nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,803
Habari
Mwandishi Wetu Toleo la 296 29 May 2013
UAMUZI wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kuazimia kutwaa viwanda vilivyouzwa ama kubinafsishwa kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wameshindwa kumudu masharti ya mkataba, kwa mara ya kwanza, utawanasa baadhi ya makada waandamizi wa chama hicho, Raia Mwema linaripoti.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ambazo gazeti hili limezipata, uamuzi huo moja kwa moja unaathiri baadhi ya makada waandamizi wa CCM ambao ni pamoja na aliyepata kuwa Mbunge wa Igunga na Mweka Hazina (taifa) wa zamani wa CCM, ambaye pia ni Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz sambamba na Mbunge wa sasa wa Morogoro Mjini, Aboud Azizi.
Wengine ni pamoja na Mbunge wa zamani wa Bukoba Vijijini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Nazir Karamagi na mmoja wa vigogo waandamizi katika Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa, Nsa Kaisi. Kwa wakati tofauti, makada hao na wengine wamepata kubinafsishwa viwanda na kushindwa kukidhi matakwa ya baadhi ya mikataba kati ya viwanda walivyobinafsishiwa. Viwanda hivyo ni pamoja na vya korosho katika mikoa ya kusini na vingine katika maeneo mbaimbali nchini, ikiwamo mkoani Morogoro.
"Kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao walipewa viwanda kwa mikataba ya ama mauziano au uendeshaji tu. Mikataba hii ilikuwa na masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuendeleza uzalishaji wa kiwanda husika kama awali, kwa bahati mbaya, wamegeuza baadhi ya viwanda walivyotwaa kuwa maghala au kwingine wanaendesha shughuli zao tofauti na matakwa ya mikataba ya ubinafsishaji," kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Kwa mfano, katika Mkoa wa Morogoro, viwanda ambavyo vilibinafsishwa na ambavyo bado vinaendelea kufanya kazi ni pamoja na Tanzania Packaging Manufactures (1998 Ltd) kinachotengeneza magunia; kiwanda cha Tanzania Tobacco Processor kinachochakata tumbaku; Pollytex (21st Century Textile Mills 1998 Ltd) kinachotengeneza nguo na kiwanda cha Morogoro Tanneries (Ace Hides Ltd), kinachotengeneza ngozi.
Viwanda vingine ni Mtibwa Sugar Estate (1998) Ltd kinachozalisha sukari, Kilombero Sugar Company - ILLOVO (K1) kinachozalisha sukari; Kilombero Plantation Ltd (KPL) kinachohusika na uzalishaji mchele na Kilombero Sugar Company – ILLOVO (K2) kinachozalisha sukari.
Lakini kwa upande wa viwanda visivyoendelea na uzalishaji licha ya ubinafsishaji ambao kwa wakati huo ulikuwa ukisimamia na aliyekuwa Waziri wa Ubinafishaji Dk. Abdallah Kigoda ambaye ndiye Waziri wa sasa wa Viwanda na Biashara ni pamoja na Morogoro Ceramic Wares Ltd, Tanzania Leather Goods Industry, Kilosa Carpets Ltd, Moro Shoes Ltd (G & T Shoe Company), Moproco na kiwanda maarufu cha Morogoro Canvas Mills (1998) Ltd, kilichokuwa kikitengeneza maturubai.
Kutokuendelea kufanya kazi kwa viwanda hivyo kumesababisha changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana mkoani Morogoro, pigo ambalo linazidi kukiadhibu chama tawala, CCM miongoni mwa makundi ya vijana.
Kwa sasa taarifa kuhusu hali ya viwanda nchini inabainisha ya kwamba kwa mwaka 2008, idadi ya viwanda vilivyokuwa vinafanyakazi kwa upande wa Tanzania Bara ni 729.
Kati ya idadi hiyo ya viwanda, vilivyokuwa katika Jiji la Dar es Salaam ni 383; Arusha 51, Mwanza 39, Singida 27, Tanga 27, Kagera 26 na Kilimanjaro 24.
Kati ya viwanda hivyo vilivyokuwapo mwaka 2008, viwanda 643 vinatajwa kumilikiwa na watu binafsi na viwanda 72 vikimilikiwa na serikali wakati vilivyobaki 14, vinamilikiwa kwa pamoja kati ya serikali na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za viwanda kutoka serikalini, viwanda 549 vinamilikiwa kwa asilimia 100 na wazawa wakati 121 vinamilikiwa na wageni kutoka nje ya nchi. Vingine vipatavyo 59 vinamilikiwa kwa ubia kati ya serikali na watu binafsi au kati ya wageni na wazawa.
Inaelezwa ya kwamba kati ya viwanda 729 vilivyokuwapo mwaka 2008, asilimia 93 au viwanda 680 ni viwanda vya uzalishaji bidhaa, kati ya hivyo asilimia 93, yaani viwanda 240 vinajihusisha na uzalishaji bidhaa za chakula,vinywaji pamoja na tumbaku na mashine za kusaga nafaka 61.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili unabainisha ya kwamba licha ya kuwapo kwa viwanda hivyo nchini sehemu kubwa ya bidhaa zinazozalishwa na baadhi ya viwanda hivyo bado zinaagizwa kutoka nje ya nchi, hali inayotia shaka kuhusu uratibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, inayoongozwa na Mbunge wa Handeni, Waziri Dk. Abdallah Kigoda ambaye hata hivyo, hadi tunakwenda mitambano hakuweza kupatikana, simu yake ya mkononi ikiita bila kujibiwa.
Kutokana na kuyumba huko kwa hali ya viwanda nchini na hususan baadhi ya viwanda vilivyobinafsishwa na kutelekezwa, wabunge wa upinzani bungeni, kupitia hotuba yao kuhusu Wizara ya Viwanda na Biashara, waliitaka serikali kuwaeleza Watanzania ni kwa vipi viwanda vitafufuliwa wakati baadhi ya waliobinafsishiwa viwanda hivyo waking'oa mitambo na kuuza kama chuma chakavu na baadhi ya viwanda husika vikibaki kuwa maghala, wakinukuu sehemu ya uchunguzi uliowahi kufanywa na gazeti hili miezi kadhaa iliyopita.
"Tutawezaje kukuza ajira kama viwanda vyetu vinauwawa makusudi, mitambo inang'olewa na kuuzwa kama chuma chakavu na serikali ipo, inaona na haichukui hatua yoyote?
Kambi rasmi (ya upinzani bungeni) imekuwa ikisema mara zote kuwa mambo haya yanatokea kutokana na ukweli kwamba waliobinafsishiwa viwanda ni washirika wa karibu na CCM.
"Jambo hilo limesababisha kutokuchukuliwa kwa hatua zozote kwa watu hao ambao wanakiuka mikataba," anasema Mbunge Highness Kiwia, ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda na Biashara, na Mbunge wa Ilemela, jijini Mwanza.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Kiwia ni kama mapokeo ya hotuba iliyowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, katika mkutano wake wa hivi karibuni mkoani Morogoro, alipotaka viwanda vilivyobinafsishwa na kushindwa kuendelezwa kurejeshwa serikalini kwa ajili ya taratibu nyingine.
Hotuba hiyo ya Kinana ni kama sasa imetekelezwa na Kamati Kuu ya CCM na kwa wakati huu, ni kama serikali, kupitia kwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Kigoda haina njia tofauti ya kufuata zaidi ya kutekeleza uamuzi wa Kamati Kuu ya chama tawala, ambayo katika utaratibu wa kawaida inatajwa kuwa na nguvu kubwa ya kubadili mwelekeo wa sera za serikali katika masuala muhimu ya kitaifa.
Alipoulizwa kuhusu azimio hilo la Kamati Kuu ya CCM kutwaa viwanda ambavyo baadhi vilibinafsishwa kwa makada wa chama hicho, Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwambia mwandishi wetu kwa kifupi; "Ni kweli kamati kuu imeazimia kutwaa viwanda vilivyobinafishwa kwa wawekezaji wanaokwenda kinyume cha masharti ya kitaifa ya uwekezaji. Ni bora Chama kikasimamia maslahi ya wananchi kuliko maslahi ya mtu mmoja mmoja bila kujali ama ni mwanaCCM au la. Hiki ni chama cha watu wengi kwa hiyo ni lazima kisimamie maslahi ya wengi."