Yah: Kuunga mkono CHADEMA kwa sasa

WanaJF,

Kwa muda nimekosa kuchangia ndani ya jukwaa hili, hata hivyo nimevutwa na mjadala huu unaondelea kuandika machache. Yapo makundi makubwa mawili ya mawazo katika michango mbalimbali inayotolewa; upande mmoja ni wale wanaojenga hoja kwamba jambo la msingi la kwanza kabisa ni KUINDOA CCM MADARAKANI na mengine yatafuata; kundi la pili ni lile linalotaka kwanza MBADALA WA CCM UONEKANE BAYANA KWANZA na ndio iwe sababu na msingi wa kuiondoa CCM madarakani. Kundi hili linataka swali la nini kinafuata baada ya kuiondoa CCM madarakani litangulie kabla ya uamuzi wa kuindoa CCM madarakani. Kwa maoni yangu, nakubaliana na wenye mtizamo kwamba mambo yote haya mawili yanapaswa kwenda sambamba ama kwa pamoja; yote ni muhimu na yote yanahitajiana.

Kwa hatua ambayo nchi yetu imekifikia hivi sasa ya dola kutekwa (state capture) na chama kinachotawala kufunga fungate na ufisadi/mafisadi ni dhamira yoyote ya kuleta sera na uongozi mbadala haiwezi kutimia bila kubadili mfumo wa utawala. Utatu uliopo baina ya watendaji wa serikali kwa upande mmoja, wanasiasa viongozi wa kuchaguliwa na wananchi na viongozi wa chama kwa upande mwingine na maslahi ya kibiashara ya ndani na nje ya nchi kwa upande wa tatu; mkazo wowote wa kufikiria sera unakuwa ni mchezo wa kinadharia kama hautaenda sambamba na kubadili mfumo wa utawala labda kama kubadili huko mfumo wa utawala kuwe ndio sera yenyewe.

Katika hali iliyofikia sasa kuiondoa CCM madarakani ambayo ni sawa na kuikomboa dola iliyotekwa kunaonekana kuwa ni suala la lazima na la dharura kwa ajili ya demokrasia, maendeleo na hata kudumisha usalama na amani ya nchi ambayo inaelekea kuwa mashakani siku za usoni kama hali itaendelea kama ilivyo sasa.

Lakini katika kutekeleza azma hii, vipo vyama vimeonyesha uthabiti na uthubutu wa kuwa mbadala, CHADEMA ikiwa moja ya tumaini jipya la watanzania ndio maana naamini mjadala huu umejikita katika chama tajwa. Unaweza kujiuliza kwanini katika msururu wa vyama kumi na nane (18) vya Tanzania, mabadiliko ya kweli yaonekane yanaweza kupatikana kupitia CHADEMA?

Harakakati za kisiasa zilizofanywa na CHADEMA ndani na nje ya Bunge kwa kushirikiana na vyombo vya habari na wadau wengine waliokubali kutanguliza mbele maslahi ya taifa kwa zimesalisha AJENDA ya kisiasa-ambayo imepewa jina la ‘mapambano dhidi ya ufisadi na kutetea rasilimali za taifa’ ambayo yamefanya uwajibikaji katika utawala kutazamwa kama moja ya sera za muhimu sana za taifa letu.

Naamini jambo hili lisingepata mafanikio ya kutosha kama CHADEMA kwa upande wake isingekuwa na misingi mizuri ya uongozi na ya kisera tangu kuasisiwa kwake. Kama falsafa, itikadi na sera za CHADEMA zingekuwa kinyume sana na matarajio tunayoyatazamia harakati hizi za miaka ya karibuni zingeonekana kama kiini macho ama upepo wa wakati.

(Falsafa, itikadi na malengo ya chama yanaweza kutazamwa kupitia katiba ya chama ambayo inapatikana pia katika mtandao www.chadema.or.tz, pia katika mtandao huo inapatikana ilani fupi(popular version) ya CHADEMA ya mwaka 2005)

Hata hivyo katika nchi yenye uoza katika utawala kwa kiwango cha Tanzania taasisi zake nyingi huru- si CHADEMA tu, hujikuta katika hali ya kupinga uozo iliopo na kukosoa badala ya kutumia muda mwingi zaidi katika kueleza mbadala na kutoa matumaini. Huu ni mtego wa kawaida kwa silika ya binadamu na ubinadamu na taasisi zake; huwezi kwenda eneo lenye rundo la takataka kubwa kuliko usafi uliopo ukazungumza usafi kabla ya kuzungumzia kuondoa uchafu. Katika mazingira hayo unaweza kujikuta unazungumzia kuliondoa rundo la taka kabla hata ya kufikiria utafanya nini mbadala baada ya kuliondoa.

Lakini maelezo haya hayaondoi wala kupinga umuhimu wa swali la msingi lililoulizwa; kwamba CHADEMA ITAFANYA NINI IKIINGIA MADARAKANI ama NINI TAIFA LITARAJIE KUTOKANA NA MABADILIKO YA MFUMO WA UTAWALA?

Jibu la muda mrefu la swali hili linapatikana katika misingi ya muda mrefu ya kifalsafa, kiitikadi, kisera, kimalengo na kitaasisi ya CHADEMA. Je, misingi hii haitoi tumaini kwa watanzania na dira ya mabadiliko ya kweli? Ni maeneo gani yanayohitaji kuboreshwa zaidi? Hapa ni muhimu badala ya viongozi wa CHADEMA kujibu, mawazo yangetoka kwanza kwa wanachama na wananchi kwa ujumla. Naamini viongozi wa CHADEMA wapo tayari kusikiliza.

Jibu la muda mfupi linapatikana katika ilani ya uchaguzi (2010-2015) ambayo kutokana na misingi ya muda mrefu na hali ya taifa ya sasa inapaswa kutolewa; jibu ya swali hili kwa maoni yangu hawawezi kulitoa kwa ukamilifu wake leo kwa kuwa chama bado hakijazindua ilani yake ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Chama kiko kwenye mchakato wa majadiliano na mashauriano ya ndani (consultations), kabla ya kupata maoni ya nje na kabla ya kupitisha ilani katika vikao vya kikatiba vya chama ambavyo ni kamati kuu, baraza kuu na mkutano mkuu.

Hivyo, chama kiko wazi kupokea maoni kuhusu nini ambacho wanachama na wananchi kwa ujumla wangependa kitiliwe mkazo katika ilani ya CHADEMA. Hivyo, nawaomba wote ambao mngependa kushiriki katika kupanga CHADEMA IFANYE NINI IKIINGIA KWENYE UONGOZI au TAIFA LITARAJIE NINI KUTOKANA NA MABADILIKO YA MFUMO WA UTAWALA mtuandikie; unaweza kuandika kupitia info@chadema.or.tz, nakala kwa slaa@chadema.or.tz na mnyika@chadema.or.tz ama unaweza kumtumia kiongozi mwingine wa CHADEMA.

Kwa tafsiri rahisi, chama cha siasa ni jumuia ya watu wenye dhamira inayoendana wenye kulenga kuchukua mamlaka ya dola kupitia uchaguzi ama njia nyingine za kidemokrasia kwa lengo la kuitekeleza azma hiyo. Kwa hiyo badala ya kuhoji tu, CHADEMA itafanyaje ama taifa litarajie nini ni muhimu kushiriki katika kuamua hatma yako na ya taifa kwa ujumla. Badala ya kusubiri chama kutoa ilani na baadaye kuikosoa ama kuikana ni muhimu kushiriki katika kuiandika.

Nitaomba kwa kadiri inavyowezekana mawazo ya awali ya ujumla yafike kabla ya tarehe 20 Julai 2010. Mawazo mahususi yanaweza kutolewa katika hatua za baadaye kwenye rasimu kabla ya mkutano mkuu wa chama ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Agosti. Hata hivyo, kuna mtanziko(dilemma) katika mchakato wa utengenezaji wa ilani kwa kuwa kwa upande mmoja unaweza kuwa na shauku ya kumhusisha kila mtu/mwanachama katika hatua zote lakini kwa upande mwingine unataka baadhi ya mambo katika ilani yawe siri hususani yale yenye ubunifu wa pekee ili yazinduliwe wakati wa kampeni au wakati wa karibu na uchaguzi kuweza kumsha hamasa ya kuungwa mkono; changamoto ipo katika kuwianisha(balancing) matakwa hayo mawili. Najua vipo vyama ambavyo vimeshazindua ilani zao, CHADEMA itafanya hivyo kwa kadiri ya ratiba yake ambayo ilishaitangaza toka Aprili 27 mwaka huu. Nawatakia mjadala mwema

JJ

Pamoja mkuu tumekuelewa.
 
Wakuu,

Naona wengi wamekazana sana kumjibu Mzee Mwanakijiji kwa madhumuni ya kutaka ‘kumshinda’ kwa hoja kiasi cha ku-miss points muhimu zinazoletwa na wachangiaji wengine.

Nampongeza Mwanakijiji, aelewe kwamba kichwa chake kimejaa ubongo na anayoyatoa humo kichwani na moyoni mwake yanachoma kama nchi ya mkuki ndio maana watu hawaishi kukereketwa na kumjibu.

Kijana ‘wetu’ Mnyika ameandika maneno ambayo yanastahili kusomwa kwa makini na kutolewa mchango. Aliyoandika Mnyika yana mantiki. Lakini nimeshangaa kidogo kusoma kwamba mpaka leo hii tunapokaribia kabisa uchaguzi CHADEMA bado kiko kwenye “mchakato wa majadiliano na mashauriano ya ndani kabla ya kupata maoni ya nje na kabla ya kupitisha ilani katika vikao vya kikatiba vya chama ambavyo ni Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu.”

Nilitarajia kwamba chama ‘kikuu’ kama CHADEMA ambacho kina umri wa zaidi ya miaka 10 na kina uelewa mpana wa matatizo ya wananchi na taifa na udhaifu uliopo ndani ya CCM na utawala wake kwa ujumla, kingekuwa tayari kimeishabainisha na kuainisha yale muhimu ambayo yanapaswa kuingia katika Ilani yake ya uchaguzi na bila kigugumizi kinaweza kutueleza kitatufanyia nini endapo kitapata ridhaa ya wananchi kuongoza taifa bila kungoja 'rubber stamp' ya vikao vya juu vya Chama.

Kwa kifupi viongozi wa CHADEMA wangekuwa tayari wameishatafuta maoni wanayoyataka yatolewe sasa na wangekuwa wameishapanga CHADEMA kikipata ushindi kitawafanyia nini wananchi au Taifa litarajie mabadiliko ya aina gani ya mfumo wa utawala wa CHADEMA. Kututangazia sasa kwamba majibu ya maswali yanayoulizwa yasubiri kukamilika kwa ilani na kwamba watu wapeleke maoni yao ni kudhihirisha upungufu uliopo wa kimkakati.

Lakini zaidi ya yote, katika kipindi hiki cha kuelekea kutafuta ridhaa ya wananchi nilitarajia kwamba CHADEMA kingelikaa chonjo na kufuatilia kwa makini na kwa kina nyendo za CCM katika matayarisho yake na harakati za kuelekea kwenye mikutano ya CCM ya uteuzi wa wagombea. Kwa kufanya hivyo, CHADEMA kama chama cha upinzani wangeliweza kuyadaka mapungufu yote na mizengwe yote iliyojitokeza kwenye mikutano hiyo ya CCM na mara moja kuyafanyia kazi mapungufu na mizengwe hiyo kwa madhumuni ya kukidhoofisha CCM kwa kukiumbua mbele ya wananchi. CHADEMA wangelikuwa wa kwanza kutoa matamko ama kwa kuwahutubia wanachama wao na wananchi. Cha kusikitisha ni kwamba kazi hiyo ikaachiwa ifanywe na magazeti na waandishi mmoja mmoja. Matokeo yake maandishi ya kwenye magazeti yamekuwa na impact kwa wale tu walioweza kusoma magazeti hayo. Na kubwa zaidi, mapungufu ya CCM yamekuwa yakizungumziwa zaidi Mwenyekiti wa CCM yenyewe badala ya viongozi wa upinzani kuwa wa kwanza kuyaanika kwa wananchi!

Kuhusu itikadi: Itikadi ya Chama cha TANU ambayo nadhani CCJ ‘damu’ walijaribu kutaka kuifufua – UJAMAA na KUJITEGEMEA ni nyepesi zaidi kueleweka kwa wananchi kuliko mambo ya “MRENGO WA KATI.” Mvidunda mwenzangu kule kijijini ukienda kujinadi kwake kwa itikadi ya 'mrengo' ili akuchague, hata umueleza mara mia maana ya siasa za ‘Mrengo wa Kati’ katu hataweza kukuelewa. Lakini, mgombea (wa CCJ) kwa kutaja neno 'KUJITEGEMEA' tu mara moja mvidunda angeelewa wazi kwamba itikadi hiyo inamtaka ajitegemee, akazane kulima mpunga ili apate chakula cha kumtosha na wanawe ili asiombe kwa jirani na cha ziada auze apate kujitegemea. Katika kujenga hoja zetu za ‘kisomi’ za mirengo, tukumbuke kwamba hao ‘wavidunda’ wenzetu ni wao watakaokwenda kujipanga kupiga kura na hatimaye kuirudisha madarakani CCM ‘yao’ waliyoizowea kwa sababu mirengo ya kushoto, kulia ama kati haiko katika misamiati yao!
 
Wakuu,

Naona wengi wamekazana sana kumjibu Mzee Mwanakijiji kwa madhumuni ya kutaka ‘kumshinda’ kwa hoja kiasi cha ku-miss points muhimu zinazoletwa na wachangiaji wengine.

Nampongeza Mwanakijiji, aelewe kwamba kichwa chake kimejaa ubongo na anayoyatoa humo kichwani na moyoni mwake yanachoma kama nchi ya mkuki ndio maana watu hawaishi kukereketwa na kumjibu.

Ndugu yangu,JF tangu mwanzo wake ilikuwa sehemu ya mjadala.Hicho unachotafsiri kama "kukazana sana kumjibu Mzee Mwanakijiji kwa madhumuni ya kutaka ‘kumshinda’ " ndio indeed unapo-miss point.Hakuna mashindano wala kutafuta mshindi bali tunafanya mjadala kwa maslahi ya Taifa letu sote.Hakuna Mtanzania mwenye exclusive rights za kuijadili Tanzania yetu pasipo wengine kuwa na haki hiyo.Tujadili hoja si watu wanaotoa hoja,whether za kuafiki au kupinga.

Naamini pia kila aliyechangia,aidha kwa kuafikiana na Mwanakijiji au kupingana na mtizamo wake ana ubongo uliojaa,vinginevyo asingemudu kutumia keyboard kuandika alichoandika,let alone kuweza kufungua tovuti ya JF.Kadhalika,ni imani yangu kuwa kinachowachoma watu ni hatma ya nchi yetu na si vinginevyo.

Hivi kuna ugumu gani katika kuwasilisha ujumbe au kutoa hoja pasipo ku-entertain lugha zinazoweza kutafsiriwa kama abusive?We could always agree to disagree pasipo haja ya kutumia provocative language.
 
mnyika kasema wewe unayeuliza what next,mimi na yule wote tushiriki kushauri what next "kuwa sehemu ya mabadiliko ".
 
Bibi Ntilie,
Nadhani hata wewe umeshindwa kuelewa hatua tuliyopo sasa hivi. Hii ni hatua ya kwanza ambayo tunataka kununua hilo shamaba kwa msemo wa Mwanakijiji,.Hii ikiwa ni kukutaka wewe ujumuike nasi kuwa mbia kukiwezesha chama kipate vijana wenye uwezo wa kufikiri,kuongoza na ushawishi ili chama hiki kipate nguvu na uwezo wa kusimama dhidi ya CCM itakapo fikia Uchaguzi..

Kama nilivyosema hii hatua ya kwanza na kichecheo cha wewe na wengine wote kujiunga ndio hiyo falsafa ya mageuzi yanayokusudiwa na sisi sote toka tukae hapa kijiweni miaka karibu 10 iliyopita. Mbiu hii ni tofauti kabisa na fikra za kwamba Chadema inaomba kura zenu. Maswali mengi ya Mwanakijiji yameegemea hatua ya pili, hatua ya kuwashawishi wananchi ili wawape kura zao.. Tofauti na ile ya kwanza hatua hii haihitaji mtu yeyote kuwa mwanachama wa Chadema kuwapa support yao (kura)..hapa ndipo unakuta maswali mengi ya what next? ni hatua ya ushawishi kwa wananchi wote na ili waichague Chadema ndipo wanatakiwa kuanika vipaumbele vyao kwa wananchi..

Hivyo basi tungo zote za ilani za chama na zile wa wagombea wake zitaweza kupatikana baada ya kuwa na wajenzi ambao ni wewe na mimi tutashiriki. Ndipo (what next na what have you done for me lately) zinapojengwa kutokana na nguvu na uwezo wa chama kusimamisha wagombea nafasi za uongozi.
Na kama nilivyosema mwanzoni yawezekana kabisa wewe na wengine woote mkasimama nafasi za Udiwani, Ubunge au hata kiti kikuu maadam muda wetu hapa kijiweni unapata nafasi ya kuwafikia wananchi jukwaani..tunatoka ktk maneno ya kijiweni JF na unafanya mavituz.

Hii ndio nafasi pekee ya wewe Mtanzania msomi mwana JF kujiunga ktk msafara huu badala ya kudandia bus jambo ambalo wengi hushindwa hata kupiga kura kwa sababu walipitwa na hatua ya kwanza hivyo hawaoni umuhimu wa kupiga kura. I bet U ukijiunga na nguvu hii ni lazima utapiga kura... na utaona umuhimu wa wewe kupiga kura yako kwa sababu wewe ni mhusika zaidi ya kuitaka haki isiyokamatika..

Chadema hawana haja wala sababu ya kuwa na Ilani leo hii kwa sababu bado wanawaiteni nyote mjumuike ktk hatua hii nahakika hata wale woote waliojiunga na CCM iwe London, au huko Dodoma hawakuwa wajinga kujiunga pasipo kujua What next...isipokuwa walijiunga kwa imani ya roho zao kama Ubatizo, what next mnakwenda nyumbani kula mpunga na baada ya hapo ni ibada tu zinazotakiwa ili upate wokovu wa roho na huku kwenye siasa unapata wokovu wa kimwili kutokana na adha za utawala wa CCM.

Ni muhimu zaidi kuelewa kwamba Rushwa itawezekana kupigwa vita tu ikiwa wewe mwenyewe una imani ya kuipinga na tusitegemee Chadema chama na itikadi zake ndizo zitaweza kuondosha rushwa isipokuwa nyie vijana viongozi wa kesho..Zingatia sana maneno ya Mpendazoe aki m quote Albert Einstein..Pia naongezea ya Barak Obama - 'Change will not come if we wait for some other person or some other time. We are the ones we've been waiting for. We are the change that we seek."
 
Wakuu,
Awali ya yote napenda kusema kuwa mjadala wenye mgongano wa mawazo una afya na tija.Ningeshangaa sana kama wote tungekuwa na uelekeo mmoja kuhusu mada hii. Lakini wakati joto la mjadala likipanda na busara zitawale.
Hapa sioni kama kuna mashandao,bali ni hoja zenye nguvu.
Nianze na hoja ya ''what next'', mimi nadhani swali hili lina maana moja, kuwa ukiiondoa CCM halafu ukawa na TLP mathalani,je hii si kutia mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya!!
MM anafikira zenye mantiki kuwa sera madhubuti ndizo zitain'goa CCM na kuweka mwelekeo na mustakabali wa taifa katika njia sahihi. Mimi ninakubaliana na kutofautiana na MM kwa mambo mawili.
1: Ni kweli sera ndio dira na hatima ya taifa. 2: Sikubaliani kuwa kwa muumdo wa nchi yetu ni lazima sera ing'oe CCM. Sababu. a] CCM ndio wanaomiliki vyombo vya dola,ushahidi wa kiamzingira,iweje mkuu mmoja wa polisi atangaze kugombea ubunge CCM na kusema yeye ni mwananchama wa muda mrefu wa CCM ili hali amestaafu mwezi december mwaka jana. Hii ina maana alikuwa kamanda wa kikosi cha polisi akiwa mwanachama wa CCM. Sheria inaruhusu? haki ipo hapo?
b] Iweje msajili wa vyama awe msemaji wa ikulu pia[ kikwete anatania hakusema...]
c] Iweje mkuu wa tume ya uchaguzi achaguliwe na mwenyekiti/rais wa nchi
d] Hivi hamkuona mahakama ikijivua wajibu,sasa mpinzani apeleke wapi kesi?

Mwaka 1995 NCCR waliingia kwa nia ya kuing'oa CCM, bila kujua kuwa uwanja si sawa
[level field]. matokeo yake box la kura kutoka city centre kwenda fire likachukua masaa 12,uchaguzi ukavurugwa Dar, CCM wakapeta.

Hata kama kuna mgombea urais kwa mazingira yaliyopo sijui atakwepa vipi off side na rafu za CCM kwa sababu wao ndio kila kitu.
Makosa haya wapinzani wameyafanya miaka 20 sasa.

Mabadiliko yaanzie wapi!! jibu ni kuingiza wabunge wengi kadri inavyowezekana. Pamoja na rafu lakini wapinzani wakiweza kuzuia 2/3 majority hapo kuna mwelekeo. Hebu fikiri,kama Dr Slaa ameitikisa serikali na kurudisha sheria ya uchaguzi,je tukiwa na akina Slaa 100 hali itakuwaje. Hapo ndipo wapinzani wanaweza sema, mkuu wa TAKUKURU,Majaji, mkuu wa polisi,tume ya uchaguzi na msajili wa vyama wasiwe chini ya mtu mmoja ambaye ana sura mbili,mwenyekiti na rais, ili wawajike na kulinda haki za wanyonge. Jiulize kwanini Hosea amekingiwa kifua pamoja na madudu yote yaliyotokea!!
Wakati mkakati huo unaendelea then sera zinaendelea KUBORESHWA ili zikidhi mahitaji wakati muafaka ukifika. Kama mkakati wa [level field] ukifanikiwa sasa CCM iingie uwanjani na wapinzani kila mtu anadi sera zake,hapo Sera na kuing'oa CCM ni asilimia 90%.

Chadema: Kuhusu sera mimi nadhani siasa wakati fulani timing, lakini pia Chadema waelewe kuwa muda si mshiriki mzuri na kuzingatia kuwa asilimi 70% ya wananchi wetu wanashangilia hata mishahara ikipunguzwa,pengine umakini na muda vinahitajika. Lakini sijui ni kwanini Operesheni sangara ambzao zilikuwa zinawagusa wananchi ziliachwa! sijui, maana ile ndio sera wanavijiji wanaielewa.
Watu wote hawawezi.

Nahitimisha kwa kusema, politics inahitaji patience na strategy. Ni procedure inayohitaji umakini sana. Lengo la kwanza liwe kuvunja miguu ya CCM bungeni ili kuwe na uwanja sawa[level field] utakaowezesha kuuza sera makini kwa njia halali. Bunge ndipo pa kuanzia.

Tukumbuke kuwa kwa wenzetu ambao tume ya uchaguzi,polisi, mahakama ni vyombo huru, SERA ndio silaha ya kutwaa dola. Hapa kwetu haiwezekani. Itawezekana tu kama kutakuwepo na mabadiliko ya mfumo utakaowezesha vyombo hivyo kuwa huru. Fikiria bunge kwanza!
Vinginevyo tume ya uchaguzi itasema chama X [chenye sera makini] kinakiuka taratibu, msajili atakifuta chama hicho, polisi watawakamata wanachama wa chama hicho kwa kuvuruga amani na utulivu, mahakama itawahukumu wanachama wa chama X kwa sababu makosa yao ni ya jinai na si KISIASA, Chama X chenye sera makini kitatoweka! nchi itabaki na jembe na Nyundo, na umasikini.

Ahsanteni
 
Nguruvi3, tunaweza kuongoza nchi bila sera? Yaani tunawafuata watu tu alimradi wanasema wao ni bora kuliko waliokuwepo kabla?
 
MM, ukisoma vizuri ninachokiandika nakubaliana na wewe asilimia 100% kuwa ni lazima kuwe na sera. Ninachotofautina na wewe ni kuwa si uzuri wa sera tu utaing'oa CCM ni lazima tuangalie factors zingine. Na mara zote nimeungana na wewe kwa uwepo wa sera tena makini, hoja yangu ni kuwa bila kuangalia namna ya kupenyeza wabunge kwa hesabu za baadaye, sera hazitafanikiwa.
Kwahilo ndio maana nimeshangaa pia chama kama Chadema iweje hakijaweka sera hadi sasa? lakini si sera tu ni lazima uwepo mkakati wa ziada kuwa na wabunge wengi.

Nashukuru sana MM, mada uliyoanzisha ni nzuri sana

Ahsante
 
Nguruvi3, tunaweza kuongoza nchi bila sera? Yaani tunawafuata watu tu alimradi wanasema wao ni bora kuliko waliokuwepo kabla?

Mbona CCM wanaongoza bila sera (ie zipo lakini hazifuatwi na zinapofuatwa zinapindishwa kwa maslahi binafsi)?Kama CCM wanaweza kuongoza "bila sera" (kama nilivyobainisha kwenye mabano ya mwanzo) kwanini basi chama kingine kama chadema kisiweze kuongoza almradi focus yake ikiwa katika matendo na si maneno matamu in form of SERA?
 
Nguruvi3, tunaweza kuongoza nchi bila sera? Yaani tunawafuata watu tu alimradi wanasema wao ni bora kuliko waliokuwepo kabla?
MKJJ chukua muda kidogo umsome tena Nguruvi3 ameeleza vizuri tu kuwa na sera makini ni muhimu lakini kama hakuna [level field] tena kataja neno hili mara mbili ni ngumu sana kushinda uchaguzi. Sasa wewe kama husomi na kuwaelewa watoa mada utabaki kuuliza swali hilo moja kwa muda mrefu sana.

Hivi unaweza kutuambia ni chama gani ambacho hakina sera ili tuanze kukijadili na ikiwezekana tuwasiliane na uongozi wake. Kama kweli kuna chama cha aina hiyo na kinataka ridhaa ya wananchi kuongoza nchi nitakiita cha kipuuzi na viongozi wake ni wapuuzi hawajui wanachokifanya.

Ninavyojua mimi kila chama kina katiba na sera zake lakini ubora wa sera unatofautiana toka chama kimoja hadi kingine. Uandaaji wa sera unategemea itikadi ya chama na malengo yake. Kwa hiyo si sahihi kusema chama fulani hakina sera kwa vile tu huzikubaliani na matakwa yako.

Mathalani chukulia sera ya Majimbo CCM haina sera hiyo, sasa kwa vile CCM say 'chama chako' hisia tu hakina sera hiyo basi haifai pia kwa Chadema. Au kwenye ilani ya CCM say kuna Mahakama ya Kadhi, kwa vile Chadema hakuna Mahakama ya Kadhi basi ilani yake si nzuri. I think that is not a good way of making judgements, we judge on merits of an article and not on the absence of an article.

MKJJ kuliko kusema chama fulani hakina sera ni ustaarabu kuwa wazi kwa kutamuka sera za chama fulani haziniridhishi naridhishwa na sera za chama fulani. Ila kama unataka sera za Chadema gonga Sera, Katiba, Kanuni, Maadili na Itifaki za CHADEMA kama huridhishwi nazo sema huridhishwi nazo zitaboreshwa si sahihi kusema hakina sera. Na ni ustaarabu wa kibinadamu kukosoa na kushauri kuliko kukosoa na kukaa kimya.
 
tunaweza kuongoza nchi bila sera?
Yes and No, Nchi inaongozwa kwa kufuata katiba na sio sera, sera inavaliwa na kuvuliwa kama shati kila asubuhi. Ndio maana chama tawala chenye sera fulani kinaweza kikapigwa chini na chama kingine chenye sera pingamizi kikapewa uongozi, ndio maana ya Uchaguzi Mkuu.
Yaani tunawafuata watu tu alimradi wanasema wao ni bora kuliko waliokuwepo kabla?
Hawa ni watu gani unaowaongelea ambao unadai wanasema wao ni bora kuliko waliokuwapo bila kusema watafanya nini tofauti.

  • Kwanza, kwa kupinga tu yanayofanyika tayari Chadema wanaonyesha kuwa kuna kitu watafanya tofauti.
  • Pili, kwa kutoa katiba, kanuni, maadaili na sera tayari Chadema wanasema wataongoza nchi namna gani.
  • Tatu, kwa kujitokeza tu kugombea nafasi mbalimbali tayari wameonyesha kutoridhishwa na uongozi uliopo wa CCM
  • Nne, ilani ya Chadema ya uchaguzi inayosubiriwa bila shaka itatoa mwanga watatekelezaje mipango ya maendeleo kwa taifa.
Sasa Mwanakijiji, hawa unaowadhihaki kwa kudai tunawafuata tu na kuuliza wanataka kuiondoa CCM ili iweje, ni watu gani hao ?
 
Wakati akizungumzia mafanikio ya Awamu ya nne, Rais Kikwete alituambia Watanzania kuwa alitumia miaka 2 ya kwanza kujifunza kazi ya Urais. Hivyo tuilpompa dhamana ya kutuongoza kwa miaka mitano, katutumikia kwa miaka mitatu tuu, huku mingine akijifunza kazi.

Alipokuwa akigombea Urais mwaka 2005, Rais Kikwete aliwaambia wenzake wa CCM kuwa alikuwa na ujuzi na uwezo wa kuongoza nchi, akajinadi kwa Watanzania wote kuwa ana uwezo na tuafikiane na uamuzi wa CCM kumteua yeye kuwa mgombea Urais na kumpa Urais ili atuletee Ari, Kasi na Nguvu Mpya.

Leo hii, ukifanya tathmini ya utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Nne, kiuchumi, kijamii, kimaendeleo, kisiasa, masuala ya haki na zaidi umasikini, ujinga na maradhi, ni kana kwama kwa miaka mitano tumekuwa tukipiga hatua tatu mbele, kisha tunarudi saba nyuma, halafu tunapanda hatua tatu mbele, kama tuko kwenye bembea hatuna hakika kama tunasonga mbele au tunarudi nyuma!

Sasa ukitafakari kwa makini, hili la wapinzani na Chadema na mtazamo wa Watanzania wengi kuwa kwanza tuing'oe CCM, lakini inaelekea bado hatujajiandaa vya kutosha kuweza kuongoza tukishaiondoa CCM.

Si kwamba nadai CCM ibakie madarakani au isiondolewe, lakini kama Bibi Ntilie alivyobainisha kwenye barua ya Mnyika, yaelekea Chadema bado hawajajiandaa na hawajiamini kuwa wana uwezo wa kuongoza Taifa. Dua lao ni CCM ianguke, ndipo wao waanze kujifunza na kujipanga ni vipi waongoze Tanzania.

Ndiyo maana Mwanakijiji anauliza, then what?

Labda turudi kwenye historia ya kupata Uhuru wetu, tulipigania Uhuru tukataka tujitawale, lakini tangu tumepata Uhuru huo miaka karibu 50 sasa , tumekuwa sawa na ile merikebu iliyoweka nanga inayoyumba mbele nyuma kufuata mkondo wa bahari.

Binafsi nimekuwa nikihoji sana mambo ya Sera an Itikadi zinazoeleweka, majibu niliyoyapata ni kuwa Watu wana njaa hawahitaji Sera au Itikadi. Mkandara akanijibu ni suala la Watu na Mazingira.

Kwa miaka mitano iliyopita (wala sitaki kurudi nyuma kabla ya hapo), tumekuwa tukihubiri, chambua toa mawazo maoni na kila unachokifikiria kifanyike na kuwasihi Chadema wakifanye. Binafsi nimeandika zaidiya thread 4 kulenga uchaguzi huu. Nilianza pale Kikwete alipoapishwa, nikaandica Focus 2010, nikaja na Chadema must Reform, nikaandika Marshal Plan ya Mchungaji, nikatoa changamoto ya TAMISEMI 2009 na mwishowe ni Udhaifu wa Operesheni Sangara.

Sasa kama kwa miaka mitano nimekuwa nikijaribu kuwashawishi Chadema japo wanisikilize kauli na maoni yangu, na majibu ni kaambiwa eti siku kwenye ground kuchacharika, nami nikawaambia wanione kama Mwewe ambaye yuko angani akiangalia chini, halafu leo hii hakuna mwenye uhakika kama Chadema (hata Chadema yenyewe) kweli ina uwezo wa kushika dhamana kubwa ya kuongoza nchi, kwa nini basi swali la kuuliza "then what" liwe gumu?

Tuaing'oa CCM ili iwe nini? Ili kuondoa Ufisadi ndio jibu na a nyongeza ni kuleta maisha bora kwa Mtanzania. Tukiuliza kazi hii itafanyikaje, tunaambiwa msiulize maswali mengi, ngojeni kwanza tuing'oe CCM. Hilo ni jibu la kijinga na ni kudharau akili za Mtanzania kumfanya ni mtoto mdogo au mtu asiye na ufahamu wa lolote. Tena mbaya zaidi ni sawa na majibu ay ki-CCM yale ya kujifungia ndani ya NEC na CC ambapo kila kitu ni siri au lile la Serikali ya CCM kudai mikataba ya Uwekezaji ni siri ya Mwekezaji na Serikali Kuu.

Ikiwa mfupa wa TAMISEMI ambapo huko ndipo safu ya kwanza ya kuongoza nchi, Chadema walikukwepa wala hawakujituma kupata viti angalao nusu ya mkoa kama Dar, iweje leo tudhanie kuwa wataweza kuwa makini na uwezo wa kuongoza nchi kwenye Serikali Kuu na Bunge?

Kwangu mimi niionavyo Chadema, ni chama ambacho kipo kwenye mpito au mvutano wa kifalsafa ndani ya chama na wanafanya siri kubwa sana kuficha udhaifu huo. Dalili za hili zilionekana na Marehemu Chacha Wangwe na hata kwenye uchaguzi mkuu ambapo Zitto aligombea uenyekiti kisha akavutwa pembeni na kuamrishwa ajitoe.

Makovu haya hayaweza kusawazishwa pamoja na hili la sasa la kuvizia mabaki ya CCM yaanguke ndipo yaingie Chadema na kuhakikisha walau Chadema wanaweza pata viti 70 vya ubunge.

Ni kutokana na hayo, ndio maana nakubaliana na Mwanakijiji kuhoji je tukishaing'oa CCM, then what? Maana inaelekea kama vile tulivyopata Uhuru au vile Kikwete alipata Urais, bado hatujajiandaa kuongoza na hatujiamini kuwa tuna uwezo wa kutawala.

Kila udhaifu wa CCM umetolewa majukwaani, lakini hapajawahi tolewa alternative solution ambayo ikakubalika hata ndani ya Chadema yenyewe, kila mara tunaambiwa "Subirini tuingie Ikulu". Je ina maana Chadema na Upinzani hauwezi kuanza kuleta maendeleo Tanzania mpaka viingie Ikulu?

Miaka mitano, bajeti ya nchi imekuwa ikiongezeka na matumizi ya hali ya juu. Ripoti ya mkaguzi mkuu CAG kwa miaka mitatu inaonyesha udhaifu wa Serikali kuu ambao umeimarisha ubadhirifu na rushwa. Lakini sijasikia hata siku moja hoja ya kutungwa Sheria au kusitisha Bajeti kutoka kwa Upinzani ili Serikali ijirudi na kurekebisha mfumo wake wa matumizi na hata kubana matumizi. Je wajibu huu ambao kawaida hufanywa na Chama cha Upinzani kama haukufanywa na Chadema na wenzao, bado mtasema tusubiri wakiingia madarakani?

Labda nihitimishe kwa kutoa mtazamo mwingine. TUfanye kwamba Upinzani umeshinda Uchaguzi Mkuu kwa asilimia 51% hiyo 49% ni ya CCM, pale Bungeni na hata Urais ni wa Upinzani. Inapokuja kwenya ufanyako kazi na utekelezaji hasa kwenye ngazi za Tawala za Mikoa (TAMISEMI), watendaji wengi wa kisiasa takriban asilimia 95% ni CCM ambao walishinda Udiwani na uchaguzi wa TAMISEMI 2009. Je Upinzani utawezaje kufanya kazi yake kwa ukamilifu bila mvurugano na hawa watu wa CCM ambao watakuwa wakisikiliza sauti za wale 49% walioko Bungeni?

Kila mtu anataka CCM iondoke, lakini hatuko tayari kukipa chama nafasi eti kikajifunze kazi kama Kikwete alivyofanya au kuwa ni Chama kisicho na wenye uwezo wa kutosha kuongoza na kufanya kazi kitendaji kama zile Tanzania ilivyopata Uhuru wake.

Baya zaidi, bado mpaka leo Chadema na Upinzani havieleweki Ki-Sera kwa Watanzania na hatujui watakuja na mipango gani ya Kisiasa na kimaendeleo kwa kueleweka kuliongoza Taifa la Tanzania.

Hivyo basi, inabidi tujiulize, je tuko tayari kuendelea kubahatisha kama Kikwete kwa miaka miwili ili kuelewa nini wajibu wa kuongoza nchi na kuwa na sera zinazoeleweka au ni lazima tujiamini na kuingia tukiwa tayari na Sera zetu zikieleweka kwa Wananchi ambao hawatahitaji miaka miwili kuzielewa na kuanza kuzifanyia kazi?
 
Rev Kishoka Labda turudi kwenye historia ya kupata Uhuru wetu, tulipigania Uhuru tukataka tujitawale, lakini tangu tumepata Uhuru huo miaka karibu 50 sasa , tumekuwa sawa na ile merikebu iliyoweka nanga inayoyumba mbele nyuma kufuata mkondo wa bahari.
Mkuu,je kwa mtizamo wako unadhani tulipaswa kujiandaa kwanza namna ya kujitawala kabla ya kupata uhuru?Je muda gani ungetosha kwa maandalizi hayo kabla ya kuwa tayari kupata uhuru?Je matatizo tuliyonayo takriban miaka 50 baada ya uhuru ni matokeo ya kupata uhuru pasipo kujiandaa au ni matokeo ya sera mbovu (au nzuri lakini utekelezaji mbovu)?Je wenzetu waliopata uhuru kisha wakamudu kufanya vizuri walikwenda kwenye chuo au taasisi ya kujifunza kujitawala?

Tukirejea kwenye hoja ya kuiondoa CCM au tusubiri kwanza kipatikane chama mbadala kitakachomudu kutufikisha tunapopaswa kuwepo.Binafsi,naona kosa kubwa linalofanyika katika hoja ya "kusubiri mazingira yawe conducive ie kuwa na chama ambacho hakitarejea yaleyale ya CCM" ni kusahaua au kupuuza ukweli kwamba CCM itakuwepo wakati maandalizi hayo yanafanyika.Na kwa vile itakuwepo,na pia kwa sababu INA NIA,UWEZO na SABABU (hata kama sio sababu halali) ya kutaka kudumisha utawala wake wa kidhalimu,NI LAZIMA ITAHUJUMU JITIHADA HIZO.Tukumbuke kuwa CCM ni kama virus au bakteria anayesababisha ugonjwa mwilini.Ili afya ya mgonjwa husika iboreke au apone kabisa ni muhimu kuteketeza virus au bakteria huyo.Ni sawa pia na ndoo yenye tundu.Hakuna namna tutakavyoweza kujaza maji kwenye ndoo hiyo pasipo kuziba tundu hilo.Ni sawa na jambazi aliyeingia ndani,swali tukishamtimua then what halina nafasi.

Hivi,kwa minajili ya mjadala huu,tukikubaliana kuwa tulipaswa kusubiri tujiandae vya kutosha kabla ya kupata uhuru wetu,na sasa tunapaswa kujiandaa vya kutosha kabla ya kukipa dhamana chama kingine (kwa hofu kinaweza kuturejesha palepale tulipoiacha CCM),je ni muda gani unatosha kwa ajili ya maandalizi hayo?Suala la muda ni muhimu sana kwani sote tunafahamu kasi ya uharibifu unaofanyika kwenye raslimali zetu,umoja wetu,mshikamano wetu na mambo mengine muhimu kwa ajili ya ustawi wa taifa.Je suppose tutakapohitimu maandalizi ya kujitawala pasipo CCM then tukajikuta tuko katika hali kama ya Somalia (naam,CCM wanatusukumia huko) maandalizi hayo yatasaidia nini?

Kama tungemruhusu mkoloni aendelee kututawala kwa vile tu hatujajiandaa vya kutosha kujitawala sie wenyewe,halafu mkoloni akakomba kila raslimali na kuteketeza nguvu kazi yetu,hivi (licha ya mark time tunayopiga hivi sasa) hali si ingekuwa mbaya maradufu?Au kwa mfano jitihada za civil rights movement huko Marekani zingechukua mtizamo huu wa "tujiandae kwanza"....na Amin alipotuvamia,"tujiandae kwanza"...na Wahutu na Watutsi nao,"tujiandae kwanza"...

Tusisahau kuwa tunaweza kusubiri muda mwafaka wa kuiondoa CCM madarakani lakini,unfortunately,muda hautusubiri sie tuwe tayari "kujitawala pasipo CCM".Na licha ya muda kutotusubiri,kila dakika ya CCM kuwa madarakani ni sawa na mazalisho ya kasi ya virusi vya ukimwi mwilini (na ndio maana matabibu wanashauri mwathirika kuanza tiba pindi CD4 count ya mwathirika inapofikia kiwango flani,nadhani 250 or something like that).

Hivi wakati tuko katikati ya "somo la kujiandaa kujitawala pasipo CCM" kisha tukabaini kuwa nchi inatumbukia kwenye handaki lenye kina kirefu,tutakatisha "kozi" hiyo?Tukumbuke pia kwamba kwa kila siku ambayo CCM inakaa madarakani inazidi kutengeneza mazingira ambayo yatatengeneza ugumu mkubwa (kuliko ilivyo sasa) kuwaunganisha Watanzania dhidi ya vikwazo vya maendeleo na stawi wetu.Wanawalaghai Waislam kuwa watawaanzishia mahakama ya kadhi ili wapate kura za Waislam,wanatumia ukabila ili waendelee kuwa madarakani (esp kwenye ubunge,udiwani,nk),wanakumbatia wahalifu hatari ili wawapatie fedha za kuendelea kubaki madarakani,wanakandamiza mawazo mbadala au/na endelevu ili kuficha maovu yao kwa umma,nk,nk,nk....Je hivyo vyote sio raw materials za vurugu hapo baadaye?SASa kama tunaafikiana katika hilo,je busara tu haiwezi kutufahamisha kuwa tunachosubiri ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa maana kwamba kila kilo moja ya jitihada za maandalizi ya kijitawala tutakayofanya,CCM na washirika wake wanaondoa kilo mbili?
 
Rev. Kishoka

Umeandika marefu lakini umekuwa kila mara huji na mapya, unaonekana unandoto za chama cha kufikirika ambacho hakijawahi kutokea, chama ambacho hakina mawaa kitakachokuwa kinagawa maziwa kwa wananchi wake.

Mwache Kikwete aendelee kujifunza huku akiwa madarakani na waache Chadema wasiwe na majibu unayoyataka ya ili iweje.Tusipoichagua Chadema tutaichagua CCM na maisha yanaendelea.

Hizo hadithi zenu mnazozitoa mkiwa huko ulaya hazitufai sisi, tutachagua hivyo hivyo vyama mnavyovidharau. Hayo mawazo yenu yakutaka kuwapotosha watu mpeane huko huko mliko.
 
Mkuu Rev. Kushoka, nimesoma maelezo yako marefu kwa umakini mkubwa lakini hadi nafikia mwisho nimeshindwa kukuelewa hasa unataka nini na tatizo lako ni nini, unataka tufanye nini katika uchaguzi mwaka huu au tuendelee tu na hadithi. Kuuliza Chadema wamefanya nini katika huu mfumo tulio nao wa chama-serikali ni kutokutaka kuukubali ukweli kuwa mabadiliko hayasubiri kesho.

Kwanza, Chadema ni kweli hawajazindua bado ilani yao ya uchaguzi wala kumteua rasmi mgombea wao wa Uraisi. Lakini pamoja na yote hayo Chadema wana sera zao ambazo ziko wazi kwa yeyote anayetaka kuzifahamu na ambazo wamejitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kuzifiksha kwa wananchi kwa njia mbalimbali kama operation sangara, mikutano na vyombo vya habari. Pia natumaini wanapata ushauri mwingi tu kutoka kwa wadau mbalimbali wengi tu lakini sidhani kama wanalazimika kukubaliana na kila jambo hata kama linatoka kwa Rev :)

Pili chama cha siasa kinaongozwa na watu, binadamu, na kwa vyovyote wote hawawezi kuelewana kwa wakati wote na kwa mambo yote na hili haliwezi kuchukuliwa kama upungufu wa chama. Huko Marekani tulishuhudia Obama na Clinton ambao wote walikuwa Democrats wakitoana macho wakati wa kumtafuta mshika kibendera lakini lilipofika swali la kuwatoa Republicans walisahau tofauti zao na hivi sasa wanafanya kazi pamoja.

Mimi, kama Mtanzania mwenye uchungu na taifa lake, hata ukiniamsha usiku wa manane sitasita kusema ndoto yangu ni kuiona CCM iking'oka madarakani kabla ya kitu chochote kile. Ninaamini kuwa kila dakika CCM inavyoendelea kubaki madarakani ndivyo nchi inavyozidi kudidimia na kuangamia - ni kama vile unamkuta mwanao anazama majini, cha kwanza unamtoa kwenye maji ndipo unafikiria pa kumpeleka.
 
Mkuu,je kwa mtizamo wako unadhani tulipaswa kujiandaa kwanza namna ya kujitawala kabla ya kupata uhuru?Je muda gani ungetosha kwa maandalizi hayo kabla ya kuwa tayari kupata uhuru?Je matatizo tuliyonayo takriban miaka 50 baada ya uhuru ni matokeo ya kupata uhuru pasipo kujiandaa au ni matokeo ya sera mbovu (au nzuri lakini utekelezaji mbovu)?Je wenzetu waliopata uhuru kisha wakamudu kufanya vizuri walikwenda kwenye chuo au taasisi ya kujifunza kujitawala?

Mlalahoi,

Pointi yangu ni kuwa sisi si wanaffunzi wazuri wa historia! Tunaamini tukipanda mahindi tutavuna kahawa. Silaumu harakati za kupigania Uhuru, bali nazionyesha kama mfano wa kuigwa kuona ni wapi tulikosea. Tulipopata Uhuru kulikuwa na kina Mtemvu, Kambona na Kawawa. Wakadai wao ni ushirika mmoja kumn'goa Mkoloni, lakini baadaye ikawa ni mivutano na watu kuwekana ndani kama si ukimbizi na kuingia mfumo wa kibabe wa chama kimoja.

Chadema na Upinzani walikuwa na uwezo wa kulisahihisha hili. Uchaguzi mkuu wa 1995 ulikuwa wa kwanza wa majaribio, kisha ukaja TAMISEMI wa 1999, ukaja uchaguzi mkuu 2000, halafu TAMISEMI 2004, ukaja uchaguzi mkuu 2005, kisha TAMISEMI 2009. Sasa kama katika chaguzi hizi zote 6, bado hawajaweza kuonekana na umahiri na uwezo au walau kujifunza kutokana na makosa ya nyuma, iweje leo tutegemee mavuno bora?

Je hawajifunzi kwa kutumia historia yetu na nchi nyingine kujipanga sawa? Je hiki si chama kilichojaa wasomi, je usomi wao una manufaa gani kama hawana uwezo wa kutumia usomi wao kunyambulisha mambo rahisi kama kufuata historia?

Kwa nini waendeleze utamaduni wa kusubiri wakati wa uchaguzi kujiuza "vizuri" kwa wananchi ilhali hawajiamini?
 
Tukirejea kwenye hoja ya kuiondoa CCM au tusubiri kwanza kipatikane chama mbadala kitakachomudu kutufikisha tunapopaswa kuwepo.Binafsi,naona kosa kubwa linalofanyika katika hoja ya "kusubiri mazingira yawe conducive ie kuwa na chama ambacho hakitarejea yaleyale ya CCM" ni kusahaua au kupuuza ukweli kwamba CCM itakuwepo wakati maandalizi hayo yanafanyika.Na kwa vile itakuwepo,na pia kwa sababu INA NIA,UWEZO na SABABU (hata kama sio sababu halali) ya kutaka kudumisha utawala wake wa kidhalimu,NI LAZIMA ITAHUJUMU JITIHADA HIZO.Tukumbuke kuwa CCM ni kama virus au bakteria anayesababisha ugonjwa mwilini.Ili afya ya mgonjwa husika iboreke au apone kabisa ni muhimu kuteketeza virus au bakteria huyo.Ni sawa pia na ndoo yenye tundu.Hakuna namna tutakavyoweza kujaza maji kwenye ndoo hiyo pasipo kuziba tundu hilo.Ni sawa na jambazi aliyeingia ndani,swali tukishamtimua then what halina nafasi.

Hivi,kwa minajili ya mjadala huu,tukikubaliana kuwa tulipaswa kusubiri tujiandae vya kutosha kabla ya kupata uhuru wetu,na sasa tunapaswa kujiandaa vya kutosha kabla ya kukipa dhamana chama kingine (kwa hofu kinaweza kuturejesha palepale tulipoiacha CCM),je ni muda gani unatosha kwa ajili ya maandalizi hayo?Suala la muda ni muhimu sana kwani sote tunafahamu kasi ya uharibifu unaofanyika kwenye raslimali zetu,umoja wetu,mshikamano wetu na mambo mengine muhimu kwa ajili ya ustawi wa taifa.Je suppose tutakapohitimu maandalizi ya kujitawala pasipo CCM then tukajikuta tuko katika hali kama ya Somalia (naam,CCM wanatusukumia huko) maandalizi hayo yatasaidia nini?

Kama tungemruhusu mkoloni aendelee kututawala kwa vile tu hatujajiandaa vya kutosha kujitawala sie wenyewe,halafu mkoloni akakomba kila raslimali na kuteketeza nguvu kazi yetu,hivi (licha ya mark time tunayopiga hivi sasa) hali si ingekuwa mbaya maradufu?Au kwa mfano jitihada za civil rights movement huko Marekani zingechukua mtizamo huu wa "tujiandae kwanza"....na Amin alipotuvamia,"tujiandae kwanza"...na Wahutu na Watutsi nao,"tujiandae kwanza"...

Tusisahau kuwa tunaweza kusubiri muda mwafaka wa kuiondoa CCM madarakani lakini,unfortunately,muda hautusubiri sie tuwe tayari "kujitawala pasipo CCM".Na licha ya muda kutotusubiri,kila dakika ya CCM kuwa madarakani ni sawa na mazalisho ya kasi ya virusi vya ukimwi mwilini (na ndio maana matabibu wanashauri mwathirika kuanza tiba pindi CD4 count ya mwathirika inapofikia kiwango flani,nadhani 250 or something like that).

Hivi wakati tuko katikati ya "somo la kujiandaa kujitawala pasipo CCM" kisha tukabaini kuwa nchi inatumbukia kwenye handaki lenye kina kirefu,tutakatisha "kozi" hiyo?Tukumbuke pia kwamba kwa kila siku ambayo CCM inakaa madarakani inazidi kutengeneza mazingira ambayo yatatengeneza ugumu mkubwa (kuliko ilivyo sasa) kuwaunganisha Watanzania dhidi ya vikwazo vya maendeleo na stawi wetu.Wanawalaghai Waislam kuwa watawaanzishia mahakama ya kadhi ili wapate kura za Waislam,wanatumia ukabila ili waendelee kuwa madarakani (esp kwenye ubunge,udiwani,nk),wanakumbatia wahalifu hatari ili wawapatie fedha za kuendelea kubaki madarakani,wanakandamiza mawazo mbadala au/na endelevu ili kuficha maovu yao kwa umma,nk,nk,nk....Je hivyo vyote sio raw materials za vurugu hapo baadaye?SASa kama tunaafikiana katika hilo,je busara tu haiwezi kutufahamisha kuwa tunachosubiri ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa maana kwamba kila kilo moja ya jitihada za maandalizi ya kijitawala tutakayofanya,CCM na washirika wake wanaondoa kilo mbili?

Mlalahoi,

Ukiwa na bondia wako na unajua ni dhaifu, utaendelea kumpeleka kwenye ulingo bila kumuandaa ipaswavyo kisa ni lazima apigane tuu? Je akipigwa mpaka kuzimia na akizinduka kisaikolojia akawa amedhoofika utaendeleza mbinu na mazoezi yale yale ambayo yalimfanya ashindwe pambano la kwanza hata la saba?

Nimekosoa ile soft approach ya kutotaka kutoana ngeu na CCM, ile soft approach ya kuogopa kunyimwa Ruzuku au mgao wa fedha. Nimewasihi Chadema watunishe msuli kwa kila jambo kila mwaka wa bajeti na kila kisichoeleweka na wasiridhike na kauli nyepesi nyepesi au ahadi mbofumbofu.

Lakini bado wameendelea kuburuzwa na barudhuli CCM, ndio maana nauliza na nakubaliana wakishinda then what ikiwa wao wako defensive na hata wakishinda ushindi wao hautakuwa na nguvu za kutosha kuwaweka kando CCM wasiharibiwe fursa yao ya kutawala?

Sisi kama Taifa, matokeo ya kupata Uhuru tukiwa wachanag tumeyaona, leo hii mkoloni karudi kiulaini kwa mikopo, misaada na uwekezaji. Leo uwezo wa kujitawala hatuna tunamtegemea Mwekezaji na tunaogopa mkorofisha kwa kuwa hatuna nguvu za kusimama wenyewe wima na kujilinda.

This is the fate of opposition ambao bado wanaonyesha woga na udhaifu. Hata huko kujitolea mhanga si kule kwa kusema "kudadeki mpaka tone la mwisho" bali ni kule kwa kuogopa kuiudhi CCM na Serikali yake na kuhofia ubabe wa CCM kama vile walivyofanyiwa Mtikila na Lamwai.

Then you have a serious problem ya watu wasio na uwezo wa kujiamini bila kutegemea. Sasa kama kwa CCM wanahofia, kwa hao wengine Mafisadi, Wawekezaji na mawakala wa Mkoloni watafanyaje , huku CCM naye anawasumbua?

HIvyo tutafakari hayo yote sasa hivi si kwa nia ya kusema tusiendelee mbele na kuing'oa CCM, lakini tujue wazi huko tunakokwenda na tujiandai kikamilifu na si kubahatisha kwa kusema ngoja tufanikiwe kwanza.

Tena kama kauli za uhakika (self assured) zingetoka mapema na hata leo hii kujiuza kwa Upinzani kumpasha Mtanzania kuwa si suala la nia na sababu tu kuwa zipo, bali hata uwezo upo, umati mkubwa wa Watanzania usingeingia mashaka.

Tuna miezi mitatu ya kuuza ujumbe wa tumaini, utakaoonyesha kuwa hili si jaribio tena bali ni kujiamini na tuko tayari kwa lolote na hata kutoa kafara kuing'oa CCM.

Je Upinzani uko tayari kutumia turufu hiyo kwa Mtanzania atakayepiga kura?
 
Rev. Kishoka

Umeandika marefu lakini umekuwa kila mara huji na mapya, unaonekana unandoto za chama cha kufikirika ambacho hakijawahi kutokea, chama ambacho hakina mawaa kitakachokuwa kinagawa maziwa kwa wananchi wake.

Mwache Kikwete aendelee kujifunza huku akiwa madarakani na waache Chadema wasiwe na majibu unayoyataka ya ili iweje.Tusipoichagua Chadema tutaichagua CCM na maisha yanaendelea.

Hizo hadithi zenu mnazozitoa mkiwa huko ulaya hazitufai sisi, tutachagua hivyo hivyo vyama mnavyovidharau. Hayo mawazo yenu yakutaka kuwapotosha watu mpeane huko huko mliko.


Luteni,

Nikuuzieni kipi kipya ikiwa nilichokuuzia awali wala hukifanyii kazi? NItaendelea kukirudia kama vile mzazi wako alivyojirudia kama santuri kuwa ni lazima uende shule mpaka siku moja utaelewa alikuwa anamaanisha nini.

Sihitaji kuja na kipya chochote, tena kama nyie Chadema mnasubiri mapya kutoka wa Mchungaji, ina maana hamko tayari na hamjijui na wala hamkumbuki mliloambiwa awali!

Hivyo unatuambia umma kuwa tusikuamini weye na Chama chako maana unasubiri mpya, za kale zimekushinda bado unataka mpya?

Nitakuuliza maswali mawili tuu, kwa nini Chadema haikushiriki kwa dhati uchaguzi wa TAMISEMI 2009? kwa nini waliudharau na kuupuzia Uchaguzi huo? kwani haukuwa na maslahi ya Taifa?
 
Mkuu Rev. Kushoka, nimesoma maelezo yako marefu kwa umakini mkubwa lakini hadi nafikia mwisho nimeshindwa kukuelewa hasa unataka nini na tatizo lako ni nini, unataka tufanye nini katika uchaguzi mwaka huu au tuendelee tu na hadithi. Kuuliza Chadema wamefanya nini katika huu mfumo tulio nao wa chama-serikali ni kutokutaka kuukubali ukweli kuwa mabadiliko hayasubiri kesho.

Kwanza, Chadema ni kweli hawajazindua bado ilani yao ya uchaguzi wala kumteua rasmi mgombea wao wa Uraisi. Lakini pamoja na yote hayo Chadema wana sera zao ambazo ziko wazi kwa yeyote anayetaka kuzifahamu na ambazo wamejitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kuzifiksha kwa wananchi kwa njia mbalimbali kama operation sangara, mikutano na vyombo vya habari. Pia natumaini wanapata ushauri mwingi tu kutoka kwa wadau mbalimbali wengi tu lakini sidhani kama wanalazimika kukubaliana na kila jambo hata kama linatoka kwa Rev :)

Pili chama cha siasa kinaongozwa na watu, binadamu, na kwa vyovyote wote hawawezi kuelewana kwa wakati wote na kwa mambo yote na hili haliwezi kuchukuliwa kama upungufu wa chama. Huko Marekani tulishuhudia Obama na Clinton ambao wote walikuwa Democrats wakitoana macho wakati wa kumtafuta mshika kibendera lakini lilipofika swali la kuwatoa Republicans walisahau tofauti zao na hivi sasa wanafanya kazi pamoja.

Mimi, kama Mtanzania mwenye uchungu na taifa lake, hata ukiniamsha usiku wa manane sitasita kusema ndoto yangu ni kuiona CCM iking'oka madarakani kabla ya kitu chochote kile. Ninaamini kuwa kila dakika CCM inavyoendelea kubaki madarakani ndivyo nchi inavyozidi kudidimia na kuangamia - ni kama vile unamkuta mwanao anazama majini, cha kwanza unamtoa kwenye maji ndipo unafikiria pa kumpeleka.

Magz,

Tuna tabia ya kufumbia macho madhaifu na mapungufu yetu kama binaadamu na ndio maana hata kaika hili la Chadema, watu wako radhi kusema ahh, acheni kichukue kwanza ushindi.

Swali ushindi unapatikanaje bil mipango inayoeleweka?

Sihitaji wala silazimishi Chadema wakubaliane na mawazo au maoni yangu, lakini ni tegemeo kuwa mambo fulani ya msingi yatafuatiliwa au kuwasaidia. Nimemjibu Mlalahoi hapo juu, hili la kuogopa kuchafuana mashati, sasa kama leo kama wao wajibu wao ni kuikaba koo Serikali na wanaogopa, je wakishika madaraka itakuwaje?

Leo hii, tumetangaziwa Slaa atakuwa mgombea wao, walikuwa na nafasi bira ya kumjenga Slaa hata kabla ya mchaato mzima wa Uchaguzi Mkuu kuanza, je walitumia nafasi hiyo zaidi ya hotuba za orodha ya EPA ambayo ilitokea humu humu JF nao Chadema wakaichukua na kuifanya yao?

Ikiwa tonge la vita vya Ufisadi wamezidiwa kete na CCM na kina Mwakyembe wanajizolea sifa na kujitapa, je huoni kuwa kuna walakini kuwa wanaendelea kupiga kura ya ndio?

Mwanzoni mwa Bajeti ya mwaka huu, nilitoa rai kuwa wajitoe Bungeni kwa kuonyesha kutokuridhika kwao na Bajeti ambayo inaendeleza deni la Taifa, nikajibiwa eti wakale wapi?

So are they ready to lead? My answer is no, they are not ready and they lack confidence and abiility to lead! Should we just go ahead and give them the mantle, sure as long as we are ready o live with the consequenses in which we are not ready to face!

Nilimwambia Luteni na Shalom, nasubiri wiki ya kwanza ya November imalizike, ndipo tuanze kulonga tena tujiuliza kama tunahitaji kugawa kile kijitabu cha Nyerere cha TUJISAHIHISHE!
 
Back
Top Bottom