Tatizo la watanzania - tuna matatizo gani?

Kisendi

JF-Expert Member
Jan 29, 2009
699
178
HII si mara yangu ya kwanza kuyakariri na kuyarudia maneno ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anayoyatumia mara kadhaa kuhoji umaskini wa Watanzania umetokana na nini huku tukiwa na rasilimali tele lakini hakuna unafuu wowote wa maisha, hali ni ngumu.

Amediriki kutamka wazi kuwa ni nani aliyewaroga Watanzania mpaka tunashindwa kwenda mbele huku tukiishi kwenye nchi ya maziwa na asali, tukiishi kwenye nchi iliyozungukwa na rasilimali nyingi kila kona na hapo ndipo jibu la wapi tunapopopaswa kujilaumu kunakoanzia.

Kiini cha makala hii ya leo hakuna maana ya kutaka kuwasimanga Watanzania wenzangu ambao wote tupo kwenye adha ngumu ya ugumu wa maisha na ambao leo hii kuna watu wanaoshindwa kunywa chai wakishindwa kununua kilo moja ya sukari ambayo hutengeneza kinywaji cha kila rika hasa kwa watoto wadogo na wazee.

Nchi ikiwa imezungukwa na bahari, maziwa, mito mikubwa, mbuga za wanyama wa kila aina, vito vya thamani, madini ya almasi na dhahabu bila kusahau madini adimu hapa duniani ya tanzanite; vitu hivyo vyote vinatufanya tuitwe maskini wa kutupwa ambao tupo kwenye kundi la watu wa dunia ya tatu.

Tanzania ni nchi ya kujivunia ambayo utalii wa ndani unazidi kukua kutokana na uwepo wa vivutio vikubwa vilivyopo bila kusahau kuwa yapo maeneo ambayo kuna dalili za kuwepo kwa mafuta chini ya ardhi lakini watu wanakufa bila kuona hata tone la mafuta likitoka katika nchi hii.

Utajiri wa Tanzania umeifanya iwe nchi yenye mbuga nzuri na za kuvutia, zenye rutuba zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha masika na kiangazi lakini hakuna tunachoweza kujivunia kwa hilo kwa kuwa wakulima wengi wanategemea mvua badala ya kuwa na miundombinu ya uhakika ya kilimo cha umwagiliaji kutoka kwenye mito na maziwa yaliyopo.

Hii ndio Tanzania ambayo leo hii imevishwa jina zuri na la kupendeza kuwa ni moja ya nchi masikini duniani, ikikaliwa na watu makini,wanaosifika kwa utulivu na amani waliyonayo ambayo inawazuia kusonga mbele na kuendelea kuzalisha kundi la watu masikini kila siku.

Hapo ndipo zinapojitokeza hoja nyingi na hatimaye hata mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali, waziri mkuu anapojiuliza maswali mara kadhaa hivi: “Watanzania tumerogwa, tuna kila kitu, kwa nini hatusongi mbele ni nani anayepaswa kutunasua kutoka hapa tulipo, hivi mchawi wetu ni nani?”

Lazima tujiulize sana na tutafute dawa ya kumjua mtu aliyewaroga Watanzania ilhali wana kila kitu lakini bado wanabaki na sifa ya kuitwa maskini, tatizo ni nini na nani anapaswa kutafuta mwarobaini wa kutibu maradhi haya ya umaskini? Viongozi wakilalamika nani analo jibu muafaka la kumjua aliyeiroga Tanzania.

Wakati tukitafakari na kutaka kujua kiini cha umaskini wetu na matatizo lukuki yanayoikumba jamii lazima ijulikane wazi ni wapi zilipokwama jitihada za kuwasukuma Watanzania hawa ili waweze kuondokana na kadhia mbaya ya umaskini ambayo haipaswi kuonekana au kuwakumba watu hawa.

Watanzania wamelalia mto wa tanzanite, godoro la almasi, shuka la dhahabu, wakinawa maji ya waridi yaliyotulia kwenye bahari na maziwa huku wakiogelea kwenye mito mikubwa na kupumzika chini ya mbuga nzuri za wanyama, kisha hupanda juu ya Mlima Kilimanjaro ili kutukuza utajiri wao waliopewa bure, wanalia kuwa ni maskini.

Wanyama wa kila aina wamekuwa wakiwatukuza Watanzania kwa utajiri walionao, huku wakiimbiwa nyimbo na ndege wa kila aina warukao angani na kulipamba vyema anga la Tanzania, hayo yote yanaonekana ni kitu bure na kuendelea kutangaziwa umaskini mkubwa tulionao.

Tanzania kuwa nchi omba omba kwa mataifa makubwa duniani kunatutia aibu, kunazifanya nchi hizo wahisani zirudishe ukoloni mambo leo na kwa masharti yao nchi huongozwa kwa nguvu zao, kinachobaki mikononi mwetu ni kuwa na bakuli la kuombea msaada huku nchi ina kila kitu.

Lazima ufike wakati tujiangalie hapa tulipofikia, haiwezekani kwa muda wa miaka 50 tangu tulipopata Uhuru, nchi ishindwe kusimama yenyewe ikiongozwa na vichwa vya viongozi wanaoiongoza nchi salama isiyokuwa na majanga makubwa kama yanavyozikumba nchi nyingine, tumekosa nini, kwanini watanzania wawe masikini.

Hivi kweli kwa kipindi cha miaka hiyo 50 ya uhuru nchi imeshindwa kuwa na vyanzo vya uhakika vya kuzalisha umeme na kujikuta nchi ikiingia kwenye mikataba inayoitokea puani, eti leo hii tunapaswa kumlipa bilionea mmoja mabilioni ya fedha za Dowans wakati wasome wengi wa mambo ya umeme na kwa kutumia vyanzo vyetu tusingefika hapo.

Haya matatizo yanayoikumba nchi, kupanda kwa gharama za maisha na kukosekana kwa huduma muhimu hasa maeneo mengi ya vijijini kumesababisha athari kubwa za utunzaji wa maliasili zetu,misitu minene imekatwa na kuyaacha mapori mengi yakigeuka jangwa kwa kukata miti ovyo na kuchoma mkaa kwa kuwa umeme haushikiki.

Kwa kuwa mafuta ya taa yanayotegemewa na Watanzania wengi huko vijijini hayashikiki kwa bei, watu wamerudi enzi za ujima, wanatumia vijinga vya moto kuangazia usiku, vikongwe wataendelea kuuawa hadi lini kwa imani za kishirikiana hasa baada ya macho yao kuonekana kuwa mekundu kwa sababu ya moshi mkali wa kuni.

Ndiyo maana nasema hivi, mtu huyu aliyeiroga Tanzania asipokufa tutakwisha kwa kuwa hakuna njia mbadala inayoleta matumaini mazuri ya kurejesha maisha bora kwa kila Mtanzania, hali inazidi kuwa tete si mijini wala vijijini kila sehemu ni kilio tu.

Ni nani aliyewaroga Watanzania ambao ujasiri wao na uvumilivu wao pengine umegeuka na kuwa fimbo ya mafisadi ya kuwapigia watu masikini ili wasiweze kunyanyuka hapo walipo, wakiliacha kundi la watu wachache wakiitafuna nchi watakavyo wengine wakizidi kulia na kusaga meno kwenye nchi ya asali na maziwa.

Ipo haja na iwe wajibu kwa serikali kutafakari kwa kina ahadi zote zilizokuwa zikitolewa na chama tawala (CCM) wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2010 zimeanza kutekelezwa au hazitekelezeki, mbona hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kwa Watanzania hawa ni nani anayeweza kuwaokoa ?

Mbona zile kaulimbiu za maisha bora kwa kila Mtanzania haziimbiki, mbona waliokuwa wakiimba wamenyamaza kimya, kwa ukimya huo ina maana kuwa tayari ahadi zote zilizokuwa zikipambwa kwenye majukwaa zimetekelezwa?

Tukimjua mchawi aliyewaloga Watanzania tunaweza kupata jibu kuwa hata viongozi wetu pengine wanawaogopa wachawi waliozingira uchumi wetu, wanawaogopa mafisadi waliotanda pembeni mwa nyumba zao bila kujali ulinzi salama uliopo, kama ni hivyo tusubiri mtu aliyeiroga Tanzania afe, asipokufa tumekwisha.

SOURCE: MAGAZETI YA LEO
 
Back
Top Bottom