Yajue mambo 22 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Meneja Wa Makampuni

JF-Expert Member
Jul 7, 2020
6,328
8,243
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambapo Jamhuri hizi mbili ziliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeorodhesha mambo 22 ya Muungano. Katika Makala hii tutapata fursa ya kuyajua kwa kina na kupata uchambuzi wake:

1. Katiba ya Tanzania na Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania​

Kabla ya Muungano, kulikuwa na nchi mbili huru zilizokuwa zikijitegemea: Jamhuri ya Tanganyika iliyoundwa mwaka 1962 baada ya kupata uhuru tarehe 9 Desemba, 1961 na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyoundwa kufuatia Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964. Kila nchi ilikuwa na mamlaka yake (sovereign) ikiwa na eneo na mipaka, Katiba na Serikali yake, na iliendesha shughuli zake kwa kujitegemea kiuitawala.

Kwa sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zipo Katiba mbili; moja ikiwa ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inahusika na masuala yote ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ina Katiba yake ya mwaka 1984 ambayo inahusu masuala yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Aidha, masuala yote ya Muungano yamewekwa bayana katika nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tangu kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, Katiba hii imeshafanyiwa mabadiliko (amendments) mara 14. Kimsingi, lengo la mabadiliko hayo ya Katiba limekuwa ni kuiboresha na kuifanya iendane na mabadiliko mbalimbali yanayotokea nchini na pia kukidhi matakwa na mahitaji ya wananchi kwa ujumla.

2. Mambo ya Nchi za Nje​

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiyo yenye dhamana ya kuratibu na kusimamia masuala yote ya Kimataifa yaliyo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Mambo ya Nje, Mikataba ya Kimataifa pamoja na kuangalia fursa zilizopo za ushirikiano ya kiuchumi baina ya Tanzania na Jumuiya za Kimataifa. Ili kutekeleza majukumu hayo, Tanzania ina Ofisi za kibalozi katika nchi mbalimbali duniani.

Hivi sasa msisitizo umewekwa katika diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati endelevu ya kuwavutia wawekezaji, kuongeza biashara na utalii kwa lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo. Aidha, kutokana na umuhimu wa lugha ya Kiswahili, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubaliana kuanzisha Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya kwa lengo la kukuza lugha hiyo katika ukanda huo. Makao Makuu ya Kamisheni hiyo yako Zanzibar.

Pande zote mbili za Muungano zimekuwa zikishirikishwa katika uwakilishi wa masuala muhimu ya kimataifa yakiwemo makongamano ya biashara, uwekezaji na mikutano yote muhimu ya kimataifa. Mwongozo Kuhusu Ushiriki wa SMZ katika masuala mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda umepitishwa na kusambazwa tarehe 21/6/2019. Mwongozo huu umezingatia maeneo ya mikutano ya kimataifa na kikanda, nafasi za masomo ya elimu ya juu na mafunzo mengine nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada na mikopo ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

3. Ulinzi na Usalama​

Suala la Ulinzi na Usalama limeendelea kutekelezwa kimuungano ambapo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimeendelea kufanya kazi ya kulinda Nchi yetu na kushiriki katika shughuli za kijamii. Vijana toka pande zote za Muungano wanapewa fursa ya kujiunga na vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo mafunzo.

4. Polisi​

Jeshi la Polisi ndilo lenye jukumu la kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa kwa wananchi pamoja na kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa. Tangu kuasisiwa Muungano. Ulipoanza Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa sio tu kudumisha amani bali hata kushirikiana na wananchi wa kawaida katika shughuli nyingine za maendeleo.

5. Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari​

Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Hali ya Hatari ya 1986 kinampa Mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza hali ya Hatari na anaweza kukasimu madaraka hayo kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha katika Sheria tajwa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamepewa madaraka kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kutangaza hali ya hatari katika maeneo yao.

6. Uraia​

Sheria ya Uraia inayotumika ni Sheria ya Uraia Na.6 ya mwaka 1995. Sheria hii ilitungwa ili kufuta sheria mbalimbali zilizohusu uraia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuleta mkanganyiko kwenye suala la Uraia.

Kwa kipindi kirefu tangu kuasisiwa kwa Muungano, utambulisho wa raia wa Tanzania na wasio raia ulikuwa unafanyika kwa kutumia Hati za Kusafiria, Hati za Vizazi na Vifo na Serikali za Mitaa (nyumba kumi-kumi). Tarehe 30 Julai, 2008, Serikali iliunda Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (National Identification Authority - NIDA) kwa Hati Maalum ya Rais, Tangazo la Serikali Na.122. Majukumu ya Mamlaka hiyo ni kuhakiki uraia wa watu waishio nchini na kusajili taarifa zao, kuwapatia vitambulisho na kutengeneza Daftari la Kudumu lenye taarifa za utambuzi wa watu ambazo pia zitatumiwa na wadau wengine pamoja na kujenga mfumo wa utambuzi na usajili wa watu kitaifa.

7. Uhamiaji​

Mwaka 1995, Sheria zilizokuwa zinasimamia majukumu ya uhamiaji, Tanzania Bara na Zanzibar zilifutwa na kutungwa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995 na Kanuni zake za mwaka 1997. Aidha, Sheria zilizokuwa zinasimamia masuala ya uraia ziliunganishwa na kuwa Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995 na Kanuni zake za mwaka 1997. Ili kuboresha huduma za pasipoti, Serikali ilitunga Sheria ya Kusimamia Utoaji wa Pasipoti na Hati za Kusafiria (Tanzania Passport and Travel Document Act) Sura Namba 42 na Kanuni zake za mwaka 2004.

Idara ya Uhamiaji imeendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu nchini; kusimamia ukaazi wa wageni nchini kwa mujibu wa Sheria; kutoa Pasi za Kusafiria na Hati nyingine za safari kwa raia wenye sifa; na kuratibu maombi ya uraia wa Tanzania kwa wageni wanaoishi nchini. Maboresho hayo yamejumuisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uchukuaji, utunzaji wa kumbukumbu za wageni wanaoingia na kutoka nchini, utoaji wa Viza kwa wageni wanaoomba kuingia nchini na uchapishaji wa Pasipoti.

8. Mikopo na Biashara ya Nchi na Nje​

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawasiliana na wahisani kupata mikopo nafuu ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Aidha, kwa utaratibu uliopo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweza kuzungumza na Wahisani moja kwa moja kwa lengo la kupata misaada kwa kutumia utaratibu uliowekwa.

Mpaka mwaka 2009, Halmashauri ya Biashara ya Nje - Board of External Trade – BET iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bodi ya Biashara ya Nje (Board of External Trade Act) Sura Namba 155 kwa upande mwingine ilihusika na kuratibu, kusimamia ukuzaji wa biashara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi na kuhamasisha biashara ya nje kupitia maandalizi na ushiriki katika maonesho ya kimataifa mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Halmashauri ya Biashara ya Nje ilifutwa kwa Sheria Na.4 ya mwaka 2009 iliyoanzisha Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (The Tanzania Trade Development Authority - TANTRADE).

Katika kuimarisha Muungano, hususan katika masuala ya biashara ya nje na ndani, Serikali imeanzisha Ofisi ya TANTRADE Zanzibar ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Hatua hiyo ni muhimu katika kuunganisha nguvu ya kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji, utalii na biashara kwa ujumla zinazofanywa na Balozi zetu nje ya Nchi.

Kutokana na juhudi za kutangaza bidhaa za Tanzania nje ya nchi pamoja na kuwajengea uwezo wajasiriamali, mauzo ya Tanzania nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

9. Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano​

Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003 zimeweka utaratibu wa wazi wa ajira katika Utumishi wa Umma na kuondoa dosari zilizokuwepo. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekuwa ikitoa fursa sawa za ajira kwa Wananchi wote wa Tanzania ambao wanaomba na kuwa na vigezo kama Elimu, Uzoefu na Sifa husika.

Kuhusu nafasi za watumishi wa kawaida kwenye taasisi za Muungano, utaratibu wa muda wa mgao wa ajira uliokubalika kutumika ni asilimia 79 kwa Tanzania Bara na asilimia 21 kwa Tanzania Zanzibar. Utaratibu huu unatekelezwa kwa mujibu wa Waraka wa Serikali wa tarehe 10 Mei, 2013.

10. Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha​

Ushuru wa forodha ni kodi inayotozwa kwa bidhaa zote zinazoingizwa nchini toka nje. Ili kuwa na utaratibu mzuri wa kukusanya na kutumia kodi ya aina hii kwa maendeleo ya Watanzania wote iliamuliwa kuwa Ushuru wa Forodha unaokusanywa Zanzibar uwasilishwe kwenye Mfuko wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Idara ya Forodha ina jukumu la kudhibiti uhalali wa kuingiza na kutoa bidhaa nchini pamoja na kutayarisha takwimu za biashara ya nje (Foreign Trade Stastistics) kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya 1977.

11. Bandari, Mambo yanayohusika na Usafiri wa Anga, Posta na Simu​

Usafiri wa majini umeboreshwa kwa kuwaruhusu watu binafsi kutumia vyombo vya kisasa kusafirisha wananchi wa pande zote mbili kati ya Bandari za Dar es salaam, Tanga, Zanzibar na Pemba. Hali kadhalika hali ya mawasiliano ya simu imeendelea kukua kwa kasi kubwa katika pande zote mbili za Muungano. Mfano matumizi ya simu za viganjani na Makampuni ya simu hizo yanafanya kazi pande zote za Muungano bila vikwazo.

12. Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti); mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni​

Kabla ya Muungano, masuala ya sarafu na fedha yalikuwa yanasimamiwa na Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki iliyojumuisha nchi za Yemen, Somalia, Zanzibar, Tanganyika, Kenya na Uganda. Mwaka 1964, Bodi hiyo ilivunjika na kusababisha kila nchi kuwa na sarafu yake ambapo Tanganyika na Zanzibar zilikubaliana kuwa masuala ya sarafu na sera za fedha kuwa Mambo ya Muungano.

Kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha Benki Kuu ya Tanzania kupitia Sheria ya Mabenki ya mwaka 1965. Jukumu la msingi la Benki hiyo ni kuandaa na kutekeleza Sera za Fedha zinazolenga kutunza thamani ya fedha na kudhibiti mfumuko wa bei ili kuchochea ukuaji uchumi nchini.

Muundo wa Benki Kuu una sura ya Muungano, hii ikiwa na maana ya kuwa na watumishi toka pande zote za Muungano. Benki Kuu pia imejenga Tawi lake Zanzibar kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi. Aidha, Zanzibar inaendelea kupata gawio la asilimia 4.5 kutokana na faida inayotokana na shughuli za Benki Kuu.

13. Leseni za Viwanda na Takwimu​

Shughuli za Leseni na Takwimu za Viwanda zipo chini ya Wizara ya Biashara na Viwanda ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na chombo cha utekelezaji ni Mrajisi wa Viwanda na Bodi ya utoaji wa Leseni za Viwanda.

Mrajisi wa Viwanda na Bodi ya utoaji wa Leseni za Viwanda wanashirikiana na Naibu Msajili wa Viwanda Zanzibar. Aidha, BRELA imeendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kila inapohitajika. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina wajumbe wawili katika Bodi ya Leseni za Viwanda.

14. Elimu ya Juu​

Kwa mujibu wa Sheria Na. 25 ya Mwaka 1978, Elimu ya juu ni mafunzo yatolewayo baada ya kumaliza mafunzo ya cheti cha kuhitimu kidato cha sita au elimu nyingine inayofanana na hiyo ambapo mhitimu hutunukiwa shahada ya kwanza au Stashahada ya juu.

Elimu ya Juu ilikuwa ni mojawapo ya maeneo yaliyopewa kipaumbele baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kabla ya Muungano, Zanzibar haikuwa na Chuo Kikuu hata kimoja wakati Tanganyika ilikuwa na Chuo Kikuu kimoja tu ambacho ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoanzishwa tarehe 25 Oktoba, 1961 kikiwa Chuo

Kishiriki cha Chuo Kikuu cha London, Uingereza. Hali hiyo ilisababisha wananchi wa pande mbili kutafuta fursa za masomo nje ya nchi, hususan Makerere – Uganda, Royal Technical College Nairobi – Kenya, na wachache katika nchi za Ulaya, India na Afrika Kusini. Mwaka 1963, Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam kilijiunga na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Makerere na Nairobi na kuunda Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki.

Kwa kutambua umuhimu wa kuwa na wataalamu wazalendo wa fani mbalimbali na kujenga uwezo wa ndani kielimu, mwaka 1967 Serikali iliamua kuingiza suala la Elimu ya Juu katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ilipofika tarehe 1 Julai, 1970 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu kamili na kuanza na wanachuo 1,283 baada ya kuvunjwa kwa Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki mwaka 1970. K atika miaka ya 1970 na 1980 vyuo vya elimu ya juu viliongezeka ambapo, Chuo cha Maendeleo ya Uongozi (Institute of Development Management - IDM) Mzumbe kilianzishwa mwaka 1972, na kilipandishwa hadhi kuwa Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 2001. Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilianzishwa mwaka 1984 na Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2006. Kwa upande wa Zanzibar, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kilianzishwa tarehe 26 Septemba, 2001.

Kupitia vyuo vya elimu ya juu vya ndani, Serikali imetoa wataalamu wa fani kama za udaktari, uhandisi, uchumi, sheria na ualimu. Pamoja na fursa za elimu ya juu zinazopatikana katika vyuo vya elimu ya Juu nchini, Serikali inasimamia masuala ya ufadhili unaotolewa na nchi na mashirika mbalimbali kwa Watanzania kuongeza fursa za masomo nje ya nchi.

Mwaka 2005, Serikali ilianzisha Tume ya Vyuo Vikuu ili kudhibiti ubora wa elimu ya juu nchini kwa kusimamia ubora wa mazingira ya kufundishia, majengo, mitaala, walimu na taratibu za mitihani. Tangu kuanzishwa kwake, udahili wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu kutoka pande zote za Muungano hufanyika kwa kuzingatia vigezo muhimu vinavyowawezesha kusoma katika vyuo wanavyopata nafasi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

15. Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya Motokaa na Mafuta ya aina ya Petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na Gesi asilia​

Suala hili liliingizwa kwenye mambo ya Muungano mwaka 1968. Kwa upande wa Tanzania Bara, suala hili linasimamiwa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania lililoanzishwa chini ya Sheria ya Petroli Sura ya 392 (The Petroleum Conservation Act, Cap 392) na Sheria ya Utafutaji wa Mafuta ya Petroli (The Tanzania Petroleum Exploration and Production Act, Cap 17). Kwa upande wa Zanzibar, suala hili linasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati.

Kulikuwa na hoja ya namna ya kugawana mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia itakapopatikana. Serikali zetu baada ya kujadiliana, ziliamua kumtumia mshauri

mwelekezi AUPEC ya Uingereza ili atoe ushauri wa kitaalam kuhusu mgawanyo wa mapato ya rasilimali ya aina hiyo kwa nchi zilizoungana. Kampuni ya AUPEC ilikamilisha kazi hiyo na kuwasilisha mapendekezo kwa Serikali zetu mbili.

Sheria zimetungwa ikiwemo Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 ya SMT ambayo ilifuta sheria ya zamani, Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta Sura ya 328 na kuipa Zanzibar Mamlaka ya kuanzisha chombo/vyombo kusimamia masuala ya mafuta na gesi asilia kwa kutumia Sheria ya Zanzibar. Hivyo, Zanzibar ilitunga sheria yake ya Mafuta na Gesi Asilia mwaka 2016.

16. Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za Baraza hilo​

Usimamizi wa mitihani ya elimu ya sekondari unafanywa na Serikali kupitia Baraza la Mitihani la Taifa ambalo ni chombo cha Muungano. Baraza la Mitihani la Taifa lilianzishwa kwa Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa, Sura Namba 107, kufuatia kujitoa kwa Zanzibar katika Bodi ya Mitihani ya Afrika Mashariki mwaka 1970 na Tanzania Bara mwaka 1971. Kufuatia uamuzi wa kujitoa katika Bodi hiyo, Serikali hizo mbili ziliendelea kushirikiana katika masuala ya mitihani hadi mwaka 1977 ilipoamuliwa kuwa miongoni mwa Mambo ya Muungano.

Chombo hiki kipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi kubwa ya Baraza la Mitihani ni kutunga na kusahihisha mitihani kwa pande mbili za Muungano isipokuwa kwa mitihani ya kidato cha tatu ambayo hutungwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baraza la Taifa la Mitihani linaendeshwa na Bodi ya Wakurugenzi ambapo Zanzibar ina wajumbe katika Bodi hiyo. Aidha, Baraza huajiri watumishi kutoka pande zote mbili za Muungano ili kuwa na uwiano wa watumishi.

17. Usafiri na usafirishaji wa anga​

Hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga hii ikiwa ni pamoja na kuuboresha uwanja wa ndege wa Zanzibar, kufungua Ofisi ndogo ya msaidizi wa Mamlaka ya usafiri wa anga Zanzibar na kuruhusu mashirika ya watu binafsi kuendesha biashara ya usafiri na usafirishaji. Aidha, suala la usimamizi, udhibiti na Sera ya usafiri na usafirishaji wa anga vimeendelea kusimamiwa na kuratibiwa vizuri katika sura ya Muungano.

18. Utafiti​

Suala la Utafiti linasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria No 7 ya Mwaka 1986 ambayo hutumika pia Zanzibar. Bodi ya usimamizi wa Tume ina wajumbe kutoka Pande zote mbili za Muungano.

19. Utabiri wa Hali ya Hewa​

Chombo hiki kinasimamiwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa chini ya Wizara ya Miundombinu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ushirikiano kati ya Ofisi za Mamlaka zilizopo Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara ni mzuri.

20. Takwimu​

Kila upande wa Jamhuri ya Muungano una Sheria na Idara yake ya kusimamia shughuli za Takwimu, hata hivyo wakati wa kuhesabu watu (census) Idara hizo mbili zinafanya shughuli hiyo kwa pamoja.

21. Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano​

Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano inasikiliza kesi zinazohusu masuala yote isipokuwa kesi zinazotokana na masuala ya dini ya Kiislamu zilizoamuliwa kwa upande wa Zanzibar. Mahakama ya Rufani ina vituo saba kwa Tanzania nzima ambayo ni:- Dar es Salaam (Makao Makuu); Mwanza; Dodoma; Arusha; Zanzibar; Mbeya; na Tanga.

22. Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana na navyo​

Kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuruhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992 na kutungwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura Namba 258, suala la uandikishaji wa vyama vya siasa liliorodheshwa miongoni mwa Mambo ya Muungano. Mara baada ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilianzishwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo ilianza kutumika tarehe 1 Julai, 1992.

Hadi kufikia mwaka 2020 Vyama 21 vimesajiliwa na vimeshiriki kikamilifu katika masuala mbalimbali ya kisiasa Nchini. Aidha, Ofisi ya Msajili wa Vyama imefungua tawi la Ofisi zake Zanzibar ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia vyama vya Siasa pande zote mbili za Muungano.

 
Kuhusu:
15. Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya Motokaa na Mafuta ya aina ya Petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na Gesi asilia

Mbona tunaambiwa hili limeshaondolewa katika mambo ya muungano, ina maana hili liliondolewa kinyemela bila kupelekwa bungeni kwanza ili kupata 2/3 ya wabunge wa Tanganyika na 2/3 ya wabunge kutoka Zanzibar?

Kuhusu:
1. Katiba ya Tanzania na Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mbona sasa katiba ya Zanzibar inapingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibr. Kwa mfano katiba ya JMT bado inatambua kuwa Zanzibar kuna Waziri kiongozi, wakati Katiba ya Zanzibar inayotumika sasa ndani mwake hakuna cheo cha Waziri kiongozi

Halafu mbona katiba ya Zanzibar inasema kuwa Zenji ni nchi, wakati katiba ya JMT inasema kuwa nchi ni JMT?

Kuhusu:
21. Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano

Kama mahakama ya rufaa ni Jambo la Muungano, mbona Katiba ya Zanzibar imeweka wazi baadhi ya makosa kuwa kama yakiamuliwa na mahakama kuu ya Zanzibar basi hayatakatiwa rufaa katika mahakama yoyote nchini, yakiwemo makosa yanayohusu haki za binadamu. Sasa hapo unawezaje kusema kuwa Mahakama ya rufaa ni chombo cha muungano 100%?
 
Kuhusu:
15. Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya Motokaa na Mafuta ya aina ya Petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na Gesi asilia

Mbona tunaambiwa hili limeshaondolewa katika mambo ya muungano, ina maana hili liliondolewa kinyemela bila kupelekwa bungeni kwanza ili kupata 2/3 ya wabunge wa Tanganyika na 2/3 ya wabunge kutoka Zanzibar?

Kuhusu:
1. Katiba ya Tanzania na Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mbona sasa katiba ya Zanzibar inapingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibr. Kwa mfano katiba ya JMT bado inatambua kuwa Zanzibar kuna Waziri kiongozi, wakati Katiba ya Zanzibar inayotumika sasa ndani mwake hakuna cheo cha Waziri kiongozi

Halafu mbona katiba ya Zanzibar inasema kuwa Zenji ni nchi, wakati katiba ya JMT inasema kuwa nchi ni JMT?

Kuhusu:
21. Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano

Kama mahakama ya rufaa ni Jambo la Muungano, mbona Katiba ya Zanzibar imeweka wazi baadhi ya makosa kuwa kama yakiamuliwa na mahakama kuu ya Zanzibar basi hayatakatiwa rufaa katika mahakama yoyote nchini, yakiwemo makosa yanayohusu haki za binadamu. Sasa hapo unawezaje kusema kuwa Mahakama ya rufaa ni chombo cha muungano 100%?
Ndio maana Katiba mpya ni muhimu sana !!
 
Back
Top Bottom