TANZIA YA SHEIKH KARUME: Kutoka kitabu Cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi

Yericko Nyerere

JF-Expert Member
Dec 22, 2010
16,987
20,271
Kutoka kitabu Cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.

::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::
Mauaji ya Sheikh Abeid Karume.

(Misheni ya Tatu)

Baada ya kuona namna mwanamapinduzi halisi, Field Marshal John Okello, alivyoondolewa Zanzibar na kupokwa mamlaka na jinsi alivyoongoza Mapinduzi ya mwaka 1964, na kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, kuliibuka lengo la Karume la kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party, na hivyo kumnyima Karume usingizi wa pono katika muda mfupi wa utawala baada ya mapinduzi hayo. Lakini, tofauti na matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, akituhumiwa vikali kushindwa kuongoza na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulikuwa nguzo muhimu kwa Karume kujijenga mamlakani. Ili kusafisha njia na kuondoa uchafu aliyoona unamghasi, aliona ni vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi za uongozi Tanzania Bara ambako wasingeweza kufurukuta. Waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma Party) na Uwaziri wa Mipango na Uchumi kwenye Serikali ya Muungano, Kassim Hanga (ASP) akateuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, na Mambo ya Muungano na Salim Ahmed Salim (Umma Party) aliteuliwa kuwa Balozi nchini Misri.

Wengine ni Othman Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga Mwl. Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa. Badala yake akateuliwa kuwa Afisa Mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali Mahfoudh (Umma Party) akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Operesheni/Mazoezi katika Jeshi la Wananchi (JWT).

Kwa wale wenye maoni tofauti na ya kukosoa serikali hasa kwa waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala kwa mkono wa chuma iliwashukia. Wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine kupotezwaa au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati timamu) Mohamed Hamoud, baba yake Luteni Hamoud Mohamed ambaye baadaye alikuja kumuua Karume.

Juu ya mapinduzi ya Zanzibar na kuuawa kwa Abeid Karume, kumekuwapo na mitazamo mingi kwa watu mbalimbali, lakini nitumie mitazamo ya wanamajumui kadhaa kama vile: Prof Harob Othuman ambaye yeye alilieleza hili katika mtazamo wake; Prof Issa Shivji, naye amelisemea katika jicho tofauti; wakaja wazee wangu wa fikra za near, Mohamed Said na Dr Harith Ghassany katika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru.

Marazini hawa wanarandana kimitazamo, ambamo kwa undani, zinabeba dhanna ya kidini, lakini mawazo tanzu na fikra tunduizi ya Joseph Mihangwa katika andishi lake kwenye gazeti la Raia Mwema la tar. 11 Aprili, mwaka 2012, Toleo Na. 234 – 237, na Toleo la tar. 2 Mai, mwaka 2012 ndio yanabeba dhanna yangu juu ya tukio hili.

Tangu Mapinduzi ya tar. 12 Januari, mwaka 1964, Zanzibar haikuwa na Katiba wala Sheria. Kinyume chake, iliongozwa kwa Amri za Rais Presidential Decrees kwa kadri Rais alivyoona inafaa. Na, kwa mujibu wa Gazeti la The Tanganyika Standard la tar. 9 Machi, mwaka 1968, Karume aliapa kutofanya uchaguzi wala kuwa na Katiba Kisiwani kwa miaka 50, tangu mwaka 1964-2014, kwa madai dhaifu kwamba chaguzi zote ni vyombo vya mabeberu kuwakandamiza wananchi. Na, kadiri kalamu ya Karume ya wino wa damu ilipozidi kuandika historia ya ukatili, udikteta na umwagaji damu kwenye kurasa ngumu za kutu ndivyo alivyojichongea na kujiongezea upinzani mkali na uadui kwa jamii ya Kizanzibari.

Kwa namna fulani, kuanzia mwaka 1964,kulikuwa na vuguvugu ama tuseme harakati za hapa na paleza kupinga utawala wa Karume, harakati ambazo Utawala wa Karume ulitumia mwanya huo kuziita ni majaribio laanifu ya hapa na pale ya kutaka kuiangusha Serikali ya Karume. Thabit Kombo Jecha katika Simulizi anayataja majaribio baadhi, likiwamo lile la Disemba 1964, lililoongozwa na Amour Zahorwa Unguja, la mwaka 1967 likiongozwa na Suleiman Hamad Suleimanwa Pemba, la mwaka 1967 tena, likiongozwa na Saleh Ali Nassorwa Unguja, na la mwaka 1968, likiongozwa na Salim Mohamed Abdullah wa Pemba. Kufikia mwaka 1967 hofu ya Karume dhidi ya wenzake na kwa nafasi yake ilitia fora kiasi cha kuogopa kivuli chake mwenyewe. Na ili kuendelea kuwamaliza wenzake, mwaka huo, zilitungwa tuhuma za uongo dhidi ya watu kumi na wanne (14) ambao ni makada waandamizi wa ASP, kutaka kumpindua, zikiwalenga hasa wenye fikra za kikomunisti.

Walioingizwa kwenye tuhuma hizo ni pamoja na Mawaziri wa Serikali yake mabwana Abdallah Kassim Hanga, Salehe Saadallah Akida, Abdul Aziz Twala; Makatibu Wakuu wa Wizara, Aboud Nadhif na Mdungi Ussi; na baadaye Othman Sharrif. Wote waliokuwa Visiwani walikamatwa, kisha wale waliokuwa bara, Karume akamuomba Mwl. Nyerere kuwarejesha Zanzibar ambapo ombi hilo la lazima liliwakumba ndugu Othman Sharrif na Kassim Hanga ambao walitakiwa hima fa hima warejeshwe Zanzibar ili wakahojiwe lakini wote wakaishia kuuawa kikatili baharini bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mmoja wa Mashahidi Bandia walioandaliwa dhidi ya watuhumiwa kwa vyombo vya Karume, alikuwa Ahmada ambaye kwa uongo wake uliokubuhu, watu wanne akiwamo Hanga, Twala, Saadallah na Othman, walinyongwa mwaka 1969. Kwa uongo huo, Ahmada alizawadiwa Cheo cha Kapteni, jeshini. Ni Kapteni Ahmada huyu, aliyeshiriki kwenye mauaji ya Karume miaka mitatu baadaye. Kwa hofu ya jamii ya Kizanzibari kufikiwa na fikra na mawazo mapya ya kimaendeleo, Karume alipiga marufuku vijana wa Kizanzibari kwenda nje, kwa masomo ya juu, ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Hakuishia hapo, pia alipiga marufuku ya ujenzi wa Chuo Kikuu Visiwani.

Mbali na kutokuwapo kwa utawala wa sheria enzi za Karume, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa misingi ya historia na kisiasa ulitia, ulipewa kipaumbele kama ilivyokuwa kwa Makaburu huko Afrika ya Kusini. Kwa mfano, mwaka 1966, Karume alitoa amri kuwanyima wazazi haki ya kuwakataa wanaume walioposa binti zao kama njia ya kuondoa ubaguzi wa rangi. Kwa sababu hii, wasichana, hasa wale wa Kiarabu walilazimishwa na Serikali, kuolewa kwa nguvu. Wakati huo, Karume mwenyewe, akiwa na umri wa miaka 65, aliwania kuoa kwa nguvu, wasichana wanne wa Kiajemi, na alipokataliwa, aliamrisha wazazi wao watiwe kizuizini na kuchapwa viboko kwa kosa la kuzuia mpango wa ndoa mchanganyiko, na baadaye kutimuliwa Zanzibar. Chini ya mpango huo, raia wa kigeni waliotaka kuchumbia wasichana wa Kizanzibari walitakiwa kuilipa Serikali kiasi kikubwa cha fedha bila hivyo hawakuruhusiwa kuwaoa. Yaani ni sawa na kusema, wanawake wa Kizanzibari walikuwa sehemu ya rasilimali mbichi za nchi ambao walipaswa kuuzwa au na kutozwa kodi kama zilivyo mali nyingine za asili kama samaki, n.k.

Kiburi cha madaraka kilipokolea, Karume alianza kuwa mwiba kwa Mwl. Nyerere, hasa juu ya Muungano. Kwa mfano, alimkatalia Mwl. Nyerere kwa lugha ya dharau na bezo juu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar. Na kuhusu akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar iliyofikia dola milioni 80 mwaka 1972, alimpa Mwl. Nyerere onyo kali, asithubutu kuitolea macho, akamwambia: “Fedha ya kichwa cha Malkia si yako na usiniulize, labda niulize juu ya hii (sh.) yenye picha ya kichwa chako.” Na kuhusu Muungano, Karume alianza kuchoka nao. Siku moja alisema, “Muungano ni kama koti tu; likikubana unalivua.”

Ufa huu kati ya viongozi hao wawili juu ya Muungano, ndio uliosababisha Kamati ya Kupendekeza Katiba isiundwe na Bunge la Katiba lisiteuliwe ndani ya muda wa mwaka mmoja tangu Muungano, kama ilivyotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa Sheria ya Muungano ya mwaka 1964. Wadadisi wa mambo ya siasa wanakubaliana kuwa, kama Karume angeendelea kutawala miaka kadhaa baada ya mwaka 1972, Muungano ungefikia kikomo kwa njia ya kutisha na kusikitisha.

Kufikia mwaka 1972, upinzani kwa Serikali ya Karume ulikwisha chukua harakati za uasi wa umma, chini kwa chini, kwa mara ya kwanza tangu Hanga na wenzake wanyongwe mwaka 1969. Kwa vigezo vyovyote vile vya utawala na uongozi, Karume alitawala kwa mkono wa chuma cha pua. Alitawala kiimla (utawala mkavu wa unyama) katika nyanja zote za maisha ya Wazanzibari kisiasa, kiuchumi na kijamii!―, pia alikuwa kero kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwl. Nyerere dhidi ya Muungano.

Kwa kusema haya, kitabu hiki hakitafsiri kwamba Karume hakutenda mema kwa Zanzibar na kwa Wazanzibari, bali kinajaribu kutafiti tu kuona ni mazingira na sababu zipi zilizochochea na kuharakisha kuuawa kwake. Ama huenda kati ya sababu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimuungano ndizo zilizoharakisha kifo chake. Tunajua kwa mfano, kwa baadhi ya Wazanzibari, Karume alitawala kikatili, mzandiki asiye na huruma wala hakujua kusamehe. Kwa upande mwingine, alikuwa na sifa za pekee nzuri kama kiongozi na binadamu; alikuwa mhimili na mtetezi wa Waafrika wa Kizanzibari na hakuyumbishwa na siasa za migogoro Visiwani. Alikuwa mwenye fikra zenye kujitegemea, alifanya maamuzi yake bila woga wala kuhofia matokeo; alikuwa kiongozi mwenye kuthubutu na mwenye kujituma.

Licha ya Karume kuitawala Zanzibar kwa mkono wa chuma cha pua, na namna alivyowaengua wote aliodhani hawakuwa upande wake ama kwa kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano, ama kwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha, jamii ya Kiarabu wasio Wazanzibari, iliamriwa kuondoka, na wale Waarabu raia waliobaki, waliishi chini ya jicho kali la Serikali; waliweza kukamatwa, kama Wazanzibari wengine na kutiwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka. Walifanyiwa jinsi serikali ilivyofikiri inafaa; mashamba na mali zao zilitaifishwa bila kufidiwa. Wapo waliohukumiwa na Mahakama ya wananchi, kifungo na kuchapwa viboko. Kuonesha kwamba Serikali ya Karume haikuwa ya mchezo mchezo, akaionya jamii ya Ki-Athnasheri wa Kiajemi kwamba kama wangeendelea kuleta mgogoro, wangefukuzwa wote Zanzibar licha ya kuwa raia.

Karume alitangaza utawala wa chama kimoja cha ASP na kuamrisha kila Mzanzibari mtu mzima, kuwa mwanachama. Kila familia ilitakiwa kutundika picha ya Karume nyumbani, na ambaye angekaidi, alikuwa amefanya kosa la jinai lenye kustahili adhabu kali. Kikosi cha Usalama wa Taifa chini ya Kanali Seif Bakari, kilichopewa jina la Viwavi Jeshi, kilichofunzwa Ujerumani Mashariki kikaiva kwa mbinu za utesi na mauaji, kilipewa mamlaka ya kukamata, kutesa, kutia kizuizini na hata kuuwa bila mashitaka (yaani sheria iliwapa haki ya kua kama haki nyingine). Yeyote aliyelalamika, hata juu ya upungufu wa chakula tu, aliitwa adui (au mchochozi kama ilivyo sasa) wa Mapinduzi na hivyo mhaini. Enzi hizo, nduguyo akigongewa mlango usiku na kutakiwa kwa mahojiano na Serikali, usingemwona tena milele na milele.

Wakati wa Karume, wakati wa mkono wa chuma, hapakuwa na utawala wa Sheria wala Katiba. Amri za Rais ndizo zilizotawala nchi. Mapema mwaka 1966, mfumo wa mahakama wa kawaida ulipigwa marufuku; na Oktoba 1966, Rais alijipa madaraka ya kuteua mahakama maalumu za watu wasiozidi kumi na wanne (14), wenye mamlaka ya kusikiliza kesi za makosa ya kisiasa kama vile uhaini, uhujumu uchumi na wizi wa mali ya umma. Mahakama hizi hazikufungwa na kanuni zozote katika kusikiliza kesi; huduma za kisheria kwa watuhumiwa zilifutwa na mawakili kupigwa marufuku Zanzibar. Upande wa mashitaka ndio uliokuwa upande huo huo wa utetezi. Yaani, mwendesha mashtaka wa serikali alipomaliza kuwasilisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa, aligeuka kuwa mtetezi wa mtuhumiwa huyo huyo. Ilikuwa vichekesho vya kutamausha. Mahakama hizi zilipewa uwezo wa kutoa hukumu ya kifo, iwapo waliona adhabu nyingine ni nyepesi kwa mtuhumiwa. Mwaka huo huo (1966), Baraza la Mapinduzi lilipiga marufuku haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki [EACA] na rufaa zote zikawa kwa Rais Karume pekee. Mwaka 1970, Karume alipitisha amri ya kuanzishwa mahakama (za kienyeji) za watu watatu. Mahakimu wapya wa mahakama hizo waliteuliwa na Karume mwenyewe kutoka miongoni mwa makada wa ASP. Moja ya sifa ya kuteuliwa ni kutokuwa msomi wa sheria, na ikiwezekana uwe hujui kusoma na kuandika. Adhabu ya kifo ilipanuliwa kuingiza makosa kama vile utoroshaji wa karafuu, uhaini na utoaji mimba. Matumizi ya vidonge vya uzazi wa majira, nalo lilikuwa kosa kubwa.

Mwaka 1971, Karume alichochea hasira na chuki kubwa ya Wafanyibiashara wa Kiasia pale alipowapa agizo la mwaka mmoja, kufungasha virago kwa madai ya kuonekana kudhibiti uchumi wa Zanzibar. Hasira yao iliungana na ile ya Waarabu ugenini waliofukuzwa mwaka 1964, na kupokonywa mali na mashamba yao bila kulipwa fidia, achilia mbali wale ambao mabinti zao waliozwa kwa nguvu kwa Wazanzibari Waafrika. Wakati huo huo, Karume aliendelea kuwaachisha kazi na kuwatimua Visiwani, watumishi wa serikali waliojulikana au ndugu zao kuwa wafuasi wa zamani wa vyama vilivyopigwa marufuku vya ZNP na ZPPP na nafasi zao kujazwa na watiifu viherehere kwake. Hata hivyo, kwa huruma ya Mwl. Nyerere, walipewa utumishi serikalini Tanzania Bara.

Kwa mara nyingine, mapema mwezi Januari, mwaka 1972, Waziri mdogo, Ahmed Badawi Qualletin, na Afisa mwingine wa Serikali, Alli Sultani Issa, walifukuzwa kazi. Kisha, Februari, mwaka 1972, ujumbe mzito wa watu sita ulitumwa kwa Mwl. Nyerere kumwambia awarejeshe Zanzibar, Abdulrahman Babu na wenzake kadhaa wakahojiwe kwa tuhuma za kutaka kuiangusha Serikali. Babu ambaye alikuwa bado mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa Zanzibar, na aliyeamua kutorejea Zanzibar ya Karume kwa kuhofia usalama wake, kivuli chake na mzimu wa wahanga wa ukatili vilimtisha na kumnyima usingizi Karume, mithili ya Macbeth kwa mzimu wa Mfalme Duncan na Banquo, aliowaua kwa upanga ili atawale.

Mwl. Nyerere, kwa kuhofia yaliyompata Hanga, Twala, Othman Sharrif na wengine tokea alipowarejesha Zanzibar mwaka 1967, safari hii alikataa kumrejesha Babu Zanzibar, ingawa alikubali shinikizo la Karume la kumwachisha uwaziri katika Serikali ya Muungano. Hatua za kuwakosa wakina Babu na wenzie zilipodunda, Karume aliwatimua wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufunga Kituo chao cha Utafiti na Udhibiti wa Malaria Visiwani, kwa madai kwamba, Wazanzibari walikuwa malaria proof, yaani hawaguswi wala kuugua malaria. Kwa hatua hiyo, ugonjwa wa malaria uliongezeka kwa asilimia arobaini na tano (45&). Na ingawa Zanzibar ilikuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni, zaidi ya pauni za Uingereza 14 milioni, kwenye Benki ya Urusi mjini London, (taarifu nyingine zinadai dola 80 milioni), Karume hakuwa tayari kutumia fedha hizo kudhibiti malaria wala kuagiza chakula. Badala yake akaona umuhimu zaidi kuanzisha Kituo cha Utangazaji cha Rangi na ya pekee barani Afrika, wakati huo. Mwaka huo huo (1971), katikati ya mrindimo wa njaa Visiwani, Karume alipiga marufuku uagizaji wa chakula (mchele, sukari, unga wa ngano) kutoka nje, kama hatua ya kujitegemea kwa chakula.

Hatua hii ilizua tafrani na malalamiko na kusababisha biashara ya magendo ya chakula kushamiri. Hapo cheche za Viwavi Jeshi na mahakama za kangaroo zililipuka, yaani wahanga walikamatwa, kushitakiwa na kunyongwa. Watu wengi wakaikimbia Zanzibar. Aprili, mwaka 1972, ukosefu wa chakula ulikithiri. Ni wakati huo huo, Karume alipouawa ghafla.

Kwa yote hayo, pamoja na tabia yake ya kutoamini wasomi na kuchukia wataalamu, hatimaye Karume alianza kuchukiwa na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, wenye siasa za mrengo wa ki-Karl Marx. Mwl. Nyerere alikuwa ameyatoa sadaka mambo mengi ya Tanganyika kwa Zanzibar, ilimradi tu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ufikiwe. Kwa mfano, Tanganyika ilipoteza hadhi ya kuwa nchi na baadaye jina lake, pale Muungano ulipobadili jina kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tan-zan-ia, huku Zanzibar ikabakia kuwa Zanzibar, na Karume akabakia Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.
Si hivyo tu, Wazanzibari watano walipewa uwaziri kamili katika Baraza la Mawaziri kumi na wanne (14) la Muungano. Na, ingawa idadi ya Wazanzibari ilikuwa asilimia tatu (3%) tu ya Watanganyika, lakini Zanzibar iliruhusiwa kuwa na Wabunge hamsini na wawili (52) katika Bunge la Muungano, wakiwamo Wajumbe wote thelathini na wawili (32) wa Baraza la Mapinduzi. Licha ya upendeleo huu, Mwl. Nyerere hakufanikiwa kudhibiti mhimili wa kisiasa Zanzibar chini ya Karume. Mfano, Zanzibar chini ya Karume, ilikataa kuhamishia kwenye Muungano mambo mengi yaliyopaswa kuwa chini ya Serikali ya Muungano mathalani Zanzibar iliendelea kudhibiti Jeshi lake la Ulinzi na Idara ya Uhamiaji, Karume akiwa amiri jeshi wake Mkuu. Ndiyo kusema, aliuawa na wanajeshi wa jeshi lake la Zanzibar, si Wanajeshi wa JWTZ? Karume alikataa Serikali ya Muungano kugusa akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar, japokuwa fedha lilikuwa jambo la Muungano.

Aidha, Karume na Baraza lake la Mapinduzi walikiuka mara nyingi mapendekezo ya kisera kutoka Bara kiasi kwamba Mwl. Nyerere hakuwa na kauli tena juu ya sera za kiserikali. Aidha, Karume akakataa mazungumzo zaidi ya kikatiba kwa hofu ya Zanzibar kupoteza hadhi na mamlaka yake. Karibu kila alichopendekeza Mwl. Nyerere, alipata jibu la mkato kutoka kwa Karume: “Kama hivyo ndivyo (basi), tuvunje Muungano.”
Mitazamo hasi ya viongozi hawa wawili juu ya Muungano, ndio iliyosababisha mchakato wa kupata Katiba ya Muungano ndani ya mwaka mmoja kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, usifanyike, na Muungano kuongozwa kwa Katiba ya Muda kwa miaka kumi na mitatu (13) hadi mwaka 1977 na baada ya Karume kufariki. Mwl. Nyerere alipowasilisha na kupitishwa kwenye Bunge la Muungano, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na kutangaza nia yake ya kuona unatumika Visiwani, Karume aliupinga. Akaja na mpango wake tofauti wa Miaka Mitatu kwa Zanzibar, ulioandaliwa na mchumi kutoka Ujerumani Mashariki. Kwa yote hayo na mengine, Mwl. Nyerere alianza kuonesha dhahiri chuki yake kwa utawala wa kimabavu wa Karume. Naye (Karume) alipotambua hilo, alizuia mwingiliano huru wa watu kati ya Visiwani na Tanzania Bara kwa hofu na kwa sababu zisizofahamika.

Si mara moja, hofu na wasiwasi wa kimaasi vilipojionesha Zanzibar, mamlaka za usalama zilimshauri Mwal. Nyerere kufuta ziara zake Visiwani. Hofu hizi zilijidhihirisha zaidi pale Othman Sharrif, baada ya uteuzi wake wa Ubalozi Marekani kufutwa kwa shinikizo la Karume na kurejea Zanzibar, alipokamatwa na kutiwa kizuizini kama si nguvuni bila kosa bainifu. Kuonesha jinsi alivyochukizwa na kitendo hicho, Mwl. Nyerere aliingilia kati na kumwita Karume Ikulu. Hata hivyo, kwa kiburi cha beberu, Karume alimkatalia katu, kuonesha kwamba Mwl. Nyerere hakuwa na mamlaka kwake. Sharriff aliachiwa baadaye kwa hiari ya Karume; na Mwl. Nyerere akamteua kuwa Afisa Mifugo Tanzania Bara. Hata hivyo, Oktoba, mwaka 1969, wakati Mwl. Nyerere akiwa ziarani nchi za nje, Sharrif alikamatwa Tanzania Bara na kurejeshwa Zanzibar alikouawa.

Mbali ya kusema kwa udhahiri kwamba, ‘Muungano ni kama koti tu, likikubana au kukuzidishia joto unalivua na kuendelea na safari yako, Karume alijipa ujasiri wa kondoo kwa kumkatalia Mwl. Nyerere hadharani kila mara juu ya baadhi ya mambo ya Muungano akisema: “(...) kama ni hivyo, sikubali, bora tuvunje Muungano.” Ni ujasiri huu wa Karume usio wa kawaida juu ya jambo nyeti kama hili, uliofanya Mwl. Nyerere atoe tamko lake maarufu juu ya hatima ya Muungano, akisema: “Kama watu wa Zanzibar, bila ya ulaghai kutoka nje, wataona ni bora kuvunja Muungano, mimi siwezi hata kidogo kuwapiga mabomu na kuwaua wananchi wa Zanzibar. Kama waliingia katika Muungano kwa hiari yao, vivyo hivyo, wanaweza kujitenga kwa hiari yao. Hatukuishinda Zanzibar (kuwafanya mateka) vitani.” (Soma, William Edgett Smith, ‘Mwalimu Julius K. Nyerere’: mf., Paul Sozigwa; uk. 154).

Mwl. Nyerere alipokuwa mstari wa mbele katika kuupinga ubeberu wa Marekani, wakati wa Vita ya Vietnam, na kupigania ukombozi wa Nchi Zinazoendelea kwa ujumla, Karume alimbeza na kutangaza adhabu kali Visiwani kwa yeyote aliyelaani na kupinga ubeberu, au kuimba nyimbo za kuikashifu Marekani. Mwl. Nyerere alipokosana na Uingereza, kwa nchi hiyo kuukingia kifua utawala wa kidhalimu, kibaguzi na wa mabavu (UDI) wa Ian Smith nchini Rhodesia Kusini (sasa Zimbabwe), na kwa sababu hiyo uhusiano wa Mwl. Nyerere na Balozi wa Uingereza nchini, Sir Horace Phillip, kuingia mkwara, Karume alionesha hadharani kila mara kusuhubiana na Balozi huyo kwa kicheko cha bashasha na uswahiba kwa chukizo kwa Mwl. Nyerere.

Tunaweza kutua kidogo hapa kuangalia nyuma, mazingira aliyokuwamo Karume, miezi michache kabla ya kifo chake. Bila shaka tupu, tutabaini kuwa, kiongozi huyo alikuwa katikati ya uhasama na uadui wa kujitakia. Kwanza, alikuwa na uhasama mkali na jamii pana ya Kizanzibari kwa udikteta wake uliokithiri, uliosababisha mauaji, watu kutiwa kizuizini au kuhamishiwa Bara. Pili, kulikuwa na tatizo la njaa na mlipuko wa malaria, mambo ambayo hakuonekana kuyajali. Tatu, kulikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa kati yake na makada wenzake wenye siasa za Ki-Karl Marx ndani ya ASP, waliomtuhumu kushindwa kuongoza, achilia mbali jamii ya Kiarabu aliyoitimua kikatili/kiuonevu Zanzibar na iliyoendelea kutema laana kwake ughaibuni. Nne, kulikuwa na Mwl. Nyerere ambaye alianza kumuona kama mzigo na kero kwa Serikali ya Muungano na kwa siasa za kimataifa. Yote haya yalikuwa baruti tosha kuweza kulipuka na kumdhuru Karume kwa namna yoyote iwayo.

Luteni Hamoud Mohamed Hamoud, alikuwa mtoto wa mzee Mohamed Hamoud ambaye alikamatwa na kutiwa kizuizini na Karume miezi kadhaa baada ya Mapinduzi ya Januari, mwaka 1964, na hatimaye kufariki dunia akiwa kizuizini. Miaka kadhaa baadaye, wakati Hamoud Hamoud akichukua mafunzo ya kijeshi huko Tashkent nchi iliyokuwa katika Shirikisho la Urusi la zamani, alifahamishwa na mmoja wa wanafunzi wenzake juu ya kuuawa kwa baba yake. Kama msemo wa Kiarabu usemao ‘kisasi ni haki’ Hamoud kwa uchungu mkubwa, aliapa sawia kwamba, angemuua Karume kulipiza kifo cha babaye. Mfumo wa Usalama wa Zanzibar ulioenea kila mahali, ulijulishwa haraka na mmoja wa Maafisa Usalama waliokuwa kwenye mafunzo pamoja na Hamoud, juu ya kusudio hilo la haki la Hamoud. Pengine, cha kushangaza ni kwamba, Hamoud aliporejea Zanzibar baada ya mafunzo, hakukamatwa wala kuwekwa kwenye uangalizi mkali. Badala yake, alipandishwa cheo kuwa Luteni Usu, katika sherehe iliyohudhuriwa na Karume mwenyewe kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Zanzibar.

Ikumbukwe kuwa, suala la Usalama wa Taifa halikuwa jambo la Muungano ambalo liliongezwa kwenye orodha mwaka 1984, kufuatia kadhia ya Aboud Jumbe ya kuchafuka kwa hewa ya kisiasa Zanzibar na yeye kuwekwa kizuizini Mjimwema Kigamboni jijini Dar es Salaam, likaunganishwa kusomeka kwa pamoja na jambo la Ulinzi kuwa Ulinzi na Usalama. Lakini kila kitu juu ya mipango na njama zote hizo, Idara ya Ujasusi Tanganyika au Tawi Maalumu, ilifahamu. Pale risasi ya Hamoud ilipochukua uhai wa Rais Karume miezi kadhaa baadaye, Serikali ilisisitiza kwamba, mauaji hayo yalikuwa sehemu ya njama kubwa ya kuangamiza Mapinduzi ya 1964, kutokana kwamba, Hamoud na wauaji wenzake walikuwa wanachama wa zamani wa Umma Party, kilichokiunga mkono ASP huko nyuma, na kukipa [ASP] mwelekeo bora wa kiitikadi [Ukomunisti] na kuheshimika kisiasa.
Kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 elfu walikamatwa na kuhojiwa kweli kweli. Babu alikamatwa na kutiwa kizuizini Tanzania Bara kwa tuhuma za kuongoza mpango mzima. Nao maafisa wa ngazi za juu wa Kizanzibari Jeshini Bara, kama Ali Mahfoudh na wengine, walishukiwa vikali na kuondolewa kwenye utumishi wa Jeshi Tanzania Bara bila kurejeshwa Zanzibar.

Kuna dhanna mbili zinazogongana lakini zote zenye nguvu. Nazo, ni juu ya sababu za kuuawa kwa Karume. Dhanna ya kwanza ni hii ya Hamoud kulipiza kisasi. Lakini suala la kulipiza kisasi linakoma pale tunapoona watu kama Kapteni Ahmada na raia Ali Chwaya ambao hawakuwa na uhusiano wa kifamilia na marehemu Mohamed Hamoud aliyeuawa, kujiingiza katika kulipiza kisasi. Lakini, kama tutakavyoona baadaye, Kapteni Ahmada alijiingiza kama hatua tu ya kujisafisha kwa kujutia ushahidi wa uongo aliotoa dhidi ya Hanga na wenzake kumi na wanane (18) waliouawa mwaka 1969, na yeye kuonekana kama adui na msaliti mkubwa wa umma wa Kizanzibari. Inapofikia hapo, inakuwa dhahiri kwamba mpango huo ulibeba hasira za jamii pana ya Kizanzibari.

Dhanna ya pili ambayo ndiyo msimamo wa Serikali ni kwamba, mauaji hayo yalikuwa na mpango mpana wa kupindua Serikali. Dhanna hii inapata nguvu kutokana na watu wengi kuhusishwa na tuhuma hizi. Lakini, kama tuhuma hizo dhidi yao si za kweli, vinginevyo dhanna ya kwanza inashinda.Chuki binafsi? Hapana. Hamoud hakuwa peke yake; ilikuwa ghadhabu ya umma kwenye jamii pana ya Kizanzibari, kila kundi au sehemu ya jamii na malalamiko yake.

Kwa mujibu wa taarifu za Usalama wa Taifa Zanzibar, mipango ya kupindua Serikali ya Karume ilianza kusukwa tangu mwaka 1967 -1972, ndani ya Zanzibar na Tanzania Bara, ambapo nyumba ya Abdulrahman Babu ilikuwa kituo cha mikutano ya Wazanzibari ya kupanga Mapinduzi hayo. Kama hivi ndivyo, Karume alikuwa na sababu tosha kumtaka Mwl. Nyerere kumrejesha Babu Zanzibar kuhojiwa vikali, mnamo Februari 1972. Mkutano wa mwisho ulifanyika kunako tar. 2 Aprili, mwaka 1972, ambapo ilikubaliwa Mapinduzi yatekelezwe tar. 7 Aprili, mwaka 1972, yakihusisha makundi mawili: kundi la Wazanzibari kutoka Bara, wengi wao wakiwa wanajeshi; na kundi la Wazanzibari ndani ya Zanzibar, likihusisha raia na wanajeshi wachache.

Pamoja na uamuzi huo, kikao kilitoa majukumu mazito kwa baadhi ya washiriki, ikiwa ni pamoja na Hamoud na Ahmada kupewa jukumu la kuiba silaha kutoka kambi ya kijeshi, Bavuai. Ilikubaliwa kuwa, Babu na wafuasi wake kutoka Bara wasafiri kwa mtumbwi kwenda Zanzibar usiku wa tar. 6 Aprili, kuamkia alfajiri ya tar. 7 Aprili, na kufikia eneo lililopo kati ya Mitambo Mikuu ya Mawasiliano na Klabu Starehe. Baada ya hapo, Babu abakie amejificha kwenye nyumba ya Hamoud Hamoud, iliyotizamana na Klabu Starehe eneo la Shangani, kusubiri saa ya mapambano ya kishujaa kuwadia. Kwa mujibu wa taarifu, Babu aliondoka Dar es Salaam kwa mtumbwi uliofungwa idhaa mbili za mawasiliano, jioni ya tar. 6 Aprili, safari iliyoelezwa kuwa ya kuvua samaki wakati madhumuni halisi yalikuwa ni kuwafikisha Babu na wafuasi wake Visiwani usiku huo wa tar. 6 Aprili, kwa maandalizi kamili ya kupindua Serikali. Jioni hiyo, tar. 6 Aprili, Uongozi wa Jeshi uligundua upotevu wa silaha nyingi kambini, Bavuai. Na ingawa uongozi ulikuwa bado haujamhusisha mtu yeyote, lakini Hamoud, Hamada na askari wengine walianza kufuatiliwa kwa siri.

Yaelekea kufikia hapo, Babu alijulishwa na kuonywa kwa njia ya idhaa akiwa baharini, juu ya kugunduliwa kwa mpango mzima wa Mapinduzi; akakatiza safari na kurejea hima, Dar es Salaam. Haijulikani kama wafuasi wake walikwisha fika Zanzibar au la ama kama nao walijulishwa na kurejea Dar es Salaam. Lakini, wanajeshi kuwapo Visiwani kama Kanali Mahfoudh (Mkurugenzi wa Operesheni JWTZ, Dar es Salaam) na Luteni Hashil Seif (Kikosi cha Wanamaji, Ukonga, Dar es Salaam) saa ya kuuawa Karume, kunaonesha baadhi yao tayari walikuwa Zanzibar kusubiri wenzao. Saa 6:00 za asubuhi, tar. 7 Aprili, Ali Khatibu Chwaya (raia) alikwenda kwa Ali Mshangama Issa (Afisa wa Tatu, meli M.V. Afrika, mkazi wa Zizi la Ng'ombe, Zanzibar), kumweleza juu ya kutowasili kwa kundi la Dar es Salaam.

Baadaye asubuhi hiyo, Ali Mshangama, Chwaya, Miraji Mpatani (Karani wa shirika moja, Zanzibar), Mohammed Abdullah Baramia (Mtunza Bohari, Idara ya Elimu), Ahmada na Hamoud, walikutana nyumbani kwa Hamoud na kuonesha kukerwa na kusikitishwa kwa kutowasili kwa wapanga mapinduzi kutoka Dar es Salaam, hasa wakijua kwamba, silaha zilizoibwa bado zilikuwa nyumbani kwa Hamoud, na hatari ya kuweza kugunduliwa. Ilipofika saa 12.00 za mchana siku hiyo, Mshangama, Hashil Seif, Amar Saad Salim, maarufu kama ‘Kuku’ (Afisa Usafirishaji, Idara ya Siha, Zanzibar) na Chwaya, walikutana nyumbani kwa Amar Saad ambako Mshangama, Hashil Seif na Baramia walipendekeza mpango wa kupindua Serikali uhairishwe hadi watakapopata taarifu tofauti kutoka Dar es Salaam.

Kwa hiyo, saa 3.00 za alasiri, siku hiyo, saa mbili tu kabla ya kuuawa kwa Karume, Baramia alikwenda nyumbani kwa Hamoud, eneo la Shangani, kuwasilisha pendekezo hilo. Alimkuta Miraji Mpatani nje ya nyumba na kumweleza Baramia kwamba, pamoja na kundi la Dar es Salaam kutowasili, Ahmada na Hamoud walishikilia Mapinduzi yafanyike tu siku hiyo, kwa sababu, Ahmada alikuwa anatafutwa na Maafisa wa Jeshi. Je, ni kwa sababu hii Luteni Hamoud, Kapteni Ahmada na Chwaya waliamua kufanya Mapinduzi, licha ya wenzao kutaka yahairishwe? Kwa mujibu wa Mkakati wa Mapinduzi uliofikiwa tar. 2 Aprili, mwaka 1972, Suleiman Mohamed Abdullah Sisi (mwanajeshi wa JWTZ, mkazi wa Ilala Flats, Dar es Salaam) alipangwa kuongoza utekaji wa Kambi ya Jeshi, Mtoni, ambapo Kapteni Ahmada, alitakiwa kuteka Kambi ya Jeshi, Bavuai, Makao Makuu ya Jeshi na Chuo cha Jeshi cha Mafunzo ya Idhaa (vyote hivi viko eneo la Migombani).

Kituo cha Polisi cha Malindi kingeshambuliwa na kutekwa na kikundi chenye silaha, kikiongozwa na Luteni Hamoud, ambacho kingeweza kuteka magari yenye Idhaa za Mawasiliano. Askari Yusufu Ramadhan angeongoza kikundi cha Maafisa wa Polisi, walioingizwa kwenye mpango huo na kuteka Kituo cha Polisi cha Ziwani. Amour Dughesh (mwanajeshi, Zanzibar), yeye angeteka Ikulu na kumkamata Karume, kisha kumpeleka Kituo cha Idhaa kumlazimisha atangaze kupinduliwa kwa Serikali yake. Baada ya hapo, Kituo hicho kingeachwa chini ya udhibiti wa Badawi, Mpatani na Mohamed Said Mtendeni (Mwandishi wa Habari, gazeti la China, mkazi wa Vuga, Unguja). Uwanja wa Ndege ungetekwa na kikosi cha wanajeshi na baada ya hapo kingeachwa chini ya udhibiti wa Ali Sultan Issa (Meneja wa Shirika la Mafuta, Zanzibar).

Mpango huo ulilenga pia kuteka Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa ASP (pia yalikuwa Makao Makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar), ikiongozwa na Kanali Seif Bakari na kuwekwa chini ya udhibiti wa Mohamed Abdullah Baramia. Kapteni Khamis Abdullah Ameir, wa Makao Makuu ya Jeshi, Zanzibar, yeye alipangwa kuzuia mashambulizi kutoka nje kama Mapinduzi yangefanikiwa. Kwa hadhari, Mapinduzi ni kitendo cha kutaka kubadili sawia hali, serikali au mfumo fulani wa kijamii kwa matumizi ya nguvu, ikiwa ni pamoja na kuondoa mhimili wa mfumo huo. Mapinduzi yanaweza kuwa kwa njia ya jeshi kama jeshi limetumika au ya kiraia kama raia walitumika, kama yalivyokuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya tar. 12 Januari, mwaka 1964 chini ya John Gidion Okello.

Mauaji ya Karume hayawezi kuitwa mapinduzi ya kijeshi wala ya kiraia kwa sababu kifo chake hakikubadili mfumo wala muundo wa serikali. Haya yanaweza kuitwa mauaji ya kisiasa yenye lengo la kuondoa chanzo au mhimili wa kero katika jamii bila kubadili serikali. Mwanazuoni mahiri Barani Afrika, Profesa Ali Mazrui, anatafsiri Mauaji ya Kisiasa kuwa ni kitendo cha siri cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri kisiasa, kinachofanywa na wakala asiye wa serikali, kwa sababu za kisiasa au zisizofahamika.

Naye Profesa William Gutteridge wa Chuo Kikuu cha Aston, anasema Mauaji ya Kisiasa kuwa ni kitendo cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri katika jamii kwa sababu za kisiasa na kinajumuisha pia jaribio la mapinduzi lililoshindwa na watu wengi kuuawa katika kutekeleza kilichokusudiwa.

Kama wasemavyo Mafarisayo, ‘afe mmoja wengi wapone au wahemee, mauaji ya Karume, kama yalivyokuwa mauaji ya Rais Anwar Sadat wa Misri, kwa kupigwa risasi wakati akiangalia gwaride la jeshi lake, yalikuwa na lengo la kuiondolea jamii kero bila umuhimu wa kubadili serikali. Katika mauaji kama hayo, mlengwa huwa mmoja tu kama chanzo au mhimili wa kero. Karume aliuawa kwa sababu ya utawala wa kimabavu, ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu kama tulivyoona hapo mwanzo. Wakati, Sadat aliuawa kwa kuisaliti jamii ya Kimisri, kwa kusaini Mkataba wa suluhu kati ya Misri na Israeli uliojulikana kama Camp David ili kusitisha harakati za Waarabu dhidi ya Uzayuni wa Kiyahudi. Sababu nyingine ilikuwa ni kukumbatia sera za kiuchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hatua iliyoathiri maisha ya Wamisri kiuchumi na matarajio ya kijamii ya Waislamu nchini humo na Jumuiya pana ya Kiarabu kwa ujumla.

Baada ya mauaji ya Karume, kamatakata (kata funua) ilipamba moto, lakini mtihani mkubwa ulikuwa kumkamata Komandoo Ali Mahfoudh. Kuhusu mshikemshike huo, Kanali Kashimiri aliyepewa jukumu la kumkamata, anasimulia kwa utulivu mkubwa: “Wakati nikiwa nipo ndani ya ofisi pamoja na askari nikiwapa maelekezo jinsi ya kumkamata kanali Ali Mahfoudh pindi atakapoingia mara kwa ghafla, Kanali Seif Bakari pamoja na kanali Ali Mahfoudh wakawasili. Kanali Ali Mahfoudh akafungua mlango akachungulia akinisalimia, ‘Kashmiri habari!’ Nikamjibu, ‘Salama bwana!’ Kisha nikamwambia, ‘Ingieni ndani bwana, tulikuwa tunawasubiria nyie tuanze kikao’. Ndipo yeye pamoja na Kanali Seif Bakari walipoingia ndani. Nakumbuka kabisa kuwa Kanali Seif Bakari alikuwa amevaa sare zake za kijeshi bila ya kuwa na silaha bali Kanali Ali Mahfoudh yeye alivaa sare za kijeshi na alikuwa amebeba pistol mbili kiunoni na pia alikuwa na visu viwili kiunoni mwake.

“Nadhani waliambiwa waje kwenye kikao hivyo walikisia kuwa kikao chenyewe ndio hiki. Nilikuwa tayari nimeshatayarisha viti vyao vya kukaa. Kanali Seif Bakari alikaa kiti kilichokuwa upande wa kushoto na kanali Ali Mahfoudh yeye alikaa kiti kilichokuwa upande wa kulia. Wakaanza kunieleza kilichotokea Zanzibar na wakaniambia kuwa wao wenyewe tayari wameshaidhibiti hali ya usalama na hivyo hapana haja ya kupeleka askari wengi Zanzibar na badala yake wapelekwe askari wachache ili kusaidia kutuliza hali ya hewa (yaani kuhakikisha usalama). Wakati nikiwa naendelea na mazungumzo nao, kila baada ya dakika tano, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Sarakikya, alikuwa akinipigia simu kuniuliza kama tayari nimeshamkamata, nikawa namjibu kimkato tu, kuwa bado huku yeye mwenyewe akiwa mbele yangu na hajui naongea na nani kwenye simu. Wakati huo, nilikuwa nawapa ishara kwa siri wale askari kuwa wamkamate Kanali Ali Mahfoudh lakini cha ajabu hakuna alithubutu kumsogelea na kumkamata.

“Kwa muda wa nusu nzima, askari wale walishindwa kumkamata. Tukamaliza mazungumzo yetu, naye kanali Seif Bakari akasema, ‘Sasa Kashmiri sisi tunaondoka zetu!’ Nikawaambia, ‘Sawa bwana!’. Wakaondoka wakaelekea kwa Kamisaa wa Siasa Jeshini ili kumueleza tulichoafikiana katika kile kikao. Unajua wao walidhania kuwa kile kilikuwa ni kikao rasmi na hawakujua kuwa ilikuwa ni mbinu yangu ya kujaribu kumkamata kanali Ali Mahfoudh.

“Kwa kweli nilichukia sana kuwa askari wale hawakufanya kazi ile niliyowapa. Nikawaambia wale askari, ‘Nyie si nimewapa amri ya kumkamata kanali Ali Mahfoudh? Kwa nini sasa hamjamkamata muda wote huo, haya nendeni sasa mkamlete mje nae hapa!’ Askari mmoja akaniambia, ‘Mkuu una arrest warrant ya kumkamata?’ Nikamjibu, ‘Nyie vipi! Kwani jeshini pana arrest warrant, embu nendeni bwana mkamlete. Hili ni agizo la serikali’. Niliona dhahiri kuwa walikuwa wanamuogopa. Unajua Mahfoudh alikuwa ni pande la mtu tena ni komandoo aliyefuzu Cuba na kwa wakati ule alikuwa akisifika sana kwa uhodari wa kivita aliokuwa akiuonesha katika vita vya kupigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na pia kumbuka alikuwa na silaha pale. Nikawa mkali. Nikazidi kuwafokea askari wale huku nikiwaona dhahiri wakionesha wasiwasi wao. Ghafla, askari mmoja wapo akaniambia, ‘Mkuu mie naenda kumkamata!’ Kwa bahati, walikuwa bado ofisini kwa Kamisaa wa Siasa Jeshini. Alipofika, akamwambia Kanali Ali Mahfoudh, ‘Kanali, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeaamuru ukamatwe. Tafadhali, fuatana nami mpaka kwa Kanali Kashmiri ukajisalimishe’.

“Katika hali ya kushangaza sana, Kanali Ali Mahfoudh alikuwa mnyonge na wala hakuleta upinzani au pingamizi. Akaja naye mpaka ofisini kwangu, nikamwambia, ‘Kanali Ali Mahfoudh salimisha silaha zako zote’. Ndipo akatoa silaha zake zote, akakabidhi. Kisha nikawaambia askari wote waliokuwepo pale, watoke ndani. Hivyo, nikabaki naye pale ofisini, tukiwa wawili, peke yetu. Nikamwuliza, ‘Una maagizo yoyote ambayo ungetaka niyafikishe kwa familia yako?’ Akanijibu, ‘Ndio!’ Akaomba nimpe karatasi aandike barua.

“Kwa kweli tupu, kwa kesi nzito kama ile, nilikuwa na matumaini madogo sana kama angetoka salama na sikutaka aende kizuizini bila ya kuacha maagizo yoyote kwa familia yake. Hivyo, akaandika barua ndefu sana na nikamuahidi kuwa itafika kwa familia yake. Muda mchache baaday,e alikuja kuchukuliwa na Maafisa wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, wakiongozwa na C.I.D Sawaya. Ndivyo ilivyokuwa bwana! Kumkamata yule jamaa ilikuwa ni shughuli (kashikashi) kweli kweli.”

“Baadaye, nilikuja kugundua kuwa yeye mwenyewe aliona ni salama kwake kukamatiwa Dar es salaam kuliko Zanzibar na ndio maana, hakufanya fujo yoyote wakati anakamatwa,” Kanali Kashmiri alimalizia kusema. Kanali Ali Mahfoudh pamoja na wenzake walihukumiwa adhabu ya kifo. Lakini, baada ya shinikizo kali kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu, washukiwa wote akiwemo Kanali Ali Mahfoudh waliachiliwa huru mwaka 1978. Baada ya kuachiliwa huru Kanali Ali Mahfoudh alipewa sharti kali la kutokukaa tena nchini. Ndipo, akachukuliwa na aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Hayati, Samora Machel. Na huko, alifanywa kuwa Mshauri Mkuu wa Masuala ya Usalama wa nchi hiyo. Wakati nduli Iddi Amin alipoivamia Tanzania mwaka 1978, Kanali Ali Mahfoudh alikuwa yupo nchini Msumbiji. Alipoona nchi yake imevamiwa, alimuomba Samora Machel awasiliane na viongozi wa Tanzania ili naye aweze kwenda kuitetea nchi yake. Lakini, taarifu zikaja kuwa hatoruhusiwa kupigana vita hiyo kwani itakuwa hatari kwake maana anaweza kuuawa na wale waliokuwa na machungu na kifo cha Mzee Karume.

Kanali Kashmiri na Kanali Ali Mahfoudh walikutana tena Mjini Maputo katikati ya miaka ya 1980s. Kanali Kashmiri anaeleza kwa uchangamfu jinsi walivyokutana: “Nashukuru sana nilipokutana naye, alinichangamkia kama kawaida, akaniambia kuwa hana kabisa kinyongo na mimi japokuwa kuna watu walimwambia kuwa eti mbaya wake ni mimi. Bila hiyana, yeye mwenyewe akaniambia ‘Kashmiri najua ulikuwa unatimiza amri ya wakuu wako na kwa vyovyote usingeweza kukataa kwani hata ningekuwa mimi, pia ningefanya hivyo hivyo na si vinginevyo. Kwani kanuni ya kwanza kabisa ya uaskari ni kutii amri za wakuu wako’. Baadaye alinikaribisha nyumbani kwake na tuliendelea na urafiki mpaka alipokuja kufariki. Aah! Kanali Ali Mahfoudh alifariki nchini Msumbiji na alizikwa huko huko katika makaburi ya mashujaa wa nchi hiyo.”

Malengo ya mauaji ya Karume yanajidhihirisha kwa vielelezo kwa yale yaliyofuatia chini ya utawala wa mrithi wake, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, aliyechukua uongozi mnamo tar. 11 Aprili, mwaka 1972. Baraza la Mapinduzi lililoketi tar. 10 na 11 Aprili, mwaka 1972, pamoja na kumthibitisha Jumbe kuanzia tar. 7 Aprili, mwaka 1972 kuhudumu kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza hilo, pia lilipitisha Azimio la kudumisha, kulinda, kutetea na kuendeleza fikra, malengo ya mapinduzi na sera alizoacha Karume. Hata hivyo, Wazanzibari wengi walitaka Kanali Seif Bakari amrithi Karume kwa kuwa alikuwa mtu wa karibu zaidi kwa Karume kuliko Jumbe, kwamba ndiye pekee miongoni mwa Wazanzibari ambaye angeweza kuendeleza fikra za kiongozi huyo wa Taifa la Zanzibar. Mwl. Nyerere aliingilia kati akiwa na hoja kwamba, kwa kuwa Rais Karume aliuawa na mwanajeshi, kumteua Bakari ambaye alikuwa mwanajeshi kumrithi kiongozi wa kiraia, kungetafsiriwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyoweka mwanajeshi madarakani. Hoja ya Mwl. Nyerere ikashinda kwa kishindo kizito.
Punde tu alipoanza kuhudumu kama rais, Jumbe alifuta Amri ya Karume ya kutoagiza chakula na bidhaa nyingine kutoka nje; akaruhusu akiba ya fedha za kigeni kutumika kuagiza chakula ili kumaliza tatizo la njaa na upungufu wa vitu, jambo lililokuwa mwiko wakati wa Karume. Vivyo hivyo, kwa mara ya kwanza, Serikali ya Zanzibar iliruhusu wanafunzi kumi na sabaa (17) kutoka Zanzibar, kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi kupeleka wengi zaidi.

Mnamo Disemba 1972, Chama cha ASP kilifanya Mkutano Mkuu wake wa kwanza, tangu mwaka 1962, uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya mia tisa (900) kutoka Visiwani, Mwl. Nyerere na viongozi wengine wa TANU, pamoja na wageni wengine kutoka nchi kumi nambili (12) za Kiafrika, wakiwamo wawakilishi wa Chama cha MPLA cha Angola. Katika hutuba yake ya ufunguzi, Jumbe alilaani tawala za kimabavu na ubabe, ukandamizaji na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya raia. Kuhusu viongozi, Jumbe alisema kwa msisitizo mkali: “Viongozi lazima wawatumikie watu, na si watu wawatumikie viongozi.” Kwa maneno hayo, alikuwa amefungua milango ya demokrasia Visiwani, utawala bora, uwajibikaji na kuongoza kwa mifano, tofauti na enzi za utawala wa Ki-ungu wa Karume.

Mnamo tar. 5 Februari, mwaka 1977, Mwl. Nyerere na Jumbe waliunganisha vyama vyao, TANU na ASP, kuunda Chama cha Mapinduzi―CCM, jambo ambalo lisingewezekana wakati wa Karume ambaye hata Muungano wenyewe aliweza kuusigida kwa kisigino cha nguvu. Vivyo hivyo, mwaka 1979, Zanzibar ilijipatia Katiba yake ya kwanza, baada ya Katiba ya Uhuru ya mwaka 1963, chini ya Serikali ya Mseto wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People's Party (ZPPP). Ni wakati wa utawala wa Jumbe, Zanzibar ilipata Bunge (Baraza la Uwakilishi) lake la kwanza kwa njia ya uchaguzi, wakati kabla ya hapo, Karume aliapa pasingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50, kuanzia mwaka 1964 hadi 2014.
Chini ya Jumbe, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1964, wanasheria waliruhusiwa kufanya kazi Zanzibar. Watu hawakugongewa tena milango usiku na kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Na tazama, yote yalifanywa kuwa mapya, ambapo isingewezekana chini ya utawala wa Rais Karume.
Mwaka 1984, Jumbe alirejea rasmi kwenye misingi na misimamo ya Karume juu ya Muungano, hasa alipokuja na kile kilichoitwa Kuvunja Katiba ya Jamhuri, kwa kurejea kauli ya ‘Tuvunje Muungano’. Hali hii ilimuudhi sana na kumsononesha Mwl. Nyerere, hadi kupelekea kuitishwa kikao cha dharula mjini Dodoma, ambapo Jumbe alivuliwa vyeo vyote vya kichama na kiserikali, ikiwemo uanachama na kuwekwa kizuizini Mjimwema Kigamboni hadi kifo chake.

********

1965NyerereandKarumeinDaresSalaamAiport.jpg
 
Kwa jinsi ilivyo ndefu na watanzania walivyo wavivu kusoma,hapa wanapita tu. Ungekua ni udaku hapo ndo penyewe
 
  • Thanks
Reactions: MTK
Daaah haya Mkuu watu wengi wanajua aliomuua Karume ni Kanali Ali Mahfoudh kumbe ni Mtoto wa Mpigania haki mzee Mohammed Hamoud yaani Luteni Hamoud Mohammed Hamoud, ahsante kwa elimu, Mkuu Yericko kidogo ufungwe daah hongera kwa kushinda kesi wape Hi Mh Kibatala, Msemo na wengine.
 
  • Thanks
Reactions: MTK
Mkuu sasa anza kutushushia mizigo ya intel, Big uppp Nifah, BAK, Kisu cha Ngariba wamewakilisha vyema kwelikweli, "nasema uongo jamani! " Msema kweli ni mpenzi wa mungu", walishusha mizigo takatifu
 
Umeacha uhusika wa maalim Seif kuvujisha siri za boss wake Jumbe kwa Matumaini kwamba yeye atakuwa rais baada ya Jumbe kutimuliwa. Huyu jamaa ameanza enzi hizo kuusaka urais lakini hadi sasa anadanganya wenzake kwamba "inshaalah hivi karibuni nitaapishwa kuwa rais!"
 
N
Kutoka kitabu Cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.

::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::
Mauaji ya Sheikh Abeid Karume.

(Misheni ya Tatu)

Baada ya kuona namna mwanamapinduzi halisi, Field Marshal John Okello, alivyoondolewa Zanzibar na kupokwa mamlaka na jinsi alivyoongoza Mapinduzi ya mwaka 1964, na kuundwa kwa Serikali ya Mseto kati ya vyama vya ASP na Umma, kuliibuka lengo la Karume la kuzivunja nguvu za wanaharakati wa Umma Party na za wakomunisti wa ASP walioshabihiana kimawazo na kimtazamo wa kitaifa na wana-Umma Party, na hivyo kumnyima Karume usingizi wa pono katika muda mfupi wa utawala baada ya mapinduzi hayo. Lakini, tofauti na matarajio ya Karume, hatua hiyo iliwaleta karibu zaidi wanamapinduzi hao na kumnyima zaidi usingizi kwa hofu ya kupinduliwa, akituhumiwa vikali kushindwa kuongoza na kusimamia madhumuni ya Mapinduzi Visiwani.
Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulikuwa nguzo muhimu kwa Karume kujijenga mamlakani. Ili kusafisha njia na kuondoa uchafu aliyoona unamghasi, aliona ni vyema awasambaratishe kwa kuwatafutia nafasi za uongozi Tanzania Bara ambako wasingeweza kufurukuta. Waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Abdulrahman Babu (Umma Party) na Uwaziri wa Mipango na Uchumi kwenye Serikali ya Muungano, Kassim Hanga (ASP) akateuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri, na Mambo ya Muungano na Salim Ahmed Salim (Umma Party) aliteuliwa kuwa Balozi nchini Misri. Wengine ni Othman Sharrif (ASP) aliyeteuliwa Balozi nchini Marekani, lakini Karume akampinga Mwl. Nyerere akidai hastahili, uteuzi ukafutwa. Badala yake akateuliwa kuwa Afisa Mifugo katika moja ya mikoa ya Kusini Tanzania, Mbeya au Mtwara, na Kanali Ali Mahfoudh (Umma Party) akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Operesheni/Mazoezi katika Jeshi la Wananchi (JWT).

Kwa wale wenye maoni tofauti na ya kukosoa serikali hasa kwa waliobaki Visiwani, hasira ya Karume aliyetawala kwa mkono wa chuma iliwashukia. Wengi walikamatwa na kutiwa kizuizini na pengine kupotezwaa au kuuwawa kikatili na katika mazingira ya kutatanisha. Mmoja ya waliouawa kikatili kizuizini ni Mzee (mwanaharakati timamu) Mohamed Hamoud, baba yake Luteni Hamoud Mohamed ambaye baadaye alikuja kumuua Karume.

Juu ya mapinduzi ya Zanzibar na kuuawa kwa Abeid Karume, kumekuwapo na mitazamo mingi kwa watu mbalimbali, lakini nitumie mitazamo ya wanamajumui kadhaa kama vile: Prof Harob Othuman ambaye yeye alilieleza hili katika mtazamo wake; Prof Issa Shivji, naye amelisemea katika jicho tofauti; wakaja wazee wangu wa fikra za near, Mohamed Said na Dr Harith Ghassany katika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru. Marazini hawa wanarandana kimitazamo, ambamo kwa undani, zinabeba dhanna ya kidini, lakini mawazo tanzu na fikra tunduizi ya Joseph Mihangwa katika andishi lake kwenye gazeti la Raia Mwema la tar. 11 Aprili, mwaka 2012, Toleo Na. 234 – 237, na Toleo la tar. 2 Mai, mwaka 2012 ndio yanabeba dhanna yangu juu ya tukio hili.

View attachment 492215
Noted
 
Ni historia tamu na nzuri sana.
Historia ina tabia sana ya kupenda kujirudia, sijui ni kwanini?
 
Mafala hawapo bungeni tu, hata hapa JF wapo.

Katafute basha huko mtaani. Sijui muambiweje ndio muelewe unaquote vipi thread ndefu hivi halafu unaleta wowowo lako eti noted, kama hutafuti basha kumbe watakani?
Roho yako imefurahi sana...stay blessed
 
Back
Top Bottom