Wenye ndoto ya kufungua biashara pitia hapa

kitoto wa vitoto

JF-Expert Member
Jul 28, 2019
360
386
Nimeona nishee na nyie ujumbe huu

JINSI YA KUCHAGUA ENEO ZURI LA BIASHARA TANZANIA.

Jinsi ya kuchagua sehemu ya biashara kwa Tanzania ni muhimu sana kwasababu itachangia na kuongeza mafanikio ya kwenye biashara.

1. Angalia Ushindani wa Biashara
Ushindani ni jambo muhimu sana linaloweza kufanya eneo la biashara kuwa zuri au baya. Hebu fikiri mtu mchanga kabisa anaanzisha biashara mahali ambapo tayari kuna wafanyabiashara wengine wakubwa wenye uzoefu, mtaji, vitendeakazi au hata mtandao mzuri wa washirika.

Bila shaka, itakuwa vigumu sana kwa mtu huyo kukua kibiashara. Ni lazima mtu apime na achague eneo amabalo lina ushindani ambao anaweza kuumudu na kukua.

2. Uhusiano kati ya biashara na mazingira
Mara nyingi biashara huhusiana na mazingira husika. Kwa mfano ni rahisi kufanikiwa kwenye biashara ya stationary kwenye maeneo ya vyuo, shule au taasisi kuliko nje ya mazingira hayo.

Kwa mfano pia ni rahisi mtu kuendesha biashara ya vyinywaji na vitafunwa, vipodozi na simu kwenye kituo cha mabasi kuliko biashara ya nafaka au pembejeo.

Hivyo ni muhimu kupima kama biashara yako itaendana na eneo husika unalotaka kulichagua.

3. Mtindo wa maisha katika eneo husika
Kila eneo lina mtindo wake wa maisha. Itakuwa jambo la kusikitisha sana wewe kufungua biashara ambayo bidhaa yake ndogo kabisa ni shilingi 100,000 na wakati nguvu ya ununuzi ya watu wa eneo husika ni 1,000.

Ngoja nikupe mfano rahisi zaidi, kwa mfano watu waliozoea kununua mafuta ya mia tano, unga robo na sabuni kipande, ukifungua supermarket katika eneo hilo ni wazi kuwa utakosa wateja hatakama unauza bidhaa nzuri kiasi gani.

4. Wingi wa waakazi
Wingi wa watu katika eneo husika ni sawa sawa na mauzo zaidi au kuonekana zaidi kwa biashara yako. Haijalishi eneo lina fremu nzuri au za gharama nafuu kiasi gani, kama halina wakaazi wa kutosha litakuchelewesha sana kufikia malengo yako.

Ikiwa ni eneo ambalo watu wanahamia kwa kasi kubwa kwa kipimo kuwa ndani ya muda mfupi utakuwa na wateja wengi basi hapo unaweza kuvumilia; lakini kama eneo ndivyo lilivyo nyumba moja ipo baada ya mita 500 basi hilo halikufai.

5. Miundo mbinu na huduma za kijamii
Unapoangalia eneo la kufanyia biashara ni zaidi ya kile chumba au nyumba unayoichagua kuitumia kama ofisi yako.

Itakuwa si jambo la busara kuendesha biashara inayohitaji maji au umeme wa kutosha mahali ambapo hakuna huduma hizo.

Pima hili mapema lisije likakusababishia changamoto au gharama kubwa za uendeshaji zisizokuwa na ulazima.

Hakikisha pia eneo hilo linafikika katika vipindi vyote vya mwaka. Kwa mfano itakuwa nijambo la ajabu mtu kufungua biashara ya kuuza gesi kwenye eneo ambalo liko uchochoroni; kiasi kwamba hata yale magari ya gesi hayawezi kufika au hata wateja wake wanamfikia kwa taabu.

Hivyo, fanya tathimini ya miundombinu kwa kina.

6. Usalama na majirani
Usalama ni nguzo muhimu sana katika kujenga mazingira mazuri ya kibiashara. Hakuna mteja atakayependa kuja kwenye biashara ambayo atajihisi kutokuwa salama.

Mfanyabiasha naye hawezi kufanikiwa ikiwa anafanya biashara kwenye mazingira ambayo siyo salama kwake na mali zake.

Hakikisha pia mazingira yanayokuzunguka, majirani pamoja na biashara za jirani hazitaathiri biashara yako. Kwa mfano siyo biashara zote zinaweza kufanywa karibu na biashara kama vile baa, karakana ya ufundi n.k.

Nimeshuhudia watu wakiacha fremu zao za biashara kutokana na kuzungukwa na majirani wabaya; nimeshuhudia watu wakigomeana kulipa luku, maji n.k. hadi kufikia kuziacha biashara zao.

Hivyo tafakari sana kabla ya kuchagua eneo la biashara.

7. Gharama za uendeshaji wa eneo husika
Haijalishi eneo la biashara ni zuri au umelipenda kwa kiasi gani, ni lazima ulinganishe kama gharama za uendeshaji zinazotokana na kufanya biashra kwenye eneo husika zitalipa.

Inawezekana umekutana na mwenye nyumba anayepangisha fremu yake nzuri sana kwa shilingi 500,000 kwa mwezi, kumbe ni ili alipe mkopo wake wa bank; lakini katika uhalisia biashra katika eneo hilo haiwezi kufikisha mauzo ya 50,000 kwa siku.

Ukidanganyika kwa mazingira hapa bila kupima uhusiano wake na gharama za uendeshaji utakuwa na wakati mgumu sana.

8. Mahitaji ya kipekee ya biashara husika
Suala hili hupuuziwa sana na watu wengi wanapotaka kuanzisha biashara, lakini huwaletea changamoto kubwa. Ni muhimu sana ufahamu biashara yako ina mahitaji gani ya kipekee ya sasa na baadae.

Juzi nilikutana na dada mmoja anauza biashara yake(ilimshinda kuendesha)Ila yéye alisema anasafiri
Nilipochunguza niligundua
Kipoto kilikuwa kidogo kuliko matumizi

Ilikuwa hivi
Kodi kwa mwezi ni 300,000/
Leseni 202,000/ kwa mwaka
T R A ana makadirio ya 480,000/kwa mwaka
Taka 5000 kwa mwezi
Kula 2000 kwa siku
Mshahara 150000 kwa mwezi
Umeme 30000 kwa mwezi
Maji 5000 kwa mwezi
Na mengineyo

Kipato
Kwa siku anauza wastan wa 100000-120000
Wastani wa FAIDA kwa siku ni 12,000

Je mtu kama huyo ana sababu ya kuendelea kufanya hiyo biashara?
Jibu ni hapana

Kuweni makini chaguen eneo linaloendana na mazingira husika.

Sent from my Infinix X680 using JamiiForums mobile app
 
Biashara inataka moyo, nguvu na pesa

Mi napenda kuanza na mtaji kidogo ukue taratibu
 
Back
Top Bottom