Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,998
Na. M. M. Mwanakijiji
Mojawapo ya vitu vinanishangaza sana wakati huu wa kampeni na hasa tangu Lowassa apewe kiti cha enzi CHADEMA ni kuwa watu waliompokea na wenye kumuuza mbele ya umma wanadai kuwa wamempokea ili aongoze harakati za mabadiliko. Utawasikia watu wanasema - bila kufikiria sana "tunataka mabadiliko" na kuwa CCM ikitoka tutapata mabadiliko. Wengi wanazungumzia "mabadiliko" kama tukio fulani ambalo litatokea baadaye.
Cha kusikitisha ni kuwa wao wenyewe hawajui au hawataki kujua, hawaamini au hawataki kuamini kuwa tayari mabadiliko yameshatokea; mabadiliko ambayo yamewabadilisha wao. Kama watu wenye akili timamu walishapata mgombea wao wa Urais, wakampitisha na kumthibitisha halafu wiki chache baadaye wakaenda kumchukua mgombea toka CCM na hivyo wakamtupa mgombea wao wenyewe, tena si mtu baki tu Katibu wao Mkuu wa chama, watu hawa hawa wanaweza vipi kuja na kusema ati wanataka "mabadiliko"? Yaani, watu waliobadilika wanataka kubadilika tena? Waweje?
Ukiangalia kwa jicho lililotulia utaona kuwa ni sisi ambao hatujabadilika au kubadilishwa na ujio wa Lowassa ndio hasa tunataka mabadiliko au tunahitaji mabadiliko. Ndio sisi ambao tunatakiwa kubadilika! Ndio maana watu wanatuona tumekuwa wagumu na hatuungi mkono harakati zao (hatujabadilika!). Kumbe kati yetu na wao ni sisi tunaweza kwa haki kabisa kuzungumzia mabadiliko kuliko wao. WAo hawana uhalali (legitimacy) wala hoja (reason) za kusema wanataka mabadiliko. Wanayataka mabadiliko yapi na ya nini?
Ndio maana mwisho wa siku jibu lao ni "kuitoa tu CCM madarakani mengine baadaye". Kumbe wakati huo huo wamechukua CCM, mgombea wa CCM na wanachama wa CCM wenye kumuunga mkono mwana CCM mwenzao ambao waliapa kuwa "alipo" na wao "wapo"!
Wenzetu mnaoimba na kushabikia "mabadiliko" yajayo, hivi hamjioni kuwa tayari mmebadilika? au mtabadilika tena ikitokea mshinde au mkishindwa tena mtabakia hivyo hivyo - naamini wengi watabadilika baada ya kushindwa na kujaribu kurudi mlikokuwa - mkitaka mabadiliko tena! Isije kuwa wenzetu ni watu wa kubadilika badilika tu na ujio wa upepo wa mabadiliko! Si kiongozi mwenyewe wa mabadiliko tayari ameshabadilika? na akija kubadilika tena sijui tutawaitaje.
Vinyonga wa kisiasa?
Fikiria.
MMM