Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,263
BARAZANI KWA RAJAB
Aibu za viongozi wa Kiafrika
Na Ahmed Rajab
KUNA matukio mawili matatu ya kisiasa yaliyotokea barani Afrika hivi majuzi ambayo yamewashangaza wengi kuona kwamba yametokea, hususan mnamo 2018. Usingetaraji matukio kama hayo kutokea kwa sababu historia imetufunza vya kutosha kuhusu athari zao. Lakini ndo yametokea. Na nadhani yatazidi kutokea madhali bado tuna wanasiasa wenye nakisi za maadili, si ya kisiasa tu bali hata maadili mengineyo pia.
Shida kubwa tuliyo nayo Afrika ni ukosefu wa uongozi wa maana. Viongozi tunao lakini wengi wao si viongozi wenye sifa za kustahiki kuitwa viongozi. Ama huwa dhaifu wakikubali kuchezewa na madola ya nje au huwa ni viongozi wenye kujihisi kwamba hakuna wengine wa kuongoza isipokuwa wao.
Matatizo ya uongozi hujihidhirisha zaidi katika nyakati za uchaguzi au zinazokaribia uchaguzi. Inasikitisha kwamba tumekuwa kama tuliokata tamaa kuhusu chaguzi zinazofanywa katika nchi mbalimbali za Kiafrika. Kitu cha kwanza kinachotujia kichwani wakati wa chaguzi, hasa za urais, ni wizi. Huwa tunajiuliza uchaguzi huu utaibiwa vipi, mizengwe gani itayofanywa kubadili matokeo ya uchaguzi.
Halafu kuna fujo na rabsha tunazotaraji kutokea wakati wa upigaji kura na hasa wakati wa kuhesabiwa kura na zaidi pale matokeo ya uchaguzi yanapotangazwa.
Jambo moja tulilojifunza kutoka historia ni kuwa ni muhali kwa nchi isiyo na taratibu au mazoea ya demokrasia kuwa na chaguzi za kidemokrasia. Haiwezekani. Ndio maana tunashuhudia taksiri kama zilizotokea hivi juzi katika uchaguzi mkuu wa Zimbabwe au katika kura ya maoni ya Comoro ambako Rais Azali Assoumane anaonyesha kuwa na kipaumbele kimoja tu katika maisha yake ya kisiasa: kurefusha muda wa urais wake.
Tukiiangalia Congo tunaona kuwa wapinzani wa Rais Joseph Kabila, kina Jean-Pierre Bemba, aliyewahi kuwa makamu wa rais, na Moise Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga, wamewekewa vizingiti vya kuwazuia wasiwe wagombea wa urais katika uchaguzi ujao wa urais. Agosti 8, ni siku ya mwisho ya wagombea kujiandikisha.
Bemba alirudi Congo baada ya kuwa nje ya nchi kwa muda wa miaka kumi. Alikuwa mjini Hague alikokuwa akifanyiwa kesi na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) akishtakiwa kwa makosa ya jinai wakati wa vita. Mahakama ya ICC ilimwachia huru Juni lakini mahakama ya kikatiba ya Congo mpaka sasa ninapoandika makala haya bado haijaamua iwapo anaweza kugombea urais au la.
Katumbi, kwa upande wake, alikimbilia Zambia Mei 2016 baada ya serikali ya Kabila kudai kwamba ina nia ya kumshtaki kwa kosa la kuajiri askari wa kukodiwa ili waipindue serikali. Katumbi amekanusha kwamba alikuwa na mpango huo. Hivi juzi alifika mpakani kutaka kuingia kwa gari Congo. Inavyoonesha ni kwamba matatizo yake na serikali yalianza mara tu baada ya kujiuzulu kutoka chama kinachotawala 2015.
Kwa mujibu wa sheria, Kabila hawezi kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi ujao lakini kuna tetesi kwamba anakula njama za kutafuta njia za kung’ang’ania madaraka. Moja ya hila anazozitumia ni kuuvunja nguvu upinzani kwa kuwazuia viongozi wapinzani wasichuane naye au wawakilishi wake.
Hayo si mageni katika historia. Mara zote tunapokuwa tunaiangalia historia huwa tunayaangalia matukio yaliyokufa. Matukio yakiwa hai, yakiwa mubashara, hayawi historia. Hayawezi kuwa ya historia ikiwa hayako hai. Ya historia huitwa ya historia kwa sababu huwa yashapita. Huwa ya kale.
Ninapokuwa nayatathmini yanayojiri sasa hupendelea sana kuifukua historia. Huwa sikubali kuiacha ilale kama mfu. Kwa hivyo, nifanyacho ni kuichokonoa ardhi ilimolala historia kwa lengo la kuifukua. Huifukua ili tuweze kuitalii na kuangalia ni yepi yake yanayoweza kutufunza kwa kutukumbusha yaliyopita.
Naamini kwamba kwa kuifukua historia, tukaisimamisha wima na tukaivua sanda yake, kama ilikuwa imevishwa sanda, tunaweza tukaiona historia kama ipasavyo kuonekana. Ninasema kwa kusudi “kama ilikuwa imevishwa sanda” kwa sababu wakati mwingine mfu huo wa historia hukukabili ukiwa uchi bila ya kuwa na sanda ya kuusitiri.
Huwa kama historia ilitupwa jaani bila ya kustiriwa. Nadhani ndo maana kuna wale wenye kulizungumzia “jaa la historia”. Kwenye jaa hilo mna mizoga mingi ya historia. Mizoga hiyo inaweza kuwa na umbo la matukio yaliyopita au ya viongozi waliopita. Wengi wa viongozi, kama si wote, huwa ni wale ambao katika zama zao za utawala wakijifanya kuwa wababe. Hawa ni wale waliokuwa wakitisha, waliokuwa hawasikii la mtu kwa sababu walikuwa hawataki kusikia wakiambiwa kweli. Waliokuwa wakijifanyia watakavyo kwa sababu wakijiona kuwa wao ndio serikali na serikali ndio wao. Waliokuwa wakizifanya kauli zao kuwa ndio sheria na waliokuwa tayari kuzipinda sheria za nchi na kuzikiuka katiba ili waweze kufanya watakavyo.
Mafunzo ya historia, ya matukio yaliyopita, yana umuhimu mkubwa kwa matukio ya leo. Hutufunza mengi kuhusu jamii na namna inavyoendeshwa na wale wenye mamlaka ya kuiendesha jamii ama kwa kukabidhiwa mamlaka hayo na wanajamii au kwa kujitwalia wenyewe mamlaka hayo kwa njia zisizo za halali au za ulaghai.
Moja ya ishara ya kiongozi wa mabavu ni namna anavyojaribu kuwa mkali na kuwatisha watu anapokuwa anahutubia. Huufanya ukali wake uonekana kuwa ni jambo la kawaida. Hivyo ndivyo wanavyoibuka viongozi wahemshaji, viongozi wa kisiasa wenye kuwashawishi watu kwa kutumia hisia badala ya fikra zao. Huwafanya wananchi waamini kwamba ni yeye mwenye uwezo wa kuyatanzua matatizo ya nchi na huwatupia wapinzani lawama kwa matatizo yanayozuka nchini. Hujifanya yeye kuwa ni “mtu wa Mungu” na mwokozi wa walio maskini nchini. Hitler, dikteta wa Ujerumani, akipenda kuitumia mbinu hii.
Nchi inapokuwa inanuka ufisadi sio tu kwamba inakuwa na matapeli, matajiri wanyonyaji wenye kuchuma utajiri wao kwa njia za rushwa, magendo na wizi. Nchi inaweza pia ikanuka ufisadi wa kisiasa. Huu ni wa hatari. Unaweza pengine ukawa wa hatari zaidi ya ule ufisadi wa kiuchumi. Nchi hukumbwa na maradhi hayo ya ufisadi wa kisiasa pale watawala wake wanapokuwa wamelewa madaraka. Huo ulevi wa madaraka ndio unaowafanya wawe wanatawala kimabavu.
Watawala wenye kutawala kwa nguvu, kwa mabavu, huamini kwamba udikteta wao ndio utaoweza kuyatanzua matatizo yote ya nchi zao. Ukweli wa mambo ni kwamba hauwezi. Udikteta huyazidisha tu hayo matatizo. Tena huyazidisha kwa gharama kubwa kwa sababu mfumo wa utawala huwa unakwenda njia kombo na ile ya haki. Wananchi hukabwa wasiweze kuwa na uhuru wa kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa katiba za nchi zao na wapinzani huumizwa na hata huuliwa.
Watawala husahau kwamba jukumu lao, dhima yao, kubwa ni kuwafanya wanaowatawala wawe salama katika nchi zao na wajihisi kuwa wana uhuru kamili wa kutoa mawazo yao na kushiriki katika harakati za kisiasa na za kijamii kwa manufaa ya nchi zao, ilimradi harakati hizo ziwe ni za amani.
Bahati mbaya watawala wa kimabavu hawafikiri hivyo. Wao humuona kila mwenye maoni yenye kukinzani na yao kuwa ni adui yao. Hapo ndipo watawala wanapozidi kuishi katika mazingira ya hofu. Kila wanakogeuka hufikiri kuwa wanamuona adui yao. Ndipo wanapoanza kamatakamata, wakitafuta kila sababu au kijisababu cha kuwatia adabu wanaowaona kuwa ni adui zao.
Hao wanaobandikwa uadui hupokonywa haki zao za kiraia na hata uraia wao huanza kutiliwa shaka. Hii ni aibu. Ni aibu kubwa kwa viongozi wenye kuona kwamba ni jambo jepesi kumpokonya mtu uraia wake, mtu ambaye siku zote hakutiliwa shaka kuwa ni raia ila pale alipoanza kufikiriwa kuwa ni adui wa mtawala au wa serikali.
Uongozi kama huo ni uongozi wa kijinga. Ni wa hatari hasa kwa nchi zilizo nyuma kimaendeleo na zilizojaa ujinga.