

JF-Expert Member
May 1, 2011
472
377
ANGUKO LA CHADEMA NA USHINDI MWEMBAMBA WA CCM KATIKA UCHAGUZI MKUU 2015.

Ndugu watanzania,
Ifuatayo ni tahariri iliyotokana na utafiti mdogo nilioufanya katika mikoa mitano (5) Tanzania bara kujua sababu zilizopelekea kushindwa kwa Lowassa na kushinda kwa Dr John Magufuli kwa ushindi mwembamba ukilinganisha na watanagulizi wake.

Nitaweka kwa ufupi ukiwa ni mhitasari tu wa tahariri ila ikiwezekana nikapata uwezekano nitaweka katika kipindi cha tv au makala mfululizo magazetini

Utafiti umefanyika katika mikoa mitano;-
1. Mkoa wa Mwanza
2. Mkoa wa Dar es salaam
3. Mkoa wa Mtwara
4. Mkoa wa Arusha
5. Mkoa wa Singida
Katika kila mkoa zilitumika namna mbili za kupata taarifa na majibu ya utafiti;-
1. Kuuliza maswali watu 100 (interview)@mkoa
2. Kuwapa watu 100 fomu maalum zenye maswali ya kujaza (questioner)@mkoa

Zoezi lilianza tarehe 01 Desemba 2015 mpaka 03 February 2016
Nitatoa taarifa hii kwa mtirirko wa tahariri na sio kwa mfumo wa takwimu (data), na kila sababu inayotajwa inaelezewa kitaaluma (kiutafiti) na kwa tafasiri ya kimtazamo (perception).

Katika kila sababu chanya kwa Lowassa iliyompa kura, sababu hiyo hiyo ilikuwa hasi kwa Dr Magufuli na ilisababisha kupungua kwa kura zake, na katika kila sababu chanya kwa Dr Magufuli iliyompa kura, sababu hiyohiyo ilikuwa hasi kwa Lowassa na ilimpunguzia kura.

a) Falsafa na itikadi za vyama kutupwa kando na kufanyika kwa kampeni za utashi wa wagombea pekee.
Hii ni sababu kubwa iliyowapunguzia kura wagombea wote wawili (Lowassa na Dr Magufuli), Wananchi wengi walitazamishwa kuwaamini au kuwashabikia wagombea na sio falsafa za vyama wala itikadi za vyama kitu ambacho hakifai na hakina afya kwa ustawi wa siasa za maendeleo kokote duniani,
Kwa upande wa chama cha Mapinduzi aliyekuwa Mgombea mwenza Mama Samia Hassan Suluhu ambaye hivi sasa ni makamu wa rais, alikuwa akikinadi chama na angalau kukumbusha umoja wa taifa na kuisema itikadi ya chama ya ujamaa na kujitegemea akiitafasri majukwaani, hii iliwafanya wananchi kuelewa dhana ya kukichagua chama ni nini na baadhi ya wagombea ubunge walifanya hivyo kwa nia ya kukitaka chama kibakie madarakani.

Kwa upande wa aliyekuwa akigombea Urais Dr Magufuli alijikita kuinadi ilani na kujitanabaisha kuwa ni mtu wa kufuata utaratibu kama ulivyopangwa, ilifikia mahali watu wakaanza kusema Dr Magufuli anajinadi pekee yake na amekiacha chama kando, ‘ kwa mujibu wa hali ya hewa ya kisiasa ya wakati huo kwa hapa Tanzania nasema Dr Magufuli alikuwa sahihi sana kwani wapinzani walikuwa wamewaaminisha wananchi kuwa adui mkubwa wa nchi ni chama cha mapinduzi na sio mgombea wa ccm ambaye ni Dr Magufuli’ anasema Mzee Kimalo Siwa wa Mkoani Arusha.
Perception, Hali hii ilifikia wakati wapinzani walipoona wamezidiwa kwa baadhi ya maeneo walianza kusema kuwa Dr Magufuli sio mbaya bali kibaya na chama anachotokea, hivyo wapinzani walijikuta wakijiingiza kwenye mtego na Dr Magufuli aliitumia kete hiyo kukwepa kuisemea sana ccm na akawa na kazi moja kubwa ya kuitangaza ilani huku akisisitiza kuwa Tanzania ijayo ni ya Magufuli, hali hii iliwavunja wapinzani nguvu kwa baadhi ya mikoa ambayo utafiti umefanyika na wengi kuelezea kuwa waliposikia wapinzani wakisema kuwa Magufuli sio mbaya bali chama chake ndio kibaya, basi walimlinganisha Dr Magufuli na Mwalimu Nyerere aliyeongoza nchi kwa ufanisi akiwa na chama hikihiki, hivyo wakagundua kuwa utashi wa kiongozi pekee bila kujali chama chake unaweza kuivusha nchi.

Hili liliwaathiri zaidi wapinzani ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wakitegemea kukikosoa ccm pekee ili waaminike, hivyo wakajikuta wakikwama kumkosoa Dr Magufuli aliyeonekana kumaanisha alichokuwa akikisema majukwaani.

Chadema wao walipoteza kabisa na kusahau kuiuza itikadi ya chama chao ya Mlengo wa kati na falsafa yao ya nguvu ya Umma, hivyo watu walipoona watu wanaozunguka kumnadi mgombea urais wao wote walikuwa ni wapya kwenye chama ingawa sio kosa lakini dosari kubwa ikiwa ni watu hao kutotaka hata kugusia juu ya faida ya watu kuichagua chadema badala yake walionekana kumfahamu Lowassa na sio chama na itikadi yake, hivyo watu wenye uelewa walijiuliza maswali kwamba lowassa ataongoza katika itikadi na dira zipi, atakuwa rais mwenye mlengo upi na misingi ipi ikiwa alijiandaa miaka 20 ndani ya ccm, miaka yote hiyo alijiandaa kimfumo,kimtandao, kiitikadi na kisaikolojia ndani ya ccm, leo ndani ya siku 14 tu baada ya kukosa kuteuliwa na chama chake atawezaje kuhama kikamilifu na akawa mpya na kuziishi itikadi mpya, alijibu Professa mmoja wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam ambaye ni mtaalamu wa sheria na katiba hakutaka jina lake litajwe.

b) Kuhama kwa wanachama kwa pande zote
Kila upande ulipoteza wananchama mahili na pia kila upande ulipokea wananchama mahili kutoka upande mwingine waliojibainisha kuvifahamu vyama walivyohama na kuwaaminisha wananchi kuchagua vyama walivyojiunga navyo;-

Kwa kipengele hiki ccm ilipoteza kura nyingi kwani Ndugu Lowassa aliyekuwa akigombea urais kupitia chadema akiungwa mkono na vyama vingine vya upinzani aliwahi kuwa waziri mkuu na alijinasibu kuwa anakifahamu chama cha mapinduzi na akawaaminisha wananchi kuwa chama hicho hakifai na amekihama kwa sababu hakifai tena kuongoza nchi, pia aliyekuwa waiziri mkuu wa awamu ya tatu Ndugu Sumaye Turway nae alihama akajiunga na timu ya Lowassa hivyo hali hii iliwafanya baadhi ya wananchi kuwaunga mkono kwa wingi na kupunguza kura za chama cha mapinduzi, makada mbalimbali wa chama cha mapinduzi walihamia kambi ya Lowassa na kuongeza kura tele kwa lowassa, akiwemo aliyekuwa kamanda wa vijana wa taifa Mzee Kingunge Ngombaremwiru, Tambwe hizza, Mzee Msindai na wengine wengi,

Ikumbukwe watu hawa walipohama walihama na baadhi ya wanafamilia na marafiki zao hivyo kura nyingi za ccm zilihamia kwa lowassa

Kwa upande wa chama cha mapinduzi kilipokea wanachama na viongozi wa upinzani ambao kwa kiasi kikubwa walifanya kazi ya kuelezea unafiki wa wapinzani na wasivyofaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi, ingawa athari ya wapinzani waliohamia ccm haikuwa kubwa kuzidi ya wanaccm waliohamia upinzani

c) Wanachama/makada wakubwa kutoshiriki kuwanadi wagombea wao wa Urais
Hili lilitokea katika pande zote mbili, kwa mfano katika moja ya majimbo ya mkoa wa Dar es salaam Mgombea mmoja wa ubunge wa upinzani hakuonekana kumnadi mgobea wao wa urais wala hakuonekana kushiriki harakati kama anavyofanya katika miaka yote, kiongozi huyo ambaye ni kiongozi wa kuheshimika katika chama chake alionekana akifanya kampeni katika jimbo lake na kuwanadi madiwani hakuwahi kusikika akimnadi mgombea wao wa urais wala kushiriki vikao vya mikakati ya ushindi ingawa ni kiongozi ndani ya secretariat ya chama.

Kwa upande wa chama cha Mapinduzi pia hali hii iliwaathiri katika baadhi ya maeneo, wapo wagombea waliojitangaza wenyewe na hawakukinadi chama hata kumuombea kura mgombea urais, kwa mfano mkoa wa tabora kuna mgombea mmoja alikuwa ametengeneza matangazo ya kujiombea kura akiwa ameweka picha yake na kutaja jina lake na kuandika chagua (JINA LAKE) kwa maendeleo ya jimbo letu hakutaja hata chama anachokiwakilisha wala hakuweka nembo ya chama, lakini pia wapo baadhi ya wagombea na viongozi waliokuwa wakihudhuria hata vikao vya upande wa wapinzani, ‘huwezi kuamini walikuja watu wa Lowassa hapa nikashangaa kumuona huyu mwenyekiti wetu wa mkoa akihudhuria kikao chao usiku akiwa amevaa hijabu akikodi bajaji’ anasema Mama mmoja ambaye ni mwanachama na kiongozi wa jumuiya ya wanawake katika mkoa Fulani hapa Tanzania

d) Kuondoka kwa Prof. Lipumba na kujitokeza kwa Dr. Slaa
Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa kampeni aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) alijiudhulu uongozi wa chama chake na kuondoka nchini kisha akarejea baadae, alifanya maamuzi hayo huku akieleza kuwa nafsi yake inamsuta na hawezi kuendelea kuwa mnafiki kuwaingiza watanzania katika shimo, akasema UKAWA imeacha misingi na miiko waliyokuwa wamejiwekea.

‘Ndugu mwandishi ulitegemea mtu kama mimi nimpinge Professa kabisa, mimi ni form four tu na Yule ni professa msomi kabisa, ikiwa amesema baada ya kupima ameona tunaweza kuanguka shimoni sasa alipojitokeza kutuwekea fumbo hilo, nisingeweza kuwaamini UKAWA’ anaeleza Bwana Nandonde Andengenye Mkazi wa mji wa Mtwara

Pia katikati ya kampeni aliyekuwa Katibu mkuu wa Chadema Dr. Peter Slaa alijitokeza na kuongea na wananchi kupitia vyombo vya habari;-

Siku hiyo ilikuwa ni kiama kwa upinzani kwani Dr. Slaa licha ya kueleza kwa nini hakubaliani na Lowassa kuwa mgombea urais, kwanza aliwaonyesha watanzania jinsi Mwenyekiti wa chadema Ndugu Mbowe Freeman alivyobobea katika siasa za ubinafsi, uyeye na ulaghai.

Akaanza kwa kukanusha taarifa za Mbowe kuwa Dr Slaa aliomba likizo na kuwa ataungana nao baadae, kitu ambacho hakikuwa kweli bali mbowe alitaka kuhalalisha hujuma zake dhidi ya viongozi wenzake wa chadema ambao hawakukubaliana na Lowassa kuwa mgombea urais

Dr Slaa alieleza chanzo cha yeye kukaa kimya na kutangaza rasmi kuachana na siasa za vyama, pia kilichoishtua jamii ni kitendo cha Dr Slaa kutishiwa na kumfanya aishi kwa hofu wakati huo, hivyo jamii iliwaogopa upinzani, kwa aina ya uongo walioufanya na kumtishia mtu tena aliyekuwa kiongozi mkuu wa chama chao.

‘Ngoja nikuambie kiongozi wangu,mimi ninapomsikia kiongozi akisema kuwa Dr Slaa ameomba likizo halafu kesho namuona Dr Slaa mwenyewe anakanusha, hao watu nitawaamini kwa lolote tena?’ anajibu kwa kuhoji Mwamini Rajabu ambaye ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha usimamizi wa fedha Dar Es Salaam

Perception, hii ilipunguza kura nyingi za upinzani na kuzipeleka ccm na ilikuwa pigo kubwa kwa upinzani kwa viongozi wawili wa ngazi ya uwenyekiti na ukatibu kujiondoa wakati wa kampeni huku wakiwa walishiriki kupanga mikakati ya ushindi katika kambi ya upinzani.

Pamoja na wananchi kujitathimini na kuona kuwa hivi vyama vya upinzani ni vyama maslahi mifukoni na sio vyama vya kuijenga nchi, ikiwa Dr Slaa ameonekana sio lolote sio chochote iweje wananchi wa kawaida? Hivyo wananchi wengi waliamua kuwapuuza wapinzani

e) Kauli za mikanganyiko za Lowassa
Inakumbukwa siku Ndugu Lowassa akitangaza nia ya kugombea urais katika uwanja wa Abeid Aman Karume Arusha aliwaeleza watanzania kuwa yeye na watanzania wasidanganywe na wapinzani bali mabadiliko ya kweli yataletwa na ccm na hakuna mpinzani mwenye jeuri ya kuleta mabadiliko, wananchi wakampigia makofi na kuyashika maneno yake.

Lakini cha ajabu watu na dunia nzima ilipata mshituko siku lowassa alipohama na kusema kuwa ccm imechoka haifai kuongoza taifa, akaenda mbali zaidi na kumkosoa mwenyekiti wa ccm taifa aliyekuwa rais wakati huo kuwa ameharibu uchumi wa nchi, akisahau siku alipokuwa akitangaza nia alimsifia juu ya maendeleo mbalimbali na kuinua uchumi

Hii iliwashangaza watanzania na kuamua kuachana na mpango wa kumuunga mkono,

‘Ningekuwa mimi ningewaambia watanzania kuwa ninatamani kuwa rais wao na kwa kuwa nimeikosa nafasi hiyo ndani ya ccm nimeamua kugombea kupitia upinzani, kwani nani angenifunga?’ Anajibu kwa kuhoji Mama Nyambabhe mkazi wa Mabatini Mwanza

Kauli za kukanganya za Ndugu Lowassa ziliwakatisha tamaa watu waliokuwa wanamuunga mkono na kuwafanaya wasipige kura au kubadili mwelekeo

Kwa mfano siku Mzee Lowassa akizindua kampeni alisema kuwa ccm hawajawahi kushinda kwa haki, bali huwa wanaiba kura miaka yote, lakini wakati huohuo akasema yeye ndiye alikuwa akimwezesha Rais kikwete kushinda, hii ikatafsiriwa kuwa yeye ndiye alikuwa fundi wa kuiba kura, hivyo wananchi wakajua kabisa huyu hata tusipopiga kura atashinda

Pia aliwakataza watu wasikusanyike kwa kile wanachokiita kulinda kura akasema wapige kura na waondoke, akasisitiza kuwa suala la tume wamwachie yeye hakuna kura yake hata moja itakayopotea na atanganzwa yeye wala wasiwe na shaka.

Kauli hizi ziliwafanya watu wengine waamini kuwa mzee ana mbinu mbadala kwa hiyo hata wasipopiga kura atatangazwa yeye.

Lakini siku chache kabla ya siku ya kupiga kura Mzee Lowassa alisikika akiwataka wananchi walinde kura kauli yake ikitangazwa na Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, hili liliwashangaza wananchi na kuonyesha kuwa ukawa hajajiandaa kuongoza bali wanaishi kwa kubahatisha tu, hivyo wananchi wengi walibadilika na kuamua kuichagua ccm.

f) Kauli ya Seif Sharif Hamad
Siku mbili kabla ya kupiga kura aliyekuwa mgombea urais Zanzibar Seif Hamad alisikika jukwaani akisema kuwa yeye atakapomaliza kupiga kura hataonekana bali anawataka vijana wakae walinde kura na kuhakikisha anatangazwa,

Kauli au agizo hili liliwafanya watu wengi kuogopa kujitokeza kupiga kura kwani waliamini wapinzani wanataka kuwatumia tu kama daraja lao la mafanikio

g) Kugawanyika kwa kura za Ukawa
Kuna vyama vitatu vya upinzani ambavyo vyote ni matokeo ya ugomvi katika vyama vinavyounda ukawa ambavyo navyo vilishiriki uchaguzi vikiwa na wagombea-;

ADC- Chama hiki kiliundwa baada ya mgogoro wa ndani ya Chama cha CUF, katika uchaguzi wa 2015 kilikuwa na mgombea urais

CHAUMA –Chama hiki ni zao la mgogoro uliotokea katika chama cha NCCR-Mageuzi nacho kilikuwa na mgombea urais katika uchaguzi mkuu

ACT – Chama hiki ni zao la mgogoro uliotokea katika chama cha CHADEMA nacho kilikuwa na mgombea urais

Vyama vyote hivyo viliondoka na wanachama wengi katika vyama vyao vya awali hata mikutano yao ya kampeni vilikuwa vikiwakosoa wapinzani wenzao kwa kile walichokiita kupoteza dira

Huku UKAWA nao wakijikita kuwaita wanachama wao wa zamani kuwa ni wasaliti, hivyo wananchi na wanachama wa vyama hivyo waliviona vyama vyao kuwa havijajiandaa kushika madaraka hivyo waliamua kukipigia kura chama cha mapinduzi na wengine wakawapigia upinzani

Pia siku moja katika mahojiano ya kipindi cha tv alionekana kiongozi mmoja wa upinzani akikiri kuwa wamesimamisha mgombea urais ili kukidhi haja ya kupata 5% ya kura ili wapate sifa ya kupewa ruzuku, hii ilisababisha kura zao nyingi ziporomoke na kuhamia kwingine.


HITIMISHO

Ccm ilipata ushindi ingawa sio wa kishindo kama ilivyozooeleka, kuna sababu nyingi zikiwa ni pamoja na hizo zilizotajwa hapo juu, lakini nyingine zikiwa ni za kimfumo wenyewe,

Ukweli ni kwamba Dr. John Magufuli na Mama Samia walikibeba chama kuliko ambavyo chama kilitakiwa kiwabebe

Dosari zilizojengeka na kukomaa hazina budi kuharibiwa na kupanda upya mbengu ya chama ili kichanue kama kilivyokuwa kabla ya uchaguzi.

Chadema ilianguka kwa kosa la kiufundi kwa kutaka kupita njia ya mkato, kuweka kando miiko na mkisingi yake na kutaka kibebwe na jina la Mgombea pekee huku kikiua misingi yake na kuona aibu kutaja neno rushwa na ufisadi jukwaani.

Naruhusu andiko hili kutumiwa katika media zote na Magazeti na makala mbalimbali

Na Nyakarungu Grayson ‘Mtemi’

Email: diplomatictable@gmail.com

Simu: +255754459572
 
Back
Top Bottom