SoC02 Wanaume: Viumbe walio hatarini kutoweka

Stories of Change - 2022 Competition

kimbomba25

Member
Jan 27, 2017
94
157
Nimesoma shule ya sekondari kata katika kijiji kimoja huko mkoani Dodoma. Wakati huo, tulipokuwa tukijadili hatima zetu kimasomo na kimaisha kwa ujumla tulikuwa tukiwaweka kando wasichana kwa kuwa hawakuonekana kama wanaelewa chochote kuhusu hatima zao na hata mazingira hayawakuwaunga mkono, tofauti na upande wetu wavulana.

Katika ubao wa matokeo wasichana walianza kutafuta majina yao katika karatasi ya pili, kwani ile ya kwanza tulikuwepo wanaume pekee. Ni kwa namna gani msichana aingie katika namba kumi bora? Je, wavulana watakuwa wapi wakati huo?

Wasichana walikuwa katika wakati mgumu, kwanza, walipambana na changamoto nyingi za kimazingira; wengi walikuwa wakisoma mbali na makwao, hivyo maisha ya kujitegemea katika vyumba vya kupanga yalikuwa yakiwawia ugumu. Mazingira yalikuwa hatarishi kwao na kusababisha wengi wao kuingia kwenye mikono ya wanaume wakware waliowatia mimba. Ilikuwa habari ya kawaida kusikia fulani amekatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, au kusikia fulani anatembea na mume wa mtu kwa kuwa humhonga fedha za kujikimu kimaisha.

Hata wale wasichana waliokuwa wakiishi makwao walikuwa wanakutana na changamoto za kazi za majumbani. Mimi nilikuwa nakaa na dada yangu nyumbani, tulipokuwa tukitoka shuleni kazi za nyumbani kama kupika na kuosha vyombo zilikuwa za kwake, wakati huo mimi nikijisomea au kucheza mpira.

Kutokana na hivyo, tukawa tunaona wavulana ndiyo wamiliki wa maisha na wasichana wanapoteza muda tu. Tulikuwa tukijiona katika sura za mafanikio makubwa siku za usoni huko mijini ilhali wasichana wakifubaa kwenye ndoa zao vijijini.

Tulifanya mitihani ya mwisho na matokeo hayakudanganya; walifaulu wavulana pekee na wasichana wote waliishia pale.

BAADA YA MIAKA KUMI
Hivi sasa imetimia miaka kumi tangu tulipohitimu kidato cha nne. Waliofaulu walishakwenda masomoni hadi kuhitimu shahada zao za kwanza. Lakini katika hali ya kushangaza, hatima hazijawa kama vile ambavyo tulidhani.

Asilimia kubwa ya wanaume wamepoteza dira za maisha na wanawake wameimarika ajabu.

NINI KILICHOTOKEA
Wavulana walienda masomoni wamemaliza na hivi sasa hawana ajira wakihangaika huku na huko na wengine wakiwa wamekata tamaa na kujiingiza katika tabia hatarishi kama ulevi uliopindukia. Wasichana waligawanyika, wengine walienda mijini kutafuta kazi, wengine wakaolewa na wengine walibaki kijijini wakijishughulisha na shughuli za kuwaingizia kipato.

Sijasikia wala kubahatika kukutana na msichana niliyesoma naye ambaye ameharibikiwa kama ilivyo kwa wanaume. Sijamwona mraibu wa dawa za kulevya wala mlevi wa kupindukia kama ilivyo kwa baadhi yetu wanaume.

Kiuwiano inaonesha wanaume wengi wamepoteza dira ukilinganisha na wanawake. Kitu ambacho ni kinyume kabisa na matarajio yetu sote.

NILICHOBAINI
Katika namna ya ajabu, nimebaini kuwa maisha ni hatarishi kwa wasichana wadogo ilhali ni salama kwa wavulana wadogo, lakini maisha ni hatarishi kwa wanaume ilhali ni salama kwa wanawake.

Kwa nini?
Kadiri mwanaume anavyokua na kuwa huru ndivyo dunia inavyokuwa hatarishi na kuwa na mitego mingi ikilinganishwa na wanawake.

Tazama walevi wa kutupa na waraibu na dawa za kulevya ni akina nani? Kamari, je?

Pindi mwanaume anapodhani yuko huru ndiyo wakati ambao vishawishi humfuata kwa kasi.
Ni wanawake wangapi unaweza kuwakuta asubuhi wakilewa? Ni wanawake wangapi wenye ujasiri wa kuvuta sigari au bangi hadharani?

Lakini wanaume kwa kuwa wako huru kufanya vitu hivyo, wamegeuka kuwa waathirika nambari moja.

Jiulize!
Je, unapoona matangazo ya kamari na pombe kali, unadhani walengwa ni akina nani, kati ya wanaume na wanawake? Kifupi ni WANAUME!

Mazingira yapo kumtega mwanaume aingie shimoni. Na uhuru uliopitiliza ndiyo mteremko wa kumwingiza shimoni. Huku kukosa usimamizi kukiwa kichocheo nambari moja.

Wakati ambao wanawake wanaona aibu kujiingiza katika tabia fulanifulani zisizofaa, wanaume wanajiona ‘wamependelewa’ kuwa na uhuru wa kufanya mambo hayo pasipo kuulizwa na yeyote. Ni kawaida kuona wanaume walevi hadi kazini, lakini ni nadra kumwona mwanamke akienda kazini akiwa kalewa.

Nikielezea kilichotokea kwetu…

Wanaume wengi hawajatimiza ndoto walizokuwa wakizifukuzia. Katika harakati za kukwepa aibu na kutaka kupunguza saa za mateso wamejikuta wakilala na kuamkia kwenye pombe kali, na wengine ili kubahatisha riziki wamejikuta wakishindia kamari.

Wakati huohuo wale wanawake ambao tulidhani maisha yao yangeishia kidato cha nne wameng’ara. Wapo walioolewa kwenye ndoa tulivu, wengine wanamiliki na kuendesha biashara za maana sana hapa kijijini. Kama wakati ule ambao tulikuwa tuna wavulana wengi waliofaulu kwenye ubao wa matokeo kuliko wasichana, ndivyo tuna wanawake wengi waliofanikiwa kuliko wanaume.

KINACHOSINGIZIWA
Kinachotajwa kuwa sababu ya uharabifu huu ni ukosefu wa ajira kwa vijana. Sipingani na hoja ya kuwa ukosefu wa ajira umefanya maisha kuwa magumu ajabu, lakini kinachonipa maswali ni kwa nini ukosefu huu wa ajira uwaathiri zaidi wanaume kuliko wanawake?

Ni kweli kuwa katika baadhi ya tamaduni wanaume tumepewa majukumu mengi na jamii kuliko wanawake, lakini huu mwendo tunaoenda nao si mzuri na ukosefu wa ajira hautoshi kuwa sababu pekee.

Kukosa ajira. Tatizo la ajira ni la wanaume na wanawake lakini wanaume wengi ndivyo limewaathiri na kuwaingiza katika mienendo inayowamaliza ukilinganisha na wanawake.

Wanawake wanaonekana wadhaifu lakini wako imara katika kustahimili changamoto, ilhali wanaume tunaonekana imara lakini tuko dhaifu katika kustahimili changamoto.

Naamini kabisa kuwa kinachotuponza ni uhuru uliopitiliza ndiyo unaotufanya hata tutafute njia za mkato katika kutafuta suluhisho la changamoto zetu. Wenzetu ambao hawana uhuru, wanajitahidi kutafuta suluhisho lisilo na madhara wakati huo sisi tukichakaa katika hiki tunachodhani ni suluhisho (pombe na dawa za kulevya).


TUNAELEKEA KUTOWEKA

Mtindo wa maisha tunayoishi unaonesha dalili kuwa miaka ya mbele hakutakuwa na wanaume, au watakaokuwepo watakuwa wadhaifu sana.

Pombe kali na lishe duni zinafubaza vijana. Kuna baadhi ya vijana unaweza kudhani ni wazee.
Kibiolojia, maisha ya wanadamu yako hatarini kwani wanaume wanapoteza ‘nguvu’ zao. Endapo kila mwanaume atatumbukia katika haya mashimo tunayochimbiwa, basi utafika wakati tutatoweka.

NINI KIFANYIKE
Mwanaume anahitaji malezi thabiti kuliko mvulana. Anapokuwa huru ndiyo wakati wa kujiogopa badala ya kufurahia kwani ndivyo hatari za kila namna zinamnyemelea.

Nashauri wanaume tuukwepe uhuru usio na mipaka, tuwajibike kwa kuanzisha familia, pia tukae karibu na ndugu zetu ambao watakuwa karibu nasi katika kutushauri na kuturudisha njiani pale tunapoelekea kupoteza dira.

Pia, tupunguze matarajio makubwa kwenye maisha kwani kutotimia kwa matarajio hayo ni moja ya sababu ya kutupeleka katika tabia hatarishi.

Na kwa wale walioathirika na matatizo hayo, watambue kuwa hawajachelewa, wajirudi na kuanza upya. Wakati huo watu waliowazunguka wawasaidie kunasuka katika mitego hiyo, badala ya kuwacheka, inatakiwa wawaone kama wahitaji wengine.

Adui mkubwa wa mwanaume ni uhuru usio na mipaka!
 
Usisahau mwanamke bdo ni tegemezi kwa mwanaume, ndio man unaona huo utulivu wao.

Asilimia 80 Hadi 85 ya wanawake mafanikio yao kun mwanaume, ambapo aidha ni mpenzi wake, baba yake au ndug yyte.

unajua sis wanaume ukishakuwa tu jamii inakuacha peke ako tofauti na mwanamke.

umesem wengi waliomaliz hpo wengi same olewa, inamaan kun mwanaume anampambania nk, na pia ht hao ambao hawajaolewa unakuta Wana wanaume kiasi fuln wanawasevu.

point kubwa utulivu wa mwanamke ni vile bado tegemezi.
 
Kwa title ilivyo na ukija na maudhui ya ndani tofauti nilijua nitakutana na biological factors zaidi naona social factors ingawa nazo hazina mashiko sana na dunia ya sasa kwa uhatari wa mwanaume kutoweka maana baadhi ya hoja ulooweka zinawakumba mpaka jinsia ( ke ) by the way kupotea kwa mwanaume ndiyo kupotea kwa human generations.
 
Back
Top Bottom