SoC03 UKIMWI Bado ni Tishio, Tukuchukue Tahadhari

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
243
615
VVU ni nini? Hiki ni kifupisho cha neno Virusi vya Ukimwi, na Ukimwi ni kifupisho cha Upungufu wa Kinga Mwilini.

Ugonjwa wa VVU/UKIMWI (Virusi vya Ukimwi/ Upungufu wa Kinga Mwilini) umeingia Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 1980, ambapo watu waliupa majina mbalimbali, yakiwemo “Juliana”, “Slim”, “Ngoma”, “Miwaya”, “Mdudu”, “Umeme” nk. Ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa unaambukizwa kwa njia ya kujamiana (ngono).

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kufikia mwaka 2014 ugonjwa wa ukimwi umeua takriban watu milioni 39, wengi wao wakiishi barani Afrika, hasa kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa mwaka 2015 pekee, wamefariki watu milioni 1.2, wengi wao wakiwa watoto.

Uoga Dhidi ya VVU/UKIMWI Umepungua
Watu wengi hasa vijana wa kiume na wa kike hawachukui tahadhari kujikinga na VVU/UKIMWI. Wengi wanafanya ngono zembe (naamanisha bila kutumia kinga), eti kwa sababu wakitumia kinga (yaani kondomu), tendo la ngono halina ladha!

Nimefanya utafiti mdogo, usio rasmi kuhusiana na swala hili. 7 kati ya vijana wa kiume 10, nilioongea nao, walisema wakifanya ngono kwa kutumia kondomu hawapati ladha, na pia hawajali uwezekano wa kuambukizwa VVU/UKIMWI.

Kwa upande wa vijana wa kike, 8 kati ya 10 walisema hawapati hisia wakifanya ngono kwa kutumia kondomu, na pia walionyesha kutoogopa kupata maambukizi ya VVU/UKIMWI. Ukweli huu unathibitishwa na taarifa kuhusu wanafunzi wa chuo kimoja cha Ualimu (sitakitaja hapa) waliokwenda kufanya mafunzo kwa vitendo katika mkoa mmoja (jina limehifadhiwa) mwaka 2022, ambao miongoni mwao, watatu walirudi chuoni wakiwa wajawazito.,

Wakati ugonjwa huu ukiwa mpya mwanzoni mwa miaka ya 1980, na dawa za kufubaza VVU (maarufu kama Anti-Retroviral Drugs - ARVs) zikiwa hazijaanza kutumika, watu wengi waliogopa sana, na unyanyapaa ulikuwepo kwa kiasi kikubwa. Ni kipindi ambacho waathirika wengi walikuwa wanakonda sana, muda mfupi baada ya kupata maambukizi.

Ndio maana kulikuwa na mwiitikio mkubwa wa matumizi ya kondomu na njia nyingine za kujikinga na maambukizi ya VVU kati ya miaka hiyo ya 1983 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Kwa sasa, waathirika wengi hawapotezi uzito kutokana na elimu ya kuishi kwa matumaini, Lishe na matumizi ya “ARVs”. Hali hii, pia imefanya watu wengi kupunguza uoga dhidi ya VVU/UKIMWI.

VVU/UKIMWI Bado ni Tishio na Unaua
Pamoja na ukweli kwamba nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, zinakabiliwa na magonjwa hatari yasiyoambukiza (kama Saratani, Shinikizo la juu la damu, Kisukari, Magonjwa ya Figo, na kadhalika); ukweli ni kwamba UKIMWI unaosababishwa na VVU upo na watu wanaugua na wanakufa.

Nimeishi miji mbalimbali hapa Tanzania, ikiwa ni pamoja na Kasulu, Kigoma, Nzega, Kahama, Shinyanga, Moshi, Arusha, Mwanza, Iringa, Morogoro, na Dar es Salaam kwa vipindi tofautitofauti. Kote huku nimeshuhudia watu wa marika tofauti (Vijana na Watu wazima) wa kike na wa kiume wakiugua UKIMWI (kutokana na VVU) na kufariki, ingawa wengi wao walikuwa wanazingatia taratibu zote za kuishi kwa matumaini, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kufubaza Virusi (“ARVs”)

Kiwango cha Maambukizi ya VVU kwa Umri na Jinsi
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania (Machi, 2019), Hali ya maambukizi ya VVU imefikia asilimia 12 kwa wanawake wenye umri wa miaka 45-49 ikilinganishwa na asilimia 6.8 ya wanaume wenye umri wa miaka 45-49.

Kielelezo Na. 1: Kiwango cha Maambukizi ya VVU/UKIMWI Tanzania Kimkoa
Kiwango Maambukizi ya VVU kwa Watu Wazima TZ Kimkoa Rev.png

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania (Machi, 2019)

Hali ya maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka15-24 ni asilimia 1.4 (kwa wanawake wenye umri huu ni asilimia 2.1 na wanaume ni asilimia 0.6). Tofauti kubwa ya hali ya maambukizi ya VVU kati yawanawake na wanaume imeonekana zaidi kwenye kundi la vijana, ambapo hali ya maambukizi ya VVU kwa wanawake wenye umri wa miaka 15-19, 20-24, 25-29, 30-34 na 35-39 ni mara mbili (au zaidi) ikilinganishwa na wanaume wa kundi la umri huo.

Kielelezo Na. 2: Kiwango cha Maambukizi ya VVU/UKIMWI Tanzania, Kiumri na Kijinsi
Kiwango Maambukizi ya VVU TZ.png

Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania (Machi, 2019)

Wanawake wana kiwango kikubwa cha maambukizi mapya ya VVU ukilinganisha na wanaume. Kwa mwaka, kuna wanawake wawili kwa kila ambukizi jipya la wanaume.

Serikali na Wadau wengine Wanapaswa Kuongeza Jitihada Kupunguza VVU/UKIMWI
Kutokana na matukio mbalimbali duniani, mfano mabadiliko ya tabia nchi, maradhi yasioambukiza kuongezeka na ujio wa ugonjwa wa Korona n.k. jitihada za kudhibiti VVU/UKIMWI zimepungua.

Ukweli huu unathibitishwa na Ripoti ya Umoja wa Mataifa (Jul, 2022), ambapo inasema, Takwimu mpya kutoka kwa UNAIDS kuhusu mapambano dhidi ya VVU duniani zinaonesha kwamba katika miaka miwili iliyopita ya COVID-19 na majanga mengine ya kimataifa, maendeleo dhidi ya janga la VVU yamedorora, rasilimali zimepungua, na matokeo yake mamilioni ya maisha yako hatarini. Kudorora kwa maendeleo kulimaanisha takriban maambukizi mapya milioni 1.5 yalitokea mwaka jana (2021), yaani zaidi ya watu milioni 1 zaidi ya malengo ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Kamati za Bunge (Februari, 2019), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, ilibaini ufinyu wa Bajeti na ucheleweshwaji wa fedha kutoka serikalini, ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 90 ya Bajeti ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi, inategemea fedha za wafadhili wa nje, hali inayopunguza ufanisi wa Tume katika mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Taarifa inaendelea kusema, Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania ilitengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.983 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Hadi tarehe 28, Februari 2018 Tume ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 3.462, sawa na asilimia 57.8 tu ya fedha zote zilizotakiwa kutolewa na Serikali kwenda katika Tume hii.

Hitimisho
Serikali, na Wadau mbalimbali waongeze nguvu katika kampeni ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI; na kila mtu awajibike kujilinda na maambukizi haya na kutoa elimu hii kwa wengine.

Marejeo
Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanzania (Machi, 2019), Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (This) 2016 – 2017.

Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, (Nov. 28, 2022), Jitihada za Pamoja ni Muhimu katika Kutokomeza VVU Tanzania.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa (Jul, 2022), Maendeleo dhidi ya UKIMWI yakidorora, Mamilioni ya Watu Hatarini.
 
Nchi ilitegemea sana misaada kutoka nje kwa muda mrefu kwa ajili ya kupambana na VVU/UKIMWI, imefika wakati ambao wafadhili wana vipaumbele vingi vinavyoshindana, na hivyo kupunguza misaada kama hiyo; ni wakati muafaka kutafuta vyanzo vya ndani na kuacha kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.
 
Back
Top Bottom