Sheria mpya ya madaktari yaja

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
waziri%20wa%20afya%20mwinyi(10).jpg

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi


Serikali inakusudia kutunga sheria mpya ya madaktari, kutengeneza kanuni za kuwasilisha malalamiko dhidi ya wanataaluma wa afya pamoja na kupitia na kusambaza miiko na maadili ya taaluma ya udaktari.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, aliliambia Bunge jana mjini hapa alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwama 2012/13.

Alisema wizara yake itaandaa nyaraka mbalimbali za Baraza la Mawaziri ili kuwasilisha serikalini na katika ngazi mbalimbali zinazohusiana na kada hiyo kwa ajili ya kutekeleza azma ya kutunga sheria ya madaktari.

"Wizara itaandaa nyaraka na kuziwasilisha katika ngazi husika kwa ajili ya maamuzi, mapendekezo ya miswada ya kutunga sheria mpya ya madaktari na madaktari wa meno," alisema.

Dk. Mwinyi alisema kazi ya kutengeneza kanuni za kuwasilisha malalamiko dhidi ya watumishi wa kada ya afya itafanywa na Baraza la Madaktari Tanganyika ambalo pia litapitia na kusambaza miiko na maadili ya taaluma ya udaktari.

Alisema baraza hilo pia kwa kushirikiana na wizara yake litafanya ukaguzi wa hospitali zinazofundisha mafunzo kwa vitendo na zile za rufaa za mikoa ili kuangalia ubora wake.

Alisema lengo nikubaini idadi ya hospitali zitakazohimili idadi ya madaktari wanaohitimu vyuo vikuu.

Alisema nyaraka nyingine zitakazoandaliwa ni za kupendekeza kutungwa kwa sheria mpya ya wazee, kufanya mabadiliko ya sheria ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) sura ya 150, marekebisho ya sheria iliyoanzisha Taasisi ya Chakula na Lishe, sheria ya kuwianisha mfuko wa afya vijijini (CHF) na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) na kufanya mabadiliko ya sheria ya chakula, dawa na vipodozi sura ya 219.

Mbali ya hilo, alisema wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa kutunga sheria ya kusimamia taaluma ya kemia, sheria ya kusimamia huduma za afya nchini na sheria ya kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Bohari ya Dawa itaanzisha na kukamilisha ujenzi na upanuzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia dawa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Tabora na Mbeya na pia itaanza kuweka alama maalum katika dawa zote za serikali.

Akizungumzia hospitali za rufaa pamoja na MHN, alisema Muhimbili itaboresha huduma za rufaa ngazi za juu kwa kufanya upasuaji kwa kutumia hadubini (endoscopic surgery), upasuaji mkubwa wa moyo na kukamilisha ujenzi wa kituo cha tiba na mafunzo ya upasuaji wa moyo.

Alisema Taasisi ya Mifupa (MoI), itaanza ujenzi wa jengo la kutoa huduma za matibabu katika fani za mifupa na magonjwa ya mishipa ya fahamu ambao utakamilika ndani ya miezi 18 na kwamba utaongeza idadi ya vitanda kutoka 136 vya sasa hadi 336.

Alisema MoI pia itaanzisha mafunzo ya shahada ya uzamili ya upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo.

Waziri Mwinyi alisema Taasisi ya Saratani Ocean Road itanunua mashine za kutibu saratani kwa ufanisi ziitwazo CT Simulator na Linear Accelerator na pia itaanzisha upasuaji wa saratani.





CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom