Spokes Mashiane, Millie Small na Mimi

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,265
SPOKES MASHIANE, MILLIE SMALL NA MIMI MAPEMA1960s

Dr. Harith Ghassany kaja Tanga kufanya utafiti wake wa mapinduzi ya Zanzibar.

Baada ya utafiti huu akaandika kitabu maarufu, ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.''

Tunakwenda huku na huku mchana na mazungumzo yetu ni yale ya kazi na tukitulia jioni tukiwa pamoja tunahama katika kazi ngumu tunazungumza mambo ya kawaida.

Siku moja nikamwambia kuwa mimi nilikuwa mpiga "flute" yaani filimbi bingwa nilipokuwa shule ya msingi Stanley Primary School Moshi.

Harith naamini hakushangaa kwa kuwa siku moja nyumbani kwake niliikalia Grand Piano nikamkwaruzia nyimbo.

Mshangao wake ulikuwa mkubwa.
Akaniuliza wapi nimejifunza kupiga piano.

Hii ilikuwa Muscat.
Hapa tupo Bombo Area, Tanga.

Basi nikamweleza vipi nilivyokuwa namuiga Spokes Mashiane na kumpatia.

Lakini pale Moshi kulikuwa na kijana mmoja jina lake Juma Ngereza yeye alikuwa mkali na sijui kati yetu sisi wawili nani alikuwa zaidi.

Kila tulipokuwa na wenzetu watatunzunguka kusikiliza tukichuana.
Juma Ngereza alikuwa na kipaji kingine.

Alikuwa anacheza mpira vizuri sana.
Yeye akisoma Muslim School na alikuwa kidogo kanipita umri.

Hizi shule zilikuwa jirani na tukitoka shule wanafunzi wa shule hizi tunakuwa pamoja katika safari ya kurudi nyumbani.

Nakumbuka Juma Ngereza alikuwa akikaa Pasua.

Basi tukikutana ni kila mtu anapiga nyimbo yake mpya kisha anamuachia mwenzake.

Hadi leo kichwa changu kinakamata tune yoyoye "unconsciously" hata kama sisikilizi.

Sasa mimi mtu mzima kipaji hiki nakiogopa lakini mitaani kote tumezungukwa.

Njia nzima mimi na Juma Ngereza tunapiga filimbi hadi tunaagana.
Miaka ikapita nikaondoka Moshi kuja Dar es Salaam.

Katika miaka ya 1970 nikawa namuona Juma Ngereza Msikiti wa Mtoro akija pale kusali mara nyingi Dhuhri na L' Asr.

Siku moja katika mazungumzo akaniambia kuwa amemuoa Asha Rashid.

Nikamwambia Asha Rashid ni dada yangu kwa sababu mama yake na mama yangu walikuwa marafiki wakubwa sisi tukiwa wadogo na nikienda kwao nikimfuata kaka yake Saleh Rashid.

Saleh na Asha tulikuwa shule moja darasa moja Stanley.
Nakumbuka tulivyokuwa wadogo kulikuwa na nyimbo:

''Asha mtoto mzuri,
Kiuno chake chembamba,
Asha acha maringo.''

Sikumbuki nyimbo hii alipiga nani.
Tukimuona Asha tunaimba na alikuwa hapendi.

Asha alikuwa na rafiki yake Amina Ali nyumba zao zinaangaliana Mtaa wa Chini.

Siku moja jioni nakumbaka ilikuwa mwaka wa 1965 nikapita kwa akina Asha nikamkuta amekaa na Amina wameweka katika ''record player,'' nyimbo ya Millie Small, ''Something's Gotta Be Done,'' wanasikiliza.

Wakanikaribisha tukawa tumekaa pamoja.
Nyimbo hii ina ''beat'' na ''melody,'' ya kuvutia sana.

Halafu mashairi ya nyimbo za mapenzi yalikuwa yanakwenda sawasawa na fikra za kijana mdogo katika ''teens'' anaeinukia na kuanza kujitambua akijijua kuwa yeye sasa ni mvulana au msichana.

Umri hawa wakichagua nguo gani avae aonekane amependeza apate kuangaliwa.

Miziki mfano wa hii ilikuwa inakwenda sawasawa na mazingira ya makuzi yetu.

Millie Small alikuwa na sauti ya kitoto kama sisi kwa hiyo tukivutiwa sana na nyimbo zake tukihisi ni katika sisi.

Kwa kweli Millie Small alikuwa umri wetu katuzidi mwaka mmoja au miwili.
Millie Small amefariki mwaka wa 2020 akiwa na umri wa miaka 72.

Wasichana wote hawa wawili Asha na Amina dada zangu walikuwa wazuri sana ukiwaona utawapenda.

Amina Ali nilisomanae Majengo Middle School na kaka yake Abbas nikichezanae mpira na alikuwa na mpira mzuri.

Amina nikimuona Dar es Salaam katika miaka ya 1970 mwishoni lakini ni miaka mingi sijamuona.

Huwa naisikiliza nyimbo hii ya Millie Small kila ninapokaa na kukumbuka udogo wetu.

Wakati naisikiliza nyimbo hii nilikuwa sijanyanyua guitar miaka hiyo.

Leo nikisikiliza nakwenda na nyimbo hii kutoka ''bar'' moja hadi nyingine katika kichwa changu.

Najua hapa Millie yuko ''key'' gani sema D anahama yuko F kaondoka kenda C.

Sithubutu leo kuligusa guitar.

Naweza kulipiga katika fikra na kuna wakati miaka ya nyuma nilikuwa najifanya katika fikra ''conductor'' wa ''orchestra'' nzima.

Naashiria wapi ''strings'' ziingie na wapi ''wind intruments'' zipokee.
Wazimu.

Turudi kwa Spokes Mashiane.

Nyimbo hiyo niliyoiweka hapa inaitwa, ''See You Later,'' lakini jina hili nimelijua baada ya Dr. Harith Ghassany kuniletea CD ya Spokes Mashiane na nikaikuta nyimbo hii.

Nyimbo hii wakati tuko Majengo Middle School 1963 Martin Kiama aliyekuwa Mkurugenzi wa TBC alikuwa na kipindi kwa ajili ya shule kinaitwa ''Viongozi wa Afrika'' akikiendesha yeye mwenyewe na tukitolewa madarasani tunakutanishwa kwenye ukumbi tuliokuwa tunalia chakula radio inawekwa na tunamsikiliza Martin Kiama akiwaeleza viongozi wa Afrika.

Kipindi hiki kilikuwa kinafunguliwa na ''See You Later'' ya Spokes Mashiane kwenye flute na Lemmy Special kwenye saxaphone.

Kwangu mimi ilikuwa furaha mara mbili kwanza nikipenda historia kumsikiliza Martin Kiama akimweleza Haile Selassie wa Ethiopia akimwita, "Simba wa Yuda."

Maisha hakika ni safari ndefu.

Miaka mingi baadae nikiwa mwanafunzi Uingereza nitabahatika kuwajua kwa mbali wajukuu wa Haile Selassie wanafunzi wenzangu.

Ufalme wao umepinduliwa na baadhi yao wakajikuta Uingereza kama wakimbizi.

Hakika ufalme ulikuwa umewatoka lakini hawa vijana ndani ya nafsi zao walikuwa bado wanajiona ni wafalme.

Walikuwa wakija mfano kwenye ''party'' za wanafunzi utawaona vichwa juu na mabega juu vilevile na hawachanganyiki na watu wao huwa katika kundi lao vijana sita, saba au kumi hivi na dada zao wamesimama pembeni wamevaa suti na hawapazi sauti kuzungumza inapobidi. waongee.

Hivi ndivyo walivyolelewa na kufunzwa.
Ukoo wa Kifalme lazima uwe tofauti kwa kila hali.

Siku moja rafiki yangu wa Kiethiopia akanieleza haya akaniambia, ''Hawa ndugu zangu hawajaamini kuwa wao si wafalme tena hata hapa Uingereza wanataka watambulike kuwa wao ni watu wa daraja la juu; hebu waangalie.''

Kabla sijafika Uingereza nilibahatika kufika Addis Ababa na kuona hali ya dhiki iliyotamalaki wakati wa utawala wa Mengitsu Haile Mariam.

Nilikaa hoteli iliyokuwa maarufu wakati wa Haile Selassie - Wabe Shebele Hotel.

Hoteli hii nimeikuta imechoka haitamaniki imebakia jina lake na historia yake ya zamani.

Miaka hii ya karibuni nilikuwa nafanya mahojiano na Hussein Shebe.

Hussein ni kijana wa Kariakoo ambae alikuwa na kipaji kikubwa cha uimbaji kiasi alihamia Nairobi akaweka jina kisha akiwa na bendi maarufu pale mjini The Ashantis walikwenda Ethiopia wakawa wanapiga Wabe Shebele Hotel, Addis Ababa Hussein akiwa ndiye nyota wa bendi.

Katiika mazungumzo yetu Hussein akaniambia kuwa wajukuu wa Haile Selassie walikuwa hawapungui Wabe Shebele kuja kucheza muziki wa The Ashantis na wakawa rafiki zake.

Siku moja mmoja katika wale wajukuu wa Haile Selassie alipembeni mvuta akamwambia, ''Hussein fanyeni muondoke hapa kwani kunakuja balaa kubwa ondokeni balaa hilo lisiwakute mkiwa nchi hii.''

The Ashantis wakafunga virago wakaenda Italy.
Haukupita muda mrefu Haile Selassie akapinduliwa.

Hussein alipokuwa ananihadithia habari hii nikawakumbuka wale wajukuu wa Haile Selassie niliokuwanao Uingereza.

Turudi kwa Martin Kiama na kipindi chake cha Viongozi wa Afrika na Simba wa Yuda.

Ilikuwa raha ya peke yake kwangu achilia mbali kumsikia Spokes Mashiane akifungua kipindi na flute yake na akifunga kipindi na flute yake.

Harith alikuwa na kawaida tukizungumza muziki na mimi nitamweleza mathalan mwanamuziki fulani basi wakati huo yuko Washington DC.

Harith akija tena Tanga kuendelea na utafiti basi katika zawadi anazoniletea ataniletea CD ya mwanamuziki huyo.

Siku moja nilimwambia kuwa mimi nimemjua Bing Crosby kutokana na baba yangu yeye akimpenda sana.

Wala simuoni kuandika mahali jina lakini akirudi Tanga anakuja na CD.

Hivi ndivyo nilivyoweza kupata CD ya Spokes Mashiane na Bing Crosby nyingine nyingi za Nat King Cole.

Hazina hizi ninazo hadi leo imefika miaka 20.


View: https://youtu.be/6Lgf9CBHpSQ?si=lP_q4Xt2pmryXwHA




Kumbukumbu ya mengi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom