Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,812
- 11,988
JamiiForums imefanya mahojiano na Rose Senyagwa, Mtaalam na Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ambapo alieleza kwa kirefu nini watu wanatakiwa kufanya ili kujilinda pale kunapokuwa na radi
====
Radi ni nini?
Radi ni umeme, umeme huu unatoka katika mawingu na hasa katika wingu linaloitwa wingu anga, wingu linalorefuka kwenda juu kwa mfano wa kichuguu, na kwa kawaida linakuwa na barafu ndani yake. Sasa pale ambapo wingu na wingu likigongana, zile barafu zinagongana na kutoa umeme. Mvua za barafu hutokea mawingu haya yanapokuwa mazito na kushuka chini kama mvua ambayo ndio inajulikana kama mvua ya mawe.
Umeme huo wa radi unapotokea unaweza kwenda sehemu yoyote, inaweza kutoka kwenye wingu kwenda juu, kwenda kwenye wingu jingine, au kutoka kwenye wingu na kuja ardhini. Inapokuja ardhini ndio inasababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine pamoja na vitu vingine ardhini, lakini ikichukua uelekeo mwingine inakuwa haina madhara kwa binadamu.
Kama radi inapiga unatakiwa kuepuka mambo gani?
Kama radi inapiga si salama kujificha/kujikinga chini ya miti mirefu kwasababu kwa kawaida radi ikipiga chaji ya umeme inapotoka kwenye wingu inaenda uelekeo wowote (yaani haichagui) kitu cha kwanza kirefu kuliko vyote katika eneo hilo itakachokutana nayo itapiga hapo.
Lakini pia miti miti ina uwezo wa kusafirisha umeme. Lakini pia minara au kitu chochote kirefu sio salama kujikinga chini yake radi inapopiga, hii inajumuisha pia nguzo za umeme, hata transfoma
Pia kunapokuwa na radi haishauriwi kutembea katika maji yanayotiririka au yaliyotuama. Mfano madimbwi au maji yanayotembea barabarani, sehemu zenye maji kama mtoni, ziwani au kwenye mabwawa, hii ni sababu radi inaweza ikawa imepiga kwenye eneo fulani ardhini au chanzo cha maji, ule umeme wa radi utasafiri kufuata uelekeo wa maji. Kwahiyo mtu unapokuw aunatembea barabarani maji yanatiririka haushairiwi kukanyaga maji hayo sababu huwezi kujua kama maji hayo yana umeme.
Mbali na hilo haishauriwi kutumia vifaa vya umeme au vinavyokamata mionzi mfano simu/Kompyuta au laptop, TV, redio, friji nk sababu vinaingiliana na radi kupitia mionzi, ambapo inaweza kusafirisha mionzi na radi na hivyo kusababisha kupigwa na shoti.
Nyumba na majengo mengine yana mfumo wa kulinda radi?
Majengo huwa yanawekewa mfumo ya kuzuia radi kupiga kwenye majengo (Erthing) ambapo radi ikipiga mfumo huo hufanya chaji ya umeme kupelekwa uelekeo wa ardhini badala ya kupiga kwenye jengo, hivyo ni vizuri kwa nyumba pamoja na majengo mengine kuwekewa mfumo huo
Mvua inayoambatana na radi inaponyesha ni vizuri uwe salama, kaa nyumbani tulia kama hakuna ulazima sababu radi inaweza kupiga sehemu yoyote na kama utakuwa kwenye maeneo hayo hatarishi ni rahisi kupigwa na radi sababu ni mazingira yanayokaribisha radi.
Nguo nyekundu zina uhusian gani na radi?
Nguo nyekundu au nguo yenye rangi yoyote haina uhusiano wowote na radi, ni imaji iliyojengeka kwa watu. Mtaalamu anasema hata yeye aliwahi kuambiwa hivyo akiwa mtoto na walikuwa na tabia ya kuwakimbia watu wanaokuwa wamevaa nguo nyekundu wakati radi inapiga lakini kitaalamu hakuna uhusiano wowote kati ya nguo nyekundu au rangi yoyote na radi.
Je, kuzima data kwenye simu inasaidia kukuepusha kupigwa na radi kupitia kifaa hicho?
Kuzima data inaondoa tu mtandao kwenye simu lakini simu za kawaida zinaweza kuingia, hii inamaanisha mionzi bado inasafiri, hivyo bado unaweza kupigwa na radi ikiwa umezima data kwenye simu yako. Ni vizuri kuizima kabisa au usipokee simu wakati radi inapiga.
Radi zinavyopiga juu wakati ndege pia zinapita na tunajua ndege zinatumia umeme, kwanini huwa haziathiriki/haziguswi?
Radi ni hatari sana kwa usalama wa anga upande wa ndege, kwasababu ndege ikipita kwenye wingu lenye radi na ikatokea ndege inapita halafu radi ikapiga kuna uwezekano mkubwa wa ndege kulipuka.
Kinachofanyika ni kuwa; wingu la radi sio wakati wote litasambaa eneo lote la anga, kunaweza kukawa na mawingu upande mmoja tu wa anga, Rubanikabla hajaanza ruti yake au anapokuwa kwenye ruti yake kuna vifaa lakini pia anapata taarifa za hali ya hewa za kujua hili wingu lipo wapi, hivyo huwa wanalikwepa wingu hilo ili kuepusha madhara.
Kabla hajaruka anapewa tarifa ya hali ya hewa kujua hili wingu lipo uelekeo gani, kwahiyo yeye anapanga mipango kulikwepa wingu hilo, ndio wakati mwingine ruti inakuwa ndefu kidogo sababu analizunguka lile wingu, sababu haifai kukatiza katika wingu hilo.