Serikali yawatenda madaktari vibaya, mgogoro haujapata suluhu

Travelogue_tz

JF-Expert Member
Sep 28, 2010
848
1,212
Kwa nini madaktari wapuuzwe?


Mwandishi Wetu

RAIA MWEMA :Toleo la 275 2 Jan 2013
Baraza la Madaktari ni tatizo jingine

JUNI 23, mwaka 2012, Tanzania iligubikwa na mgomo mkubwa wa madaktari. Sina nia ya kufufua machungu yaliyotulia. Najua wapo waliopoteza ndugu, jamaa na hata marafiki. Mungu awafariji.

Wakati mgomo ule ukiendelea, aliyekuwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka alitekwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa pande. Hilo lilikuwa tukio la kinyama, linalopaswa kuendelea kulaaniwa.

Lakini mgomo ule wa madaktari ulilenga kuishinikiza serikali kuboresha huduma za afya ikiwamo dawa, vifaa tiba na uboreshwaji wa mazingira ya kazi. Hii ikiwa ni pamoja na kuboresha majengo ya hospitali, zahanati na vituo vya afya sambamba na uboreshaji au ununuzi wa vifaa muhimu kama CT scan, mashine za x-ray na uongezwaji wa vitanda kwa wagonjwa ili kuepuka tatizo la wagonjwa kulala chini hata katika Hospitali ya Taifa Muhimbili achilia mbali hospitali zilizopo mikoani.

Lakini pia madaktari waliitaka serikali kuongeza mishahara na posho mbalimbali ili ziendane na hali ya maisha. Yaliyotokea sote tunajua. Vitisho na ubabe vilitawala huku baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali wakitoa matamko ya kuvunja moyo "asiyetaka kazi aache, serikali haina uwezo"

Ninakumbuka vema madaktari hawakuishia kuainisha madai yao ya msingi ila walitoa mapendekezo ya kiwango cha mshahara na posho mbalimbali. Hili ni jambo la kawaida mahali popote duniani. Hata kampuni za uchimbaji madini hutoa mapendekezo ya kiwango wanachoweza kuilipa serikali halafu serikali huangalia na kuamua kuikubali au kuzungumza zaidi na hatimaye kuelewana.

Itakumbukwa kwamba serikali ilitumia Mahakama, vitisho na matamko ambayo hayakulenga kutatua mgogoro wake na madaktari. Vitisho na unyama uliofanyika ni wazi kuwa hakukuwa na nia ya dhati ya kutatua tatizo. Madaktari waliokuwa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa (interns) ambao kwa kiasi kikubwa ndio hufanya kazi nyingi katika hospitali takribani zote za rufaa hapa nchini walifukuzwa maeneo ya kazi.

Baada ya tukio hilo ni wazi kuwa madaktari pia waligawanyika na kupoteza mwelekeo. Siwalaumu lakini nadhani hilo lilikuwa haliepukiki maana kama wasingepoteza mwelekeo na kugawanyika huenda yangetokea yale yaliyotokea nchi za Tunisia na Misri. Kwa namna moja au nyingine japo haki na madai ya madaktari yamekandamizwa na kuzimwa kwa sasa lakini nadhani wameepusha mauaji na vita kati ya serikali na wananchi.

Ni kweli vita hii si njema lakini pale watawala wanapoiomba kutoka kwa wananchi kwa kuwanyamazisha na kuwakandamiza basi ni afadhali vita ya aina hiyo kuliko mateso kwa wananchi, tena mateso yanayofanywa na baadhi ya watu waliowachagua.

Madaktari zaidi ya 394 walisimamishwa kwa zaidi ya miezi sita, tangu Juni 29, 2012. Najiuliza kama mgomo ulikuwa unahatarisha maisha ya Watanzania; je, kipindi chote hiki ambacho madaktari hawa walikuwa wamesimamishwa maisha ya wagonjwa yalikuwa salama? Na ni kitu gani hasa kilichosababisha serikali kuwasimamisha na kisha kukaa kimya kwa zaidi ya nusu mwaka, hadi Novemba 6, mwaka 2012 ndipo waanze kuwahoji?

Tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa pande Dk. Steven Ulimboka limefikia wapi hasa? Je, kweli haki itatendeka na ionekane ikitendeka kuhusu wahusika wa tukio hilo? Na kama haki haitatendeka nini kitafuata?

Baada ya kimya cha zaidi ya nusu mwaka ndipo Baraza la Madaktari Tanzania, ambalo kwa sasa sidhani kama ni chombo huru lilianza kuwahoji interns, tena kwa kuwaita Dar es Salaam.

Ifahamike kuwa hawa ni vijana wadogo tu kutoka vyuoni kwa hiyo unaweza ukatambua uwezo wao kifedha hasa ukizingatia kuwa hawakuwa na kazi kwa muda wa zaidi ya nusu mwaka.

Kabla ya kuzungumzia kilichotokea kwa hao walioweza kufika na kuhojiwa kisha kuadhibiwa ni wazi kuwa wapo wengi ambao hawakuweza kuhudhuria kwa sababu mbalimbali, hali ya kifedha ikiwa mojawapo, lakini pia kutopata taarifa za uhakika.

Baraza la Madaktari ni chombo kinachofanya kazi kwa mfumo wa kimahakama na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahusika moja kwa moja. Kwa kifupi ni chombo kikubwa kilichopaswa kuwa huru. Kwa mtazamo wangu kwa sasa chombo hiki si huru kwa sababu kuu moja, kuwa chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo ni serikali. Sidhani kama mtu mwenye akili timamu anaweza kutegemea serikali ijihukumu yenyewe na kujiadhibu.

Nikiangalia na kufuatilia kwa makini utendaji kazi wa Baraza la Madaktari (MCT), na kwa kuzingatia hatua na uamuzi uliofanywa kuhusu hawa madaktari waliokuwa wamesimamishwa najisikia aibu. Binafsi simo ndani ya MCT, lakini walichokifanya ni aibu ambayo haikutegemewa.

Makosa ambayo madaktari hawa walishtakiwa nayo katika chombo hiki ni kushiriki mgomo batili na kuvunja kanuni na maadili ya kazi ya udaktari. Lakini kosa jingine ni kuhatarisha maisha ya wagonjwa. Hakuna daktari hata mmoja aliyekuwa na kosa tofauti na haya. Hukumu iliyotolewa na Baraza la Madaktari, inashangaza kama ifuatavyo.

Kwanza onyo, adhabu ya pili ni onyo kali, nyingine ni kusimamishwa kwa muda. Na katika waliosimamishwa, wapo waliosimamishwa mwezi mmoja, wapo waliosimamishwa miezi miwili, wengine miezi minne na wapo waliosimamishwa miezi sita.

Na kwa hawa waliosimamishwa miezi sita kuwafanya kukaa bila kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kumbuka hawa ni wanataaluma wanaohitajika kwa kiasi kikubwa hapa nchini na zaidi wanaweza kwenda kufanya kazi popote duniani. Lakini pia, pamoja na kwamba wote walishitakiwa kwa makosa yanayofanana lakini adhabu ni tofauti kwa kiasi cha kushangaza.

Kwa macho ya kawaida, yasiyohitaji elimu ya kisheria, ni kwamba inawezekana vipi kukawa na tofauti kubwa ya hukumu kwa watu waliotiwa hatiani kwa makosa yanayofanana?

Baraza la Madaktari wanaweza kutuambia ni vifungu gani vilitumika kumhukumu kila mmoja? Na imetokea vipi kosa moja au makosa yanayofanana kuwa na aina nyingi za hukumu kiasi hicho?

Nilipochunguza kwa makini na kufuatilia nani kapewa adhabu gani nimegundua kuwa waliosimamishwa wengi wao ni wale ambao ama walisikika wakizungumza au kuandikwa kwenye vyombo vya habari kuhusu madai ya madaktari. Tujiulize, hawa walikuwa na mashitaka ya ziada? Kama hapana, kwa nini watendewe hivi?

Swali jingine la kujiuliza ni kwamba wakati haya yakitokea na interns hawakupewa adhabu na baadhi yao kutakiwa kurudi kazini kuanzia Januari 14, mwaka huu, hali katika hospitali zetu ikoje? Mazingira yameboreshwa? Dawa na vifaa tiba vipo vya kutosha?
Achilia mbali adhabu zilizotolewa na baraza hilo lakini pia taarifa kutoka ndani ya baraza hilo zinasema madaktari 49 wamefutiwa mashtaka, baada ya kutokukutwa na hatia.

Ifahamike hawa ni wale ambao ama walikuwa wagonjwa, au katika ruhusa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na misiba, ugonjwa au harusi. Lakini ifahamike kuwa hawa nao hawakuwa kazini kwa kipindi kisichopungua nusu mwaka kabla ya kufutiwa mashitaka.
Hii inatupa taswira gani hasa ya utendaji wa baraza na serikali kwa ujumla? Ilkuwaje hawa nao wakasimamishwa kwa muda wote huo? Ni nani aliyeamua hivyo na kuhatarisha maisha ya wagonjwa ambao wanateseka kwa ukosefu wa madaktari nchini?

Ni nani anayeweza kusimama kifua mbele na kusema serikali ipo makini? Ni nani anayeweza kutuambia kuwa Baraza la Madaktari ni chombo makini? Kama baraza liliweza kuwasimamisha kazi madaktari ambao hawakuwapo katika mgomo, je, linaweza kutenda haki pasi na shaka?

Baraza hili limeonesha udhaifu mkubwa pale lilipokaa kimya bila kueleza hatima ya madaktari interns ambao hawakuweza kufika Dar es Salaam ili wahojiwe kwa sababu mbalimbali, tatizo la kifedha likiwa mojawapo. Lakini si hivyo tu, ifahamike kuwa baraza hili halikutumia njia inayofaa kuwataarifu madaktari juu ya kufika wizarani Dar es Salaam ili wahojiwe.

Baraza lilibandika tangazo wizarani na kuwatumia meseji ya ujumla ikisema interns ambao majina yao yamebandikwa wizarani wafike hapo kuhojiwa kulingana na tarehe waliyopangiwa. Baraza halikutoa taarifa kwa mhusika mmoja mmoja kuwa unahitajika kufika wizarani lini na kwa ajili gani. Nasema baraza hili limetia aibu maana nina uhakika wa taarifa kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa baraza hilo kuwa hata sasa hawana uhakika kama hao madaktari ambao hakuweza kuhudhuria walipata taarifa au la.

Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la Madaktari wameoneka kutoridhishwa na utaratibu na uamuzi uliofanyika. Hili limethibitika kwa maneno yao wenyewe. Wengine wamesikika wakisema haki ilikuwa ikitendeka kipindi cha Nyerere na si sasa.

Swali ambalo Watanzania tunapaswa kujiuliza ni, je, mazingira ya kazi kwa madaktari hawa ambao waligoma kwa sababu ya mazingira magumu yameboreshwa? Je, dawa zinapatikana? Siku hizi sioni matangazo ya Mseto (ALU) dawa yenye nembo ya jani. Najiuliza imekwenda wapi?

Maana najua inauzwa elfu moja. Kwa sasa haipo yenye nembo ya jani na zilizopo ni shilingi elfu saba kwa dozi moja. Swali ni kwamba Waziri wa Afya ana lipi la kutueleza? Mbona amekaa kimya?

Katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambayo imepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa hali ya vitendea kazi ni mbaya. Kati ya Desemba 2 hadi 18, mwaka jana (2012), nimethibitisha hospitali kukosa dawa ya uchungu (Oxytocin) kwa wazazi wanaotaka kujifungua.

Lakini kipindi hicho hicho pia hakukuwa na vitambaa (gauze) na hivyo wagonjwa kutakiwa kununua halafu ndio wafanyiwe upasuaji baada ya vitambaa hivyo kuwa sterilized. Desemba 23, 2012, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma haikuwa na chlorine kwa ajili ya kusafishia vifaa vilivyotumika kwenye upasuaji.

Hivi karibuni Hospitali ya Bunda, mkoani Mara haikuwa na umeme wala maji. Hospitali ya Temeke Dar es Salaam mgonjwa anatakiwa kununua sindano, maji ya dripu na karibu kila dawa.

Hivi kweli kati ya madaktari na serikali nani anahatarisha maisha ya wagonjwa katika hospitali? Hivi hawa madakatari waliotendewa dhuluma kama hii kweli wanaweza kufanya kazi kwa moyo mmoja? Mungu tusaidie Watanzania.

Binafsi nimeshuhudia baraza hili la madaktari, likitoa hukumu kwa jazba na hasira hasa daktari anayehojiwa anapoeleza ukweli wa hali mbaya ya huduma katika hospitali zetu na pale anapoeleza uonevu uliofanywa na unaoendelea kufanywa na serikali, ikiwamo yenyewe MCT.

Sidhani kama huu ndio utakuwa mwisho wa madaktari kudai haki yao stahiki na sidhani kama wataacha kupigania huduma bora kwa Watanzania.

Inawezekana wasigome leo au kesho ila nina uhakika wa kutokea mgomo mbaya zaidi ikiwa hali ya huduma za afya na mazingira ya kazi yasiposhughulikiwa ipasavyo.

Maana si madaktari watakaoanzisha mgomo bali wagonjwa na ndugu zao na Watanzania kwa ujumla. Nguvu ya umma haitazuiliwa na chochote. Si vitisho, si Mahakama wala risasi itakayoweza kuwazuia wananchi wakichukua hatua ya kudai haki yao kwa pamoja.
Zipo namna nyingi ambazo Watanzania wanaweza kutumia kuitia adabu serikali. Nimekuwa nikisikiliza sana hotuba za Rais wa Marekani, Barack Obama.

Mara nyingi amekuwa akisema ushindi wake ni ushindi wa Wamarekani na maendeleo yaliyofikiwa na Marekani yanatokana na Wamarekani. Hapa kwetu nadhani mnaelewa kiongozi haoni aibu kusema maendeleo yanaletwa na chama chake.
Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), Wizara ya Afya ni vema mkatoa ufafanuzi wa ukiukwaji, ukandamizaji na uonevu huu mkubwa waliofanyiwa madaktari (Interns na registrars).

Nadhani ni wakati wa wanaharakati, chama cha madaktari na yeyote aliye na nia njema kwa nafasi yake kuandaa muswada wa kuirekebisha MCT ili kiwe chombo huru na kurudisha heshima iliyopotea ya chombo hiki.
Ili kiweze kuwa huru kutenda haki na kuepusha hisia za chombo hiki kusukumwa na watawala kifanye watakavyo wao.

Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika

Mwandishi wa makala haya, Dk. George Adrian, amejitambulisha kuwa ni daktari wa binadamu. Anapatikana kwa simu; 0715 182 106
 
Dr. Godbless, tatizo lipo kwenu wenyewe Ma Drs. Mnamgawanyiko usiokubaalika, akigoma Residents, Registrar hawagomi, akigoma Intern Specialist na Ma Chief hawagomi, akigoma Nurse, Drs hawagomi. Hili ndo tatizo la msingi kwanza!
 
Ipo siku watawala watakapa adhabu yao hata kama watakuwa wamestaafu. Siwalaumi madaktari, nature ndivyo ilivyo kila mtu ana matatizo yake na kuna wengine wanatumika humohumolakini ukweli huwa unabaki vingine vyoote huwa ni temporal solution tu.
 
Hii nchi nadhani tunahitaji kuing'oa serikali iliyopo kwenye boksi la kura.. tena kwa kishindo hiyo 2015..
 
Dr. Godbless, tatizo lipo kwenu wenyewe Ma Drs. Mnamgawanyiko usiokubaalika, akigoma Residents, Registrar hawagomi, akigoma Intern Specialist na Ma Chief hawagomi, akigoma Nurse, Drs hawagomi. Hili ndo tatizo la msingi kwanza!
eti wanagomea ubovu wa majengo na x-ray.halafu madaktari wakigoma hawataki kuchanganyikana na wauguzi?yaani hawa jamaa wanatia hasira aisee?wewe waache tu.heri yao madakrari wenye nia njema ambao hawagomi maana hawa mungu atawabariki.
 
Ipo siku watawala watakapa adhabu yao hata kama watakuwa wamestaafu. Siwalaumi madaktari, nature ndivyo ilivyo kila mtu ana matatizo yake na kuna wengine wanatumika humohumolakini ukweli huwa unabaki vingine vyoote huwa ni temporal solution tu.
kwa nini huwalaumu madaktari na kwa nini serikali inahitaji adhabu?
 
Mgomo haukuwa njia sahihi ya kuzikabili changamoto za sekta ya afya. Inahitajika mikakati endelevu ya muda mrefu na yenye affordable sequelae, lakini si kugoma kuwatibia akina mama, watoto, wazazi wetu na vijana wenzetu.
Kwa hiyo mgomo was an act of provocation kwa serikali, wananchi na wadau wote wa afya. Ukiprovoke tegemea kuwa the other side itareact na LAZIMA ujiandae kwa aina zote za reaction. Je, madaktari walijiandaa vipi na potential reactions za serikali na wadau wengine wa sekta ya afya?
 
serikali inayosubiri watumishi wagome ndio ifanyie kazi madai yao haiwezi kufanza tofauti na ilivyofanza.!

kidumu chama
 
serikali inayosubiri watumishi wagome ndio ifanyie kazi madai yao haiwezi kufanza tofauti na ilivyofanza.!

kidumu chama

ingekuwa inasubiri hivyo haya yaliyofanyika yasingekuwepo.kama huoni papasa mkuu au uliza uambiwe
 
Madaktari wanapaswa kushirikiana na serikali kwa kuwaeleza mahitaji yao.
 
Huwezi kuwa na baraza huru kama kila kitu kinapewa na serikali kuanzia pango mpaka mishahara yao.Madkatari wenyewe ndio mno takiwa kubadilisha baraza lenu na kuwa la kisasa zaidi.Kwanza ondokeni kwenye lile jengo la serikali mkapange sehemu nyingine.Pili mjihudumie kwa kila kitu msitegemee serikali mkiweza hapo mtakuwa mmepiga hatua moja mbele ya kumsaidia huyo daktari.Ama sivyo mgomo baridi utaendelea mpaka mwisho wa dahari.
 
In actual fact hii ni habari ya kutia huruma na kusikitisha sana.
Itafika wakati wananchi watachagua kufa kwa njaa au kwa risasi. this is too much.
 
In actual fact hii ni habari ya kutia huruma na kusikitisha sana.
Itafika wakati wananchi watachagua kufa kwa njaa au kwa risasi. this is too much.
hebu onesha uhusiano wa mchango wako na uzi?wanaokufa kwa njaa ni madaktari au?
 
sekta ya afya itakombolewa siku wananchi watakapogundua kuwa ni haki yao ya kikatiba kupata huduma bora ya afya kuanzia kinga mpaka matibabu na serikali inawajibu wa kutekeleza hilo bila kikwazo.
 
Madaktari wanapaswa kushirikiana na serikali kwa kuwaeleza mahitaji yao.

Wawaeleze kwakuwatundikia Iv drips au kwanjia gani? wazunguke na magari ya matangazo ili serikali isikie? Fungua macho uone kinachoendelea. Sikio lakufa halisikii dawa. Ndo maana serikali yako inasema UTII BILA SHURTI Ikimaanisha kukaa kimya bila kuhoji hata kama unanyanyaswa. Hayo yamepitwa na wakati. Something has to be done.
 
shauri yao maana akili nyingi ni mauti mbeleni ndio matunda wanayotakiwa kuvuana leo baada ya kusalitiana
 
Ajabu miaka hii kuna madaktari wasaliti,wamerudisha nyuma haki na heshima ya udaktari utakubalije mtu kasoma CUba kama mwinyi awaelekeze wajumbe wa Baraza la madaktari nini cha kufanya na nyie mulilikoroga pale muliposambaratika sasa watawafirigisa na majiti makalioni wamegundua hamna umoja
 
sekta ya afya itakombolewa siku wananchi watakapogundua kuwa ni haki yao ya kikatiba kupata huduma bora ya afya kuanzia kinga mpaka matibabu na serikali inawajibu wa kutekeleza hilo bila kikwazo.

Hizi sasa ni porojo. Katiba ipi unayozungumzia? hakuna haki isiyo na wajibu, je wajibu wa mwananchi kwenye haki hiyo ni nini?
 
Back
Top Bottom