Amiri Jeshi mkuu, iambie CCM isiilazimishe CUF ifuate njia ya ASP

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
AMIRI JESHI, IAMBIE CCM ISIILAZIMISHE CUF IFUATE NJIA YA ASP.

Salamu.



Mie si mchambuzi wa mfano katika mambo ya kisiasa katika nchi yetu, ila niko na nafasi kama mtanzania kutoa mawazo yangu kwa lolote linalotokea katika nchi yeti ili mradi sivunji sheria, na ndio maana huwa mara moja moja najaribu kutazama changamoto au matatizo yetu kadiri ya upeo wangu na kisha kutoa maoni yangu pia kadiri ya upeo wangu uleule. Leo, nimejaribu kuutazama mkwamo wa kisiasa Zanzibar.

Kitendo cha ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kutangaza tarehe ya kurudiwa uchaguzi kimepingwa na watetezi wa demokrasia wa ndani na nje ya nchi yetu,na Seif chini ya CUF hatashiriki uchaguzi huo wa marudio. Kama Maalim Seif alishinda urais, na akishawishi kila mzanzibar asijitokeze kupiga kura, na endapo kwa mfano Shain atapata kura 5000 kati ya kura 6000 zilizo pigwa, Tanzania na dunia watajua Maalim Seif ndio aliyeshinda uchaguzi wa mwaka wa jana.

Hata hivyo, kama mawakala wa CUF hawata kuwepo katika vituo vya kupigia na kujumlishia kura, na kama makamishina wa ZEC waliokataa ubabe wa Jecha hawatakuwako katika TUME, hivi hawa CCM na ZEC watashindwa kuficha aibu yao kwa kudanganya umma kuwa Wazanzibar wengi wamejitokeza hata kama vituo vilikuwa vitupu na watendaji wa ZEC hawakuwa na kazi zaid kuchapa usingizi? Huo upande mmoja wa sarafu

Upande wa pili wa sarafu, kwa kubaki wenyewe CCM na ZEC katika zoezi hili bila uwepo wa upande wa pili, hivi ikitokea wazanzibari wamejitokeza kwa wingi, na kwa wingi wao huo wakamchagua Dk Shein, hivi hawa CUF/UKAWA si wataubeza huo ushindi na kukataa kumtambua Shein kama rais kwa kisingizio cha ZEC na CCM kuwa wenyewe katika uchaguzi bila jicho la wapinzani(CUF)?

Kwa misingi hiyo, tutapimaje kukubalika na kukatalika kwa ZEC na CCM kwa wazanzibar? Kama halali walisema haramu, hivi watashindwa kusema tena haramu kuwa halali? Hivi tarehe 20/03/2016 hawaendi kumuhalalisha Shain kwa mamia elfu ya kura hata kama hajafika ndururu ya kura hizo?

MWISHO; si mwisho kivile, naumia, wenzetu hawana imani na mahakama, hawana imani na ZEC, na amiri jeshi mkuu kasema hataki fyokofyoko zaidi ya katoa ushauri wa kuwaomba wapingaji waende mahakamani kusaka tafasiri ya kisheria; chombo ambacho tumeshuhudia hivi karibuni kikipewa fedha kwa sharti la kiufundi la kumaliza kesi ili serikali ipate ushindi ambao utaingizia tirioni moja, chombo ambacho jaji mkuu aliyekuwa anakiongoza bila haya kajitosa kugombea urais kwa tiketi ya CCM kiasi wenzetu wadhani kijani ndio rangi halisi ya mahakama zetu.

Rangimoto nimechanganyikiwa? nimechanyanykiwa! huenda nimeandika pumba leo, ila hakuna namna sababu mambo ya Zanzibar tangu enzi ya ukoloni wa Muingereza yalikuwa yanachanganya, na kwa kuchanganya kwake ndio maana uchaguzi halali wa mwaka 1963 matokeo yake yalibatilishwa kwa kisingizio cha "sisi wa wazanzibar wenye haki ya kutawala na waleo sio wazanzibar hivyo hawana haki ya kutawala"

Bila haya, na bila kujua wale wanao jiita Wazanzibar kimsingi walienda Zanzibar kufanya makazi na kwasababu zilezile nao warabu wakawa na wameenda. Iweje vizazi vya kiarabu wasiwe wazanzibar alafu vizazi vya bara wawe wazanzibar? Ikamwagwa damu kwa jina la "mapinduzi matukufu".Jina la "mapinduzi matukufu" tangu mwaka 1964 hadi sasa linatumika kuhalalisha batili na kuwazima au kuwaziba vinywa wanasiasa na wanaharakati wanaotaka usawa, upendo, amani, maendeleo hasa ya kiuchumi, na utulivu miongoni mwa wazanzibar wote bila kujali rangi zao, asili zao na mahala watokapo.

Hichi nilichoandika katika kuchanganyikiwa kwangu, kinathibitishwa na kauli za mara kwa mara za viongozi wa CCM na wa serikali zote mbili, kwa nyakati tafauti, katika kauli zote, kauli ya funga kazi ni ile iliyotolewa na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa UWT marehem Asha Makame alipotamka bila hofu kuwa "Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar haiwezi kutolewa na vikaratasi"

Maneno hayo aliyatamka marehem Asha Makame mwanzoni mwa mwaka 2000 katika baraza la wawakilishi na akayarudia tena kwenye bunge la katiba pia bila hofu yoyote. Maneno yenye maudhui kama hayo yalitamkwa na Lukuvi kanisani, yalitamkwa na vingozi wa UVCCM na hivi majuzi tuliyaona kwenye mabango ya wanaCCM katika sherehe za mapinduzi na katika maskani ya SAUTI YA KISONGE.

UBAGUZZIZI.jpg


Tunaweza kuyapuuza maneno kama haya kwa kudhani ni vijembe tu vya kisiasa na kwa hivyo havina madhara katika dhana nzima ya kubadilishana madaraka kwa mujibu wa katiba na udumishaji wa demokrasia, lakini tukirejea ya mwaka 1963 tunagundua wazanzibar walipiga kura, na kwa hiyari yao walichagua akinani toka vyama gani wawe viongozi wao.

Waweza kukubaliana na mimi kuwa kitendo cha mwaka 1964 si kwamba kilizaa mapinduzi tu, lakini pia kiliasisi kwa mara ya kwanza tabia ya kudharau mamlaka ya wananchi wa Zanzibari ya kujichagulia viongozi wao wenyewe. Ndio maana, kwa kujua kuwa mwaka mmoja baada ya uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1963 waliweza kubatilisha matokeo ya uchaguzi ule kwa kisingizio cha "sisi wazanzibar na wale ni warabu" na mwaka wa jana wakarejea tena kwa kisingizo cha Pemba kulitokea udanganyifu mkubwa katika zoezi la upigaji kura, lakini kwa wanaojua siasa za Zanzibar wanajua sababu ni ushindi wa hao waitwao warabu(hizbu) na ya kwamba warabu hawapewi nchi kwa vikarakati(kura) sababu wenye nchi(CCM) waliichukua kwa MAPINDUZI.

JECHA AKAFUTA UCHAGUZI kaitisha uchaguzi mwingine, hivi kwa uchaguzi wa sasa ndio wataachia kwa vikaratasi? Kama wataachia nchi kwa vikaratasi tutajuaje uthabiti wa kauli yao ikiwa kwa miaka yote wanawaona wenzao waarabu na wenyewe ndio wazanzibar? Kama hawataachia, kuna umuhimu gani wa kushiriki uchaguzi ambao matakwa ya wapiga kura hayaheshimiwi isipokuwa yale tu yanayo kidhi haja ya chama dola? Au tusiulize haya maswali kuchelea kutafasiriwa na amiri jeshi mkuu kama fyokofyoko?

Tujiulize, kwanini Pemba kuwe na udanyanyifu na si Unguja? jawabu jepesi, asilimia kubwa ya waPemba ni watu wenye asili ya uchotara wa kiafrika na kiarabu, na kimsingi ndio hao hao walioambiwa mwaka 1963 kuwa sio Wazanzibar kiasi mwaka 1964 yafanyike mapinduzi matukufu.Kabla hata ya mfumo wa vyama vingi kurudi tena, wanasiasa wanye asili ya Pemba walikuwa wakipata misukosuko ndani ya CCM hasahasa kama wakiwa na nia ya kutaka kiti cha uenyikiti wa baraza la mapinduzi.

Kama lilivyo jina lake, baraza la mapinduzi, kwa hivyo mwenyekiti wake lazima aidha awe mwana mapinduzi au muumini aso shaka juu ya mapinduzi. Kwakuwa wanamapinduzi waliinasibisha serikali ya Zanzibar iliyopinduliwa mwaka 1964 na uarabu, na kwakuwa wanasiasa wengi wenye nguvu watokao Pemba wana asili uarabu, hivyo basi ilikuwa ngumu na hata sasa bado ngumu kwa wanasiasa wa WAKIPEMBA kuaminiwa kukalia kiti cha uenyekiti wa baraza la mapinduzi, ni wachache waliaminiwa na tena baada kupita katika vigezo ambavyo hata sasa ni wachache wanao vijua.

Ukizingatia kuwa TANU(CCM BARA) ilishiriki kwa asilimia kubwa katika mapinduzi ya mwaka 1964, kwa vyovyote vile yenyewe kama mdau mkubwa wa mapinduzi haitakubali hata kidogo kiti cha baraza la mapinduzi kukaliwa na mzanzibari ambaye imani yake kwa mapinduzi ni ya kutia shaka, hapa ndipo ilipozaliwa hisia kuwa rais wa Zanzibar hachaguliwi na wazanzibar bali na watu wachache toka Dodoma wanao amini CCM ndio MAPINDUZI, na bila MAPINDUZI hakuna CCM, lakini mbaya zaidi na ukizingatia maneno ya video hii utajua kuwa wenzetu hawa wana amini CCM ndio ZANZIBAR.Kwa hivyo nashawishika kusema katika vichwa vyao wanaamini CCM(ASP)=MAPINDUZI=ZANZIBAR.

Huku ni kujitia ujuha wasiokuwa nao sababu wanajua fika kuwa Zanzibar ilikuwako kabla hata ya ASP, na wanajua fika kuwa waarabu walikuja Zanzibar zaidi ya miaka 2000 iliyopita na walioa waafrika, na hata visiwa vya Unguja na Pemba vilipoanza kutambulika kwa jina la Zanzibar ilijumuisha vizazi vya hao waarabu pamoya na vizazi vya waafrika, sasa iweje ASP iliyozaliwa mwaka 1957 ije waone watu wenye asili kiarabu(ZNP) kuwa si wazanzibari ila wao tu wenye asili ya bara(ASP) ndio wazanzabar?

ZNP wanachama wake wengi walikuwa na asili ya kiarabu, na kwa sababu hiyo hata viongozi wake watakuwa ni watu wa namna hiyo, na tunajua kwa kura ilizopata ZNP peke yake haikuweza kuunda serikali hadi pale waliposhirikiana na ZPPP. Kwa mashirikiano yale ni kama vile wazanzibar wenye asili ya kiarabu walipewa mamlaka kupitia sanduku la kura kuunda serikali. Kwakuwa wengi wao walikuwa wazanzibar wenye asili ya kiarabu, ASP wakafanya propaganda kuwa serikali ile ni serikali ya waarabu.

Kinachoisumbua Zanzibar ni UBAGUZI, na UBAGUZI huu ulipandwa na ASP. Hivi kwa mfano, kwa nchi kama ya Zanzibar ambayo ina watu wengi machotara wa kiarabu na watu wengi weusi, hivi ni halali kwa chama cha ASP ambacho chenyewe kwa jina lake la awali (AFRO PARTY) na ukijumlisha wingi wa wanachama na viongozi wake ambao ni WEUSI kwa rangi, kisha chama hicho kiwaite wenzao walio unda serikali kuwa ni WABAGUZI WA RANGI na SI WAZINZIBAR kisa tu wanaungwa mkono na watu wengi wenye asili ya kiarabu? Hivi kwanini ASP chama chenye watu wengi weusi na vingozi wake weusi kisiwe chama cha KIBAGUZI lakini ZNP ndio kiwe cha kibaguzi? Au ni halali kwa mtu mweusi kumbagua mtu mweupe lakini haramu kwa mtu mweupe kumbagua mweusi? Katika nukta hii ndio tunaona ujasiri na ushujaa wa Mandera.

Mtagundua kinacho sumbua katika siasa za Zanzibar ni ubaguzi wa rangi wa ASP kwa wenzao wenye asili ya kiarabu, kinachosumbua siasa za Zanzibar ni ASP(CCM) kujiona wao ndio chama cha kiZanzibar na vyama vingine(CUF) ni vyama vya kiarabu.Na kwasababu hiyo wakapindua serikali kwa kile walichodai kuwa wanairudisha nchi kwa wenyewe ambao ni waafrika. Mara baada ya mapinduzi Karume Sr. (ASP) akajitangazia urais wa maisha pale aliposema uchaguz hautafanyika hadi baada ya miaka 50.

Laikini kwangu mimi, kuhusu tangazo la Karume Sr., ule ulikuwa woga wa hawa wabaguzi wenye asili ya Kiafrika kwa kudhani ukifanyika tena uchaguzi baada ya miaka mitano au chini ya hapo bado ASP na ZNP mmoja wao asingeweza kuunda serikali mwenyewe bila kuungana na ZPPP, na kwakuwa serikali iliyopinduliwa ZPPP ilikuwa mshirika, kwa vyovyote vile ASP isingerudi madarakani kama ungefanyika uchaguzi sababu ilikuwa rahisi sana ZPPP kushirikiana na ZNP kuliko kushirikiana na ASP.

ZNP na ZPPP baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar na baadae nchi kuwa na chama kimoja, hivi vyama vyote vilikufa, wote baadae mojakwamoja(automatically) wakajikuta ni wanaCCM, huko ndani ya CCM kama nilivyosema huko juu walikuwa wanabanwa wasipate nafasi za juu, na wale waliopata ujue waliaminiwa sana, tena sana.

Wale walio aminiwa na kisha wakaonekana kama wana usaliti walitimuliwa bila simile, na hii timuatimua ndio iliyo irudisha ZNP kwa jina la CUF baada ya kurudi mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na ASP imeendelea kufanya UBAGUZI wake chini ya koti la CCM hadi leo hii. Kwahivyo yale mabango yalosema "machotara ni hizbu, Zanzibar nchi ya waafrika" yalimaanisha CUF(ZNP) ni warabu na CCM(ASP) ni ya waafrika, na Zanzibar wenyewe waafrika, CUF waarabu hawana chao.

Mabango kama haya, yale ya sauti ya kisonge, na kauli za akina marehemu Karume, marehemu Asha Makame, Lukuvi, na za hawa makinda wa CCM yaani UVCCM Zanzibar na ukijumlisha kitendo cha Jecha kufuta matokeo kinyume cha sheria yanathibitisha bila kigegezi chochote kuwa tatizo la mkwamo wa ZANZIBAR ni CCM kujiona wao ndio chama cha kizanzibar na CUF ni chama cha kiarabu, tatizo la Zanzibar lilisababishwa na mapinduzi ya mwaka 1964.

UBAGUZI.jpg


Imani ya CUF kwa serikali na mamlaka za nchi yetu haikupotea, ingawa imepungua kwa kiasi kikubwa, ombi langu CCM isiwalazimishe CUF ipoteze imani yake yote kwa serikali na mamlaka zilizopo Zanzibar kama vile ASP ilivyoamua kwa makusudi kujibagua na kisha kuamua kutoitambua serikali iliyoundwa na ZNP na ZPPP na hatimaye wakafanya mapinduzi mwaka 1964 bila sababu zozote za msingi; kama walikuwa na sababu za msingi, tangazo la uchaguzi kufanywa tena baada ya miaka 50 lilikuwa na maana gani kama si kuwazuia watu au vyama vingine kuingia madarakani kwa sanduku la kura? Je, kitendo hichi si cha kibaguzi?

NINI KIFANYIKE?
Ili imani iendelee kuwepo ni aidha kwa ZEC kumtangaza mshindi wa uchaguzi uliofanyika mwaka wa jana hata kama kwa kufanya hivyo kutamaanisha ni kuwapa Zanzibar wa waarabu kwa kutumia vikaratasi, sababu na amini ni bora hao waarabu wapewe Zanzibar kwa vikaratasi kuliko kwa ncha jambia au kwa kufanyika mazungumzo ya kisiasa yatakayo lenga kuzika makandokando ya mwaka 1963 na yale ya mwaka 1964.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1963 na baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 wanasiasa hawakufanya jitihada zozote za maana za kuwaunganisha Wazanzibar, lakini kubwa hawaja kaa kitako maalum chenye lengo la kuzika siasa za uchotara na uafrika.

Serikali iliyoingia mwaka 1963 ilishindwa kufanya hilo na serikali ya kwanza ya mapinduzi hadi ya sasa ya umoja wa kitaifa zimeshndwa kufanya hivyo. Karume Jr. na Maalim Seif walijaribu lakini walishindwa sababu hayo yalisababishwa na utashi wa watu hao wawili na si utashi wa vyama vyao na Wazanzibari kwa ujumla.

Pamoja na kwamba amiri jeshi alisema wapingaji waende mahakamani, mimi naona huu sio mgogoro unao hitaji tafasiri za kisheria, huu ni mgogoro unao hitaji wadau wakuu wakae chini na kuzika mambo ya mwaka 1963 na 1964 kisha watu hao watoke kwa umma kama wamoja. Wafanye haya kisha ndio uchaguzi ufanyike kwani kwa mtazamo wangu pia sidhani kama ni jambo la kukwepeka.

Njano5
0622845394
 

Attachments

  • UBAGUZI.....jpg
    UBAGUZI.....jpg
    23.7 KB · Views: 94
  • UBAGUZI,,,.jpg
    UBAGUZI,,,.jpg
    14.2 KB · Views: 128
100% your right Mkuu!! Sina hata chakuchangia zaid ya kuunga mkono hoja! Kuna Black America mmoja nilimuuliza hvi nyie weusi wahuku Marekan hamjisikii kurudi au kujiona kwamba kwenu ni Afrika? Jamaa aliniambia waafrika hatupendani na hakuna anayemjali mwenzie, hivyo hawaoni umuhimu wa wao kujiona ni wakutoka afrika. Ukiangalia ni kweli!
 
CCC wapo sahihi woga kwa zNP ni lazima , waarabu walituuza kama wanyama hawawezi kuaminiwa , mtu yeyote anayejitanabaisha na mwarabu aogopwe kama ukoma. Seif anapewa fedha nyingi na hao waarabu hili awe Rais hili awarudishe hao
 
Baada ya tarehe 20 March Joho safi jeupe la Mh JM litaanza kuchafuka kwa madoa
Ni bora kuepuka dosari hizi mapema ili joho liendelee kuwa ng'aavu
 
CCC wapo sahihi woga kwa zNP ni lazima , waarabu walituuza kama wanyama hawawezi kuaminiwa , mtu yeyote anayejitanabaisha na mwarabu aogopwe kama ukoma. Seif anapewa fedha nyingi na hao waarabu hili awe Rais hili awarudishe hao

biashara ya utumwa haikufanya na waarabu peke yao, washiriki wa biashara ile baadhi wa machifu wa kiafrika, wafanya biashara wa kiarabu na wazungu. sasa kwanini ubaya wote abebe mwarabu, tunasema hizi ni propaganda tu.

hata hivyo wakat wa ZN P utumwa ulikwisha koma miaka mingi sana, na hakukuwa na nchi yoyote au shirika lolote la kimataifa ambalo lilikuwa linafanya biashara hiyo, na hata wazungu ambao ndio waliokuwa wateja wakubwa wa watumwa waliacha kununua, sasa woga wa ASP ujue hakusababishwa na hilo bali UBAGUZI.

NDIO HAWA ASP waliopandikiza hadithi za ukatili wa waarabu dhidi waafrika, hadithi nyingi zilikuwa hazina ukweli zaidi ya kutafuta uhali wa kubagua.
 
biashara ya utumwa haikufanya na waarabu peke yao, washiriki wa biashara ile baadhi wa machifu wa kiafrika, wafanya biashara wa kiarabu na wazungu. sasa kwanini ubaya wote abebe mwarabu, tunasema hizi ni propaganda tu.

hata hivyo wakat wa ZN P utumwa ulikwisha koma miaka mingi sana, na hakukuwa na nchi yoyote au shirika lolote la kimataifa ambalo lilikuwa linafanya biashara hiyo, na hata wazungu ambao ndio waliokuwa wateja wakubwa wa watumwa waliacha kununua, sasa woga wa ASP ujue hakusababishwa na hilo bali UBAGUZI.

NDIO HAWA ASP waliopandikiza hadithi za ukatili wa waarabu dhidi waafrika, hadithi nyingi zilikuwa hazina ukweli zaidi ya kutafuta uhali wa kubagua.

Wape kisomo hao waliokuwa wamekuwa brainwashed au labda niseme bewitched kwamba chama cha upinzani kikishika dola eti waarabu watarudi! Ndio hao wengine mungu anawalani wanafia huko huko kwa waarabu. Mwisho wa fitina ni fedheha
 
Wape kisomo hao waliokuwa wamekuwa brainwashed au labda niseme bewitched kwamba chama cha upinzani kikishika dola eti waarabu watarudi! Ndio hao wengine mungu anawalani wanafia huko huko kwa waarabu. Mwisho wa fitina ni fedheha
wanaelewa sana, ila UBAGUZI ndio wanajifanya hawaelewi
 
Back
Top Bottom