Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,329
- 33,138
Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Spika wa Bunge, Samuel Sitta, amewataka wananchi kuepuka kasumba ya kuchagua viongozi wenye uchu wa kutafuta maslahi binafsi badala ya kuutumikia umma.
Amesema viongozi wa aina hiyo wanapatikana kupitia uteuzi unaofanywa na mamlaka zenye dhamana, ama kuchaguliwa kwa njia ya kura katika chaguzi mbalimbali hapa nchini.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wananchi jimboni humo kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, alisema hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa kama changamoto kwa viongozi waliopo madarakani kuepuka matumizi ya vyeo kwa lengo la kujineemesha, bali kuwahudumia wananchi.
Alisema pamoja na kuwepo changamoto zinazotokana na baadhi ya viongozi kutowajibika kwa umma, serikali ina mkakati na mipango inayolenga kupata suluhu itakayochangia kuibua hali bora ya maisha.
Pia alizungumzia kero ya pembejeo inayowakabili wananchi jimboni humo, na kusema imechangia kuathiri uvunaji wa tumbaku.
Hata hivyo, alisema wakati serikali inaanza mkakati wa kuingiza pembejeo, viongozi wasio waaminifu walitafuta njia ya kuhujumu.
Katika mazingira ya kutatanisha pembejeo zilizokuwa zimesalia katika msimu uliopita na ambazo kama kawaida zinatangulia kusambazwa kwa wakulima ili waanze kufunga mitumba ya tumbaku, zilipotea na matokeo yake zikapatikana kwa wafanyabiashara zilipokuwa zinauzwa kwa bei ghali zaidi.
CHANZO: NIPASHE