Upotevu wa maji ni janga, lidhibitiwe

Feb 13, 2017
5
8
Mvujo wa maji 1.jpg

Gharama ya upotevu wa maji (Non-Revenue Water- NRW) kwa mwezi mmoja jijini Mbeya inatosha kujenga mradi wa maji wa kijiji nchini.

Mathalani, Mradi wa Maji wa Mwashaali unatumia shilingi milioni 400 na utanufaisha wakazi 6,000 wa maeneo ya Isyesye Mlimani na Block D jijini humo.

Gharama za mradi huo ni ndogo ukilinganisha na kiwango cha hasara inayosababishwa na upotevu wa maji ndani ya mwezi mmoja tu katika jiji hilo ambayo ni shilingi milioni 465.

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini humo (MBEYAUWSA), Barnabas Konga anaeleza kuwa mwenendo huo wa hasara ni sawa na shilingi bilioni 5.6 kwa mwaka ikiwa ni kutokana na upotevu wa maji wa asilimia 28.

Kiwango hicho cha fedha zinazopotea kutokana na upotevu wa maji, kilitosha kugharamia mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika Kata za Mwansekwa na Iganzo, utakaonufaisha wakazi 42,000 katika maeneo ya Mwansekwa, Iganzo, Ilemi, Ikoloti, Igodima na Ilolo jijini humo.

Mradi huo unagharimu shilingi bilioni 5.2, hivyo inakuwepo ziada ya shilingi milioni 400 ambazo zinatosha pia kujengea mradi mwingine wa maji katika kijiji.

Hasara hii inayotokana na upotevu wa maji katika Jiji la Mbeya inatoa picha halisi ya namna tatizo hilo lilivyo kubwa na kuathiri uchumi wa taifa, kwani Mbeya ni eneo moja dogo tu, vipi kwa Jiji la Dar es Salaam na nchi nzima, hali ikoje.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, MBEYAUWSA inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitatu (2022-2025) unaolenga kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kutoka asilimia 28 hadi chini ya asilimia 20 kwa kuchukua hatua kadhaa.

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa kukabili hali hiyo ni pamoja na kubadili mabomba chakavu, kufunga "Bulky meters" ili kujua kiasi cha maji yanayozalishwa na kubadili dira chakavu za wateja.

“Dira zikikaa muda mrefu zinapoteza readings, unajua huduma ya maji ilianza tangu miaka ya 50 na 60, kuna baadhi ya wateja bado wanatumia hizo dira, sasa kuna kipindi zinaenda zinakwama, unakuta dira haisomi lakini maji yanatoka,” anasema Mhandisi Konga.

Hatua zingine ni kufanya tathmini yay a wataje na miundombinu (customer and infrastructures survey) na kufunga ball valves kwenye matenki.

Pamoja na hatua hizo Mamlaka hiyo pia inawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaobainika kujihusisha na wizi wa maji, na zaidi ni kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi bora ya maji.

“Sisi mabomba yakikatwa tu, ujue tayari hapo ipo shughuli, ipo “Non-Revenue Water,” kwa hiyo tunahangaika kuishusha tufikie ile elekezi, chini ya asilimia 20,” anasema Konga.

Wasimamizi wa huduma ya wanateswa na tatizo la upotevu wa maji, vipi kwa upande wa wateja, hivi nao wanaliona na kuteseka wakizingatia kuwa zinazopotea ni fedha zao wenyewe.

Ni muda muafaka sasa tukatafakari wote kwa pamoja na kuamua kulikabili tatizo hili ili kiwango cha upotevu kishuke hadi chini kabisa ya asilimia 20.
 
Back
Top Bottom