Yaliyosemwa Iringa kuhusu Dr Slaa na Mengi

Serayamajimbo

Senior Member
Apr 15, 2009
191
38
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAMKO LA CHADEMA IRINGA MJINI KUHUSU MSIMAMO WA DR. SLAA
(MB) NA KATIBU MKUU WA CHADEMA KATIKA MASUALA YA MASLAHI YA WABUNGE NA VITA DHIDI YA UFISADI.
1.CHADEMA na wanachama wa Iringa mjini tumefurahishwa na kitendo cha kizalendo alichokionyesha Mbunge wa Karatu ambaye pia ni katibu Mkuu wa CHADEMA taifa, cha kutangaza na hatimaye kukosoa mishahara na maslahi makubwa wanayopata waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania. Hiki ni kitendo cha kizalendo hasa kwa taifa maskini kama hili. Kwa kupitia maandamano haya tunaelimisha umma wa Tanzania kuchagua Wabunge wenye moyo wa kizalendo kama huo katika Uchaguzi wa mwaka 2010.

2. Wananchi na wanachama walio wengi wa Iringa mjini wameonesha kusikitishwa zaidi na kitendo cha Wabunge hasa wa CCM wakishirikiana na Wabunge baadhi wa vyama vya upinzani, kumzomea na kufanya fujo za wazi na aibu ndani ya kikao cha Bunge dhidi ya Mh. Slaa wakiungwa mkono na kiongozi wa Wabunge yaani Spika. CHADEMA Iringa tunaamini walipaswa kufanya yafuatayo endapo Mh. Slaa ameupotosha UMMA.

v Kukanusha kwamba hawalipwi kiwango hicho na kutaja kiwango halisi cha maslahi wanayolipwa.
v Kutumia hoja za msingi na za kistaarabu bila kukiuka kanuni za Bunge kuunga mkono au kukanusha hoja na madai ya Dr. Slaa (MB).
v Kufuata kanuni za bunge za adhabu katika kumshughulikia endapo wanaamini ameudanganya UMMA wa Watanzania.
v Kutambua kwamba pesa na maslahi uwanayolipwa ni kodi za wananchi na walalahoi wa Tanzania, na wao ndio waliowachagua hivyo wana haki ya kujua maslahi ya watumishi wao ili wapate fursa ya kutathmini endapo yanalingana na uchumi wa taifa, ufanisi, na tija ya kazi zao majimboni kwao.

Izingatiwe kuwa wakati wabunge wanalipwa mamilioni ya fedha kwa mwezi, wafanyakazi wengine hususani watumishi wa umma kama walimu, wauguzi, maaskari nk wengi wao wanalipwa kima cha chini ambacho ni chini hata ya fedha anazolipwa mbunge kwa siku moja. Kwa upande mwingine wakulima ambao ni sehemu kubwa ya watanzania wamekuwa wakipata kipato kidogo kutokana na jasho lao. Njia pekee ya wabunge kukwepa wananchi kuhoji kiwango cha mishahara na posho kubwa wanazolipwa ni kuwa na bunge lenye wabunge mahiri na bunge makini lenye kupambana na ufisadi, kutetea rasilimali za taifa na kutoa sera mbadala za kuinua uchumi wa taifa na hatimaye kukuza mishahara na vipato vya wananchi walio wengi. Inasikitisha kwamba wakati wabunge wakizuia mjadala kuhusu maslahi yao, serikali kwa upande wake kupitia Hotuba ya Rais Kikwete iliyosomwa kwa niaba yake kwenye sherehe za Mei Mosi, 2009 Mkoani mara imetangaza kwamba suala la wafanyakazi kuongezewa mishahara yao halitatekelezwa kikamilifu kutokana na visingizio mbalimbali. Hii ni ishara ya matabaka katika taifa, kwani wakati wabunge wanajiongezea wenyewe kipato na kupata mapato ya kiwango cha kufuru ukilinganisha na hali ya taifa; wabunge hao hao wanashindwa kuibana serikali kutekeleza ahadi zake. Baadhi ya wabunge wamegeuka kama wenye shibe wanaosahau wenye njaa.

Tunachukua fursa hii kuhamasisha wananchi kupitia maandamano yetu kuitaka serikali kuweka rasmi wazi kwa umma, kiwango cha mishahara na posho wanacholipwa watumishi wakuu wa serikali wakiwemo viongozi wa kisiasa. Kadhalika, tunaitaka serikali iweke wazi ripoti ya Tume ya Ntukamazima ambayo iliteuliwa mwaka 2006 na kukamilisha kazi yake mwaka 2007 ya kupendekeza nyongeza ya viwango na maslahi ya wafanyakazi. Hii itawezesha watanzania kuwianisha vizuri mapato ya kada zote za wafanyakazi na kuunganisha nguvu katika kuhakikisha mapendekezo ya ripoti hiyo na matakwa ya umma kuhusu uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi nchini yanatekelezwa.

3. Tunapinga msimamo wa serikali unaoungwa mkono na Wabunge wa CCM wa kuhalalisha nyaraka zenye mwelekeo wa kuhujumu uchumi wa taifa hili kutunzwa katika makabati ya serikali na kudaiwa ni siri halali za serikali. Kuficha nyaraka kama hizo ni sawa na kuficha siri za uwizi na ufisadi ambalo ni kosa la jinai. Ikumbukwe kwamba ni nyaraka kama hizo zilipoibuliwa na kutumiwa na Dr. Slaa ziliasisi vita kali zaidi dhidi ya UFISADI unaoshabikiwa na baadhi ya Wabunge wa CCM kama vile; EPA, DEEP GREEN, MEREMETA, ALEX STEWART, KAGODA, TWIN TOWERS nk. Ikumbukwe kwamba kabla ya Orodha ya Mafisadi(List of Shame) kutajwa Septemba 15, 2007 maneno “UFISADI na MAFISADI” yalikuwa mageni masikioni mwa watanzania walio wengi. Hata baada ya kutajwa kwa orodha hiyo, viongozi wa Serikali, na hata wabunge wa CCM wengi wao walipinga tuhuma hizo na kukataa hata kuposha tafsiri ya msamiati wa ufisadi. Sasa kuna watanzania wengi ambao bila kujali itikadi tunazungumza pamoja lugha ya kupinga ufisadi. Matunda haya ni matokeo ya wakina Dr Slaa na baadhi ya watumishi wanaotanguliza mbele maslahi ya taifa, kutoa nyaraka zinazoitwa za siri ambazo zililenga kuficha ufisadi ndani ya serikali. Kati ya nyaraka hizo zinazoitwa za Siri ni pamoja na ule waraka toka Idara ya Usalama wa Taifa ulioelekeza Waziri Mkuu wa wakati huo auzie hoja ya Dr Slaa ya Ufisadi wa Benki Kuu isiingie Bungeni kwa kuwa ‘serikali haina majibu’. Hizi ndio aina ya nyaraka ambazo serikali inataka ziendelee kufichwa badala ya kutolewa hadharani zilaaniwe na hatua zichukuliwe.

Pia madai ya serikali ya kutaka ushahidi dhidi ya mtumuhiwa kama ambavyo wamemtaka Reginald Mengi mwenyekiti wa IPP kufanya ili washughulikie tuhuma zake, yatatekelezwaje endapo nyaraka kama hizo batili zinalindwa na serikali yenyewe kisheria? Kwa kauli moja CHADEMA Iringa mjini tunapenda kutoa pongezi kwa kauli ya kishujaa na ya kizalendo ya Ndugu Reginald Mengi iliyotaja baadhi ya MAFISADI PAPA wa uchumi wa Tanzania, na kuelezea athari zake, kitendo hiki tunatambua ni cha kijasiri na kinafaa kuigwa na watu wanaoitakia mema nchi hii. Kitendo hicho kimeendeleza pale ambapo Dr Slaa alianzia kwa kutaja Orodha ya Mafisadi 11 na kimechangia katika harakati za kuwaanika mafisadi ambazo CHADEMA imekuwa ikizifanya kupitia Operesheni Sangara inayoendelea katika maeneo ya nchi yetu. Kitendo hicho pia kimeunga mkono jitihada za baadhi ya vyombo vya habari, viongozi wa dini na Asasi za kiraia za kufichua ufisadi. Sambamba na hilo tunapinga kwa nguvu zote kauli ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Sophia Simba, iliyokejeli hatua ya mzalendo huyu jasiri dhidi ya UFISADI na MAFISADI. Je Waziri huyu amepata wapi ujasiri wa kuwa wakili muaminifu wa MAFISADI? CHADEMA Iringa mjini tunawasiwasi na USAFI wa Waziri huyu aliyeshika wizara nyeti ukirejea vitendo vyake wakati akigombea Uenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na maneno yake anayoyatamka hivi sasa. Mwisho kabisa tunamuomba Mh. Mengi asikate tama kwani Watanzania wengi hasa wanyonge wapo nyuma yake; hata hivyo aelewe kwamba ufisadi umejikita katika mfumo mzima wa CCM na serikali yake. Hao wanaitwa mafisadi mapapa wakishirikiana na mafisadi Sangara na mafisadi dagaa na wengineo kwa ujumla wao wamehodhi mwelekeo wa dola(state capture) hususani kupitia kufadhili chaguzi na makundi ya kugombania mamlaka. Mpaka sasa, Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM ameshindwa kupambana na hali hiyo kikamilifu ndani ya CCM na Serikali yake. Suluhisho la muda mfupi ni kuunganisha nguvu za umma katika kuhakikisha mafisadi wote wanaanikwa na kuchukuliwa hatua ili kuepusha mafisadi hao kuendelea kuligawa taifa. Hivyo, suluhisho la kudumu ni kufanya mabadiliko ya uongozi na mfumo mzima wa utawala.

Tunaamini Mkoa wetu una nafasi ya pekee katika taifa letu katika historia ya harakati mbalimbali. Ni mkoa ambao ulishuhudia Chifu Mkwawa akipambana ukoloni na kutaka uhuru. Ni mkoa chimbuko la mijadala kuhusu Kilimo katika taifa letu. Hivyo, tunachukua fursa hii kuwakumbusha watanzania wote kwamba katika nchi ambayo takribani asilimia 80 ya watanzania wote wanategemea kilimo, mapambano dhidi ya ufisadi lazima yalekea pia kuboresha hali za wakulima na sekta ya kilimo nchini. Matokeo ya jitahada za wakina Dr Slaa waliotoa nyaraka za siri za serikali ni baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi kulazimishwa kurejesha fedha zao walizoiba. Serikali ilitangaza kutumia sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya wakulima. Hata hivyo, Dr Slaa ameeleza bungeni hivi karibuni kuwa fedha hizo hazijaenda kwa wakulima badala yake zimetumiwa kwa matumizi mengine tayari. Ndio maana tunarudia tena kutoa mwito wa kutaka nyaraka za siri za serikali ikiwemo kama hizi zinazohusu kupindisha matumizi ya fedha yaliyokubaliwa hapo awali ziweze kuanikwa hadharani. Aidha tunatoa mwito, kwa watumishi wa serikali hapa katika mkoa wetu wa Iringa kuwezesha nyaraka zinazohusu masuala ya ugawaji na usambazaji wa pembejeo na mbolea ya ruzuku zianikwe zitolewe ili umma uweze kufahamu ufisadi uliopo pamoja na udhaifu mkubwa wa kisera uliopo katika mchango mzima. Hii itawezesha wakulima wa mkoa wa Iringa kuweza kupata stahili zao.

Kutokana na hali hiyo, ndio maana leo Mei 2 mwaka 2009 tumeandaa maandamano kuanzia Viwanja vya M/Togwa, ili kuungana na wananchi wenzetu katika kuwasilisha tamko letu na kutoa mwanya pia kwa wananchi wengine kuweza kuwasilisha maoni na misimamo yao kuhusu masuala haya yanayoligusa taifa letu.

MUNGU MLINDE Dr. SLAA NA UONGOZI MZIMA WA CHADEMA,
MUNGU TUOKOE WATANZANIA,
MUNGU IBARIKI TANZANIA,
MUNGU IBARIKI AFRICA.

IMETOLEWA NA;

Rev. Peter Msigwa.
Mwenyekiti wa CHADEMA Manispaa ya Iringa.

0754 360 996
0788 558 888
aabctz@yahoo.com



 
Back
Top Bottom