kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
2016 Ni Mwaka wa kazi
Dar es Salaam. Wakati Watanzania leo wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha mwaka mpya, wasomi na watu wa kada mbalimbali wamesema utakuwa wa mabadiliko.
Mwaka huu unaanza baada ya kukamilisha 2015 ambao kwa Tanzania mbali na kuwa wa uchaguzi, ulikumbwa na matukio ya uhalifu, wizi, ubadhirifu, rushwa, ufisadi, ukwepaji kodi, ujangili na mauaji, kwa kutaja baadhi.
Wasomi, majaji, viongozi wa dini, watendaji wa Serikali na taasisi zake, wastaafu, wanaharakati, wanasiasa wamesema mambo hayo ya 2005 yanapaswa kuwa historia na kuitaka Serikali ya Awamu ya Tano kujipanga na kuendeleza mazuri iliyokwishaanza kuyafanya ili kuonyesha mabadiliko.
Baadhi ya mambo waliyotaka yatatuliwe haraka ni mkwamo wa kisiasa Zanzibar ulioibuka baada ya kufutwa kwa uchaguzi, rasilimali za nchi kuwanufaisha wazawa, ajira, haki za wafanyakazi kuboresha na kujenga mfumo imara wa utawala na kudumisha amani.
Balozi Sefue: Mabadiliko makubwa
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema utakuwa mwaka wa mabadiliko lakini ili kufikia malengo yaliyowekwa, ni lazima wananchi washirikiane na Serikali iliyopo madarakani.
“Ni mwaka wa mabadiliko makubwa. Serikali imeanza kazi kwa kasi na kasi hiyo pia wakiwa nayo wananchi, hakika tutafanya kitu kikubwa ambacho kitalibadili Taifa letu. Mungu atujalie amani na upendo,” alisema Balozi Sefue.
Jaji Lubuva; Kazi kwa bidii
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alisema Watanzania wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa muda wao mwingi wanautumia katika shughuli muhimu ili kuliletea Taifa maendeleo.
“Tudumishe amani yetu lakini tusisahau masilahi ya Taifa. Hiki ni kitu muhimu na tunatakiwa kukiweka mbele kuliko jambo lolote lile.
“Kama ambavyo tulifanya uchaguzi mkuu wa amani na utulivu, ndivyo tunavyopaswa kuwa katika mwaka huu. Katika hili vyama vya siasa vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha vinapigania maendeleo ya nchi,” alisema.
Kuhusu mvutano wa kisiasa visiwani Zanzibar, Jaji Lubuva alisema ana imani mazungumzo yanayoendelea baina ya viongozi wa CCM na CUF yatamalizika kwa amani.
Profesa Gabagambi: Taharuki kiuchumi
Kuhusu mwenendo wa uchumi, Profesa wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Damian Gabagambi alisema iwapo vitafanyika vipimo vizuri, kuna kila dalili kuwa na taharuki ya kiuchumi mwaka huu kutokana na mikakati mikali ya Serikali ya kubana matumizi na mapambano ya rushwa.
Alisema biashara nyingi nchini zilikuwa zikiendeshwa kwa ujanjaujanja wa kutolipa kodi na rushwa, hivyo utamaduni mpya wa kulipa kodi na utawala bora utazifanya kampuni nyingi kuyumba kimapato kwa kuwa siyo kawaida na zitatakiwa kujipanga upya.
“Rais ameanza kubana matumizi serikalini kwa kupunguza safari za nje na kupiga marufuku kukodi kumbi mahotelini.
“Hii itayumbisha sekta ya usafiri wa anga na hoteli. Kampuni za ndege zitapunguza safari zao nchini hivyo kampuni hizo huenda zikapunguza idadi ya wafanyakazi wake ili kuendana na hali ya kibiashara iliyopo,” alisema Profesa Gabagambi.
Alisema matukio kama hayo yatasababisha uchumi kushuka kidogo japo siyo vibaya kwa kuwa ili mabadiliko yatokee lazima kuwe na maumivu.
Kwenye sekta kubwa kama za kilimo, Profesa huyo alisema haoni kama yatatokea mabadiliko yoyote kwa kuwa hadi sasa Serikali haijafanya jambo lolote hasa ikizingatiwa kuwa sekta hiyo inategemea huruma za mvua ya Mungu.
Profesa Ngowi: Tutarajie bajeti inayojitosheleza
“Mustakabali wote wa uchumi na maendeleo kwa mwaka 2016 upo chini ya Rais Magufuli na timu yake kwa asilimia 90,” alisema Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam, Honest Ngowi.
Alisema anatarajia Serikali ifanye kazi kubwa kuboresha utawala bora na demokrasia kwa kumaliza mgogoro wa Zanzibar ili kufungua fursa nyingine za kibiashara na kiuchumi zilizofungwa kwa sababu ya masuala hayo.
Profesa Ngowi alisema mkakati wa Serikali kusimamia utawala wa sheria inabidi ufanywe kwa umakini na lugha nzuri kwa kuwa unaweza kuwakimbiza wawekezaji wakihofia biashara zao kuathiriwa.
“Mikakati ya kuongeza nidhamu ya matumizi serikalini na kubana ukwepaji wa kodi unaonyesha dalili njema. Tukienda na matarajio ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ya kukusanya Sh1.5 trilioni kwa mwezi bila shaka mwaka huu tutarajie bajeti inayojitosheleza kwa fedha za ndani bila kusubiri misaada,” alisema Profesa Ngowi.
Jaji Mihayo: Zanzibar tatizo
Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Thomas Mihayo alisema Watanzania watasherehekea mwaka mpya huku kukiwa na sitofahamu kuhusu uchaguzi wa Zanzibar. Aliitaka Serikali kuhakikisha inamaliza msuguano huo aliodai kuwa unaweza kukwamisha mipango mingi ya maendeleo.
“Kama mwanasheria kilichofanyika Zanzibar kinanichekesha. Ukitizama Katiba ya Zanzibar utabaini kuwa uchaguzi ule haukufutwa, maana aliyeufuta (Mwenyekiti Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salum Jecha) hana mamlaka hiyo.”
“Wanaohusika walitatue jambo hili kwa umakini mkubwa ili tuondoke katika mtanziko huu. Natarajia kuona hili likimalizwa kwa busara zaidi mwaka 2016,” alisema.
Jaji Mihayo alisema mwaka mpya utakuwa na mabadiliko kutokana na baadhi ya mambo ya msingi yaliyoanza kufichuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano na kuwataka wananchi waiunge mkono ili iweze kupambana na mambo yote maovu.
“Ni mwaka ambao ninatarajia kuona uchumi ukikua kwa kumaanisha, kwa maana ya mwananchi mmojammoja kuwa na mabadiliko ya kiuchumi,” alisema.
Mgaya: Mishahara minono
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicolaus Mgaya alitaja mambo matano aliyosema yanapaswa kufanyiwa kazi na Serikali ya Rais Magufuli.
“Natarajia kuona Serikali ikimaliza tatizo la wafanyakazi kulipwa mishahara midogo na kukatwa kodi kubwa. Jambo jingine ni pensheni kwa wastaafu kutolipwa ipasavyo.
“Jambo jingine ni ajira kwa wageni ambao wamejaa nchini na wanafanya kazi bila kufuata sheria na taratibu. Pia, tunatarajia kuona Serikali ikianzisha vyanzo vingi vya mapato na kupunguza makato ya kodi kwa wafanyakazi. Kama kasi ya Serikali ikiendelea hivi nadhani mengi niliyoyataja yatapatiwa ufumbuzi na mishahara itakuwa minono,” alisema Mgaya.
Kaiza: kujitegemea kibajeti
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalojishughulisha na Masuala ya Kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza alisema mwaka 2016 anatarajia kuona Serikali inayojitegemea kibajeti, kuachana na utegemezi kutoka nchi wahisani ambazo wakati mwingine hazitoi fedha za maendeleo na hivyo kukwamisha miradi mbalimbali.
“Huduma za jamii ni jambo ninalotarajia kuona likiboreshwa zaidi. Utafiti ufanyike ili tujue nini kinakwamisha huduma hizi, kumbuka kuwa kuboresha huduma hizo ndiyo mwanzo wa maendeleo. Pia, Serikali ihakikishe rasilimali za nchi zinawanufaisha wazawa,” alisema.
Profesa Mpangala: Inahitajika dira na sera
Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala alisema anatarajia 2016 kuwa mwaka wa mabadiliko kwa kuwa tayari Rais Magufuli ameonyesha nia ya kuleta mabadiliko yanayotakiwa kwa wananchi.
Alisema Rais ameanza kwa kuibua madudu ya Serikali zilizopita ya kupambana na rushwa na kuzuia ukwepaji wa kodi lakini hajaandaa dira na sera ya kitaifa ya moja kwa moja.
“Mambo anayoyafanya kwa sasa hayawezi kuwa endelevu na kuleta mabadiliko tunayoyatarajia iwapo hakuna dira na sera ya muda mrefu, mabadiliko hayawezi kuja hivi bila Dk Magufuli kukibadilisha chama na kutuletea Katiba Mpya,” alisema Profesa Mpangala.
Alisema kuwa anatarajia Dk Magufuli ataendeleza mchakato wa Katiba Mpya hasa kuirudisha ile rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba yenye maoni ya wananchi vinginevyo, atakuwa anakataa mabadiliko.
Aidha, Profesa Mpangala alisema macho ya Watanzania yote yatakuwa kwenye utatuzi wa mkwamo wa kisiasa Zanzibar na njia rahisi ya kutatua mgogoro huo ni CCM kukubali kushindwa pale upinzani unaposhinda.
Dk Makuliko: Kutokomeza mazoea
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema 2016 unaonekana kuwa mwaka wa mabadiliko kwa kutokomeza mazoea yaliyokuwa yakirudisha ufanisi katika uendeshaji wa Serikali, utawala wa sheria na masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Tayari tumeshaanza kuona wanaoishi mabondeni wameanza kupata maumivu ya kubomolewa nyumba zao kwa sababu ya kutotii sheria hivyo tutarajie mengi mwaka huu ya namna hiyo,” alisema Dk Makulilo.
Alisema pia anatarajia kuona mchakato wa Katiba Mpya ukiendelea katika nusu ya pili ya mwaka kutokana na kuhitajika maandalizi makubwa miezi ya awali.
Kuhusu Zanzibar, alisema kuna kila dalili za Uchaguzi Mkuu Zanzibar kurudiwa mwaka huu japo baadhi ya wahusika katika mgogoro huo, ulioanza Oktoba 28 baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha kuufuta.
Lusekelo: Matokeo yatangazwe Zanzibar
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo, Dar es Salaam, Anthony Lusekelo alikuwa na maoni tofauti kuhusu sakata la Zanzibar: “Sababu zinazotolewa kuhusu kufutwa kwa uchaguzi ule ni porojo. Kila mtu ana haki ya kuongoza nchi. CCM walipaswa kujipanga kwa uchaguzi mwingine. Ni vyema matokeo yakatangazwa tu ili kumaliza mvutano.”
Alisema suala hilo limeitia aibu nchi na kuwataka viongozi kumaliza tatizo hilo mwaka huu kwa kumtangaza aliyeshinda katika uchaguzi huo.
Pia, mchungaji huyo alikosoa utaratibu wa baadhi ya mawaziri kuwachukulia hatua watendaji mbalimbali wa Serikali, mashirika na taasisi zake kwa maelezo kuwa wanachokifanya hakiwezi kusaidia kama hakutakuwa na mfumo imara wa ufanyaji kazi.
“Kama ukichunguza uovu wa kila mtu hakuna atakayesalimika na utafukuza kazi wengi. Hivi unawaondoaje watendaji wa bandari huku aliyekuwa waziri wa wizara ya uchukuzi ukimuacha? Hivi yanayofanyika bandarini alikuwa hayajui?
“Tazama hii bomoabomoa inayoendelea nchini. Iweje mtu akae sehemu miaka 20 leo avunjiwe nyumba? Serikali ilikuwa wapi siku zote? Mambo haya sitarajii kuyaona mwaka 2016 maana si utu kabisa,” alisema.
Mwasota: Katiba Mpya
Katibu wa Makanisa ya Pentekoste, Mchungaji David Mwansota aligusia suala la Katiba Mpya: “Kukosekana kwa Katiba Mpya kulisababisha kuibuka kwa malalamiko mengi wakati wa uchaguzi mkuu. Natarajia mchakato wa kupata Katiba nzuri utaendelea na kumalizika.
“Kuhusu Zanzibar, viongozi husika wanapaswa kukaa chini na kujadili mkanganyiko wa kisasa maana ndiyo njia sahihi ya kumaliza migogoro. Natarajia kuona mabadiliko makubwa.”
Kigwangalla: Uwajibikaji
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla alisema vipaumbele vyake mwaka huu ni kuboresha mfumo wa kuchangia huduma na mifuko ya afya ya jamii na malipo katika hospitali kufanyika kwa njia ya kielektroniki: “Mfano katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya walikuwa wakikusanya Sh50milioni lakini tulivyotaka wakusanye fedha kwa njia ya kielektroniki sasa wakusanya mpaka Sh500milioni.”
Alisema mkakati mwingine ni kuitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kukununua dawa moja kwa moja kutoka viwandani na ziwekwe nembo maalumu za Serikali.
“Jambo jingine ni kuwatawanya madaktari bingwa na watumishi katika hospitali mbalimbali nchini, zikiwamo za kanda na za mikoa. Tumebaini kuwa miji mikubwa ina madaktari bingwa wengi hivyo ni lazima tuwapeleke katika mikoa yenye uhaba wa madaktari ili kuwe na uwiano sawa,” alisema.
Lukuvi: Nitanyoosha yaliyopinda
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema mwaka huu amejipanga “kuyanyoosha yaliyopinda” kwa kuhakikisha anarahisisha maisha ya wananchi kwa kuboresha upatikanaji wa ardhi, upimaji na umiliki.
“Hii itawapatia fursa wananchi kupata haki ya kumiliki ardhi. Tunataka kuondoa unyonyaji unaofanywa na watumishi wa ardhi na matapeli kwa kuwaonea maskini katika umiliki wa ardhi na kila mtu atapata haki yake,” alisema Lukuvi.
Alisema kuna mikakati kabambe anayotarajia kuifanya katika sekta yake ikiwamo kuanza kutekeleza mradi wa majaribio wa kupima na kugawa hati kwa wananchi wa wilaya za Kilombero na Ulanga mkoani Morogoro.
Mpango huo, alisema utasaidia kufahamu kiwango cha ardhi kilichopo na kumaliza migogoro ya muda mrefu ya wakulima na wafugaji.
Chanzo: Mwananchi