Tuitazamane Ilani ya ukomunisti(The communist manifesto)

Red Giant

JF-Expert Member
Mar 9, 2012
15,658
20,890
Pengine ukitoa Biblia na Quran, hakuna kitabu kingine kilichokuwa na impact kubwa katika maisha ya watu kama The communist manifesto. Miaka ya katokato ya 1800 wakomunisti ndiyo walikuwa magaidi wa enzi hizo. Basi katika mikutano yao ya siri wakampa kazi bwana Karl Marx kuandaa ilani yao ambayo itakuwa muongozo kwa wakomunisti wote. Basi Marx na mhisani wake, Friedrich Engels wakaandaa ilani hiyo.

Ni moja ya vitabu vilivyofasiriwa sana duniani. Nafikiri kwa nchi yetu ambayo tumetoka, au bado ni ya kijamaa tulitakiwa tuwe na fasiri ya kitabu hiki zamani sana. Maana hiki ndiyo msingi wa ujama duniani.
Kina sehemu nne. Si kirefu lakini najua watu humu si wavivu kusoma makala ndefu.

UTANGULIZI​

Kitabu hiki ni fasiri ya kitabu(makala) “The Communist Manifesto” Kilichoandikwa na wanafalsafa wa kijerumani, Karl Marx na Friedrich Engels mwaka 1848. Kwa ufupi, kinazungumzia misuguano ya kitabaka katika jamii, matokeo yake, kukomeshwa kwake na nafasi ya ukomunisti katika hayo yote.

Kabla ya kuanza kusoma ni vizuri ukajua maneno/fasiri hizi.

  • Nguvu za uzalishaji(Productive forces)-Muunganiko wa njia za uzalishaji mali kama ardhi, mashine, miundombinu nk.
  • Zama za kati(Medieval/Middle ages)-Kipindi kutoka karne ya 5-15 A. D huko Ulaya.
  • Utawala wa wateule(Aristocracy)-Utawala wa wachache wanaosemwa kuwa ni wa uzao wa nasaba bora(Nobles). Aina hii ilifanyika sana kwenye zama za kati.
  • Ukabaila(Feudalism)-Mfumo wa uchumi ambao kunakuwa na mabwana na watwana. Ulikuwepo sana kwenye zama za kati.
  • Kazi ya ujira(Wage labour)-Kazi ya kibarua
  • Wahafidhina(Conservatives/Reactionaries)-Watu wanaopinga mabadiliko, Reactionaries wakiwa wahafidhina wenye msimamo mkali wakitaka mambo kurudi kama zamani.
  • Wanamageuzi(Reformists)-Watu wanaotaka mageuzi lakini si mabadiliko


ILANI YA UKOMUNISTI​

  • ILANI YA CHAMA CHA KIKOMUNISTI
  • KUNA PEPO linaisumbua Ulaya—Pepo la Ukomunisti. Mataifa yote yenye nguvu toka zamani katika Ulaya yameungana katika ushirika mtakatifu ili kulikemea na kulifukuza pepo hilo: Papa na Czar, Matternich na Guizot, wenye itikadi kali wa Ufaransa na mashushushu wa Ujerumani.
  • Ni chama gani cha upinzani kimewahi pigiwa kelele na wapinzani wake walio madarakani kama chama kikomunisti? Wapi ambapo upinzani unarushiana shutuma na kukashfiana kuwa wakomunisti dhidi ya vyama vingine vya upinzani na dhidi ya adui zao wa kihafidhina?
  • Mambo mawili yanatokea kutokana na ukweli huo.
  • Tayari mataifa yenye nguvu ya Ulaya yanautambua ukomunisti kuwa nao ni chombo chenye nguvu.
  • Ni wakati muafaka kwa wakomunisti kutangaza waziwazi duniani maono yao, malengo yao, tabia zao, na kukabiliana nah ii hekaya ya kitoto juu ya Pepo la Kikomunisti kwa Ilni ya Chama chao.
Kufikia lengo hili, wakomunisti kutoka nchi mbalimbali wamekusanyika jijini London, na wameandika Ilani. Ilani hiyo itachapishwa katika lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kiitaliano, Ki-Flemish na Ki-Danish



  • MABEPARI NA MAKABWELA
Historia yote ya jamii iliyopo ni historia ya misuguano ya kitabaka.

Watu huru na watumwa, watu wa tabaka la juu na wa tabaka la chini, mabwana na watwana, wataalamu wakuu na wasaidizi wao. Kwa lugha nyingine, wakandamizaji na wakandamizwaji, wamekuwa wakikabiliana, wakipigana vita siku zote, wakati mwingine vya wazi na wakati mwingine vya siri. Vita ambayo mara zote imemalizika kwa mapinduzi yanayojenga jamii mpya, au maangamizi ya pamoja ya matabaka yanayopambana.

Katika nyakati za mwanzo za historia, tunaona kuwa karibu sehemu zote kulikuwa na mpangilio tata wa jamii katika vitengo mbalimbali, ikiwa imepangwa katika madaraja mbalimbali ya kijamii. Katika dola ya kale ya Roma kulikuwa na tabaka la watu wa uzao bora, mashujaa, masikini na watumwa; katika nyakati za kati kulikuwa na makabaila, vibaraka, wataalamu wakuu, wasaidizi wa wataalamu, wanafunzi, watwana; na kariribu ndani ya matabaka yote haya kulikuwa na madaraja zaidi.

Kwenye jamii ya kisasa ya kibepari, ambayo ilitokana na mabaki ya mfumo wa ukabaila, misuguano ya kitabaka bado haijakoma. Ulichofanya ni kuanzisha matabaka mapya, mifumo mipya ya ukandamizaji, aina mpya ya mapambano mahali pa ile ya zamani.

Zama zetu hizi, zama za kibepari, zina sifa ya pekee sana: zimerahisisha misuguano ya kitabaka: jamii nzima inagawanyika kwa kasi sana kutengeneza kambi mbili kuu zinazokinzana, katika matabaka mawili makubwa yanayokabiliana: Mabepari na makabwela.

Kutoka kwa watwana wa nyakati za kati, walitoka watu wa tabaka la kati walioishi kwenye miji ya mwanzo-mwanzo. Kutoka kwa watu hawa wa tabaka la kati ndipo ubepari wa mwanzo ulianza kuchipuka.

Kugunduliwa kwa bara la Amerika na meli kuweza kuzunguka kusini mwa Afrika, kulifungua maeneo mapya ya kukuza ubepari. Soko la India na China, ukoloni kwenye bara la Amerika, biashara na makoloni, kupanuka kwa namna ya kufanya biashara na kuongezeka kwa bidhaa kwa ujumla, kulivipa biashara, usafiri wa majini na viwanda msukumo ambao haujawahi shuhudiwa hapo kabla, na matokeo yake chachu za kimapinduzi zikapata kukua kwa kasi ndani ya jamii ya kikabaila iliyoanza kudhoofika.

Mfumo wa viwanda wa kikabaila, mfumo ambao uzalishaji viwandani ulihodhiwa na vikundi vya watu wachache, haukufaa tena kwa mahitaji makubwa ya masoko mapya. Mfumo mpya wa uzalishalishaji ukachukua mahali pake. Wataalamu waliohodhi uzalishaji walisukumwa pembeni na watu wa tabaka la kati walioanza uzalishaji; mgawanyo wa kazi ambao ulikuwepo kati ya kikundi na kikundi cha wataalamu hao ulipotea mbele ya wazalishaji mmoja-mmoja.

Wakati huohuo, masoko yalizidi kukua. Hata wazalishaji hawa nao hawakuweza kutosheleza mahitaji yake. Hivyo basi, zikagunduliwa mashine za mvuke ambazo zilileta mapinduzi ya uzalishaji viwandani. Kazi ya uzalishaji ikachukuliwa na viwanda vikubwa vya kisasa, sehemu ya wazalishaji mmojammoja wa tabaka la kati ikachukuliwa na mamilionea wenye viwanda, viongozi wa jeshi lote la viwanda, mabepari wa kisasa.

Mfumo wa kisasa wa viwanda ndiyo umeanzisha soko la kidunia, na mwanzo wake ilikuwa ni kugunduliwa kwa bara la Amerika. Soko hili limesababisha ukuaji mkubwa sana wa biashara, usafiri wa baharini na mawasiliano ya nchi kavu. Na kadri biashara, usafiri wa majini na wa reli ulivyosambaa, ndivyo ubepari ulivyozidi kuendelea, mtaji wake ukiongezeka huku akisukumia mbali matabaka yote yaliyokuwepo toka zama za kati.

Kwahiyo tumeona jinsi ambavyo ubepari wa kisasa nao ni zao la mambo yaliyotokea kwa kipindi kirefu, matokeo ya mapinduzi mengi juu ya mifumo ya uzalishaji mali na biashara.

Kila hatua ya ukuaji wa mabepari iliambatana na ukuaji wa nguvu za kisiasa za tabaka hilo. Tabaka lililokuwa likikandamizwa na mabwana wa kikabaila; wakiwatumikia makabaila na wafalme, na wakati mwingine wakitumiwa na wafalme waliotaka kujilimbikizia madaraka kuwadhibiti watu wa nasaba bora. Kiukweli wao ndiyo walikuwa msingi wa tawala kubwa za kifalme.

Hatimaye mabepari, toka kuanzishwa kwa mfumo wa kisasa wa viwanda na soko la kidunia, wamefanikiwa kuteka nguvu za kisiasa za serikali za kisasa za kuchaguliwa. Serikali za kisasa si kitu kingine zaidi ya kamati tu za kusimamia masuala ya mabepari.

Kihistoria, mabepari ndiyo waliofanya mapinduzi makubwa zaidi.

Kila mara ubepari ulipopata nguvu, ulihakikisha umeikomesha mifumo ya uhusiano ya kikabaila. Bila huruma umevunja mfumo wa mahusiano wa hovyo wa kikabaila ambao mtu alijifunga kwa yule aliyemuona kuwa “Kiasili ni bora zaidi yake,” na uhusiano pekee uliouacha kati ya mtu na mtu ni uhusiano wa kimaslahi, uhusiano katili wa “malipo taslimu.” Umezamisha hamu ya watu juu ya dini, utauwa, huruma na kuridhika ndani ya maji baridi ya kujikweza.

Unapima thamani ya mtu kwa pesa, na mahali pa uhuru mwingi wa asili umeweka uhuru mmoja usiopatana na akili—Biashara Huria. Kwa maneno mengine, sehemu ya unyonyaji uliojivika kilemba cha dini na viini macho vya kisiasa, umeweka unyonyaji wa wazi, katili na usiojua aibu.

Ubepari umezivua vilemba vyake taaluma zote ambazo zimekuwa zikiheshimiwa na kuthaminiwa sana. Umewabadilisha wanasheria, madaktari, makuhani, washairi na wanasayansi kuwa wafanyakazi wa kulipwa mishahara.

Ubepari umevunja uhusiano wa kifamilia uliojengwa na hisia kuwa uhusiano wa kipesa tu.

Ubepari umeonyesha jinsi ulivyopita nguvu na ukatili vilivyokuwepo kwenye zama za kati, zama ambazo wapinga wabadiliko wanazihusudu sana, wakiona ni sifa jinsi walivyoisha kwa anasa na kizembe. Ubepari ndiyo umekuwa wa kwanza kuonyesha kile kinachoweza kutimizwa na binadamu. Umefanya maajabu ambayo yanaacha mbali mapiramidi ya Misri, mifereji ya Roma, na mahekalu ya kigothic; umefanya safari za uvumbuzi ambazo zinafanya uhamaji wote wa mataifa uliowahi kutokea hapo kabla kuwa si kitu.

Ubepari hauwezi kuwepo bila kuhakikisha kuwa muda wote unafanya mapinduzi ya nyenzo za uzalishaji, na hivyo uhusiano katika uzalishaji, na kwa ujumla uhusiano katika jamii. Kulinda njia za zamani za uzalishaji, bila kuzibadili, ilikuwa ndiyo kigezo cha kwanza cha uwepo wa matabaka ya uzalishaji ya kale. Mapinduzi katika uzalishaji yasiyokoma, kuvuruga hali za kijamii utakavyo, na kutotabirika kwa wakati ujao na pilikapilika ndiko kunaitofautisha zama ya ubepari na zilizopita.

Kuhusiana kwao kusikobadilika, maoni yao, kunyanyaapaana na mambo yao mengine ya kale yamefagiliwa mbali. Na mapya yanayoundwa yanapitwa na wakati hata kabla hayajakomaa. Yote yaliyo imara yanayeyuka hewani, yote ambayo ni matakatifu yanadharauliwa, na hatimaye binadamu analazimika kukabiliana na hali halisi ya maisha yake na uhusiano wake na jamii yake.

Mahitaji ya bidhaa zake kwenye soko linalokua kila siku yameutawanya ubepari duniani kote, unalazimika kujishikiza kila sehemu, umetengeneza mtandao kila sehemu.

Kwa kutumia soko la dunia, ubepari umefanya uzalishaji na utumiaji wa bidhaa kuwa sawa kwenye kila nchi. Wapinga mabadiliko wamepata aibu kubwa maana ubepari umetoa chini ya miguu yao utaifa ambao walikuwa wamesimama juu yake.

Viwanda vyote vilivyoanzishwa na taifa hapo zamani vimeuliwa au vinauliwa kila siku. Vinang’olewa na viwanda vipya, ambavyo uwepo wake umekuwa suala la kufa na kupona kwa mataifa yote yaliyostaarabika, viwanda ambavyo havitumii tena malighafi za ndani, bali zilizotolewa kwenye maeneo ya mbali kabisa; viwanda ambavyo bidhaa zake zinatumika si tu nyumbani, bali kwenye kila pembe ya dunia.

Badala ya mahitaji ya zamani, yaliyotimizwa na uzalishaji wa nchi husika, tunapata mahitaji mapya, yakihitaji kutimizwa kwa uzalishaji unaofanyika kwenye nchi za mbali. Mahali pa nchi kujitenga na kujitegemea, kuna mahusiano kuelekea kila upande, kutegemeana kwa mataifa ya dunia nzima. Kwenye bidhaa na kwenye ujuzi vilevile. Ujuzi uliozalishwa na nchi moja huwa mali ya wote. Na suala la nchi kuegemea upande mmmoja linazidi kuwa gumu kila siku, na kutoka kwenye kazi za uandishi nyingi za kitaifa na kienyeji, yanaibuka maandiko ya dunia nzima.

Ubepari, kwa kuboresha njia za uzalishaji mali kwa kasi, kwa mifumo ya mawasiliano iliyoboreshwa sana, umezivuta nchi zote, hata zile za kishenzi kabisa kwenye ustaarabu. Bei ya chini ya bidhaa zao ni mizinga mizito ambayo inapiga kuta zote za wachina, kwa kutumia hiyo, unazimisha chuki kali za washenzi dhidi ya wageni.

Unalazimisha nchi zote, kwa kitisho cha maangamizi, kufuata njia za uzalishaji za kibepari; unazilazimisha kukubali kitu unachoita ustaarabu, yaani nao kuwa mabepari. Kwa maneno mengine, unatengeneza dunia kwa mfano wake.

Ubepari umeziweka nchi kwenye utawala wa miji. Umetengeneza majiji mengi, umeongeza wakazi wa mijini kwa kiwango kikubwa sana ukilinganisha na wale wa vijijini, na kwa namna hiyo, imeokoa sehemu fulani ya watu kutoka kwenye ujinga wa maisha ya vijijini. Kama tu ulivyofanya nchi itegemee miji, ndivyo ulivyofanya nchi za kishenzi na zile zilizostaarabika kidogo zitegemee zile zilizostaarabika, nchi za wakulima kutegemea za mabepari, Mashariki wategemee Magharibi.

Ubepari kila siku unazidi kukusanya pamoja, watu, njia za uzalishaji na mali. Umekusanya watu, na umeweka mali na njia za uzalishaji kwenye mikono ya wachache. Matokeo yasiyoepukika ya jambo hili yalikuwa ni wachache kuhodhi siasa. Mikoa huru au inayohusiana kwa kiasi fulani. Yenye matakwa, sheria, serikali na mifumo ya kodi tofauti, inakusanywa pamoja kuwa nchi moja, yenye serikali moja, sheria moja, na matwakwa sawa ya kitaifa, mipaka na na ushuru wa forodha mmoja.

Ubepari, ndani ya utawala wake wa miaka mia moja tu, umetengeneza nguvu kubwa ya uzalishaji kuliko vizazi vyote vilivyopita vikiwekwa pamoja. Utawala wa binadamu dhidi ya nguvu za asili, matumizi ya mashine, kutumia kemia kwenye viwanda na kilimo, usafiri kwa kutumia injini za mvuke, reli, telegraphs, kusafisha mabara mazima-mazima kwaajili ya kilimo, kutanua na kujenga mito kwaajili ya usafiri, jamii nzima ya watu imeamshwa kutoka usingizini—ni watu gani wa kale walikuwa hata na wazo kuwa nguvu kazi kubwa hivyo ya uzalishaji imelala kwenye mapaja ya jamii ya wafanyakazi?

Kwahiyo tunaona kuwa: njia za uzalishaji na biashara, vitu ambavyo ubepari umejijenga juu yake, vilianzishwa wakati wa ukabaila. Katika hatua fulani ya kukua kwa njia hizi za uzalishaji na biashara, wakati ambao biashara, kilimo na uzalishaji wa viwandani vilifanyika chini ya mazingira ya kikabaila; ikatokea kuwa mazingira hayo hayaendani na nguvu za uzalishaji zilizokwisha endelea mbele, yakawa ni kikwazo. Kukawa na uhitaji wa kukomesha ukabaila. Ukakomeshwa kabisa.

Sehemu yake ukatokea ushindani huru, ukiambatana na katiba ya kijamii na kisiasa ili kuendana nao, na uchumi na siasa zilizoegemea tabaka la mabepari.

Harakati kama hizo zinaendelea mbele ya macho yetu. Jamii ya kisasa ya kibepari, na uhusiano wake na uzalishaji, biashara na mali, jamii ambayo imeziita pamoja na kwa ukubwa sana njia za uzalishaji na biashara, imekuwa kama mchawi ambaye hawezi tena kudhibiti nguvu za kuzimu alizoziita.

Kwa watu wengi muongo mmoja wa viwanda na biashara si kitu bali historia ya uasi nguvu za kisasa za uzalishaji dhidi ya mazingira ya kisasa ya uzalishaji, dhidi ya suala umiliki mali na sheria za kibepari , vitu ambavyo ni nguzo ya uwepo wake. Inatosha kutaja migogoro mikubwa ya kibiashara ambayo hujirudiarudia inavyouhukumu ubepari, na kila wakati ikizidi kutishia jamii nzima ya kibepari.

Na kwenye migogoro hii, sit u bidhaa za sasa, bali hata nguvu za uzalishaji mali zilizotengenezwa huko nyuma huharibiwa. Kwenye migogoro hii huibuka gonjwa ambalo hapo zamani lingeonekana kitu cha ajabu sana—gonjwa la kuzalisha kupita kiasi. Ghafla, jamii inajikuta imerudishwa kwenye ushenzi; inaonekana kama janga la njaa, vita ya dunia vimekata ya njia zote za kijitegemea; uzalishaji na biashara huonekana kama vimekomeshwa; kwa nini? Kwa sababu kuna maendeleo kupita kiasi, kuna njia nyingi za kuendesha maisha kupita kiasi, viwanda vingi kupita kisai, biashara nyingi kupita kiasi Nguvu za uzalishaji kwenye mikono ya jamii haziendelezi tena mazingira ya uwepo wa ubepari; kinyume chake, zimekuwa na nguvu sana hivyo haziwezi fanya kazi chini ya mazingira hayo, hivyo yanakuwa ni kikwazo, na mara tu zinapovishinda vikwazo hivyo, vurugu hutokea kwenye jamii ya kibepari, zikihatarisha mali za mabepari.

Mazingira ya uwepo wa ubepari ni uwanja mdogo sana kuweza kumudu utajiri unaotengenezwa nao. Na ubepari unaishindaje migogoro hii? Njia moja ni kwa kuharibu nguvu nyingi za uzalishaji; na nyingine ni kwa kuteka masoko mapya, na kwa kuhakikisha wanayashikilia yale ya zamani vilivyo. Hivyo tunaweza sema; unatatua migogoro kwa kutengeneza njia kwaajili ya matatizo mengine makubwa na mabaya zaidi, na kwa kupunguza njia za kuzuia migogoro hiyo.

Silaha ambazo ubepari ulitumia kuangusha ukabaila, sasa zimewageuka.

Si tu kwamba ubepari umetengeneza silaha ambazo zinauua; lakini pia umekusanya watu wa kutumia silaha hizo—tabaka la wafanyakazi wa kisasa—makabwela.

Kadri ubepari unavyokua; mfano kimtaji, ndivyo tabaka la makabwela nalo linavyozidi kukua. wafanyakazi wa kisasa—tabaka la vibarua, ni tabaka la watu ambao wanaishi iwapo tu wanaweza kupata kazi, na kazi zilizopo ni zile tu ambazo kwa kuzifanya wanaongeza mtaji. Vibarua hawa, ambao wanajiuza polepole, ni bidhaa kama tu kitu kingine chochote cha kibiashara, na wanaathiriwa na kubadilika-badilika kwa ushindani, na mabadiliko yote ya soko.

Na sababu ya matumizi makubwa ya mashine na mgawanyo wa kazi, kazi za wafanyakazi zimepoteza upekee wake, na matokeo yake furaha yote ya mfanyakazi imepotea. Amekuwa kama sehemu ya mashine. Na kazi anayotakiwa kufanya ni ile rahisi kupita zote, isiyohitaji ujuzi mkubwa na ya kujirudiarudia, hivyo ya gharama ya uzalishaji kwa kumtumia mfanyakazi inakuwa chini, hadi kwenye kiasi kinachomtosha kuishi tu na kuendeleza kizazi chake.

Lakini gharama ya bidhaa, ya hivyo ya nguvu kazi(Nguvu kazi kama bidhaa), ni sawa na gharama ya kuizalishaji wake. Kwahiyo, jinsi kazi inavyochukiza, ndivyo mshahara wake unavyozidi kupungua. Na zaidi, kadri ambavyo matumizi ya mashine na mgawanyo wa kazi unavyoongezeka, pia ugumu wa kazi kwa mfanyakazi huongezeka, iwe kwa kuongeza masaa ya kazi, kuongezeka kwa kazi inayotakiwa kufanywa kwa saa au kwa kuongeza kasi ya mashine na njia nyinginezo.

Mfumo wa kisasa umebadilisha karakana ndogo ya mtu mwenye ujuzi kuwa kiwanda kikubwa cha bepari. Mamia ya wafanyakazi hujazana kwenye kiwanda, wakipangwa kama wanajeshi.

Wakiwa kama makuruta wa jeshi la viwanda, chini ya usimamizi wa maofisa na masagenti. Si tu kuwa ni watumwa wa tabaka la mabepari, na nchi ya kibepari; lakini kila siku, na kila saa wanafanywa watumwa wa mashine, wa wasimamizi, na zaidi; wa bepari mwenye kiwanda. Na kadri ambavyo mfumo huu katili unavyoweka wazi kuwa lengo lake ni kuongeza mapato, ndivyo unavyokuwa mbaya zaidi, na ndivyo unavyozidi kuchukiza na kuudhi.

Kadri ambavyo ujuzi na nguvu ndogo vinapotumika kwenye kazi za mikono, kwa maneno mengine, kadri viwanda vinavyoboreka ndivyo ambavyo kazi za wanaume zinavyochukuliwa na wanawake. Utofauti wa umri na jinsia hauna maana yoyote tena kwenye tabaka la wafanyakazi. Wote ni nyenzo za kazi, gharama zao zikitofautiana kulingana na jinsia na umri wao.

Na mara tu mfanyakazi anapokwisha kunyonywa na bepari, mara tu anapochukua mshahara wake, idara zingine za kibepari nazo humshukia, mwenye nyumba, muuza duka, dalali, nk.

Watu wa tabaka la kati la chini—wafanyabiashara wadogo, wauza maduka, wafanyabiashara wastaafu kwa ujumla, mafundi na wakulima wadogo—hawa wote huzama polepole kwenye ukabwela, kwa sehemu ni sababu mitaji yao midogo haitoshi kumudu namna ambayo shughuli za kisasa zinaendeshwa na huku wakiwekwa pamoja kushindana na mabepari wakubwa, na sababu nyingine ni kuwa, mbinu mpya za uzalishaji hufanya ujuzi wao kuwa si kitu tena. Kwahiyo, makabwela hutoka kwenye matabaka yote ya watu.

Ukabwela hupitia hatua mbali mbali katika kukua kwake. Kuzaliwa kwake ndiyo mwanzo harakati zake dhidi ya ubepari. Mwanzoni, mapambano huendeshwa kibarua mmojammoja, kisha na wafanyakazi wa kiwanda, kisha wafanyakazi wa idara moja kwenye eneo moja, dhidi ya bepari mmoja anayewanyonya. Wanalenga mashambulizi yao, si kwa mazingira ya uzalishaji ya kibepari, bali dhidi ya nyenzo za uzalishaji; wanaharibu bidhaa zilizoingizwa kutoka nje ya nchi, wanavunja mashine vipandevipande, wanachoma moto viwanda, wakitaka kurudisha kwa nguvu hadhi iliyopotea ya mfanyakazi wa zama za kati.

Kwenye hatua hii, vibarua bado wanakuwa ni kundi tu lisiloeleweka, lililotawanyika nchi nzima, likiwa limetenganishwa na ushindani wa wao kwa wao. Na kama kuna sehemu wamejiunga kutengeneza kikundi imara, basi si sababu ya kutaka kwao, bali sababu ya muungano uliofanywa na mabepari ambao ili kufikia malengo yao ya kisiasa, wanalazimika kuwahamasisha na kuwaleta pamoja makabwela, na kwa kipindi fulani wanafanikiwa katika hilo.

Kwahiyo, bado hatuwezi kusema makabwela wameungana, kwenye hatua hii, makabwela hawapigani na adui zao, bali adui wa adui zao, mabaki ya watawala wa kifalme, wamiliki ardhi, mabepari wasio na viwanda, mabepari uchwara. Hivyo harakati zote zinakuwa chini ya mabepari; ushindi wowote unaopatikana ni ushindi wa mabepari.

Lakini kadri ambavyo viwanda vinazidi kukua; si kwamba tu makabwela wanaongezeka; pia wanazidi kuwa pamoja, nguvu zao hukua, na wanaiona nguvu yao hata zaidi. Matakwa na hali ya maisha ya makabwela huzidi kufanywa kuwa za aina moja kadri ambavyo mashine zinavyoua mgawanyo wa kazi, na karibu kila mahali zikishusha mishahara kuwa kima kimoja cha chini.

Kukua kwa ushindani kati ya mabepari na migogoro ya kibiashara inayozalishwa nao, hufanya mishahara ya wafanyakazi ibadilikebadilike hata zaidi. Uboreshaji wa mashine usiokoma; zikizidi kuwa bora kwa kasi kila siku, kunafanya maisha ya makabwela kuwa ya mashaka hata zaidi. Migongano kati ya mfanyakazi mmoja na mwingine na kati ya bepari na bepari, hatua kwa hatua huchukua sura ya mgongano wa kitabaka.

Hivyo wafanyakazi huanza kuunda umoja dhidi ya bepari; wanajiunga pamoja ili kuhakikisha wanapata mshahara mkubwa; wanaunda ushirika wa kudumu ili kuandaa migomo hiyo. Mara kwa kwa mara, hapa na pale, mizozo hii huibuka kuwa ghasia.

Kuna nyakati wafanyakazi huibuka washindi, lakini ni kwa muda tu. Matunda ya kweli ya mapambano yao hayapo kwenye matokeo ya mara moja bali kwenye umoja wa wafanyakazi unaokua kila uchwao. Umoja huu; kwa namna fulani unasaidiwa na njia nzuri za mawasiliano zilizoboreshwa na mfumo wa kisasa wa viwanda, hilo linawezesha wafanyakazi walio kwenye maeneo tofauti waweze kuwasiliana.

Ni kuwasiliana huku tu ndiko kulihitajika ili kuleta pamoja harakati zinazofanana zilizokuwa zinaendelea kwenye maeneo mbalimbali, kuwa harakati moja ya kitaifa kati ya matabaka. Lakini harakati zote za kitabaka ni harakati za kisiasa. Kilichowachukua wafanyakazi wa zama za kati; na barabara zao mbovu, karne kadhaa kufanikisha, makabwela wa sasa, na hasa kwa msaada wa reli; wanafanikisha ndani ya miaka michache tu.

Kitendo cha makabwela kujiunga pamoja kutengeneza tabaka, na baadaye kuwa chama cha siasa, kinavurugwa bila kukoma na ushindani wa wafanyakazi wenyewe kwa wenyewe. Lakini mara zote wanaibuka tena, wakiwa na nguvu, uthabiti na na ukuu zaidi. Hilo hulazimisha matakwa fulani ya wafanyakazi kutambulika kisheria, hasa kwa kutumia fursa ya mgawanyiko baina ya mabepari. Hivyo ndivyo sheria ya masaa kumi ilivyopitishwa Uingereza.

Na kwa ujumla wake, migogoro baina ya matabaka ya zamani, kwa kiasi kikubwa inasaidia kusongesha mbele kukua kwa makabwela. Ubepari unajikuta muda wote ukiwa kwenye mapambano. Mwanzo kabisa, dhidi ya utawala wa wateule(Aristokrasi); baadaye, dhidi ya kundi fulani la mabepari ambao maslahi yao yanapingana na kuendelea kwa mfumo wa viwanda; na muda wote, dhidi ya mabepari wa nchi zingine.

Na katika mapambano yote haya, ubepari unajikuta ukilazimika kukubaliana na makabwela, ukiomba msaada wao, na hivyo kuvuta makabwela kwenye uwanja wa siasa. Kwahiyo, ubepari wenyewe ndiyo unawapa makabwela nyenzo zake za kisiasa na elimu, kwa maneno mengine, unawapa makabwela silaha za kupambana nao.

Zaidi, kama tulivyokwisha ona, sehemu nzimanzima ya tabaka tawala, hasa kutokana na kukua kwa viwanda, wanaangukia tabaka la makabwela, au nafasi zao za saa zipo kwenye kitisho. Hawa huwapatia makabwela maarifa na msukumo mpya.

Na mwisho, wakati ambapo misuguano ya kitabaka inapokaribia mwisho, zoezi la kuvunjika linakuwa linaendelea ndani ya tabaka tawala, ukweli ni kuwa linakuwa linaendelea kwenye jamii nzima, fikiria jinsi ukabwela utakavyokuwa baada ya sehemu fulani ya tabaka tawala kujitenga na kujiunga na tabaka la wanamapinduzi, tabaka ambalo ndilo linaamua mustakabali wa wakati ujao.

Kama tu hapo mwanzo ambavyo sehemu ya tabaka la wateule lilivyoungana na mabepari, basi sasa sehemu ya mabepari inajitenga na kuungana na makabwela, na hasa sehemu ya mabepari ambao ni wanaitikadi, wale ambao wameweza kuelewa jinsi ambavyo harakati na historia huwa vinaenda.

Katika matabaka yote ambayo yanasimama dhidi ya ubepari leo, ni tabaka la makabwela pekee ndilo la kimapinduzi. Matabaka mengine yote hudhoofika na kupotea chini ya mfumo mpya wa viwanda; lakini makabwela wao ni zao muhimu na la kipekee la mfumo huo.

Watu wa tabaka la kati la chini, wazalishaji wadogo, wamiliki maduka, mafundi, na wakulima wadogo nk, hawa wote wanapambana dhidi ya ubepari ili kulinda nafasi zao kwenye tabaka la kati. Hivyo si wanamapinduzi bali wahafidhina. Na hata zaidi, ni wapinga maendeleo, maana wanataka kurudisha nyuma gurudumu la historia.

Na kama wametokea kuwa wanamapinduzi kwa bahati, wanafanya hivyo kwa sababu ya kuogopa uhamisho wa kuwa makabwela unaowakabili, kwa hiyo hawapigani kwaajili ya hali yao ya sasa, bali kwaajili ya manufaa yao ya baadaye. Wanaikimbia sehemu yao na kujiweka sehemu ya makabwela.

Watu hawa ni “tabaka hatari,” uchafu wa jamii, umati unaooza polepole na hivyo kutupwa nje kutoka mtaabaka ya chini kabisa la mfumo wa kijamii wa zamani. Hapa na pale wanaweza kusombwa na harakati za makabwela na hivyo kuingia kwenye mapinduzi; lakini hali ya maisha yao, inawaandaa kuwa chombo cha kuhongwa na hila dhidi ya mapinduzi.

Tunaweza kusema kuwa wale wengi wa jamii zilizopita tayari wameingia kwenye mazingira ya kikabwela. Kabwela hana mali yeyote, uhusiano wake kwa mkewe na watoto wake haufanani tena na ule wa bepari na familia yake; kazi za kisasa za viwandani, utumikishwaji chini ya mtaji, umewaondolea makabwela sifa zote za kitaifa. Hali yao ipo vile vile katika Uingereza na katika Ufaransa, kama ilivyo Marekani ndiyo ilivyo Ujerumani. Kwake yeye; sheria, maadili na dini ni vitu tu vya kibepari, vitu ambavyo nyuma yake kuna maslahi ya mabepari yakivizia.

Matabaka yote ya juu katika historia, yalihakikisha yanalinda hadhi yao kwa kuiweka jamii kwenye mazingira ya kunyonywa. Makabwela hawawezi kuwa mabwana wa nguvu za uzalishaji, isipokuwa kwa kukomesha mfumo uliowanyonya, na hivyo kukomesha kila mfumo wa unyonyaji uliowahi pata kuwako. Hawamiliki kitu chochote cha kukilinda; kazi yao ni kuharibu mifumo yote iliyolinda umiliki mali binafsi.

Harakati zote za wakati uliopita zilikuwa ni harakati za walio wachache, au kwaajili ya maslahi ya wachache. Harakati za makabwela ni harakati za wanaojielewa, harakati huru za walio wengi. Kwaajili ya maslahi ya walio wengi. Makabwela, tabaka la chini kabisa la jamii yetu ya sasa, haliwezi kujiamsha, bila ya tabaka lote la juu linalowakalia kurushwa hewani.

Mwanzoni, harakati za makabwela dhidi ya mabepari, ni harakati za kitaifa. Ukabwela wa kila nchi unatakiwa kwanza kabisa kuweka mambo sawa na ubepari wake.

Katika kuonyesha hatua kuu za ukuaji wa makabwela, tulichunguza vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyojificha ikipamba moto ndani ya jamii ya leo, mpaka pale vita hivyo vinapokuwa mapinduzi ya waziwazi, na ambavyo kungo’olewa kwa ubepari kwa kutumia nguvu kunavyoweka msingi wa utawala wa makabwela.

Hata hivyo, na kama tulivyokwisha ona, kila mfumo wa jamii umekuwa na upinzani wa kati ya tabaka la wanyonyaji na wanaonyonywa. Lakini ili kulinyonya tabaka fulani, hali fulani zinatakiwa kuwekwa ili walau liendelee kuishi katika maisha yao ya kitumwa. Mtwana wa wakati wa ukabaila, aliweza kujiinua na kuwa mshirika wa jumuia, kama tu ambavyo mabepari uchwara, chini ya ukandamizaji wa ukabaila walivyoweza kuwa mabepari kamili.

Lakini kibarua wa kisasa ni tofauti, badala ya kuendelea kadri ambavyo mfumo wa viwanda unavyoendelea, wao wanazidi kuzama chini, chini ya na hali zinazowafaa kuishi. Anakuwa masikini wa kutupwa, na umasikini wa kutupwa unakuwa kwa kasi kuliko idadi ya watu na utajiri. Kufikia hatua hiyo kunakuwa na ushahidi usiyo na shaka, kwamba ubepari hawafai tena kuendelea kuwa tabaka tawala wala kuweka mazingira wayatakayo kwenye jamii kuwa sheria.

Haufai kutawala kwa sababu hauna uwezo wa kuhakikisha maisha ya watumwa wako chini ya mfumo wake wa kitumwa yakiendelea, kwa sababu hauwezi kumsaidia asizame kwenye umaskini wa kutupwa na kumlisha badala ya kulishwa naye. Jamii haiwezi tena kuendelea kuishi chini ya huu ubepari, kwa maneno mengine, uwepo wa ubepari hauendani tena na jamii.

Jambo la muhimu kwa uwepo, na utawala wa tabaka la mabepari ni kuundwa na kukuzwa kwa mtaji; na kwa mtaji ukuzaji wa mtaji hutegemea uwepo wa kazi ya mshahara. Na uwepo wa kazi ya mshahara hutegemea ushindani kati ya wafanyakazi. Ukuwaji wa viwanda, ambao unachagizwa na ubepari. Unatoa utengano wa wafanyakazi unaoletwa na ushindani na kuwafanya washirikiane na kuungana kimapinduzi.

Ukuwaji wa mfumo wa kisasa wa viwanda unaondoa msingi chini ya miguu yake wenyewe, msingi ambao ubepari unazalisha na kupata mali. Hivyo basi, kitu ambacho mabepari wanazalisha kuliko vyote ni kaburi lake wenyewe. Kuanguka kwake na ushindi wa makabwela haviepukiki.
 
Back
Top Bottom