Tumefikia Utimamu wa Uwazimu

Filipo Lubua

JF-Expert Member
Nov 18, 2011
339
578
Twajaa utimamu wa uwazimu, bila dhima twamhukumu imamu
Huzunini twajifanyia karamu, Ramadhani twabugia kharamu
Wenye wehu tumewapa hatamu, dhiki yetu itadumu dawamu
Maumivu yatujia kwa jamu, watoto wetu watatulaumu

Isikize yangu nudhumu, niambapo kwa yangu taalimu
Niseme hilaze bin-Adamu, kutakasisha yaliyo kharamu
Kukidhi hajaze na hamumu, ya utamu ayatia sumu
Kupata wafwasi na taumu, hata aua na kumwaga damu

Kwa hakika gharika imetimu, mafuriko yametinga kwa ufumu
Ukakasi watiwa kwenye utamu, hata kula yatuishia hamu
Ni sharti ipigwe baragumu, ama sivyo tutakuwa marehemu
Tokeni kwa marungu na jumu, hima tushambulie kwa zamu

Ghiliba zao hazyandiki kalamu, mana nazo wamezijaza damu
Udhalimu waishinda elimu, kazi yetu yajazwa shutumu
Tujue kamwe Mola si wa msimu, na shetani katu si wa dawamu
Wenye dhulma na walo dhalimu, yaja siku ya yao hukumu

Siku zote tumefanywa hamamu, utesaji ndo yao rajamu
Nawambia wazee na hirimu, tuinuke tuwapinge mahasimu
Mateso yao hayana rakamu, tukiungana tutawatupa jahimu
Kuteswa kwetu akuona Rahimu, asilani hatutaona ugumu

Watendapi siku ya hukumu, ipigwapo ya mwisho baragumu?
Kizimbani mbele ya Hakimu, wajibuje maswali magumu?
Hakika nyoto za Jehanamu, zitawachoma kwa ramramu
Ziwalapo nyama na damu, watauma ndimi na kujilaumu


© Filipo Lubua, 21 Disemba 2011
 
Back
Top Bottom