Takukuru yatia mbaroni madiwani 10 wa CCM

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo iliwafanya wanasiasa kukosa usingizi wakati wa mchakato wa kura za maoni kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wameibuka tena mafichoni na wamewatia mbaroni madiwani 10 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaodiwa kujichimbia nyumba ya kulala wageni wakipeana rushwa. Madiwani hao ni wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya. Walikamatwa na kuhojiwa na Takukuru kwa tuhuma za rushwa.
Kwa pamoja wanadaiwa kuwa walisafiri kutoka Chunya hadi jijini Mbeya kwa lengo la kupeana rushwa ili wakubali kumchagua mmoja wao kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, lakini wakajikuta wakiishia mikononi mwa Takukuru wakiwa jijini hapa.
Kamanda wa Takukuru mkoani Mbeya, Daniel Mtuka, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa yeye mwenyewe baada ya kupata taarifa za tukio hilo alilazimika kuelekea eneo la tukio na hatimaye kufanikiwa kuwakamata.
Mtuka alisema juzi alipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuwa kundi la madiwani wa chama kimoja cha siasa walikuwa wamesafiri kutoka Chunya kwenda Mbeya kwa ajili ya kupeana rushwa ili wamchague mmoja wao ili asimamishwe na Chama chake kugombea uenyekiti wa halmashauri.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, alichukua vijana wake kadhaa na kuelekea kwenye eneo la tukio kushughulikia suala hilo.
“Juzi saa 9:00 jioni baada ya kupewa taarifa hizo na mzalendo mmoja, niliamua kuondoka mwenyewe na vijana wangu, tulifanya kazi ya kuwasaka usiku mzima hadi tukawapata,” alisema Mtuka.
Alisema walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa katika nyumba mbili za kulala wageni katika maeneo ya Soweto na kuwachukua hadi katika ofisi za Takukuru za mkoa kwa ajili ya mahojiano.
“Tuliwakuta watu 10 wote wakiwa ni madiwani wa chama fulani kutoka Chunya, kati yao wawili wanawake, tukawaomba waje hapa ofisini kwa mahojiano, wakakubali. Tuliamua kuwahoji kwa sababu haileti picha nzuri kwa wao kukusanyika pamoja kwa namna ile wakati kesho (leo) wanafanya uchaguzi wa mwenyekiti wa Halmashauri ndani ya chama chao,” alisema Mtuka.
Alisema baada ya mahojiano hayo yaliyoendelea hadi jana saa 9:30 jioni, madiwani wote walipewa dhamana na kuruhusiwa kwenda kuendelea na uchanguzi.
Hata hivyo, alisema ingawa wameruhusiwa kuendelea na uchaguzi, tuhuma dhidi yao bado zinaendelea kuchunguzwa na kuwa baada ya kukamilika, hatua zaidi zitachukuliwa.
“Sisi tumetekeleza hatua ya kwanza ya kuzuia, lakini hatua ya pili ya kupambana tunaendelea na uchunguzi, wakibainika kuwa kweli walijihusisha na vitendo vya rushwa, tutachukua hatua zaidi,” alisema Kamanda Mtuka.
Kauli hiyo ya Mtuka ilithibitisha kuwa madiwani waliokamatwa wote wanatoka CCM ambao leo wanafanya uchaguzi wa ndani ya Chama utakaompata diwani mmoja atakapeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mwenyenyekiti wa Halmashauri utakaofanyika hivi karibuni.
Habari ambazo NIPASHE ilizipata kutoka kwa vyanzo vyake zinadai kuwa madiwani hao baada ya kuwasili jijini Mbeya, mmoja wao (Jina tunalihifadhi) ambaye anawania nafasi ya uenyekiti wa halmashauri hiyo aliwagawia kila mmoja wao Sh. 40,000 ili wakubali kumpigia kura.
Pia inadaiwa kuwa katika kundi hilo alikuwepo diwani anayewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia aliamua kuwakatia madiwani hao Sh. 10,000 kila mmoja kwa lengo la kuwashawishi wamchague.
Wakati wa Mchakato wa kura za Maoni ndani ya CCM, Takukuru pia iliwakamata wagombea udiwani wa viti maalum wa CCM jijini Mbeya wakiwa baa wakinywa na kugawana fedha. Suala la madiwani hao bado linaendelea kufanyiwa kazi na Takukuru.
Pia waliokuwa wanawania ubunge kupitia CCM katika mchakato wa kura za maoni walikamatwa, akiwamo mwanasiasa mkongwe nchini, Joseph Mungai ambaye ana kesi mahakamani ya kutoa rushwa.
Pia yumo aliyekuwa Katibu wa TFF, Frederick Mwakalebela, ambaye naye kesi yake iko mahakamani. Pia kuna makada kadhaa wa chama hicho wanaokabiliwa na mashtaka ya kutoa rushwa wakati wa mchakato wa kura za maoni.
CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom