Simulizi: Msako Wa Mwanaharamu - Sehemu 1 & 2

leadermoe

JF-Expert Member
Feb 15, 2017
1,392
4,573
Silimulizi : Msako Wa Mwanaharamu

Sehemu Ya Kwanza (1)

Katika Pori fulani huko BAGAMOYO

PORI LILIONEKANA TUPU, hakukuwa na kipya zaidi ya miti ileile ya kila siku, kila mmoja ukiwa mahala pake. Kutokana na miti hiyo kuwa mbalimbali kiasi, iliwezekana kiumbe chochote kutembea katika pori hilo bila kupata shida. Mvumo wa upepo wa wastani kutoka baharini vilipiga mruzi kila mara, ukipanda na kushuka. Ndege wa porini kama dudumizi na tetere na wengine wengi walikuwa wakitoa sauti zao kuashiria Magharibi imekaribia huku wengine wakionekana angani wakirudi kwenye viota vyao wakiwa makundimakundi. Ndani ya pori hili lenye miti mikubwa na midogo na mimea yenye mfano wa kamba kamba ambazo zingetoa upinzani kwa binadamu kutembea kwa kuwa si mazingira yake kulikuwamo na watu watatu wakitafuta kitu, mwanaume mmoja na wanawake wawili.

“Una uhakika Chiba kuwa ni eneo hili?” Gina akauliza.

“Ndio ni eneo hili, maana kila nikiangalia kwenye rada yangu hapa, ishara inaishia hapa,” Chiba akajibu wakati huo Jasmine akiwa ameketi juu ya mzizi wa mti mkubwa. Gina akachukua ile rada kutoka katika mkono wa Chiba na kuitazama; juu katika kioo chake kulionekana mchoro kama wa ramani iliyopigwa picha kwa satellite na kitu kama doti nyekundu ilikuwa ikiwakawaka kwa kufifia.

“Mbona hii signal kama inafifia?”

“Betri inakwisha muda si mrefu, kumbuka tangu asubuhi inafanya kazi na sijaichaji ina wiki sasa,” Chiba akajibu na kufungua chupa yake ya maji. Jasho lilikuwa likimtiririka bila mafanikio ya kile anachokitafuta. Jasmine akiwa na begi lake mgongoni lenye vifaa vyake vya kazi alikuwa akisikiliza tu hakujua nini cha kuongea.

“Lakini Chiba, uelekeo ndio huu, tuko sahihi?” Jasmine aliuliza kwa taabu kidogo kutokana na uchovu uliomkabili. Watu hawa watatu walikuwa katika pori hilo katikati ya Bagamoyo na Mbegani kwa operesheni maalum ambayo ilikwishawachukua siku mbili katika eneo hilo na isioneshe mafanikio.

“Yaani kiukweli kabisa eneo hasa ni hili, tatizo ni wapi kwa maana signal yangu inaishia hapa na haiendelei kuonesha kama kuna eneo lingine, hatuna budi kupiga kambi hapa na kulala usiku huu,” Chiba aliwaeleza wenzake.

“Ha, nani alale hapa porini?” Jasmine aling’aka huku akiwa kapata nguvu ya kusimama.

“Wote lazima tulale hapa,” Chiba akasisitiza.

“Hakuna kulala hapa ni mpaka tupate jibu ndiyo itakuwa njia ya kutoka ndani ya pori hili,” Gina naye akasisitiza kwa kuongezea sentensi nyingine.

“Enhe! Hilo ndilo nilikuwa nalisubiri kwa muda mrefu sana, nilifikiri mmechoka kumbe bado mna nguvu,” Chiba aliwaeleza. Wakapeana moyo na kuendelea kutafuta humo porini kwenye vichaka na juu ya miti huku jua likichwea na kagiza kuanza kuingia taratibu.

* * *

Dakika chache baadae giza lilikuwa juu ya uso wa nchi wakati Gina, Jasmine na Chiba wakiwa wametawanyika kila mtu upande wake, wakiendelea kuwasiliana kwa walk talk zao ambazo ziliunganishwa kwa mtambo mdogo uliobebwa katika begi la Gina. Majira kama ya saa nne usiku hivi ndipo Gina alipoona kitu kilichomshtua.

“Shiiit!” akang’aka na kuwaita wenzake kwa kutumia chombo hicho. Dakika nne baadae wote waliungana wakimulika eneo hilo na tochi zilizofungwa vichwani na kuwekwa katika paji la uso wa kila mmoja wao, zote tatu zikamulika mahala pale.

“Hii ni simu ya Scoba!” Chiba akawaambia kisha akasimama wima na kuwa kama anayeangalia kitu katika vichaka hivyo huku akihema kwa nguvu.

“Vipi?” Gina akauliza.

“Kwa vyovyote hapa ni eneo la tukio”.

Jasmine akaiokota ile simu kwa mkono wenye gloves na kuiweka ndani ya mfuko wa plastiki kisha wakaanza kupita vichakani polepole huku wakiangalia kwa makini. Saa moja baadae Gina akakutana na kitu kingine, mkufu, wakauokota na kuuweka kwenye mfuko mwingine wa plastiki. Wakati msako huo ukiendelea Gina alikuwa akijawa na machozi lakini alijaribu kujibana asilie kwa sauti, moyo wake ulipoteza matumaini.

Saa sita usiku, ukimya ukiwa mkubwa katika mapori hayo, Jasmine alijikwaa vibaya na kuangukia kitu kama binadamu.

“Oh, Shiit!” akapiga kite huku akijiinua kutoka pale alipoanguka. Kurunzi yake ikamulika mwili wa binadamu uliolala kimya ukiwa na damu iliyoganda katika nguo yake iliyofanana na ovaroli la kijani cha mgomba.

“Scoba! Aiyaaaa!!!” Chiba alijikuta akichanganyikiwa alipouona mwili wa Scoba na kuutambua kwa ile beji yake iliyobanwa katika mkanda wake wa kiunoni. Alikuwa amelala kimya akiwa katapakaa nyasi kila mahali na parachute lake likiwa kando juu ya miti midogo midogo.

Daktari Jasmine harakaharaka, akashusha begi lake na kutoa kifaa cha kupima mapigo ya moyo ‘Stethoscope’ na kuipachika masikioni mwake huku tayari Chiba amekwishafungua jaketi la juu la Scoba na kumwacha kifua wazi. Jasmine baada ya kupachika masikioni mwake kile chombo, upande wa pili akauweka juu ya kifua cha Scoba upande wa kushoto na kutulia kimya huku akikihamisha hamisha lakini eneo lile lile.

Wote walibaki kimya wakiweka matumaini yao kwa mwanadada huyo daktari. Baada ya kusikiliza kwa makini mkubwa huku akifinya sura na kuiachia akachukua kitu kingine na kumfunga katia kiungo cha sehemu ya juu ya mkono na ile ya chini, kile chombo kilikuwa kama mpira Fulani wenye kitu kama saa upande mmoja, kisha akapachika kile kidubwasha cha kwanza pale upande wa juu wa kiwiko na kufanya kama anajaza upepo kwa kuminyaminya kitufe kingine na mara ule mpira ukajaa upepo na kubana sawia mkono wa Scoba, Jasmine akawa akiangalia kile kitu kama saa huku akiusoma ule mshale wake uliokuwa ukitikisikatikisika huku ukirudi chini. Aliporidhika akauachia ule upepo na kutoa ile mashine.

“Vipi?” Chiba akawahi kuuliza.

“Mzima, ila mapigo ya moyo yako chini sana,” Jasmine akajibu huku akichukua kitu kingine ndani ya begi lake, akatoa chupa ya maji ‘drip’ na kumpa Chiba aishike kwa juu kwa mtindo wa kuinging’iniza kisha akachukua sindano na kutoboa moja ya mishipa ya Scoba katika mkono wake na kupachika ule mpira, akachezea kidubwasha fulani na kisha akasimama akiwa kajishika kiuno. Akitazama huku na huko.

“Tumsogeze hapo kwenye hako kamti,” akasema na kisha Chiba akampa Gina ile chupa aendelee kuishika wakati yeye na Jasmine wakimsogeza Scoba mpaka walipopataka na kumuweka vizuri.

“Piga kambi mwanaume, tufungue zahanati,” Jasmine akamwambia Chiba ambaye tayari alitoa katika begi lake aina ya kitambaa kigumu kisichopitisha maji, akakibana kwa vyuma Fulani alivyovito humohumo na kisha akafyatua kitu kama mwamvuli mkubwa na kufunika mahali hapo, wote wakawa ndani ya kijumba kidogo kilichoweza kuwahifadhi dhidi ya wadudu sumbufu.

“Atapona?” Chiba aliuliza.

“Bila shaka,” akajibiwa na Jasmine.

“Sasa Amata atakuwa wapi? Au inawezekana akawa jirani hapa hapa?” Gina aliuliza kwa dukuduku.

“Nafikiri ni maeneo haya haya kama alifanikiwa kuruka kama mwenzake, maana Scoba inaonekana aliruka na hapa anaonekana ameumia sehemu ya nyuma ya shingo kwa kuwa ndiyo inayoonesha uvimbe,” Jasmine alieleza.

“Tuendelee kumtafuta maana bibi yake huko aliko kila dakika anapiga simu mpaka kero,” Chiba aliwaambia wenzake.

“Na anavyompenda, yaani leo halali, na bila kumzuia angekuja huku porini,” Gina akaongeza.

“Eeh jamani huko mbali, kwani sisi hatupendi?” Jasmine akauliza kwa shaka.

“Sijasema hivyo, wote anatupenda kama watoto wake, ni jambo zuri sana”. Wakiwa katika kuongea mara wakasikia michakacho ya watu au wanyama, hawakujua ni kitu gani, Chiba akanyanyuka na kukamata shotgun yake mkononi tayari kwa lolote na wakati huohuo Gina naye alikuwa tayari upande wa pili wa kibanda kile naye shotgun ikiwa mkononi inasubiri amri tu.

Ndani ya kile kibanda Jasmine naye alikuwa tayari na bastola mkononi.

Kutoka katika kile kichaka wakaibuka vijana wanne wakiwa na mbwa watatu, mikononi mwao walikuwa wameshikilia mavisu makubwa na mikono yao ikiwa imelowa damu.

“Amani jamani!” mmoja wa wale vijana akasema.

“Amani kwa wote,” Chiba akajibu wakati huo Gina alikwishasimama pembeni na bunduki yake ilikuwa ikwaelekea vijana hao.

“Vipi porini hapa na usiku huu? Hamuogopi? Hili pori sio zuri kabisa ndugu zangu, fanyeni hima muondoke,” mmoja wa wale vijana aliyekuwa kifua wazi aliwaeleza Chiba na wenzake.

“Tupo kazini kaka,” Chiba akajibu.

“Najua lakini hili eneo lina mambo ya ajabu, watu wengi hupotea humu na hawajulikani wanakokwenda, vitu vya ajabu hunekana na kukipambazuka huwa tunashuhudia mabaki ya miili ya binadamu,” mwingine akaeleza.

“Hapa ndio Mlingotini, wakiwakamata watawatoa sadaka,” Yule wa kwanza akaeleza.

“Nimewaelewa, nisikilizeni, mnamwona huyu?” Chiba akawafunulia kile kihema na wale jamaa wakamwona Scoba aliyekuwa amelala kimya na ile drip ya maji ikiendelea kushuka na kuingia mwilini mwake.Wale jamaa wakatazamana na kisha kurudisha macho kwa Chiba.

“Huyu ni nani?” wakauliza.

“Rafiki yangu, nimekuja kumtafuta huku tangu jana asubuhi haonekani,” Chiba akaeleza.

“Hamjaona mwingine kama huyu?” Gina akadakia swali.

“Hapana ila jana kuna kitu cha ajabu kimetokea huko baharini, tuliona kama ndege sijui ikiwaka moto anagani kisha ikaanguka baharini nafikiri, kwani tulipokuja kutazama hatukuona chochote,” wakeleza. Ikawa zamu ya Gina na Chiba kuangaliana.

“Eneo gani mlipoona huo moto au mlipuko?”

“Huku, usawa wa baharini, halafu ule moto ukaangukia huko huko,” wakajibu huku wakionesha uelekeo wa tukio lile kwa vidole vyao. Chiba akamtazama Gina kisha wote wakatikisa vichwa vyao kuashiria wameelewa jambo.

“Tunafanyaje?” Gina akauliza. Chiba akabaki kimya akifikiri jambo.

“Jamani twendeni kijijini hapa mahala si pazuri hata kidogo,” mmoja wa wale watu akatoa ombi na kisha msafara ukaanza kwa kumbeba Scoba huku na huku kwa kutumia miti iliyofanywa kama machela.

“Tukiwa kijijini tutawaonesha vizuri kule ambako tuliona tukio hilo,” mwingine akaeleza huku msafara ukiendelea katika mapori na usiku wa giza nene.

* * *

Siku iliyofuata…

MADAM S aliweka sawa pazia la dirisha ofisini kwake kisha kurudi kitini kukaa kama mwanzo huku kichwa chake kikiwa hakijatulia hata kidogo. Aliitazama saa yake ya ukutani na kurudisha macho yake mezani kwa mara nyingine kabla hajagutuliwa na mlio mkali wa kengele ya simu. Akainyakua kwa shauku na kuiweka sikioni, akashusha pumzi kwa nguvu huku mkono mmoja akiwa kajishika moyoni.

“Ndiyo, Chiba…” akaitikia namna hiyo huku uso wake ukijawa na shauku ya kujua kilichojiri.

“Operesheni imefanikiwa kwa asilimia hamsini, tumempata Scoba katika hali mbaya lakini sasa anaendelea vyema…”

“…Endelea…”

“…bado hatujampata Kamanda Amata na pia hatuna fununu yoyote juu yake,” Chiba akajibu na kutulia kimya.

“kwa hiyo nini kimewakuta hasa kwa maelezo ya Scoba?”

“Scoba bado hawezi kuongea, ila tunafanya utaratibu wa kumfikisha hospitalini kwa matibabu zaidi, ila kwa haraka haraka tumegundua kuwa ndege waliyokuwa wakitumia ama imepata hitilafu na kuanguka au imetunguliwa…”

“Mungu wangu! Mmeona mabaki yoyote ya ndege au imekuwaje?”

“Hapana Madam, hakuna mabaki ya ndege tuliyoyaona ila kwa uchunguzi tulioufanya inaonekana ndege hiyo imeangukia baharini…”

“Sawa, kwa hiyo tunahitajika kugeuka samaki sivyo?” Madam akauliza kwa lugha tata.

“Ndiyo Madam, inabidi iwe hivyo,” Chiba akajibu.

“Sawa, aaaaaaa… nipe dakika kadhaa kisha nitakupigia,”

“Copy!” Chiba akakata simu.

Madam S alitulia na kutuliza akili yake huku akiizungusha huku na kule, kisha akapiga ngumi mezani na kuinua simu yake akaiweka sikioni na kubofya tarakimu kadhaa. Upande wa pili ukaitikia.

“Hello!” sauti nzito ikalipenya sikio la mwanamama huyo.

“Msaada wa haraka tafadhali…”

“Wapi?” ile sauti ikauliza.

“Nyumba ya samaki,

“Copy!” ile simu ikakatwa. Madam S akatoka ofisini na kuvaa koti lake la suti alilokuwa amelitundika kwenye kining’inizio kilichochongwa kwa fimbo ya mpingo, akatoka na kuubana mlango nyuma yake.

* * *

KURASINI…

Ndani ya meli mbovu iliyotelekezwa kwa miaka mingi katika eneo hilo watu wawili walikutana kwa mazungumzo ya dakika zisizozidi tano. Madam S alikuwa akitazamana na Inspekta Simbeye katika mkutano huo wa dharula.

“Ndiyo Madam!” Simbeye alianza namna hiyo mara tu baada ya kuingia katika meli hiyo chakavu iliyozama nusu na kubaki nje nusu ilihali ndani yake kuna mitambo ya kuchunguza usalama wa baharini kama rada ambazo huweza kuona kitu chochote kisicho samaki kikiwa zaidi ya maili mia moja chini ya maji. Vijana wanaoijua kazi hiyo wa Jeshi la Polisi na lile la Wananchi walikuwa wakifanya kazi humo usiku na mchana; hakuna aliyewaona wakiingia wala wakitoka, na hakuna aliyewahi kujua kama meli hilo linalozidi kuoza kwa nje kwa nini lilikuwa halihamishwi mahala hapo.

“Njiwa wangu amepigwa manati, kadondoka majini, alikuwa na mayai mawili, moja nimelipata lakini lingiine mpaka sasa sijalipata wala kuliona…” Madam alimwambia Simbeye.

“Oh, pole sana, nilipata taarifa ila sikujua mayai ya nani! Sasa unatakaje?” akauliza Simbeye.

“Nahitaji samaki, japo wawili tu wakaangalie kule chini?”

“Umesomeka Madam,” Simbeye akajibu kisha akaagana na Madam S na kuondoka zake kutoka ndani ya meli hilo.

Dakika mbili baadae, boti iendayo kasi inayojulikana kwa jina la ‘KINYAMKERA’ inayoweza kupita juu na chini ya maji ilichomoka ndani ya meli hiyo ikiwa na vijana watatu waliovalia tayari kwa kuendesha maisha majini. Safari kuelekea katika bahari ya Bagamoyo ilikuwa imewiva.

* * *

Simu ya Chiba akafurukuta mfukoni akainyanyua na kiuiweka sikioni.

“Tuko njiani!”

“Copy!” kisha ile simu ikakatwa. Chiba akawatazama wenzake.

“Madam yuko njiani!” akawaambia.

Wakaitikia kwa vichwa huku wakiwa tuli wakiangalia huku na kule kwa vifaa vyao maalum, pia wakitumia kompyuta kumtafuta Kamanda Amata kwa picha za satellite wakijaribu ku-ping tarakimu za utambulisho wake lakini haikuonekana hata dalili za mtu huyo kuonekana. Chiba alimtazama Jasmine aliyekuwa na Gina muda huo.

“Dokta, vipi mgonjwa?” akamuuliza.

“Yuko poa, naona sasa anaweza kuongea japo si kwa ufanisi sana,” Jasmine akajibu na kisha wote wakarudi kwenye ile hema yao ambayo sasa walikuwa wameijenga tena kijijini pembezoni kidogo. Nukta hiyo hiyo kifaa cha mawasiliano mgongoni mwa Gina kikakoroma, akaukwanyua mkonga wa chombo hicho na kuupachika sikioni.

“Unasomeka,” akitikia.

“Nipe uelekeo tafadhali…”

“ Nyuzi 278 Kaskazini kwa kipimo wima na 120.56 Mashariki kwa kipimo ulalo,” Gina akajaribu kujibu kwa kutumia vipimo vya ardhini kuielekeza helkopta hiyo ya polisi kufika eneo lile bila tabu. Haikuchukua muda lile helkopta liliwasili eneo hilo na kutafuta uwazi ili litue. Lilipopata nafasi ya kufanya hivyo likatua katika uwanja wa shule. Chiba, Gina na Jasmine sasa wakisaidiwa na vijana wa pale kijijini walimbeba Scoba hadi kwenye dege hilo na kumpakia kisha wakaondoka zao bila kuchelewa.

“Poleni kwa kazi vijana,” madam aliwapa pole.

“Asante lakini kazi haijaisha,” Gina akawa wa kwanza kujibu.

“Najua msijali, mnaweza kutazma chini?” akawauliza. Kisha wote wakajaribu kuangalia kwa kupiti kioo kikubwa kilicho chini ya dege hilo.

“Nini kile?” Gina akauliza.

“Vijana washafika wanajaribu kutazama kama Kamanda atakuwa kabaki huko au vipi, wamekuja na boti inayopita ndani ya maji,”

“Waoh!” Gina akashangaa

“Lakini sina uhakika kama Amata atakuwa huko kwenye maji, maana kama yuko huko basi amekwishakufa,” Jasmine akaeleza dukuduku lake.

“Usiseme hivo Jasmine,” Chiba alimkata kauli.

“Kamanda hawezi kufa kijinga hivyo!” Scoba alijibu kwa tabu kidogo, wote wakageuka kumtazama kutoka pale alipolala.

“Naona ana nguvu sasa, anaweza kuongea” Dkt. Jasmine alimweleza Madam S.

“Yeah, ila ngoja tufike mahala salama,” akaeleza Madam na wote wakahafiki.

* * *

Wale vijana watatu wakiwa chini ya maji waliweza kufika eneo ambalo ndege ile iliangukia, vilikuwa vipande vichache vilivyonasa katika miamba na mapango ya baharini, haikuwa ndege kamili au vile vipande havikukamilika. Waliendelea kuchunguza hapa na pale ndipo wakagundua kuwa ndege ile ilidunguliwa kutokana na alama kubwa nyuma kabisa upande wa chini, kipande hiko hakikuathiriwa na mlipuko ule.

Walifanya juu chini na kufanikiwa kupata kisanduku cheusi (black box) ambacho kazi yake ni kurekodi mwenendo mzima wa ndege ikiwa angani. Walipokipata na kukihifadhi kazi iliyobaki ilikuwa ni kutafuta binadamu wa pili kama ataonekana. Saa nzima ilipita hawakufanikiwa, walipekuwa kila kona ya mwamba na pango lakini hakukuwamo mtu yeyote wala mabaki yake. Walipokamilisha awamu hiyo ya zoezi wakaondoka zao na kurudi kwenye boti yao. Wakiwa ndani ya boti hiyo ya kisasa walitoa taarifa kwa Simbeye na wakatakiwa kurudi mara moja.

* * *

SHAMBA (Safe HOUSE)

Scoba aliketi kimya juu ya kiti cha vono, mbele yake kulikuwa na Madam S na Jasmine.

“Nina uhakika Kamanda hajafa, ama ameangukia mbali au yuko mahala, kwa sababu yeye alikuwa wa kwanza kutoka kwa parachute,” Scoba alieleza.

“Kwani nini hasa kimewatokea?” Madam alisaili.

“Tumedunguliwa, lakini hatujui hata kombola limetokea upande gani, sasa inakuwa ngumu kueleza, mi nilmestuka kitu kimeshafika mkiani, kilichofuatia sikuwa na jinsi zaidi yaku – evacuate. Mwamvuli wa Amata ulikuwa wa kwanza kufyatuka na kumtoa nje na mimi ulifuatia,” akaeleza. Madam S akabaki kimya kabisa akiwa hajui la kusema, baadae akarudisha uso kwa Gina.

“Mwanaharamu aliyefanya hivi lazima apatikane,” Madam S akasema kisha akamgeukia Scoba.

“Lakini kuna mlichogundua?”

“Kiukweli bado, pale tulikuwa tunakiona kijiji cha Kaole na vile vya pembezoni zaidi ni mapori mpaka Mbegani”.

“Sasa nani kawatungua?”

“Inawezekana kabisa ni wanajeshi wa kambi ya Mlingotini kwani tulipita pande hizo hatukuwa na ruhusa yoyote,” Scoba akaeleza na Madam S akatikisa kichwa. Kisha akatoka na kuwaacha Jasmine na Scoba yeye akatokomea katika chumba kingine.

Dakika kama tano baadae akarudi na taarifa nyingine kwa Scoba kuwa kambi ya jeshi ya Mlingotini hawajadungua ndege yoyote eneo hilo kwani wao hawawezi kudungua ndege bila idhini ya mkuu wa kikosi.

“Basi, kutakuwa na kambi ya siri eneo hilo, hili ndio tatizo la serikali kuuza viwanja kiholela, hata mnayemuuzia hamumjui wengine magaidi hawa,” Scoba akazungumza huku akisimama.

Madam S alimtazama Scoba kwa tuo na kisha akamtupia swali.

“Hatujamuona kamanda kabisa hata kwenye mitambo yetu haonekani, kama hajafa atakuwa wapi?”

“Kamanda hawezi kufa, tuendelee kumtafuta,” Scoba akajibu.

Rudi siku tatu nyuma… ‘siku ya tukio’

SHAMBA

KAMA NI SURA YA HASIRA basi ilionekana wazi kwa Madam S alipokutana na vijana wake ndani ya nyumba yao ya siri huko Gezaulole. Kikao hiki kiliitishwa haraka sana baada ya tukio lisilotegemewa kutokea eneo la Darajani katika Barabara ya Nyerere, saa sita mchana kweupe.

Kamanda Amata alikuwa kajiinamia kama awazae jambo wakati wengine wakijaribu kuchanganya akili kwa hili na lile juu ya hilo.

“Lakini mi nilisema kuwa mtu yule asilindwe na askari wa kawaida kwani ana mbinu nyingi za kujiokoa,” Chiba akaeleza.

“Yeah ni kweli lakini kumbuka pia sisi si kazi yaetu kulinda watuhumiwa,” Madam akamjibu. Ukimya mwingine ukatawala.

“OK!” sauti ya Madam S ikawazindua vijana wale watano waliokuwa katika lindi la mawazo ya sintofahamu.

“Lazima tumsake na tumtie mkononi, mtu mmoja hawezi kutunyanyasa sisi tena wanataaluma wa kazi hii. Tutamsaka na kumleta tena hapa, Chiba jaribu kufuatilia wapi anaweza kuwa ameelekea ili tuone la kufanya,” Madam akatoa amri na Chiba akaondoka eneo hilo kuelekea kati kachumba chake maalum.

“Usione niko kimya yaani huyu bwana ananiumiza kichwa, nikikumbuka jinsi nilivyompata kwa shida, we acha tu!” Kamanda Amata alimwambia Madam S huku akitoka eneo hilo.

“Najua lakini naamini tutampata tena,”

“Ndiyo tutampata lakini kwa jinsi ile ina maana huyu jamaa bado ana nguvu sana na hatujui kajipanga namna gani,”

“Unalosema ni kweli, kwani hata mbinu iliyotumika kutekwa kwake mbele ya mikono ya polisi haijawahi kutokea na wala hatukutegemea, imekuwa kama filamu ya Hollywood, aisee!” Madam alimweleza Amata huku wote wakitembea kwenye ujia mrefu ndani ya jengo hilo.

“Yatupasa tuwe makini sana, hatujui mara hii ataibukia wapi. Na tukimpata safari hii atajuta kuzaliwa dume,” Amata akaongea kwa uchungu.

Madam S akasimama na kumtazama kijana huyo aliyekuwa amekwishasonga mbele kwa hastua kama tatu hivi, naye akasimama baada ya kumwona bosi wake kafanya hivyo, wakatazamana.

“Utamfanya nini?” Madam akauliza.

“Nitamtoa korodani!”

“Na we’ unaweza!”

Kisha wakaendelea na safari yao katika jingo hilo.

* * *

CHIBA alikuwa ametingwa kwenye mitambo yake, kompyuta kadhaa zilimzunguka na mashine nyingine mbalimbali. Ndani ya chumba hicho aliweza kuikusanya dunia yote na kuiweka ndani ya kioo kimoja cha kompyuta. Msako wake aliuanzia palepale eneo la tukio, Darajani, akijaribu kufuatilia uelekeo wa chopa iliyombeba mtuhumiwa wao mara tu baada ya kukombolewa kutoka katika mikono ya polisi, ndani ya gari ya chuma alipofungwa minyororo miguuni na mikononi na kuacha askari sita wakiwa hawana uhai.

Chombo chake kilimuonesha uelekeo wa Kaskazini Mashariki, yaani maeneo ya Mbweni mpaka Bagamoyo, lakini alishangaa kila akifika eneo fulani la Mbegeni ule mtambo ulikiuwa unashindwa kueleza uelekeo sahihi wa kile chombo, akajaribu na kujaribu lakini alishindwa. Akashusha pumzi ndefu na kujiegemeza kitini kabla ya kunyanyua simu na kumjulisha Madam S juu ya hilo. Ilichukua dakika moja tu mwanamama huyo kuwasili ndani ya chumba hicho maalum cha mawasiliano. Baada ya kuongea mawili matatu na Chiba walifikia azimio la kumsaka mtu huyo iwe angani au ardhini. Kikao kikaitishwa tena na wote wakakutana.

Meza hii ndiyo daima hufanyiwa maamuzi mazito na mepesi, ya kukata au kuua, kutesa au kutekenya, vyote huamuliwa hapa. Ukiitazama utaiona tu, kwanza inaviti sita kwa idadi yao, kila mtu hukaa kiti hicho hicho kila wakati, ni sawa na kusema ndicho ‘afisi’ yake kwa hapo, meza ya duara.

Mara tu baada ya kukutana, kikao kikaanza kwa kumsikiliza Chiba akieleza kile alichokigundua katika mtafuto wake wa kimtandao.

“Haya kama alivyotueleza Chiba, sasa hapa tunakwenda kimakundi, kundi moja na la kwanza litakuwa angani hili ni Scoba na Amata, kundi la pili Gina na Chiba mtakuwa ardhini mkifuatilia kwa chini na la tatu ni mimi (Madam S) na Jasmine tutakuwa katika uokoaji. Hivyo basi sasa tuingie kazini”. Madam S alipanga kikosi chake, hakuna aliyekuwa na mashaka katika hilo kwani walijua kuwa mwanamama huyo huwa hakosei kwenye kupanga. Kila kitu kikawekwa sawa, kila mmoja na mwenzake wakajipanga ni wapi pa kuanzia, kazi ikaanza.

JESHI LA WANAMAJI KIGAMBONI

KAMANDA AMATA NA CHIBA waliwasili katika kambi hiyo majira ya saa tisa alasiri wakiwa tayari kwa shughuli hiyo ngumu. Wakati huohuo Chiba na Gina walikuwa tayari katika gari wakielekea Tegeta mpaka Mbweni kuendeleza msako.

Baada ya Kamanda na Chiba kusaini kabrasha fulani fulani pale jeshini tayari kuchukua ndege ndogo inayoweza kutua na kuruka majini, walikabidhiwa kofia ngumu za kuvaa na kupewa maelekezo machache na rubani wa jeshi kisha wakaingia katika ndege hiyo ndogo yenye uwezo wa kubeba watu watatu tu. WAkaketi na kufunga mikanda, Scoba kama kawaida yake ndiye alikuwa rubani mkuu wa kuirusha ndege hiyo.

“Hivi wewe kuna kitu hujawahi kuendesha?” Amata akauliza kwa utani.

“Kipo,”

“Kipi?”

“Ungo”.

Wote wakaangua kicheko na wakati huo tayari injini ilikuwa ikizunguka na Scoba akiitoa ndege hiyo mahala pake kuelekea katikati ya bahari tayari kuruka na kuanza safari ya msako.

Dakika tano baadae walianza kuliona jiji la Dar es salaam kutoka juu jinsi linavyopendeza. Muda wote walikuwa wakiwasiliana na Chiba na Gina waliokuwa wakisafiri kwa gari kuelekea upande huo. Walipofika eneo ambalo walihisi ndipo hasa wanapopataka, juu kabisa ya anga la Bagamoyo, pande za Mbegani kuja Kaole walikuwa wakitumia darubini maalumu yenye nguvu kutazama chini kama wanaweza kuona chochote chenye maana kwao huku picha zile moja kwa moja zikirushwa mpaka kwenye kompyuta ya Chiba ambayo alikuwa nayo ndani ya gari hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi na mwanadada Gina.

“Mpaka sasa hatuoni chochote zaidi ya misitu na nyumba za wenyeji,” Kamanda alimwambia Chiba.

“Scoba Scoba, shusha ndege chini zaidi angalau futi elfu mbili tuone kama twaweza kugundua chochote,” Chiba akatoa maagizo na Scoba akateremsha ndege hiyo kama alivyoagizwa, wakaanza tena kutazama kwa kile chombo huku ndege hiyo ikizunguka huku na huko bila kutua chini. Baada ya mzunguko wa muda mrefu, wakaingia na upande wa bahari na kwenda mbali karibu na pwani ya Zanzibar, kisha wakarudi tena upande wa Pumbuji.

“Hey! Amata, hebu cheki pale!” Scoba akamshtua Amata, naye akatazama kwa ile darubini.

“Shiit, kile ni kisiwa sivyo?” Amata akauliza.

“Hiki kisiwa nakijua, kulikuwa na kitu pale cheupe kinang’aa kama paa jipya lakini kimepotea na kuchukua rangi ya uoto uliopo,” Scoba aliongeza.

Kamanda Amata akamwonesha ishara ya kidole ya kwamba aizungushe ndege hiyo na kukizunguka kile kisiwa ikiwa ni pamoja na kuteremka chini zaidi.

“Scoba unaanza kuzeeka, lile ni pori tu!” Amata akamwambia Scoba huku akigeuza ile darubini upande mwingine wa Kaole. Bado ndege ilikuwa haijamaliza kuzunguka kile kisiwa, Scoba aliendelea kutazama kwa makini sana.

“Kwa hiyo tunafanyaje?” Scoba akauliza.

“Tucheki na upande ule kuleeeee,”

“Ok!” Scoba akajibu na kuiweka sawa ile ndege kisha akainyanyua juu ili kuendelea mbele.

* * *

Scoba hakuwa amekosea kwa kile aichokiona, na Amata vilevile hakuwa amekosea kwa kile alichokisema, hivyo basi kila mmoja alikuwa sawa kwa wakati wake. Katika eneo hilo kulikuwa na kisiwa kikubwa kilichozungikwa na mikoko na uoto mwingi wa baharini.

Hiyo kama haitoshi, ndani ya kisiwa hiki kulijengwa jingo kubwa lenye vitu vingi sana, na ujenzi wa jingo hili ulikuwa ukifanyika kwa siri sana, hakuna mwananchi aliyejua wala kiongozi wa serikali. Walichokiona wao ni nyumba moja tu ya kawaida sana iliyojengwa juu ya kisiwa hicho, lakini kumbe chini yake kulikuwa na ngome kubwa iliyojengwa kwa ustadi sana. Na kati ya vyumba vingi vilivyopo, kimojawapo kilikuwa na mitambo ya rada, inayoweza kuona chombo chochote kinachopita angani usawa wa kisiwa hicho au kinachokuja majini usawa wa kisiwa hicho. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na wataalam wanaofanya kazi kwa siri na zamu kila siku kwa saa ishirini na nne.

Siku hii, watu watatu walikuwa ndani ya chumba hicho wamejifungia, walikuwa wametingwa kusoma kitu kikubwa kama saa lakini hiki hakikuwa na tarakimu yoyote isipokuwa kilikuwa na mistari ya duara kadhaa na mstari mmoja wa rangi ulikuwa unazunguka huku na kule.

Mlio wa kitu kama bip ukaanza kusikika ndani ya chumba kile. Mlio huo ulianza kusikika kwa mbali sana lakini baadae ukawa na sauti kubwa.

“Vipi?” mmoja akauliza.

“Kuna kitu kama ndege hapa naiona inaelekea upande huu wetu,” akajibiwa. Yule bwana akasogea karibu na kile chombo na kuangalia.

“Mmmhh! Ni ndege hii hebu washa ile camera kubwa tuone,”

Nukta hiyo hiyo, kitu kama antenna kikaibuka kutoka katikati ya mapori na kusimama wima kati ya miti. Ndani ya chumba hicho waliweza kuona picha halisi ya ndege ile.

“Nani hawa?” mwingine akauliza huku akiwa katumbua macho.

“Sijui, hebu toa taarifa kwa mkuu wa kikosi,”

Yule kijana akatoka na kuelekea pembeni kisha akachukua simu na kukoroga tarakimu fulani.

“Mkuu, kuna ndege tunaiona kwenye rada inaelekea upande huu, hatua gani tuchukue?” Yule kijana akaongea huku akitweta.

“Subiri nakuja hukohuko,” akajibiwa.

Sekunde kumi hazikupita mlango ukafunguliwa na mtu mmoja mwenye tambo kubwa la kimazoezi akaingia; moja kwa moja akaiendea ile meza na kutazama ile picha iliyopigwa kwa kamera ya siri.

“Shiit! Hii ni ndege ya jeshi, fanyeni hivi, ikifika mbali jaribuni kuona nini kinaendelea ndani kisha mitumie hizo picha afisini kwangu,”akawaambia. Wale jamaa wakaendelea kuisoma kila inavyozunguka, na baada ya kukaa kwenye kona nzuri waliweza kuipiga picha na kuona nini kipo ndani ya ndege hiyo. Wakapeleka taarifa kuwa kuna watu wawili wanaoonekana kupiga picha fulani. Kutoka kwa Yule jamaa akawaamuru wajaribu kunasa mawasiliano yao ili kusikia nini kinazungumzwa.

Zoezi hilo halikuchukua hata dakika mbili, kutoka katika kile chumba, wakaweza kunasa mawasiliano kati ya Amata na Chiba. Baada ya kujua kuwa ni wao wanaowindwa amri tu ikatolewa na mkuu wa kikosi.

“Ilipue,” akawaamuru.

“Haiwezi kutuletea matatizo tukiilipua?” kijana mmoja akauliza.

“Nimesema lipua tena haraka!”

Hakukuwa na lingine, missile equipment ikafunguliwa na kujitokeza juu kidogo ya ardhi lakini ndani ya msitu huo wa mikoko kisha ikafyatuliwa na moja kwa moja ikafuata ndege ile iliyokuwa na Amata na Scoba ndani. Mlipuko haukuwa wa kutisha sana lakini ndege ile ilikatikavipande na kuangukia baharini.

* * *

Ndani ya ile ndege, Scoba alisikia kengele iliyopiga kwa nguvu, akatazama kwenye dashboard yake na kuona ishara kuwa wapo kwenye shabaha

“Amataaaaaa!” akapiga kelele baada ya kuona kwenye kuwa wamedunguliwa. Kitendo bila kuchelewa, Kamanda Amata akabonyeza kidubwasha kilicho chini ya kiti chake na vyuma vilivyoshika kiti hicho vikaachiana wakati huo tayari Scoba keshabinya kinobu kilichoandikwa neno ‘Evacuate’. Ile ndege ikafunguka juu na kiti cha Amata kikatolewa nje na kuiacha ile ndege.

Hakuna alichokishuhudia zaidi ya mlipuko mkubwa angani na ile ndege kupasuka vipandevipande.

“Scoobbbaaaaa!!!!!” Kamanda Amata alipiga kelele akiwa hewani lakini hakumwona Scoba. Vyuma vilivyoruka kimojawapo kikampiga kichwani Amata akapoteza fahamu akiwa anaelea angani huku parachute lililokuwa tayari limefunguka likimbeba na kumteremsha taratibu.

Scoba, mara tu baada ya Amata kutupwa nje alifyatua kiti chake lakini alichelewa nukta kadhaa, wakati kile kiti kikimrusha nje lile kombora likawa tayari limeshaipiga ile ndege eneo la kati kati, akajikuta ananasa kwenye vyuma vya ndege hiyo. Akajitahidi na kujifyatua lakini parachute lake liliharibika vibaya, akajitahidi kuliongoza ili adondokee nchi kavu akafanikiwa. Kutokana na kuchanika kwa parachute hilo alifika chini kama mzigo na kujipiga vibaya akatulia kimya kwa sekunde kadhaa, macho yake yakiwa bado yanatazama anga la dhahabu jioni hiyo na taratibu akaanza kuhisi giza huku sauti za ndege zikipote kwa mbali, akazirai.

Amata akiwa hana fahamu alidondokea baharini na kupigwa pigwa na mawimbi mpaka kando kidogo. Jua la jioni lilikuwa tayari linang’aza sehemu hiyo na misafara ya ndege nayo ilikuwa ikirudi viotani.

* * *

Huku chini kwenye gari, kioo cha kompyuta ya Chiba kikawa cheusi ghafla, hakuna chochote kilichoonekana.

“Vipi tena?” akajiuliza.

“Vipi kwani?” Gina akauliza.

“Nahisi hatari, maana sauti ya mwisho nilioisikia ni ya Scoba akimwita Amata, hebu weka gari pembeni kwanza,” Chiba akamwambia Gina. Naye akafanya hivyo, ile gari ikasimama kando mwa barabara katika eneo la Zinga. Chiba akajaribu kucheza na kompyuta yake lakini hakuna alichoweza kuona zaidi ya ujumbe wa ‘Error 706’ uliokuwa ukijitokeza mara kwa mara, akaifunga ile kompyuta na kumgeukia Gina.

“Vipi?” Gina akauliza, lakini kutoka katika macho ya Chiba aliweza kuuona mshangao uliokosa mwelekeo.

“Huko hali si shwari, siwapati Amata na Scoba,” Chiba akajibu huku akijiweka sawa kitini na kuinua simu ndogo iliyofungwa ndani ya gari hiyo.

“Unataka kuniambia nini?” Gina akauliza huku mikono yake iliyokuwa imeshika usukani sasa ilianza kutetemeka na alionekana kubana meno yake ama akizuia kilio au akinyima uchungu nafasi ya kujiweka hadharani.

“Mawili, ama ndege ina hitilafu au wamedondoka,” Chiba akajibu na wakati huo tayari simu iko sikioni akimwitikia Madam S.

“Nakusoma Chiba!” Madam S akaitikia

“Kuna hali isiyoeleweka, Simpati ndege angani, mawasiliano yamekatika,” Chiba akamwambia.

“Unataka kusema nini?”

“Sauti ya mwisho niliyoisikia inaashiria hatari, Scoba alimwita Amata kwa nguvu kisha nikasikia kishindo na ukimya kwa asilimia 101,” akaeleza.

Kupitia simu hiyo ya upepo, Chiba aliweza kumsikia Madam S akishusha pumzi kwanguvu.

“So?” Madam S akarudi hewani mara hii sauti yake haikuwa kama kwanza, ilikuwa imejaa kitetemeshi.

“Probably, men down!!” Chiba akamaliza hhuku macho yake yakitona machozi.

Akatulia kumsikiliza bosi wake akimpa maelekezo kadhaa kisha huku akiitikia tu kwa kuguna pasi na kusema neno lolote.

“Clear and out!” akaitikia na kukata simu kisha akaipachka mahala pake na kumtazama Gina.

“Madam anasemaje?”

“Anasema tuwahi na Dkt. Jasmine anakuja na vitendea kazi vya kutosha kwa msaada wa haraka. Gina akaingiza gari barabarani na kutimua mbio kama kichaa, akageuza na kurudi nyuma kidogo kisha akaikamata Mapinga aliiacha barabara ya kwenda Dar es salaam na kupinda kushoto kuchukua nyingine kuelekea Mbegani

“Shiiit!” Gina aliendelea kugugumia huku akikanyaga mafuta kama kichaa, mshale wa mwendo kasi ulikuwa katika namba 110 na vumbi lililoachwa nyuma halikuwa la kawaida. Baada ya mwendo wa takribani dakika arobaini na tano, Gina alisimamisha gari karibu na kijiji fulani, Chiba akajitokeza juu ya gari na darubini yake na kuangalia kwa darubini katika uwanda wa nyasi fupifupi. Darubini hii ilikuwa ni ya kisasa sana, yenye madini yanayiwezesha kuona hata katikati ya giza, na kupambanua kila inachokiona na kukupa maelekezo kuwa kitu hicho kipo kilomita ngapi. Baada ya dakika kadhaa akaingia ndani, na kuchukua kifaa kingine kama simu lakini kilikuwa kikubwa zaidi, akakiwasha na kubonya vitu fulani fulani kisha akaanza kuangalia, rangi na michoro mbalimbali inayotokea katika kile kioo, baada ya sekunde kadhaa kukawa na kijitaa kinachowaka eneo Fulani la kioo cha kile kidubwasha.
 
Silimulizi : Msako Wa Mwanaharamu

Sehemu Ya Pili (2)

“Gina, twende mbele zaidi,” akamwambia Gina, na ile gari ikaondolewa mahala pale mpaka kwenye njia panda ya kuwenda kwenye magofu ya Kaole na ile ya kwenda Bagamoyo mjini.

“Subiri!” Chiba alimwambia, kisha akamwambia aelekee kulia. Gina moja kwa moja akachukua barabara hiyo na kupita magofu ya Kaole akaendelea mbele mpaka alikokuta njia inaishia na kukutana na mkondo wa maji uliokatisha eneo hilo.

“Tunafanyaje?” akauliza.

“Tuache gari hapa, twende kwa miguu tufuate hii signal inawezekana ni Amata au Scoba, ila mmoja kati yao signal yake imepotea kabisa sijui tutampataje,” Chiba alijibu huku akiwa tayari kakanyaga ardhi ya eneo hilo akichukua hiki na kile ndani ya begi lake kabla hajaliweka mgongoni. Wakiwa bado wanaendele kutafuta hapa na pale katika vichaka hivyo, saa moja baadaye ndipo Jasmine alipoungana nao na kuweka nguvu pamoja jioni hiyo kufanya mtafuto huo mgumu.

Rejea sasa…

KURASINI

MARA BAADA YA KUMALIZA SHUGHULI za Shamba, Madam S alirudi katika afisi ile ya siri iliyotengenezwa ndani ya meli mbovu katika bahari ya Kurasini, wapiga mbizi waliotumwa kuutafuta mwili wa Amata walirejea na boti yao ‘KINYAMKERA’. Inspekta Simbeye na Madam S walikuwa wakisubiri kwa hamu huku wakiwa hawana mazungumzo mengi. Taarifa hiyo haikutangazwa na mtu yoyote wala hakuna chombo cha habari kilichothubutu kuvunja amri hiyo ya usalama wa taifa.

“Hatujapata mwili wa mtu yeyote kule majini!” kijana mmoja kati ya wale watatu waliokwenda kuchunguza yale mabaki ya ndege, ikiwezekana na kuupata mwili wa Amata walifikisha taarifa hiyo kwa Inspekta Simbeye na Madam S waliyekuwa ndani ya lile meli bovu.

“Isipokuwa tumepata hiki kiboksi cha kurekodi mwenendo wa ndege, taarifa ambazo tumezipata kutoka humu ni kuwa ndege hii ilipoteza mawasiliano angani kwa ghafla kwa kitu kama mlipuko. Baada ya uchunguzi kule chini ya maji, tumegundua kuwa ile ndege imedunguliwa, na kombora lililotumika ni RPG Rocket kwa kuwa tumefanikiwa kuona mabaki yake,” kijana mwingine akaelelzea kwa ufasha zaidi na kuwasilisha vyuma vya kombora hilo.

“RPG Rocket?” Madam S akadakia kwa kuuliza.“Unataka kunambia kuwa ndani ya nchi hii kuna watu wanamiliki silaha nzito za kivita kama jeshi, hii ni hatari, ni hatari sana,” Madam S alizungumza huku akionekana wazi kukosa utulivu wa mwili na roho kwa swala hilo.

Oh! Shit, atakuwa wapi Amata? Madam akajiuliza pasi na kupata jibu sahihi ndani mwake.

“Sawa naomba hiyo taarifa yote katika nakala laini tafadhali,” Madam S aliomba huku akilielekea dirisha dogo na kutazama nje kwa nukta kadhaa kabla ya kugutuliwa na sauti ya kijana yule akiwa tayari na taarifa ile mkononi mwake ikiwa ndani ya CD. Akaipokea na kuondoka katika ofisi ile ya ajabu.

Baada ya kujiridhisha na kila kitu, akaagana na Simbeye na kutolewa katika ile afisi mpaka eneo maalumu la nchi kavu upande wa Kigamboni, kutoka hapo akatembea hatua chache na kuchukua gari yake aliyoiacha kwenye afisi moja ya chama na kuelekea tena Shamba.

* * *

Madam s aliwasili katika jumba hilo kwa njia anayoijua mwenyewe, shughuli za ndani humo zilikuwa zikiendelea kama kawaida. Ni Chiba tu aliyekuwa anajua ujio huo kwani kila anayeingia ndani ya jumba hili huweza kumwona kupitia kamera ndogo za usalama ambazo si rahisi kugundulika na mtu wa kawaida. Ndani ya sebule kubwa alipomwacha Scoba alimkuta palepale akifunua funua gazeti na kusoma hapa na pale.

“Kweli, tulifanya kosa kuwakabidhi wale askari lindo la mtu hatari kama yule, lakini tungefanyaje wakati hao ndiyo wenye jukumu la kulinda wahalifu?” Madam S akauliza huku akitembea na kujitupia kochini. Sauti hiyo ilimgutua Scoba, kwa sababu hakusikia hata kelele ya wayo wa mwanamama huyo.

“Yeah, ni sahihi sana kwa hilo lakini yule mtu uhatari wake ni wa kimataifa zaidi, tazama jinsi walivyo muokoa hao majahiri wake, ile ni mbinu ya kivita Madam,” Scoba aliongea.

“Kiukweli walidhamiria, maana hata kumkamata kwake yule bwana hakukuwa rahisi, tulipata tabu sana pale Bombay, lakini tulimleta. Halafu kumuona anatutoka mikononi kirahisi namna ile, lo, nina uhakika Amata huko aliko si ajabu bado anamsaka, na akimpata hawezi kumleta na roho yake,” Scoba akazungumza.

Ukimya ukatawala kati ya hao watu wawili, kila mmoja akiwaza lake. Scoba akarudisha mawazo yake kwenye mtanange wa Bombay.

Miezi mitatu nyuma

SAFARI YA BOMBAY – INDIA

“Una uhakika utamleta?” Madam S akamwuliza Amata.

“Tumeanza kudharauliana siyo?” Amata akajibu swali kwa swali.

“Siyo kudharauliana, maana wewe nakujua, mi nikikwambia umlete hai we utaleta viatu vyake tu nikiwa na maana utakuwa ushanyofoa roho yake,”

“Inategemeana, daima nikiona mtu mbishi kufika mzima lazima nimgawanye mara mbili, yaani nimtenganishe mwili na roho na hapo ndipo nambeba kirahisi,” wote wakacheka kwa maneno hayo.

“Sawa, serikali iko tayari kukupa msaada wowote utakaouhitaji, maana waziri mkuu kaagiza mtu huyo aletwe hapa,” Madam akamwambia Amata kwa msisitizo.

“Tawile, zimefika na ataletwa,” kisha akapiga saluti na kugeuka kulitazama jengo la Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

“Kamanda Amata, Pancho Panchilio ana mtandao mkubwa sana ndani na nje ya nchi, uwe makini, timu ya utafiti ipo huko siku nne zilizopita na wameshafanya kazi kubwa sana wanakusubiri wewe ukamalizie,” Madam S aliendelea kutoa rai yake kwa kijana huyo shupavu.

“See you soon!” (Tutaonana punde tu) akamuaga Madam na kuondoka zake.

* * *

“Wapi tena? Maana mwenzetu huishiwi safari weye,” Mhudumu wa ukaguzi wa Swissport akamtania kwa kuwa alikuwa akimfahamu hasa kwa kumwona mara nyingi uwanjani hapo.

“Umeanza Lulu, naenda Uhindini mara moja,”

“Uje na zawadi tu,”

“Usijali, kacholi zenye pilipili utapata,” Kamanda akajibu na kuishia kwenye chumba cha kupumzikia wasafiri. Baada ya nusu saa kupita aliondoka na ndege ya Shirika la Air India.

UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA

CHHATRAPATI SHIVAJI – BOMBAY

KAMANDA AMATA aliingia katika jiji hilo usiku wa manane, moja kwa moja alitoka nje ya jengo hilo. Kando tu ya maegesho ya uwanja huo, aliweka begi lake chini, akaingiza mkono mfukoni na kutoa sigara akaibana kwa midomo yake miwili huku kichungi cha sigara hiyo kikiwa ndani ya kinywa chake. Mkono mwingine ukatoa kiberiti cha gesi na kukiwasha. Mara baada ya kuiwasha akavuta kavuta pafu mbili kisha akaizima na kuisigina na kiatu chake.

Mbele yake akapita mzee mmoja na kujikoholesha, umbali wa sentimeta kama mia hivi akaonesha ishara ya mkono ya kumtaka Amata amfuate. Kamanda Amata akaona ishara ile na kumfuata mpaka kwenye gari moja ya kizamani, Ford Anglia.

“Mr. Spark!” akaita kwa sauti yake nzito.

“Mavalanka,” Kamanda naye akajibu. Yule mzee akachukua lile begi na kulitupia ndani, kisha akaingia mlango wa dereva na kumwacha Amata akiufungua ule wa abiria.

“Karibu sana Bombay. Ni mara yako ya kwanza kufika?”

“Ndiyo, sijawahi kuja Bombay wala India kwa ujumla,”

“Ha! ha! ha! ha! Hakika utafurahia maisha katika kila nukta ambayo utapata nafasi ya mapumziko, wasichana wazuri wenye maumbo ya kuvutia watakuburudisha sana kwenye maklabu ya usiku na kadhalika, ila uwe mwanagalifu wengine wanakuwa kazini,” Yule mzee alimwambia Amata.

“Mi najua hii nchi ya kidini bwana, inakuwaje kuna klabu za usiku?”

“Akh! Klabu za usiku zipo duniani kote…”

“Ila sina tabia hiyo,” kamanda akajibu kwa mkato.

“Ah weeeeeeee! Nakujua vyema kijana. Ok, tuyaache hayo, Hoteli ya Grand Hyatt inakufaa sana,” alimwambia huku akikunja kona na kuingia katika lango kuu la hoteli hiyo na kuegesha gari yake.

“Unaona?” akauliza.

“Nini?”

“Hoteli kubwa nzuri ya kisasa ina bwawa la kuogelea kule juu na casino nzuri kabisa,” Yule mzee akamwambia huku akimsaidia kushusha lile begi.

“Asante sana, tutaonana tena,” Kamanda akamuaga huku akivuta hatua kuelkea ile hoteli lakini kabla hajafika lango kuu la kuingilia mapokezi akapokelewa na vijana waliondaliwa kwa kazi hiyo kwa kila msafiri anayekuja.

Akafanya itifaki zote za mapokezi na kuingia katika chumba chake. Mara baada ya kuufunga mlango alikitazama chumba hicho kikubwa jinsi kilivyo na kilivyopangwa samani zake kwa mtindo wa kuvutia. Akainua saa yake ya mkono na kuifyatua upande wa juu, lile eneo lenye mishale ya saa likafunuka kama kifuniko na kuacha sehemu ya chini ikiwa na kitu fulani chenye uwezo wa kutambua aina yoyote ya mlipuko na kuonesha kama kuna mitambo ya kunasa sauti lakini akakuta kuna usalama wa kutosha. Akairudisha saa yake kisha akaliendea dirisha kubwa na kusogeza pazia pembeni. Majengo marefu kwa mafupi yalimkaribisha, taa za kupendeza za barabarani na majumba ya starehe zilionekana wazi zinavyopishana angani.

“Bombay!” akasema kwa suti ndogo.

Akiwa bado dirishani hapo akagutushwa na hodi iliyobishwa mlangoni, akauendea taratibu na kuufungua kwa hadhari kubwa. Sura ya mwanadada mrembo wa Kihindi ilimpokea kwa tabasamu lenye bashasha lililojaa na kuufanya uso wa mwanadada huyo kuwa wa mviringo, vishimo vilivyojitokeza katika mashavu yake vikawa kama vidimbwi vya maji katika jangwa.

“Samahani kuna mzigo wako hapa, tulisahau kukupatia pale kaunta,” yule msichana aliyekadiriwa kuwa na miaka ishirini hivi alimwambia Amata kwa sauti tamu iliyozitikisa kwa upole ngoma za masikio yake. Akainua mkono na kuipokea bahasha iliyokuwa mkononi mwa dada huyu huku akiking’ang’ania kiganja cha mkono huo.

“Mmm asante, unaitwa nani?” Kamanda akaanza ubembe wake.

Yule binti hakujibu kwanza, akamtazama Amata juu mpaka chini, akameza mate.

“Sukaina!” akajibu.

“Oh! Sukaina, jina zuri sana, asante kwa mzigo au kuna lingiine?”

“Hapana!” akajibu na kuanza kuondoka.

“Sukaina!” Kamanda akaita na yule binti akageuka.

“Napenda kuonana nawe ukimaliza kazi leo,”

“Mmmmm! Bwana wangu anakuja kunichukua, kwaheri,” akajibu na kuondoka zake.

Kamanda Amata akabaki katumbua macho akimwangalia yule mrembo akipotelea kwenye lifti huku vazi lake zuri lenye kumetameta likimfanya kuonekana mrembo zaidi. Macho yaliposhiba akarudi ndani na kuifungua ile bahasha.

Bastola moja ndogo ililala ndani yake ‘Beretta 92FS 99mm’, Kamanda Amata akaichukua na kuigeuzageuza, bado ilionekana mpya na haijatumika kabisa. Pembeni yake kulikuwa na kasha iliyojaa risasi, akaichukua na kuichana kisha akazijaza katika ile bastola na kuipima kidogo kama inafiti mkononi mwake. Bastola kama hii aliitumia zamani kidogo hivyo alishaanza kuipoteza ufanisi wake, kifaa chake cha kuzuia sauti nacho kilikuwa pamoja nayo. Akavuta memo ndogo na kuisoma.

‘Mgahawa wa Dinasty saa 2:15 asubuhi, meza namba 5’

Alipomaliza kuisoma akainkunja na kuitia kwenye begi lake kisha akaliendea bafu. Baada ya kuoga na kujiweka vizuri aliutafuta usingizi usiku huo na kuupata kwa tabu.

MGAHAWA WA DINASTY – saa 2:10 asubuhi

Akiwa ndani ya suti safi Amata aliteremka katika taksi na kuingia ndani ya mgahawa ule, mlangoni alipokelewa na mwanadada wa Kihindi aliyevalia vazi la kitamaduni, akamkaribisha na kumwonesha ukumbi wenye ukubwa wa wastani ambao ndani yake kulikuwa na watu walioketi wakipata ama kahawa au chai kila mmoja na kile alichopenda. Harufu ya vyakula na marashi ya Kihindu viliikinaisha pua ya Amata kwa sekunde chache, moja kwa moja akaiendea meza namba tano ambayo haikuwa na mtu yeyote aliyeketi hapo.

Pembeni mwa meza hiyo dirisha kubwa la kioo liliruhusu mtu yeyote kuona mandhari safi ya jiji la Bombay, na pia ungeweza kuwaona kwa uzuri watu waliokuwa wakipita huku na kule kwa shughuli mbalimbali. Katika usawa kabisa wa meza ile lakini upande wa nje kulikuwa na barabara kubwa iliyokuja kuungana na hiyo iliyo hapo. Amata aliitazama ile barabara iliyokwenda asikokujua.

N Ave Road! Amata alisoma kibao kikubwa cha rangi ya kijani kilichoonekana kupitia dirisha hilo kikiitambulisha barabara hiyo iliyonyooka kiasi kwamba mtazamaji aliweza kuona mpaka mwisho wake kama sio mbovu wa macho. Akiwa katika kushangaa huko akahisi kama mtu anaketi katika kiti cha mbele yake, akageuka taratibu na kugongana macho na Chiba aliyekuwa kajigeuza kidogo sura yake kwa kujiweka vichunusi vya hapa na pale na uvimbe wa bandia katika paji lake la uso.

“Karibu Bombay!” aliongea kwa sauti iliyoonesha kuwa na kikohozi kikali kwani mara kwa mara alikuwa akikohoa.

“Nimeshakaribia komredi,” akajibu na kujiweka sawa huku kifungua kinywa kikiteremshwa mezani taratibu na mhudumu aliyeijua kazi yake, wakasitisha mazungumzo yao kusubiri zoezi hilo lifanyike.

“Hapa kazi iliyopo ni ndogo tu lakini ni ngumu,” akaongea huku akiangalia huku na huko.

“Mbona unaongea kama una wasiwasi na jambo?”

“Lazima kuwa na wasiwasi kwani jamaa wamenishuku tangu juzi wakati nafuatilia nyendo za mwanaharamu, lakini niliwatoka hawakunipata tena”.

“Ningeshangaa!” Amata akaongezea.

“Sasa Kamanda, mpango upo hivi, Pancho Panchilio ana makazi yake ndani ya Hekalu Hanuman. Hili ni hekalu la Kihindu. Geuka kulia, tazama hiyo barabara,”

“N Ave Road,” akasoma tena yale maandishi kwenye lila bango.

“Barabara hii moja kwa moja mbele inakutana na barabara ya SB Patil na kufanya njia panda,”

“Enhe!”

“Hapo sasa ndipo penye hilo hekalu, nimemwona kwa macho yangu japo ilikuwa kazi ngumu sana, sijui tutamchukuaje,” Chiba alimweleza Amata aliyekuwa kanyamaza kimya akisikiliza huku akili yake ikizunguka kwa kasi ya ajabu.

“Kuna ulinzi mkali au vipi?” akauliza.

“Kuna kamera sabini na nne nje, na ndani zisizopungua thelethini, pale wanaingia Wahindu tu, mtu mweusi huna nafasi, kuna walinzi pande zote ndani na nje wenye vifaa vinavyoweza kumtambua yeyote mwenye nia mbaya na eneo hilo. Isitoshe ni eneo la hekalu ambalo hata viongozi wengi hupenda kuabudia hapo,” Chiba aliuliza.

“Nakusikiliza,” Kamanda alimwambia.

“Inabidi tumchukue akiwa hai,”

“Na tukimchukua tunampeleka wapi?”

“Bahrain House, pembezoni mwa Bombay karibu na bahari, jengo hilo halitumiki, limetelekezwa, tutafanya shughuli yetu humo na kuondoka naye.”

“Safi sana Chiba, nitahitaji kutembelea hekalu hilo ili nilione kwa ukaribu,” Kamanda akasema.

“Haina haja,” akaingiza mkono mfukoni na kuchomoa kipande cha karatasi, akakikunjua na kukiweka mezani.

“Hii hapa ni ramani ya jengo hilo,” akamwonesha.

Wakatazama pamoja, Chiba akamwonesha Amata kila kona yenye kamera na ulinzi wa binadamu, walipojiridhisha, akairudisha mfukoni ramani ile.

“Sawa Chiba, nimeona, lakini bado mi na wewe hatujui hasa huyu mtu anaishi kona gani pale au anakuja na kutoka,” Kamanda akazungumza..

“Aaaa aisee halafu kweli, hapo sikutumia umakini,” akakiri.

“Usiwe na shaka, huyu mtu atakamatika tu hata awe na mizizi mingi kama mnazi, atang’oka tu,” Kamanda alisema.

“Nakuamini kamanda, Madam S atakuwa hapa muda si mrefu,” Chiba akazungumza.

“Safi, sasa fanya hivi kama inawezekana Madam aombe usafiri binafsi, aje na ndege ili tukimtia mkononi huyu jamaa tuondoke naye kiurahisi, kumbuka kwenye ndege ya abiria akileta vurugu ni hatari kwa mamia ya watu,” Kamanda alimpa maagizo Chiba.

* * *

Kama kawaida ya Jiji la Bombay, watu walikuwa wengi barabarani, pikipiki za magurudumu matatu, usiseme, zilikuwa zikisafirisha watu huku na kule. Kwa ujumla kulikuwa na magari machache sana lakini pikipiki zilitawala kila kona. Kamanda Amata alikuwa ndani ya moja ya ‘Bajaj’ hizo akielekea upande mwingine wa jiji.

“Mwenyeji wetu hapa ni Sha Kapur, yeye ni mwanausalama mstahafu, anajua mengi na Madam S alinishauri kukutana naye,” Chiba aliendelea kuongea huku akiwa katika bajaj nyingine tofauti na ile aliyopanda Amata. Lakini kwa kutumia kifaa kidogo kabisa cha mawasiliano aliweza kusikilizana vyema na swahiba wake huyo,

“Lazima tumuone, lakini kwanza ngoja nilione hilo hekalu hata kwa nje,” Amata akajibu.

“Yote heri,”

Kamanda Amata aliteremka na kumlipa yule dereva, alipoinua uso wake mbele akaona lile hekalu kubwa linalopendeza kwa macho. Hekalu la Hanuman.

Ilikuwa mchana wa saa saba watu wakipishana kuingia na kutoka ndani ya hekalu lile huku ibada zikisikika kwenye vipaza sauti, watu waliopendeza kwa mavazi mbalimbali ya tamaduni za Kihindi walikuwa eneo hilo akina mama kwa akina baba, watoto kwa vijana. Umbali kama wa mita ishirini kutoka katika lango kuu la hekalu hilo kulikuwa na kundi la watu waliokuwa wakinunua vitu fulani ambavyo hakuvijua vizuri ni vitu gani. Akavuta hatua mpaka eneo lile. Amata alikuwa tofauti kwa mavazi, hakuna aliyevaa suti eneo lile, kila jicho lilimtazama yeye.

Karimati, kachori na vyakula mbalimbali vya Kihindi vilikuwa hapo, Kamanda Amata akasogelea mahala pale na kuinama kutazama kwa ndani kumuona muuzaji.

“Svagata,” (Karibu) sauti nyororo ya kike ikapenya masikioni mwa Amata.

“Dhan’yavada,” (Asante sana) akajibu kawa lugha hiyo ya Kihindi na kumtazama mwanadada huyo, macho yao yalipogongana kila mmoja akabaki kakodoa. Amata hakuamini anayemwona na wala mwanadada huyo hakuamini aliye mbele yake.

“Amata!” akabaki kama aliyepigwa shoti ya umeme.

“Hapa si salama, njoo huku, nifuate,” Yule msichana akaondoka na kumwachia kijana wake aendelee na kazi hiyo.

* * *

Chiba alitikisa kichwa na kumtazama Amata akiondoka na Yule mwanamke.

“Hili ndilo tatizo la huyu jamaa, keshanasa,” Chiba alinung’unika. Akajitoa pale aliposimama na kusogea upande wa pili ili amwone vizuri Kamanda anaelekea wapi, akasimama mahali penye kiduka, akaagiza kinywaji na kuendelea kumtazama swahiba wake akipotelea ndani ya nyumba mojawapo katika eneo hilo, hatua kama mia mbili kutoka katika lile hekalu. Naye taratibu akaachana na kinywaji chake na kuendelea kutembea huku akipiga mruzi kuelekea eneo lile, alipofika hakuwaona kabisa isipokuwa lango lililofungwa na kubaki bila mlinzi. Akatazama huku na huku hakuna mtu; akavuka na kuliendea lile lango, alipolisukuma, likasukumika; akajipenyeza ndani taratibu na kusimama wima huku lile lango likijifunga nyuma yake.

Ukimya wa eneo lile ulimtia wasiwasi Chiba, akapepesa macho yake huku na kule hakuona mtu wala kiumbe hai chochote chenye uwezo wa kujongea. Mimea mirefu ilikuwa ikiyumbayumba kwa upepo wa taratibu. Kati ya mimea mingi iliyoshikana na kushonana kulionekana nyumba moja ndogo iliyonakshiwa kwa nakshi za kiajemi.

Hapa hakuna usalama! akawaza na kuichomoa bastola yake kutoka mafichoni na kuiweka kiganjani tayari kwa lolote. Mwendo wake wa minyato ulifanya aonekane kama mvamizi wa eneo hilo.

* * *

“Amata! Nini kimekuleta India?”

“Sikutegemea kabisa kukuona SaSha,”

“Hapa ni nyumbani vyovyote ujavyo tegemea kuniona,” SaSha alimwambia Amata huku akiwa amekumbatiwa na kuegemea ukuta, nyuso zao zikitazamana na pumzi kupishana kwa kasi. Taratibu vinywa vya wawili hawa vikaanza kukaribiana huku mihemo ikiongezeka.

Mlio wa kengele ulimshtua SaSha na kumsukuma Amata pembeni, akasogea dirishani na kuvuta pazia taratibu; kutoka ndani aliweza kumwona Chiba. Lakini Chiba hakuweza kumwona SaSha kutokana na dirisha lile kufichwa na mimea iliyotambaa kwa nje.

SaSha akachomoa bastola na kuiweka tayari akiulelekea mlango. Kamanda Amata taratibu akavuta pazia kutazama kilicho nje.

“SaSha!” akaita kwa sauti ndogo. SaSha akageuka kumtazama akampa ishara ya kurudi.

“Kijana wangu huyo, ananilinda, anaitwa Chiba”. SaSha akarudisha bastola yake na kufungua mlango huku akinyosha mikono yake juu kuonesha ishara ya amani.

“Karibu Chiba, tafadhali hapa ni mahala salama,” SaSha akamwambia Chiba na wakati huo Chiba akashusha bastola yake na kuiweka katika kikoba chake.

“Karibu ndani,” akamwambia huku akiingia ndani ya ile nyumba. SaSha akaweka vinywaji mezani na wote wakaendelea kunywa taratibu huku wakibadilishana mawazo.

“Amata, kuna nini Bombay? Maana wewe huwezi kuja sehemu kama hii kwa likizo,” SaSha akauliza tena.

“Nimemfuata mwanaharamu,”

“Nani na yuko wapi?”

“Mwanamke! Hutakiwi kumjua we endelea na kazi yako hili halikuhusu, nimeshakujibu,” Amata akajibu kwa ukali kidogo. Akamgeukia Chiba na kumtambulisha.

“Anaitwa Sasha, ni agent wa shirika la kijasusi la CBI hapa India, alikuwa Tanzania miaka kadhaa nyuma katika sakata lileee la yule gaidi, kama unakumbuka,”

“Nakumbuka, sakata la Jegan Grashan?” Chiba akauliza.

“Ndiyo,” akajibiwa na kisha ukimya ukatawala. Kamanda Amata akanyanyuka na kuliendea dirisha la upande wa nyuma akatazama na kuona shughuli mbalimbali zikiendelea, hakuweza kujua kama ni za uvuvi au ni kitu gani, akampa ishara Chiba asogee pale dirishani. Nukta chache, Chiba alikuwa pamoja na Amata huku mkono akiwa na darubini ndogo lakini yenye nguvu kubwa, inayoweza kupima na kukuandikia umbali wa hicho kitu kilipo kutoka uliposimama wewe. Amata akiweka machoni na kutazama, kwa mbali kulikuwa na boti iliyoonekana ikija upande huo.

“Tazama hiyo boti,” akamwambia Chiba huku akimpa ile darubini na yeye akaiweka machoni na kutazama.

“Amata!” akaita baada ya kutazama kwa sekunde kadhaa.

Ile boti ilifika karibu na pwani lakini ilishindwa kusogea kutokana na kupwa kwa maji, watu kama nane walisogea kule baharini na kumbeba mtu mmoja kwenye kiti maalumu kama mfalme wa kikoloni. Huku watu wengine wakirusha maua na kuonekana kama wanampa heshima mtu huyo.

“Shiit!” Chiba aling’aka na kumpa ile darubini Amata.

“Vipi?”

“Pancho Panchilio,” akajibu Chiba, “laiti ingekuwa tummalize, basi hapa ndipo tungeiushangaza Dunia,” akaongeza.

“Bibi yako anataka amnase kofi kabla hajafungwa,” Amata akasema na wote wakacheka. SaSha akafika hapo dirishani na kumnyang’anya darubini Amata kisha akaanza kuangalia yeye.

“Waoh! Chief anarudi,” SaSha akajisemea kwa sauti huku akirudisha darubini kwa Amata.

“Ni nani Yule?” Chiba akahoji baada ya kugundua kuwa mwanamke huyo anamjua Pancho kama Chfu.

“Yule ni Chief wa ukoo fulani ambao unamiliki hilo hekalu hapo, ni mtu mwema sana kiasi kwamba watu wa ukoo wake umtukuza kama mfalme,” SaSha akawaeleza Chiba na Amata wakati huo Chiba alikuwa akinasa mazungumzo yale kwa kutumia pete aliyokuwa ameivaa kidoleni mwake.

“Kwa hiyo anakuja kuwasalimu watu wake?” Kamanda akauliza lakini swali lake lilikuwani la kutaka tu uhakika wa jambo ambalo Chiba hakulichunguza sawasawa.

“No! hapo ndipo anapoishi,” SaSha akajibu huku akimtazama Amata.

“Nitakwenda kumsalimu au vipi Chiba?” Amata akapendekeza.

“Oh! No! hamuwezi kumuona, huwa haonekani kwa urahisi hivyo hususan kwa ninyi watu weusi. Watu wake humuona kwa nadra sana, kupata muda wa kuzungumza naye labda ni dakika tano tu na ni mara moja kwa mwezi,” SaSha akaendelea kueleza.

“Anaitwa nani?” Chiba akauliza.

“Premji Kanoon,” SaSha akajibu; Chiba na Amata wakatazamana na kubaniana macho. Amata akarudisha darubini machoni na kutazama ule msafara. Wale vijana waliombeba waliendele kutembea na kuiacha pwani kisha wakaingia kwenye ngome kubwa ambayo ndani yake ndiko kuna hilo hekalu. Walipopotelea ndani yake, akashusha ile darubini na kumrudishia Chiba ambaye aliificha ndani ya koti lake. Amata akamwangalia SaSha.

“Anaishi wapi?” akauliza.

“Humo humo ndani, chini ya hilo hekalu kuna kasri kubwa sana ambalo ndilo anloishi siku zote. Kesho ni sikukuu ya Diware, watu wengi kuliko hapo unapoona watakuja, nafikiri utaweza kumwona vizuri kwani baada ya ibada kuna sherehe kubwa kwenye uwanja huko nyuma zinazoambatana na michezo mbalimbali,” SaSha akaeleza.

“Ok, natamani kuhudhuria,”

“Bila shaka, jioni ni kwa kila mtu,” SaSha akamaliza kuongea na kuwapa vinywaji wawili hao.

* * *

Premji Kanoon aliteremshwa kutoka katika kile kiti akakanyaga chini kwa miguu yake na moja kwa moja akaingia kwenye kijimlango kidogo na kujifungia. Akateremshwa chini ya ardhi ambako kulikuwa na kasri lake lisilo na bugudha. Alipofika tu akapewa huduma zote zilizomstahili ikiwa pamoja na kukandwakandwa mabegani, kuoshwa miguu kupakwa mafuta ya kunukia katika nyayo zake na mambo mengine mengi. Chumba chote kilinukia udi, aliinuka na kusogea karibu na sanamu moja lenye ukubwa wa wastani, akainamisha kichwa chake huku akiwa kabana viganja vya mikono yake kifuani kwa uchaji wa hali ya juu. Sekunde kadhaa akamaliza na kutoka eneo hilo huku akimwagiwa maua mazuri ya kunukia naye akakanyaga juu yake.

Hatua chache akalifikia sanamu lingine, akasimama mbele yake na lile sanamu likasogea pembeni taratibu, akapita na likarudi mahala pake. Kilikuwa chumba kidogo chenye giza, kikamteremsha chini zaidi na huko akaingia kwenye ukumbi wa wastani uliokuwa uking’azwa kwa taa zinazobadilisha rangi. Akaketi kwenye kiti kimoja kikubwa kilichokuwa nyuma ya meza yenye nakshi za kupendeza. Mbele yake kulikuwa na watu wanne, vijana wakakamavu wenye miili ya wastani, vichwani mwao walivaa vilemba ambavyo viliwatambulisha kuwa wao ni Singasinga.

Akajikohoza kidogo na wale vijana waliendelea kusimama pale wakiwa kimya kabisa. Pancho Panchilio au wao wanamwita Premji Kanoon.

“Sina lingine, nataka auawe au wauawe,” akasema.

Wale jamaa wakaitikia kwa vichwa tu, hawakuongea lolote; pembeni yao kukatokea picha kubwa ya Amata.

“Mnamwona huyu?” akawauliza, wote wakageuka na kuitikia kwa vichwa.

“Mna uhakika ndiye mliyemwona uwanja wa ndege?”

Wakajibu tena kwa kutikisa vichwa.

“Vizuri, sasa nataka auawe mara moja yeye na yule wa mwanzo, watu wa jamii kama hii hawafai kuishi kwa sababu huaribu mipango ya watu. Sikilizeni, huyu mnayemwona kwenye picha ni mtu hatari sana, mnapokwenda kumshambulia hakikisheni mmejipanga vizuri, mnanielewa?” akawauliza.

“Ndiyo, tunakuhakikishia jua la kesho hawezi kuliona kamwe!” mmoja aliyesimama mbele ya wenzake akajibu kwa ushupavu. Zile taa zikazimika na Pancho akapotea kwenye milango yake ya siri.

MKESHA WA DIWALI

“Kamanda Amata!” SaSha akaita kwa sauti ya chini.

“Niambie mtoto mzuri,” Amata akajibu.

“Unalala hapa siyo?”

“No! natoka sasa maana usiku huu tuna kazi ya kufanya. Kesho uje pale Grand Hyatt Hoteli, utanikuta,” kamanda akamwelekeza.

“Mmmmm! Nikikufumania maana wewe huwezi kulala bila mwanamke,”

“Acha uongo,” akamjibu huku akijinasua kutoka katika mikono ya SaSha iliyokuwa imembana pale kitandani, akaingia bafuni na kujiweka sawa, alipojitumbukiza ndani ya suti yake na kutokomea nje ya jengo lile.

“Swiiiiiiiiiih!” sauti ya mruzi ilimshtua Amata akasimama na ghafla gari moja ikatokea mbele yake na kusimama.

“Twenzetu kumekucha!” Ilikuwa sauti ya Chiba, akajipakia garini na wakaondoka kwa kasi.

“Kamanda tuko matatani, jamaa wamejipanga wanajua kama upo hapa, nilichofurahia ni kuwa wanakuzungumzia wewe na hawajui kama mimi niko hapa,” Chiba akaeleza huku akiongeza kasi ya gari yake kumbe hakuwa akijua kuwa wenzake walishammaizi muda mrefu.

“Asee, watakuwa wamejuaje kama niko hapa?”

“Ah hapo ni sehemu mbili tu ama uwanja wa ndege au hotelini, watu kama hawa huwa na macho mengi na masikio kila mahali,” Chiba akaongea harakaharaka.

“Sasa Chiba na sisi tugeuze kibao, kazi yetu tuifanye leo hii hii usiku tukichelewa kitanuka, maana wanaweza kusali wale tukageuka panya kwenye nchi ya watu,” Kamanda akaongea huku akijiweka vizuri kitini,

“Twende hotelini, nikachukue begi langu niliweke humu garini maana kuanzia sasa kambi popote”.

Chiba akakunja kona kali na kujikuta kapita katika taa nyekundu, honi za magari zikasikika kila upande, lakini hakusimama akakanyaga mafuta na ile gari ikazidi kuunguruma kwa nguvu.

HOTELI YA GRAND HYATT

GIZA LILIKUWA likishindana na taa za umeme zilizopendezesha jengo hilo la hoteli. Siku hiyo ambayo ilikuwa ni usiku wa kuamkia sherehe kubwa sana kwa dini za Kihindi ulijawa na watu wengi. Wale waliopenda ibada walienda mahekaluni na wale waliopenda starehe walienda kwenye makasino.

Gari moja, dogo, jeusi likaegesha katika maegesho na vijana wawili wakateremka, vijana hao wenye mandevu na maviremba vichwani mwao hawakuwa na la kuongea wala kusalimiana na yeyote waliomuona. Mmoja wao akainua simu na kupiga, akaongea maneno machache na kuiweka mfukoni ile simu kisha akauendea mlango mkubwa wa ile hoteli. Moja kwa moja alisimama mbele ya kaunta na kubadilishana maneno kadhaa na mhudumu aliyekuwa hapo na kutoka kuelekea kunako lifti za kupanda juu.Yule mwenzake alibaki kwenye makochi ya mapokezi akivuta gazeti hili na lile, mtego.

* * *

“Chiba wewe nisubiri upande uleeee, mi naingia kutoa begi tu napitia mlango wa nyuma kisha tunaondoka bila kuaga,” Amata akamwambia Chiba wakati akiufunga mlango wa gari hiyo na kumwacha Chiba akiondoka taratibu kuelekea upande wa pili wa ofisi hiyo. Amata akavuta hatua za nusu kukimbia na nusu kutembea, akazikwea ngazi na moja kwa moja akaifuata kaunta na kukaribishwa na yule binti wa jana yake, Sukaina.

“Ndiyo mrembo! Ujumbe wangu wowote?” akauliza.

“Ujumbe wako nimekupelekea chumbani tayari,”

“Sasa mbona hukusubiri hukohuko unikabidhi?” Amata akaanza maneno yake ya ubembe.

“Mmmm na wewe, tangulia nakuja,”

“Waja kweli au ndiyo kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa?”

“Naja kweli we tangulia dakika kumi nitakuwa nimefika maana ndiyo nafunga ofisi natoka. Nikukute kitandani sawa bebi?” Sukaina akarusha maneno ya kumlegeza Amata huku akijuwa wazi kuwa ni kitu gani kitakachomtokea kijana huyo. Yule jamaa aliyekaa pale kwenye kochi akamwoneshea ishara ya dole gumba Sukaina na kunyanyuka taratibu kuelekea kule ndani alikoenda Amata.

Kamanda Amata alibofya kitufe cha kuiita lifti lakini alihisi vinyweleo vyake vikisimama na mwili ukisisimka, akarusdi nyuma hatua mbili na kugeuka akapanda kwa ngazi za kawaida mpaka ghorofa ya nne kulikokuwa na chumba chake. Alipoufikia mlango, akautazama juu hadi chini, kisha akatupa jicho pale kwenye kitasa kile cha kielektroniki ambacho kufungua ulipaswa ku-chanja kwa ‘smart card’ kisha mlango ungefunguka. Moyo wake ukawa mzito kufanya jambo hilo, jicho lake lilipotua kwenye ile sehemu akagundua uwa mlango ule umefunguliwa kwa maana alama yake ya kiuzi alichokitengeneza kama kifundo fulani na kukipachika katika ule mfereji wa kuchanjia kadi haukuwepo. Akachomoa bastola yake ‘Berreta’ na kupachika kile chombo cha kupoteza sauti kisha akachomoa kadi yake nyingine na kuchanja, mara mlango ukajinasua loki zake. Akaufungua ule mlango kwa kasi na kubamiza kwa nyuma, kumbe yule mjinga alijificha upande huo. Akajikuta akipigwa na mlango usoni, akatoka pale huku bastola ikimwanguka chini na mkono kajishika pua.

Amata alirudisha bastola yake kikobani na yule bwana alipogeuka, alikutana na makonde mawili ya maana yaliyopita yote usoni, akayumba na kujibamiza mezani kabla hajaenda chini ambako hata hakufika kwani teke kali la Amata lilitua usoni na kumtupia upande wa pili wa kitanda. Kamanda Amata akaweka tai yake vizuri na kufunga upya saa yake, kisha akaruka kitanda na kutua upande wa yule bwege ambaye alikuwa akijiandaa kunyanyuka ilhali hali yake tayari ilikuwa tete. Alipotua sakafuni alihisi mlango ukifunguka tena nyuma yake, bila kuuliza, alichomo bastola na kujirusha chini huku tayari keshafyatu risasi mbili zilizoishia tumboni mwa yule mjinga wa pili na kumbwaga chini huku akigombania roho yake isimwache.

Amata akageuka haraka na kumrudia yule wa kwanza ambaye tayari alikuwa amesimama na kujiandaa kwa mapambano.

“Umemuua Rajiv! Sasa zamu yako,” akaunguruma huku shati lake likiendelea kulowa kwa damu zilizokuwa zikichirizika kutoka puani mwake.

“Tulia mpumbavu wewe,” Amata alimjibu kwa lugha hiyo ya Kihindi aliyokuwa akijarobu kumwemwesa japo maneno mawili.

“Tupa bastola tupambane, hujui kama nchi hii ndiko alikozaliwa Amitah na Mithun?” lile jamaa likamwambia Amata.

“Hamna tabu,” Amata akaipachika kwenye kikoba chake. Wakati akifanya hilo Yule jamaa alitua kifuani mwa Amata kwa miguu yake miwili. Amata akapepesuka na kujibamiza ukutani huku akimwona jamaa akitua sakafuni kwa miguu yake ileile. Kabla hajatulia, Amata alijizungusha huku akiwa amebonyea na kuwa mdogo kama mbuzi, mguu wake wa kulia uliozunguka kwa kasi ulimchota ngwala yule bwana aliyekuwa akijaribu kuruka ili akwepe pigo hilo, lakini haikuwa hivo kwani alichotwa vibaya na kubamiza kisogo chini huku kiwiliwili kikimfuatia juu yake. Alijitahidi kunyanyuka lakini guu la Amata likatua kwa nguvu kifuani na kumafanya ateme damu.

“Unamjua Premji Kanoon?” akamwuliza.

“Husilitaje bure jina la mtu huyo,”

Kamanda Amata akamwinamia na kumchapa kofi moja kali lililomwacha taabani.

“Nani mshirika wenu hapa?”

“Hatuna mshirika,” akajibu kwa taabu. Kamanda Amata akachomoa kisu cha kukunja na kukifyatua hewani, ile ncha yake ikachachamaa juu, alipokishusha kilitua kwenye nyama ya paja.

“Aaaaaiiiiiggghhhh! Sukaina wa mapokezi,” akajibu huku akifumba macho na kubana meno.

“Shenzi kabisa wewe,”

Akakichomo na kukifuta damu kwa nguo za yule jamaa huku akisimama na kukipachika mahala pake. Damu ilikuwa ikimbubujika pale chini. Amata akafungua kabati na kutupia vitu vyake ndani ya begi lake.

‘Haina haja ya kupoteza muda’ akawaza na kuivuta bastola yake.

“We mjinga salamu hii umpe mungu wako Premji Kanoon, mwambie Kamanda Amata yuko hapa,” akafytaua risasi na kuvunja goti la mguu wake mmoja, kisha akasonya na kupotea akiacha maumivu, kifo na kilio ndani ya chumba hicho.

* * *

Amata akatupi begi lake katika kiti cha nyuma na kujiweka kiti cha mbele.

“Vipi?” Chiba akauliza.

“Mmoja kafa, mwingine atakuwa kiwete milele na wengine tunawafuata leo hii hii,” Kamanda akajibu huku Chiba akiondoka eneo lile na kutokomea gizani.

“Itawezekana kufunga kazi usiku huu? Maana nilikadiri saa sabini na mbili,” Chiba akauliza huku akiiacha barabara kubwa na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyopita katika miti mingi ambayo moja kwa moja ilikuwa ikielekea Bahrain House.

“Usijali, hapa kazi tu, ndani ya saa hizi arobaini na nane tayari huyu mtu atakuwa mikononi mwetu. Naamini Madam atafanya ulivyomwambia,” Kamanda akaeleza huku akiweka bastola yake na silaha nyingine tayari tayari.

“Usihofu juu ya Madam, ameona jua kabla yetu”.

Chiba akaegesha gari ndani ya jengo hilo na kuteremka kisha akaingia mahala fulani na kuchukua silaha mbili tatu na mavazi ya kutumia katika hali halisi itakayowakumba, mabomu ya machozi na vinyago vya kuzuia sumu hiyo, mavazi ya kuogelea na mitungi ya hewa mine. Sehemu nyingine ya jengo hilo akafungua boti ndogo iliyokuwa kwenye kitoroli na kuivuta kwa mikono yake mpaka, ndani yake akatupia vile vitu na kuisukuma mpaka majini. Bahari haikuwa mbali na jengo hilo kuukuu: Kamanda Amata na Chiba wakaingia kwenye boti na kuiwasha, safari ikaanza.

“Watatusubiri kwa njia ya barabara, sisi tutaingia kwa njia ya maji!” Chiba akasema
 
Sehemu Ya Tatu (3)



“Ulijiandaa sana kijana!” Amata akamsifia.


“Ndiyo, maana maelekezo mengi tayari nilipewa na Madam S nimwone Yule mzee ndiye akanipa ramani ya mji huu na lile kasri la Pancho,” Chiba akaeleza.



“Amekwisha, Gabacholi yule!” Amata akasema huku akifungua chupa ndogo ya Grants na kuigugumia kinywani.



“Aaaaaaakkhhhh!” akashusha pumzi iliyoashiria ukali wa kinywaji hiko.



* * *



Chiba alizima mlio wa injini ya boti na kuiacha iseleleke taratibu mpaka ilipo karibia umbali kama wa mita mia tano hivi. Wakati huo Amata alikuwa tayari amekwishavaa nguo zake za kupigia mbizi, mitungi yake mgongoni na begi dogo lilisiloingia maji mbele ya tumbo lake.



“Chiba, hapa kazi tu, mi naingia kwa njia ya maji nafikiri ni njia rahisi kama ulivyonambia, na wewe pitia hii hii lakini upande wa pili sote tukaibukie ndani na kutafuta njia ya kumnasa mtu huyo, tukishamtia mkononi kila mtu aangalie ustaarabu wa kuitoka hiyo himaya lakini tukutane Bahrain,” Kamanda Amata alimweleza mkakati mzima Chiba kisha akajitupa majini na kupotelea humo.

Chiba akaendele kupiga kasia kuisogeza ile boti mpaka kwenye mimea ya baharini iliyojazana upande mmoja wa peninsula hiyo. Akaegesha naye akavaa vifaa vyake na kujitupa majini kwa uelekeo mwingine.

* * *


Ndani ya hekalu hilo sherehe za mwanga ‘Diwali’ zilikuwa zikiendelea, watu walikuwa wakiimba na kucheza, kwa ujumla palichangamka. Premji Kanoon au Pancho Panchilio alikuwa ameketi sehemu ya juu kabisa akifuatilia michezo na burudani zote zilizokuwa zikiendelea katika ukumbi huo. Kando yake alikaa na watu wengine kadhaa huku wanawake kama nane hivi warembo wa kuvutia walikuwa wakimpepea, wengine wakileta vinywaji na kadhalika. Nyuma yake alisimama mtu mmoja, mwanaume mwenye tambo kubwa, aliyefuga sharubu zake na kuzichanua huku na kule kama askari wa Kijerumani enzi za mkoloni. Mikono yake aliifungamanisha nyuma. Macho yake yalionekana kutopepeswa upande wowote ule. Na katika kila upande au kona ya jengo lile walionekana vijana waliovalia sare na vitambaa vyao vichwani mwao wakirandaranda huku na kule.



Kamanda Amata aliibuka majini na kujikuta kwenye chumba ambacho ndani yake kuna boti kubwa la kifahari lililoegeshwa.



‘Nimekuja wakati mzuri, ningekuja mchana kusingekuwa na maji hivi,’ akawaza huku akivua ule mtungi na kuuweka kando, akatoa na yale mavazi yake kisha akafungua begi lake na kujipachika kila silaha aliyoihitaji mwilini mwake. Sauti ya viatu vya mtu aliyekuwa akija upande huo vilimfanya atulie tuli huku kisu chake kikiwa ngangari kiganjani.



“Inabidi tuiwashe kwanza ili injini ipate moto. Mkuu anasema hana budi kwenda Punjawar usiku huu,” Sauti ya kwanza iliongea.



“Mbona ghafla hivi wakati sherehe hii yote kaandaa kwa ajili ya watu wake?” Sauti ya pili ikauliza.



“Mi mwenyewe sielewi aisee, ngoja tuwashe kabisa yeye akifika ni kuondoka tu,” ile sauti ya kwanza ikarudia.



‘Nimsubiri kwenye boti?’ Amata akajiuliza moyoni.



‘Uamuzi mbaya utakuwa’ akajijibu mwenyewe na nukta hiyohiyo yule jamaa akaibukia kwenye mlango mmoja wa chumba hicho. Amata akaruka kwa wepesi na kumvamia huku akiwa tayari kamdidimiza kisu moyoni. Akamshusha chini taratibu na kumsukumia kwenye maji. Kisha akatulia kwani bado mwingine alikuwa akija upande huo.



“Kumar! Kumar!” Yule wa pili akaita. Lakini hakukuwa na jibu kutoka kwa swahiba wake, akaendelea kwenda na alipofika kwenye kile chumba hakuamini anachokiona. Mwili wa Kumar ulikuwa ukielea kifudifudi majini. Mshtuko wake ulikuwa zahiri shahiri, akainua redio yake na kuomba msaada.



“Kumar mara cuka hai! Kumar mara cuka hai!” (Kumar amekufa! Kumar amekufa), Amata akajibana kimya nyuma ya pipa kubwa lililojaa vipuli mbalimbali. Dakika hiyohiyo watu kama saba wenye silaha wakaingia katika kile chumba.



‘Nimecheza blanda’ akajiambia, akachomoa bastola yake iliyofungwa kifaa cha kuzuia sauti na kuiweka tayari. Risasi ya kwanza akapiga mtungi wa kuzimia moto na poda iliyokuwa ndani yake ikatoka kwa kasi na kuwachanganya wale jamaa. Kamanda Amata akapita kwa kasi huku watatu waliokuwa mbele yake wakiwa chali kwa risasi kutoka kwenye bastola yake, sekunde mbili tu alikuwa keshafika mlangoni na kuufunga kwa nje akiwaachia kizaazaa. Ujia mrefu ulimkaribisha. Ving’ora vya hatari vikalia kila kona, mvurugano ukaanza kila kona, burudani zikasimama na kelele za vilio nzikaanza huku na kule.



* * *



Chiba aligundua hali ile baada ya kusikia kelele za watu, akapachika head set yake masikioni tayari kwa kazi.



“Amata vaa barakoa yako kazi inaanza,” Chiba akaongea kwenye kile kifaa na kisha akavaa kinyago chake cha kuzuia gesi ya machozi na kinachoweza kumfanya aone gizani bila tabu. Akatazama huku na kule akaona sensor ya moshi ambayo ikipata moshi basi huruhusu maji kumwagika, akatazama huku na kule akaona ua jirani, akavuta karatasi la urembo lilikuwa hapo akawasha moto na kisha akasogeza karibu na ile sensa, nukta hiyohiyo jengo zima likaanza kutiririsha maji, Chiba akaifuata swichi kubwa ya umeme na kuizima kisha akaondoa fyuzi na kuzitupa mbali. Sasa jengo lote lilikuwa giza na jenereta liligoma kuwaka, tayari kijana huyo wa TSA alishapita na kuondoa betri. Yale maji yaliyokuwa yakimwagika nayo yakakatika ghafla.



* * *



UKUMBI wote ulishikwa na kimuhemuhe, Amata alichomoa bastola yake yenye mabomu ya machozi na kutawanya huku na kule. Moshi huo mzito uliwafanya watu kukohoa bila kikomo, wakiishiwa nguvu na wengine kuanguka chini hawajiwezi.



Pancho Panchilio, aliinuliwa pale alipoketi na vijana wake kama saba hivi wakawa wamemzunguka kwa kumlinda wakiwa na silaha zisizojua huruma. Kutokana na gia lile walishindwa kumwona sawasawa Amata hivyo ilikuwa ni rahisi kwake kuwatawanya kwa risasi. Zilipomwishia akaruka sarakasi na kutua karibu kabisa na Pancho Panchilio huku miguu yake ikiwatandika mateke walinzi wawili waliobaki. Pancho alitaka kukimbia kuingia kwenye mlango mmoja lakini hakufanikiwa, ngwala moja maridadi ilimbwaga chini vibaya, wale vijana walipojaribu kunyanyuka, risasi za Chiba ziliwarudisha chini na Amata akapata nafasi ya kuinuka na kukutana uso kwa uso na Pancho.



“Twende nyumbani mwanaharamu wewe!” kamwambia huku akimtandika konde moja kali lililomfanya ayumbe na kupoteza mwelekeo. Konde la pili likamrudisha chini akiwa hoi, pamoja na ule moshi kumlegeza. Amata alijikuta akishikwa na hasira akikumbuka mtu huyo alichowafanyia yeye na wenzake kule Kerege katika mkasa uliopewa jina la Kitisho.



Kabla hajafanya lolote, akajikuta akipigwa na kitu kizito kisogoni, lakini mpigaji hakulenga sawasawa, Amata akageuka na kupeleka mashambulizi makali yaliyolifanya lile jitu lipoteane lenyewe kwa lenyewe. Lilipotulia likajikuta likitandikwa risasi mbili za kifua.



“Hatuna muda wa kupoteza, nasikia ving’ora vya wanoko huko nje,” Chiba alimwambia Amata, na wakati huo huo, Amata akamkamata mkono Pancho na kumkokota kwa nguvu. Mirindimo ya risasi bado ilikuwa ikiendelea, moshi wa machozi ulikuwa umechanganyika na ule wa baruti na kulete harufu ya tatu.



“Ondoka naye Amata, mi nalinda mkia wako,” Chiba alimwambia tena braza ‘ake na Kamanda Amata akatoka na Pancho, alipoona upinzani umekuwa mkali akambeba Pancho na kuruka naye ghorofa ya chini yake wakafika hoi. Amata akawahi kunyayuka na kutumia bastola yake nyingine kupambana na wawili watatu waliokuiwa mahali hapo na kujaribu kumletea zengwe.

Haraka akaiwahi gari iliyokuwa imeegeshwa hapo na kufungua mlango.



‘Asante sana’ akashukuru baada ya kukuta funguo ikining’inia, akafungua buti.



“Ingia!” akamwamuru Pancho huku akiwa amekiinua kile kinyago chake na kukiweka kwa juu, Pancho akapigwa butwaa kumwona kiumbe huyo matata.



“Unashangaa nini? Ingia unanipotezea muda,” kamanda akang’aka lakini Pancho hakutaka kufanya hivyo. Konde moja la tumbo likamfanya Pancho ajiinamie huku amejishika tumbo lake, teke la kusukuma lilipeleka mpaka kwenye buti na Kamanda Amata akamalizia kufunga buti hilo kwa mguu kisha akaingia kwenye usukani, akaiwasha gari hiyo na kutoka kwa kasi huku akigonga geti na kukunja kushoto. Mfukuzano na gari za polisi ulichukua nafasi katika barabara za Bombay. Amata aliwapeleka nje ya mji kwenye barabara ya hatari kabisa, yenye mteremko mkali na wenye kona za ajabu, ambapo wengine waligwaya na waliojaribu walijikuta wakiishia shimoni.



Baada ya kuhakikisha wote kawaacha mbali Amata alichukua uelekeo wa Bahrain house na kuliacha jiji hilo. Saa tisa za usiku akaegesha gari ndani ya jengo hilo kuukuu, akateremka akiwa hafai kwa vumbi lililomkaa mwilini. Akafungua buti na kumtoa Pancho aliyekuwa kajikunyata ndani yake.



“Shuka!” akamwamuru naye akashuka. Akamkokota mpaka ndani ya chumba kimoja kikubwa.



“Pancho Panchilio au Premji Kanoon, karibu katika himaya yangu, mara hii ni zamu yako,” Sauti ya Madam S ikasikisa na taa yenye nuru hafifu ikawaka. Madam S akainuka alipoketi na kumjongelea mtu huyo. Kofi moja kali lilitua shavuni mwa Pancho na kumwacha akitetemeka.



“Ulifikiri utafanikiwa kunikimbia? Twende nyumbani nikakuoneshe kama mimi ni Head of T.S.A,” Madam akaunguruma na kumpa pingu Amata naye akamfunga mikono yake na mnyororo akautia miguuni mwake. Akamkokota mpaka kwenye ile gari waliokuja nayo na Chiba mara ya kwanza.



“Nafasi yako ni kwenye buti tu, akamwingiza na kulifunga kisha akatulia nyuma ya usukani huku kushoto akimwacha Madam S.



“Chiba, Chiba, wapi?” Kamanda akauliza kwenye kile chombo chake.



“Naegesha boti nimefika,” akajibu.



“Weka kiberiti,” akampa agizo. Baada ya sekunde chache Chiba aliungana na wenzake na kuingia siti ya nyuma.



“Mzigo uko wapi?” akauliza Chiba.



“Upo mahala pake,” akajibu huku akiondoka eneo lile na kupita njia za vichochoroni.



“Kilomita ishirini na mbili kijiji cha Malve” Madam S alimwambia Amata na moja kwa moja akaelekea huko nje kabisa ya mji.



Hali ya utulivu ilitawala kijiji kile watu wote walikuwa wamelala ndani ya nyumba zao, ni miti tu iliyokuwa ikitikiswa na upepo wakati Amata akiegesha ile gari katika moja ya kichaka karibu na barabara kubwa inayoelekea baharini, barabara ya vumbi. Dakika mbili tu Scoba akatua na ndege ndogo aina ya Boeing yenye uwezo wa kubeba watu watano lakini yenye nguvu na kasi ya kutosha. Ndege hii ilinunuliwa na serikali ya Tanzania kwa kazi maalumu kama hizi na pia kwa ulinzi wa haraka wa Rais wa nchi inapobidi. Nje ya kumhudumia Rais, ni TSA pekee waliweza kuitumia ndege hii na ni kwa kibali cha Rais tu.



Scoba, akatumia barabara hiyo kutua kwa kutumia mwanga wa tochi alizowasha Madam S akiwa chini kwa ishara aliyompatia. Hakuna kusubiri, walimkokota mtu wao na kumpakia ndegeni, huku kwa mbali wakisikia ving’ora vya polisi vikielekea upande wao.



“Haraka, haraka, haraka,” Madam alihimiza na mlango ukafungwa, Scoba moja kwa moja aliiongeza nguvu ile ndege na kuodoka kwa kasi huku akiwaacha wale polisi wakijaribu kufyatua risasi bila mafanikio. Dakika moja ndege ile ikawa angani ikikata bahari na kuelekea katika anga ya kimataifa ambako huna ruhusa kuifanya lolote.



* * *



“Na leo hii utatakiwa kusema siri zote ulizozificha mwanaharamu wewe!” Madam S alimwambia Pancho kwa ukali mara baada ya ndege ile kukaa sawa angani na kila mtu kuweza kufanya shughuli yoyote. Pancho Panchilio alitulia kimya akiangalia kwa jicho la kukata tamaa huku mwili wake ukionekana bado kukosa nguvu kwa kipigo cha rasha rasha alichokipata kutoka kwa Amata.



“Kamanda mwondoe hapa mpeleke kwenye chumba cha mwisho,”



Kamanda Amata akanyanyuka na kumchukua Pancho kwa kuushika ukosi wa shati lake, akamkokota mpaka katika chumba hicho na kumtupia humo. Mlango ukafungwa na ukimya ukatawala.



“Najua hauko peke yako kwenye mtandao huu, Mahmoud na mwenzake tulishawakamata wewe ukatutoroka kijanja. Na wale vibaraka wako wengine kule Kerege tumewakamata na wengine wamekufa wenyewe lakini wewe bado umetukimbia. Hukutukimbia tulikuwa tunaendelea kukuchunguza na sasa arobaini zako zimefika, haya nitajie mmoja baada ya mwingine kabla hatujatua Dar es salaam,” Madam S alionekana kuwa na hasira kali juu ya mtu huyo. Pacho alibaki kimya hakuzungumza lolote.



“Jeuri!” Amata akasema, kisha ghafla akapiga teke kwenye korodani lililomfanya Pancho apige kelele za maumivu na kuikusanya mikono yake yenye pingu katika eneo hilo.



“Utasema?” Kamanda akauliza. Lakini Pancho bado alibaki kimya huku akigugumia kwa maumivu makali. Amata akachukua kiberiti cha gesi na kukiwasha kisha moto wake akauweka chini ya kidevu cha Pancho. Maumivu aliyoyapata kwa moto ule uliokuwa ukiichoma ngozi akashindwa uvumilivu.



“Aaaaaaiiigghhh! niache! niache! nasema! nasema!” akapiga kelele.



“Sema, upo na nani kwenye mtandao?” Amata akauliza.



“Kamba Sebule, Kamba Sebule,” akataja jina la mtu mkubwa ambaye ni balozi wa nchi wa Tanzania katika nchi fulani.



“Na mna misheni gani hapa?”



“Mapinduzi ase aaaaiyyayayay aaaaiiiggghh! We muuaji wewe,” akalia kwa uchungu.



“Mwingine nani?”



“Alibaki huyo huyo, aaaaaaghhh!”



“Hutaki kusema ee? Sasa nakutupa nje kwa huna faida wewe,” Kamanda akamwambia Pancho kisha akamtazama Madam S.



“Madam! Jishike vyema namtupa nje huyu mshenzi,”



Akabonyeza kitufe fulani na mlango ukafunguka taratibu, upepo mkali ukaingia ndani na kuleta ufumbufu mkubwa huku ndege ile ikiwa juu futi 40000.



“Utasemaaa au husemiii?” Kamanda aliuliza kwa kelele huku akimtazama Pancho. Akabaki kimya bila jibu. Amata akamsukuma na kumtanguliza kichwa nje, akamsukuma nje. Pancho akatoka mlangoni na kuning’inia vibaya.



“Aaaaaiihhhh, weweeeeeee! Niache nasema kila kituuu, ohhhhh! Nooooo!” Pancho akapiga kelele.



“Sema, mna misheni gani?”



“Mapinduzi, mapinduzi asee,” kutokana na upepo mkali Pancho aliyumba na kujigonga kwenye ubavu wa ndege. Kamanda Amata akatumia nguvu zake zote na kumvuta ndani akambwaga kando huku ule mlango ukijifunga taratibu. Pancho alipoteza fahamu na kutulia kimya.



“Kamba Sebule,” madam S akarudia jina hilo.



“Vipi?” Amata akauliza.



“Inabidi achunguliwe mara kwa mara asije kutupotea kuanzia sasa,” akajibu.



Madam S na Amata wakatoka katika chumba kile na kumwacha Pancho akiwa hajitambui damu ikitiririka usoni huku pingu na mnyororo vikiwa vimemdhibiti.



“Vipi?” Chiba akauliza.



“Poa, yupo huko kapumzika,”



“Yuko down?” (amekufa?)



“Hapana anaelea tu,” (hapana amezimia tu)



“Kinachoendelea?” Chiba akauliza.



“Kamba Sebule, yupo kwenye mtandao,” Amata akajibu huku akiketi sawia kitini. Chiba alibaki kakodoa macho kwa taarifa hiyo, hakutegemea mtu kama Kamba Sebule kuhusika kwenye mtandao wa maovu kama huo.







DAR ES SALAAM – saa 2:30 asubuhi



Saa tano ziliwaweka hewani na asubuhi ya saa mbili na nusu waliwasili uwanja wa ndege wa jeshi, Dar es salaam. Gari jeusi lenye boksi kubwa nyuma lilisogea taratibu mpaka kwenye ile ndege na kusimama jirani kabisa. Pancho Panchilio aliteremshwa na kuingizwa kwenye hiyo gari haraka na kufungiwa humo, askari wawili wenye silaha wakaingia pia sehemu ya nyuma, milango ikafungwa na safari ikaanza.



“Asanteni sana kwa kazi vijana,” Madam S aliwashukuru Amata na Chiba.



“Ndiyo wajibu wetu,” Chiba akaitikia.



“Sasa mpumzike kisha kesho jioni tuonane ili tuweke mambo sawa juu ya mtu huyu,” Madam akamaliza kusema na kuingia garini, Scoba akaondosha gari iliyombeba Madam S. Chiba na Amata waliingia kwenye gari jingine alilokuja nalo Gina wote wakaondoka uwanjani hapo.

Siku hiyohiyo …



BAGAMOYO



VIJANA KAMA SABA hivi walikuwa katika chumba kimoja cha jengo lililochini ya ardhi katika kisiwa kimojawapo kati ya visiwa vinne katika bahari ya Bagamoyo. Vijana hao wote walivalia mavazi meusi na kofia zao zilificha hadi nyuso na kuruhusu macho tu kuonekana. Mikono yao waliifutika kifuani na kufanya wote wawe katika mtindo mmoja wa kupendeza. Kati yao mmoja ndiye alikuwa na mkanda mpana mwekundu katika kiuno chake.



Vijana hawa walikuwa ni jeshi la siri sana la Pancho Panchilio, walikuwa wamefuzu mafunzo Ninjutsu huko Uchina kwa nyakati tafauti. Gabacholi huyu aliwaajiri na kuwaweka katika himaya yake, maalum kwa kazi maalum.



“Komredi ametekwa,” akawaambia wale vijana wengine.



“Usiku wa kuamkia leo pale Bombay, washenzi wamemchukua komredi na mpaka tunavyoongea sasa ameshafikisha hapa nchini,” akaendelea kusema; “hii inaonesha dharau kubwa sana kwetu, kwa kuwa wale jamaa tulifanikiwa kuwateka wote wakatutoka kwa namna ya kibabe sasa naona wametugeukia sisi. Hatuwezi kuwaacha, sasa ni vita na vita hii ninaitangaza sasa. Komredi lazima akombole ndani ya saa sabini na mbili hata kama atakuwa amefichwa Ikulu, ohi?”



“Oha!” wakajibu kwa pamoja kumaanisha kuwa wanajua na wanaelewa kile walichoambiwa, wakaiondoa mikono yao kifuani na kukutanisha viganja kisha wakainama. Baada ya mazungumzo mafupi wakatawanyika na wawili kati yao wakabaki pamoja na Yule aliyevaa vazi lenye mkanda mwekundu wakaketi katika meza hiyo ya duara pamoja wakijadiliana jambo.



“Tutatumia gharama yoyote tumpate,” mmoja wao akasema.



“Hilo ndilo hasa nalitaka tuzungumze, mambo waliyoyafanya Bombay kule si madogo, wamedhalilisha hekalu la Hanuman,” mwingine akadakia.



“Yote tuyaache, mpango wao ukoje mpaka sasa na wapi amehifadhiwa?” Yule wa kwanza akavunja mazungumzo.



“Kutoka chanzo chetu cha habari wanasema jamaa kahifadhiwa Keko, lakini kesho kutwa atafikishwa Kisutu mahakamani,” Yule kiongozi akajibu.



“Baaasi mpaka hapo kazi imekwisha, lazima atekwe ama anavyokwenda au anavyotoka,” mwingine akajibu huku akipiga ngumi mezani.



“Nani wa kulainisha mipango? Si unajua wote wapo lupango,” Kiongozi akauliza.



“Aaaaa Mkuu hilo ni dogo, Kamba Sebule na Maliapopo si wapo? Watafanya kazi,”



“Na hata hizi habari ni Maliapopo aliyenipatia na yuko sambamba na kila linaloendelea atatujulisha,” akamaliza na kuwaomba vijana wakae tayari kwa lolote watakaloambiwa.






GEREZA LA KEKO



PANCHO PANCHILIO aliketi sehemu ya peke yake, mikono yake ikiwa na pingu kama alivyoletwa siku iliyotangulia. Chumba chenye mtindo wa duara kilichojengwa kwa vyuma imara pande zote, ndimo alimohifadhiwa mtu huyo. Taa yenye mwanga mkali wa watts 750 ikawashwa na kummulika mtu huyo muda wote, joto kali likamtesa, mwili ukatota kama aliyemwagiwa maji.



“Aaaaaigh Shit!” aling’aka baada ya taa ile kummulika usoni moja kwa moja kila ajigeuzapo.



“Acha kupiga makelele ya kitoto bwege we!” Madam S alimwambia huku akisogea taratibu na vijana wake Chiba na Amata wakiwa nyuma yake.



“Kesho mahakamani,” akamwambia.



“Afadhali haki ikatendeke maana hapa mnanionea tu,” Pancho akajibu.



“Haki? Unaijua haki wewe? Ungeijua haki ungefanya yote uliyoyafanya? Pancho au nikuite Premji Kanoon, nchi iliyokulea unaweza kuifanyia haya? Kudhulumu haki, haki ya mwananchi mdogo anayevuja jasho la chumvi na kulilamba kwa kukosa maji safi ya kunywa lakini wewe na mabwanyenye wenzio wenye matumbo makubwa yasiyo na shukrani mnahamisha fedha na kuzificha ughaibuni,” akameza mate, na kuendelea, “Pancho! Kweli kabisa unadiriki kukifutilia mbali kikosi hiki unachokiona ili tu uendeleze biashara yako haramu, unaniteka mimi wewe, unateka vijana hawa uwaue halafu ufanye nini kwenye nchi hii? Kila anayekaribia kung’amua madhambi yako unataka ummalize. Siku yako imefika, nimekufuata India kwa gharama ili nikuoneshe kama mimi ndiye Madam Selina, mwanamke wa chuma tena chuma cha pua, kama kukuua ningeshakuua long time ila nilitaka kwanza nikuoneshe jeuri yangu kisha nikusweke jela maisha yako yote …”



“Kamwe, Pancho Panchilio hawezi kuingia jela, ha! Ha! Ha! hiyo sahau we mwanamke, utaiona miujiza yangu kabla ya kufika jela au hata mahakamani, mtatafutana ninyi nakwambia na hapo ndipo mtashuhudia mmoja mmoja wenu akianguka na kufa wakati mi narudi kuishi maisha yangu ya anasa. Ikitokea wewe ukabaki hai basi nitakualika kwenye tafrija kubwa pale Kilimanjaro Hoteli kisha utaona nani na nani wamealikwa, ndipo utakapojiona upumbavu wako we mwanamke ni mwanamke tu…”



Madam S alijikuta akishikwa na hasira akachomoa bastola yake.



“Rudia maneno yako nikupasue fuvu hilo,” aliongea kwa hasira.



“Ha! ha! ha! ha! Muoneni bibi yenu huyu, hana akili kabisa,” aliwaambia kina Chiba na Amata. Kama alifikiri anamuuzi mwanamama huyo pekee, basi alikosea sana, kitendo cha ghafla, Pancho alijikuta akipoke teke moja la kilo nyingi usoni, akajipiga kisogo ukutani kisha akaanguka sakafuni, kimya!



“Funga domo lako! Punguani wewe,” Amata akaunguruma. Sekunde chache Gabacholi huyo akajiweka sawa tena mara hii sura yote ilikuwa nyekundu.



“Tena wewe! Wewe! Wewe! Ipo siku yako. Nitakutoa huo utumbo niuanikie nguo,” Pancho alimwambia Amata.



“Utafanya hayo kabla bastola yangu haijafumua ubongo wako,” Amata akamaliza na kumtazama Madam S aliyekuwa amekunja sura kwa uchungu.



“Kesho Mahakamani,” Madam akamwambia Pacho na kugeuka kuanza kutoka ndani ya chumba kile maalum.



* * *



SIKU ILIYOFUATA



Asubuhi ya siku iliyofuata, Pancho Panchilio aliandaliwa tayari na kupelekwa mahakamni ili kusikiliza shitaka lake. Magari ya magereza na lile la FFU yalikuwa tayari mbele ya gereza hilo la Keko. Ulinzi mkali uliimarishwa kuzunguka ngome hiyo kwani taarifa kwa vyombo vya usalama ilikwishatolewa kuwa mtuhumiwa huyo ni mtu hatari sana. Vijana wa kazi walikuwa tayari kwa lolote.



Akiwa chini ya ulinzi mkali, Mhindi jeuri huyo alitembezwa taratibu huku miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo na kisha mnyororo huo huo kuunganishwa na kuishika pingu iliyoifunga mikono yake. Msafari ulianzia Keko kuelekea Kisutu ambako shauri lake lilitakiwa kusikilizwa. Kwa kuwa barabara zote yaani ya Chang’ombe, Nyerere, Bibi Titi zilizuiwa magari kupita kwa dakika kadhaa, iliwachukua dakika kama kumi na tano tu kuwasili katika mahakama hiyo huku Pancho akiwa ndani ya gari maalumu iliyozibwa pande zote.



Mahakama ilifurika watu, kama kawaida, waandishi wa magazeti na wale wa televisheni walikuwa bize kutafuta habari lakini zaidi kuipata picha ya mtu huyo. Baada ya yote kukamilika na shauri hilo kuahirishwa, Pancho alitakiwa kurudishwa rumande mpaka baada ya mwezi mmoja ambapo ushahidi utakuwa umekamilika. Gari lile lililomchukua kutoka Gereza la Keko, ndiyo iliyokuja gerezani hapo kumbeba kwa mara nyingine na sasa ilikuwa na kazi ya kumrudisha mahabusu. Alitolewa akiwa chini ya ulinzi mkali mnyororo wake miguuni na pingu mkononi, moja kwa moja akaingizwa ndani ya gari hiyo isiyo na dirisha hata moja katika eneo la kuifadhi wahalifu. Baada ya kufungwa mlango wake askari wawili wenye silaha walikaa katika kijichumba kidogo wakiwa na bunduki zilizoshiba vyema.



Msafara ukaanza kutoka katika gereza hilo, gari la polisi likatangulia mbele likipiga ving’ora vya kuomba njia, kisha likafuatia hilo lililombeba mhalifu na mwisho kulikuwa na gari jingine la askari magereza wenye silaha, safari kuelekea Gereza la Ukonga na sio Keko tena ikaanza kwa kasi huku gari nyingine zikiacha njia na kuupisha ule msafara uende. Kasi iliyokuwa kwa gari zile haikuwa ya kawaida, kila mtu alishangaa na kujiuliza ‘kuna nini?’







Wakati huohuo…



Barabara ya Shaurimoyo na Nyerere



Ndani ya gari moja lililoegeshwa muda mrefu katika Barabara ya Shaurimoyo, watu sita walikuwa kimya kwa muda mrefu, na mara ukimya ule ukakatishwa kwa biip moja ya simu ya kiongozi wao. Kutoka kiti cha mbele alichoketi akageuka nyuma na kuwatazama viajan wake.



“Mko tayari? Tunafanya kazi sasa, dakika tatu kila kitu kiwe kimekamilika, kwa kuwa wao hawajajiandaa kwa hilo basi itakuwa ushindi ni upande wetu, ohi?”



“Oha!” wakaitikia vijana wa kazi waliovalia nguo za khaki, na bunduki zenye risasi tele migongoni mwao, nyuso zao zilikuwa tayari kufunikwa na barakoa za kukinga gesi ya machozi, walikamilika.


Kiongozi wa operesheni hiyo aliinua redio yake ya upepo na kuiweka karibu na kinywa chake.



“Namba one, namba one, stand by!” akaongea.



“Umesomeka, namba one stand by,” akajibiwa.



“Namba one on your marks… Get set… go!” Yule kiongozi alitumia mtindo unaotumika na wanariaadha kutimua mbio.



Kutoka upande wa Keko, karibu kabisa na eneo la daraja la leri pembezoni mwa Kiwanda cha Uchapaji cha Taifa, liliwashwa tingatinga na kuchomoka kwa kasi kuelekea barabara ya Nyerere. Hamad! Wakati ule msafara unafika na lile tingatinga linafika, ajali mbaya isiyosemeka ikatokea. Lile tingatinga likaigonga gari ya mbele ya polisi na kuharibu vibaya, haikuishia hapo, iliigonga ile gari ya kubeba mhalifu na kuikunga njia, ikaibana karibu na gema la daraja. Mtafutano wa watu ukaanza asubuhi hiyo katika eneo lile.



Kutoka kwenye lile gari la askari maalum wa magereza, waliruka na kutua nje kila mmoja akachukua sehemu yake kwa kuangalia nini kinatokea. Kabla hawajakaa sawa, gari aina ya Range Rover ikaingia kwa kasi na vijana kama sita hivi wakateremka haraka na kulizunguka eneo lile, mabomu saba ya machozi yakatua ardhini na wao wakavaa barakoa zao tayari kuzuia adha ya gesi ile ya machozi. Wawili kati yao haraka wakaenda kuufungua ule mlango wa lile gari, risasi zikaanza kulindima kutoka kwa wale vijana wa magereza na polisi, wakashambuliana na wale majambazi. Jambazi mmoja akapigwa risasi na kudondoka lakini hakufa bali alijeruhiwa vibaya.



Mlango ukafunguka, mmoja wa askari bado alikuwa ana nguvu zake, alimpiga yule jambazi kwa kitako cha SMG kichwani, akapepesuka na kushindwa kustahimili akaaguka chini, Yule mwenzake akatumia risasi ya moto na kupiga askari wote wa ndani kisha akaingia na kumfungua bosi wake. Mabomu ya machozi yaliongezwa na mosi ukatapakaa eneo lote.

Yule jambazi aliyetoka na Pancho akapiga aina Fulani ya mluzi na wale wenzake wote wakakimbili garini, lakini jambazi mmoja aliyekuwa mwisho ambaye kiutaratibu lazima apande mwisho, akamchapa risasi yule jambazi mwenzake aliyekuwa na hali mbaya pale chini ili kuzuia asije ongea lolote, nukta hiyo hiyo ukasikika mlio wa helkopta eneo lile, nalo likazidisha vumbi, wale majambazi na mtu wao wakajitupa ndani yake na lile dege likapotelea angani.



“Upo Salama Mkuu,” Kiongozi akamwambia Pancho.



“Yeah, hongereni kwa kazi,” akawapongeza wakati huo wakimwondoa ile minyororo na pingu mikononi mwake.



“Ha! Ha! Ha! Ha! mmewapiga chenga ya mwili,” Pancho aliwasifu vijana wake kwa lugha ambayo Yule dereva hakuielewa.



“Ijapokuwa tunasikitika tumepoteza wawili,”



“Usijali, hiyo ni najali kazini,”



“Sawa Boss”.



Ilikuwa kama filamu hivi, kwa ughafla wa tukio lile ambalo halikuchukua hata dakika tatu, askari waliokuwa wakisindikiza mhalifu huyo walijikuta hoi. Wamezidiwa ujanja, ijapokuwa waliwapiga risasi wawili lakini wao walipoteza wawili pia. Utulivu ukarudi, kilichobaki kilikuwa na mtapakao wa moshi na harufu ya baruti inayoishia kwa upepo. Watu walikuwa wakisogea taratibu kuona kulikoni. Polisi nao walifika na kuweka ulinzi eneo hilo ikiwa pamoja na kufunga barabara.

Mkuu wa polisi mkoa wa Dar es salaam alikuwa hapo akiangalia hali halisi, sura yake ikikunja ndita sehemu ya juu ya macho yake, hasira isiyojificha ilionekana wazi wazi.



“Washenzi hawa,” akang’aka kwa hasira.



Wakati polisi wengine wakiendelea kupima hapa na pale yeye bado alikuwa akiendelea kuwasiliana kwa redio yake.



“Nipo eneo la tukio, mmeona helkopta yoyote ikipita maeneo hayo?” akawauliza polisi wa anga ambao daima kazi yao ni kuvichungulia vya juu.



“Vipi Mkuu?” sauti ya Inspekta Simbeye ilimfanya yule RPC kushtuka na kumwangali mtu huyo. Wakapigiana saluti za kijeshi kisha mazungumzo yakaendelea.



“Kwa hiyo wamekuja na helkopta mpaka hapa na kumchukua mtu wao?”



“Ndiyo, lilikuwa ni shambulizi la ghafla na la ufundi wa hali ya juu ijapokuwa hata vijana wetu wamefanya kazi kubwa mpaka kuwalaza hawa wawili, sema tu ndiyo hivi wameshakufa, laiti wangekuwa hai pangechimbika,” akamaliza kusema RPC na kumwacha Simbeye akikagua hapa na pale kuona kama kuna lolote la ajabu katika ajali hiyo, alitazama hiki akagusa kile, alipindua hiki na kusimamisha kile kule arimuradi tu afanye kitu.





SHAMBA

Mchana huohuo



Simu ya mkononi ya Madam S iliita kwa fujo, alipotupa jicho mezani akaona simu inayowakawaka ni ile ya taarifa nyeti.



“Shiit, nini tena?” akaongea kwa sauti ya kuonesha kuwa hajafurahia simu hiyo, akainyakuwa na kuitega sikioni kwanza.



“Hello Sellina!” mara moja akaitambua sauti hiyo.



“Ndiyo Simbeye vipi (…) what! Unasema, (…) acha masihara katika kazi asee,”



“…Madam habari ndiyo hiyo, Pancho Panchilio kaokolewa na jamaa zake kwa njia za kikomandoo”.



Madam S akakata simu na kuitupia mezani kisha yeye mwenye akajitupa kitini na kushusha pumzi ndefu. Akawaita vijana wake wote na kuwapa taarifa hiyo ambayo iliwachanganya mpaka wakachanganyikiwa. Lakini la kutokea tayari lilikuwa limetokea.






04

KIJIJI CHA MINDE – BAGAMOYO



“Babu! Babu!” kijana wa makamo alimwita babu yake huku akiwa anahema kama aliyefukuzwa na mbwa.



“We, nini?” babu yake aliyekuwa ameketi chini na wavuvi wenzake wakiwa wanasuka nyavu zao alimjibu kwa kumwuliza.



“Ame- ameam- amemka, yule mtu ameamka…”

Yule mzee akawatazama wale wavuvi wenzake na wote wakakurupuka na kukimbimbilia kwenye ile nyumba walimomlaza huyo mtu. Walipofika waliingia taratibu bila kufanya kelele na kumtazama.



“Oooh! Ameamka, asante binti kwa dawa ulizompatia,” yule babu alimshukuru binti aliyekuwa kando na chungu chake kikubwa kilichojaa maji ya kijani.



“Bila asante, ni wajibu wangu kumsaidia,” akajibu.



Wale wazee wakasogelea kitanda na kumzunguka wakimtazama, naye pia alizidi kuwatazama kwa kuwashangaa.



“Niko wapi? Niko wapi hapa?” akauliza kwa ukali na kumkunja kanzu mzee mmoja aliyekuwa jirani na yeye.



“Aaah a a a! kijana tulia kwanza, hapa upo mahali salama kabisa,” mzee mwingine alimsihi mtu huyo kwa lugha ya pwani.



“Wewe ni nani kijana?” Yule mzee akauliza.

Yule mtu akawashangaa tena, akawatazama na kuwakazia macho, kisha akajitahidi kukaa na kuegemea ukutani.



“Naitwa Amata,” akajibu kwa kifupi.



“Amata! Pole sana Amata, tumekuokota baharini ukisukwasukwa na mawimbi makali. Mungu mkubwa kwani yalikupeleka mpaka kwenye mikoko nasi tumekuona huko, nini kilikupata kijana,”



Amata akanyamaza kimya akifikiria jambo, akijaribu kuvuta kumbukumbu kwa lile lililotokea.

Saa 20 Zilizopita…

Ajali ya ndege.



Mara tu baada ya kiti cha Amata kufyatuka na kutoka nje wakiwa angani, parachute alilokuwa akitumia Amata likagoma kufyatuka, akahangaika nalo huku msukosuko ukiendelea. Kutoka kwenye ile ndege akaanza kuanguka kwa kasi huku akielekea baharini.



“Scobaaaaaa!!!!” aliita kwa nguvu lakini mwito wake haukuwa na nguvu kwani Scoba naye alikumbwa na maswahiba yake. Kutokana na lile parachute kushindwa kufunguka, Amata alitua baharini kwa kishindo na kuzama kwa sekunde kadhaa kabla ya kuibuka juu. Kwa mbali aliiona kitu kama boti ikija kwa kasi na kupunga mikono kuomba msaada lakini badala ya msaada wale jamaa wakafyatua risasi kumshambulia, Amata akapiga mbizi na risasi mbili zikampata eneo la mbavu. Maumivu yake yalimweka kwenye hali mbaya kiasi kwamba alijikuta akipoteza nguvu. Jua lilififia machoni pake, kiza kikayafumba macho, akajikuta anapoteza nguvu na ukimya mkuu ukamchukua.



“Nimekwisha!” akajitahidi kutamka kwa taabu.



“Ma-da-m S” akajitahidi kuita kwa nguvu lakini bado aliona giza likimzidi nguvu.



* * *



“Shabash, nimempata kwisha habari yake,” kijana mmoja alikuwa akishangilia kwenye ile boti. Huku akipiga risasi nyingine hewani.



“Una uhakika?” Mwenzake akauliza.



“We sogeza mashine pale uone, maiti tu ile,”



Ile boti ikasogea mpaka pale na kuukuta mwili wa Amata ukiwa kifudifudi juu ya maji baada ya kuibuka. Wakautazama na kuondoka zao.



“Buriani, hatuna historia ya kubeba maiti,” yule nahodha wa chombo akageuza na kuondoka zao mpaka katika kambi yao iliyojengwa katika moja ya visiwa vilivyozunguka eneo hilo huku bado wakipiga risasi hewani kuoneshya.

* * *


Mawimbi ya bahari yakausukasuka mwili wa Amata na kuutupia kwenye mikoko iliyofungana katika pwani ya eneo hilo, na kunasa huko. Jioni ya saa kumi na mbili hivi wavuvi kutoka kijiji cha Minde walikuwa wakipita kuelekea katika shughuli zao huko katikati ya bahari, wakiwa na karabai zao wakipita pembezoni kabisa karibu na ile mimea ndipo walipouaona mwili huo.



“We hebu mulika pale,” mzee mmoja akamwambia nahodha wa chombo hicho.



“Nini?”



“Yule siyo mtu Yule?” wakatazama kwa makini na kugundua ni mwili wa binadamu, wakashuka na kutumbukia majini mpaka eneo lile.



“Oh Shit, si ajabu akawa hai huyu, mtazame!” wakamgeuza geuza na kuamua kumbeba. Safari ya kwenda uvuvini ikaghairishwa na wazee wale wakaamua kurudi kijijini. Walifika na kumshusha Amata kisha wakamlaza chini mkekani huku wakisogeza moto jirani ili kumpa joto. Mzee mmoja alikwenda kumwita binti anayesifika kujua dawa za asili, akaja na kuanza kumfukizia Amata moshi wa mchanganyiko wa majani na magome makavu ya miti.



“Hajafa bado huyu?” mzee mmoja akauliza.



“Hapana hajafa huyu, ila amezimia na yuko mbali sana katika mzimio wake, ninamwita polepole ataamka tu,” yule binti akajibu.



Matibabu hayo ya kienyeji yaliendelea mpaka asubuhi yake na mchana wa siku hiyo Amata alirudiwa na fahamu







Siku ilofuata



Amata alitoka nje ya nyumba hiyo majira ya saa nne asubuhi, akasimama nje na kuangalia upande wa baharini, akiwa hajui ni wapi alipo mpaka dakika hiyo. Akiwa bado hajisikii vyema sana hasa sehemu fulani za mwili wake ambako kulikuwa na kitu kama jeraha aliendelea kutembea hapa na pale pale kijijini akiangalia hiki na kile. Kila hatua chache alisimama kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia katika maeneo ya mbavu. Kila alkisjidhika aligundua kuwa kulikuwa na majeraha. Nyuma yake akahisi mchakacho wa nyayo za binadamu, akasimama na kusubiri.



“Naona una nguvu sasa,” sauti nyororo ya kike ikasikika nyuma yake, akageuka na kugongana macho na mwanadada mrembo aliyekuwa ndani ya mavazi ya kawaida kabisa ya kijijini.



“Ndiyo, sasa najisikia nafuu zaidi, ila maumivu tu eneo hili,” akamjibu na kumwonesha eneo lenye maumivu.



“Pole, unywe ile dawa niliyokupa, ndani ya saa sita mpaka kumi zijazo utajisikia sawa kabisa, ni dawa nzuri kwa majeraha kama hayo,” Yule mwanadada akamweleza.



“Unaitwa nani?” Amata akauliza.



“Minde!” akajibu huku wakiwa wanatazamana na Amata.



“Asante Minde, umeokoa maisha yangu, unastahili zawadi, zawadi kubwa kabisa. Niambie hapa ni wapi?”



“Hapa ni Minde,”



“Minde tena?” Amata akauliza kwa kupata uhakika.



“Ndiyo, usishangae, kijiji hiki kinaitwa Minde na mimi naitwa Minde,” yule mwanadada akamweleza Amata kisha akauchomoa mfuko wa plastiki ndani ya kanga yake kuukuu na kumpa Amata. Alipoupokea alihisi wazi uzito wa kiasi wa mfuko huo, akaufungua ndani na kuangalia, akatabasamu kisha akamwangalia binti yule kwa kumkazia macho.



“Minde!” akaita kwa sauti tulivu.



“Umevipata wapi hivi?” akauliza.



“Nimevitoa kwenye nguo zako ulizovaa,” akajibiwa. Kamanda Amata akavimwaga juu ya jiwe lililokuwa jirani. Kwanza akachukua bastola iliyokuwa hapo, akaivuta slider yake na kuirudisha, akaifyatua kitako na kuchomoa magazine iliyojaa risasi, akazipachua moja moja na baadae akazirudishia tena. Akamtazama Minde akamwona jinsi alivyojawa na woga.



“Mbona unaogopa?” akamwuliza.



“Mmm umejuaje kama naogopa?”


“Nikimwangalia mtu usoni huwa najua kila kinachofanyika ndani ya ubongo wake,” wote wakacheka.



“Basi we unafaa kuwa mtabiri!”



Amata akachukua waleti iliyokuwa pamoja na hivyo, akaifungua na kukuta kila kitu chake kipo salama, ndani yake licha ya vitambulisho kulikuwa na fuba la pesa za kitanzania kama shilingi laki tatu hivi, akachomoa noti kadhaa zilizofungwa vyema. Akazihesabu harakaharaka zilikuwa shilingi laki moja.



“Hii zawadi yako Minde,” akamkabidhi, binti yule akamtazama Amata kwa jicho la uchu na kumshukuru kwa kibantu. Amata alimkumbatia Minde mikononi mwake huku akimwangalia usoni na kuyaona macho yanayojaa machozi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom