Wanafunzi 140 UDSM wamejifukuzisha chuo’

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,150
Habari zaidi!
Wanafunzi 140 UDSM wamejifukuzisha chuo’
Theopista Nsanzugwanko
Daily News; Tuesday,February 03, 2009 @20:00

WANAFUNZI 138 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mlimani, wamejifukuzisha chuo baada ya kutojaza fomu za kudahiliwa upya huku wengine 715 wakiwa hawajatimiza masharti wakiwamo waliokata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya elimu nchini.

Aidha, uongozi wa chuo hicho umesema wanafunzi 9,516 sawa na asilimia 93 wametimiza masharti na kudahiliwa kati ya 10,231 waliojaza fomu kuomba kurudi chuoni. Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri), Profesa Makenya Maboko, alisema jana kuwa takwimu hizo ndizo sahihi mara baada ya chuo kukaa na kufanya uchambuzi upya.

Alisema awali walidhani kuwa wanafunzi 11,369 badala ya 10,369 ndio waliorudishwa nyumbani baada ya chuo kufungwa, lakini wamegundua kuwa wanafunzi 610 wa mwaka wa kwanza hawakuripoti chuoni na wengine 390 hawakujisajili mwaka uliopita.

Alisema wanafunzi waliodahiliwa upya wanaendelea vizuri na masomo, huku wengine wakiwa wameanza kufanya mitihani ya majaribio. Maboko alisema tayari wamefikia wiki ya 10 katika muhula, hivyo wanafunzi waliokata rufaa kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, watarudia muhula kwani wakisema waendelee baada ya kutolewa uamuzi, wanaweza kufeli kutokana na kuwa nyuma kimasomo.

“Muhula wetu una wiki 15 na mpaka sasa tunaingia wiki ya 10 na mchakato kwa waliokata rufaa unaweza kuchukua muda, kwani unahitaji kupata uhakiki, hivyo baada ya uamuzi huo ambao utafanyika mapema iwezekanavyo, wanafunzi watakaorejeshwa chuoni itabidi warudie muhula kwa manufaa yao,” alisema Profesa.

Akizungumzia suala la Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) alisema uongozi wa chuo unawasaidia wanafunzi hao kupata Serikali mpya baada ya uongozi wa awali kufutwa kwa kuzingatia Katiba na itaundwa Bodi ya DARUSO, ili kufanya utaratibu wa uchaguzi na kupata wawakilishi wao. Mchakato wa kuwarejesha chuoni wanafunzi wa UDSM, ulianza rasmi Januari 18 mwaka huu na kukamilika Januari 29 kwa wanafunzi wote waliotimiza masharti kudahiliwa upya ambapo pia walipewa vitambulisho vipya.

Chuo hicho kilifungwa kwa muda usiojulikana Novemba 12 mwaka jana, baada ya wanafunzi kugoma kwa muda siku tatu mfululizo, wakiitaka serikali iwape mikopo kwa asilimia 100 badala ya utaratibu wa sasa wa kukopeshwa kwa kuangalia uwezo wa mwanafunzi kujilipia gharama hizo. Baada ya hatua hiyo, wanafunzi hao waliamriwa kujaza upya fomu za udahili na kulipa asilimia 40 ya ada kabla ya kurejeshwa vyuoni.
 
Back
Top Bottom