Sumbawanga: Mfanyabiashara azikwa akiwa hai

TAJIRI MKUU WA MATAJIRI

JF-Expert Member
Dec 1, 2010
5,722
10,225
Sumbawanga. Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumpiga na kumpora fedha zaidi ya Sh 1.8 milioni kisha kumzika akiwa hai mfanyabiashara wa mazao, Baraka Nyangala (30) na kumsababishia umauti.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Kamishina msaidizi wa Polisi (ACP), Shadrack Masija alisema tukio hilo lilitokea juzi kijiji cha Katazi wilayani Kalambo, ambako walikwenda kununua maharagwe wakiwa wote wanne; watuhumiwa na mfanyabiashara huyo.

Alisema mfanyabiashara huyo mkazi wa mtaa wa Kasisiwe Manispaa ya Sumbawanga akiwa na wenzake hao waliotambulika kwa majina kama Frank Simsokwe (33), Edfonsi Simsokwe (28) na Nikas Lunguya (38) wakitumia usafiri wa pikipiki, walipofika maeneo ya porini walimtaka asimamishe pikipiki yake.

Kamanda huyo alisema baada ya kusimamisha pikipiki hiyo mmoja kati ya watu hao alimpiga kwa rungu kichwani kisha kumpora fedha taslimu Sh1.84 pamoja na pikipiki.

Alisema baada ya kumjeruhi na rungu kichwani, waliamua kuchimba shimo porini kisha kumfukia mfanyabiashara huyo akiwa bado yupo hai na wao kutokomea kusikojulikana.

Alisema baada ya kutoweka ghafla kwa mfanyabiashara huyo, ndugu wa marehemu walitoa taarifa Polisi ambao kwa kutumia intelijensia na wataalamu wa uhalifu wa kimtandao, walifanikiwa kuwakamata watu hao.

ACP Masija alisema watuhumiwa hao waliwaongoza hadi eneo ambalo waliufukia mwili wa marehemu ambapo ulifukuliwa kwa uchunguzi na taratibu nyingine za kuukabidhi mwili huyo kwa ndugu zao kwa ajili ya maziko.

Alisema watuhumiwa hao bado wanashikiliwa na Polisi na watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
 
Back
Top Bottom