Umuhumu wa maandalizi kabla ya kutengenza Website

Kilongwe

JF-Expert Member
Feb 7, 2008
423
115
Kuna usemi wa kiswahili unaosema, "mali bila daftari, hupotea bila habari". Maana ya msemo huu sio kwamba kwenye daftari ndio utahifadhi mali zako, la hasha, bali kwa kuwa na mipango na kumbukumbu za matumizi ya mali zako kwa maandishi, basi utaweza kufuatilia mwenendo wake. Hili ni sawa na kwenye Website, kuwa na website bila kuwa na maandalizi ni sawa na kujenga nyumba bila msingi, ndio maana siku ya mwisho utaona Website ni mzigo usio na maana.

Kuna wakati niliwahi kufanya kazi na mmoja wa wanablog maarufu Tanzania ambaye hadi leo hii amekuwa akiogopa mabadiliko baada ya kufeli kwenye badiliko moja alilotaka kufanya kwenye blog yake.Baada ya kukutana na mimi aliniambia, Nyoni, nimewahi kujaribu, ila tulifeli vibaya, nikamuambia, mulifeli kwakuwa mulikuwa munajaribu na sio muliamua. Kwani kama mungeamua, basi mungekuwa na maandalizi na mipango ya awali kabla ya kuanza maboresho ya blog yako, hivyo mulifeli kupanga, ndio maana mukaja kufeli kutekeleza.



mpango-kazi-na%20-direction.jpg



Kuwa na mipango kabla ya utekelezaji husaidia kukupamuelekeo na kujua nini kinahitajika, hii sio tu itasaidia kuokoa muda bali pia kujua wapi mulikosea au kunaenda sivyo. Hii ni kwa wamiliki wa website, watengenezaji na hata wanaomiliki biashara ambao wanafikiria kuwa na website. Jiandae kabla ya kuwa na website, kama utakutana na kampuni inayojishughulisha na utengenezaji wa Website na wanajua wanachokifanya, basi watakusaidia katika hatu ahii muhimu ya kupanga.

Hivyo, ni vitu gani muhimu unatakiwa kupanga au kujiandaa navyo kabla haujatengeneza Website?

1. Weka malengo na uelekeo wa Website yako.

Katika makala ya wiki iliyopita, nilizungumzia makosa wanayoyafanya wamiliki wa website, na kosa kubwa ni kutokuwa na malengo ya website zao. Hivyo, hatua ya kwanza kabisa kabla ya kutengeneza / kumiliki website yoyote ni kujua malengo ya website, je nini malengo ya website yako? au kwa lugha nyingine, kwanini unataka kuwa na website? Je kwakuwa kampuni A ambayo ni mshindani wako ana Website basi na wewe unataka kuwa na Website?.
Kama unataka mafanikio ya website yako, basi ni lazima uwe na malengo ya website yako, kaa chini na uandike nini unataka kukifanya kwenye website yako, kwa kushirikiana na watengenezaji wa website ambao wana ujuzi wa Tehama na Biashara, watakusaidia kutafsiri malengo yako katika lugha Tehama.
Epuka wale waliojikita kwenye tehama bila kuangalia upande wa pili ambao ni biashara. Baada ya kujua malengo, unatakiwa uwe na vigezo vyako, kwa mfano, ndani ya mwaka mmoja ninataka watu 1000 wawe wanaifahamu website yangu, watu 600 wawe wamejiunga na mlisho wa habari, ni kiasi gani cha mauzo yanatakiwa kutoka kupitia Website nk. kwa kutumia programu nyingi ambazo zipo online kama Google Analytics, utaweza kupima utendaji wa Website yako siku hadi siku hivyo kujua kama umefikia malengo, na kama haujafikia ni kwa nini haujafikian na ni jinsi gani utaweza kufikia malengo.

bajeti-ya-website.jpg


2 .Tenga bajeti kulingana na ubora wa kazi


Katika mambo ambayo tumekuwa tukipambana nayo ni wateja wengi kutokuwa na bajeti kwa ajili ya Website, kwa wao website ni kitu cha hiyari ambacho hakina bajeti yoyote. Hivyo, kama wewe ni mmiliki wa makini wa biashara, unatakiwa kuwa na bajeti kwa ajili ya website yako. Kwenye bajeti hii kuna mambo mengi kama utengenezaji wa website (website design), kuhost website, matangazo ya online na mengine mengi yanayofanana nayo. Fanya tafiti kabla ya kuamua hili, kuna watu wengi ambao wanaweza kukusaidia kwenye tafiti.

Dudumizi tumekuwa tukiwasaidia wateja wetu wengi juu ya bajeti na mambo muhimu kwa ajili ya ustawi wa website zao. Kumbuka, kwenye bajeti yako, usijifunge kwa kulalia kwenye bei za chini tuu, kwani kuna wakati ubora huathiriwa na bei, hivyo jiepushe na kulalia kwa sana, kama unaona huna bajeti inayokidhi mahitaji, ni bora ukaivunja bajeti na mahitaji kwenye vipindi, kwa mfano awamu ya kwanza nitatengeneza website, halafu baada ya miezi sita nitaihost kwenye server nzuri, mwakani nitaanza kuifanyia matangazo nk. Huu ni muendeo mzuri kuliko kuanza vyote kwa pamoja kwa bei ya chini na ukajikuta Website yako ipo offline muda wote.

Wateja Wengi tunaopokea kwa Dudumizi Hosting ni wale wanaokuja toka kwa makampuni mengine, kuna mteja alikuja amechanganyikiwa kwani aliwekwa ndani na bosi wake kwakuwa website ilikuwa off kila muda na bosi wake akadhani ni yeye mwenye matatizo.Kwanini, inawezekana yeye kama IT manager alishindwa kutoa bajeti nzuri kitu ilichopelekea kuihost website yake sehemu za vichochoroni.
Kumbuka, vya rahisi ndio ghali.

timu-ya-website-design-in-tanzania.jpg


3. Kuwa na timu itakayohudumia Website


Katika Wateja wetu wa Tanzania, zaidi ya 90% wao kazi ya website huishia baada ya kutengeneza, na wengi wao hawana timu inayojihusisha na uchungani wa Website. Na wengi wamekuwa wagumu kulipia gharama kidogo ili sisi tuwasaidie kuchunga website zao. Hivyo, siku ya mwisho wanajikuta wanashindwa kufikia malengo kwakuwa hawana timu na pia hawaoni umuhimu wa uwepo wake.

Hivyo, kama wewe ni mmiliki au unajiandaa kuwa na website, hakikisha unakuwa na timu ambayo itahusika katika uchungaji na uongozi wa Website yako, na kama unaona hauwezi, basi unaweza kuipeleka kazi hii kwa makampuni mengine (Outsource). Dudumizi tunatoa hii huduma kwenye Website Maintenance.
Kwenye timu yako, unatakiwa uwe na watu kama

- Wamiliki wa website / kampuni ambaye anajua malengo na sababu za kuwa na website na huyu atakuwa kiongozi mkuu,
- Wataalamu wa kutenegeza website, wajue lugha za kutengeneza Website kama PHP, HTML, CSS, Javascripts nk, pia wawe na uzoefu wa kutumia baadhi ya CMS maarufu kama Joomla, Wordpress, Drupal nk,
- Waandishi na wahariri,
- Watu wa sanaa za michoro kwa kompyuta (Graphics),
Hakikisha kila mmoja katika timu anajua wajibu na mipaka ya kazi yake.

4. Kuwa na mpango kazi wa utumaji taarifa

mpango-kazi-wa-website-design-in-tanzania.jpg


Baada ya kujua nini unataka, ukawa na timu nzuri, kinachofuatia ni kuwa na mpango kazi wa taarifa, yaani ni kitu gani kitatumwa na kwa nini.

Hili ni moja ya tatizo kubwa kwa website nyingi mno za Tanzania, wengi hawana mpango kazi wa taarifa,ndio maana leo hii unakuta, habari moja ipo kwenye blogu zote. Zile za michezo, zile za Urembo, zile za habari nk.
Wengi wa wamiliki wa Website hawajui umuhimu wa kuwa na mpango kazi wa taarifa, yaani kwao kila kitu ni twende kazi. Kwenye mpango kazi huu, unatakiwa kupangilia na kufafanua muundo, aina na mtindo wa utumaji wa taarifa zifuatavyo;

-Makala za blog
-Taarifa
-Video
-Picha
-Mipasho kwenda na kutoka kwenye mitandao ya jamii.
-Maoni
-Taarifa za watembeleaji unazokusanya

Kumbuka, kwenye mpango kazi huu, lazima kuwe na ratiba za utumaji, nani muhusika nk. Kwa wale wanaomiliki blog za makampuni, unaweza kuamua kutuma makala moja kila mwezi, au kila wiki. Huu ni mpango wa utumaji wa makala.

Pia, usisahau kukipa umuhimu mkubwa sana kipengele cha mwisho nacho ni taarifa za watembeleaji. Hakikisha unakuwa na sehemu ya kukusanya anuani za barua pepe na ikiwezekana na taarifa kadhaa kulingana na aina ya biashara yako. Kwa mfano, wewe ni mmiliki wa website ya urembo, basi ungependa kujua taarifa za jinsia na umri ili pale utakapoamua kuwasiliana na wateja wako, basi utatuma ujumbe unaowalenga.

website-design-muonekano.jpg


5. Panga muonekano wa Website yako.


Kuna mdau aliwahi kuandika na kulalamika juu ya mpangilio wa Blogs nyingi Tanzania, yaani unakuta ukifungua Website tuu, unakutana na matangazo kama kumi na tano, sasa chukulia yule anayetumia simu na intanet ya mafungu, yaani unakuta umekula bando lake lote hata kabla ya website haijafunguka. Pia kwa namna nyingine, hata wale wanaotangaza, kwa njia moja au nyingine hawafaidiki. Hii ni kwa sababu, wamiliki wengi hawakuwakupanga kabla ya kuwa na website. Website ilikuja kwa mapenzi ya manani.

Hivyo, iwe ni website ya kampuni, iwe ni blog au hata website yako binafsi, hakikisha unakuwa na mchoro wa muonekano wa website, hapa kiwe nini, pale kiwe nini nk. Kumbuka kutumia mfumo unaojulikana na kuzoewa na wengi, kwa mfano watu wote wanajua kitufe cha kutafuta (search button) huwa kulia juu, menu huanzia kushoto kuja kulia wakati wasiliana nasi ni ya mwisho kabisa. Kwa kufanya hivi utasaidia watu kutumia muda mfupi kuperuzi website yako (Usability).
6. Ijaribu Website

Baada ya kupanga, halafu ukatengenezewa website, hakikisha unaijaribu.Majaribio haya yawe ni ya kiutendaji na kimuonekano. Inamaana, inafanya kazi kama ilivyotakiwa na pia, inaonekana kama unavyotaka bila kuwa na makosa. Hakikisha Website yako inaonekana vyema kwenye vifaa vyote na sio kwenye kompyuta tuu bali kwenye vifaa vyote, kama kwenye simu, kompyuta za mpakato na hata kwenye Tv kubwa, mara nyingi kwenye Design za Dudumizi, jaribio la mwisho la muonekano ni kwenye LED Tv ya nchi 42, kwani kwa kuifanyia majaribio kwenye TV kubwa na kwenye simu ndogo, inamaanisha website itaonekana vyema kwenye kila kifaa.

Pia usisahau kuijaribu kwenye kila kifungulia website (browsers), kuanzia kwenye Internet Explorer, Chrome hadi kwenye Mozilla Forefox. Kwa kutumia analytics, utaweza kujua ni vifaa au vifungulia tovuti vipi watembeleaji hutumia kwa wingi, hivyo kuvipa kipaombele zaidi kwani kuna wakati inakuwa ngumu sana kukidhi sehemu zote, kwa mfano, website zetu tunazotengeneza sasa, huwa hatufikirii tena watumiaji wa Internet Explorer 7 kushuka chini, ila huonesha ujumbe kwa watumiaji pindi ikijitokeza anatumia browser hizo.

Watu wengi wamekuwa na kiherehere cha kuiweka website hewani hata kabla hawajaijaribu. Hii hupelekea kupoteza ule mvuto haswaa pale mtu anapokuja kwa kasi zote kuona website yako baada ya kusikia kwa rafiki yake, ila akifika hamu yote inamuisha, waswahili husema," Ng'ombe hanenepi siku ya mnada", hivyo, ijaribu na rekebisha makosa kabla ya kuirusha hewani na ubora uwe tangu siku ya kwanza.

website-maintenance-in-tanzania.jpg


7.Uchungaji na Uboreshaji wa Website yako.


Kwa wengi, mpango wa Website huisha pale siku ya mwisho website inapowekwa hewani.Website ni kitu endelevu, hivyo uchungaji na uboreshaji wa Website ni moja ya vitu muhimu mno kwa maisha ya biashara / kampuni.Fuatilia muenendo wa watembeleaji wa website kwa kutumia programu za takwimu, jua nini wanakipenda, wanakuja toka wapi na wanafanya nini wawapo kwenye website yako. Malengo haya lazima yawekwe kabla haujatengeneza website.

Pia, nilazima uwe unafanya maboresho pale yanapohitajika, sio kila siku hakuna jipya, uwe unafanya maboresho ya programu zilizotumika kutengenezea website nk. Pia Usisahau kupata mrejesho toka kwa wateja na watembeleaji wa website. Mrejesho ni roho ya bishara / website yako kwani website ipo kwa ajili ya wateja, hivyo kujua maoni yao ni muhimu kwa uwepo wako.

Leo tumeangalia mambo muhimu ambayo wewe kama mmiliki wa Website unatakiwa kuyaangalia / kuyajua kabla haujaanza kutengeneza website yako. Usikurupuke, kwani waswahili wanasema, Samaki mkunje angali mbichi, hivyo weka sawa mambo yote kabla jua halijazama na kujikuta upo kwenye giza totoro. Na pia acha kufanya kazi kwa mazoea, kwani inawezekana leo hii umeendelea kuwa juu ingawa hauna ubora kwakuwa watu hawana chaguo lingine au kuna sababu fulani zinakupa wewe kipaombele kupita wengine. Siku sababu hizo zikiisha, hautoweza tena kushindana, hivyo siku zote, shindana kwa ubora na si kwa mazoea.


Chanzo: Dudumizi.com
 
Admin mi huwa napata tabu sana kuedit makala, yaani ni msuli mno pia editor huwa inaondoa styling, check it
 
Back
Top Bottom