SoC02 Utawala wa haki si sheria Afrika

Stories of Change - 2022 Competition

mkalimani nyakaya

New Member
Aug 25, 2022
3
0
UTAMBULISHO

Andiko hili limeandikwa na Mkalimani Nyakaya, kama mwandishi mkuu wa andiko, kwa upana, linakwenda kuangazia nyanja ya utawala bora na demokrasia, likigusa sheria kandamizi na vitendo vya ukiukwaji wa haki na uhuru vinavyofanyika sehemu mbalimbali ndani ya bara la Afrika.

Mwandishi analiangazia bara la Afrika kama sehemu kuu ya andiko hili kwa sababu kuu mbili:- Kwanza, Afrika, kama bara bado liko katika mageuzi ya awali ya kiuchumi, kisiasa na hata kiteknolojia, hivyo lina nafasi ya kujifunza na kwenda sambamba na mabadiliko chanya na yenye tija. Sababu ya pili, ikiwa ni kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na viongozi kadhaa katika nchi za kiafrika kupitia serikali zao zilizopo madarakani.

Mwandishi anazungumzia ugeni (Afrika kuwa kwenye hatua za awali za mageuzi) wa bara hili kwenye mapinduzi ya uchumi, siasa na teknolojia akiwa na maana kuu moja, kuchelewa kwa bara hili kwenye upatikanaji wa uhuru wa nchi zake kumepelekea kuchelewa kwa maendeleo ukilinganisha na nchi zinazotoka kwenye mabara mengine kama Marekani na Ulaya hivyo kuchelewesha maendeleo ya kiuchumi, kiteknolojia na hata kisiasa.

UTANGULIZI
Utawala wa sheria ni filosofia inayotoa mwongozo wa uwajibikaji kwa raia wote au taasisi katika nchi au taifa, wakiwajibishwa na sheria zenye mlengo mmoja wa usawa, pasipo kujali cheo au nafasi ya muwajibishwaji katika taifa au nchi husika. Mwanafalsafa John Locke alitanabainisha kuwa “uhuru katika jamii Fulani hutokea pale tu unapokuwa chini ya sheria zilizotungwa na chombo chenye mamlaka ya utungaji sheria, sheria husika zinapaswa kuwa sheria zitakazomgusa kila mmoja wetu, pasipo vizuizi vyoyote kutoka kwa serikali au vizuizi binafsi vinavyoweza kutatiza uhuru huo”.

Utawala wa sheria unapaswa kuwa msingi imara wa taifa lolote katika kujenga uongozi bora, wenye tija na uliotukuka. Unapaswa kuwa msingi unaojenga mfumo mzima wa katiba.

Mwanafilosofia wa kale kutoka ugiriki aliyefahamika kama Aristotle anatukumbusha kuwa “ni vyema na sahihi sheria ikatuongoza kuliko kuongozwa na mtu yeyote”. Katika andiko lake linalokwenda kwa jina la “Politics”, Aristotle anaandika “Utawala wa sheria ni kanuni inayoelekeza kuwa, watu wote na taasisi katika taifa au jamii wanapaswa kuwajibishwa kupitia sheria zilizopo na zenye usawa kwa wote”.

Kiongozi kutoka taifa la Roma aliyefahamika kama Cicero anatuambia kuwa “Sisi sote ni vijakazi wa sheria, ili tuwe huru”.

Tunapoiangazia kwa ukaribu tafsiri halisi ya neno “Utawala wa sheria” ndani ya mataifa au nchi zinazopatikana ndani ya bara la Afrika, tunakutana na mwelekeo tofauti kabisa na ule ambao ulijengwa na wanafilosofia wa mwanzo kama Aristotle, Plato, John Locke, James Harrington, Mchungaji John Ponet, Cicero na wengineo. Kwa upande wa Afrika, tunakutana na nguvu ya wenye madaraka dhidi ya wale wasio na madaraka, tunakutana na nguvu ya chama tawala dhidi ya vyama vya upinzani, tunakutana na sheria ya mtawala kuwa na nguvu dhidi ya sheria za nchi husika.

Kwa bara la Afrika utawala wa sheria ni ule ambao mtawala ataamua kuwapa wananchi wake na si vinginevyo, haki na uhuru ni ule ambao mtawala husika ataamua kwa wakati husika, na si vinginevyo. Lakini Thomas Payne katika kijitabu chake kilichoitwa “Common sense” anatueleza kuwa “katika taifa la Marekani, sheria ndiye mfalme. Serikali yoyote iliyo timilifu Sheria ndiye mfalme, hivyo katika nchi yoyote iliyo huru sheria inapaswa kuwa mfalme na haipaswi kuwa vinginevyo”.

Katika nchi nyingi za kiafrika, Mabunge na vyombo vingine vya kisheria kama mahakama na mabaraza ya haki vinazidiwa nguvu na upande mmoja wa Serikali, hivyo basi sheria pekee zitakazotungwa na Bunge ni zile ambazo mtawala na Serikali yake watavutiwa na kupendezwa nazo, haki pekee zitakazopatikana ndani ya vyombo vya haki kama Mahakama ni ile tu ambayo mtawala ataamua inafaa na inayofanya kazi kwa niaba yake.

Haya yote yamepelekea kuwa na woga kwa viongozi mbali mbali ambao kwa nafasi zao wanapaswa au walipaswa kukemea uovu au unyimwaji wa haki unaofanywa na Serikali husika, kukosekana kwa ujasiri wa kumkosoa au kumshauri mtawala kumepelekea kuwa na Serikali ambayo Rais au mtawala ndiye sheria, ndiye katiba, ndiye Bunge na pia ndiye Mahakama, hivyo kuleta tafsiri halisi ya andiko hili kuwa “utawala wa sheria si haki” mtu anayopaswa kupewa katika bara la Afrika.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema “Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa”.


KUWA NA KATIBA BORA, IMARA NA INAYOHESHIMIWA KAMA MSINGI WA UTAWALA BORA.
Taifa lolote lenye msingi mzuri wa utawala bora, si tu linatakiwa kuwa na Katiba imara na yenye kushirikisha raia wa kada zote, bali pia kuwa na Katiba inayofuatwa na kuheshimiwa na pande zote na kwa nyakati zote. Hood Phillips anasema “Katiba inatumika kuzielezea kanuni zote zilizoandikwa na zisizoandikwa, zikielekeza utendaji wa taifa na watu wake”.

Wana filosofia kadhaa wamekwenda mbali na kuitafsiri Katiba kama chombo muhimu kwenye utendaji wa taifa lolote dhidi ya Serikali inayowaongoza. Mwanafilosofia George Cornewell lewis anatafsiri katiba kama “Mfumo na mgawanyo wa nguvu ya umma katika kuiongoza jamii au serikali”. Nae Leacock anatuambia kuwa “katiba ni muundo mkuu wa serikali”.

Mwanafilosofia Gilchrist anaenda mbali Zaidi kwa kusema “Katiba ya taifa ni muundo wa kanuni au sheria, zilizoandikwa au kutoandikwa zinazoamua utendaji wa serikali, mgawanyiko wa madaraka kwa mihimili ya Taifa na nguvu zake au kanuni kuu zinazoelekeza namna ya utumiaji wa nguvu husika”.

Yafuatayo yanapaswa kuwa sehemu ya katiba inayolinda maslahi ya utawala bora:-

(i). Katiba husika inapaswa kuyalinda maslahi ya raia wake kwa usawa
Katiba ya taifa lolote ndiyo sheria mama, hivyo inapaswa kutoa mwongozo wa namna gani taifa linapaswa kuendeshwa, inapaswa kutoa usawa baina ya wananchi na serikali yao pasipo kuweka tabaka baina ya wanaoongoza na wanaoongozwa.

(ii). Katiba inapaswa kuhakikisha usawa baina ya mihimili mitatu ya kimamlaka yaani Bunge, Mahakama na Serikali pasipo muingiliano, au upande mmoja kuwa na nguvu kuliko mwingine na kupelekea kuingilia shughuli za mihimili mingine

Kwenye nchi nyingi kutoka Afrika, kuna tatizo la Serikali kuingilia shughuli za mihimili mingine yaani Bunge na Mahakama, Bunge ndilo linalopaswa kuwa chombo pekee cha utungaji wa sheria zenye manufaa na maslahi kwa taifa zima, lakini Afrika ya leo, Serikali inalitumia Bunge kama chombo cha kupitisha miswada na sheria zenye maslahi tu kwa Serikali iliyopo madarakani, hata kama hazina maslahi na taifa zima au wananchi.

Bunge pia lina kazi ya kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa sheria ilizozitunga pamoja na miradi mbali mbali ya maendeleo, hali imekuwa tofauti kwa Serikali nyingi za kiafrika ambazo zimekuwa sehemu ya utungaji wa sheria zake nje ya Bunge, kuzipitisha sheria husika na kuzitumia pasipo baraka za Bunge.

Lakini si tu kwenye utungaji wa sheria, hali imekuwa tofauti hata kwenye usimamiaji wa shughuli za serikali kwa Bunge kukosa nguvu na sifa za kuikemea na kuikosoa Serikali, Afrika imeshuhudiwa miradi mingi inayofanywa na serikali pasipo usimamizi wala ukemeaji wa Bunge, mfano nchini Tanzania kupitia serikali ya awamu ya tano chini ya hayati Rais Magufuli, Taifa limeshuhudia miradi mingi iliyofanywa na Serikali kinyume cha utaratibu kama ununuzi wa baadhi ya ndege za shirika la ndege la Tanzania yaani ATCL, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato, hii ni mifano michache ya namna ambavyo Serikali inaweza kuwa na nguvu zaidi kuliko mihimili mingine, hili linaleta mgogoro wa kimaslahi kwa kulinyima Bunge haki yake ya kikatiba ya kutunga sheria na kuisimamia serikali kwenye shughuli zake.

Mahakama ni chombo cha haki kinachopaswa kuwa huru, lakini hali iko tofauti kwa nchi nyingi za kiafrika, kwa Mahakama kutumika kama chombo cha Serikali dhidi ya wale wote wanaoonyesha kutoridhishwa na mwenendo mbaya wa Serikali yao, tumeshuhudia wapinzani kutoka mataifa kadhaa wakikamatwa mara kwa mara na kupewa kesi zisizo na mashiko kama sehemu ya kuwanyamazisha kutetea maslahi ya raia wenzao, Nchi kama Rwanda imekuwa na mfumo wa kuwakamata wapinzani na kuwafunga, Uganda imeshuhudia mara kadhaa waliokuwa wagombea wa kiti cha urais kutoka upinzani Kizza Besigye na Robert Kyagulanyi Ssentamu “Bobi Wine” wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka pasipo utaratibu, Tanzania imeshuhudia Freeman Mbowe akisota gerezani kwa kipindi kirefu pasipo dhamana kwa kesi ya ugaidi ambayo baadae ilikuja kufutwa kwa kuwa tu mwendesha mashtaka hakuwa na nia ya kuendelea nayo.

Katiba ya taifa lolote, inapaswa kuweka mkazo zaidi kwenye eneo hili, kwani msingi wa utawala bora na unaofata sheria unapaswa kuanzia kwenye msingi wa kuwa na mihimili isiyoingiliana kwenye mamlaka na madaraka.

(iii). Katiba inapaswa kuainisha uwajibishwaji wa viongozi wote wa serikali na taasisi mbalimbali pasipo upendeleo
Katiba za mataifa mengi ya kiafrika, zina mapungufu makubwa kwenye namna viongozi wakubwa wa kitaifa wanavyopaswa kuwajibishwa kwa makosa wanayoyafanya wakiwa madarakani, mfano Katiba ya Tanzania imeweka wazi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatowajibika kwa makosa yoyote atakayoyafanya akiwa kwenye kiti cha Urais, hivyo basi kutoa nafasi ya Rais kuwa juu ya sheria pasipo kuwa na wajibu kwa yoyote au chochote katika kipindi chake chote cha madaraka, anaweza kufanya makosa ambayo yanaweza kuwaathiri wananchi fulani au taifa zima pasipo kuwajibika.

Mapungufu haya ya kikatiba yanapelekea kuwa na sheria nyingi kandamizi, zenye mapungufu na zinazobadilika badilika kutoka Serikali kuu moja kwenda nyingine pasipo kuwa na uwajibikaji zinapoleta madhara, mfano, Serikali ya Tanzania chini ya hayati Rais John Pombe Magufuli ilipitishwa sheria ndogo ya wafanya biashara wadogo wadogo maarufu kama “Wamachinga” kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali ambavyo walivilipia kiasi cha shilingi 20,000/= kila kimoja, kupitia vitambulisho hivi kilikusanywa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja ya kitanzania na Serikali, kitambulisho hiki kilitambulika kisheria na kuwapa nguvu kufanya biashara kwenye maeneo rasmi na yasiyo rasmi kwa uhuru na hata kuwasaidia kwenye ulipaji wa kodi mipakani kwa bidhaa zisizozidi kiasi cha shilingi 5,000,000/=.

Baada ya miaka kadhaa kupita na utawala kubadilika, leo tunaona kitambulisho hiki hakitambuliki tena, wafanya biashara waliolindwa hapo mwanzo na vitambulisho hivi hawalindwi tena, haya ni matokeo ya mapungufu ya kikatiba ambayo kama yangeelekeza uwajibikaji wa kiongozi wa juu, basi wafanya biashara wadogo walioathirika na usitishwaji wa vitambulisho walipaswa kufidiwa na hata kuishtaki serikali kuu na Rais kwa hasara hii na hasara zote zinazotokana na kubadilika kwa sheria pasipo kujali maslahi ya wananchi na hasara wanazokutana nazo.

(iv). Katiba ihakikishe usawa unapatikana kwenye utafutaji wa haki kwa raia wote
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 13 ibara ndogo ya 6 kifungu A inatukumbusha juu ya kuhakikisha kuwa usawa unapatikana wakati wa utafutaji haki, na kwa kila aliyekosa kupewa nafasi ya kusikilizwa, lakini pia kupewa stahiki kwa yule aliyetendewa uovu.

Katiba inapaswa kuhakikisha kuwa, mahakama ni kimbilio la wale wote wenye njaa na kiu ya haki, kwa kuweka mazingira rafiki kwa kila mwananchi kuyamudu, leo kiuhalisia, wananchi wengi wanashindwa kupata haki zao za msingi kwa kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wa kesi, kupitia hili mataifa ya kiafrika, Tanzania ikiwemo yanaweza kuwa na mipango inayotambulika kikatiba ya kutoa huduma za bure za kisheria kwa wale wote wenye uhitaji wa kweli, hili litasaidia kwenye upatikanaji wa haki.

(V). Katiba inapaswa kujilinda
Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia nchi nyingi za kiafrika na watawala wake, wakibadili Katiba zao au baadhi ya vifungu katika Katiba zao, wakiwa na lengo la kuongeza muda wa kukaa madarakani, lakini pia kuwa na Katiba inayolenga kuwakandamiza wale wote wanaoonyesha kupingana na serikali au matakwa ya watawala. Mifano halisi, tuna nchi kama Burundi wakati wa Pierre Nkurunziza, Rwanda ya paul Kagame, Togo ya Faure Gnassingbe na Uganda ya Yoweri Kaguta Museveni ikiwa sehemu ya mifano hai ya Katiba zilizobadilishwa kukidhi matakwa ya watawala kukaa madarakani zaidi ya muda waliopaswa kuwepo madarakani.

Katiba kama sheria mama inapaswa kuwa na ulinzi binafsi, kwa kuwa na vifungu vigumu zaidi ambavyo vinaweka ugumu kwa watawala kuibadili kwa urahisi ukilinganisha na sasa.

Kuwa na kura ya wazi kwa wananchi wote ni sawa, lakini kura ya wazi kuamuliwa na matokeo ya ushindi wa asilimia 50 ili katiba ibadilishwe si sawa, hilo bado haitoshi kuwa ulinzi mzuri dhidi ya viongozi wachafuazi na waharibifu wa haki.

Lakini pia, mabunge mengi ya nchi za kiafrika yametawaliwa na upande wa chama tawala kwa kuwa na viti vingi bungeni, hivyo kuwa rahisi kwa mtawala na chama chake kupiga kura ya kuendelea kumbakisha madarakani hata baada ya muda wake wa kikatiba kuisha, hivyo kuna haja ya kuwepo kwenye Katiba sharia elekezi zinazowabana wabunge juu ya kubadili muhula na muda wa kukaa madarakani kwa Rais au mtawala.

DEMOKRASIA INAVYOPASWA KUWA MSINGI WA UTAWALA BORA
Neno demokrasia kwa mara ya kwanza lilianza kutumika rasmi na wagiriki, likiwa na maana ya “watu na kanuni”.

Demokrasia ni msingi unaopaswa kugusa moja kwa moja maisha ya kila mwananchi pasipo kujali itikadi za chama, Imani za kidini, eneo au sehemu anakotokea, katika kuleta maendeleo chanya ya mtu mmoja mmoja yanayoguswa na sera zenye lengo la kufanya mageuzi ya kimaendeleo kwa taifa zima. Abraham Lincorn anasema “demokrasia ni serikali ya watu, inayoongozwa na watu, kwa ajili ya watu”.

Kiuhalisia, imekuwa tofauti sana na ngumu kwa viongozi wengi wa nchi za bara la Afrika kufata na kutii sheria wanazopaswa kuziheshimu ikiwemo Katiba, sio tu kwenye maisha ya kila siku bali hata katika kipindi cha chaguzi mbalimbali zinazofanyika.

Uvunjwaji wa sheria unajidhihirisha kwa mfano ulio hai katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, nchini Tanzania wa mwaka 2019, ambapo kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa demokrasia. Viongozi wengi wa Vyama vya upinzani walitolewa kasoro mbalimbali na kufutiwa ushiriki wao katika uchaguzi kama wagombea hivyo kupelekea maeneo mengi ya mitaa katika nchi kufanyika uchaguzi uliohusisha chama kimoja cha CCM (chama tawala) kwa asimilia 98, mfano katika wilaya ya Kinondoni pekee ambayo ilikuwa na mitaa 106 inayowaniwa kulikuwa na mitaa 105 ambayo wagombea wa CCM walipita bila kupingwa, na kubakisha mtaa mmoja pekee ambao ulikuwa na mwakilishi au mgombea wa chama cha upinzani.

Hali hii ilipelekea viongozi na vyama vya upinzani wakiongozwa na Chadema, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD, ACT-Wazalendo na UMD kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo.

Tukiangazia maneno ya Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Ally Hassan Mwinyi kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM mwezi juni mwaka 1995 alipozungumza kama Rais anayemaliza muda wake, alisema kuwa “mtihani wa demokrasia ya ukweli utaonekana pale ambapo kila mmoja wetu analazimika kufanya maamuzi ya busara yeye binafsi badala ya kushabikia msimamo wa kundi lake”.

Matokeo ya uvunjwaji wa haki na sheria katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, unapingana moja kwa moja na maneno ya Rais Mwinyi, uchaguzi huu uliongozwa na msimamo wa ushabiki wa kundi lililoongozwa na utawala wa CCM katika kuhakikisha wanashinda uchaguzi huo kwa hali yoyote ile dhidi ya upinzani, kitu ambacho ni kinyume cha demokrasia na mwongozo wa utawala bora.

Katika mfano mwingine, tunamuangazia mwanamama kutoka Rwanda, Diane Rwigara aliyejitoa kugombea uchaguzi wa Rwanda mwaka 2017 ndidi ya Rais aliyeko madarakani Mh. Paul Kagame. Kabla ya kufika kipindi cha uchaguzi Diane alikamatwa na polisi kwa makosa kadhaa ikiwemo ukwepaji wa kodi na ulaghai, lakini pia alishutumiwa kuwa tishio kwa usalama wa nchi na mwenye lengo la kuzuia uchaguzi. Haya yote yakiwa na lengo la kuzuia ushiriki wa Diane katika uchaguzi husika, hatimaye alifunguliwa mashtaka na kuhukumiwa kifungo Octoba 2017 na baadae kuachiwa huru na mahakama Octoba 2018.

Uchaguzi huu wa Rwanda 2017, unatupa taswira halisi ya namna gani viongozi waliopo madarakani wanavyoweza kutumia madaraka yao kupindisha demokrasia ili kujihakikishia kuendelea kusalia madarakani ikiwa ni kinyume cha misingi ya utawala bora.

Yafuatayo yanapaswa kuwa msingi kwenye taifa lolote lenye demokrasia imara katika kuchochea utawala bora:-

1. Sheria za nchi zinapaswa kuwa wazi na za haki, lakini pia serikali kuwa tayari kukosolewa na watu, ambao wanaweza kuandamana au kukusanyika pasipo shaka wala uoga na kueleza hisia zao juu ya sheria kandamizi au hali mbaya ya uchumi na siasa
Msingi huu unaonekana kutokuwa na nafasi kwenye nchi nyingi za Afrika, mfano halisi tunaweza kuuona kwenye mataifa kadhaa tukianza na taifa la Mali ambalo hivi karibuni limeshuhudia mauaji ya mwanaharakati Hassan Dumbuya aliyeuawa na polisi wakati wa uvamizi katika msako wa wahusika wa maandamano yaliyofanyika wiki moja nyuma.

Wakati huo huo Rais wa taifa hilo la Mali Mh Julius Maada Bio anayataja maandamano yaliyofanyika kama jaribio la kuipindua serikali yake.

Kilichotokea nchini mali ni kinyume cha mwongozo wa utawala wa sheria, kwani demokrasia na utawala wa sheria unatoa nafasi kwa kada zote kufikisha malalamiko yao kwa njia zinazotambulika kikatiba ikiwemo maandamano ya Amani na mikusanyiko.

2. Sheria zinapaswa kuwa na uwakilishi wa wananchi, kuwa zenye uwazi kwa nyakati zote
Lengo la demokrasia, ni kuwa na viongozi wanaotanguliza maslahi ya wananchi kwanza kuliko chama au kundi la watu fulani, hili limedhihirika katika chaguzi zilizomalizika mwezi Agosti 2022 nchini Kenya ambapo dunia imeshuhudia kuchaguliwa kwa viongozi wasiofungamana na chama chochote, mfano mwanamama Kawira Mwangaza kutoka Meru alifanikiwa kuwa Gavana mteule wa Meru kama mgombea binafsi asiye na chama.

Uchaguzi huu unatoa sura mpya kwenye demokrasia na utawala wa nchi ya Kenya kwa kuwa na kiongozi waliochaguliwa na wananchi kwa ubora wa Sera na mipango ya maendeleo waliyoionyesha dhidi ya mfumo wa kuchagua viongozi kwakuwa tu wanatoka kwenye chama au taasisi wanayoishabikia, hili ni jambo geni kwa nchi nyingi za kiafrika ambazo hazitoi nafasi ya mgombea binafsi (Tanzania ikiwa sehemu ya nchi hizo), hivyo nchi ya Kenya imefanikiwa kuonyesha kwa mfano namna utawala bora na wa sheria unavyopaswa kuwa.

Uchaguzi wa Kenya ulikwenda mbele Zaidi na kuwa moja ya chaguzi zenye uwazi mkubwa, ambaopo chombo cha habari cha “BBC News Swahili” kupitia andiko lake la tarehe 19 mwezi Agosti 2022 lililokwenda kwa jina la “Mambo 10 yanayotofautisha uchaguzi wa kenya na nchi nyingine za afrika” waliuita uchaguzi huo kuwa ni wenye “Uwazi mkubwa usio wa kiafrika”.

Raia wa nchi ya Kenya na Dunia nzima, walipewa nafasi ya kuangalia matokeo ya uchaguzi kwa kila hatua na kupakua matokeo hayo kupitia “Portal” au mlango katika tovuti ya uchaguzi ambayo iliweza kutoa nafasi kwa mtu yoyote kupakua na kuangalia matokeo yanayoendelea kutangazwa kwa wakati wote.

3. Sheria inapaswa kuwa huru na kujiendesha yenyewe pasipo kuwa na ushawishi kutoka nje ya muundo wake (serikali).

Chombo kikuu kinachopaswa kuwa mtafsiri wa sheria katika taifa lolote ni mahakama, hivyo basi muundo mzima wa mahakama unapaswa kuwa huru na usiofungamana na upande wowote kuepuka ushawishi na kuingiliwa katika kazi zake.

Nchi nyingi za Afrika ikiongozwa na Tanzania, muundo wake wa juu wa mahakama, kuanzia jaji mkuu, na majaji wengine unatokana na mapendekezo na hatimaye teuzi za Rais, ambaye kimsingi ni kiongozi mkuu wa serikali, hivyo kuifanya mahakama kutokuwa sehemu salama na huru kwa utoaji wa haki, kwani kupitia teuzi hizi chembe chembe za ushawishi na muingiliano wakati wa utendaji kutoka serikali kuu hautoepukika, na hili litajidhihirisha haswa kwenye mashauri au kesi ngumu zitakazoihusu serikali kuu na washirika wake.

Mahakama kama chombo kikuu cha haki, inapaswa kuwa huru kama taasisi inayojitegemea kuanzia watendaji wake hadi namna inavyojiendesha, jaji mkuu na majaji wengine wote wa mahakama hawapaswi kuwa wateuzi wa Rais, wanapaswa kuajiriwa kupitia mfumo maalum wa ajira kwa viongozi wa mahakama kulingana na vigezo husika, mfumo huu wa ajira utakuwa huru na hautoweka chembe chembe ya ushawishi kutoka serikali kuu, kwa matokeo hayo jaji hatokuwa mwajiriwa wa serikali kuu bali mwajiriwa wa mahakama na sekta ya sheria kwa ujumla.

4. Mahakama kuwa na mfumo madhubuti na imara kwenye uendeshaji wa kesi kujiepusha na kesi za kisiasa.

Kuna mifano mingi iliyo hai namna serikali inavyotumia mfumo dhaifu wa kimahakama kutekeleza matakwa yake ya kisiasa, tuna serikali ya Paul kagame dhidi ya mgombea wa chama cha upinzani mwanamama Diane, Serikali ya Tanzania dhidi ya viongozi wa upinzani wanaokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya mara kwa mara yasiyo na tija, tuna serikali ya Kaguta Museven wa Uganda dhidi ya viongozi wa upinzani na wengineo wengi.

Kuepuka mahakama zetu kutumiwa kisiasa na viongozi wa serikali, yafuatayo yanapaswa kuwa sehemu ya msingi na uimara wa mahakama kama sehemu ya kutekeleza utawala bora na unaofata sheria:

5. Mahakama kukataa kuwa na kesi ambazo ushahidi wake haujakamilika, hili litapunguza na hatimaye kuondoa kesi nyingi za kisiasa, Serikali kupitia polisi na waendesha mashtaka wake watalazimika kufungua mashtaka pale tu ambapo ushahidi utakuwa umekamilika,na hii itapunguza au kuondoa mrundikano wa kesi ndani ya mahakama na hata mrundikano wa watuhumiwa ndani ya magereza, na hata pale ushahidi utakapoonekana kukamilika na kesi kufunguliwa, kesi nyingi zisizo na mashiko hazitosimama kwa muda mrefu ndani ya mahakama kwa kuwa na ushahidi wenye mapungufu na hatimaye haki kupatikana kwa haraka na urahisi kwa wale wote wanaofunguliwa mashtaka kisiasa.

6. Ufutwaji wa kesi kiholela, tumeona kupitia mahakama za Tanzania mara kwa mara DPP kueleza kutokuwa na haja ya kuendelea na kesi, hili mara nyingi hufanyika wakati ambao watuhumiwa wa kesi hizo wameshakaa kipindi kirefu magerezani, wengine pasipo dhamana kwa kesi zisizo na mashiko kwa sababu ya siasa, hivyo basi mahakama zetu zinapaswa kuwa na sheria ngumu na zinazowajibisha linapotokea jambo la namna hii ili kupunguza uchezewaji wa haki na uhuru wa wengine kisiasa.

Adhabu zinapaswa kutolewa katika mfumo wa fidia, dhidi ya DPP na serikali pindi inapotokea DPP kutokuwa na haja ya kuendelea na kesi husika, hii itachangia kupunguza kesi nyingi za kisiasa zisizo na mashiko.

7. Makosa yasiyo na dhamana kutumika kama moja ya siraha kubwa ya Serikali dhidi ya watuhumiwa wa kisiasa, Mahakama kama chombo cha haki hakipaswi kuruhusu uwepo wa makosa yasiyo na dhamana, kwani kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Katiba, Katiba ya Tanzania kupitia ibara ya 13 ibara ndogo ya 6 inaweka wazi kuwa “kila mtu hana hatia hadi pale itakapothibitishwa vinginevyo”, hivyo basi kitendo cha watu kuendelea kukaa gerezani kwa makosa yasiyo na dhamana ni kuwatia hatiani kabla ya uthibitisho wa hatia kutoka kwenye chombo chenye dhamana ya kufanya hivyo.

Mahakama zinapaswa kuruhusu utolewaji wa dhamana kwa makosa yote pindi kesi zinapofika chini yake, pia mahakama kama chombo cha haki zinapaswa kuwa mshauri wa chombo cha utungaji sheria yaani Bunge, kuzifanyia marekebisho sheria kadhaa na kuondoa kipengele cha unyimwaji wa dhamana kwa baadhi ya makosa.

8. Mahakama kuchezewa na mfumo wa Magereza na Polisi, Mahakama kama chombo cha haki inapaswa kuheshimiwa na kuogopwa na taasisi zote kwenye utendaji wake, lakini hili limeonekana tofauti kwa upande wa Magereza na Polisi ambao mara kadhaa wameonekana kutoheshimu ukubwa wa mahakama kwa makusudi na kushindwa kuwaleta watuhumiwa haswa wa kisiasa mahakamani kwa visingizio kadhaa ikiwemo ubovu wa magari au kukosekana kwa usafiri wa kuwaleta watuhumiwa mahakamani.

Mahakama inapaswa kuwa na makali kwenye hili kwa kutoa adhabu kadhaa zikiwemo fidia kwa watuhumiwa kwa kuwakosesha haki yao ya kikatiba ya kusikilizwa na mahakama,hii itapelekea kuzuia unyanyaswaji unaofanywa na magereza na polisi kwa makusudi kwa lengo la kuendelea kuwaweka magereza au vizuizini watuhumiwa wengi wa kisiasa kama mbinu ya mateso, wakijua fika kukosekana kwao mahakamani kutasababisha uhairishwaji wa kesi au kutosikilizwa kwa kesi hivyo kuendelea kukaa gerezani au kizuizini katika kipindi chote wakiendelea kusubiri tarehe mpya ya kusikilizwa kwa kesi zao.

9. Sheria inapaswa kutumika kwa usawa na haki, sababu hakuna anayepaswa kuwa juu ya sheria zaidi ya sheria yenyewe.

Mwisho, wananchi kama walivyo viongozi, wanapaswa kuwa na sauti dhidi ya sheria zinazowaongoza pindi zinapoonekana kuwakandamiza, wananchi wanapaswa kuwa na sauti dhidi ya viongozi wa Serikali wasiofata sheria au kutokidhi matakwa ya utendaji wao kazi kwa wananchi.

Wananchi wanapaswa kuwa huru, kufungua mashtaka kupinga uteuzi wa mtendaji yoyote wa Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa zima, kama tunavyoona kwenye kesi iliyopelekea kufutiwa leseni ya kufanya shughuli za kisheria kwa Mwanamama Fatma Karume, Fatma Karume ni mwanasheria mzoefu, na kwa wakati mmoja alishawahi kuwa Rais wa chama cha wanasheria Tanzania, Fatma Karume kwa mara ya kwanza alisimamishwa kufanya shughuli za sheria na mahakama kuu ya Tanzania, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutenda makosa ya kinidhamu wakati wa shauri la usikilizaji wa kesi akimuwakilisha mteja wake “Alliance for change and trasparency”, akipinga uteuzi wa Adelardus Kilangi kama mwanasheria mkuu wa serikali, kauli zote zilizoongelewa na Fatma karume zilikuwa sehemu ya uhuru na haki yake ya kikatiba ya kujieleza kwa uhuru, Fatma Karume alinyang’anywa leseni yake tarehe 23 Septemba mwaka 2020 na kamati ya maadili ya wanasheria yaani “Advocate committee”.

Fatma Karume na Alliance for change and transparency walikuwa na haki ya kikatiba ya kufungua shauri mahakamani kupinga teuzi ya kiongozi wa serikali, kitendo cha kumfutia leseni Fatma karume kwa kutekeleza jukumu lake la kikatiba ni ishara tosha ya utawala wa haki kutokuwa sheria ndani ya Taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla.

HITIMISHO

Mwandishi wa andiko hili, anahitimisha kwa kuziasa Serikali za mataifa ya Afrika, kuheshimu na kuzifata Katiba walizoapa kuzilinda wakati wa kuingia madarakani.

Lakini pia kuhakikisha wanatawala kwa msingi wa demokrasia na utawala bora kipindi chote cha utawala wao, kwani kiongozi bora ni yule mwenye baraka na heshima za wananchi anaowaongoza, kuliko yule anayeogopwa kwa utawala wa mabavu, wenye ukandamizaji wa haki na usiozingatia sheria.


TAMATI.
 
Back
Top Bottom