WATANZANIA wametakiwa kujitokeza na kushiriki katika Kongamano la kitaifa linalotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, ili kujadili mustakabari wa rasilimali zilizopo nchini.Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sheikh Rashid Kayumbo, alisema ameazimia kuandaa kongamano hilo, ili kuona ni namna gani rasilimali zilizopo zinamnufaisha mwananchi tofauti na ilivyo sasa.Alisema kongamano hilo litashirikisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge, vyama vya siasa, viongozi wa dini pamoja na asasi za kiraia.Sheikh Kayumbo alisema anakerwa na baadhi ya viongozi ambao wanawapa fursa kubwa wageni kutoka nje na kushindwa kuwasaidia Watanzania kupitia rasilimali zilizopo.Ukipitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndiyo utaamini kuwa serikali haina dhamira ya kweli katika kuwasaidia Watanzania, alisema.Alisema kripoti hiyo inaonesha jinsi baadhi ya wawekezaji nchini walivyoweza kusaidiwa katika mitaji yao huku wakiwepo Watanzania waliokosa mitaji na serikali kushindwa kuwasaidia.Alibainisha kuwa kabla ya kufikia uamuzi wa kuandaa kongamano hilo, alijaribu kuwasilisha taarifa zake Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, lakini baadhi ya barua zake hazikujibiwa.
source: tanzania Daima
source: tanzania Daima