Uchambuzi: Athari za Tozo za Laini ya Simu kwa ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano nchini

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Wakati kilio cha wananchi kikiongezeka kuhusu tozo mpya za serikali kwenye miamala ya kifedha kupitia simu, Watanzania wanajiandaa kukabiliana na tozo mpya kwenye laini za simu kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.

Serikali imekusudia kukusanya jumla ya Tsh. bilioni 396.3 kutokana na tozo hizo ndani ya mwaka mmoja. Katika Bajeti iliyopitishwa mwezi June Bungeni, serikali imekusudia kutoza kati ya Tsh. 5 hadi Tsh. 200 kwa kila laini ya simu, kiwango hicho kikitofautiana kulingana na matumizi (kiwango cha kuweka vocha) kwa laini.

Kwa kila mteja atakayeongeza salio la chini ya Tsh. 1,000 atatozwa Tsh. 5; atakayeongeza Tsh. 1,001 hadi Tsh. 2,500 atatozwa Tsh. 10; salio la Tsh. 2,501 hadi Tsh. 5,000 litatozwa Tsh. 21; Tsh 5,001 hadi Tsh. 7,500 litatozwa Tsh. 40; Tsh. 7,501 hadi Tsh. 10,000 litatozwa Tsh. 76, Tsh. 10,001 hadi Tsh. 25,000 litatozwa Tsh. 113; Tsh. 25,000 hadi Tsh. 50,000 litatozwa Tsh. 153 na Tsh. 50,001 hadi Tsh. 100,000 litatozwa Tsh. 186.

Mchanganuo Tozo.png


Kwa mujibu wa Gazeti la The Citizen, mjadala wa utekelezaji wa tozo hizo unaendelea, na kuna uwezekano wa tozo hizo kubaki kwenye vocha tu na si vifurushi vya simu.

Tozo hizi ni nyongeza ya mzigo kwa mlipakodi mtumiaji wa huduma za simu ambapo, katika tozo ya miamala, makato katika miamala ya simu yalifikia Tsh. 31,000 kwa muamala unaofikia Tsh. Milioni 1, ikijumuisha makato ya kutuma na kutoa pesa.

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema siku ya Jumatatu kuwa amepokea maelekezo kutoka kwa Rais Samia kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu ongezeko la tozo ya miamala.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Research ICT Solutions mwezi Julai mwaka 2021 unaonesha kuwa ongezeko la tozo za laini ya simu zitachochea mdororo wa sekta ya mawasiliano kinyume na matumaini ya serikali. Katika ripoti iliyoandikwa na Dkt. Christoph Stork na Steve Esselaar, inapendekeza suluhisho la kuongeza mapato ya serikali kupitia sekta ya mawasiliano kwa kuongeza idadi ya watumiaji wa mtandao badala ya kodi.

Upatikanaji wa mtandao wa 3G nchini unafikia asilimia 85 huku watumiaji wa internet wakikadiriwa kuwa asilimia 49 tu. Hata hivyo, idadi hiyo inaweza kuwa ndogo zaidi kutokana na watumiaji wengi kuwa na laini zaidi ya moja.

Uchache huu wa watumiaji wa intaneti unasababishwa na gharama kubwa ya vifaa (simu janja, modem nk.), vifurushi vya intaneti na upatikanaji mdogo wa umeme hasa vijijini ambapo asilimia 35 tu ya maeneo yote nchini yana nishati ya umeme (kwa mujibu wa Benki ya Dunia).

Mlinganyo.png


Hata hivyo, utafiti unaonesha kuwa ongezeko la upatikanaji wa mtandao wa intaneti kwa asilimia 10 linaweza kusababisha kukua kwa pato la taifa (GDP) kwa hadi asilimia 2.46 kwa nchi za Afrika. Ukuaji huu wa kiuchumi si wa wakati mmoja tu, bali ni ukuaji endelevu utakaoifaidisha nchi kwa kipindi kirefu mbeleni.

Hii si mara ya kwanza kwa serikali kujaribu kuweka tozo kwenye laini za simu. Mwaka 2013 serikali ilipeleka muswada kama huu bungeni, lakini haukutekelezwa. Nyongeza hii ya tozo ya laini za simu inakuja juu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18; makato ya asilimia 17 ya Huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki; Shilingi 278.4, ikiwa gharama ya chini zaidi (minimum charge) kwa dakika kwa kupiga simu za kimataifa; asilimia 25 kwa gharama, bima na usafirishaji kwenye laini za simu na vocha za kukwangua pamoja na makato ya asilimia 10 kutoka kwenye kamisheni ya mawakala wa fedha za simu.

Mtandao wa Vodacom, ambao unamiliki asilimia 30 ya soko la mawasiliano nchini, umepata hasara ya Tsh. Bilioni 30 mwaka 2021, huku baadhi ya sababu zilizopelekea hasara hiyo zikiwa ni pamoja na kupoteza mamilioni ya watumiaji kutokana na usajili kwa alama za vidole (biometric registration), kununua vifaa kwa jailli ya usajili wa alama za vidole, kodi kubwa inayotozwa kwenye simu janja ambayo imepekekea uchache wa simu janja nchini pamoja na bei elekezi za vifurushi kuwa chini ya uhalisia wa gharama za soko, hivyo kulazimika kuuza vifurushi kwa bei ya hasara ili kukidhi matakwa ya bei elekezi.

Tozo hizi, licha ya kuongeza mapato kwa serikali, zinaweza kuwa na matokeo hasi kibiashara hasa kwa wawekezaji (mitandao ya simu). Serikali inatarajia kukusanya mapato ya Tsh. milioni 396 kutokana na mapato ya tozo ya Tsh. 20 kwa siku. Hiki ni kiwango kizuri cha mapato, lakini, ukikadiria kuwa hakuna mtumiaji anayeweza kutumia zaidi ya kiwango anachokitumia kwa sasa, tozo hizi mpya zinamaanisha kuwa hata kwa makato ya Tsh. 10 tu kwa siku, mapato ya Vodacom yatapungua kwa zaidi ya Dola milioni 25 za Kimarekani (sawa na Tsh bilioni 57.9); kwa makato ya Tsh. 200 kwa siku, mapato ya Vodacom yatapungua kwa zaidi ya dola za Kimarekani nusu bilioni.

Kutokana na tozo hizi za laini za simu, kwa tozo ya Tsh. 200 kwa siku, mtandao wa Vodacom utakusanya mapato makubwa kuliko mapato yake inayokusanya kwa mwaka mzima. Kwa tozo ya Tsh. 10 kwa siku, Vodacom itakusanya mapato ambayo ni sawa na asilimia 6 ya mapato yake kwa mwaka huku ikikusanya asilimia 12 ya mapato yake kwa mwaka ikiwa itakusanya tozo ya Tsh. 20 kwa siku.

Vodacom.png


Mtandao wa Airtel, kwa upande wake, utalazimika kukusanya mapato kutokana na tozo ya Tsh. 200 kwa siku, ambayo ni makubwa mara mbili ya mapato yake ya jumla ya mwaka 2019. Makato hayo hayamwathiri mtumiaji wa mwisho pekee, lakini yanaathiri pia uwekezaji wa makampuni ya mawasiliano na kuwasukuma mbali zaidi kutokana na gharama wanazolazimika kuzibeba.

Airtel.png


Athari za makato haya mapya zinatarajiwa pia kujitokeza katika bei za vifurushi vya simu. Ikiwa serikali itakata Tsh. 20 tu kwenye laini za simu kwa siku, gharama za vifurushi vya intaneti kwa GB 1 zinatarajiwa kuongezeka kwa kati ya asilimia 6 hadi 30. Kwa upande wa vifurushi vya kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), tozo hizi mpya zinatarajiwa kuongeza gharama ya kiwango cha kupiga simu 30 na kutuma SMS 100 kwa mwezi kwa kati ya asilimia 8.8 hadi 24, ikitegemea na mtoa huduma (mtandao wa simu).

Kwa upande mwingine, ongezeko la upatikanaji wa huduma za intaneti nchini kwa asilimia 10 tu linaweza kusababisha kuongezeka kwa pato la ndani (GDP) kwa zaidi ya Dola milioni 178.5 za Marekani (sawa na zaidi ya Tsh bilioni 41.3), ambayo ni zaidi ya fedha zitakazokusanywa kutokana na mapato yatokanayo na makato ya laini za simu.

Makato ya laini za simu yanakwenda kuongeza mzigo wa makato ambao tayari umekwishaielemea sekta ya mawasiliano nchini, na kwenda kupunguza ukuaji wa matumizi ya sekta hiyo kwa kupunguza idadi ya watumiaji. Badala ya kuongeza makato, serikali inapaswa kuongeza wigo wa kupata mapato kupitia sekta ya mawasiliano ambayo itasaidia kukuza sekta hiyo badala ya makato yanayodumaza ongezeko la watumiaji na matumizi ya mawasiliano nchini.

Janga la mlipuko wa virusi vya corona limeongeza zaidi uhitaji wa teknolojia ya mawasiliano kufanikisha mahitaji muhimu. Kama ilivyoshuhudiwa kote ulimwenguni, katazo la mikusanyiko limesababisha watu kuwa tegemezi kwa sekta ya mawasiliano. Serikali nyingi duniani zimewekeza kuondoa vikwazo kwenye sekta ya mawasiliano huku vikihakikisha wananchi wake wanaheshimu sheria za kutokaribiana kuepusha maambukizi. Nchini Tanzania, maambukizi ya virusi vya corona yanaipa serikali changamoto ya kuangalia sekta ya mawasiliano kwa jicho la fursa na kuwekeza kuondoa vikwazo vyote vinavyoweza kukwamisha ukuaji wa sekta hiyo kwa namna moja ama nyingine.

Hata hivyo, serikali ilitangaza, katika bajeti ya mwaka 2021/2022, kuondoa Tozo ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja, vishikwambi (tablets) na modem, lengo likuwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya intaneti kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwaka 2025. Hii ni hatua nzuri kuelekea mwelekeo sahihi. Pamoja na hayo, serikali inapaswa kuondoa tozo ya asilimia 17 katika salio ili kuongeza uwezekano wa kufikia lengo hilo.
 
Back
Top Bottom