Tukibaki Hai, Tutasimulia

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,536
23,985
Ni muda mrefu sana kwenye hizi anga za simulizi, sasa hatimaye nimerejea na hadithi hii.


Kwa wale wageni, waweza tazama hizi ... ni kazi ya mikono yangu ...









Haya sasa, tuingie kwenye uraibu. Happy Addiction.
View attachment 2474247
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.


Na Steve B.S.M


Sehemu ya Kwanza



Queens, New York. 2019.


"Mwaka 1962 nilifungua ofisi hii ya uchapishaji wa vitabu. Ni ofisi ndogo sana lakini ina nafasi kubwa katika moyo wangu kwasababu kuu tatu.

Mosi, nayaenzi mapenzi yangu katika uandishi kwani nimekuwa nikiandika tangu utotoni, madarasa ya chini kabisa. Lakini pili mimi ni mpenzi sana wa kusoma vitabu, hivyo ofisi hii itanipa fursa ya kuishi mapenzi hayo milele. Na tatu ..."

Mlango ulifunguliwa.

Macho ya Bryson yalibanduka toka kwenye 'stika' aliyokuwa anasoma ukutani, yakatazama mlango mwembamba unaotenganisha sebule ya ofisi na hii aliyomo ndani.

"Hilda?" Aliita.

Kimya.

"Richie?"

Kimya.

Alisikia mlango unafungwa kisha pakawa kimya kama awali. Kutazama saa ya ukutani, ni saa mbili na robo usiku. Wenzake wawili, Hilda na Richie walishamuaga wakaondoka lisaa limepita sasa.

'Huyu atakuwa nani?' Alijiuliza kifuani.

Uso wake ulikunja ndita akiusogeza mwili wake mrefu kwenye mlango wa kioo uliokuwa wazi.

Kidogo...

"Hello, Bryson!"

Macho yake yalitua juu ya mwanamke mwembamba, makamo miaka ya thelathini, amevalia gauni zambarau lililombana. Miguu yake imo ndani ya viatu vyeusi vyenye visigino virefu. Kichwa chake kimefunikwa na kofia nyeusi yenye paa mduara iliyolegea. Mkononi ana saa nyeusi ya gharama na kwenye meza tayari alishatua pochi yake nyeusi yenye mkanda mrefu.

Macho yake yalijieleza ni mtu mwenye asili ya Ashia. Mdomo wake wenye rangi nyekundu ulikuwa unatabasamu kwa mbali mno lakini kwasababu ya udogo wa 'lips' zake usingebaini hilo bila ya kuongeza umakini.

"Naweza kukusaidia?" Bryson aliuliza akisogea taratibu, mikono yake imo mifukoni.

"Labda," mwanamke akamjibu akipandisha mabega. "Mimi ni mgeni wako, nimekuletea aidha pepo au jehanamu." Muda huu 'alikunja nne' na kuuweka mkono wake mwembamba mezani.

Macho yake madogo yenye dhamira kali yalikuwa yanamtazama Bryson bila kupepesa. Ni kama vile alikuwa anajaribu kusoma kilichomo kichwani mwa mwanaume huyo.

Alikuwa ni mwanamke mtulivu ajabu.

"Samahani, Miss," Bryson alisema kwa sauti ya chini. "Huu si muda wa wateja, tumeshafunga ofisi."

"Bryson, najua muda wa wateja umeshaisha ila mimi sijaja kama mteja. Mimi ni mgeni wako kama nilivyokuambia, na nini nilichokuletea inategemea na wewe utakavyoona baada ya kupitia ujumbe wangu huu."

Mwanamke huyo alifungua pochi yake maridhawa akatoa bahasha ndogo ya kaki iliyojazia, akaiweka mezani na kusimama. Mkanda wa pochi akauvesha begani.

"Ni juu yako, Bryson."

Aliufuata mlango na kujiendea, mwendo wake mithili ya walimbwende jukwaani. Nyuma yake alisindikizwa na sauti ya visigino vya viatu.

Bryson alimtazama mwanamke huyo kwa udadisi. Hakumaliza hamu yake. Alipokuja kupata ufahamu wa kuuliza mwanamke huyo amefahamu vipi jina lake, tayari alikuwa ameshachelewa. Alishatokomea.

Alikuna kidevu chake chenye kutu za ndevu kisha akaisogelea bahasha na kuitwaa. Aliifungua akaitazama ndani. Akatoa macho! Kulikuwa na barua na burungutu moja la dola mia mia za kimarekani!

Aliifunga bahasha upesi na kuitia mfukoni. Alitazama kushoto na kulia kuhakikisha kama kuna aliyemuona alafu akasema na nafsi yake,

"Huyu ni nani?"

Haraka alielekea kwenye ofisi yake, huko alitwaa mkoba wake uliokuwapo mezani alafu akapiga hatua tatu kubwa kuufuata mlango kabla hajasimama na kutazama tena 'stika' ile aliyokuwa anaisoma hapo awali.

Ni kama vile alikuwa anaidai stika hii. Muda huu hakuisoma bali aliitumbulia tu macho kwa kama sekunde tatu kisha akaondoka zake.

Ofisi ilibaki pweke, 'stika' imesimama ukutani na maneno yake yaliyomalizia ...

" ... Na tatu, ni kuwapa nafasi wote wenye mapenzi na uandishi lakini wanashindwa kutimiza ndoto zao kwa ukosefu wa pesa."

Nukuu hiyo kwenye stika ilimalizia na neno - 'Baba'.

...

Punde Bryson alipotoka ndani ya ofisi, alitembea kama mtu anayeshuku kuwindwa na mdunguzi. Macho yake hayakutulia. Mwendo wake ulikuwa wa haraka kuliko kawaida.

Alipokaribia gari lake, ford taurus, toleo la miaka ya themanini, alijitweka kitini, aka 'lock' milango na kutimka! Muda si mrefu akawa ameishika barabara kuu ya Montauk akielekea East Hampton yalipo makazi yake.

Siku hiyo hakunyookea nyumbani kama ilivyo ada. Hamu ilikuwa imemkaba koo. Kila alipokuwa anazidi kujongea na kusogea, alihisi anazidi kupungukiwa na pumzi.

Alipojiaminisha ya kwamba yu salama, akaegesha gari lake na kutoa tena ile bahasha kuipekua.

Aliyatoa macho yake akiipitia barua ile iliyoambatanishwa na donge nono la pesa,
akawa anasoma neno kwa neno, kituo kwa kituo.

Punde alipapasa koti lake kutafuta pakti ya sigara.

"Shit!"

Hakuwa na kitu mfukoni bali kiberiti tu.

Mithili ya mtu aliyechanganyikiwa, akafunguafungua droo za gari na bahati akakuta humo pakti moja yenye sigara mbili, akanyofoa moja upesi akaipeleka mdomoni. Aliiwasha akainyonya kama mtu aliyekuwa amebanwa na kiu kikali!

Alivuta na kutema moshi kwa mikupuo mitano mfululizo ndipo akayarudisha tena macho yake kwenye barua kuendelea kusoma.

Hata alipoimamaliza kuisoma barua hiyo, aliirejea tena na tena. Tena na tena. Ni kama vile alihisi kuna kitu hakipo sawa. Kuna kitu kimekosewa.

Lakini kila alipoirejea aliikuta ni vilevile. Kila neno katika mstari wake. Kila kituo katika nafasi yake.

"Ni upuuzi gani huu?"

Alitulia akiwazua kwa sekunde kadhaa. Mazingira yalikuwa yametulia mno. Akili yake ilienda mbali na kwenye gari alilomo. Ni ghafla simu ilinguruma mfukoni akashtuka mno.

"Fuuuck!!"

Alipayuka akiugonga usukani kwanguvu. Alihema kama mwanambio. Aliitoa simu mfukoni akaitazama. Namba ngeni.



Masaa Matatu Nyuma:




Mwanamke mwembamba mwenye kuvalia gauni la zambarau, kofia nyeusi na viatu virefu vyeusi aliingia mgahawani akiwa ameshikilia pochi yake inayoning'inia toka kwenye bega lake la kushoto. Mwendo wake mpole na macho yake madogo yanaangaza huku na kule.

Kulikuwa na takribani wateja wanne. Watatu Walikuwa ni wanawake na mmoja mwanamume. Wanawake hao watatu walikuwa wamekaa meza moja wakila 'ice cream' na kupiga soga. Mwanaume alikuwa amekaa mpweke, karibu na ukuta wa kioo wa mgahawa, akiwa na glasi ya sharubati baridi mezani. Mrija mpana mwekundu. Amevalia koti la ngozi (leather jacket) rangi nyeusi ndani yake akiwa na tisheti rangi ya samawati.

Mbali na wateja waikuwapo wahudumu wawili waliokuwa wamevalia sare na 'apron' nyeusi zenye kola nyeupe.

Mwanamke yule alipotazama pande zote za mgahawa, akaendea upande wa magharibi alipokuwapo yule mwanaume mpweke. Naye yule mwanaume alipomwona mwanamke huyo anamjia, alipandisha kichwa kutoa ishara.

"Karibu."

Mwanamke aliketi na punde tu mhudumu akafika.

"Naomba kahawa bora uliyonayo," aliagiza kwa sauti ya chini kisha akamtamzama mwanaume yule aliyeketi mkabala naye.

"Nimehakikisha sehemu hii ni sahihi," alisema mwanaume. "Ni kampuni ndogo, haiwezi kukataa ofa hii nono."

"Mbali na hilo?" Mwanamke aliuliza huku akiwa anatazama nje kupitia kioo cha mgahawa. Macho yake yalikuwa yanatazama jengo lililokuwa mbele upande wa kushoto mwa barabara inayokatiza pembeni ya mgahawa aliomo. Jengo hilo lilikuwa kuukuu lenye maandishi makubwa yanayowaka taa rangi nyeupe 'OLYMPUS PRINTING PRESS'.

"Mmiliki wa kampuni, alifariki miaka nane iliyopita akamwachia mwanae, Bryson," Mwanaume yule aliongezea taarifa, "lakini kwa mwenendo wa kampuni ulivyo, ndani ya miaka miwili au mitatu itakuwa imejifia. Mauzo yake yako chini sana. Ina ushawishi mdogo sokoni. Imepunguza wafanyakazi toka kumi mpaka kufikia watatu tu, akiwemo mkurugenzi mwenyewe, Bryson. Kwa namna hii, kamba yoyote itakayotupwa, huyu mfamaji ataidaka anusuru maisha yake."

"Mbali na hilo?"

"Hilo halitoshi?"

"Halitoshi, Ferdinand. Makampuni yanayojifia yapo mengi. Lazima kuwe na sababu ya ziada."

"Ok. Bryson ameshajaribu mara kadhaa kunyanyua kampuni hii bila mafanikio. Nimepitia rekodi zake za majaribio kadhaa benki na kwenye mataasisi mbalimbali ya kukopesha. Lakini zaidi, tofauti na ilivyokuwa kwa baba yake, Bryson hana mahaba na uandishi bali pesa."

Ferdinand aligeuza shingo akatazama kule anapotazama mgeni wake. Kwa kama sekunde tatu hivi pakawa na ukimya kabla hajauvunja kwa sauti ya chini,

" ... ana mke na watoto wawili wa kike. Ni mtu wa --"

"Kahawa hii hapa!" Mhudumu aliwakatiza. Aliiweka kahawa mezani kwa tabasamu kisha akaenda zake.

"Ni mtu wa familia," Ferdinand alimalizia. "Naamini anaweza fanya lolote kwasababu ya familia yake."

Mwanamke yule alikunywa mafundo mawili ya kahawa, bado macho yake yalikuwa kwenye lile jengo. Tangu alipolitazama kwa mara ya pili hakubandua macho yake hapo. Alinyamaza kwa kama sekunde tatu kisha akashusha kikombe chake chini kwenye kisosi.

"Hilo ndo' nililokuwa nahitaji," alisema kwa kunong'ona kisha akapandisha sauti yake kidogo, "Pengine huo ndo' utakuwa msingi wa kazi yangu."

Ferdinand aligeuza tena shingo yake kutazama lile jengo alafu akatazama saa yake ya mkononi.

"Muda wa kufunga ofisi unakaribia. Ataanza kutoka mwanamke, Hilda, atafuatiwa na mwanaume, Richie. Bryson huwa ni wa mwisho. Picha yake --" Ferdinand alijipapasapapasa.

"Sina haja ya picha, Ferdinand," mwanamke akasihi. "Napendelea kumwona mtu kwa macho yangu mwenyewe. Macho yake yatanipa jibu kama ni yeye ndiye namuhitaji."

Alimalizia kahawa yake kwenye kikombe alafu akamtazama Ferdinand machoni.

"Hakikisha kila kitu kinakuwa tayari. Baada ya usiku wa leo, kamwe haitakuwepo njia ya kurudi tena."

Ferdinand akatikisa kichwa ishara ya kuridhia.


Muda wa Sasa...


Bryson kwenye gari.


"Hallo! ... wewe ni nani?"

"Una usiku huu tu kwa ajili ya kufikiria, Bryson," sauti ya kiume ilimjibu. "Alfajiri, jua halijakucha, nitakupigia kuulizia maamuzi yako."

Simu ikakata.

Hakuelewa.

"Ni nini hiki?" Aliuliza akitaza-matazama ndani ya gari lake kana kwamba kuna kitu amepoteza. Kwa muda mchache alikuwa anahisi kama kichwa chake kimeganda. Hakuna lililokuwa linaingia ama kutoka. Honi ya gari lililokuwa linapita barabarani ndiyo ilimshtua na kumrudisha kwenye fahamu zake.

Aliwasha gari akaendelea na safari. Njia nzima mambo yakizunguka miduara mikubwa na midogo kichwani. Sauti zikimshauri na kumwonya. Zingine zikimpongeza na kumsifu.

Hakudhania kama siku hii ingeishia hivi.


----

East Hampton, New York. Saa sita usiku.


Runinga ilikuwa imewashwa lakini hakuna aliyekuwa anaitazama. Picha tu zilikuwa zinahama hapa na pale, hizi na zile, pasipo sauti.

Sebule ilikuwa imezama kwenye kiza chepesi, shukrani ziende kwenye mwanga wa runinga, mbali na hapo, ilikuwa imejazwa na moshi mzito wa sigara uliokuwa unatoka kwenye mdomo mkavu wa Bryson.

Mwanaume huyo alikuwa ameketi kwenye kiti, amevalia bukta fupi nyepesi, mguu mmoja umejiegesha juu ya mwingine, kifua chake kipana kilichojawa na nywele kilikuwa wazi kikipunga upepo.

Mezani kulikuwa na kisosi chenye vipisi vya sigara, kwa harakaharaka idadi kama kumi na mbili hivi. Pembeni ya kisosi hiko kulikuwapo na pakti mbili za sigara chapa Marlboro.

Mkono wa kuume wa Bryson ulikuwa na sigara inayowaka, wa kushoto ulikuwa umeshikilia barua, ileile aliyokuwa anaisoma kwenye gari.

"Bryson!" sauti ya kike iliita. Haraka Bryson aliitambua sauti hiyo ni ya mkewe. Kabla hajafanya chochote, aliifinyaga barua iliyopo mkononi mwake akaitupia chini.

"Mbona hauji kulala?"

Mkewe alimsogelea kwa ukaribu akasimama mbele yake. Alikuwa amevalia gauni maalum la kulalia. Nywele zake ziko hovyo. Mikono yake ameikumbatisha chini ya matiti yake. Macho yake madogo yalikuwa yamejawa na mang'amung'amu ya usingizi.

Ijapokuwa mwanga ni hafifu, uzuri wa sura ya mwanamke huyu ulijionyesha dhahiri. Kama si mwili wake kuwa mnene na kifua chake kuwa cha 'mama', basi ungekubali endapo ungeambiwa ana miaka ishirini tu.

Alimtazama mumewe kwa macho ya kuwazua.

"Kuna mambo kadhaa nilikuwa nayafikiria," alisema Bryson akiifinyangia sigara yake kwenye kisosi alafu akauegemeza mgongo wake kitini.

"Mambo gani hayo, Bryson? Kuna mapya?"

"Hapana. Ni yaleyale ya kila siku."

Mkewe alitazama kweye kisosi kisha akayarudisha macho yake kwa mumewe.

"Mara ya mwisho kukuona unavuta sigara nyingi hivi ilikuwa ni kwenye msiba wa baba yako. Bryson, kuna jambo linakutatiza?"

Bryson hakusema kitu. Alikuwa katika vita ya maamuzi kichwani, amshirikishe mkewe au lah.

Mkewe alichuchumaa mbele yake akamshika magoti.

"Mimi ni mkeo, unaweza nishirikisha tukapeana mawazo. Najua tunayoyapitia ni magumu lakini hii haitasaidia ... leo mchana nilipata bahati ya kukutana na Afisa Gideon wa Assurance Fund. Sikukuambia hili mapema maana niliona upo muda mwingi na watoto. Gideon amesema --"

"Hatotusaidia kitu!" Bryson alimkatisha mkewe. Alimtazama kwa macho yenye ghadhabu huku mdomo wake ukiwa wazi.

"Mara ngapi tumeshahangaika huko bila msaada? Kila tunapoenda wakifanya tathmini ya dhamana wanaona hatukopesheki. Kwenye mabenki ndo' kabisa hapashikiki. Tunadaiwa kiasi kingi cha pesa, hamna mjinga anayeweza kupoteza pesa yake kwetu!"

"Lakini, Bryson, tutaacha kujaribu? Kwahiyo tukae tukingoja kuangamia?"

Bryson hakusema tena kitu. Alishusha pumzi ndefu puani alafu akalaza kichwa chake kwenye kiti.

Sasa ni jambo moja tu ndilo lilikuwa bayana kichwani kwake. Jambo moja tu. Nalo ni juu ya barua ile.

Barua iliyoambatana na dola za kimarekani alfu thelathini. Kwa pesa za kitanzania shilingi milioni sitini na kenda na ushee!


****


GIZANI.


Simu iliita kidogo kisha sauti ikalia 'beep' ...
upande wa pili mtu alikuwa anahema.


"Nimeridhia."

"Umeridhia nini?"

Zilikuwa ni sauti mbili za wanaume. Hali ilikuwa tulivu sana kana kwamba wanaongelea ndani ya maktaba yenye sheria kali.

"Nimeridhia yale yaliyokuwepo kwenye barua."

"Yapi hayo? Taja moja baada ya jingine."

"Kuna haja ya kufanya hivyo? .... unanirekodi?"

Kimya.

"Ok ... moja, kuandika mwanzo mpaka mwisho kitabu chenye SURA KUMI NA MBILI kuhusu maisha ya Mitchelle. Haitajalisha nini kitakachotokea, maishani mwangu ama maishani mwake, sitaweka kalamu chini mpaka pale nitakapomaliza kazi niliyopewa.

Pili, nitachapisha kazi kwenye kila mfumo, mathalani mfumo wa maandishi, lugha nne tofauti, sauti, nukta nundu na 'codes' nitakazopewa kama muongozo kutoka kwa mhusika.

Tatu, nitahakikisha, hata kama ikiwa kwa kumwaga damu, kutokutoa taarifa yoyote ile ya maisha ya mteja wangu kwa yeyote yule chini ya shinikizo la aina yoyote ile.

Nne, nitatumia majina na kadi bandia kufanyia miamala yangu yote ya pesa itakayohusu kazi hii, vilevile nitatumia namba za siri kwenye mawasiliano yangu pale yatakapohitajika."

"Vema, Bryson," sauti ya upande wa pili ilipongeza. "Na mwisho utambue hayo makubaliano yamewekwa kwa chapa ya familia yako." kisha simu ikakata.

Baadae, majira ya saa moja na nusu asubuhi, Bryson, akiwa wa kwanza kabisa kuufungua mlango wa jengo, alinyookea moja kwa moja kwenye chumba chake cha ofisi akakuta bahasha mpya mezani.

Kabla hajaisogelea bahasha hiyo alitazama pande zote za ofisi. Hakukuwa na alama wala uharibifu wowote uliofanyika. Mlango mkubwa ni yeye ndo' aliufungua na vilevile huu mdogo. Yote ilikuwa imefungwa kwa funguo.

Alipekua ndani ya bahasha, humo akakuta kadi mpya ya benki na laini sita za mitandao tofautitofauti ambazo zipo kwenye kifuko kidogo cha 'nylon'.



**
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.


Na Steve B.S.M


Sehemu ya Pili



Queens, New York. Olympus Printing Press.

Saa mbili na dakika arobaini na nne asubuhi.


Bryson alilegeza tai iliyokuwa inamkaba shingoni, akaitazama feni inayoning'inia kwenye dari.

Feni ilikuwa inapuliza kwa kasi sana lakini aliisikia kwa mbali mno. Alishavua koti akalining'iniza mgongoni mwa kiti lakni bado haikusaidia.

Aliitazama ile bahasha iliyokuwepo mezani kwake na punde kidogo mtu akagonga mlango.

"Naweza kuingia?" Alikuwa ni mwanaume mwembamba mrefu, nywele za kahawia, macho makubwa na masharubu machanga. Amevalia tai nyembamba nyeusi, suruali ya kitambaa rangi ya kijivu na viatu vyeusi vinavyong'aa. Mkononi ameshikilia mafaili mawili, moja rangi ya njano na jingine rangi ya kijani.

"Richie!" Bryson alipaza sauti. "Unataka nini?"

Richie alilichukulia hilo swali kama karibu. Aliingia ndani akaweka mafaili mezani.

"Boss, haya ni ma ... ma ... mm ...ma ... malalamiko ya wale waandishi. Wame ... me ... me ... mm.. mepeleka kesi mahak ... kkk ... kamani, aidha kazi zao zitolewe nda ... nd ... nd ... ndani ya juma hili ama warejeshewe fedha zao na faini juu. Juma lijalo sha ... sh .. sh ... sha ... shauri litaanza kusikilizwa mahakamani."

"Juma lijalo na wewe unanipa taarifa leo?" Bryson alitoa macho.

"Boss, nili .. li ... li...l ..likuwa nakuambia tangu juma lililopita. La .. la ... l...l ... lakk ..."

"Aaagh, Richie!" Bryson alifoka. "Naomba uende. Nimekuelewa."

Richie alijiondokea taratibu. Alifika mlangoni akageuka kumtazama Bryson.

"Nini? Kuna kitu umesahau?" Bryson alimtolea macho ya ukali. Richie akatikisa kichwa kisha upesi akaenda zake.

"Hivi huyu Hilda kwanini anampa hii kazi Richie?" Bryson aliongea mwenyewe. "Anajua kabisa mtu mwenyewe anaongea sentensi moja nusu saa alafu bado anamwachia alete maelezo?" Alisonya akatikisa kichwa. Alitazama yale mafaili aliyoletewa, wala hakujichosha nayo, akaendelea na kazi yake kwenye tarakilishi iliyokuwapo mezani.

Bado jasho lilikuwa linamtiririka huku feni inahangaika kumpuliza.

"Vipi, umemuuliza?" mwanamke mnene aliyevalia miwani ya macho alimuwahi Richie aliyetoka punde kwenye ofisi ya Bryson
akiwa anatembea uso chini.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia shati jeupe alilolichomekea kwenye sketi yake fupi nyeusi. Miguu yake minene ilikuwa imezama ndani ya viatu vyeusi visivyokuwa na visigino. Nywele zake ndefu nyeusi zilikuwa zinasalimiana na mabega. Uso wake wenye mashavu mapana ulikuwa umejawa na hamu lakini pia tahadhari.

Alikuwa anaongea kwa kunong'ona. Macho yake yalikuwa yanatazama mlango wa ofisi ya Bryson kila baada ya sekunde chache.

Richie alitikisa kichwa bila kusema kitu.

"Richie, ina maana hujasema kitu? Sasa kwanini uliniambia nikupe mafaili uende wewe?"

Richie alishusha pumzi bila kuongea. Bado alikuwa anatazama chini.

Hilda alishika kiuno chake kinene kilichoshikana na tumbo, akakagua ofisi kwa macho yake manne. Macho ya mawazo.

"Sasa tutaishi hivi mpaka lini?" Alimuuliza Richie kwa kunong'ona. "Mwezi wa ngapi huu hatupati mshahara na yeye amekalia kimya?" Alipiga paji lake la uso kwa kiganja chake chenye nyama. "Aaaagh! Aaaagh!"

Aligeuza shingo kutazama upande wake wa kulia. Hamaki. Moyo wake ulipasua paaah! Uso kwa uso alikutana na Bryson akiwa amesimama mlangoni.

Mwili ulikuwa wa baridi ghafla. Mate yalitawanyika mdomoni kinywa kikabaki kikavu.

"Nakuhitaji mara moja."

"Mi ... mimi?" Hilda alijinyooshea mkono kifuani.

"Ndio, wewe Hilda," Bryson alijibu.

Hilda alimtazama Richie, Richie akatazama pembeni kana kwamba hakuwa kwenye maongezi leo hii. Kama haitoshi, alimpita Hilda akaenda zake kuketi kwenye kiti.

"Funga mlango," Bryson alimsihi Hilda aliyekuwa anaingia ndani ya ofisi yake.

"Karibu uketi, Hilda. Nina mambo kadhaa ya kuongea na wewe."

Hilda aliketi mikono yake akiiweka mapajani. Alikuwa anatazama kwa woga.

"Hilda, hii ni nafasi yetu sasa," alisema Bryson kwa uso wa kujiamini. "Najua tumehangaika sana lakini hakuna lisilokuwa na mwisho. Hatimaye mwisho wa haya umefika sasa."

"Boss, bado nahitaji kazi. Tafadhali, usinifukuze."

"Hildaaa ..." Bryson aliufinyanga uso wake kwa huruma. "Hamna wa kukufukuza. Sijakuitia hapa kwa ajili ya hilo bali nimekuitia hapa kwa neema. Nataka kukupatia nafasi ya kubadli maisha yako kufumba na kufumbua. Uko tayari."

Hilda alitikisa kichwa chake kabla hajajibu kwa furaha, "niko tayari!"

"Lakini kuna gharama za kulipa," Bryson akatahadhaharisha. Alisema huku akiuegemeza mgongo kitini.

"Shilingi ngapi?"

"Hilda, sio kila gharama ni pesa. Kuna gharama kubwa ya kulipa kwenye hili, na endapo ukikubali pia kuna faida kubwa ya kubadili kila kitu kwenye maisha yako."

"Niko tayari. Niambie gharama ninazotakiwa kulipa."

Bryson akatabasamu.


***


Bronx, New York. Saa saba mchana.


Gari jeusi, Cadillac Escalade toleo la mwaka 2019, lilikuwa limejiegesha pembeni ya jengo refu la 'The Dorothy apartment' katika mtaa mashuhuri wa McGowan.

Ndani ya gari hilo alikuwamo mwanaume aliyevalia suti nyeusi katika kiti cha dereva, na nyuma yake akiwepo mwanamke mwembamba aliyevalia nguo nadhifu mithili ya mwanamitindo. Gauni rangi ya maziwa iliyoambatana na kofia yake. Mstari wa vifungo ulikuwa upande wake wa kushoto. Shingo yake nyembamba ina cheni yenye kito cha almasi, na kama ilivyo ada mkono wake wa kushoto una saa ya gharama.

Alikuwa ni mwanamke yuleyule aliyefanya makubaliano na Bryson siku ya nyuma yake. Alikaa hapo kitambo kidogo, akaja mwanaume mzee, makamo ya miaka sabini, aliyevalia suti rangi ya 'bluu'.

Mwanaume huyo alifungua mlango wa nyuma akaketi pembeni ya mwanamke yule. Haikuwa na haja ya salamu, moja kwa moja walienda kwenye mada.

"Dr. Lambert, umefanikiwa?" Mwanamke aliuliza. Macho yake yalikuwa yanatazama mbele.

Mzee yule aliingiza mkono wake ndani ya koti akatoka na 'flash drive' rangi nyekundu pamoja na bomba mbili za sindano akamkabidhi mwenyeji wake.

"Nimefanikiwa, Mitchelle."

"Vizuri," Mwanamke alipongeza. "Sasa unaweza kwenda nyumbani."

Mara moja aliweka mzigo wake kwenye pochi.

"Lakini Mitchelle," Dr Lambert alisita. "Una uhakika hili litafanikiwa?"

"Nina imani. Vipi kuhusu wewe?"

"Si kwamba sina imani lakini vita hii siyo ndogo. Wenzako wote wameshakamatwa na kuuawa. Umebaki mpweke. Unadhani unaweza ukabadili yote kwa mkono mmoja?"

"Ndio."

Mitchelle alimtazama Dr. Lambert kwa macho yasiyokuwa na hisia, akasema;

"Labda pale utakaponisaliti."

"Mimi?" Dr. Lambert alitoa macho yake ya kizee. "Unajua wazi siwezi fanya hivyo." alitabasamu ila si kwa furaha. "Kwa yote yale mpaka kufikia hapa, kwanini nikusaliti, Mitchelle?"

"Kila mtu ana bei, Dr." Alisema Mitchelle kisha akakaza macho yake madogo akiongezea, "lakini tambua siku utakaponisaliti, sitaharakisha kifo chako mpaka pale nitakapohakikisha kila kiungo kilichopo katika mwili wako kimeshiba maumivu makali."

"Hamna haja ya kufika huko, Mitchelle. Mimi na wewe ni washirika."

Mitchelle alijiegemeza kitini akatazama mbele mithili ya dereva aliyekwenye mwendo.

"Pesa yako utaikuta benki. Uwe na jioni njema."

Dr. Lambert hakuwa na la ziada, alishuka kwenye gari akaenda zake. Gari likawashwa na moja kwa moja likanyookea Midland beach, huko Mitchelle alikutana na Ferdinand ambaye aliongozana naye mpaka Queens.

Waliingia ndani ya Halletts Point Apartment, jengo refu lenye makazi ya kifahari. Makazi ya mwanamke Mitchelle. Humo ndani ya muda mfupi, walijikuta ndani ya sehemu mahususi ya kujipumzisha.

Mahali hapa palikuwa na makochi mapana ya kijivu yenye mito minene minene rangi nyeupe na bluu. Sakafu ilikuwa na manyoya marefu malaini yanayomeza miguu mpaka kwenye enka. Madirisha ya kioo mapana na marefu kimo cha binadamu yakitoa picha mwanana ya jiji la New York, namna maghorofa yanavyoshindana kuikuta anga. Napo dari ilikuwa imesanifiwa kwa maua ya urembo na taa zenye kupendeza machoni.

Rangi tulivu na 'design' ya hili eneo vilimalizia kuonyesha kuwa hapa hapakuwa eneo la makabwela.

Pasipo kupoteza muda, Mitchelle aliutoa ule mzigo aliokabidhiwa na Dr. Lambert akampatia Ferdinand. Ferdinand, kwa macho yake makali, aliukagua upesi mzigo huo kabla hajaitengua ile 'flash drive', ndani yake akakuta 'microchip' na 'tube' ndogo nyembamba yenye kimiminika cha kijani.

Alifyonza kimiminika hiko chote kwenye bomba la sindano alafu akaifanyia majaribio.

Alipoona kila kitu ni chema, alifunga mkono wa kushoto wa Mitchelle, juu kidogo ya kiwiko, kwa kutumia kitambaa alichopewa na mwanamke huyo toka kwenye pochi yake alafu akamdunga sindano.

Mitchelle aliikunja sura kwa mbali wakati sindano inapenya mwilini. Zoezi lilipokamilika, ilimchukua kama sekunde tano hivi kuanza kuhisi kichwa kizito na uono wake unafifia. Ikafikia muda akawa haoni kabisa!

Ferdinand alimlaza taratibu kwenye kochi kisha akairejesha ile flash katika hali yake ya kawaida.

Alimtazama Mitchelle kwa macho ya huruma, hasa namna mkono wa mwanamke huyo ulivyojawa na makovu ya sindano, makovu ambayo hufunikwa na mikono ya magauni yake ya gharama anayoyavaa, akaishia kutikisa kichwa.

Aliinuka akaita jina la Jennifer, Punde akatokea mwanamama aliyevalia sare rangi ya maziwa. Makamo ya umri wake miaka arobaini. Nywele zake zilikuwa mkorogo wa rangi nyeusi na nyeupe.

Ferdinand alimpatia mwanamke huyo ishara ya mikono ya kwamba amtazame Mitchelle yeye anatoka, naye mwanamke huyo akarudisha taarifa kwa ishara ya mikono vilevile akimaanisha hamna shida, atafanya hivyo.

Jennifer alikuwa ni bubu.


**


Olympus Printing Press: Saa mbili ya usiku.


Bryson alitazama saa yake ya mkononi. Alikuwa peke yake ndani ya ofisi. Kuondoa upweke, alikuwa ameweka 'earphones' zenye muziki laini kwa mbali masikioni. Muziki ambao usingemnyima kusikia sauti ya jambo lolote lile likitukia.

Mshale wa saa ulisogea taratibu. Mara kwa mara Bryson alikuwa akiukagua kisha anaendelea na shughuli zingine za hapa na pale.

Mshale ulipogota kweye robo ya saa, mlango ulifunguliwa akaingia Ferdinand. Bila shaka alishawasiliana na Bryson kwani alinyookea kwenye ofisi yake moja kwa moja bila kupoteza sekunde.

Aliketi, akatoa 'flash' ambayo alimpa Bryson na maelezo machache; "Anza kuandika yaliyomo humu ndani kama dibaji. Andika kila jambo."

Bryson aliitikia kwa kutikisa kichwa. Aliiweka ile 'flash' kwenye mfuko wake wa koti alafu akampatia Ferdinand mkono wa kheri.

"Ondoa shaka."

Ferdinand hakuupokea huo mkono, badala yake alinyanyuka akaaga.

"Samahani kidogo," Bryson alipaza sauti. Alijikenulisha meno, akauliza; "Vipi kuhusu ... ku-kuhusu hela?"

Ferdinand alimtazama kwa kama sekunde tatu hivi, Bryson akashikwa na haya. Ni jana tu alikua amepewa pesa na hivi leo anaulizia tena.

"Au basi, haina shida, mkuu."

"Pesa imeshawekwa kwenye Account," Ferdinand akamjibu akimkazia macho. "Na kumbuka kuheshimu makubaliano yetu, Bryson."

Alihitimisha kikao kwa namna hiyo alafu huyo akaenda zake.

Bryson naye baada ya hayo hakuwa na cha kungoja, alifunga ofisi akashika njia kwenda nyumbani.

Safari haikuwa ndefu. Pengine sababu hakuwa amegubikwa na mawazo kama ilivyokuwa kawaida yake.

Mara kwa mara alijikuta anatabasamu asijue anatabasamia nini. Hakuamini. Ila kila kitu kilikuwa bayana kama jua kavu la saa nane. Pesa inakuja. Mabega yake yalianza kupata unafuu wa mzigo aliokuwa ameubeba miaka nenda rudi.

Hatari kitu gani bwana kama usalama wenyewe unaambatana na umasikini uliokithiri? Alijiuliza hilo swali akajikuta anahisi amani ya moyo.

Akatabasamu tena.

Alipofika nyumbani, watoto wake walimpokea kwa kumkumbatia kwa furaha. Naye aliwabeba kila mtoto kwa mkono wake. Aliwabusu na kuwajulia hali, aliwatania na kucheza nao.

Watoto hawa wa kike, Cecy na Celina, walikuwa ni mapacha waliotofautiana dakika tu. Miaka yao ilikuwa sita. Nywele zao walizibana kutengeneza mikia mirefu. Nyuso zao zilikuwa na furaha tele, hasa wakiwa na baba yao. Kila saa walikenua kuonyesha meno yao madogo yenye nafasinafasi za mapengo.

Hawa ndo' walikuwa tumaini la Bryson. Kila alipowatazama, aliona sababu ya kupambana maishani tena na tena.

Wakati huo akiwa anahangaika hivyo na watoto huku na kule, mara kidali mara kubebana, mke wake alikuwa akiwatazama tu akicheka mithili ya mtu anayetazama runinga yenye kuonyesha vipindi vizuri vya kusisimua.

Zoezi hilo lilidumu kwa kama lisaa hivi kabla ya familia nzima haijaketi kwa ajili ya chakula cha pamoja. Haikuchukua muda mrefu, watoto walioga wakaaga kwenda kupumzika. Baba aliwabeba akawapeleka mpaka chumbani.

Aliwabembeleza kwa kuwasomea kitabu cha hadithi, wakalala. Aliwatengenezea shuka vema, akawabusu kwenye mapaji yao ya uso kisha akazima taa na kutoka humo ndani. Sasa ukabakia wasaa wake na mkewe.

Kwa muda wote hakuwa amebadili hata nguo alotoka nayo kazini.

"Umekumbuka kuwapatia dozi yao ya kila siku?" Bryson aliuliza akiwa anatembea na mkewe koridoni kuelekea sebuleni.

"Naanzaje kusahau, Bryson," akajibu mkewe akimsogelea karibu. "Unajua kabisa dozi hiyo ndo' maisha yao. Naikumbuka kuliko kula yangu."

Alimbusu mumewe kwa muda kidogo kisha wakaachana wakitazama kwa mahaba. Mke aliegemea ukutani wakati mume akijigemezea kwake.

"Vipi leo usiku nitakupata?" Mke alinong'ona. Hata kama mwanamke huyu asingesema jambo, tayari macho yake yalishaeleza kila kitu. Aliufungua tu mdomo kuthibitisha kile alichojiskia, na mumewe alilitambua hilo.

"Unataka kuwatafutia kina Cecy wadogo zao?" Bryson aliuliza kwa chini.

"Natamani ningekuwa na uwezo huo, Bryson." Ghafla uso wa mwanamke ulinywea. Rangi yake ya mahaba iliyokua imemea usoni iligeuka kuwa nyeusi ya msiba.

"Samahani, kipenzi. Sikulenga kukuumiza." Bryson alikumbatia mkewe kwa kumfariji. "Hawa tulionao wanatosha. Usijihisi mkosefu."

Alimtazama mkewe machoni akamwambia akiwa anatabasamu.

"Kwanza nina habari njema sana. Haustahili kuwa na huzuni kabisa!"

"Habari gani hiyo?" Mke akauliza. Alishindwa kujizuia, akatabasamu. Macho yake yalirudi nuruni ghafla.

Mambo yalikuwa hivyo mazuri mpaka pale ambapo Bryson alijikuta mpweke baada ya mkewe kulala.

Majira ilikuwa ni saa sita na madakika yake usiku, muda muafaka na tulivu kwake kufanya kazi aliyokuwa ameidhamiria.

Kama ilivyo kawaida, aliiwasha runinga isiyokuwa na sauti kwaajili ya kampani kisha akaiweka tarakilishi yake mezani pamoja na pakti ya Marlboro yenye sigara tatu tu.

Alikuwa amevalia bukta pekee. Kifua chake kikiachwa wazi. Vinyweleo vimesimama kama antena.

Akaiwasha sigara yake na kupiga mikupuo miwili kwanza mikubwa kuweka akili sawa ndipo akaiwasha tarakilishi yake apate kufanya kazi.

Lakini ngoja ...

Ah - ah ...

Kuna jambo alilikumbuka ...

Hapana ...

Mmh ...

Alisimama upesi akapapasa bukta yake. Alisahau kabisa kuwa bukta ile haikuwa na mifuko. Haraka alizirejea nguo zake alizotokanazo kazini, nazo akazipapasa kila pahala.

Hapana. Hapana. Hapana. Alijisema moyoni.

Alijaribu kutazama kila alipopafikiria, lakini kote huko hakuona anachotafuta.

Kote huko hakuona 'Flash drive' aliyopewa na Ferdinand akainakili.

Kidogo kidogo nyayo za miguu yake zikaanza kuwa za baridi.


***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA


Na Steve B.S.M


Sehemu ya Tatu


"Mitchelle! ... Hey! ... Mitchelle! ... Kimbia! ... Kimbia Mitchelle, kimbia!"

Mitchelle alijaribu kunyanyuka. Mwili wake ulikuwa mzito. Viungo vyake vilikuwa vinauma. Alitazama mkono wake wa kushoto akaona unatiririka damu nyingi. Ni hapo ndipo akabaini ana jeraha kubwa begani.

Jeraha la risasi.

Alijaribu kuelewa kinachoendelea lakini hakufanikiwa abadani. Alikuwa anasikia sauti nyingi kwa wakati mmoja: huku mitutu ya bunduki ikitapika risasi kwa fujo, kule makelele ya watu wazima wakipayuka mithili ya wendawazimu, hapa kelele kali za magari asiyojua yanaelekea wapi na huku juu ndege zikikatiza karibu kana kwamba zinanyunyuzia dawa kwenye mshamba makubwa ya zabibu.

Ilikuwa ni tafarani!

Akiwa anabung'aa hapo, asijue lipi la kufanya wala wapi pa kukimbilia, alimwona mtu akimjia kwa kasi. Alitambua mtu huyo ni mwanaume kwasababu ya umbo lake lakini hakuweza kumjua ni nani hasa.

Kila alipojitahidi kumtazama usoni hakufanikiwa. Macho yake yalikua yamepooza. Yameishiwa nguvu. Kila alichokiona kilikuwa hafifu.

Alifumba macho kwanguvu. Aliamini pengine yatakuwa sawa akiyafungua. Alipoyafungua alimwona yule mwanaume amemfikia, ameinama akimpa mkono.

"Amka tuondoke!" sauti ilimwamuru. "Haraka, Mitchelle, hatuna muda. Amka, utakufa hapa!"

Mitchelle alijitahidi lakini jitihada zake hazikumridhisha mwanaume yule. Kufumba na kufumbua, alijikuta amenyanyuliwa kama mzigo wa kuni! Aliwekwa begani mwanaume yule akaanza mbio.

Mbio! Mbio! Mbio!

Alitupa miguu yake kwa kasi. Ni kama vile hakuwa amebeba kitu. Alienda kushoto, akarudi kulia. Alienda kulia, akarudi kushoto. Yote katika kukwepa mashambulizi ya risasi.

Mwanaume huyu alikuwa mwepesi ajabu. Na vipi kuhusu nguvu zake? Hakika alikuwa ni shupavu.

Alikimbia kwa kama mita mia mbili bila kupumzika lakini punde hivi, akasimama ghafla!

Ghafla sana.

"Nisamehe, Mitchelle."

Bwana yule alisema kwa utulivu. Sijui aliona nini lakini sauti yake haikuwa na matumaini tena ndani yake. Alisimama kama mshumaa. Mshumaa unaoteketea katika moto.

Haikupita hata sekunde tatu hapo, sauti kubwa ya mlipuko ikaita .. BOOOOOM!! ... Kufumba na kufumbua, yeye na Mitchelle walipotea katika vumbi na moshi mzito.

Moshi huo ulitawala kwa kama dakika tatu hivi kabla ya taswira ya Mitchelle, amelala kifudifudi, kuonekana kwa mbali, hatua kama thelathini toka eneo la tukio. Ni bayana alikuwa ametupwa na nguvu ya bomu. Kheri ni kwamba alikuwa mzima wa mwili.

Upande wa pili, yule mwanaume hakuwa amebakia kitu. Ni vipande vya nyama ndo' vilisambaa huku na kule. Kama ungevikusanya vipande hivi visingetoshea hata kwenye rambo.

Masikini alikanyaga mtaro wa mabomu bila kujua.

Mitchelle alinyanyua uso wake uliojawa udongo na vumbi, akatazama. Hakuona kitu. Ni kama vile mambo yalikuwa yanatukia ndani ya mvuke hivi.

Ingawa macho hayo yalimpatia tabu ya kuona, alifahamu fika kilichotokea. Yule mwanaume aliyemsaidia hakuwapo tena. Mlipuko ule ulienda naye.

Alilia kwa uchungu sana.

Alipiga yowe aliloamka nalo kitandani alipokuwa amejilaza kwa masaa kadhaa tangu alipodungwa sindano na Ferdinand.

Alitazama kushoto na kulia. Alikuwa anahema kwanguvu. Alizika uso wake kwenye viganja vyake vidogo akijaribu kufikiria kile alichokiota, kidogo mlango ukafunguliwa.

Alikuwa ni Jennifer, mwanamama mfanyakazi. Aliwasha taa upesi, kwa kupiga makofi mawili tu, kisha akamsogelea Mitchelle kitandani.

Japo mwanga wa taa hii ya chumbani ulikuwa ni hafifu, ulitosha kabisa kuonyesha uzuri uliokuwemo humu ndani. Kitanda kikubwa cha glasi, godoro lenye inchi zake za kutosha, shuka jeupe na mito laini ni baadhi tu ya vingi vilivyokuwamo.

Jennifer alipanda kitandani akaketi kando ya Mitchelle.

"Nini shida?"

Alimshika mwanamke huyo kama mwanaye, akamlaza kifuani kwake.

"Umewaota tena? ... Pole. Usijali, mimi nipo hapa ... usijali, Mitchelle."

Mitchelle alitanua mikono yake akamkumbatia mwanamama Jennifer. Macho yake yalilenga chozi. Alipojibandua kwenye mwili wa mwanake huyo, alivuta vikamasi vyepesi puani akauliza, "Nimelala kwa muda gani?"

"Si muda mrefu sana," Jennifer akamjibu. Alikuwa anamtazama Mitchelle kwa macho ya mama zaidi kuliko yale ya mfanyakazi kwa 'boss' wake.

Mitchelle alisukumia shuka kando akatoka kitandani. Hakutaka kulala tena. Alitwaa taulo jeupe toka kabatini, akamtazama Jennifer ambaye bado alikuwa kitandani, akamuuliza,

"Ferdinand alikuja tena?"

"Hapana," Jennifer alijibu akitikisa kichwa. Alinyanyuka toka kitandani akaongezea, "Alipiga simu majira fulani kuulizia hali yako, nikamwambia umelala."

"Ok. Mimi natoka, siwezi kulala tena. Usingizi wote umeniisha. Tafadhali niandalie nguo yangu ya kutokea."

"Haina shida."

"Nguo ya usiku tafadhali."

"Sawa."

Jennifer alielekea kabatini kutimiza zoezi aliloagizwa wakati Mitchelle akijivesha taulo baada ya kuvua nguo yake ya kulalia ili apate kuoga.

Aliingia kwenye bafu lake kubwa, akaenda mahali mahususi kwa ajili ya 'shower'. Hapo akatundika taulo lake kando kisha taratibu akaanza kuupooza mwili wake na maji ya baridi ili kuondoa mang'amung'amu ya usingizi.

Mwili wake mwembamba ulikuwa na uwiano sahihi katika kila upande. Wakati huu akiwa anaoga ilikuwa ni fursa nzuri ya kushuhudia hilo. Alielekezea sura yake bombani maji yakitiririka toka kichwani mpaka miguuni.

Alishika nywele zake nyeusi, ndefu kwa wastani, akazipindulia begani kuja kifuani. Hapo akaaacha shingo yake kwa nyuma ikiwa wazi.

Chini kidogo ya shingo hiyo, kwenye makutano ya shingo na mgongo, kulikuwa na 'tattoo' ndogo ya mistari midogomidogo iliyosimama. Chini ya mistari hiyo kulikuwa na tarakimu kadhaa na herufi tatu;

00/89/31/12-CKM.


***


Masaa Mawili Mbele: Eneo la Manhattan, mbele ya baa ya kisasa ya The DL.



Mitchelle alishuka toka kwenye 'uber' iliyomleta punde tu baada ya kufanya malipo. Mara nyingi anapotoka nyakati za usiku, hupendelea kutumia usafiri wa kukodi kama wa namna hii.

Alikuwa amevalia suruali nyeusi ya jeans iliyombana, koti jeusi la ngozi lenye kola ndefu, ndani blauzi nyekundu yenye kumetameta, kapelo nyeusi na viatu vilivyopanda karibia na magoti.

Alitembea kufuata milango mipana ya kioo ya baa ya The DL huku akibofya simu yake kubwa. Alipoingia ndani alinyookea kwenye viti vinavyowakarimu wageni, haswa wanywaji, hapo akakutana na Ferdinand.

Mazingira ya hapa yalikuwa ni hafifu sana kwa mwanga. Inajulikana walevi hawapendi mwanga mkali wakiwa kwenye starehe zao hivyo taa zilizokuwepo hapa zilikuwa ni zile za urembo tu, nyekundu na bluu, zakuwafanya watu wasigongane kwa kutoonana kabisa.

"Umejuaje nipo hapa?" Ferdinand aliuliza baada ya kushusha glasi yake ya kinywaji chini. Mezani kulikuwa na chupa kubwa yenye kinywaji robo ujazo.

"Kwani wewe ni mgeni kwangu, Ferdy?" Mitchelle aliuliza. Kidogo naye aliletewa ulabu akaungana na Ferdinand kwenye unywaji.

"Nimeshindwa kulala. Kama ningebaki nyumbani huu usiku ungekuwa mrefu sana."

"Umeota tena?"

"Ndio."

"Ilikuwa mbaya kiasi gani?"

"Mbaya tu."

"Pengine unafikiria sana yaliyopita. Kuna muda inabidi uache yaende, Mitchelle. Ukifikiria sana, hautapata wasaa wa ya sasa."

Mitchelle alinyamaza. Aliacha kwanza mdomo wake unywe na kichwa chake kifikiri. Kwa muda wa kama dakika sita hivi kukawa na ukimya.

Ferdinand alimaliza ile chupa yame ya ulabu, akaagiza aletewe nyingine.

"Ferdy, hiyo ni ya ngapi? Huoni inatosha sasa?"

"Ndo' kwanza ya pili," alijibu mwanaume huyo akimtazama Mitchelle. Uso wake ulikuwa mchangamfu, macho yake yanang'aa na mwaga mwekundu wa baa.

Mitchelle hakutaka kubishana naye. Aliamua kuamini kile alichoambiwa. Lakini akifanya hilo kwa tahadhari.

"Vipi kwenye uchapishaji, kazi imeshaanza?"

"Ndio. Nilivyokuacha tu nyumbani nilipeleka ule mzigo akaanze nao ... lakini, Mitchelle?"

"Nini?"

"Kwanini uliamua hili jambo? Huoni ni hatarishi?"

"Jambo gani?"

"La kupeleka taarifa kama hizo sehemu kama ile?"

"Ferdinand, kanuni ya kuficha kitu inasemaje? ... ficha pale ambapo hamna anayepadhania. Unadhani kila kitu kikienda kombo, kuna sehemu yoyote ndani ya makazi yangu itakuwa salama? ... nilihitaji sehemu na watu ambao hawatafikiriwa KABISA hata pale adui yangu atakapowaza mara mia moja. Vitu hivyo vinapatikana nje ya mduara wangu wa maisha ya kila siku."

"Lakini mimi huwa naenda pale Olympus?"

"Ndiyo maana nilikuambia utafute njia mbadala. Weka mzigo mahali, mhusika aupitie. Makutano ya mara kwa mara yanaweza leta shuku."

"Lakini vipi kama taarifa hizi tungezitunza kwenye vyombo alafu tukavifukia ama kuviweka mahali pa mbali ambapo mtu hawezi fika kwa urahisi mfano kama vile visiwani huko au baharini au ..."

"Ferdy, umelewa?"

"Mie? Akha!"

"Mara ngapi tushawahi ongea hili? Hii ndo njia rahisi na salama ya kunakilisha taarifa nyeti. Haiwezi kufuatiliwa wala kuathiriwa na virusi maalum waliotengenezwa. Kwa muda wote huo Olympus itakuwa ni ghala letu la siri lisilodhaniwa, zoezi likikamilika tutakua tuna data kwenye kila mfumo wa uwasilishaji na kwenye lugha tatu za dunia. Hapo ndo tutaanza mapambano rasmi."

"Vipi kuhusu wale watu wa Olympus na unyeti wa taarifa zetu?"

"Unamaanisha Bryson?"

"Ndio."

"Ferdy, ni wewe ndiye uliyefanya utafiti wa kina kumhusu Bryson na kampuni yake. Sivyo?"

"Ndio, najua kila kitu kumhusu yeye. Njia anayopitia kutokea na kurudia nyumbani, anakula nini asubuhi mpaka jioni, mahali anapoishi, madeni aliyonayo, anapofanyia kazi mkewe, anapoishi mama yake, anapopenda kwenda kustarehe, mpaka hospitali na dozi ambayo watoto wake wanaitumia. Najua kila kitu."

"Na hivyo vyote unavyovijua ndo' dhamana ya kazi yetu. Hakikisha anajua hilo. Na punde kazi yetu itakapokwisha, kila mmoja aliyehusika nayo hakikisha anaiga dunia."

"Usijali."

Ferdinand alimalizia kisha akainyanyua chupa yake ya kilevi na kuinywa kwa mtindo wa tarumbeta. Aliona glasi inamchelewesha. Alibeua mara tatu alafu akanyanyuka.

"Naenda maliwato, nakuja," aliaga akaenda zake.

Mitchelle akamsindikiza kwa macho yake madogo mpaka alipotokomea. Kichwani mwake kuna mambo kadhaa alikuwa anayawazua.

"Sio kila kitu ni cha kujua kwa undani, Ferdy," alisema kifuani mwake. "Mengine acha yawe surprise. Maisha bila surprise yanaboa."

Alitabasamu mwenyewe mithili ya mtu anayejitazama kwenye kioo kisha akanyanyua glasi yake ya kilevi kikali akalipasha koo.

Kwasababu ya upweke huu wa dakika kadhaa, alipiga mikupuo mingi ya kileo. Alipokunywa kama glasi nne hivi bila ya Ferdinand kurudi, akapata walakini.

Alitazama njia aliyoendea nayo mwanaume huyo lakini hakumwona. Ni watu wengine tu ndo' walikuwa wanapita huku na kule wakiendelea na yao.

Alimalizia kinywaji chake akasimama. Kabla hajaenda popote, akaita 'uber' kisha akaiweka simu yake mfukoni.


--


Choo cha wanaume


Mlangoni kulikuwa na kibao cheupe kilichoandikwa 'occupied' kumaanisha kuna mtu ndani, lakini kama ungelisimama hapo, kwa mbali, ungelisikia maongezi yanayoendelea ni ya zaidi ya mtu mmoja. Moja ya sauti ilikuwa ni ya Ferdinand.

"Hauna mzigo mwingine?" Ferdinand aliuliza. Macho yake yalikuwa yamelegea mno. Pombe sasa ilikuwa imefika penyewe.

Mbele yake walikuwa wamesimama wanaume wawili waliovalia suti bubu; koti tu na mashati tofauti ndani. Mmoja alikuwa mwenye upara na masharubu makubwa, mwili wake mpana. Mwingine alikuwa mwembamba mfupi, nywele nyingi nyeusi, mwenye kujawa na michoro mingi shingoni.

Yule mwenye upara aliguna kwa kebehi.

Alimtazama Ferdinand kwa macho ya dharau kisha akamtazama mwenzake wakatabasamu pamoja.

"Toa pesa. Si unajua huu mzigo ni gharama kubwa?"

"Si nimeshawapa?" Ferdinand alifoka. Mbali na kwamba macho yake yalikuwa legevu, mwili wake haukuwa na nguvu tena. Alisimama akiyumba, mdomo ameuachama.

"Mnataka mamilioni ama? Enh! Mnataka mamilioniii?"

Puani, upande wake wa kushoto, alikuwa na mabakimabaki ya unga uliochora alama ya 'nike'. Sasa ilikuwa bayana kumbe mbali na pombe alokunywa, alikuwa pia yupo kwenye ulevi mwingine.

"Toa pesa. Kama huna acha kutusumbua, sawa?" Yule mwanaume mwembamba alifoka akimnyooshea kidole. "Hatuna muda wa kupoteza hapa. Ni aidha tufanye biashara au twende zetu. Tuna wateja wanatungoja!"

Yule bwana mwenye upara alitoa kifuko kidogo cha 'nylon' chenye unga mweupe, akamwonyeshea Ferdinand bila kusema jambo. Alitabasamu tu akiyakodoa macho. Aliutikisatikisa mkono wake wenye dawa kama bwana amfanyiavyo mbwa wake.

Ferdinand alitazama mkono huo kwa hamu. Alijipapasapapasa mifukoni lakini hakuwa na kitu tena. Pesa yote imeshakwisha.

Hawajakaa sawa, mlango ukagongwa kwanguvu, BAM-BAM-BAM! Wote wakatazama kwa hamaki.

"Huoni kuna watu!" Bwana upara alifokea mlangoni. "Nenda vyoo vingine kabla sijaja hapo kukung'oa meno!"

Ajabu mlango uligongwa tena. Mara hii aliyekuwa anagonga alifanya hivyo mfululizo bila kukoma!

Bwana upara alimtazama mwenzie akampa ishara ya kichwa. Yule mwenzake akasonga mbele kuufuata mlango. Aliposhika tu kitasa, hakujua nini kilichojiri. Kitu pekee alichokumbuka ni kuruka juu baada ya kugongwa na kitu kizito kifuani.

Alijitambua yuko chini hajiwezi. Kichwa chake kinavuja damu.

"Alaa!!" Bwana upara alistaajabu. Aliyatumbua macho yake haswa. Alirudisha macho yake mlangoni akamwona mwanamke akiwa amesimama papo. Alikuwa ni Mitchelle.

Mlango ulibakia nusu, kipande kingine kinaning'inia kando.

Ilikuwa ni ajabu kuona mwanamke, tena wa umbo lile dogo, ndiye aliyefanya hayo. Hata bwana upara hakuamini hilo. Alidhani pengine kuna watu wa ziada pamoja naye lakini haikuwa hivyo.

Kilichofuata baada ya dakika tano ni yeye kuungana na mwenzie chini. Hajielewi. Kichwa chake kimekuwa chekundu.

"Ferdinand, tulikubaliana nini kuhusu madawa?" Mitchelle aliuliza kwa ukali. Macho yake madogo yalimezwa na ndita za usoni. Kwa muda wote huo Ferdinand alikuwa amesimama akinyoosha mikono juu kama mtu aliyenyooshewa bunduki.

Kwa kumtazama tu, ungembaini sio mzima.

Muda mfupi mbele Mitchelle na Ferdinand wakawa wako ndani ya 'uber' wakielekea nyumbani. Sura ya Mitchelle ilikuwa imefura. Alikuwa akitazama nje kupitia dirishani.
Ferdinand yeye hakuwa na hili wala lile kwani ufahamu haukuwa pamoja naye.

Ndani ya muda mfupi polisi wakawa wamefika katika eneo la The DL. Magari mawili yanayowaka taa nyekundu na bluu yalitema polisi watatu kwa idadi, wakazama ndani kuhakiki taarifa walizopewa kuhusu mashambulizi.

Muda si mrefu polisi hao waliungana na polisi wengine wa nyongeza walioambatana na wanakitengo cha habari walioharakisha kuchukua taarifa za picha mnato kwaajili ya kusaidia upelelezi.

Miongoni mwa polisi hao waliofika hapa, alikuwa ni bwana huyu mrefu, mwili mpana, aliyevalia shati maridadi jeupe la mistari, kachomekea vema ndani ya suruali yake nyeusi na mgongo wake umefunikwa na koti refu kwa wastani, rangi ya kahawia iliyokoza, kifuani amening'iniza beji ya nembo ya polisi kilichoandikwa:

NEW YORK POLICE DEPARTMENT (KITENGO CHA POLISI NEW YORK)

DETECTIVE (MPELELEZI)

005789.

Tayari eneo la tukio lilishazungushiwa utepe wa polisi. Hakuruhusiwa raia kuingia eneo hilo isipokuwa wanausalama pekee.

Bwana huyo alisogea eneo hilo kwa hatua zake za wima. Alingia moja kwa moja mpaka maafa yalipojiri, akatazama miili miwili iliyokuwa imelala mfu.

Aliikagua miili hiyo kwa kitambo kidogo kisha akamuuliza moja wa mapolisi waliowahi eneo la tukio.

"Umesema ni mtu mmoja ameyafanya haya?"

"Ndio, afande. Ni mwanamke mmoja."

"Mwanamke?"

"Ndio. Kamera za koridoni zilimwonyesha mtu mwenye umbo la kike akija upande huu wa vyoo."

"Zimekamata sura yake?"

"Hapana. Alikuwa amevaa kofia."

"Usafiri?"

"Hakuja na usafiri. Kamera zinamwonyesha aliingia na gari ya kukodi."

"Mmelitambua gari hilo?"

"Hapana. Alishukia mbali kwa kamera kukamata picha vema."

"Hapana!" Bwana yule aling'aka akitoka katika eneo la tukio. Polisi aliyekuwa anaongea naye akamfuata nyuma kama mkia. "Haiwezekani, lazima kuwe na kitu!"

Walifika nje, hapo wakasimama bwana yule akiyakagua mazingira.

"Shida mwanga ulikuwa hafifu sana alipokaa," aliongezea yule polisi. "Ni ngumu sana kuona sura ya mtu vizuri, na kwa vielelezo vile inaonekana ulikuwa ni ugomvi wa madawa ya kulevya."

Mara yule bwana mpelelezi alinyooshea kidole barabarani. "Kule hakuna kamera iliyonasa gari hilo?"

"Hapana, mkuu," polisi aliwahi kujibu. "Kamera inayofanya kazi ipo kilomita tatu kutoka hapa. Kutambua gari itachukua muda kidogo."

"Shit!"

"Lakini kuna mtu alinaswa na kamera."

Bwana mpelelezi alimtazama mwenziwe kwa macho ya hamu, akamuuliza;

"Nani huyo?"

"Mwanaume fulani aliyekuwa na mwanamke huyo."

"Kwanini hukuniambia mapema yote?"

"Niliona ina msaada kidogo."

"Unamaanisha nini?"

"Picha ya bwana huyo ilishatumwa makao kwaajili ya utambuzi lakini hamna kilichopatikana."

"Kivipi?"

"Picha yake imeingizwa katika mfumo wa kutambua vitambulisho vya taifa na vyote vile vilivyo rasmi lakini hakuna rekodi yeyote ile inayomhusu. Hakuna taarifa yake yoyote rasmi. Si anwani, taaluma, kazi wala miamala!"

Bwana mpelelezi akatabasamu asijue hata cha kufurahisha ni nini. Alitafakari hapo kwa muda kidogo kabla hajaamua kurudi tena ndani. Kule sehemu lilipojiri tukio.

"Naomba kila kitu! .. kila kitu kinachohusu kesi hii!"

Alipayuka.


**


Queens, New York. Olympus Printing Press


Saa nne asubuhi.


"Hildaa!" Sauti ya Bryson iliitia ndani. "Njoo upesi, tafadhali."

Hilda aliyekuwa amekalia kazi yake ya kuchapa alinyanyuka upesi kwenda kuonana na mkuu wake wa kazi. Kama ilivyo ada, alikuwa nadhifu kwa sketi zake fupi na viatu vyake visivyo na purukushani.

Kwa ufupi mwanamke huyo alishajijua aende vipi na mwili wake wenye utajiri wa nyama. Kipi aonyeshe, kipi afiche. Kipi avae, kipi aache.

Aliingia ofisini akasimama kwa nidhamu kabla hajaruhusiwa kuketi kitini.

Bryson alikuwa amevalia shati alilofungua vifungo viwili vya juu. Uso wake ulikuwa mzito na macho yake mekundu kama nyanya zilizooza. Kila saa alikuwa akipiga mihayo akitazama kwa huruma.

Hilda alimtazama 'boss' wake namna alivyokuwa anapangilia mafaili kivivu. Alitamani kumuuliza nini kimemsibu lakini alikosa pa kuanzia.

"Hilda, katika siku ambazo nimeteseka, jana ilikuwa mojawapo!" Bryson aliongea kidogo kisha akafikicha macho yake. Yalikuwa yanamuuma kwa kujawa na usingizi.

"Usiku mzima sijalala kabisa, nipo huku na kule natafuta nilipoweka flash ya watu ya kazi. Aisee! Mungu tu ndo' anajua."

"Pole, boss. Kwani ilikuaje?" Hilda alipata pa kuanzia kuikata kiu yake.

"We acha tu! Hizi sigara zitakuja kuniua siku. Kutafuta koooote hukoo, unajua nikaja kuipatia wapi? ... nashangaa natoa sigara nivute, naiona kwenye pakti. Sijui hata ilifikaje? Yani sijui!'

Hilda alitamani kweli kutabasamu lakini alivumilia.

"Pole sana, boss."

"Laiti nisingeipata," Bryson aliendeleza maneno, "sijui ningekuja kuwaambia nini wale mabwana?"

"Ni wale ulioniambia?"

"Ndio. Yani wale sitaki nao mchezo kabisaa. Anyways, shika hii flash, sijaifungua hata kidogo. Najua hamna kazi nitakayoifanya humo. Nimechoka mno. Sasa fanya kuandika yaliyomo humo, sawa? ... achana na kazi zote fanya hiyo!"

Hilda alipokea flash akasimama.

"Utakapomaliza, utanambia. Pesa yako nzuri sana ipo. We hakikisha unaifanya kazi kwa stadi na siri."

"Haina shida, boss."

Hilda alitoka akaekelekea kwenye kiti chake. Cha kwanza kabisa alichomeka flash aliyopewa, akaifungua. Mbali na kwamba ilikuwa ni kazi, alikuwa na hamu kubwa ya kujua yaliyomo ndani.

Taarifa alizopewa na boss wake kuhusu kazi hiyo hakika zilimpatia hari kubwa ya udadisi. Kwake ilikuwa ni kazi ya kipekee.

Alitengenezea miwani, akatumbua macho akisoma kila jambo aliloliona. Taratibu na kwa umakini. Akili yake yote ilizamia humo. Hakusikia wala kuona kingine chochote nje ya tarakilishi ya kazi yake. Alikuwa yupo kwenye ulimwengu wa peke yake.

Lakini ghafla alisikia sauti inamnong'oneza;

"Ni ... nni ...n ... nini hiki, Hilda?"

Alikurupuka mithili ya mbwa aliyeona chatu! Kutazama ni Richie. Upesi akafunga tarakilishi yake.

"Umeona chochote?" Alimuuliza Richie akiwa ameyatoa macho yake ndani ya miwani.

Richie akatikisa kichwa kukubali.

"Ndio."


***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.


Na Steve B.S.M


Sehemu ya Nne




Mgahawani: Mita chache toka ofisi ya uchapishaji ya Olympus.

Majira ya saa saba na robo mchana.


Hilda alivuta juisi kwa mrija wake huku akimtazama Richie aliyekaa mkabala naye.

Mezani kulikuwa na sahani mbili za chakula, lakini ya Hilda haikuwa imeguswa mara nyingi.

Tangu walipoagiza, ni Richie pekee ndo' alikuwa anakula. Hilda yeye aliishia kunywa tu, tena kwa kugusagusa.

Hakuwa na hamu. Utumbo wake si kwamba ulijawa na chakula, bali hofu.

Ni siku yake ya kwanza katika kazi hii na tayari ameshayakoroga.

Alimtazama Richie kwa macho ya mashaka.

Alitafakari ni namna gani anaweza kumpotosha mwanaume huyo yeye akabaki salama lakini kila alichokifikiria aliona kama kinagoma.

Uongo ni talanta.

Akanyonya tena juisi yake.

"Richie!"

"Mmh!"

Richie aliitikia akiwa na chakula mdomoni.

Hilda alimtazama mwanaume huyo akaona ni busara angoje ameze.

"Niambie umeona nini?"

"Kila kitu!"

"Ushanambia kila kitu, nataka kujua ni kitu gani. ulichoona."

"Nimeona mi ... mi ... maalama na mi ... mi ... mmm ... mi .. maelezo ya kisayansi," Richie alijibu pasipo kumtazama Hilda usoni, "Nimeona michoro na mar ...rrr .... ra .. rangirangi mee ... ee .. engi!"

"Umeyaelewa?"

"Hapana!"

Hilda alihisi moyo wake umepooza baada ya kusikia hilo.

Alishusha pumzi ndefu.

Macho yake yaling'aa kama anga jeusi lililojawa na nyota.

Muda huu akapata hamu ya kula.

"Laa ..kkk ... kini nnn ... nimm ... nime .... nimepatwa na maswali mengi!" Richie aliweka neno. Saa hii alikuwa anamtazama Hilda usoni kwa macho yake makubwa.

"Maswali gani hayo?"

Hilda aliuliza upesi.

Richie alivuta pumzi ndefu akasogezea kando sahani yake ya chakula alomaliza kuifanyia kazi, kisha akamtazama Hilda.

Macho yake yalionyesha dhamira dhahiri.

Kwa kigugumizi chake alipambana kueleza yale yaliyokuwamo kichwani mwake, moja baada ya jingine.

Mosi, kampuni yao, kwa mara ya kwanza, kuchapisha kazi za kisayansi mbali na hadithi na bayografia.

Pili, kutokupewa taarifa yoyote kuhusu kinachoendelea ingali yeye ni mhariri mkuu msaidizi wa kampuni.

Ni bayana, kuna jambo.

Hiki kitendo cha Hilda kumtoa 'lunch' kilizidi kusakafia hoja yake.

"Hivi uko serious?" Hilda aliuliza.

Alimtazama Richie usoni na ni kweli bwana huyo hakuonyesha masikhara yoyote.

Akacheka.

Lakini kiongo.

"Richie, ebu acha kutengeneza mitumbwi na mabwawa kichwani mwako. Hayo unayoyawaza ni tofauti kabisa na uhalisia. Kile ninachochapa si kazi ya kampuni bali kazi yangu binafsi, ni jaribio la mdogo wangu anayesoma chuo."

"Kweli?"

"Ndio. Ni jaribio! Ndo' maana sikutaka mtu yeyote aone."

Richie hakuamini.

Alimweleza Hilda shaka lake kuwa alitoka ofisini kwa mkurugenzi ndipo akaianza kazi hiyo maramoja.

Kwenye hilo Hilda alikataa kuwapo kwa mahusiano. Alijitetea kuwa aliongea mengine na mkurugenzi.

Mengine ambayo ni ya kikazi mbali na mambo yake binafsi.

Lakini kuna kitu ambacho Hilda hakuwa anakifahamu ...


Siku ya Nyuma.


"Richie, ina maana hujasema kitu? Sasa kwanini uliniambia nikupe mafaili uende wewe?"

Richie alikalia kimya.

"Sasa tutaishi hivi mpaka lini? ... mwezi wa ngapi huu hatupati mshahara na yeye amekalia kimya? ... Aaaagh! Aaaagh!"

Ghafla Hilda alinyamaza akitazama nyuma ya Richie.

Uso wake ulipaliwa na hofu iliyokuwa wazi machoni mwake.

Richie aligeuka kutazama kinachosibu, akakutana na uso wa mkurugenzi Bryson mlangoni.

"Nakuhitaji mara moja."

Richie aligeuka akamtazama Hilda ambaye alilengwa na ujumbe wa mkurugenzi.

Aliona namna hofu ilivyomkaba mwanamke huyo, mwili wake mnene unamtetemeka.

Alitamani kusema jambo lakini alihofia huenda akasikika.

Hilda alipomtazama, alikwepesha macho yake upesi kisha akaenda kuketi kwenye nafasi yake.

Kwa macho yake alimshuhudia Hilda akiingia ofisini mwa Bryson na kisha mlango ukafungwa.

"Mungu wangu!" Alisema akifunika kinywa.

Aliamini amemwingiza Hilda matatani kwa yale waliyokuwa wanajadiliana. Laiti angelifanya yale waliyokubaliana, ya kwamba amkumbushe mkurugenzi kuhusu mishahara yao, basi yasingefikia hapa.

Alijihisi mkosefu.

Akiwa anawazua hapo, alijikuta anapatwa na hamu ya kujua matokeo ya makosa alofanya.

Upesi alinyanyuka akaendea mlango. Hapo akasimama, ametega sikio, akisikiliza kwa umakini yanayoendelea ndani.

Alichokisikia kikawa tofauti na alivyokuwa anadhania.

Kumbe yalikuwa ni maagano na si malumbano.

Aliketi na hata akaongea na Hilda akitegemea mwanamke huyo atasema jambo kwake lakini haikuwa hivyo.

Alingoja mpaka muda wa kutoka kazini ukafika.

Aliamini pengine wakiwa barabarani watakuwa na uhuru unaotosha, Hilda angemshirikisha kwenye swala lake, lakini jambo hilo haikutokea abadani.

Hilda alimuaga akaenda zake. Akabaki anamtazama mwanamke huyo akiyoyoma.

Aliwaza.

Pengine Hilda hakuwa anamchukulia kama yeye amchukuliavyo.

Kwake Hilda alikuwa ana nafasi maalum mbali na kwamba ni mfanyakazi mwenzake.

Laiti Hilda angekuwa naye anahisi hivyo, asingeweza kumficha jambo.

Swala hilo lilimuumiza moyoni.

Hilda alitokomea kwenye macho yake akienda zake lakini kichwani alibakia.

Aligeuka na kushika njia ya kuelekea yalipo makazi yake akiwaza na kuwazua sana.

Aliikumbuka ile kauli ya Bryson juu ya gharama ambazo Hilda anapaswa kulipa kwasababu ya kazi waliyopeana.

Kauli hiyo ilimvuruga kabisa.


Masaa ya Nyuma Kidogo Siku ya Leo


"Hildaa! ... Njoo upesi tafadhali!"

Ilikuwa ni sauti ya maagizo toka kwenye ofisi ya Bryson.

Richie aliyekuwa ameketi kwa utulivu kwenye dawati lake, punde aliposikia sauti hiyo, alirusha macho yake makubwa kutazama uso wa Hilda.

Kulikuwa na jambo tofauti.

Aliligundua hilo.

Kwa mara ya kwanza kati ya nyingi, Hilda hakuwa amenuna kabisa aliposikia anaitwa na mkurugenzi. Na wala hakulaani.

Hii si kawaida.

Kama haitoshi alichangamsha miguu yake minene akielekea huko.

Katika hali isiyoeleweka, Richie aliumia moyo kuona Hilda anaharakia huko.

Upesi alinyanyuka, punde baada ya mlango kufungwa, akasogelea na kutega sikio mlangoni.

Alisikia kila jambo, kila agizo.

Alirudi kwenye kiti chake punde aliposikia Hilda anaaga ndani.

Alimtazama mwanamke huyo kwa umakini akiwa anatembea. Mkononi alikuwa na flash aliyoichomeka kwenye kifaa chake punde tu alipoketi.

Kwa wakati wote huo akiwa anafanya kazi, Richie akawa anamtazama kwa umakini.

Alimwona mwanamke huyo amezubaa. Alitamani kujua kilichomteka na ndipo alinyanyuka kwenda kuzuru.

Mpaka anafika, alibaini kuwa Hilda hakuwa na habari kabisa kuhusu ujio wake. Akili yake ilikuwa imepotea na kulowea kwenye kioo cha tarakilishi.

Hapo ndo' akatazama yanayofanyika.


Muda wa Sasa: Mgahawani.


"Nadhani umenielewa, Richie," alisema Hilda akiwa ananyanyuka. Alishamaliza chakula na juisi yake.

Kitendo cha kubaini kuwa Richie hakuwa na madhara, na pengine angeamini uongo wake, kulimrejeshea 'appetite' yake ya kula ya kila siku.

Alitamani aongeze sahani nyingine lakini muda ulishawatupa mkono, walihitajika kurudi kazini. Alichofanya ni kuagiza juisi ya baridi apate kwenda nayo.

Mwili haujengwi kwa tofali na mbao.

Lakini kwa Richie, moyo wake ulikuwa umezizima.

Aliumia.

Alidhani pengine Hilda angesadiki baada ya kumkuta na nyama mkononi lakini haikuwa hivyo.

Alijiona amepoteza.

Ingawa aliongozana na Hilda kurudi ofisini, alijihisi yu mpweke.

Aliridhia na nafsi yake kuwa yampasa afanye jambo, lakini bado hakulijua.

Alishindwa pambano ila si vita.

Aliamini vivyo.


***


Halletts Point Apartment: New York.


Saa nane na dakika zake mchana.


Mitchelle alisimama kando ya dirisha kubwa la kioo lililopo sebuleni mwake akiwa anatazama nje.

Dirisha hili, kwa juu, lilikuwa linatazamana na maghorofa lukuki ya New York.

Lilikuwa limekaa juu sana na mahali pema kabisa kufurahia mionekano tofautitofauti ya jiji hili maridhawa.

Mitchelle alikuwa amesimama hapo, macho yake yanaangaza, akiwa amevalia gauni jepesi rangi ya fedha lililokata mikono yake begani.

Nywele zake zilikuwa huru kama mwili wake mzima. Mbali na viatu vya manyoya, chapa ya Gucci, alivyovaa mguuni, hakujiveka vingine. Si mkufu, bangili, pete wala saa.

Ni mkononi alikuwa ameshikilia glasi yenye mvinyo mwekundu.

Glasi aliyokuwa anaipeleka mdomoni taratibu kujipa 'kampani' wakati akitazama uzuri wa jiji hili na kutafakari yanayomsibu.

Mandhari haya tulivu, yaliyokuwa yanafurahiwa na Mitchelle, yaliharibiwa na ujio wa Jennifer.

Mwanamama huyo aliyekuwa ndani ya sare yake ya kila siku, nadhifu yenye rangi za kukoza, alikuwa ameshikilia simu mkononi.

Alimsogelea Mitchelle akampa ishara kuwa simu yake inaita.

"Nani?"

"Taiwan," Jennifer alijibu kwa kumpa ishara.

Mitchelle alipokea simu akaiweka sikioni

"Ulikuwa wapi nilivyokupigia asubuhi?"

"Samahani, kuna shughuli nilikuwa nafanya nikawa mbali na simu."

Sauti iliyomjibu ilikuwa ni ya mwanaume. Lugha waliyoitumia ilikuwa ni ya kichina (kimandarin).

"Ulifanikiwa?" Mitchelle aliuliza.

"Ndio, madam. Nilifanikisha mapema tu baada ya kunituma. Kika kitu kimeenda sawa."

"Jumla kiasi gani?"

"Dola za kimarekani milioni mbili, nimeingiza kwenye akaunti ya kwanza. Kwenye ya pili nimeingiza milioni tano, jumla milioni saba."

"Vizuri. Maendeleo ya Kiellin na Truce?"

"Hali zao hazijabadilika ... mkuu, nadhani hakuna cha ziada tunachoweza kufanya kwa sasa. Tumetumia pesa nyingi la --"

"Na endelea kutumia!" Mitchelle alikaza sauti akimkatiza Taiwan. "Yakuhusu pesa niachie mimi. Nipo radhi kutumia pesa zote nilizonazo hata ikinibidi. Endelea kutafuta wataalamu zaidi na wape pesa yoyote watakayotaka. Umenielewa?"

"Sawa, boss."

Jennifer aliichukua simu toka kwa Mitchelle, akaifungua na kutoa chip ya mawasiliano, akaitia mdomoni kuitafuna.

Mitchelle alikunywa fundo moja la mvinyo akauliza,

"Vipi maendekea maendeleo ya Ferdinand?"

"Anaendelea vizuri baada ya sindano niliyomdunga," Jennifer alimjibu. Mwanamama huyo alieleza haya yote kwa lugha ya ishara.

Mikono yake na vidole vilienda huku na kule, upesi, kwenye kutengeneza maumbo ya herufi ambayo Mitchelle aliyafafanua vema.

Mikono hii ndo' ilikuwa sauti yake kwenye mazungumzo.

"Naomba ujitahidi kumtazama," Jennifer aliongezea. "Siku ikitokea akazidisha dozi hii ya madawa, tutamkosa kabisa."

"Haitatokea!"

Sauti ya kiume ilipaza.

Waligeuka wakamwona Ferdinand akiwa anakuja mwelekeo wa sebuleni.

Alikuwa amevalia kaushi nyeupe na bukta ya kijani yenye midolimidoli ya 'The Hulk. Macho yake yalikuwa mekundu na yamelegea, uso wake umechachuka kwa usingizi.

Jennifer alimuaga Mitchelle akaenda zake, akawaachia wawili hawa faragha ya kuzungumza.

Mitchelle alimalizia mvinyo wake kisha akaketi pembezoni mwa Ferdinand akiweka glasi mezani.

Aliegesha mguu wake wa kushoto juu ya wa kulia, akamtazama Ferdinand machoni.

"Ferdinand, unajua ulichosababisha?"

"Najua nimekosa, Mitchelle. Nitajirekebisha."

"N'shachoka kauli zako, Ferdy. Ni mara ngapi unaniambia hiyo kauli?"

Ferdinand alifikicha macho yake pasipo kutia neno. Uso wake ulijawa na haya.

"Hauchoki haya maisha, Ferdy? Unataka kifo ndo' kikufundishe, sio?"

"Mitchelle, najitahidi kuacha!" Ferdinand aling'aka. Macho yake yalianza kujawa maji.
"... napambana sana ... napambana lakini sioni nikiishinda vita hii."

Alitazama chini akikandakanda vidole vyake kwa msongo.

"Kila ninapokuwa mzima, timamu wa akili, siachi kukumbuka. Kheri wewe unayaota usiku, tena mara mojamoja, kwangu mimi ni tofauti."

Mara hii machozi yalimshuka yakamtambaa mashavuni.

"Nakumbuka wenzangu waliokufa mikononi mwangu. Nasikia sauti zao zikiniita niwasaidie. Naumia maana sikuwa na msaada wowote kwao zaidi ya kushuhudia wakiiacha pumzi."

Ferdinand alifikicha pua yake iliyokuwa nyekudu kama hoho, akamtazama Mitchelle.

"Mimi sipo kama wewe. Siwezi kuyahimili muda mwingine. Namna pekee ya kuondoa uhalisia wangu kichwani ni ulevi.

Ninapokuwa katika hali hiyo, nasahau kila kitu. Najihisi salama. Kila kitu ni chema."

"Hapana, Ferdinand!" Mitchelle alisema kwa mkazo. "Hapana, haiwezekani kuishi kwa mtindo huu. Huo unafuu unaoutafuta ndio utakaokuangamiza!"

Mitchelle alipendekeza Ferdinand aende kuonana na mwanasaikolojia kwaajili ya 'therapy'. Aliamini ni njia bora zaidi. Alishauri pia matumizi ya tahajudi kwenye kusafisha kichwa na marejeleo ya nyuma yanayoumiza.

"Tafadhali, Ferdinand," Mitchelle alisihi. "Inabidi ushinde vita hii."

Ferdinand aliridhia ushauri huo, akaahidi kuufanyia kazi.

Alinyanyuka akajimwagie maji kuuchangamsha mwili lakini Mitchelle akamsihi aketi, kuna jambo la muhimu wanapaswa kulijadili.

Jennifer alileta simu ya Mitchelle, mwanamke huyo akaingia mtandaoni. Alipekua kurasa kadhaa, kwa sekunde chache, kisha akampatia Ferdinand simu.

Ferdinand alitazama akaona sura yake.

"Unatafutwa, Ferdy," Mitchelle alisema akiongezea, "Sura yako imesambaa kwenye tovuti zote za New York."

Ferdinand alisoma maelezo yote yaliyoambatanishwa na picha yake. Neno kwa neno. Alipomaliza alimtazama Mitchelle kwa macho ya maswali.

Alikuwa anajaribu kukumbuka. Kichwa chake hakikuwa kinampa taarifa sahihi.

"Mitchelle, uliwaua wote?"

"Haikuwa dhamira yangu."

"Mitchelle, serious?"

"Sure. Nashangaaa wamekufaje kirahisi hivyo."

"Uko serious? Watu wamekufa, Mitchelle."

Ferdinand alitikisa kichwa akisikitika.

"Kulikuwa na haja gani ya kuua watu, Mitchelle?"

"Sijui nilikuwa nafikiria nini. Hasira zilishinda uwezo wangu wa kufikiri, Ferdy. Nilikuwa nimekwazika sana."

Ferdinand alishusha pumzi ndefu. Aliwaza mengi kichwani mwake. Shida si watu waliokufa. La hasha. Shida ni sura yake kutandazwa kwenye vyombo vya habari.

Alijihisi yupo uchi.

Aliegemea kiti akashika kichwa.

"Najua muda ungefika, Mitchelle. Tusingeweza kuishi hivi maisha yetu yote, lakini hii imekuwa mapema sana kuonyesha sura zetu," alisema Ferdinand. "Huoni tai wataanza kuutafuta mzoga?"

"Unachosema ni kweli," Mitchelle aliunga mkono, "Nimefanya kosa kubwa sana. Sikufikiria matokeo yangekuwa hivi. Tulitakiwa kuishi 'very low' mpaka pale tutapokuwa tayari."

Alimsogelea Ferdinand akamshika bega.

"Maji yameshamwagika, inabidi tuyadeki."

"Unataka nifanye nini?" Ferdinand aliuliza.

"Nataka hii kesi iishe," Mitchelle alijibu. "Niletee kila kitu kinachohusu hii kesi. Nataka kufahamu kila kichwa na kila mikono uliopo hapo, alafu n'tajua cha kufanya.

Ferdinand akatikisa kichwa.

Huu ndo' ulikuwa uwanja wake. Katika vitu alivyoletwa duniani kuvifanya kwa ufanisi, basi ni hiki.

Bwana huyu alikuwa mkufunzi haswa kwenye utafutaji wa taarifa. Hakuwa na mpinzani abadani. Alikuwa na njia zake za kipekee kabisa kwenye kufanikisha hilo. Njia ambazo hata Mitchelle hajawahi kuzielewa mpaka leo.

Palipohitaji nguvu, alitumia. Palipotaka akili, alifikiria, na palipokuwa na udhia, hakusita kupenyeza rupia.

Alienda bafuni kukoga.

Aliyafungua maji, taratibu akayasikiliza namna yanavyomtiririka kuondoa uchovu wake mwilini .

Maji yalimburudisha haswa, lakini zaidi yalimfanyia tahajudi kamilifu. Akili yake ilitamba huku na kule, ikipanga na kupangua mambo, wakati mwili wake ukiwa unapoozwa.

Nyuma ya kiuno cha mwanaume huyu, juu kidogo ya makalio kulikuwa na mchoro mdogo mweusi.

Tarakimu na herufi.

003/67/ADH

Mchoro huo ulionekana vema machoni kabla Ferdinand hajaufunika na taulo alipokwisha kuoga.



Masaa Matano Mbele


Utepe mwekundu wenye maneno meupe ulikuwa unakatiza kwa chini kwenye chaneli ya FOX NEWS.

Utepe huo ulisomeka:

'Breaking News ... Breaking News ... Breaking News ...'

Kideoni alikuwapo mwanamke mwembamba aliyevalia suti rangi ya njano, ametupia nywele zake nyeusi nyuma, mkononi ameshikilia kinasa sauti chenye chapa rasmi ya chaneli.

Mwanamke huyo, akiwa ananyooshea mkono wake nyuma ambapo kulikuwa kumejawa na watu pia magari, alitangaza kukutwa kwa mwili mfu wa mwanaume wa makamo ya miaka arobaini ndani ya gari aina ya Lexus GS-F nyeusi.

Kwa mujibu wa vielelezo vya tukio, mwili huo ulipokonywa uhai kwa kunyongwa mapema alasiri hii.


***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.


Na Steve B.S.M


Sehemu ya Tano


Westchester, New York.


Saa moja kasoro usiku.


Waandishi wa habari walishatapakaa kila kona ya eneo la tukio kuhakikisha hakuna kinachowapita.

Kamera zao zilikuwa zinawaka huku na kule zikichukua picha mnato na kila mahali katika eneo hili dogo walikuwapo wawasilishaji habari waliosimama mbele ya kamera zao kubwa cha chaneli kuripoti kilichojiri.

Ilikuwa ni kitambo kidogo tu kubaini ya kwamba aliyeuawa alikuwa ni afisa wa polisi katika kitengo cha usalama cha jiji la New York, Afisa Parker Wales.

Mazingira yake ya mauaji yalikuwa tata.

Kutokana na maelezo yaliyokuwa yametolewa na kiongozi wa polisi wa kanda hii, gari alilokutwa amefia polisi huyu halikuwa lake. Wanaamini pengine alitekwa na muuaji kabla ya kumkuta dhahma.

Wanalifanyia kazi kulibaini hilo.

Lakini pia afisa huyo hakuwa ameripoti kazini siku hiyo mbali na kwamba kifo kilikuwa kimemkuta akiwa amevalia sare za kazi.

Juu ya hayo, kiongozi huyo alitoa ahadi ya kumkamata mhalifu ndani ya siku chache na atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Katika hekaheka hizo, waandishi wa habari, polisi na raia, bwana mpelelezi, aliyepewa jukumu la kesi ya kesi ile iliyotokea katika klabu na baa ya The DL, alifika mahali palipotukia jambo.

Alikuwa amevalia suti nyeusi isiyokuwa na tai. Mdomoni akitafuna 'bubble-gum'. Shingoni beji yake ya polisi inaning'inia.

Kama ilivyokuwa kwa wengi, bwana huyu alizipata taarifa hizi kupitia mtandaoni kwanza kabla hajapigiwa simu rasmi na mkubwa wake wa kazi.

Kwa nafasi yake, lazima angalikuwapo hapa. Matukio haya yasingepita bila kujuzwa ama kuhusika kwa namna fulani ama namna nzima kabisa.

Alikuwa ni Homicide Detective. Mpelelezi aliyesomea na kufuzu kwenye sanaa ya mauaji. Huu ulikuwa ni uwanja wake.

Alisogea taratibu kuufuata umati, kabla hajafika, simu ikatoa mlio. Alisimama akaitazama, ilikuwa ni 'notification' ya kamari alocheza.

Alitazama upesi, akaona ameshinda.

Alitabasamu akipiga ngumi hewani. Takribani dola za kimarekani 500 zilikuwa zimeingia kwenye simu yake.

Alitabasamu kwa mbali akiirejeshea simu yake mfukoni, akasafisha koo kujirejesha kwenye mazingira yake ya kazi, akendelea na safari yake.

Aliutazama mwili mfu. Ilikuwa ni kama mchezo wa kuigiza lakini kweli isiyobadilika.

Mara ya mwisho, haijapita hata siku mbili, alionana na Afisa Parker kituoni wakizingumzia kesi ya mauaji ya The DL.

Afisa huyo alikuwa anamuulizia kama amefanikiwa kupata wasifu wa mtu wanayemsadiki kuwa mshirika wa mwanamke yule muuaji. Leo hii amelala mfu kwenye gari geni ndani ya sare zake.

Detective alitazama shingo ya marehemu. Ilikuwa nyekundu. Kwenye paji lake la uso, upande wa kushoto, alikuwa na jeraha.

Alikagua gari husika kwa mikono yake ndani ya 'gloves' kwa macho yake makali. Hakupata kitu.

Hakuna alama wala kielelezo chochote, kilichokuwa kinaonekana kwa macho, walau kusaidia pa kuanzia mbali na lile gari lililotelekezwa.

Tukio lilifanywa kwa ustadi.

Aliyefanya au waliofanya walidhamiria hivyo. Bila shaka alikuwa ama tuseme walikuwa ni wenye uweledi wa kimafunzo, uzoefu au vyote. Detective aliamini hivyo. Lakini dhamira yao ilikuwa ni nini?

Alifanya maongezi machache na watu wa 'Forensics' lakini nao hawakuwa na la kuongeza mpaka pale mwili utakapofanyiwa uchunguzi wa kisayansi.

Gari zima litakapofanyiwa upembuzi kuona kama kuna mabaki ya alama za vidole ama chochote kile kinachoweza kusaidia kupata DNA (vinasaba) vya wahalifu.

Detective alirejea kwenye gari lake akiwa na mambo kadhaa ya kufikiria.

Alifanya mawasiliano makaoni akaomba taarifa zote za mawasiliano ya mwisho kufanywa na Afisa Parker. Vilevile alihitaji kujua 'location' ya mwisho Parker kuonekana kwa mujibu wa simu yake.

Kutoka makaoni, alipata pia anwani ya makazi ya Afisa huyo, akawasha gari kushika barabara kuelekea magharibi mwa mji.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, ukitamatishwa hapa na pale na vijifoleni vya mataa, Detective alifika kwenye makazi ya marehemu Parker.

Alishuka akaegemea gari lake akikagua mazingira ya eneo hili kwa macho.

Ilikuwa ni nyumba nyeupe ya ukubwa wa wastani, ilionekana kwa nje tu kuwa ni sebule na vyumba viwili tu.

Nje kulikuwa na bustani ndogo yenye nyasi fupi za kijani kibichi.

Bustani hiyo, kwa upande wa kushoto, ilikuwa imetenganishwa na fensi fupi ya mbao, rangi nyeupe, iliyomaanisha mwisho wa makazi ya Parker na mwanzo wa makazi jirani.

Kwa upande wa kulia nyumba hii ilipakana na barabara ndogo ya lami ya mtaa huu.

Kwa maelezo yaliyopo, Afisa Parker alikuwa akiishi hapa mwenyewe. Hakuwepo na wa kumuuliza kuhusu siku yake isipokuwa majirani tu.

Detective alifanya ukaguzi wake kwa kama dakika tano. Kwa utulivu mkubwa.
Hakuona jambo la kushuku.

Aliendea nyumba hiyo ili apate kutazama na mazingira ya ndani.

Alipofika kibarazan alibaini mlango haukuwa umefungwa vema. Kulikuwa kuna ka uwazi kembamba kati ya mlango na mbao yake ya ukutani.

Kwa mikono yake yenye 'gloves' nyeusi aliusukuma mlango huo akaingia ndani.

Upesi alirusha macho yake kule na kule. Kulikuwa ni salama na tulivu.

Alikagua kitasa cha mlango, kilikuwa cha chuma chenye kichwa cha rungu, akabaini kilikuwa kimetenguliwa lakini si kwa hali ya kawaida.

Kwa macho ya juu, kitasa hiko kilikuwa kimefunguliwa na funguo, lakini kwa macho ya ndani, ambayo bwana huyu ndo' alikuwa akiyatumia kutazamia, kilikuwa kimepachikwa. Hii ndo' sababu mlango haukuwa umefungika vema.

Detective alipata shaka namna kitasa hiko kilivyokuwa kipya tofauti na mlango wake. Mbali na hivyo, nafasi ya kitasa kilichokuwapo mwanzoni haikufunikwa ipasavyo na hicho kipya.

Lakini haya yote ni kwa kutazama vema sana.

Alikigusa kitasa hicho kipya. Kilikuwa ni kigumu. Alikishika kukifungua, kwa kutumia nguvu kidogo, kikameguka.

Kilining'inia upande.

Bwana huyo alikagua mazingira yote ya ndani. Sehemu kwa sehemu. Hatua kwa hatua.

Alibaini kulikuwa na chapa mbili za viatu koridoni. Mlango wa chumba, pale alalapo Afisa Parker, ulikuwa upo wazi na kabati la nguo vilevile.

Ndani ya kabati la nguo, sehemu yanapotundiwa mashati, kwa chini yalikuwapo mashati mawili, mojawapo lilikuwa ni sehemu ya sare ya polisi.

Kitanda, upande wa kichwani, kilikuwa kimesogezwa. Bwana huyu alitazama miguu ya kitanda hicho akabaini alama za mjongeo.

Mbali na hapo, aliona alama ya kupondwa nyuma ya mlango wa chumba hicho. Alitazama kimo cha alama hiyo, akajipimishia na urefu wake.

Alinusa hapo. Kulikuwa na harufu ya pombe (alcohol).

Kwa hayo aliyoyaona, akajiridhisha kuwa uvamizi wa Afisa Parker na huenda hata mauaji yake yalifanyikia hapa.

Kuvaa kwake sare za kazi kulifanyikia humu chumbani, chini ya shinikizo. Uholela wa kabati la nguo ulimfanya aamini hivyo. Aidha Parker alichukua nguo mwenyewe katika hali ya kujawa na woga, akikosa umakini, au nguo ilikwapuliwa kwanguvu na waliomvamia.

Kusogezwa kwa kitanda kulimaanisha purukushani ilijiri hapa na kupondwa kule kwa mlango ndiyo ilikuwa sababu ya jeraha la paji la uso alilokuwa nalo Parker.

Swala la kwanini palikuwa pananuka pombe ni kwasababu ya kufutwa kwa ushahidi.

Alcohol, katika ulimwengu wa uhalifu, hutumika kama nyenzo ya kudhoofishia viambata mwili vinavyoweza kubainishwa na wataalamu wa upelelezi wa kisayansi (forensics).

Hilo ndilo lilikuwa lengo la mhalifu.

Kupoteza mwelekeo wa upelelezi.

Detective alitoka ndani, akaelekea nyumba jirani. Wakati huo alishapiga simu makaoni kuagiza wataalamu wa sayansi ya upelelezi kuja kwenye makazi ya Parker kufanya uchunguzi.

Baada ya dakika chache, wapelelezi hao walifika, wakaizungushia nyumba ya Parker utepe wa usalama na kazi ikaanza kufanyika. Kupiga picha, kuandika maelezo na kuchukua chochote kile kilichokuwa kina manufaa kiupelelezi.

Wakati yote hayo yanafanyika, mbali na eneo la tukio, kwa kama kilomita moja na robo hivi, picha zilikuwa zinachukuliwa na bwana mmoja hivi ambaye hakuonekana.

Bwana huyo alikuwa ameshikilia kamera kubwa yenye lenzi yenye nguvu.

Alipiga picha nyingi kadiri alivyoweza na mara zote kamera yake alikuwa anaielekezea mwelekeo wa Detective.

Huyo ndo' alikuwa 'target' yake.

Picha zilikuwa safi na zenye ubora wa hali ya juu.

Alipopiga za kumtosha, alizikagua picha zake moja baada ya nyingine.

Katika 'gallery' yake hiyo, alikuwa na picha za tukio zaidi ya moja. Mandhari tatu tofauti. Kote humo mlengwa akiwa ni mmoja.

Tangu alipotoka eneo lake la kazi, kituo kikubwa cha polisi katika jiji la New York, akafika eneo ulipokutwa mwili wa Afisa Parker na mwisho katika makazi ya marehemu huyo.

Kila nyendo.

Bwana huyo aliimaliza kazi yake. Aliwasha gari akayoyoma.


**


Baada ya Siku Tatu


Bronx, New York. Majira ya mchana wa saa sita.


Dr. Lambert alishuka ngazi kwa mwendo wa taratibu. Mwili wake wa kizee haukumruhusu kutupa miguu kwa kasi japo alikuwa bado mkakamavu.

Alikuwa amevalia koti kubwa la mvua kuendana na hali ya hewa ya siku. Miwani ya macho usoni na suruali ya kadeti iliyopokelewa na buti kubwa la njano chini.

Alijivesha kofia ya koti lake punde alipofika nje. Mvua kubwa ilikuwa inanyesha.

Alitazama kushoto na kulia.

Kwa mbali aliona gari alilolilenga; Escalade nyeusi, akalijongea akitazama chini.

Aliyekuwemo kwenye gari hilo alitazama kioo cha pembeni akamwona mgeni wake akiwa anajongea. Aka 'unlock' milango.

Punde mzee huyo akawa ndani ya gari.

Walikuwa wawili tu, Dokta na bwana Ferdinand aliyekaa kwenye kiti cha usukani. Bwana huyo alikuwa anamtazama mgeni wake kupitia kioo kilichopo juu ya kichwa chake.

"Leo umekuja wewe?" Dr. Lambert aliuliza swali lisilokuwa na haja ya jawabu. Alifanya hivyo akiwa anaingiza mkono wake mfukoni, ndani ya koti.

"Mzigo wetu huu hapa," alisema akiunyoosha mkono wake wa kuume.

Ferdinand alipokea alichopewa kisha maramoja akauweka mfukoni.

"Kuna la ziada?" bwana huyo akauliza

"Hapana," Dr. Lambert alijibu akitikisa kichwa. Aliendelea kumtazama Ferdinand.

"Unataka kusema nini?" Ferdinand aliuliza.

"Hamna kitu." Dokta alitabasamu. "Ni kwamba tu niliona tangazo kuwa unatafutwa na polisi."

"Vizuri. Inaonekana bado macho yako yanafanya kazi."

"Huoni ni hatari kuja huku badala ya Mitchelle?"

"Ni nini unataka kusema, Dokta?"

Macho ya Ferdinand yalikuwa kwenye kioo.

"Ni usalama tu ndo' neno langu. Unajua tunategemeana. Endapo mmoja akienda chini, myororo wetu wote utabainika na kutokomezwa."

"Dokta?"

"Ndio."

"Kuna pesa unayodai?"

"Hapana. Labda hii ya sa--"

"Ishatumwa kwenye akaunti yako. Hiko ndo' kitu pekee unachotakiwa kuhofia. Pesa yako. Sawa? Zaidi ya hapo ni labda kama miaka ulonayo imekutosha."

Dr. Lambert alitoa tabasamu lisilotoka moyoni. Alivaa kofia ya koti, akashuka toka kwenye gari. Alipopata pa kujiegesha akafanya hivyo akilitazama gari la bwana Ferdinand likiyoyoma.

"Hivi huyu jamaa anajiona nani?" alisema kwa ngebe. Aliubinua mdomo wake wa kizee akaguna kwa shari.

"Wewe ni kajibwa tu ka Mitchelle, kijana. Acha kujiotesha mapembe yasiyokuwa ya kwako. Kuna siku ntakufundisha adabu ujue nafasi yako."

Alipohisi ahueni ya hasira yake, alitoka hapo alipokuwa amejibanza akashika njia ya kwenda ndani.

Kidogo alihisi simu yake inanguruma. Alitoa akaitazama, ni 'Boss'. Alihakiki mazingira yake mara mbilimbili kabla hajapokea na kuiweka sikioni.

"Ndio, mkuu ... enh? ... mbali kidogo ... naam ... saa hii? ... sawa, nitakuwepo hapo si muda ... ndio."

Aliirejesha simu mfukoni akajitahidi kukaza mwendo.

Walau kidogo.


***


Queens, New York. Olympus Printing Press


Saa Moja Usiku


"Leo itabidi ungoje, Hilda," alisema Bryson aliyekuwa amevalia 'casual'. Ni Ijumaa hii hivyo alijipumzisha kidogo na 'manguo' ya kiofisi.

Alivalia tisheti jeupe, suruali ya jeans na raba za New Balance rangi nyeusi

Kwa upande wa Hilda, yeye mwendo wake ulikuwa uleule. Sketi nyeusi ya kitambaa na shati jeupe. Alichobadili ilikuwa ni fremu ya miwani yake tu. Rangi ya orange. Macho ya nyoka.

Mwanamke huyo alikuwa ameketi. Mikono yake mapajani.

"Abee?"

"Ndio," alisema Bryson akijizungushazungusha kwenye kiti. "Kazi iliyopita umeifanya vema. Nakupa kongole. Leo hii inakuja kazi nyingine, ningependa uipokee, ukaanze kuifanya usiku huu."

Hilda hakujibu kitu lakini uso wake ulisema.

Alitazama chini akiwa ameparamiwa na mawazo.

"Sikia, Hilda. Nitakuambia jambo na wewe utafanya uchaguzi wako. Utaifanya kazi hii kwa nguvu zako zote, kesho asubuhi nikupatie pesa yako, nadhani unajua vema sina maneno maneno kwenye hilo, ama utaiacha hii kazi niifanye mwenyewe na mgao mzima?"

"Shingapi?" Hilda aliuliza. Macho yake ndani ya miwani yalikuwa na uchu.

Hiki ndo' alichokuwa anangoja.

Alikuwa anasiginasigina vidole vyake vinene.

"Hilda," Bryson aliita. "Pesa nlokupatia mara ya mwisho ilikutosha?"

Hilda alitabasamu. Hilo ndo' lilikuwa jibu lake.

"Basi ntakuongezea zaidi."

"Kweli?"

Macho ya Hilda yaling'aa. Alihisi mwili wake umepatwa na nguvu upya.

"Ndio. Kwahiyo vipi? Utaifanya kazi?"

"Ndio. Nitaifanya, boss."

"Safi. Sasa naomba ungoje kidogo, sawa?"

"Sawa. "

"Sasa nenda kangoje ofisini kwako. Atakapokuja mgeni, utulie vivyo hivyo. Akiondoka, nitakuita nikupe maelekezo."

Hilda alinyanyuka akaaga, na hapo ndipo Richie, upesi kabisa, alipotoka mlangoni alipokuwa ametega sikio kuskiza kinachoendelea, akaenda kwenye kiti chake.

Aliketi akiigiza anafanya kazi.

Hilda alitoka ofisini, macho ya Richie yakimtazama na kumsindikiza mpaka anaketi.

Kukawa kimya kidogo.

Hilda alitoa simu yake akawa anachati.

"Hatuondoki?" Richie aliuliza.

"Hapana, kuna kazi nataka kumalizia kisha ndo nifungashe virago."

Richie alimuuliza ni kazi gani lakini Hilda hakuwa bayana. Alisisitiza tu kuwa ni kazi anatakiwa kuifanya.

Swala hilo likamfanya Richie apatwe na fundo kooni. Alimeza mate akahisi yanagoma kushuka.

Alitakafari cha kufanya.

Endapo akiketi hapo kwa muda, haitaeleweka. Muda wa kuondoka kazini ni saa moja. Akikaa zaidi, atajitetea na nini?

Lakini hapohapo hakuwa anataka kuondoka. Kumwacha Hilda nyuma, pamoja na boss au tuseme mwanaume, ni kitu ambacho roho yake haikumtuma kabisa.

Hapana. Alisema na nafsi yake.

Baada ya kuwazua, alipata la kufanya. Alinyanyuka akaaga kwenda zake. Alibeba begi lake akatoka nje.

Badala ya kwenda nyumbani, alielekea kwenye mgahawa ule uliokaribu. Hapo alihakikisha anapata mahala pazuri, akaketi akiagiza kinywaji.

Alidhamiria kubaki hapo mpaka Hilda atakapotoka ofisini.

Alidhamiria pia kumwona huyo anayeileta kazi ambayo amekuwa akiisikia kwenye mlango wa mkurugenzi wake.

Kazi ambayo ni SIRI.

Taratibu alikunywa kinywaji chake akiwa anategea muda muafaka ufike. Hakuwa na papara, alikunywa fundo moja kwa madakika. Muda mwingine akiutumia kwenye kioo cha simu yake.

Alisubiri hapo lisaa likapita, kinywaji kikaisha.

Haikuwa tabu, aliagiza kingine akaendelea kungoja.

Likapita lisaa lingine.

Alipotazama saa yake ya mkononi, ilikuwa ni saa nne yenye dakika za mwanzoni. Si Hilda wala mgeni wao aliyeonekana.

Aliamua kuvuta subra.

Japo alikunywa kidogokidogo, kinywaji kilizidi kushuka kwenye glasi, na taratibu alianza kuona wahudumu wa mgahawa wakifanya taratibu za kufunga eneo.

Muda ulisogea.

Ilifika saa tano, kwa mujibu wa saa yake, ila alipotazama palikuwa ni pakavu. Hakika alipata mashaka.

Si yeye tu, hata Bryson aliyekuwa ndani ya ofisi alitazama saa yake mara kwa mara akijiuliza kinachoendelea.

Ubaya ni kwamba hakuwa na namna yoyote ya kuwasiliana na watu wake. Kwenye mawasiliano na washirika hawa, ni yeye ndo' alikuwa anatafutwa, si vinginevyo.

Alisimama akatembea huku na kule.

Punde simu ikaita.

Aliiwahi.

Alipoitazama, akaona ni mkewe!

"Aaaagghh!"

Alilalama. Aliipokea simu hiyo akamsihi mkewe angoje, punde atampigia, kisha akaendelea kungoja.

Likaongezeka tena lisaa limoja. Hamna aliyekuja. Hamna aliyepiga.

Hapana. Hii haikuwa kawaida.


**
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.



Na Steve B.S.M



Sehemu ya Sita



Queens, New York.


Masaa Mawili Nyuma Katika Usiku Huu.


Ferdinand alitoka kwenye 'supermarket' akiwa ameshikilia mfuko mweusi. Alikuwa amevalia kofia, kapelo nyeusi, kuuficha uso wake ulioanikwa kwenye vyombo vya habari.

Si muda mrefu sana tangu apitie makazi ya Mitchelle kwaajili ya kuushusha mzigo aloupokea toka kwa Dr. Lambert.

Aliingia kwenye gari aka - 'lock' milango, akaivulia kofia pembeni. Kabla hajafanya kingine, akaufungua mfuko huo na kutoa chakula humo.

Tumbo lilinguruma. Mate yalimjaa mdomoni. Hakuwa amekula kwa muda tangu asubuhi. Hata alipopita kwenye makazi ya Mitchelle hakupata hiyo fursa. Kuna mahali aliharakia.

Ilikuwa ni 'burger' nene aliyoishika kwa mikono miwili. Alitoa na soda kwenye mfuko ule mweusi akaifungua na kuisimamisha kwenye dashboard ya gari.

Aliifakamia chakula chake upesiupesi akiishushia na soda ya baridi kwa mafundo makubwa makubwa.

Wakati huo macho yake, ambayo hayakuwa na kazi ya kufanya, yakawa yanazungukazunguka huku na kule kuangazia mazingira huku mdomo ukiujaza tumbo.

Kidogo alimwona mwanaume aliyekatiza nyuma ya gari lake akielekea upande wa pili wa barabara.

Mwanaume huyo alikuwa amevalia 'hood' nyeusi iliyomfunika kichwa chake. Mwendo wake ulikuwa wa taratibu. Chini amevalia raba nyeusi zenye unyayo mweupe.

Alikuwa na kimo kirefu kwa wastani, na mwili wake usio mnene ama mwembamba. Kwa mwendo, alikuwa ni mkakamavu.

Mwanaume huyo alinyookea gari moja ya kawaida, matoleo ya miaka ya zamani ya kampuni ya Chevrolet, rangi ya chungwa. Akafungua mlango na kuzama ndani.

Huo ndo' ukawa mwisho wa Ferdinand kumtazama mwanaume huyo. Hakujua kwanini alimzingatia.

Mwanaume yule, ni wazi, alikuwa ametoka ndani ya 'Supermarket' lakini alipojaribu kidogo kukumbuka, hakupata kumwona kule ndani.

Supermarket ni kubwa hivyo hilo halikuwa la kushangaza.

Aliendelea kutafuna chakula chake na si muda akawa amemaliza chote.

Alimalizia na soda yake kisha chupa akaiweka ndani ya mfuko aliouweka kwenye kiti cha pembeni.

"Hapa sasa niko sawa," alisema akipetipeti tumbo lake.

Alitazama saa yake ya mkononi, akawasha gari na kutimka hapo.

Alishika barabara akiendesha kwa mwendo wa wastani. Alipozimaliza kona mbili, alitazama kioo kilichopo juu ya kichwa chake. Hapo aliona magari matatu yakiwa nyuma yake.

Aliendelea na mwendo wake, alipoikamilisha kona nyingine, alitazama tena kwenye kioo.

Kati ya yale magari matatu aliyoyaona awali, aliyaona mawili. Moja lilishashika njia nyingine.

Aliendelea na zoezi lake, tofauti na ilivyokuwa kawaida ya njia anayoelekea, alikata kona nyingine. Kona ambayo ilimfanya ashike njia ndogo zaidi, 'feeder road', ambayo iliingia ndani ya mtaa.

Katika njia hiyo, alitembea mita chache, mwendo wa taratibu, macho yake yakatazama kioo.

Sasa kuna jambo aliling'amua.

Miongoni mwa magari yale matatu aliyoyaona awali, moja lilikuwa linamfuatilia.

Gari hilo lilikuwa ni Chevrolet caprice, rangi ya machungwa.

Gari lilelile aliloliona kule Supermarket.

Gari alilolipanda yule mwanaume aliyekuwa amevamalia 'hood' nyeusi iliyofunika kichwa chake.

Hapa Ferdinand aliwaza zaidi. Mwanaume huyo alianza kumfuatilia muda gani? Je, aliingia ndani ya Supermarket kwa ajili ya kumfuatilia pia? Na kwenye gari yupo peke yake ama na wengine? Wanataka kunikamata au kuniua?

Maswali hayo yalikuwa yanajirudiajirudia kwenye kichwa chake.

Aliamini kabisa, ndani ya nafsi yake, bwana yule aliyemwona hakuwa polisi.

Laiti ingalikuwa hivyo, basi angeshalimfuata akamweka chini ya ulinzi kwa muda ule aliopata nafasi.

Alitazama kwa umakini kiooni kana kwamba anataka kuona jibu la kila swali analojiuliza kichwani mwake.

Aliwaza namna ya kufanya.

Ghafla aliongeza kasi ya gari yake! Ilikuwa ni kufumba na kufumbua. Alikata kona mbili tatu, akapotea machoni!

Barabara hii ndogo, iliyokuwa inakatiza katika mtaa huu mdogo, ilibakia kuwa pweke. Kama si watembea kwa miguu wawili waliokuwa wanakatiza kwa muda huo, basi gari lile la rangi ya machungwa lingebaki lenyewe.

Gari hilo lilipunguza mwendo wake likitembea tararibu mno. Aliyekuwemo ndani alikuwa anatazama huku na kule kulisaka gari Escalade alilokuwa analitafuta.

Hakuelewa lilitokomea wapi lakini kwa mwendo huu maeneo haya, ni bayana aliamini gari hilo linaweza likawepo maeneo hayahaya ya karibu.

Kwa kama dakika moja, gari hilo lilisonga. Njia ilipokata kuume, nalo likaelekea huko, punde kidogo likasimama!

Mbele, mita ishirini tu toka alipo, gari alilokuwa analitafuta lilikuwa limejiegesha kando, tuli.

Gari likajiegesha pembeni, taa zikazimwa.

Mahali hapa palikuwa pametulia sana. Mwanga ulikuwa hafifu sababu ya uwepo wa majengo marefu yaliyokuwa yametelekezwa hii mitaa ya Manhattan, Queens ndani ya jiji la New York.

Baadhi ya majengo yalishaotewa mpaka na miti. Yamekuwa meusi kwa rangi, meusi kwa kiza.

Baada ya muda kidogo wa kutathmini, bwana aliyekuwamo ndani ya gari lililokuwa linamfuata Ferdinand, alishuka akiwa ameshikilia bunduki ndogo mkono wake wa kuume.

Uso wake ulikuwa umwefunikwa na soksi nyeusi iliyoacha macho tu yakiwa wazi.

Mwendo wake ulikuwa ni wa tahadhari na hakujiendea kwa upesi. Wakati huo macho yake yalikuwa kibaruani huku na kule kutazama kama kuna cha kukitilia maanani.

Kwa akili ya kawaida tu ya binadamu, wazungu huita 'common sense', huu ulikuwa ni mtego.

Pengine bwana huyu aliliwazia hilo lakini aidha hakujali au alikuwa anajiamini kupita kiasi.

Alilifikia gari, mkono wake wenye bunduki ukiwa mbele, akapaza sauti kwanguvu ya kwamba alokuwemo ndani atoke haraka!

Kimya.

Hakuna kilichotokea.

Alitazama dirishani. Hakuona mtu ndani.

Punde alisikia kitu kinagusa kisogo chake. Kabla hajafanya lolote lile, sauti iliyotokea nyuma yake ilimwamuru;

"Tupa silaha yako chini."

Aliiachia bunduki yake ikaangukia chini.

Kih!

"Wewe ni nani? Kwanini unanifuata?" sauti ya Ferdinand iliuliza.

Bwana yule, aliyekuwa amenyoosha mikono juu kwa ku-surrender, alikaa kimya.

"Sitarudi tena kuuliza," Ferdinand alisema akiiandaa bunduki yake kwa shambulio. Aliikoki, masikio ya adui yake yakapata ujumbe.

"Wewe ni nani na kwanini unanifuata?" Sasa hivi Ferdinand alipaza sauti yenye amri ndani yake.

Uso wake haukuwa na lepe la utani.

Bwana yule, kwa sauti isiyotetemeka, alimjibu,

"Siwezi kukujibu, Ferdinand."

Jibu hilo lilimshangaza Ferdinand. Si tu kwamba bwana huyo alikuwa anamfuatilia, bali pia alikuwa anajua na jina lake!

Jina ambalo amezoea kuitwa na watu wawili tu, Mitchelle na Dr. Lambert. Hata polisi wanaomtafuta huku na kule hawakuwa wanajua jina lake pamoja na mtandao wao mpana wa rekodi.

Sasa huyu ni nani?

Mwale huo wa mawazo ulipoteza umakini wa Ferdinand. Ndani ya sekunde mbili ni kama vile alikuwa anasaka ndani ya kichwa chake kuona kama kuna kumbukumbu inayoweza kumsaidia. Na ndani ya sekunde hizo, jambo lilijiri!

Kwa upesi usio na kifani, bwana huyo aliyeufunika uso wake, alisogeza kichwa chake kando na mdomo wa bunduki kisha akainyaka silaha hiyo kwa mkono wake wa kuume, akaipindua haraka kumnyooshea Ferdinand.

"Nimetumwa kukuua!"

Alisema na bila kujivuta akafyatua bunduki .... Puuh! Risasi ilitwanga kifua cha Ferdinand, ikamlaza mwanaume huyo chini.

Mdomo wazi.


***


Halletts Point Apartment: New York.


Saa Tano Usiku na Madakika. Siku ya Leo.


"Umempata hewani?" Mitchelle aliuliza. Macho yake yalikuwa yamejawa na hamu ya kufahamu. Mbele yake alikuwa amesimama Jennifer aliyekuwa ameshikilia simu mkononi.

Mwili wa Mitchelle ulikuwa ndani ya taulo jeupe akiwa ametokea bafuni kuoga muda si punde. Mgongo wake mweupe ulikuwa na majimaji ambayo hayakukaushwa vema.

"Hapana, sijampata," Jennifer alijibu kwa ishara.

"Shit!" Mitchelle akalaani. "Atakuwa yuko wapi? Sidhani kama ingemchukua muda mrefu hivi."

"Je atakuwa ameenda kwenye madawa?" Jennifer aliuliza.

Mitchelle alinyamaza kidogo akitafakari kisha akasema,

"Sidhani. Anajua kuna kazi inamngoja. Ni kheri ungeniamsha alipokuja, saa hii nisingekuwa na hofu ya kumwazia mtu huyu mzima."

Mitchelle alibanwa na mawazo. Muda ulikuwa unaenda. Kila alipotazama saa ya ukutani alihisi anapagawa.

Alimwambia Jennifer kuwa endapo Ferdinand hatofika mpaka kufikia saa sita, yani siku mpya, basi hali yake itakuwa mbaya.

Kabla siku haijageuka anapaswa kudungwa dawa na mtu pekee anayefanya kazi hiyo kwa usahihi ni yeye. Ferdinand.

Jennifer, kwasababu muda ungalibado, alimtuliza na kumsihi bosi wake awe na subra. Alitegemea Ferdinand angefika kila kitu kikawa sawa.

Mitchelle alichukua simu yake akaandika namba akapiga. Punde kidogo simu ilipokelewa na mwanaume upande wa pili. Ilikuwa ni sauti ya Bryson.

Bila kupoteza muda, Mitchelle alimuuliza mwanaume huyo muda ambao Ferdinand ametoka huko lakini ajabu aliambiwa Ferdinand hakuonekana mpaka muda wa sasa.

"Nipo hapa namngojea. Muda umeenda sana, sijui kama mke wangu atanielewa leo nikifika nyumbani."

Mitchelle alimsihi mwanaume huyo aende nyumbani kisha akakata simu.

"Nini kimekutokea, Ferdinand?" Mitchelle alijiuliza akikunja sura.

Akili ilimwambia avae upesi akamtafute Ferdinand popote anapohisi atakuwapo lakini alitazama muda akaona ni jambo lisilowezekana.

Muda ulishamtupa mkono. Ilikuwa imebakia dakika tano tu kabla ya muda kupinduka kuwa siku mpya, hivyo kabla ya kumwazia Ferdinand ilibidi ajue kwanza hatma yake.

"Jennifer, inabidi unisaidie kwenye hili, tafadhali. Sijui Ferdinand atafika muda gani hapa. Siwezi tena kungoja. Ulishawahi kuniambia una ujuzi wa unesi, nadhani leo ndiyo siku ya kuutumia ujuzi huo."

Alimpatia Jennifer kila kitu; bomba ya sindano na dawa yake. Kimiminika rangi ya kijani.
Alimweleza cha kufanya na Jennifer akaapa ya kwamba ameelewa. Lakini alimwonya bosi wake kuwa yeye hajafanya hilo zoezi kwa muda mrefu.

Ni kweli alipata mafunzo katika usichana wake lakini hakupata wasaa na fursa ya kutumia mafunzo hayo kwa vitendo zaidi. Mara zile chache alizoshika bomba chuoni, ndizo zilikuwa hizohizo tu.

"Jennifer, unaona huu ni muda wa machaguzi kwangu?" Mitchelle aling'aka. "Sina namna nyingine ya kufanya zaidi ya hii. Wewe pekee ndiye upo hapa, na wewe ndiye utafanya hili jambo."

Mitchelle aliufunga mkono wake vema. Jennifer, akiwa anahema pakubwa na moyo wake ukiwa umeongeza kasi kidogo, alijitahidi kuifanya kazi alopewa kwa umakini alobarikiwa.

Aliidunga sindano, akaingiza dawa akimtazama Mitchelle usoni. Aliomba Mungu kila kitu kiende sawa. Alipokamilisha kazi hiyo, aliamini hilo limetendeka. Mitchelle alitabasamu akimshukuru.

"Umeokoa maisha yangu."

Jennifer alitabasamu. Alihisi moyo wake umekuwa wa baridi kwa furaha.

Alichukua kifuniko cha sindano akafunika nyenzo hiyo. Ilikuwa ni saa sita na madakika yake sasa. Mitchelle alisimama akaendea kabati lake la nguo akilenga kuchukua nguo kadhaa humo ili akafanye zoezi la kumtafuta mwenzake, Ferdinand.

Akiwa anafanya hivyo, kichwani mwake alikuwa anawaza ni wapi pa kuanzia msako wake.

Alitengeneza mabunio mengi kuhusu kilichomkuta mwanaume huyo na yote hayo yalikuwa yanamuumiza kichwa. Mwishowe aliomba tu awe mzima, haijalishi atakuwa yupo kwenye mikono gani.

Amkute salama.

Jennifer alitoka chumbani akapeleka nyenzo alizotumia kwenye ndoo ya taka, baada ya hapo alirudi tena chumbani mwa Mitchelle kwaajili ya kumtazama usalama wake.

Alimuuliza mwanamke huyo anajisikiaje, Mitchelle akamjibu yuko vizuri. Lakini kuna jambo lilimtatiza Jennifer kiasi cha kuhisi pengine kuna kitu hakijaenda sawa.

Siku zote ambazo amekuwa akifanya kazi hapo ameshuhudia mara kadhaa Ferdinand akimdunga sindano Mitchelle.

Kila amdungapo, mwanamke huyo hupoteza nguvu, hulala na kuchukua masaa kadhaa kurejea katika hali yake. Mbona leo ni tofauti?

Alimuuliza tena Mitchelle kama yuko sawa, mwanamke huyo akastaajabu maswali hayo.

"Kwani kuna shida, Jennifer?"

Jennifer alimweleza mashaka yake lakini Mitchelle alimtoa hofu kuwa kila kitu kipo sawa tu.

"Huenda wewe ndo' umenidunga vizuri. Hujadhania hilo?"

Angalau hiyo kauli ikampa Jennifer ahueni ya mashaka. Aliaga akaelekea chumbani mwake baada ya Mitchelle kumwambia kuwa anatoka kwenda kumtafuta Ferdinand.

Alioga kisha akarejea sebuleni alipowasha runinga akikaa hapo kutazama tamthilia.

Huwa anafanya hivi pale Mitchelle anapotoka usiku. Hukaa kungoja hapo sebuleni mpaka atakaporejea. Hata usingizi ukimkuta, huumaliza papo hapo.

Alikaa hapo kwa kama dakika tano hivi kabla hajasikia kengele nyepesi inalia. Ilikuwa ni kengele ya mlangoni.

Alihisi pengine amesikia vibaya lakini kengele ilipolia kwa mara nyingine, alipata uhakika. Alisikia sawa. Lakini ni nani?

Alinyanyuka akauendea mlango akiomba iwe ni Ferdinand mlangoni. Alipoufungua akakutana uso kwa uso na mwanamke mwembamba mwenye nywele fupi nyeusi na uso uliochongoka.

Mwanamke huyo alikuwa ni moja ya watu wanaoishi kwenye 'apartment' hii. Si mbali sana na hapa aliposimama Jennifer.

Mwanamke huyo, bila salamu, alimwambia Jennifer kuwa Mitchelle ameanguka huko chini, hali yake si nzuri kabisa hivyo aende upesi kumtazama.

Jennifer alitoka upesi akiurudishia tu mlango bila ya kuu-lock. Alikimbilia kweye lift humo akabofya kitufe cha kuelekea chini.

Lifti ilishuka lakini si kwa kasi aliyokuwa anaitaka. Aliona kama inamtania. Alitamani iporomoke lakini hilo halikuwezekana.

Mlango ulipofunguka tu, alichumpia nje akakimbilia kule alipoelekezwa.

Huko alimkuta Mitchelle yuko chini akiwa amezungukwa na watu kadhaa. Aliposogea karibu, alibaini mwanamke huyo alikuwa ameumia kichwani, anavuja damu.
Mdomo wake umejawa na povu la kijani.

Mmoja wa waliokuwapo hapo, kwa upesi, alimweleza Jennifer kilichojiri ya kwamba alimshuhudia Mitchelle akishika kichwa kama mara mbili kabla ya kuanguka chini vibaya.

"Niliwahi kumtazama, hakuwa anaweza kusema kitu. Alikuwa akirukaruka povu jingi likimtoka mdomoni!"

Lakini shuhuda huyo aliongezea kwa kusema alitaka apige 911, simu ya msaada, lakini alibaini punde kuwa mwanamke huyo alifariki dunia.

"Hakuwa anahema. Mapigo yake ya moyo pia yalisimama. Niliona haina haja tena."

Jennifer alihisi anaota. Alidhani akifunga macho na kuyafungua haya yote yatakoma lakini haikuwa hivyo. Kila alipofunga macho na kuyafungua, alikuta ni yaleyale.

Hakuwa anaota bali ndo' uhalisia wenyewe.

Ina maana amemuua bosi wake?

Amemuua Mitchelle?

Aliunyanyua mwili wa Mitchelle akaubeba katika mikono yake.

Macho yake yalikuwa mekundu yakimwaga machozi. Moyo wake ulikuwa unamuuma kana kwamba kuna mtu ameutia mkononi akiufinyangafinyanga.

Akiwa ameyang'ata meno yake kwanguvu, aliingia ndani ya lifti akabonyeza kitufe cha kupanda juu.

Aliharakisha kuingia nyumbani, akamweka Mitchelle kitandani. Kwa muda wa kama dakika mbili, mwanamke huyo akawa analia.

Uso wake uligeuka kuwa mwekundu kama macho yake. Kwikwi za kilio zilikuwa nyingi kiasi kwamba alihema kwa tabu.

Alitaka apige simu ya msaada ama ampeleke mwanamke huyo hospitali lakini alikumbuka jambo. Mitchelle alishawahi kumuonya na kumsihi kuwa haijalishi nini kimetokea, hatakiwi kupelekwa hospitali.

Ni daktari wake tu ndiye atakuja nyumbani kumwangalia na kumuuguza, si vinginevyo.

Alipokumbuka hilo, alichukua simu ya Mitchelle ambayo aliikuta mfukoni mwa suruali ya mwanamke huyo, akaanza kusaka majina.

Hakukuwa na majina mengi. Kumi tu. Aliyapitia yote asione jambo la maana. Majina hayo yalitunzwa kwa herufi na ishara. Hayakuwa wazi.

Kichwa kilimuuma. Akili iliganda kufanya kazi. Mikono ilitetemeka. Jasho jingi lilikuwa linamshuka.

Alitazama simu ile kwa mara ya pili, akijaribu kutuliza akili kadiri awezavyo, akaona jina alilolishuku linaweza kuwa na msaada.

Lilikuwa ni jina ambalo mwisho wake liliambatanishwa na 'emoji' ya sindano. Nafsi yake iliamini huenda akawa daktari. Akapiga.

"Namba unayopiga, haipatikani kwa sasa. Jaribu tena baadae."



***
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA.

Na Steve B.S.M



Sehemu ya Saba



Haikujalisha ni mara ngapi Jennifer alipiga simu, hakumpata aliyemlemga.

Kila alipopiga ujumbe ulijirudia uleule! namba anayopiga haipatikani kwa sasa. Ilifikia kipindi alitamani kuivunja simu ile kwa kuona inamfanyia kusudi lakini mkono ulisita.

Kama ingekuwa yake, bila shaka angefanya hivyo. Kichwa chake kilichokuwa kizito kwa mawazo na hofu sasa hakikuwa na msaada wowote zaidi ya kuwa kifuniko cha shingo tu.

Kila alipojaribu kuwazua, mambo yaligoma. Kiwiliwili kilikuwa cha baridi wakati kichwa kikiwa cha moto. Tangu azaliwe hakuwahi kumbana na kadhia kama hii.

Alikaa hapo, pembeni ya mwili wa Mitchelle, akiwa hana anachokiwaza. Macho yake yalinywea, uso wake ulikosa matumaini.

Aliunyanyua mkono wa Mitchelle akauweka kiganjani mwake. Machozi yalimbubujika sana. Nafsi ilimsuta kwa masimango makali. Alishindwa kuvumilia akaurejesha mkono huo kitandani.

Mara kengele ya mlango ililia keng-keng-keng!

Alishtuka mno. Nusura moyo uvunje mbavu.

Kabla hajanyuka kwenda kutazama, alisikia mlango unafunguliwa na hapo ndipo hofu yake ilizidi mipaka.

Alitetemeka akitoa macho yake ya woga. Alitamani kupaza kuuliza ni nani aliyeingia ndani lakini maumbile yake hayakumruhusu. Hakuwa na sauti.

Kidogo alisikia sauti ya kiume ikitokea sebuleni ikisema;

"Ni Ferdinand, nipo hapa!"

Sauti ilikuwa ni halisia lakini Jennifer hakuamini alichokisikia. Alitulia tuli akiwaza vipi endapo ikiwa ni mtego au ni wanausalama?

Akiwa hapo haelewi nini cha kufanya, alisikia vishindo vya mguu vikisogelea mlango wa chumba cha Mitchelle.

Chumba ambacho yeye yumo pamoja na mwili mfu.

Mlango ulifunguliwa, akaingia mwanaume mrefu aliyevalia kapelo nyeusi. Umbo na mavazi yake yalikuwa yako bayana. Na uso wake alipoangaza ... Alaa! Alikuwa ni Ferdinand.

Uso wake ulikuwa na jeraha na michubuko kadhaa.

Jennifer alinyanyuka upesi akamwendea mwanaume huyo na kumkumbatia. Kile kilio kilichokuwa kimetulia kwa muda, kilianza tena. Machozi yalimshuka kama mto. Mafua yalibana pua yake akashindwa kabisa kuitumia kuhema.

Alimweleza Ferdinand yale yote yaliyotukia kumhusu Mitchelle. Kama hadithi lakini ni uhalisia. Aliomba msamaha mara hamsini akisema hakudhamiria kuyafanya hayo, lengo lake lilikuwa ni kusaidia tu, lakini kwa wakati huo akili ya Ferdinand ilikuwa mbali mno.

Hakumtazama Jennifer aliyekuwa anampatia maelezo kwa ishara, badala yake alikuwa anamtazama mpendwa wake kitandani.

Macho yake yaliyotua katika mwili wa Mitchelle yalimsafirisha mbali kifikra. Kwa muda fulani hivi alikuwa amezubaa kama paa wa mbugani aliyemulikwa na taa kali.

Alimsogelea Mitchelle kwa hatua za haraka.

Alimtazama mwanamke huyo namna alivyotulia akambusu paji lake la uso.

"Nipo hapa, Mitchelle," alinong'ona.

Alimwambia Jennifer ajiandae upesi kwani kuna mahali wanapaswa kuelekea. Ndani ya muda mfupi, Jennifer alikuwa tayari wakaongozana kwa pamoja kwenda nje.

Ferdinand alikuwa amembeba Mitchelle mithili ya mtoto anayedeka kwa mamaye.

Jennifer alimtazama Ferdinand usoni, akamwona mwanaume huyo akiwa anaugulia maumivu. Alitamani kumuuliza lakini alihofia. Aliona sio muda sahihi kwa jambo hilo.

Walijiweka ndani ya gari, wakaondoka kuishika njia kuu. Walielekea upande wao wa kaskazini. Ndani ya muda mfupi waliwasili mbele ya majengo marefu ya kahawia ya 'The Dorothy McGowan Apartment'.

Walishuka, kila kitu katika upesi, wakaingia ndani ya jengo hilo.

Ubaya jengo halikuwa na lifti. Iliwapasa kutembea ngazini wakipandisha kwenda juu.

Ilikuwa ni kazi ya kuchosha mno lakini haikuwa na mdhamana. Kikombe hiki kilikuwa hakiepukiki.

Ferdinand, huku akiwa anaugulia maumivu yake makali, alitupa miguu yake kwa mikupuo kupandisha ngazi mbilimbili. Mikononi amembebelea Mitchelle ambaye mpaka sasa hakuwa amejigusa kwa namna yoyote ile.
Alikua ametulia tuli, kichwa kikitikisika kila ngazi inaporukwa. Mdomo wake ulikuwa umeachama. Macho yake yamefumba.

Nyuma ya Ferdinand, Jennifer alikuwa anakazana kweli kuendana na kasi ya mwanaume huyo.

Jasho linamtiririka. Miguu inamvuta. Mara kadhaa alikuwa anasimama ili avute pumzi. Moyo wake ulipiga sana.


***


East Hampton, New York.


Saa nane ya usiku huo.


"Hapana, Bryson!" Mwanamke alifoka. "Siwezi kukuelewa kwenye hili. Sijawahi kuona kazi ya namna hii maishani mwangu. Kazi gani hiyo ya kukurudisha nyumbani saa nane?"

Sauti kali ya mwanamke huyo ilipenya vizuri kwenye mazingira tulivu ya usiku. Japo Bryson alimsihi apunguze, ni usiku mkubwa huu na watu wamelala, bado hakufanikiwa.

Mwanamke alishindwa kumudu jazba yake. Macho yalikuwa yamemtoka, koo likisimamisha mishipa. Alibweka kwelikweli.

Hata mtu angalisimama barabarani, angalisikia yote haya yanayoendelea. Shukrani ni kwamba nyumba hii ilikuwa pweke. Majirani walikuwa katika umbali wa kutosha kuwapatia faragha waliyohitaji.

Bryson, kwa kutumia utashi wake wote, alijaribu kumweleza mkewe mambo yaliyotukia ofisini katika kweli kabisa Namna gani alivyopoteza muda mwingi kungoja kazi muhimu ambayo kamwe haikufika, lakini kadiri bwana huyo alivyoeleza, ndivyo alivyozidi kumtengenezea mke wake maswali mengi.

Ndivyo alivyozidi kuzamia kwenye matope.

Ni kazi gani muhimu iliyokuwa inangojewa mpaka usiku huu mkubwa? Tangu lini ratiba na masaa ya kazi yamebadilika kiasi cha kumngoja mteja wa muda wowote? Ni mteja gani huyo? Kwanini hakuwasiliana na mteja huyo ili kama ana udhuru aondoke mapema?

Kati ya hayo yote, Bryson alishindwa kujibu hata moka kwa ufasaha. Yalikuwa ni maswali magumu kwake kwani kila jibu lilikuwa ni kueleza makubaliano ya siri ambayo hakutaka kumjuza mkewe.

Badala yake aliendelea kusihi tu mkewe amwamini. Hana nia mbaya. Yote anayofanya ni kwaajili ya mustakabali wa familia yao, kitu ambacho kilikuwa ni kigumu kuingia kichwani mwa mwanamke huyu. Ndani ya akili yake aliunganisha vitu vingi ambavyo vilizidi kumnyima imani kuanzia siku ile alipomkuta mumewe yu sebuleni akiyavuta masigara mengi.

Mambo hayakuwa sawa. Hakuwa amekosea. SIRI zilianzia pale.

Bryson kuchelewa nyumbani, kutokumtimizia mahitaji yake nyakati fulani za usiku, kupunguza muda wake wa kuwa na watoto. Vyote hivyo vilianzia siku ile.

Alitamani sana kujua kinachoendelea. Alitamani pia kumjua mwanamke aliyekuwa anawasiliana na mumewe nyakati za usiku hivi majuzi. Kitu pekee alichokuwa anakijua kuhusu mwanamke huyo ni jina lake.

Alikuwa anaitwa Hilda.

Alimsikia mumewe akimtaja kwenye maongezi yao.

Maongezi gani ya kazi usiku hivyo?

Mwanamke huyo, akiwa amefura, aliukwapua mto kitandani. Alimuaga mumewe anaenda sebuleni. Bryson alijaribu kumzuia kwa kumshika mkono, ila mwanamke aliuchoropoa akatoka zake.

"Siku utakaponieleza, tutalala wote!"

Alisema akiufungua mlango.

Alihamaki alipokutana uso kwa uso na watoto wake wawili wakiwa wamesimama kando ya mlango.

Moyo wake ulipasuka kiasi kwamba aliusikia hadi wenye ngoma zake za masikio.

"Cecy ...Cellina ..." aliita akiigiza tabasamu. Nyuso za watoto zilikuwa zimenywea. Cellina alikuwa analengwa na machozi.

Watoto hao waliokuwa wamevalia nguo nyepesi za kulalia, mikononi mwao walibebelea midoli.

"Watoto, mbona hamjalala mpaka saa hii?"

Badala ya kujibu, watoto walilia. Waliingia ndani ya chumba cha wazazi wao, wakikatiza pembeni ya mama ambaye alikuwa amesimama akiwatazama.

Walimwendea baba yao wakamkumbatia. Baba aliwabembeleza akijaribu kuwaambia hamna kitu kilichotokea. Yeye anawapenda na mama anawapenda sana. Hawana haja ya kuhuzunika.

Kidogo watoto walilala, baba yao akawalaza pembeni yake.

Kwa muda alisahau kama ana mke. Alijilaza hapo kwa amani pembeni ya watoto wake wakati mkewe akiwa sebuleni kwenye kiti, kichwa kipo juu ya mto mlaini.

Mwanamke huyo aligeuka huku na kule. Si mumewe aliyekuwa anamuwazia hivi sasa bali wanawe.

Alihofia juu ya afya yao. Alijilaumu kupaza sauti kiasi cha kuwatia hofu watoto.

Aliomba Mungu kuwa yote yawe sawa. Tabu anazopata na hao watoto ni kitu asichotaka kukiona kabisa. Ni mateso.

Haikupita muda, mume wake alifika hapo sebuleni akamsisitizia jambo hilohilo alilokuwa analifikiria. Afya ya watoto.

Alimweleza kwa ukali mkewe kuwa matatizo yao yasije yakapelekea majanga watakayoshindwa kuyamudu. Na endapo basi majanga hayo yakitokea, basi afahamu hatomsamehe kamwe.

"Wanaendeleaje? ... wako vizuri sio?"

Macho ya mama yalijawa na hamu kubwa. Alimtazama mumewe kwa butwaa la mawazo.

"Ndio," Bryson alimjibu. "Mapigo yao ya moyo yako kawaida tofauti na nilivyowapokea hapo awali. Nadhani kila kitu kipo sawa."

Mama alishusha pumzi akiuweka mkono wake kifuani.


***


Bronx, New York. The Dorothy McGowan Apartment.


Saa kumi alfajiri.


Dr. Lambert alivua 'gloves' zake nyeupe alafu akatengenezea miwani yake usoni.

Alikuwa amevalia shati jeusi la mikono mirefu, suruali ya kitambaa na viatu vyeusi vya ngozi. Hapa alipokuwapo palikuwa ni maabara yake binafsi ndani ya makazi yake ya kila siku.

Ni mahala padogo, chumba tu, lakini pamepangiliwa kwa ustadi wa hali ya juu. Mbali na mabenchi imara na mazuri yenye 'masink' ya kutosha, pia ukutani kulitumika kama sehemu ya hifadhi ambapo 'handles' nyingi za kisasa zilikuwa zinaning'inia zikiwa zimebeba vitu kadha wa kadha.

Mbali na hayo kulikuwa na pazia kubwa la buluu lililoning'inia toka kwenye machuma yenye matairi kwa chini yake.

Pazia hizo zilikuwa zimetenganisha chumba hiki kwenye magawio mawili; moja huku Dr. Lambert alipo kwa sasa na pili kule ambapo mwili wa Mitchelle ulikuwa umehifadhiwa.

Mwili huo ulikuwa umeveshwa gauni jeupe na umefunikwa na shuka jeupe pia. Umelala kifudifudi.

Dr. Lambert alipovua gloves zake, alirejea sebuleni ambapo alikutana na Ferdinand na Jennifer waliokuwa wanamgoja kwa takribani lisaa sasa.

Walimtazama bwana huyo kwa hamu ya kusikia neno lolote la faraja toka kwake.

Mzee huyo aliwatazama, mmoja baada ya mwengine, kwa macho ya upole kisha akashusha pumzi ndefu kwa pua yake.

Alifungua kifungo cha shati kinachokaba shingo yake alafu akaupumzisha mgongo wake kwenye kiti.

"Nadhani kila kitu kimeenda sawa," aliwatoa hofu kwa sauti yake ya ukombozi.

Kufumba na kufumbua matabasamu yalirejea kwenye nyuso zao. Hawakuamini hizo habari. Ilikuwa ni kama mpotea baharini aliyeona kisiwa hatimaye.

Dr. Lambert alienda mbali zaidi kwa kuwaeleza kilichotokea ya kwamba Mitchelle alikuwa ameingiziwa dawa sehemu ya mwili wake ambayo haikuwa sahihi lakini hilo halikuwa tabu sana kwani mwili wake ulikuwa unaweza kuhimili pasipo na tatizo, shida ilikuja pale muda ulipogeuka kwenda siku nyingine wakati mwili huo ukiwa haujapata 'antidote'.

"Kama ingefikia nusu ya siku mpya ikiwa bado hajapata dawa, basi tungempoteza kabisa!" alimalizia kwa kusema hilo kisha akakaa kimya.

Ferdinand alimshukuru sana. Alimpatia mkono wa shukrani lakini pia aliahidi kurejesha fadhila kwa kadiri watakavyoweza kwani hicho alichofanya ni kikubwa sana kwao. Ni jambo watakalolienzi siku na siku.

Dr. Lambert alirejesha shukrani, na hakukaa tena hapo sababu muda wa kwenda kazini ulishafika, hivyo kwasababu Mitchelle alikuwa anahitaji mapumziko zaidi, aliwasihi wakae hapo kwa muda wa kama masaa mawili kisha ndo' waende kwa pamoja nyumbani.

Dokta huyo alishuka ngazi akielekea nje ya jengo akiwa na furaha sana. Alikuwa anacheka na kutabasamu mwenyewe kama mwehu.

Hii furaha haikuwa sababu ya kuokoa maisha ya Mitchelle. La hasha. Furaha hii ilikuwa inamjia kwa kishindo kila alipoikumbuka sura ya Ferdinand wakati anamwomba na kumshukuru.

Mwanaume huyo alimeza fahari yake yote akiwa anaomba kama mtoto anayetaka kuadhibiwa na mama yake.

Kwa Dokta hili lilikuwa ni la kumfurahisha sana nafsi yake.

"Naomba umsaidie ... naomba tafadhali ... niko chini ya miguu yako ..." Dr. Lambert aligiza namna Ferdinand alivyokuwa anaomba kisha akaangua kicheko.

"Si unajijkutaga mwamba? ... umwamba wako uko wapi sasa unaomba mpaka makamasi?" Alicheka tena. "Nilikuambia nitakufunza somo. Umeona sasa? ... bila shaka utakuwa na adabu kuanzia sasa ... mapembe nimeyakata!"

Mpaka anafika nje, meno yake yalikuwa yanasabahi kana kwamba anafanya tangazo la dawa ya meno. Alihisi vema na nafsi yake.

Alitoa simu yake mfukoni akapiga namba fulani. Ndani ya muda mfupi taksi ilifika mbele ya jengo, akakwea na kuanza safari ya kuelekea kazini

Kabla hajafika mbali, alipiga tena simu kwa mara ya pili. Muda huu simu ilivyopokelewa alisema;

"Ndio, boss."

Maongezi yaliendelea, lakini mengi yake yakiwa ni kukubali na kuitikia. Yalipokoma, alirejesha simu mfukoni aka-relax.

Masaa mawili yalipotimia, kama vile walivyoelekezwa, Ferdinand akiongozana na wenzake wawili; Jennifer na Mitchelle walitoka ndani ya makazi ya Dr. Lambert kufanya jitihada za kuelekea nyumbani.

Majira yalikuwa ni saa kumi na mbili ya asubuhi.

The Dorothy Apartment ilikuwa imechangamka. Watu walikuwa wanapita huku na kule katika mihangaiko ya kwenda kazini.

Ferdinand aliyekuwa amevalia kapelo kwa ajili ya kujificha, alikuwa ameuweka mkono wa Mitchelle begani mwake, akimsaidia mwanamke huyo kutembea.

Alikuwa amerejesha fahamu zake lakini nguvu bado hakuwa nazo. Macho yalikuwa yamemlegea. Kichwa chake amekiegemeza kwenye bega la Ferdinand.

Kwa taratibu walishuka ngazi za jengo hili, wakiongozana na Jennifer.

Walienendea kwenye gari lao wakaondoka. Walipofika, Mitchelle alipelekwa chumbani apumzike, Jennifer na Ferdinand wakajiweka sebuleni.

Hakika ilikuwa usiku wa kipekee kwa wote. Kila mmoja alikuwa na la kusimulia lakini kwa Jennifer habari ilikuwa kubwa zaidi. Alihisi amechomoza toka jehanamu.

Hawajakaa hapo sana, Mitchelle alifika akitaka kuungana nao. Alisema amechoka kujilaza, anahisi atakuwa vema endapo akiutumikisha mwili wake zaidi.

Alikuwa mchangamfu japo hakuwa na nguvu za kutosha. Muda mwingi alikuwa anawatazama wenzake wakiongea huku yeye akitabasamu na kuonyesha macho ya kuvutiwa na maongezi.

Kitambo kidogo aliona ni muda muafaka wa kuuliza Ferdinand juu ya kilichomtokea usiku uliopita kiasi kwamba hakuwa anapatikana wala hakupeleka kazi aliyotakiwa.

Walipofika hapo, Ferdinand aliikunja sura yake. Kwa kitambo hiko akawa amepoteza furaha aliyokuwa nayo muda si mrefu uliopita.

Alimweleza Mitchelle yote, mwanzo mpaka mwisho, yaliyomsibu. Namna gani alivyokutana na mtu anayemfuatilia, mpaka pale walipokutana katika kombati.

Kwa maelezo ya Ferdinad mtu huyo alikuwa na nguvu mno na mwepesi wa kutumia akili. Alitumwa kumuua na alikuwa anamfahamu fika.

"Alinipiga risasi ya kifua. Hakujivuta wala kujiuliza mara mbili kufyatua bunduki. Ndani ya muda mfupi nikapoteza fahamu yangu. Nadhani alijua amemaliza kazi."

Mitchelle na Jennifer walimtazama Ferdinand kwa macho ya taharuki. Jennifer alipata majibu sasa ni nini kilikuwa kinamfanya mwanaume huyo augulie maumivu alipokuwa anambeba Mitchelle.

Lakini zaidi alipatwa na maswali mengi sana kuhusu watu hawa wawili. Maswali ambayo alikuwa anayaulizia ndani ya kifua chake.

Huyu mwanamke nilimshuhudia kwa macho yangu akiwa ahemi. Mapigo yake ya moyo yamesimama kabisa na mwili umekuwa wa baridi, ila hivi sasa yu hapa amerudi kwenye uhai, anaongea na kutabasamu.

Huyu mwanaume naye, kumbe usiku alikumbwa na maswahibu mpaka akapigwa risasi kifuani. Risasi iliyopenya na kuishia kumwondolea ufahamu tu badala ya uhai. Sasa hivi yupo hapa anaongea na kuyajenga.

Mambo hayo yalimfanya Jennifer asisimkwe na vinyweleo pale alipoyafikiria. Kwa muda fulani akili yake ilipotea katika mazingira haya akazama kwenye dimbwi la mawazo.

Alirudi kwenye ufahamu wake aliposikia Mitchelle akimuuliza Ferdinand;

"Na vipi kuhusu microchip ya dokta?"

Ferdinand alitikisa kichwa chake akasema alipoamka hakupata kuona mzigo huo. Ulikuwa tayari umechukuliwa.

"Serious?" Mitchelle aliuliza akiyatoa macho yake madogo.

Ferdinand hakujibu, badala yake alitikisa kichwa akatazama chini.


***
 
Back
Top Bottom