Wabunge wanaotishia kujiuzulu wafanye hivyo haraka

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
mwananchilogo.jpg
SIKU nzima ya jana ilitawaliwa na gumzo katika redio na vyombo vingine vya habari vya hapa nchini, kutokana na kauli iliyotolewa juzi na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba kutopandishwa kwa viwango vipya vya posho za vikao kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh230,000 kwa kila kikao kumesababisha nusu ya wabunge kutishia kujiuzulu kwa madai ya hali ngumu ya maisha inayowakabili.

Akiwahutubia wananchi mwishoni mwa wiki katika Jimbo la Njombe Kusini ambalo analiwakilisha bungeni, kiongozi huyo alisema wabunge hao wamemwendea wakitaka kuacha ubunge lakini aliwakatalia kwa kuhofia gharama kubwa za kufanya chaguzi ndogo katika majimbo watakayotoka. Spika huyo alisema wabunge hao wamechoka kabisa na kwamba hawakujua kwamba kuacha taaluma zao na kuwa wabunge kungewatia umaskini.

Kauli yake hiyo ambayo ilikuwa inarudiwa mara kwa mara jana katika vipindi vya redio za hapa nchini wakati wananchi walipokuwa wakijadili tishio hilo la wabunge, iliibua hisia kali kutoka kwa wananchi ambao walisema wabunge wa namna hiyo hawafai na kumtaka Spika awaache waondoke kwa kusema ni wabunge maslahi.

Katika hotuba hiyo, Spika Makinda alisema miaka 10 kuanzia sasa, mtu mwenye taaluma yake hatagombea ubunge kwa sababu ni eneo la umaskini wa kutupwa. Alisema wabunge wa Kenya wanawacheka wenzao wa Tanzania kwa kushindwa kujipitishia fedha zinazoendana na kazi wanayoifanya, huku akisahau kwamba amani, umoja na mshikamano wetu umetokana na sera zinazojenga usawa.

Tumeshangazwa sana na kauli hiyo ambayo hakika imelipa Bunge taswira mbaya ya umamluki wa posho. Tangu posho hizo zisitishwe wiki kadhaa zilizopita baada ya wananchi wengi kuzipinga, wabunge wengi wamejitokeza hadharani na kuzitetea kwa kusema maisha yao yamekuwa magumu, hasa wawapo bungeni mjini Dodoma ambapo wanadai gharama za maisha ni kubwa mno kuliko sehemu nyingine nchini.

Wabunge hao, akiwamo Spika wamekuwa wakitoa sababu zisizo na mashiko ilihali wahalalishe posho hizo. Spika alikaririwa na vyombo vya habari akisema hivi karibuni kuwa, wabunge wanakatwa fedha nyingi kutokana na mikopo ya benki na kwamba fedha zinazobaki haziwezi kuwakimu muda wote wawapo Dodoma kwenye vikao vya Bunge. Spika anasahau ukweli kwamba mikopo hiyo siyo ya lazima ambayo mara nyingi imechukuliwa na wabunge kufanya matanuzi tu.

Tunachoweza kusema hapa ni kwamba kauli ya Spika kuhusu tishio la kujiuzulu kwa nusu ya wabunge kwa madai ya ukata imetufungua macho kwa kuelewa aina ya wabunge tuliowapeleka bungeni. Sasa tumeelewa kwamba baadhi ya wabunge waliomba kura siyo kwa lengo la kutaka kutatua matatizo ya wananchi, bali kwa maslahi binafsi. Vinginevyo, haiingii akilini kusikia mbunge akisema bila kumung’unya maneno kwamba laiti angejua ubunge hauna fedha nyingi asingeacha taaluma yake kuganga njaa bungeni.

Tunapata shida kuwaelewa wabunge wanaodhani bungeni ni mahali pa kuchumia matumbo au kupata ukwasi. Tulidhani kelele za wananchi dhidi ya ongezeko la posho za vikao zilitosha kuwaamsha wabunge watambue kwamba posho hizo za vikao siyo tu zilikuwa nyingi, bali pia zilikuwa ni wizi wa mchana kweupe kutokana na malipo hayo kufanyika kwa kazi ambayo tayari wamelipwa kuifanya kupitia mishahara yao.

Ni kichekesho cha mwaka Spika anaposema wabunge wa Kenya wanawacheka kwa kutojiidhinishia fedha nyingi wakati ndio wanaopitisha bajeti ya serikali, wakati akijua fedha wanazojilipa wenzao wa Kenya zilipingwa sana na wananchi lakini hawakusikilizwa. Hapa nyumbani serikali yetu ni sikivu na ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete alisitisha posho hizo baada ya wananchi kusema hapana.

chanzo. Wabunge wanaotishia kujiuzulu wafanye hivyo haraka

Sisi tunasema wabunge wanaotishia kujiuzulu eti kwa kutiwa umaskini na ubunge waachwe waachie ngazi haraka na wasibembelezwe kwa kauli kwamba wakijiuzulu nchi yetu itapata gharama za kufanya chaguzi ndogo. Tunasema litakuwa jambo la kheri iwapo wabunge maslahi wataondoka ili tuwapate wengine wenye dhamira na moyo wa kuwatumikia wananchi. Tunawataka wabunge wenye ujasiri wa kujiuzulu wafanye hivyo sasa.
 
Back
Top Bottom