Uraia wa Nchi mbili ni Kitendawili!

kbm

JF-Expert Member
Oct 5, 2012
5,222
1,670
"Mjadala wa Katiba: Mjumbe K. Singo amesema kuwa kuwatambua raia waishio ughaibuni kwa kuwapa Uraia pacha kutaifanya Tanzania kuongeza pato la taifa!"




"wadau mbalimbali wameijadili hoja hii, lakini bado ni kitendawili. Je wewe unasemaje kuhusu Uraia pacha au Uraia wa nchi mbili ?"


*HOJA...

Evarist Chahali
chahali@about.me
kutoka Ughaibuni

NIANZE kwa kumpongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwa jitihada zake kubwa kupigania kupitishwa kwa sheria ya uraia pacha.
Pamoja na upinzani mkubwa katika suala hilo, Waziri Membe ameendelea kusimama kidete na majuzi tu aliendeleza jitihada hizo katika mkutano wa rasimu ya Katiba Mpya uliofanyika katika wizara yake.
Binafsi, ninaelewa mantiki ya hoja za wanaopinga uraia pacha. Hata hivyo, mantiki hizo zimepitwa na wakati. Kimsingi, moja ya sababu za kuharamisha uraia pacha ni siasa yetu ya nje katika zama za Ujamaa. Wakati huo, nchi yetu ilielemea upande wa Wakomunisti, na kwa hakika enzi hizo za kinachofahamika kama Vita Baridi zilitawaliwa sana na matishio ya kiusalama. Kwa wakati huo, raia mwenye uraia wa nchi mbili angeweza kuonekana kama kibaraka wa nchi za Magharibi na hivyo kuwapo kwa uwezekano wa raia huyo kutumiwa kuihujumu nchi.
Kwa sasa hakuna hoja nzito dhidi ya uraia pacha. Kama ni suala la utiifu kwa nchi (hoja ambayo imekuwa ikipigiwa mstari kwa nguvu na wapinzani wa uraia pacha), sote tunafahamu jinsi nchi yetu inavyohujumiwa na kutafunwa na Watanzania wenzetu ambao naamini baadhi yao hawajawahi kutoka nje ya mipaka ya nchi yetu.
Kadhalika, baada ya kuua na kuzika itikadi ya Ujamaa, tumeshuhudia sio tu wageni kutoka nchi mbalimbali wakija huko nyumbani kwa minajili ya uwekezaji au ajira bali pia watawala wetu wamekuwa wakizunguka kila kona ya dunia kuhamasisha wageni kuja huko nyumbani, si kutalii bali kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao kwingine (second home).
Sasa kama ni ruksa kwa wageni ambao hawana ¡®udugu¡¯ na nchi yetu kuwa na haki ya kuifanya Tanzania kuwa nyumbani kwao, kwa nini isiwe hivyo kwa Watanzania ambao kwa sababu moja au nyingine walilazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine?
Na kwa vile kwa mujibu wa sheria zilizopo, Mtanzania akichukua uraia wa nchi nyingine anapoteza uraia wa Tanzania, basi pengine kuwahukumu waliolazimika kuukana uraia wa Tanzania ili wapate uraia wa nchi nyingine sio kuwatendea haki.
Ninatambua kunaweza kuwa na hoja ¡°kwa nini utake uraia wa nchi nyingine ilhali tayari una uraia wako wa kuzaliwa (wa Tanzania)?¡± Jibu jepesi ni kwamba sio kila aliyeamua kuchukua uraia wa nchi nyingine (na hivyo kulazimika kuukana uraia wa Tanzania) alifanya hivyo kwa kupenda. Kuna baadhi ya wenzetu waliolazimika kutafuta hifadhi ya ukimbizi nje ya nchi yetu na hatimaye kupatiwa uraia wa nchi zilizowapa hifadhi (mfano ni kundi la Wazanzibari waliopewa hifadhi Uingereza kutokana na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000)
Lakini kubwa zaidi katika suala hili la uraia pacha ni ukweli kwamba kumlazimisha Mtanzania anayetaka uraia wa nchi nyingine akane uraia wa nchi yetu ni kinyume cha haki za binadamu za raia huyo kwa sababu kimsingi ni Mtanzania kwa kuzaliwa. Huwezi kumnyima mtu haki kwa sababu za kufikirika kama hizo za kukosa utiifu kwa nchi. Kama ni hivyo basi hata wanasiasa wanapogombea kutuongoza katika chaguzi tungelazimika kuwanyima haki ya kuongoza kwa hisia tu ya ¡°kuna wanasiasa wasio na utiifu kwa nchi yetu.¡±
Majuzi nimemsikia Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akizungumzia suala la uraia pacha. Binafsi nadhani japo tunaaswa kusikiliza ushauri wa wazee wetu lakini sababu za kibaiolojia zinaweza kutufundisha kuwa uwezo wa kiakili huathiriwa na umri. Tumeshasikia habari za wazee ¡°wanaozeeka vibaya,¡± na japo ninamheshimu Mzee Kingunge lakini nadhani anazeeka vibaya.
Nisingependa kumjadili Kingunge kwa undani katika makala hii bali binafsi nimekuwa nikimwona mzee huyo kama mmoja wa watu waliomsaliti Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, walishirikiana katika jitihada za kujenga jamii ya usawa na haki lakini akamsaliti kwa kuungana na makundi ya kifisadi yaliyoifikisha Tanzania ilipo sasa. Ushauri wangu mwepesi ni kumpuuza Mzee Kingunge kwani mitizamo yake iliyopitwa na wakati haina nafasi katika Tanzania tunayoihitaji sasa.
Kimsingi, suala la Mtanzania kuishi nje ya nchi yake linaambatana na hisia za kibaguzi kwa namna fulani. Majuzi tu niliingia katika malumbano na ndugu yangu mmoja kuhusu mustakabali wa taifa nililolizungumzia. Alidai kuwa kwa vile nipo mbali na huko nyumbani (Tanzania) basi nitakuwa ¡°mtu wa kuambiwa tu¡± (kana kwamba kila tunachoambiwa si sahihi).
Kuna kasumba ya kibaguzi iliyoshamiri kwa muda mrefu kwa baadhi ya wenzetu huko nyumbani kutoangalia Watanzania tulio nje ya nchi yetu kama ¡°Watanzania vipande¡± (yaani si Watanzania kamili). Japo ni ruhusa kwao kubobea kwenye uchambuzi wa Ligi Kuu ya England kana kwamba wanaishi hapa, ni ¡°kosa la jinai¡± kwa sie tulio mbali na nyumbani kuzungumzia masuala yanayoigusa Tanzania yetu. Hawa ni wabaguzi tu wasiotaka kuelewa kuwa kwa sie wengine uwepo wetu huku unapelekea ¡°kukabwa koo¡± na swali ¡°Kwa nini iwe hivi kwa wenzetu lakini kwetu sivyo?¡±
Sina maana kila linalofanyika hapa Uingereza, kwa mfano, ni jema na ningetamani liwe hivyo huko nyumbani. Lakini kuna maswali kadhaa, hususan katika mfumo wa utawala unaotanguliza maslahi ya taifa badala ya watu binafsi au itikadi za kisiasa, au kufanikiwa kutenganisha taasisi na mtu binafsi. Kadhalika, wenzetu hawa licha ya wengi wao kutokuwa wacha Mungu wamefanikiwa sana kutilia mkazo maadili katika uongozi, huduma kwa umma na utawala bora kwa ujumla.
Ninaamini kuna wazalendo wengi tu Watanzania waliolazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine lakini nafsi na akili zao zipo huko nyumbani. Na hiyo ni kuweka kando ukweli kwamba wengi wetu bado tuna ndugu, jamaa na marafiki huko nyumbani. Kuwanyima Watanzania hawa haki ya kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu ¡®changa¡¯ (na sasa kushiriki katika jitihada za kupigania uhuru wa pili dhidi ya maadui wa nchi yetu kama vile ufisadi) ni kutowatendea haki.
Ninatambua kuwa baadhi ya wasomaji watahusisha mtizamo wangu katika suala la uraia pacha na ukweli kuwa nami ni miongoni mwa Watanzania walio nje, lakini ukweli ni kwamba hakuna sababu japo moja ya msingi ya kuwabagua Watanzania wenzetu, iwe ni kwa waliochukua uraia wa nje au kwa sababu nyingine yoyote ile. Ubaguzi ni suala lisilokubalika.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa Watanzania wenzangu kuunga mkono jitihada za Waziri Membe katika suala la uraia pacha, huku nikitegemea kuwa Katiba Mpya itatambua umuhimu wa suala hilo na hatimaye kuliruhusu. Umoja na nguvu.
=====


Joseph Mihangwa
jmihangwa@yahoo.com
Raia Mwema.

Uraia haubinafsishwi na mwekezaji wa kweli haulizwi uraia


BILA shaka wengi tunakumbuka kwa uchungu kabisa jinsi tulivyoshuhudia viwanda vilivyotengenezwa kwa mikopo ambayo ni sehemu ya deni la Taifa, vilivyouzwa kwa bei ya ¡¯kutupa¡¯ kwa wanaoitwa ¡¯wawekezaji¡¯.
Wengi wa ¡¯wawekezaji¡¯ hawa walichofanya ni kugeuza viwanda vile kuwa maghala na kuuza majumba na mtandao wa rasilimali ambazo zilikuwa chini ya viwanda; na kwa kuwa hawakuwa na nia hasa ya kuzalisha wengi waliuza mitambo au waliitelekeza kwa walinzi ambao hawakuwa na mwajiri wa moja kwa moja, kufanya walinzi wale waendelee kujilipa ¡¯mishahara¡¯ kwa kuuza mitambo ile ya gharama katika vipande vidogo vidogo kama vyuma chakavu.
Matokeo ya ubinafshaji katika maisha ya wanachi yalishuhudiwa kwa katika eneo la ukosefu wa ajira, ajira isiyo na uhakika na kutokuwa na hakika ya maisha ya kila siku na kupanda kwa gharama zisizoepukika za maisha.
Hiki ndicho kipindi ambacho nchi yetu ilishuhudia kina ¡¯Ngapulila¡¯ wengi ambao kwenda nje kutafuta maisha ndio lilikuwa suluhisho pekee la matatizo yao ya kiuchumi waliyokuwa wakipambana nayo, ambayo kwa bahati mbaya na kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yao walijikuta hawakuwa na mtu wa kuwasemea.
Ikumbukwe, msingi mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Azimio la Arusha ilikuwa ni kuwasemea wanyonge, ¡¯kubatilishwa¡¯ kwa Azimio la Arusha kule Zanzibar na kuachia nguvu ya ¡¯mitaji¡¯ kutamalaki, kulidhoofisha sana misingi ya utu na imani ya watu kwa serikali yao.
Walioondoka wakati ule wengi wao walikuwa ¡¯waathirika¡¯ wa mabadiliko yale yaliyoruhusu ubinafsishaji katika sekta zote muhimu, na ndiyo hawa tunawazungumzia leo kama ¡¯diaspora¡¯.
Kati ya masuala yanayozungumzwa sana ni kuruhusu uraia-pacha. Naamini na nimepata kusikia mara kwa mara viongozi wetu waandamizi wakitoa kauli za kukubaliana na suala hili la kuruhusu uraia-pacha wakitumia sababu zile zile walizotumia kwenye ubinafsishaji wa viwanda; sababu kuu inayotumika sasa katika kutaka kuhalalisha ¡¯uraia-pacha¡¯ eti ni kuvutia mitaji, kuongeza ajira na kuongeza pato la serikali kupitia kodi.
Imekuwa ni mazoea kwetu kuenenda kwa matukio. Kufanya maamuzi makubwa na yenye athari kubwa kwa spidi ya ¡¯kufa mtu¡¯. Kwa sababu hii, mara kwa mara tumejikuta tukifanya makosa, na kwa kuwa tu wazito kutambua makosa yetu, mara kwa mara tumejikuta tukirudia makosa yale yale, kwa kuwa hatujifunzi.
Safari hii pia, suala la uraia-pacha ¡¯tumeshauriwa¡¯ na sasa utekelezaji wake ni moja ya mambo yanayoenda kwa kasi kubwa, kwa hulka yetu si jambo la kustaajabisha. La kustaajabisha hapa ni jinsi gani suala hili linavyopelekwa-pelekwa, ni suala linalostaajabisha kwa kila mtu anayetaka kujisumbua kujifikirisha.
Kwa kuwa nchi yetu imejaa ¡¯wawekezaji¡¯ kutoka kila taifa, bila shaka wengi wangetamani kuitumia fursa hii; swali ni kwa kiasi gani uraia huu pacha utaendelea kuwafaidisha wengine (Wazungu, Wachina na wahamiaji wengine) na si Watanzania ni swali linalohitaji mjadala, lakini dalili za mvua ni mawingu.
Kuna kila dalili, suala hili linashabihiana kama ilivyo kwa wawekezaji wakati tunawafungulia milango, Watanzania waliaminishwa ¡¯uwekezaji¡¯ ni kwa faida ya Watanzania, kwa kuwa umasikini wetu umetokana na kutokuwa na mitaji. Kilichotokea kila mtu anafahamu, Watanzania waligeuka manamba kwenye nchi yao, na kwa kuwa tumecheza na hatima yetu katika maeneo nyeti tumebaki watazamaji pale raia wa nje wanapokuja kuchukua fursa za kazi, biashara na uwekezaji.
Kama ilivyo katika uwekezaji, uraia wa nchi pacha hauna hakika kama utamnufaisha Mtanzania aliyepo Tanzania au yule aliye ughaibuni. Hata kama wenzetu wamefaidika nao, mazingira ya Tanzania ni tofauti na wenzetu, na hata sababu za Watanzania kuondoka na kuishia ughaibuni hazishabihiani kihivyo na wengine.
Hivyo basi utafiti ni muhimu kufanyanyika kabla ya maamuzi. Bila utafiti haiyumkini uamuzi huu ukawa na athari za muda mrefu; hata kama utawafaidisha Watanzania wasiozidi milioni tatu wanaoishi nje, ukawa janga kwa Watanzania zaidi ya milioni 42 wanaoishi Tanzania, na kwa hakika fursa chache zilizopo na zilizotengwa kwa ajili ya Watanzania zikapotea hasa kwa kuwa kuna kila dalili kuwa ¡¯wawekezaji¡¯ walio nyumbani ndio watakaochangamkia zaidi ¡¯fursa¡¯ hii.
Haishangazi basi, suala hili la uraia pacha linachagizwa na serikali za nje kama Canada na Oman (ndizo zilizotajwa) na kuingizwa kwenye ajenda kama mahitaji muhimu ya Watanzania wanaoishi nje. Swali la kujiuliza hapa kwa nini Canada na Oman ndizo vipaumbele na si Afrika Kusini, au Ulaya?
Sipendi kuhisi, lakini isije ikawa huu ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu kuwarudisha wale waliokimbia Azimio la Arusha na Mapinduzi ya Zanzibar kwa mlango wa nyuma, hasa kwa kuwa mpango huu unawezeshwa na serikali hizo (rejea Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje Uk. 43-44)
Mheshimiwa Spika,
...katika mwaka huuwa fedha, Wizara yangu imechukua jitihada zamakusudi za kupanua wigo kwa kuwafikia Diaspora waishio Canada na Oman. Mikutano na Watanzania hao iliandaliwa sanjari na ziara za Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika nchi hizo mwezi Oktoba 2012. Nchi hizi mbili, kwanza zina Watanzania wengi walio jizatiti kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Lakini pili, Serikali za nchi hizo zinaunga mkono jitahada zetu na zipo tayari si tu kuwawezesha ila kushirikiana na Diaspora hao kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Kama ilivyo gesi na madini, suala la sera lilikuwa ni muhimu sana katika mjadala na kwa kiasi kikubwa watu walijiuliza; ¡±hii kasi yote ni ya nini?¡±
Kama ilivyo muhimu kuwa na sera ya madini kabla kuuzwa kwa vitalu, vivyo hivyo kuna umuhimu wa kuwa na sera ya ¡±Watanzania wanaoishi nje¡± kabla hatujaruhusu kinachoitwa ¡±uraia-pacha¡±. Ni muhimu sana kuwa na sera ambayo Watanzania wanaoishi nje na wadau wa nyumbani wakashiriki kuitengeneza. Mchakato wa kuitengeneza sera hii haiyumkini utatoa nafasi kwa serikali kuwafahamu hao ¡±diaspora¡± ni kina nani, wanafanya nini, wako wapi, na maeneo gani ya kimkakati tunahitaji kushirikiana nao katika kuiendeleza nchi yetu.
Matokeo ya kitaalamu na kitafiti yanaweza kutoa mwelekeo mzuri katika kuangalia njia bora zaidi ambayo serikali inaweza kuitumia kuwaleta karibu Watanzania (pengine bila hata ya kulazimika kuwa na uraia-pacha).
Ifahamike kuwa ni nchi chache sana ambazo zinatoa uraia-pacha usio na masharti tena kwa sababu za kimkakati. Nchi nyingi zinatumia njia mbalimbali na tofauti kuwafanya wananchi kuwa sehemu ya nchi wanazotoka na kuwafanya wawajibike katika kushiri katika juhudi za maendeleo.
Mexico wana mpango unaitwa ¡¯Tres Por Uno (3x1)¡¯ ambao unamuwezesha kila diaspora anayetuma pesa moja nyumbani kuwekeza, serikali inamuongea 3; mpango huu ni bora na nafuu zaidi kuvutia uwekezaji kuliko ule wa kusamehe kodi ¡¯wawekezaji¡¯; njia nyingine ya kuvutia diaspora ni pamoja na kutambuliwa na kuchukuliwa kama raia ikiwemo kupewa hadhi maalumu ya ukazi ambao hauna masharti kwa mwananchi yeyote anayeamua kurudi kufanya kazi au kuwekeza (Ethiopia wana utarativu wa yellow card)
Pamoja na hayo, serikali inaweza kutathmini changamoto wanazokumbana nazo Watanzania nje na kuangalia ni jinsi gani na kwa kiasi gani serikali inaweza kubeba baadhi ya changamoto ambazo zipo nje ya uwezo wa diaspora wenyewe, kurahisisha maisha yao na kushiriki kwa karibu katika ujenzi wa Taifa, changamoto hizi ni kama gharama ya usafirishaji pesa nyumbani (ambazo ni kubwa ukilinganisha na nchi nyingine za jumuiya ya Afrika Mashariki), haki za Watanzania wanaoishi nje, na hata kubadilishana kodi na nchi nyingine (kama nchi zinavyobadilishana wafungwa).
Ingawa tumebinafsisha vingi, bado hatujachelewa, kuna vingine hatupaswi kuvibinafsisha, uraia ni suala mojawapo.
===

Uraia wa nchi mbili shinikizo la mafisadi?


Makala yangu juu ya uraia wan chi mbili utaua uzalendo, katika gazeti hili toleo namba 209 la Oktoba 26 hadi Novemba mosi, 2011, imezua mjadala mkubwa. Nimepokea hoja mbalimbali kwa njia ya simu, nyingi za kuunga mkono na chache za vitisho kutoka kwa wapigaji wasiojitambulisha, nami nimeona vyema kuziweka wazi hisia hizo ili viongozi wetu wapate kuelewa mtizamo wa baadhi ya wananchi wanaowaongoza.
Kwa kuwa ajenda hii inaonekana kugusa na kuzua hisia kali za sehemu kubwa ya jamii ya Kitanzania, hasa kutokana na kauli nyingi za Waziri wetu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na kauli ya Rais, Jakaya Kikwete; aliyoitoa kwa Watanzania raia wa Marekani wakati wa ziara yake nchini humo hivi karibuni na kuwapa matumaini kwamba suala hilo linashughulikiwa kikamilifu.
Kwa jinsi ninavyoiona ajenda hii, inaweza kutugawa Watanzania. Ni ajenda nzito na nyeti iliyowahi kutolewa kwa miaka 50 ya Uhuru wetu, ukiondoa ile ya mwaka 1962 juu ya ¡°uraia¡±, iliyomgharimu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, nafasi yake ya Uwaziri Mkuu, kwa kujiuzulu na kurejea kijijini.
Hapa, nitatoa baadhi tu ya hoja nilizopokea kutoka kwa wasomaji kuhusu makala hiyo, kuonyesha jinsi jamii inavyoliona suala hili la uraia pacha kwa mtizamo na hisia hasi.
Awali ya yote, naomba ifahamike kuwa, si kwa Tanzania pekee kwamba hoja ya uraia pacha inatia hofu na kero. Utafiti uliofanywa unaonesha kuwa, kati ya nchi 53 huru za Afrika, ni nchi 11 tu zimeonyesha kutaka uraia huo; 42 zilizosalia zimesema HAPANA!
Kati ya nchi 173 zinazounda dunia hii, ni nchi 17 (asilimia 9.8) tu zilizoridhia uraia pacha kwa sababu zinazofahamika. Nchi hizo ni pamoja na Australia, iliyoanzishwa na wafungwa huru (ex-convicts) wa Kingereza miaka mingi iliyopita; Canada na New Zealand, ambazo hadi sasa zimo kwenye himaya ya Malkia wa Uingereza; Costa Rica na Columbia.
Nyingine ni Cyprus, ufaransa, Ireland, Israeli, Italia, Jamaica na Jordan. Zipo pia Ureno, Urusi, Syria, Uingereza na Marekani yenyewe, nchi yenye utamaduni wa vurugu na ambayo raia wake hawajui uzalendo, hawajui watokako wala waendako.
Kwa Marekani na Mmarekani, utamaduni wa fujo na ghasia ndio mtaji wake mkuu katika maisha; hana uzalendo, hana utamaduni wala maadili ya kuigwa. Kwa sababu hii Amerika ni Taifa kubwa lisilo na roho, wala uhai wa kibinadamu.
Na kwa kuwa Taifa lolote lisilo na utamaduni ni sawa na mti usio na mizizi, vivyo hivyo, Marekani isiyo na utamaduni wa kizalendo, iko hatarini kuanguka kwa kishindo, kama ilivyoanguka himaya ya Rumi ya kale, kwa kuingiza mamluki katika mkondo wa kijamii na kuuwa uzalendo.
Tuangalie wasemavyo wasomaji wetu juu ya umamluki huu. Mmoja anasema: ¡°Makala yako katikaRaia Mwemani ya kweli na nzuri. Hebu muombe huyo Waziri (Bernard) Membe atupe orodha ya hao wanaotaka kuwa ¡°ndumilakuwili¡± na maeneo wanayotaka kuwezesha kwa kiwango cha uwekezaji. Kwani ¡°terms¡± (masharti) za TIC (kituo cha uwekezaji) haziwatoshi?¡±
Wa pili naye anasema: ¡°Fanya utafiti: Idara ya ¡°diaspora¡± (ughaibuni) pale ¡°Foreign¡± (mambo ya nje) wanadai wana ¡°database¡± (takwimu muhimu) ya Watanzania ¡°waliopoteza¡± uraia wao kwa kulazimika kuukana Utanzania ili wafanye kazi NASA (Idara ya mambo ya Anga) au BOEING (Shirika la ndege la BOEING) ¡°or wherever¡± (au mahali popote pengine). Hawa ni wachache sana, na kwa kweli wana ¡°secret information¡± (wana taarifa za siri) juu ya BOEING¡±.
Akaendelea kuhoji: ¡°Kwa nini sisi ¡°secret information¡± yetu tuiachie? Lakini ¡°majority¡± (wengi wao) ni wazamiaji na wabwia unga au ¡°refugees¡± (wakimbizi) toka Pemba. Kuna wengine ¡®University graduates¡¯ (wahitimu wa Chuo Kikuu) au ¡°Lawyers¡± (Wanasheria); hawa, walitafuta ¡°green pastures¡± (kazi mpya zenye maslahi) tu, hawakulazimika kuukana uraia wetu. ¡°You cannot eat your cake and have it(huwezi kukila kitumbua chako na kudai kubakia nacho)¡±, kwa maana ya kuwa hawa wamejimaliza.
Mwingine anabaini kuwa; ¡°Kudai uraia wa nchi mbili, kwanza, tunakaribisha Wazalendo wanafiki waje kuvuna na kuhamia huko kwenye makao yao mengine waliyohamia tangu zamani. Pili, kwa raia wa kawaida mwenye kipato cha chini ya dola moja, si rahisi akanufaika na sheria hii. Tatu, ni rahisi viongozi wetu kuongoza kisha wakaiba, wakaua au hata kutukana kisha wakakimbilia nchi zao zingine; uraia wa nchi mbili ni kukaribisha uhaini, haukubaliki¡±.
Lakini Msomaji mmoja kutoka Mwanza, yeye aliona kuwa, hawa waliokimbilia ughaibuni ni Wazalendo zaidi kuliko Viongozi wanaojiita Wazalendo lakini wanakimbilia huko huko ughaibuni kupata tiba; yeye anahoji kwa ukali kidogo, anasema:
¡°Unazungumzia uzalendo upi? Kama Nyerere alifia Uingereza ni uzalendo na watawala kwenda India na Uswizi kutibiwa ni uzalendo, basi, kwa wale Watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili ni uzalendo (zaidi)¡±.
Msomaji mwingine anauliza: ¡°uraia wa nchi mbili wa nini? Hii si hoja ya Watanzania waishio ughaibuni, bali ni shinikizo la Wahindi na wanasiasa ambao wanataka iwawie rahisi kuiba, kuficha mali na kukimbilia nchi ya pili. Haufai!, Haufai kabisa!¡±.
Msomaji mwingine kutoka Singida anasema Makala hii imewafumbua macho Watanzania na kuwapa ujasiri wa kusimama kidete kupinga njama na hujuma zote za wasomi waliojiunga na kambi ya ubeberu wa kimataifa kuangamiza Taifa letu na watu wake; kisha anaonya na kuuliza: ¡°Aksante sana kwa kuliona tatizo hili la uraia wa nchi mbili. Tanzania inanyemelewa na ukoloni mpya, tuweni macho; vizazi vijavyo vitakuta nini?¡±
Vivyo hivyo, yupo mwingine aliyehoji akisema: ¡°Injili ya uraia pacha kwa faida ya nani? INJILI TAKAFUJO YA MEMBE IMESHINDWA KABLA HAIJAANZA. Mungu akubariki; makala hii iibue mjadala¡±.
Bila shaka mjadala umeibuliwa. Watanzania tulijadili kwa umakini na kwa kina, kwa manufaa ya nchi yetu!
===


Uraia wa nchi mbili utaangamiza nchi, uzalendo


MNAOJALI kusoma historia na kazi za uandishi za watu wenye uchungu na nchi yao, msikieni Shaaban Robert katika shairi lake, ¡°Fahari ya mtu¡±, akisema:
¡°Fahari ya kila mtu, kwanza ni taifa lake,
Kutimiza wake utu, afe au aokoe,
Pasipo hofu ya kitu, halipendi liondoke
Fahari ya kila mtu, ya pili nchi yake,
Mtu hakubali katu, kutawaliwa pake,
Hilo haliwi kantu, halina heshima kwake.
Fahari ya kila mtu, ya tatu ni nchi yake,
Kuwaye chini ya watu, wageni wa nchi yake,
Ni jambo gumu kwa mtu, japo vipi aridhikie,
Pasipo hofu ya kitu, hulipenda liondoke¡±.
Ni jambo la kuhuzunisha na kugadhabisha pia, kuona zama hizi, baadhi ya Watanzania wenzetu, hasa wanasiasa, wametekwa nyara na ubepari na mitaji ya kimataifa kiasi cha kupoteza uzalendo na moyo wa kuona fahari kwa taifa lao na kuabudu vya nje.
Na kwa kuwa Watanzania walio wengi hawana kiwewe na vya nje, wala fikra kwamba siku moja watafika au kuishi Ughaibuni; wananchi sasa wanaanza kuona ufa uliopo unavyozidi kupanuka kati yao na viongozi wao wenye kuabudu vya nje, badala ya kushikamana na wanaowaongoza kwa matatizo, mafanikio na kwa kila kilicho cha nchi hii.
Wananchi wanaanza kutambua kwamba, wao na viongozi wao hawaabudu kwenye madhabahu moja, wala hawachangii sala. Wakati sala ya wananchi kwa mama Tanzania ni kuona maendeleo ya nchi yao waliyoitolea jasho wakati wa kupigania uhuru na ustawi wa jamii, sala ya viongozi wao ni tofauti, inasema hivi:
¡°Baba yetu uliyeko Ulaya na Amerika,
Jina lako litukuzwe, ufalme wako uje,
Utakalo lifanyike katika Tanzania yetu tajiri kama huko uliko,
Mapenzi yetu ya kukukaribisha nchini yatimie,
Kama tulivyokukaribisha wakati wa ukoloni,
Tupatie riziki yetu ya kila siku,Mapesa ya dola,
kwa kuwa vishilingi vyetu si thamani tena.
Tusamehe kwa mapungufu na udhaifu wetu kiuchumi na kisiasa.
Tusaidie kuwanyuka, kuwashinda wote wanaokusakama
Kwa kupora utajiri wa nchi yetu, eti huo ni ukoloni maboleo.
Tusaidie kuwanyuka ipasavyo wanahabari wa nchi yetu,
Kwa makeke na kidomo domo chao.
Fadhili kutungwa Sheria ya kuwabana, wakome.
Tupe nguvu, utukufu na misaada tele;
Utujalie moyo wa kukupenda wewe tegemeo letu,
Tufanye wanyeyekevu na wenye shukrani;
Milele na milele, Amina.
Watanzania wengi wamestushwa na kugadhabishwa na taarifa ya Serikali kwamba inakusudia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria kuruhusu uraia wa nchi mbili(dual citizenship). Akijibu swali la Mbunge Mwadini Abbas Jecha wa Wete, wakati wa kikao cha 12 cha Bunge, mjini Dodoma, hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Khamis Kagasheki, alisema, anawahurumia ¡°Watanzania wengi walioko nje waliopoteza uraia wao kwa kutokuwapo sheria hii¡±, hivyo lazima wasaidiwe.
Watetezi wa muswada huu wanadai kuwa, Sheria hiyo itawasaidia mabilionea wa Kitanzania waliochukua uraia wa kigeni kurejea nchini na ¡°vijisenti¡± vyao na kutoa msisimko kwa uchumi wa nchi; na pia kwamba raia wa kigeni wenye mitaji wataweza kuchukua uraia hapa nchini bila kutakiwa kufuta uraia wa nchi zao, wakiishi nchini, bila wasi wasi kuliko ilivyo sasa.
Kuna maswali mengi yanayotaka majibu juu ya muswada huu: Uraia wa nchi mbili utamsaidiaje Mtanzania wa kawaida kwa kugawana uraia na wageni? Kwa nini muswada huu unaletwa leo na si miaka iliyopita?
Tanzania imebarikiwa kwa utajiri mkubwa wa maliasili za aina mbali mbali; imefungua milango kwa wawekezaji hadi upana wote wa bawaba. Je muswada huu si kuruhusu ¡°Wageni kupigana vikumbo¡±(scramble)kugombea rasilimali za Tanzania, kama enzi za kina Karl Peters, Cecil Rhodes na wengine, mwanzoni mwa ukoloni barani Afrika? Nini hatima ya yote haya?
Tunaambiwa, dunia sasa ni kama kijiji ambapo watu wanaweza kuwekeza na kufanyakazi popote. Je, kwa muswada huu si kujikanganya na dhana hiyo ya ¡°utandawazi¡± ambayo tayari tumeipokea kwa pupa bila kuelewa madhara yake? Wanaotetea utandawazi na kututaka turuhusu uraia wa nchi mbili kwa manufaa ya wenye mitaji, wanaitakia nini nchi yetu na uzalendo uliosimikwa na waasisi wa Taifa hili?
Haya ni maswali magumu yanayotaka ukomavu wa kisiasa kuyatolea majibu sahihi kuweza kuwaridhisha wazalendo wa nchi hii. Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha na Naibu wake Kagasheki, wanaweza wasilijue hili, na hivyo kuonekana wepesi wa kusali bila kuhoji, ¡°Baba yetu uliyeko Ulaya na Amerika¡-..¡±, lakini wasubiri hisia za wananchi wazalendo, pale watakapowasilisha muswada huo tata bungeni. Kusema kweli wanajitengenezea baruti.
Tunaamini muswada huo haukubuniwa na wazalendo wenye kutetea na kujivunia fahari ya taifa na kwa maslahi ya walio wengi, bali chimbuko lake ni watu wenye matanuzi, wenye kuchumia kivulini na kulia kivulini, wakiwamo wazalendo mamluki wasioweka mbele maslahi ya taifa, wakishirikiana na kina Karl Peters wa zama hizi, kila mmoja akiwania kwa staili yake kujinufaisha na maliasili za nchi hii.
Ni matokeo ya fungate ya ¡°uwili mtakatifu¡± kati ya ubeperi wa kimatifa kwa kufunga ndoa na siasa za nchi hii na kwa viongozi kutumika kama mkondo(conduit)wa kuingiza ukoloni mpya (na kwa historia kujirudia) kwa kujali zaidi maendeleo ya miradi kuliko maendeleo ya watu. Huu ni uhaini ulio dhahiri.
Sheria hii itawawezesha wageni kupata haki zote za kiraia sawa na Wazalendo; lakini wao (wageni) kwa shabaha ya kuifanya nchi kuwa kituo cha ¡°kuwekeza¡± na kupora uchumi wa nchi, wakirandaranda kati ya nchi na nchi wasiweze kukamatika kwa urahisi iwapo watahusishwa na hujuma nchini.
Wako wapi akina Jeetu Patel (kashfa ya EPA), Saileth Vithlani (kashfa ya rada), Chavda na wengine, ambao tuliwakubali kama raia wenzetu, na mwisho wa yote wakatupora wasikamatike? Tuambieni, ni raia gani wa aina hiyo ameonyesha fahari kwa taifa, na aliye tayari kuitetea nchi kwa lolote, kama hawa si mbwa mwitu ndani ya ngozi ya kondoo? Tuambieni, nani kati yao, au watoto wao ameshiriki kujenga nchi kama afisa kilimo, polisi au mwanajeshi?
Baadhi ya wazalendo wachache wanaotetea muswada huu ni wale waliowatelekeza Watanzania, wakakimbilia nje na kuwaacha wakipambana na ujenzi wa nchi yao wanayoipenda; au ni wale waliojiunga na ufisadi wa kimataifa na kutumika kama mawakala wa ufisadi nchini.
Hawa hawana Watanzania na nchi moyoni mwao. Wanaona bora sheria hii ipite, ili wanachopora na watakachopora kwa kushirikiana na wageni (ambao nao sasa watapewa uraia) waweze kuwekeza nje na kukimbilia huko mambo yanapowaharibikia. Ni uasi, uzandiki na umamluki ulioje kwa Mtanzania wa aina hii. Wasaliti hawa.
Hivi Watanzania tumelogwa? Kwamba wakati hatujatatua ¡°mgogoro¡± wa kuwapo kwa ¡°Wazanzibari na Watanzania, au Wazanzibari na Wazanzibara, tunajibebesha hima mzigo mwingine mkubwa zaidi wa ¡°uraia wa nchi mbili¡±!
Fahari ya mzalendo wa kweli ni taifa lake, na ambalo kwake anapaswa kutimiza wajibu wake; yupo tayari kulitetea na kulifia. Tuambieni, mtu mwenye uraia wa nchi mbili ataimbaje ¡°Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote?¡±, wakati moyo wake umegawanyika kwa ¡°mapenzi¡± ya nchi mbili? Atawezaje kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja?
Tunasema wanaotetea muswada huu hawana lengo la kutumikia taifa na watu wake, bali agenda yao ni kupora utajiri na maliasili za taifa hili.
Na kwa kuwa sheria hii itawapa wageni haki sawa za kiraia na wazalendo, tusishangae siku moja nchi hii ikatawaliwa na Rais ¡°Mtanzania¡± kutoka Japan, Waziri Mkuu ¡°Mtanzania¡± kutoka China, au Spika wa Bunge ¡°Mtanzania¡± kutoka Iran, Irak au Canada. Utawazuiaje kutawala wakati nao watakuwa ni Watanzania bila kutuhumiwa kuvunja Katiba ya nchi kwa ubaguzi wa rangi na wa asili ya mtu? (Angalia ibara 13(2) na (5) ya Katiba , 1977).
Kwa wanaosoma historia ya nchi hii, watakubali kwamba suala la uraia ni jambo nyeti tangu enzi za uhuru na ambalo lilitaka kumgharimu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nafasi ya urais wa nchi hii, mwaka 1962. Mwaka 1961 Serikali, chini ya Waziri Mkuu Nyerere, iliwasilisha muswada wa uraia kwa watu wote bila kubagua rangi au asili ya mtu, mradi tu awe amezaliwa au mmoja wa wazazi wake awe amezaliwa Tanganyika.
Muswada huo ulipita kwa upinzani mkali wa wabunge na wananchi, waliotaka uraia uwe kwa Waafrika tu ambao ndio wenye nchi na wenye kustahili kufaidi matunda ya uhuru.
Kwa kukerwa na sheria hiyo, chama tawala cha ¡°Tanganyika African National Union¡± (TANU) kiliitisha Mkutano Mkuu, Januari 16, 1962 ambapo wajumbe walimshambulia na kumlaumu Nyerere, wakishinikiza kuona maendeleo ya haraka, kuanzishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika, kufutwa kwa viti 20 maalumu kwa weupe Bungeni(minority races)wenye uraia wa nchi mbili, na kutoa madaraka kwa Waafrika katika utumishi wa umma na vyama vya Ushirika.
Wakati mkutano huo ukiitishwa, tayari TANU ilikuwa imeanza kugawanyika na wanachama wengine kuunda Chama cha ¡°The Nationalist Enterprises Party¡± (NEP).
Kwa kutetea msimamo wake, na hasa kutokana na kile kilichoitwa ¡°kukosa ujasiri wa kuwatimua Waingereza kwa kasi iliyotakikana¡±, ilibidi Mwalimu aachie ngazi na kuwaachia Rashid Kawawa na Oscar Kambona kuwaondoa Wazungu kwenye vyeo walivyokuwa wakishikilia.
Uraia wa nchi mbili ni chukizo linalolenga kuigeuza Tanzania kuwa ¡°Shamba la Bibi¡±; ni hatari pia kwa uchumi wa nchi, uzalendo; na umoja wa kitaifa. Ni sheria ya kudhalilisha wazalendo na uzalendo. Mwenye masikio na asikie, Watanzania wanaisubiri siku ya muswada huo.
===


Chanzo: Raia Mwema
 
Sioni sababu ya kuipiga danadana hoja hii. Iko wazi na faida zake ziko wazi kabisa. tatizo la viongozi wetu wanataka cha juu toka huko mlioko Diaspora si wanajua mnazo? Wanataka muwabembeleeeeeze.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom