BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,020
Shibuda awashangaa wanaoogopa urais
Thursday, 09 April 2009 16:30
Na Peter Masangwa
Majira
Thursday, 09 April 2009 16:30
Na Peter Masangwa
Majira
MBUNGE wa Maswa (CCM), Bw. John Shibuda ameshangazwa na kitendo cha Kamati Kuu ya Mkoa wa Shinyanga kutoa tamko katika Jimbo lake kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye mgombea pekee katika uchaguzi wa mwakani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Bw. Shibuda alisema kitendo hicho kinafanywa na wanasiasa wenye mawazo mgando na maoni yaliyopauka kwani mwana demokrasia hawezi kuthubutu kukandamiza katiba kwa kiasi hicho.
"Inasikitisha sana kwa mtu kama Shibuda niliyeonesha nia ya kugombea urais kuwachanganya watu namna hii na kuanza kujihami kwa kutoa matamko na kufanya maandamano kushinikiza kuwa mgombea abaki kuwa Rais Kikwete," alisema Bw. Shibuda.
Alisema kuwa demokrasia bila utii ni wendawazimu kwani kitendo cha kumtisha kwa jinsi hiyo haitabadili utashi wake wa kugombea urais kwani anaamini kile anachokisimamia.
Bw. Shibuda alisema tamko la CCM linasema milango iko wazi kwa mwanachama mwenye sifa kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho lakini tamko la Mkoa wa Shinyanga linasema mtu akijitokeza atafukuzwa.
"Viongozi ndani ya chama na nje ya chama wanahitaji kufundishwa haki elimu za kiraia ili wajue na kuisemea demokrasia na si kukurupuka kwa kujikosha kwa kiasi hicho," alisisitiza.
Alifafanua kuwa kitendo chake cha kuonesha nia ya kugombea si kuwa Rais Kikwete hafai na wala hajafanya kazi ila anatambua kazi yake, hivyo kugombea kwake ni jambo la kikatiba na kidemokrasia na kuwaonya wanaojaribu kuvunja katiba kwa kiasi hicho.
Je, kama Rais Kikwete angekuwa na huruka kama Bw. Idd Amin wananchi wangekubali kumpa vipindi vyote viwili?" Alihoji Bw. Shibuda.
Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Shinyanga juzi ilitoa tamko kuwa mgombea urais wa chama hicho atakuwa Rais Kikwete kwani ndiyo utamaduni waliojiwekea.
Pia Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam imeunga mkono Rais Kikwete kuwa mgombea pekee kwa tiketi ya chama hicho.